5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
Sura Ya Thelathini na Nne: Surat Saba. Imeshuka Makka. Ina Aya 54.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَهُ الْحَمْدُ فِي الْآخِرَةِ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١﴾
1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na sifa ni zake katika Akhera. Naye ni Mwenye hekima, Mwenye habari.
يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ الرَّحِيمُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾
2. Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda huko na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwingi wa maghufira.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَأْتِينَا السَّاعَةُ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ عَالِمِ الْغَيْبِ لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٣﴾
3. Na walisema wale ambao wamekufuru: Haitatufikia Saa. Sema: Ndio! Naapa kwa Mola wangu, itawafikia. Mjuzi wa ghaibu. Hapana kinachofichikana kwake hata chenye uzito wa chembe, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo katika hivyo wala kikubwa zaidi; ila vimo katika Kitabu chenye kubainisha.
لِّيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٤﴾
4. Ili awalipe wale ambao wameamini na wakatenda mema. Hao watapata maghufira na riziki yenye heshima.
وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مِّن رِّجْزٍ أَلِيمٌ ﴿٥﴾
5. Na wale ambao wamehangaika kuzipinga ishara zetu wakiona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
وَيَرَى الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ الَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ هُوَ الْحَقَّ وَيَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٦﴾
6. Na wale ambao wamepewa ilimu wanaona kuwa uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ni haki na huongoza kwenye njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
SIFA NJEMA ZOTE NI ZA MWENYEZI MUNGU
Aya 1 – 6
MAANA
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na sifa ni zake katika Akhera. Naye ni Mwenye hekima, Mwenye habari.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye kustahiki kusifiwa kwa sifa njema katika nyumba mbili. Ni mmliki wa ulimwengu na mpangiliaji wake kwa vyote vilivyomo ndani yake, kulingana na elimu yake na hekima yake.
Kwenye Nahjul-Balagha, imesemwa: “Tunamsifu kwa ukubwa wa hisani yake na wema wa dalili yake na ziada ya fahila zake na neema zake. Sifa ambazo ni haki yake (sisi) kuzitekeleza na kulipa shukrani zake na kujikurubisha kwenye thawabu zake na kutaka ziada ya wema wake.”
Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda huko na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwingi wa maghufira.
Maana ya Aya hii yamekaririka katika Aya kadhaa; ikiwemo Juz. 7 (6:59) na Juz. Juz. 11 (10:61). Ufupisho wake ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Na walisema wale ambao wamekufuru: Haitatufikia saa ya Kiyama. Sema: Ndio! Naapa kwa Mola wangu, itawafikia.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 11(10:53).
Mjuzi wa ghaibu. Hapana kinachofichikana kwake hata chenye uzito wa chembe, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo katika hivyo wala kikubwa zaidi; ila vimo katika Kitabu chenye kubainisha.
Kitabu chenye kubainisha ni kinaya cha kuhifadhi. Maana ni kuwa hakuna anayejua wakati wa Kiyama isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Tazama Juz. 9 (7:187).
Ili awalipe wale ambao wameamini na wakatenda mema. Hao watapata maghufira na riziki yenye heshima. Na wale ambao wamehangaika kuzipinga ishara zetu wakiona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
Huu ni ubainifu wa hekima ya ufufuo, ambayo ni kulipwa mema waliofanya wema na wale waliofanya uovu walipwe kwa uovu wao. Tazama Juz. 11 (10:3-4). Kifungu cha “Hisabu na malipo ni lazima.”
Na wale ambao wamepewa ilimu wanaona kuwa uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ni haki na huongoza kwenye njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
Makusudio ya wale waliopewa ilimu ni kila mwenye ilimu aliye na insafu, wakati wowote na mahali potepote. Na makusudio ya uliyoteremshiwa ni Qur’an. Maana ni kuwa yeyote mwenye ilimu atakayeisoma Qur’an kiusahihi, lazima ataishia kuwa ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu; kwa sababu iko sawasawa kwenye itikadi yake, sharia yake na mafunzo yake yote.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا هَلْ نَدُلُّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ يُنَبِّئُكُمْ إِذَا مُزِّقْتُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ إِنَّكُمْ لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ﴿٧﴾
7. Na wale ambao wamekufuru walisema: Je, tuwajulishe mtu anayewaambia mtakapocham- buliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya?
أَفْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَم بِهِ جِنَّةٌ بَلِ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ فِي الْعَذَابِ وَالضَّلَالِ الْبَعِيدِ ﴿٨﴾
8. Amemzulia Mwenyezi Mungu au ana wazimu? Bali wale ambao hawaamini akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali.
أَفَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِن نَّشَأْ نَخْسِفْ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ نُسْقِطْ عَلَيْهِمْ كِسَفًا مِّنَ السَّمَاءِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ ﴿٩﴾
9. Je, hawaoni yaliyo mbele yao na nyuma yao ya mbingu na ardhi. Tungelipenda tungeliwadidimiza ardhini, au tungeliwateremshia vipande vya mbingu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa kila mja aliyetubia.
WANAOPINGA SIKU YA MWISHO
Aya 7 – 9
MAANA
Na wale ambao wamekufuru walisema: Je, tuwajulishe mtu anayewaambia mtakapochambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya? Amemzulia Mwenyezi Mungu au ana wazimu?
Hivi ndivyo washirikina walivyomwambia Muhammad, ni muongo au mwendawazimu – Mungu apishie mbali. Kwa nini walisema neno la ukafiri kama hilo? Ni Kwa sababu Mtume aliwaambia kuwa mtu atafu- fuliwa baada ya mauti. Hawana dalili yoyote ya kupinga kwao huku isipokuwa kushangaa tu; kama walivyosema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ ﴿٥﴾
“Amewafanya miungu wote kuwa ni mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu.” (38: 5).
Hali yao hii, kama inavyonekana, inategemea vile wanavyofikiria. Maana yake ni kupinga hali halisi kwa fikra na mawazo; pamoja na kuwa fikra haiwi ya kweli ila ikiwa inaakisi hali halisi na kwamba yeyote anayeikum- batia nadharia yoyote hana budi kutafuta dalili ya ukweli wake kwa kuweko uhalisi unaoitafsiri, na haifai kukana uhalisi kwa fikra isiyokuwa na msingi wowote.
Katika hili Imam Ali
anaashiria kwa kusema:“Watu wanajulikana kwa haki, wala haki haijulikani kwa watu.”
Bali wale ambao hawaamini akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali.
Hao ni wajinga na wapotevu, kwa sababu wameipima haki na uhalisi kwa fikra zao na mawazo yao; na walitakiwa wapime fikra zao kwa haki na uhalisi.
Je, hawaoni yaliyo mbele yao na nyuma yao ya mbingu na ardhi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia wakadhibishaji: Kuna ajabu gani ya kufufuliwa kwenu baada ya mauti:
أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم ﴿٨١﴾
“Kwani aliyeziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao?” (36:81).
Je, umbile hili halifahamishi umoja wake na ukamilifu wa uweza wake; ukiwemo kuwarudisha watu baada ya mauti?
Tumelizungumzia hilo mara nyingi. Tazama Juz. 1 (2:28 -29), Juz. 5 (4:85 – 87) na Juz. 11 (10:3–4).
Tungelipenda tungeliwadidimiza ardhini, au tungeliwateremshia vipande vya mbingu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa kila mja aliyetubia.
Hayo ni ishara ya kuumba mbingu na ardhi. Kwa sabubu hilo, kwa mwenye akili, linafahamisha ukuu wa Mwenyezi Mungu na uweza wake wa kuipa uhai mifupa iliyochakafuka. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:
‘Tungelipenda tungeliwadidimiza ardhini,’ ni karipio na makemeo kwa yule anayepinga siku ya mwisho, kwamba anaweza kumezwa na ardhi au kupigwa na kimondo kutoka mbinguni, kimuunguze.
وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ مِنَّا فَضْلًا يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ وَأَلَنَّا لَهُ الْحَدِيدَ ﴿١٠﴾
10. Na kwa hakika tulimpa Daud fadhila kutoka kwetu. Enyi milima sabihini pamoja naye na ndege. Na tukamlainishia chuma.
أَنِ اعْمَلْ سَابِغَاتٍ وَقَدِّرْ فِي السَّرْدِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١١﴾
11. Kwamba utengeneze nguo za chuma pana na kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika ninayaona mnayotenda.
وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ غُدُوُّهَا شَهْرٌ وَرَوَاحُهَا شَهْرٌ وَأَسَلْنَا لَهُ عَيْنَ الْقِطْرِ وَمِنَ الْجِنِّ مَن يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَمَن يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿١٢﴾
12. Na kwa Suleiman upepo. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamtiririshia chemchem ya shaba. Na katika majini kuna waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na anayejitenga na amri katika wao tunamwonjesha adhabu ya moto unaowaka.
يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾
13. Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na masanamu na sinia kubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyoondoka mahali pake. Fanyeni amali enyi watu wa Daud kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru.
فَلَمَّا قَضَيْنَا عَلَيْهِ الْمَوْتَ مَا دَلَّهُمْ عَلَىٰ مَوْتِهِ إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿١٤﴾
14. Tulipomkidhia mauti, hapana aliyewajulisha mauti yake ila mnyama wa ardhi aliyekula fimbo yake. Alipoanguka majini walitambua lau kuwa wangelijua ya ghaibu wasingelikaa katika adhabu ya kufedhehesha.
DAUD NA SULEIMAN
Aya 10 – 14
MAANA
Na kwa hakika tulimpa Daud fadhila kutoka kwetu. Enyi milima sabihini pamoja naye na ndege. Na tukamlainishia chuma.
Katika Juz. 6 (4:163) Mwenyezi Mungu anasema: “Na Daud tukamapa Zaburi,” kwenye Juz. 19 (27:15) anasema: “Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu” na kwenye Aya hii tuliyo nayo anaseama kuwa amempa neema ya sauti nzuri ambayo ilikuwa inakurubia kwenda sambamba na sauti ya milima na ndege.
Katika Juz. 17 (21:79) tulisema kuwa inawezekana kuwa tasbihi ya milima na ndege ni tasbihi halisi hasa pamoja na Daud, Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kuna msemaji aliyesema kuwa makusudio ya kusabihi milima na ndege pamoja na Suleimani ni kuwa ilikuwa ikimfanya asabihi; alipokuwa akiiona husema: “Subhana man khalaqa wa swawwara...” (Kutakasika ni kwa aliyeumba na akatia sura...).
Pia Mwenyezi Mungu alimneeemesha Daud kwa kukifanya chuma vile anavyotaka yeye bila ya kukitia motoni au kukigonga na nyundo. Inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu alimfahamisha sababu na nyenzo za kukilainisha chuma.
Kwamba utengeneze nguo za chuma pana na kadiria sawa katika kuunganisha.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Daud atengeneze deraya kutokana na chuma na atengeneze vizuri kuzuia panga mishale na mikuki na ziwe pana kwa namna ambayo mvaaji haitamzuia na harakati zozote.
Na tendeni mema. Hakika ninayaona mnayotenda.
Maneno yanaelekezwa kwa Daud na kizazi chake. Mwenyezi Mungu anawaamrisha wafanye mema na kuwa ameayaandalia malipo na thawabu. Umetangulia mfano wa Aya mbili hizi katika Juz. 17 (21:79 – 80).
Na kwa Suleiman upepo. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja.
Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa upepo ulikuwa ukimchukua Suleiman, anakotaka, kwa amri ya Mungu na kwamba masafa ya mwezi mzima kwa ngamia au kutembea kwa miguu alikuwa akienda kwa asubuhi moja na vile vile jioni.
Na tukamtiririshia chemchemi ya shaba.
Makusudio ya kumtiririshia hapa ni kumyeyushia. Yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimyeyushia chuma Suleimani kama alivyomyeyushia baba yake Daud. Inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu alimuongoza kwenye sababu za kuyeyusha.
Na katika majini kuna waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na anayejitenga na amri katika wao tunamwonjesha adhabu ya moto unaowaka. Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na masanamu na sinia kubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyoondoka mahali pake.
Imetangulia pamoja na tafsiri yake katika Juz. 17 (21:82).
Fanyeni amali enyi watu wa Daud kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru.
Ibn Al-arabi ameitaja Aya hii katika Futuhat Juz. 4, akasema: Shukrani ni kuiona neema kuwa imetoka kwa Mungu si kwa mwingine. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimpa wahyi Musa akamwambia: Nishukuru kwa haki ya kushukuru. Akasema Musa: “Ni nani anayeweza hilo ewe Mola?” Akamwambia: “Ikiwa unaona neema imetokana na mimi basi umenishukuru.”
Tulipomkidhia mauti, hapana aliyewajulisha mauti yake ila mnyama wa ardhi aliyekula fimbo yake. Alipoanguka majini walitambua lau kuwa wangelijua ya ghaibu wasingelikaa katika adhabu ya kufedhehesha.
Aliyekidhiwa na mauti ni Suleiman. Mnyama wa ardhi ni mchwa anayekula miti. Maana ni kuwa Suleimani alifikiwa na mauti akiwa ameegemea fimbo yake; akabakia hivyo mpaka muda aliotaka Mwenyezi Mungu, majini na watu wakimwangalia na kumdhania kuwa yuko hai, mpaka pale mchwa walipokula fimbo yake kwa ndani, ikavunjika na Suleiman akaanguka; hapo wote wakajua kuwa amekufa; ikadhihirika kwa watu kuwa majini hawajui ghaibu. Kwa sababu lau wangelijua basi wasingelikuwa katika utumishi wa Suleiman akiwa ni maiti.
Ikiwa baadhi ya yaliyo katika Aya hii yanaonekana, kwa kawaida, ni vigumu kutokea, lakini kiakili inakubalika kutokea. Ndio maana tunayasadiki na kuyakubali; tukiwa tunaamini msingi wa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume(s.a.w.
w
)
wake mtukufu.
Tazama Juz. 3 (3:45 – 51) kifungu cha “Lisilowezekana kiakili na kidesturi.”
KUPINGA FIKRA YA KIDINI
Kutoka na kutajwa majini na mambo yasiyo ya kawaida katika Aya hii, ni vizuri tutaje yaliyoelezwa kwenye kitabu kilichotoka hivi karibuni, kina- choitwa Naqdu lfikri ddiniy. (Kupinga fikra ya kidini).
Hivi sasa tuko katika mwezi wa Novemba 1969. Yamezungumzwa mengi kuhusu kitabu hicho na mtungaji wake. Mwenye kusoma kitabu hicho mara moja atamhukumu mtungaji wake kuwa ana shaka na wasiwasi na dini zote. Hilo amelisema waziwazi kwenye Uk. 29, 77 na nyinginezo.
Lakini mwenye kukifuatilia kitabu na kuchukua dhahiri yake, ataona kuwa yaliyopelekea shaka na wasiwasi huu ni mambo yafutayo:
Kwanza
: Kujaribu baadhi ya waumini kulazimisha kuoanisha nukuu za Qur’an na ugunduzi wa kisayansi, na kuzama sana kuleta taawili iliyo mbali na matamshi. Mtunzi wa kitabu hicho amelitolea ushahidi mwingi hilo, yakiwemo yale aliyoyanukuu katika Uk. 37, kwamba ugunduzi wa chembe za mwanga unafahamisha kuweko malaika na majini.
Mtungaji akielezea kauli hii alisema: “Sijui kuna uhusiano gani baina ya nadharia ya mwanga na kuweko majini.”
Pili
: Mazoweya na nembo za kidini zilizoganda haziendani na maendeleo ya karne ya ishirini; kama anavyodai mwandishi.
Tatu: Baadhi ya wakuu wa dini kuunga mkono ukabaila na ukoloni kwa kutumia jina na Uislamu au Ukristo. Kitabu kimejaa ushahidi wa hilo; kama vile kwenye uk. 23: “Dini huko ulaya ilikuwa rafiki mkubwa wa serikali za kikabaila, hali ambayo inaendelea hadi sasa katika miji mbalimbali, hasa ndani ya miji ya kiarabu na nje, na vile dini inavyoungana moja kwa moja na ukoloni mambo leo unaongozwa na Marekani.”
Mtungaji aliongeza katika kupinga kitabu “Almasihiyya wal Islamu fi Lubnan” (Ukiristo na Uislmu Lebanon) ambacho ni mkusanyiko wa mihadhara ya Lebanon ya mwaka 1965, iliyotolewa na wakuu wa kidini wane: mmoja wa kisunni, mwengine wa kishia na wawili wa kikiristo.
Na wengine wane wa wasiokuwa na dini yoyote, lakini walizungungumza kwa niaba ya dini. Wote wakamwahidi Mwenyezi Mungu kuwa watafanya bidii ya kudumu kuondoa pingamizi zinazowekwa baina ya Uislamu na ukiristo.
Miongoni mwa aliyoyasema mtungaji huyu, katika kuwarudi wale waliotoa ahadi, ni yale yaliyo katika ukurasa wa 64, wa Kitabu chake hicho: “Lengo la kwanza la mihadhara na ahadi hizo ni wakristo kuunga mkono serkali ya Lebanon, kwa vile inawanufaisha wao zaidi kuliko waislamu walio na ufukara sana.
Baadhi ya waislamu nao wanaikubali serikali na kuungana na wakiristo, na kuaiachia serikali usimamizi wote wa kisiasa, kijamii na kiuchumi, si kwa lolote ila ni kwa kuwa wanapata manufaa fulani na faida kutoka serikalini. Kiasi ambacho maovu ya serikali yamesahaulika na kuelekea kwenye nembo ya mshikamano wa wakiristo na waislamu.”
Dalili mkataa kuwa malengo ni masilahi sio mshikamano wa kidini, mwandishi anaiweka wazi kwenye Uk. 60, katika kitabu chake, akisema: “Hakika Uislamu hauikubali Biblia, utatu, mhanga, kusulubiwa Bwana Masih, kuzikwa kwake na kutoka kwake kaburini n.k. Kama ambavyo wakiristo nao hawaikubali Qur’an wala utume wa Muhammad(s.a.w.
w
)
n.k. Sasa hawa wahadhiri na ahadi zao wataondoa vipi pingamizi hizi? Usawa hasa ni kufahamiana na kuelewena Walebanoni kwa uzalendo wao tu na misingi ya ushirikiano kwa masilahi yao, lakini dini aachiwe hiyari kila mtu kulingana na alivyokinai na mazoweya yake.”
Kutokana na kauli ya mwandishi huyu na wengineo wengi, katika kupinga fikra ya dini, inatubainikia kuwa siri ya upinzani wao, kama tulivyodokeza mwanzoni, imetokana na wakuu wa dini kuukumbatia ukoloni, udhalimu na ukandamizaji na kuupamba kwa jina la dini.
Lau wakuu wote wa dini wangeifanyia ikhlasi, wakaifahamisha kwa ufahamu sahihi na wakaibanisha kama alivyoiteremsha Isa na Muhammad na wasiiuze kwa thamani ndogo, basi wapinzani au washambulizi wa kulipwa wasingelipata mwanya wa kuituhumu au kuwa na shaka na dini ya kiislamu wala ya kikiristo.
Lakini jambo la kuvunja moyo ni kuwa watu wamelitumia jina la dini kwa uzushi na wengine wakasimama kuiharibu na kuingiza shaka baada ya kulipwa na maadui wa Mwenyezi Mungu; ndio ikawa radiamali hii kuto- ka kwa mwandishi huyu wa kitabu ‘Kupinga fikra ya dini’ na wengineo. Inasemekana pia mwandishi huyu ni katika wanaolipwa.
Hata hivyo, kwani dini itakuwa imekosea nini ikituhumiwa na wazushi na wenye upendeleo? Ilitakikana mwandishi aangalie ushahidi mwingi ulio katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na suna za Mtume wake na pia katika historia ya Uislamu kuwa dini ni nguvu inayomwelekeza mtu kwenye maisha bora na kwamaba iko mbali na kila jambo lisiloingilika akilini na kugongana na hakika ya maisha.
Hakika hii wanakubaliana nayo wataalamu wengi wa mashariki na wa magharibi wasiokuwa waislamu. Tazama Juz. 1 (2:1-5) kifungu cha ‘Qur’an na Sayansi,’ Juz. 9 (8:24) kifungu cha ‘Dini na maisha,’ na Juz. 15 (17:9-12) kifungu cha ‘Uislamu ni dini ya maumbile.