9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
Sura Ya Thelathini na Tano: Surat Fatir. Imeshuka Makka. Ina Aya 45.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾
1. Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili, tatu tatu na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.
مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾
2. Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hakuna wa kuizuia na anayoizuia hakuna wa kuiachia isipokuwa Yeye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾
3. Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Je, yuko muumba mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayewapa riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana Mola ila Yeye basi mnageuzwa wapi?.
SIFA NJEMA NI ZA MWENYEZI MUNGU
Aya 1 – 3
MAANA
Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili, tatu tatu na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.
Mwenyezi Mungu amejisifu Yeye mwenyewe ili atufundishe jinsi ya kumsifu na kumshukuru. Aya inafahamisha kuwa katika Malaika kuna walio na mbawa mbili, wenye tatu na wenye nne na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu huzidisha mbawa vile atakavyo. Haya na yanayofanana nayo yanaafikiana na uwezo wa Mwenyezi Mungu na akili haiyakatai. Yasiyokuwa hayo tunamwachia Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa vile sisi hatutaulizwa wala hayana uhusiano wowote na maisha yetu, wala hayana dalili na Aya au Hadith mutawatir.
Ninahofia wale wanaolazimisha kuzifanyia taawili nukuu za dini ziende sambamba na elimu ya kisasa waseme kuwa mbili mbili ni ishara ya ndege yenye injini mbili, tatu tatu ni yenye tatu, nne nne ni yenye nne na kuzidisha katika kuumba ni kuwa ndege zitakazokuja baadaye zenye injini nyingi.
Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hakuna wa kuizuia na anayoizuia hakuna wa kuiachia isipokuwa Yeye, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Makusudio ya rehema hapa sio mali tu; kama walivyosema baadhi ya wafasiri. Wala sio mali, afya na cheo; kama walivyosema wengine. Kwani mali inapelekea uasi na ukandamizaji. Tumewaona wengi wenye mali wamewageuza wengine wanyonge kuwa ni mashirika wanayoyamiliki na kuwageuza kuwa ni watumwa wao wanaowatumikia au wawe wakimbizi.
Afya nayo inampelekea mtu kwenye hatari. Ama cheo, ndio kabisa, aghlabu kinakuwa ni chombo cha dhulma na uadui. Elimu nayo mara nyingine inakuwa ni afadhali ujinga; kama vile elimu iliyotengeneza bomu la nyukilia na silaha za maangamizi.
Hapana! Makusudio ya rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika Aya hii, sio mali peke yake, wala afya pekee yake wala sio cheo na elimu tu. Isipokuwa makusudio ni huruma ya Mwenyezi Mungu, mwongozo wake wa heri na kinga yake ya shari.
Imam Ali
anasema:“Shida inapofika kikomo huja faraja na inapokaza sana minyororo ya dhiki hupatikana raha.”
Mara nyingi tumeshuhudia matatizo madogo yanazidi kuwa makubwa kila mwenyewe anavyojitahidi kuyatatua, na tunaona yale makubwa yanatatu- ka kwa wepesi au kwa haraka. Hakuna siri ya hilo ila matakwa ya Mwenyezi Mungu na rehema yake. Amesema kweli aliyesema: “Mtu anaweza kulala kwenye miba, pamoja na rehema ya Mwenyezi Mungu, akaamka kwenye tandiko. Na anaweza kulala kwenye hariri bila ya rehe- ma ya Mwenyezi Mungu akaamka kwenye miba.”
.
Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Je, yuko muumba mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayewapa riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana Mola ila Yeye basi mnageuzwa wapi?
Ukumbusho huu wa neema ya Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye peke yake ndiye muumba na mwenye kuruzuku ni kuisisitiza Aya iliyotangulia: ‘Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu...’
Katika Nahjul-Balagha imeelezwa:“Mara ngapi Mwenyezi Mungu amewahusisha na neema yake na akwaunganisha na rehema yake. Mmekuwa uchi akawasitiri, mkafanya ya kuwaadhibu akawapa muda. Basi zikamilisheni neema za Mwenyezi Mungu kwa kuwa na subira ya kumtii na kujiweka mbali na maasi, kwani hakika kesho kuanzia leo ni karibu.”
وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٤﴾
4. Na kama wakikukadhibisha, basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ فَلَا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَلَا يَغُرَّنَّكُم بِاللَّـهِ الْغَرُورُ ﴿٥﴾
5. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Basi yasiwadanganye maisha ya dunia, wala mdanganyifu asiwadanganye juu ya Mwenyezi Mungu.
إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿٦﴾
6. Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa motoni.
الَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿٧﴾
7. Wale ambao wamekufuru watakuwa katika adhabu kali na wale ambao wameamini watapata maghufira na malipo makubwa.
أَفَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا فَإِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٨﴾
8. Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema - basi hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoa amtakaye. Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.
WALIKADHIBISHWA MITUME KABLA YAKO
Aya 4 – 8
MAANA
Na kama wakikukadhibisha, basi wamekwisha kadhibishwa Mitume kabla yako na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu,
amlipe thawabu muumini mwenye kusubiri katika jihadi yake na amuadhibu mwenye kuikadhibisha haki kwa sababu ya kukadhibisha kwake.
Lengo la Aya hii ni kumpoza Mtume(s.a.w.
w
)
na kuwakaripia mahasimu na maadui wake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 ( 3:183) na Juz. 17 (22:42).
Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Basi yasiwadanganye maisha ya dunia, wala mdanganyifu asiwadanganye juu ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya ahadi hapa ni hisabu na malipo baada ya mauti. Udanganyifu wa dunia ni mali, jaha, wanawake, watoto na udanganyifu wa shetani. Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (31:33).
Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa motoni.
Shetani ametangaza waziwazi uadui wake na binadamu kwa kusema: “Kwa ulivyonipoteza, basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote.” Juz. 14 (15:39).
Kundi lake ni wale wafuasi wake wanaosikiliza wasiwasi wake na udanganyifu wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuhadharisha kumtii, kwa sababu mwito wake ni wa ufisadi na wa maangamizi, na Mwenyezi Mungu anatoa mwito wa kheri na rehema.
Wale ambao wamekufuru watakuwa katika adhabu kali na wale ambao wameamini watapata maghufira na malipo makubwa.
Kila mtu atakuwa na mwisho, mtamu au mchungu. Mwisho wa mwenye kukufuru na akafanya ufisadi ni Jahannam, makazi maovu; na mwisho wa mwenye kuamini na akatenda mema ni Pepo ambayo ni raha ya daima.
Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema.
Kinahaw, hapa kuna maneno ya kukadiriwa kuwa: ‘ni kama ambaye hakupambiwa’ Hakuna mtu yoyote anayeishi bila ya falsafa na kuchukulia mfano wa juu; hata wale wanaokataa falsafa na mfano, huko kukataa kwao ndio falasafa yao na mfano wa juu. Ndio maana ikasemwa: Mwenye kukataa falsafa ndio amekuwa na falsafa.
Tofauti ni kuwa kuna yale anayeijengea falsafa yake kwenye majaribio na uchambuzi, mwengine anaijengea kwenye akili au dini na kuna yale anayeijengea kwenye dhati yake, mapendeleo yake na kupinga mengine yote.
Hafanyi utafiti wala kufikiri au kufanya uchambuzi, kwa sababu haamini akili wala dini; hakuna kitu isipokuwa kilicho kwenye rai yake na mapendeleo yake.
Mtu wa aina hii anaangalia nafsi zake kuwa ndio kipimo pekee cha haki heri na usawa, na kwamba yeye siku zote yuko sawa, hana upungufu wala hakosei.
Huyu tunaweza kumwita shahidi wa upumbavu na mwenye ghururi ya kuua. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwashiria mtu huyu, katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: “Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo?” Juz. 16 (18:103) Nyingine ni:
وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ ﴿١١﴾ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَـٰكِن لَّا يَشْعُرُونَ ﴿١٢﴾
“Na wanapoambiwa msifanye ufisadi katika ardhi husema, Hakika sisi ni watengezaji tu. Ehe! Hakika wao ndio wafisadi, lakini hawatambui.” Juz. 1 (2:11-12).
Basi Hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoa amtakaye.
Hii ni sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu iliyotangulia ‘Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona ni jema.’ Yaani kwamba Mwenyezi Mungu amemuweka kwenye upotevu na mwisho mbaya kwa sababu amefuata njia inayopelekea hilo; sawa na alivyomuweka kwenye kifo mwenye kunywa sumu na kufa maji aliyejitia baharini akiwa hajui kuogelea.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:27) na Juz. 14 (16:93).
Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.
Usisikitike wala usihuzunike, ewe Muhammad, kwa wale ambao hawakuitikia mwito wako madamu wamefuata wenyewe njia ya uovu na ya maangamizi. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti mambo yao, madogo na makubwa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:2).
وَاللَّـهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا كَذَٰلِكَ النُّشُورُ ﴿٩﴾
9. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndio kama hivyo kufufuliwa.
مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾
10. Mwenye kutaka enzi basi enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu. Kwake hupanda neno zuri na amali njema huuinua. Na wanaopanga njama za maovu watapata adhabu kali, na njama za hao zitaangamia.
وَاللَّـهُ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿١١﴾
11. Na Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na udongo. Kisha tone, kisha akawafanya aina kwa aina. Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai ila kwa elimu yake. Wala hapewi umri mwenye umri mrefu wala hapunguziwi umri wake, ila yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
AMALI NJEMA HUIPANDISHA
Aya 9 – 11
MAANA
Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndio kama hivyo kufufuliwa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:57).
Mwenye kutaka enzi basi enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu.
Enzi ni ya Mwenyezi Mungu na ya dini ya Mwenyezi Mungu hasa; na kwa mawili hayo ndio binadamu anakuwa na enzi. Mwenye kujienzi kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu atadhalilika. Ibn Arabi katika kitabu Futuhatul-Makkiyya, anasema:
“Enzi ya haki hasa ni kuwa hakuna Mola ila Yeye, na enzi ya Mtume wake ni kwa Mwenyezi Mungu, na enzi ya waumini ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi yanathibiti kwenye tanzu yale yaliyonayothibiti kwenye asili.”
Kudhalilika kwa waislamu leo kumetokana na kuwa wao wanajienzi kwa usiokuwa Uislamu. Hapo mwanzo walikuwa ni wachache kuliko sasa, lakini walikuwa ni wengi kwa kujienzi na jamii na umoja wao dhidi ya adui wa Mwenyezi Mungu na adui wao.
Kwake hupanda neno zuri na amali njema huiinua.
Kupanda maneno na kuinuka matendo kwenda kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kinaya cha kuyakubali na kuyalipa thawabu. Maneno mazuri ni yale yanayonufaisha, na vile vile amali njema.
Aya inaashiria kwamba sababu ya kuenziwa na kutukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kauli na vitendo vinavyowanufaisha watu.
Na wanaopanga njama za maovu watapata adhabu kali, na njama za hao zitaangamia.
Kupanga njama za maovu ni kupanga kuwaudhi waumini na viongozi wema. Lakini njama zao zitaambulia patupu. Maana ya Aya hii ni kama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).
Kisha akawafanya aina kwa aina,
mweusi na mweupe na mume na mke.Na mwanamke yeyote hachukui mimba wala hazai, ila kwa elimu yake,
kwa sababu yeye amekizunguka kila kitu.
Wala hapewi umri mwenye umri mrefu wala hapunguziwi umri wake, ila yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
Kupunguziwa umri ni kuwa na umri mfupi; na kuwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kuwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu. Maana kwa ujumla ni kuwa umri wote uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Katika Nahjul-Balagha imeelezwa:
“Hampati neema katika dunia ila ni kwa kuimaliza nyingine; wala hapati umri mwenye umri miongoni mwenu ila ni kwa kuumaliza mwingine.” Tazama Juz. 4 (3:144 – 148) kifungu cha ‘Ajali haina kinga’.