5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾
59. Ewe Nabii! Waambie wake zako na wake za waumini, wajiteremshie jalbab zao. Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
لَّئِن لَّمْ يَنتَهِ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْمُرْجِفُونَ فِي الْمَدِينَةِ لَنُغْرِيَنَّكَ بِهِمْ ثُمَّ لَا يُجَاوِرُونَكَ فِيهَا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٠﴾
60. Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na wale wanaoeneza fitna Madina, hawataacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.
مَّلْعُونِينَ أَيْنَمَا ثُقِفُوا أُخِذُوا وَقُتِّلُوا تَقْتِيلًا ﴿٦١﴾
61. Wamelaaniwa! Popote waonekanapo, na wakamatwe na wauliwe kabisa.
سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾
62. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.
WAJIBU WA HIJABU
Aya 59 – 62
LUGHA
Kuna kauli nyingi kuhusu neno Jalbab: kuna wanaosema kuwa ni nguo inayomfunika mwanamke kutoka kichwani hadi nyayoni. Wengine wakasema ni ushungi unaofunika kichwa cha mwanamke na uso wake. Kauli hii ndio aliyo nayo mwenye Majmaul-Bayan.
MAANA
Zimekwishatangulia Aya mbili zinazofahamisha wajibu wa hijabu kwa wanawake:
Ya kwanza ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao.” Juz. 18 (24: 31). Ya pili ni ile Aya ya 53, katika Sura hii tuliyo nayo: “Na mnapowaomba chombo cha nyum- bani, basi waulizeni nyuma ya mapazia.”
Aya iliyo wazi zaidi ya hizi mbili ni hii tuliyo nayo, isemayo:
Ewe Nabii! Waambie wake zako na wake za waumini, wajiteremshie nguo zao.
Kusema kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘wajiteremshie nguo zao’ inaenea kusitiri na kufunika sehemu zote za mwili, kikiwemo kichwa na uso. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana wasiudhiwe.
Waislamu, mwanzoni walikuwa wakitoka bila ya kujitanda, kama ilivyokuwa desturi ya kijahiliya, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamtaka Mtume wake mtukufu, katika Aya hii, awaamrishe wake zake kujisitiri na kuvaa hijabu. Na amri inafahamisha wajibu. Kwa hiyo hijabu ni wajibu.
Hata hivyo uso na viganja viwili havimo kwenye wajibu huu, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ﴿٣١﴾
“Wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika.” Juz. 18 (24:31).
Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana
kutokana na kujistahi na kujichunga. Kwani hijabu ni kinga baina ya mwanamke na tamaa ya watu wenye shakashaka na mafasiki,wasiudhiwe
kwa kuangaliwa na mafasiki.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Anasamehe yaliyopita na anamuhurumia mwenye kutubia na kurejea nyuma.
Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na wale wanaoeneza fitna Madina, hawataacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.
Wanafiki walificha ukafiri na wakadhihirisha imani. Wanaoeneza fitna ni watu katika wananfiki waliokuwa wakieneza propaganda dhidi ya Mtume(s.a.w.
w
)
na maswahaba na wakawatia shaka wale wadhaifu wa imani ambao Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea ibara ya wenye mardhi nyoyoni mwao. Aya inatoa onyo la kuuawa na kufukuzwa wanafiki, waeneza fitna na wale watakaowasikiliza, ikiwa hawatajizuia na upotevu na ufisadi wao.
VITA VYA NAFSI
Siku hizi kueneza fitna kunaitwa ‘vita vya nafsi.’ Nguvu ya shari imetafuta njia nyingi sana za kueneza uongo na mambo ya ubatilifu kwa kila nyenzo. Kuanzia magazeti, radio, runinga, sinema, hotuba, vipeperushi, shule, vyuo, vitabu n.k.
Vyombo hivi vimekaririka masikioni mwa watu kila siku, kiasi ambacho uhakika haupati nafasi kwa watu na wenye ikhlasi, isipokuwa kwa mwamko mkamilifu na elimu itakayotangulia propaganda za wakoloni na wazayuni.
Nimesoma kwenye gazeti linaloitwa Akhabar Al-yawm la Misr, la 13/12/69, kwamba Israil ina magazeti ya propaganda yanayofikia 890 ulimwenguni kwa ajili ya kueneza habari za uongo. Zaidi ya hayo wametawala vyombo vingi vya habari ulimwenguni, kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja; kama vile runinga, radio n.k.
Kwenye mahisabu haya hayaingii magazeti ya Beiruti yenye uhusiano mkubwa na wakoloni na wazayuni.
Kwa vyovyote iwavyo, Alhamdu lillah, Israil imehisi mapigo kutoka kwa waarabu na kwamba propaganda zao zilizotengenezwa na Marekani, na kutangazwa na vibaraka, zimeanza kujulikana.
Wamelaaniwa! Popote waonekanapo na wakamatwe na wauliwe kabisa.
Wamelaaaniwa na kila ulimi, kwa sababu dini yao ni pesa na matendo yao ni udanganyifu, uwongo na hadaa. Hawana dawa isipokuwa kuuawa popote walipo; kama kiungo kilichoharibika, kisipokatwa kitaharibu mwili wote.
Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya desturi ya Mwenyezi Mungu hapa ni hukumu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mpotevu anayepoteza, ambayo ni kuuliwa ambako amekuwekea sharia, ambaye imetukuka hekima yake, tangu zamani. Hukumu hii itabakia milele bila ya mabadiliko wala mageuzi.
يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا ﴿٦٣﴾
63. Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Na nini kitakachokujulisha? Pengine hiyo saa iko karibu.
إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا ﴿٦٤﴾
64. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri moto unaowaka.
خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا لَّا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿٦٥﴾
65. Watadumu humo milele. Hawatapata mlinzi wala wa kuwanusuru.
يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾
66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu na tungelimtii Mtume!
وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾
67. Na watasema: Mola wetu! Hakika sisi tuliwatii mabwana zetu na wakubwa wetu, wakatupoteza njia.
رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾
68. Mola wetu wape adhabu mara mbili, na walaani laana kubwa.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾
69. Enyi ambao mmeamini! Msiwe kama wale ambao walimuudhi Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtaksa na waliyoyasema; naye alikuwa ni mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.
WANAKUULIZA KUHUSU SAA
Aya 63 – 69
MAANA
Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Na nini kitakachokujulisha? Pengine hiyo saa iko karibu.
Makusudio ya saa ni Kiyama Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:187).
Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri moto unaowaka. Watadumu humo milele. Hawatapata mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu na tungelimtii Mtume!
Makafiri na waasi kesho watasukumwa kwenye adhabu ya moto, hawatakuwa na msaidizi wala udhuru. Watauma vidole vyao kwa kujutia walivyomuasi Mwenyezi Mungu na Mtume, lakini ‘majuto ni mjukuu.’
Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (25:27).
Na watasema: Mola wetu! Hakika sisi tuliwatii mabwana zetu na wakubwa wetu, wakatupoteza njia. Mola wetu wape adhabu mara mbili, na walaani laana kubwa.
Makusudio ya mabwana na wakubwa ni viongozi wa dini na dunia. Laana ni kufedheheka. Wadhaifu watawageuzia adhabu na watamtaka Mwenyezi Mungu awaongezee adhabu.
Mwenye kuichunguza historia ataona kwamba aghlabu umma wa kijinga unaongozwa na mataghuti na waovu. Lakini watu wenye mwamko na maarifa hawaamini kuweka masilahi yao isipokuwa kwa waaminifu wenye ikhlasi.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:38).
Enyi ambao mmeamini! Msiwe kama wale ambao walimuudhi Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtaksa na waliyoyasema; naye alikuwa ni mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.
Waliomuudhi Musa
ni Wana wa Israil, hilo halina shaka; ambapo walimsifu sifa zisizokuwa za mitume.
Aya hii inaashiria kwamba badhi ya swahaba walimuudhi Mtume mtukufu(s.a.w.w)
na wakambandika mambo asiyokuwa nayo, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawakataza waislamu hilo.
Kuna riwaya inayosema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
siku moja aliapa, basi mtu mmoja katika Answar akasema: “Kiapo hiki hakikusudiwa radhi ya Mwenyezi Mungu.” Hapo uso wa Mtume ukaiva wekundu na akasema:“Amrehemu Musa, hakika aliudhiwa zaidi ya hivi na akasubiri.”
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾
70. Enyi ambao mmeamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni kauli ya sawa.
يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
71. Atawatengenezea matendo yenu na atawaghufiria dhambi zenu. Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amefuzu kufuzu kukubwa.
إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا ﴿٧٢﴾
72. Kwa hakika tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima na vikakataa kuichukua na vikaiogopa, lakini mwanadamu akaichukua. Hakika yeye ni dhalimu mkubwa, mjinga sana,
لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ وَيَتُوبَ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٣﴾
73. Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na washirikina wanaume na washirikina wanawake; na awapokelee toba waumini wanaume na waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
TULIZITOLEA AMANA
Aya 70 – 73
MAANA
Enyi ambao mmeamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni kauli ya sawa. Atawatengenezea matendo yenu na atawaghufiria dhambi zenu.
Kauli ya sawa ni kusema haki na ukweli, bila ya kuficha kitu; hata kama inamuhusu mwenyewe. Makusudio yake hapa ni ile inayowanufaisha watu kwa kulinganisha na kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Atawatengenezea amali zenu;’ ambapo Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejaalia kauli ya haki ni sababu ya matendo mema; kwa mfano kumwongoza aliyepotea kwenye njia ya heri na amani, kumsaidia aliyedhulumiwa kwa neno la usawa au kauli ambayo italeta suluhu baina ya watu wawili na mengineyo yanay- owanufaisha watu kwa namna moja au nyingine.
Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amefuzu kufuzu kukubwa.
Atafuzu duniani kwa kufaulu na kuwa na sera nzuri na katika Akhera atafuzu kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake.
Kwa hakika tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima na vikakataa kuichukua na vikaiogopa, lakini mwanaadamu akaichukua.
Wafasiri wametofautiana kuhusu maana ya amana. Kuna waliosema kuwa ni taklifa na twaa. Wengine wakasema ni tamko la Lailaha illahha (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu). Kuna waliosema ni viungo vya mwanadamu; kama masikio yake, macho yake, mikono yake na miguu yake. Kwamba ni juu yake kuvitumia kwa ajili ya lengo lilioumbiwa. Pia kuna wale waliosema kuwa ni amana katika mali.
Tuonavyo sisi maana yake ni kujitolea muhanga kwa ajili ya manufaa ya jamii, si kwa lololote isipokuwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na ya ubinadamu.
Kwa sababu kujitolea huku ni kuzito na kukubwa kiasi ambacho maumbile yenye nguvu zaidi, kama mbingu, ardhi na majabali yangelikataa kubeba, kama yangelikuwa na hisia.
Kwa hiyo lengo la kutaja mbingu na ardhi ni kuashiria ukubwa wa kuji- tolea huku, na kwamba binadamu ni kiumbe pekee anayeweza kupingana na nafsi yake na matamanio yake.
Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:Hakika yeye ni dhalimu mkubwa, mjinga sana,
maana yake ni kuwa binadamu atajidhulumu yeye mwenyewe na mwingine ikiwa ataifanyia hiyana amana hii na kutojua mwisho muovu utakotokana na hiyana yake hiyo.
Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake
ambao wanajionyesha kuwa wanatekeleza amana, lakini kumbe ni wahaini.
Na washirikina wanaume na washirikina wanawake.
Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa vile kosa la ushirikina haliwezi kufutwa hata na kujitolea muhanga.
Na awapokelee toba waumini wanaume na waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Yaani anawaghufiria wenye kutubia na kuwahurumia wanyonge. Ewe Mwenyezi Mungu mrehemu Muhammad na kizazi chake, rehema ambayo atatuombea nayo siku tutakapohitajia.
MWISHO WA SURA YA THELATHINI NA TATU: SURAT AL-AHZAB