TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Juzuu 21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 27171
Pakua: 4453


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 32 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 27171 / Pakua: 4453
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Juzuu 21

Mwandishi:
Swahili

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

وَمَا يَسْتَوِي الْبَحْرَانِ هَـٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ سَائِغٌ شَرَابُهُ وَهَـٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ وَمِن كُلٍّ تَأْكُلُونَ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُونَ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا وَتَرَى الْفُلْكَ فِيهِ مَوَاخِرَ لِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢﴾

12. Na bahari mbili haziwi sawa; hii ni tamu mno, kinywaji chake kinateremka uzuri, na hii ni chumvi sana. Na kutokana na zote, mnakula nyama freshi. Na mnatoa humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ ﴿١٣﴾

13. Anauingiza usiku katika mchana na anauingiza mchana katika usiku. Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, ufalme ni wake. Na wale mnaowaomba badala yake hawamiliki hata utando wa kokwa ya tende.

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

14. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu. Na wakisikia hawajibu. Na siku ya Kiyama watakataa shirki yenu. Na hapana atakayekuambia kama Yeye mwenye habari.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾

15. Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍ جَدِيدٍ ﴿١٦﴾

16. Akitaka atawaondoa na alete viumbe wapya.

وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ بِعَزِيزٍ ﴿١٧﴾

17. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si gumu.

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ إِنَّمَا تُنذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَمَن تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿١٨﴾

18. Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Na kama aliyelemewa akiomba achukuliwe mzigo wake, hautachukuliwa hata kidogo, ingawa ana ujamaa. Hakika unawaonya wale tu wanaomcha Mola wao kwa ghaibu na wakasimamisha Swala. Na anayejitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

BAHARI MBILI HAZIWI SAWA

Aya 12 – 18:

MAANA

Na bahari mbili haziwi sawa; hii ni tamu mno, kinywaji chake kinateremka uzuri, na hii ni chumvi sana.

Aya hii ni miongoni mwa Aya za kilimwengu, inayoashiria aina za maji tamu na chumvi. Kutofautiana huku, hata kukitegemezwa moja kwa moja kwenye sababu zake za kimaumbile, lakini bado sababu hizo zinakomea kwa muumba wa ulimwengu na mbunifu wake.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (25:53).

Na kutokana na zote, hizo bahari mbili,mnakula nyama freshi [4] ; kama samaki.

Na mnatoa humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.

Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 14 (16:13).

Anauingiza usiku katika mchana na anauingiza mchana katika usiku.

Sayari zinazunguka na nyingine zinazunguka kando kando ya nyingine, na kupatikana vipindi. Wakati mwingine mchana unachukuliwa kutoka kwenye usiku na kipindi kingine usiku unachukuliwa kutoka mchana. Nidhamu hii ya hali ya juu inayoendela katika mamilioni ya miaka ni dalili mkataa wa kuweko mpangiliaji mwenye hekima wa ulimwengu huu; sawa na kinavyofahamaisha chombo kinachotekeleza kazi iliyotakiwa, kuwa kuna aliyekitengeneza na kukipangilia vizuri.

Sadfa inakuwa ni batili katika hukumu ya kukaririka; yaani sadfa haiwezi kukaririka.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:27).

Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa.

Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 13: (13:2).

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, ufalme ni wake. Na wale mnaowaomba badala yake hawamiliki hata utando wa kokwa ya tende.

Utando wa kokwa ya tende ni kinaya cha vitu vilivyo duni zaidi. Maana ni kuwa mambo haya ya kustaajabisha yaliyo dhahiri mnayoyaona katika ulimwengu huu, ni katika matengenezo ya Mwenyezi Mungu, na wale manowabudu na kuwatarajia badala ya Mwenyezi Mungu, hawana wala hawezi chochote.

Mkiwaomba, wakiwa hawana hisia wala utambuzi, kama vile mawe na miti,hawasikii maombi yenu. Na wakisikia , wakiwa ni watu, majini au malaika,hawajibu, kwa vile wao wenyewe hawawezi kujinufaisha wala kujizuilia na madhara, itakuwaje waweze kuwasaidia wengine.

Na siku ya Kiyama watakataa shirki yenu.

Watajitenga na ushirikina na upotevu.

Na hapana atakayekuambia kama Yeye mwenye habari ya mwisho wa hawa wanaokadhibisha utume wako, na wengineo katika waasi, ewe Muhammad.

Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

Mahitaji ya muumbwa kwa muumba wake hayakatiki milele; kama mahitaji ya sababu kwa msababishi wake.

Ibn Al-arabi anasema katika Kitabu Futahitul- Makkiya: “Mtu ana pande mbili: upande mmoja anamuhitajia Mwenyezi Mungu na upande mwingine anajitosheleza na ulimwengu. Kwa hiyo yeye ni dhalili muhitaji kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mwenye kujitosheleza kwa yule anayetosheka naye.”

Akitaka atawaondoa na alete viumbe wapya. Na hilo, la kuwamaliza waasi na kuwaleta watiifu,kwa Mwenyezi Mungu si gumu.

Lau Mwenyezi Mungu (s.w.t) akitaka lolote linakuwa tu, kwa sababu Yeye ni Muweza wa kila kitu.

Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 13 (14: 19 – 20). Vile vile Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:133) na Juz. 8 (6:133).

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.

Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 8 (6:164).

Kila mwenye dhambi atahisabiwa na kuadhibiwa kwa madhambi yake tu, lakini Taurat imeeleza kinyume: “Bwana ni mpole... mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao...” (Hesabu 14:18).

Na kama aliyelemewa akiomba achukuliwe mzigo wake, hautachukuliwa hata kidogo, ingawa ana ujamaa.

Aliyelemewa ni yule mwenye mzigo wa madhambi. Maana ni kuwa siku hiyo hakutafaa kunyenyekea wala kuomba msaada kwa ndugu au mpenzi, kwa sababu kila mtu atajishughulikia mwenyewe:

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾ وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾ وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾

“Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye na mama yake na baba yake na mkewe na wanawe. Kila mtu siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.” (80:34 – 37).

Hakika unawaonya wale tu wanaomcha Mola wao kwa ghaibu na wakasimamisha Swala.

Wanaoitikia mwito wako, ewe Muhammad ni wale tu wanaomwogopa Mwenyezi Mungu na kutarajia thawabu zake. Ama wale wasiomwamini wala kuamini siku ya mwisho, maonyo na nasaha haziwafai chochote.

Na anayejitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake.

Hii ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٤٦﴾

“Mwenye kutenda mema ni kwa ajili ya nafsi yake na mwenye kutenda uovu ni juu yake. Na Mola wako si Mwenye kuwadhululumu waja” (41:46)

Katika Nahju-Balagha imeelezwa: “Ihisabu nafsi yako, kwani nafsi nyingine ina wa kuihisabu asiyekuwa wewe.”

Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu, Ampe thawabu mwenye kuamini na akatenda mema na amwadhibu mwenye kufanya ufisadi na uovu.

وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ ﴿١٩﴾

19. Hawi sawa kipofu na mwenye kuona.

وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ ﴿٢٠﴾

20. Wala giza na nuru.

وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ ﴿٢١﴾

21. Wala kivuli na joto.

وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاءُ وَلَا الْأَمْوَاتُ إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ ﴿٢٢﴾

22. Na hawawi sawa walio hai na walio maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.

إِنْ أَنتَ إِلَّا نَذِيرٌ ﴿٢٣﴾

23. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ ﴿٢٤﴾

24. Hakika sisi tumekutuma kwa haki, uwe mbashiri na mwonyaji. Na hakuna umma wowote ila alipita humo muonyaji.

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ وَبِالزُّبُرِ وَبِالْكِتَابِ الْمُنِيرِ ﴿٢٥﴾

25. Na kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibisha wale waliokuwa kabla yako. Waliwajia Mitume wao kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na kwa kitabu chenye nuru.

ثُمَّ أَخَذْتُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٢٦﴾

26. Kisha nikawakamata wale waliokufuru; basi je, kulikuwaje kukanya kwangu?

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ ثَمَرَاتٍ مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهَا وَمِنَ الْجِبَالِ جُدَدٌ بِيضٌ وَحُمْرٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهَا وَغَرَابِيبُ سُودٌ ﴿٢٧﴾

27. Je, huoni kuwa tumeteremsha kutoka mawinguni maji kutoka mbinguni na kwayo tumetoa matunda yenye kuhitalifiana rangi. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbalimbali na myeusi.

وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴿٢٨﴾

28. Na katika watu na wanyama na wanyama howa pia rangi zao zinahitalifiana. Hakika si mengineyo wanaomcha Mwenyezi Mungu, katika waja wake ni wale wajuzi Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye maghufira.

HAWI SAWA KIPOFU NA MWENYE KUONA

Aya 19 – 28

MAANA

Hawi sawa kipofu na mwenye kuona, wala giza na nuru, wala kivuli na joto. Na hawawi sawa walio hai na walio maiti.

Makusudio ya kipofu ni yule mwenye kuacha njia ya haki na ya uongofu; kinyume chake ni mwenye kuona. Giza ni ujinga na upotevu, na nuru ni elimu na uongofu. Kivuli ni neema na joto ni moto wa Jahannam. Ama walio hai ni wale walio na nyoyo zinazosikia mazuri na zikayafuata; kinyume chao ni wafu.

Maana ni kuwa hawi sawa, mbele ya Mwenyezi Mungu na kihali halisi ilivyo, mwenye kuamini akafanya matendo mema na yule mwenye kukufuru akafanya ufisadi. Bali tofauti baina yao ni sawa na tofauti baina ya kipofu na mwenye macho, mwanga na giza, kivuli na joto na mauti na uhai.

Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.

Maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu yanaathiri na kufanya kazi katika nafsi za wale wanaotafuta haki kwa ajili ya haki na kuisikiliza kwa ajili ya kutaka kuifanyia kazi.

Ama wale ambao hakuna linalowashtua isipokuwa masilahi yao wala hawafanyi lolote isipokuwa masilahi, wao hawasikilizi maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala Yeye, ambaye imetukuka hekima yake, hawasukumi kwenye uongofu. Vinginevyo zitabatilika thawabu na adhabu.

Hakika sisi tumekutuma kwa haki, uwe mbashiri na mwonyaji.

Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.), kwa hoja za kutosheleza, kulingania kwenye haki na kuwa shahidi kwa viumbe. Basi akafikisha ujumbe kwa ukamilifu na akawa ni rehema kwa viumbe wote, hasa waarabu; pale alipowatoa kwenye ujinga wa wajinga na kuwapeleka kwenye nuru ya Uislamu na karama yake.

Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 11 (10:42) na Juz.20 (27:80).

KILA UMMA UNA MTUME

Na hakuna uma wowote ila alipita humo muonyaji.

Katika Qur’an kuna Aya zinazofahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuma Mtume kwa kila umma; miongoni mwa Aya hizo ni hizi zifuatazo:

Aya hii tuliyo nayo.

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ ﴿٤١﴾

“Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi.” Juz. 5 (4:41).

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا ﴿٣٦﴾

“Na kwa hakika tulimtuma Mtume kwa kila umma.” Juz. 14 (16:36).

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ ﴿٤٧﴾

“Na kila Umma una Mtume.” Juz. 11 (10:47).

Kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾

“Naapa kwa Mola wako tutawauliza wote Juz. 14 (15:92)

Na pia kauli yake:

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى ﴿٣٦﴾

“Hivi anadhani mtu kuwa ataachwa bure?” (75:36)

Sio mbali kuwa makusudio ya mjumbe, muonyaji na shahidi ni kila linalosimamia hoja na kukata nyudhuru, liwe limetoka kwa Nabii, Mtume, Kitabu cha dini, kiongozi mwema au hukumu ya akili ya kimsingi, isiyopingika na wenye akili salama na umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu; kama ubaya wa dhulma na hiyana, na uzuri wa uadilifu na uaminifu n.k. Wala hatujui umma ulioishi kwa vurugu bila nidhamu na kumwachia kila mtu afanye atakavyo bila ya kumhisabu kwa kauli na vitendo.

Unaweza kuuliza : Je, hii haipingani na kauli yake Mwenyezi Mungu, iliyo katika Juzuu hii: “Wala hatukuwatumia muonyaji kabla yako.” (34:44). Ambapo Aya tuliyo nayo inathibitisha kuwa kila kaumu ina muonyaji na ya pili inakataa kuwa kaumu ya Muhammad(s.a.w. w ) ilikuwa na muonyaji kabla yake?

Jibu : Muonyaji katika Aya tuliyo nayo inachanganya kila muonyaji awe mtume au la. Ama katika Aya ya pili inahusuiana na Mtume. Kwa hiyo hakuna kupingana baina ya Aya mbili na maana ni kuwa kaumu ya Muhammad(s.a.w. w ) hawakujiwa na Mtume kabla ya kutumwa yeye, lakini walijiwa na muonyaji wa akili na maumbile; nayo ni muonyaji tosha wa kuwapa hoja; hasa katika kuabudu kwao mawe.

Ndio maana Mtume(s.a.w. w ) alikuwa akiwajadili kwa mantiki ya akili na kuwaambia:

قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَاللَّـهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٧٦﴾

“Sema: Je, mnamwabudu badala ya Mwenyezi Mungu, ambaye hawezi kuwadhuru wala kuwanufaisha? Juz. 6 (5:76).

Na kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibisha wale waliokuwa kabla yako. Waliwajia Mitume wao kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na kwa kitabu chenye nuru.

Makusudio ya maandiko hapa ni hikima na mawaidha. Kitabu chenye nuru ni Tawrat iliyoteremshwa kwa Musa, Injil iliyoteremshwa kwa Isa na vitabu vinginevyo vilivyotermshwa kabla ya Mtume wa mwisho. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:184).

Kisha nikawakamata wale waliokufuru; basi je, kulikuwaje kukanya kwangu?

Makusudio ya kukanya hapa ni adhabu. Yaani Mwenyezi Mungu aliwakanya kwa kauli na vitendo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:44) na Juzuu hii tuliyo nayo (34:45).

Je, huoni kuwa tumeteremsha kutoka mawinguni maji kutoka mbinguni na kwayo tumetoa matunda yenye kuhitalifiana rangi na ladha yake na harufu yake.

Hakuna mwenye shaka kwamba kutoafautiana huku kunatokana na sababu za kimaumbile, lakini zote hizi zinaishia kwa muumba wa hayo maumbile. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:4) katika kifungu cha ‘Sayyid Afghani na wanaomkana Mungu.’

Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbalimbali na myeusi.

Anasema, mkuu wa wasemaji, kwamba Yeye amefanya kwenye majabali njia; kuna nyeupe, nyekundu na nyingine ni nyeusi. Kila moja katika njia hizo tatu inatofautiana rangi.

Mazingatio katika kutofautiana huku ni kufahamisha juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na matakwa yake; sawa na tofauti ya matunda.

Na katika watu na wanyama na wanyama howa pia rangi zao zinahitalifiana.

Kuunganisha wanyama na wanyama hoa, ni katika kuunganisha maalum kwenye ujumla, kwa sababu neno lililotumika kwa wanyama, Dawab, lina maana ya wanaotemebea ardhini, wakiwemo wanyama howa (mifugo) ambao ni ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi.

Maana ni kuwa kutofautiana rangi za watu na kutofautiana wanyama, kunafahamisha uweza wa Mwenyezi Mungu; sawa na kutofautiana matunda na njia.

Hakika si mwengineyo wanaomcha Mwenyezi Mungu, katika waja wake ni wale wajuzi.

Makusudio ya wenye ujuzi hapa ni wale walioamini kwa kujua, sio kwa kuiga, na wakaujua utukufu wake kwa dalili na hoja.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kujua uweza wa asiyeshindwa na kitu wala kupitwa na kitu, hawezi kuacha kumuogopa; ndio maana wanaomjua Mwenyezi Mungu ndio wanaohofia zaidi hasira za Mwenyezi Mungu na ndio walio na matarajio zaidi ya fadhila na msamaha wake.

Sisi ni katika wale wanaoamini kuwa hakuna imani ya kweli bila ya takua wala hakuna takua bila ya mwamko. Ndio maana Mtume mtukufu(s.a.w. w ) akasema: “Ubora wa mjuzi juu ya mwenye kuabudu ni ubora wa mwezi usiku kwenye nyota.” Pia kuna Hadith mashuhuri ya Mtume(s.a.w. w ) :“Usingizi wa mwenye ujuzi ni bora kuliko ibada ya mjinga.”

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye maghufira.

Mwenye nguvu katika kuwawaadhibu wenye kupituka mipaka na kufanya dhulma, na ni mwenye maghufira kwa mwenye kutubia na kurejea.

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾

29. Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Swala, na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika tuliyowapa, wanataraji biashara isiyoangamia.

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾

30. Ili awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani.

وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ هُوَ الْحَقُّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ إِنَّ اللَّـهَ بِعِبَادِهِ لَخَبِيرٌ بَصِيرٌ ﴿٣١﴾

31. Na yale tuliyokupa wahyi kutoka Kitabuni ni haki yenye kusadikisha yaliyokuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ ﴿٣٢﴾

32. Kisha tumewarithisha Kitabu wale ambao tumewachagua katika waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ ﴿٣٣﴾

33. Mabustani ya milele watayaingia. Humo watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na mavazi yao humo ni hariri.

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٤﴾

34. Na watasema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) ambaye ametuondoloea huzuni. Hakika Mola wetu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani.

الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِن فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ ﴿٣٥﴾

35. Ambaye ametuweka katika nyumba ya kukaa, humo haitugusi tabu wala humo hakutugusi kuchoka.

ALIYEJIDHULUMU, ALIYE KATIKATI, NA ALIYETANGULIA KWENYE KHERI

Aya 29 – 35

MAANA

Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasi- mamisha Swala, na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika tuliyowapa, wanataraji biashara isiyoangamia.

Makusudio ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni Qur’an Tukufu. Kusoma ni kuzingatia maana yake na kuyatumia. Kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu.... ‘iliyokuja baada ya kauli yake: ‘Hakika si mengineyo wanaomcha Mwenyezi Mungu, katika waja wake ni wale wajuzi.’ Inaashiria hivyo.

Katika Nahjul-Balagha kuna maelezo:“... Katika zama hizo hakutakuwa na kitu kisichokuwa na thamani zaidi kuliko kusomwa Qur’an inavyopaswa kusomwa kwake. Wala hakutakuwa na kitu kilicho na thamni zaidi kuliko Qur’an kutowekwa mahali pake.”

Maana ya Aya ni kuwa wale ambao wanazingatia Qur’an na wakatumia hukumu zake, wakikusudia radhi ya Mwenyezi Mungu, basi watakuwa wamepata faida kwenye biashara yao na watakuwa ni wenye kufuzu.

Amesema tena kwenye Nahjul-Balagha:“ Na wameuza machache kati- ka dunia hii isiyodumu kwa mengi ya akhera isiyoisha.”

Ili awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fad- hila zake. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani.

Waliamini na wakamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu, kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, thawabu zake, msamaha wake na rehema zake, na wakapata waliyoyataka.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:274) na Juz. 13 (13:22).

Na yale tuliyokupa wahyi kutoka Kitabuni ni haki.

Makusudio ya Kitabu ni Qur’an ikiwa inachukua dalili na hoja za ukweli wake na uhakika wake; ambazo ni hukumu zake na mafundisho yake yanayoipa kipaumbele imani ya uadilifu wa Mwenyezi Mungu na umoja wake na heshima ya mtu na uhuru wake.

Yenye kusadikisha yaliyokuwa kabla yake katika vitabu na sharia zinazosimama kwenye misingi hii – misingi ya kumwamini Mwenyezi Mungu na utu.

Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona yale yaliyo na masilahi kwao na yaliyo na ufisadi. Anawaamrisha lile na kuwakataza hili. Lakini Waislamu wameacha yaliyoamrishwa na Qur’an na wakafanya waliyokatazwa nayo. Wamesadikisha aliyoyasema Mtume mtukufu(s.a.w. w ) aliposema:“Utakuja wakati kwa umma wangu watakataza mema na kuamrisha maovu.” Kwa hiyo si ajabu kusalitika na viumbe waovu.

Kisha tumewarithisha Kitabu wale ambao tumewachagua katika waja wetu.

Makusudio ya Kitab ni Qur’an, hilo halina shaka yoyote; isipokuwa wafasiri wametofautiana katika makusudio ya waliochaguliwa. Wengi wakasema ni umma wa Muhammad(s.a.w. w ) .

Tuonavyo sisi ni Muhammad(s.a.w. w ) , Ahlu bayti wake, maswahaba wake na maulama wa umma wake wanaokwenda na sera yake na wakatumia sunna yake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hawezi kuwachagua isipokuwa wenye takua walio wema.

Qur’an Tukufu imelitumia neno hili kwa maana haya katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni:

إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِيمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿٣٣﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na watoto wa Ibrahim na watoto wa Imran juu ya walimwengu wote.” Juz. 3 (3:33).

Ama dhamiri katikakati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, inarudia neno waja wetu, kwa vile ndilo lililo karibu.

Mwenye kujidhulumu ni yule ambaye maovu yake yamekuwa makubwa kuliko mema yake. Aliyetangulia katika heri ni ambaye mema yake yamekuwa makubwa kuliko maovu yake; hasa yule ambaye hana maovu. Aliye katikati ni ambaye mema yake na maovu yake yamekuwa sawa.

Hiyo ndiyo fadhila kuu. Mabustani ya milele watayaingia. Humo watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na mavazi yao humo ni hariri.

‘Hiyo’ ni hiyo hali ya kurithi na kuchaguliwa. Mabustani ya milele na kuendelea, ni ubainifu wa hiyo fadhila kuu ambayo ameifanya ni malipo ya wale aliowachagua.

Dhahabu, lulu na hariri ni ibara nyingine ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ﴿٧١﴾

“Humo vitakuwemo ambavyo nafsi inavipenda na macho yanavifurahia.” (43:71).

Kuna Hadith kuwa bedui mmoja alimuuliza Mtume: “Je, Peponi kuna samai, yaani nyimbo? Mtume(s.a.w. w ) akasema: “Ndio.”

Na watasema:, sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) ambaye ametuondoloea huzuni. Hakika Mola wetu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani. Ambaye ametuweka katika nyumba ya kukaa, humo haitugusi tabu wala humo hakutugusi kuchoka.

Watamshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu kwa kuwandolea hofu na kuokoka na moto na adhabu. Pia kuondokana na tabu na mashaka na kudumu kwenye neema na shangwe.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ ﴿٣٦﴾

36. Na wale ambao wamekufuru watakuwa na moto wa Jahannam, hawahukumiwi wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyomlipa kila mwenye kuzidi ukafiri.

وَهُمْ يَصْطَرِخُونَ فِيهَا رَبَّنَا أَخْرِجْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُم مَّا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَن تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ ﴿٣٧﴾

37. Na humo watapiga makelele: Mola wetu! Tutoe tufanye mema, sio yale tuliyokuwa tukiyafanya. Je, hatukuwapa umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka, na akawajia mwonyaji? Basi onjeni! Na madhalimu hawana wa kuwanusuru.

إِنَّ اللَّـهَ عَالِمُ غَيْبِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٣٨﴾

38. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

هُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ فَمَن كَفَرَ فَعَلَيْهِ كُفْرُهُ وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ إِلَّا مَقْتًا وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ إِلَّا خَسَارًا ﴿٣٩﴾

39. Yeye ndiye aliyewafanya nyinyi makhalifa katika ardhi. Na anayekufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila hasara.

HAWAHUKUMIWI WAKAFA

Aya 36 – 39

MAANA

Na wale ambao wamekufuru watakuwa na moto wa Jahannam, hawahukumiwi wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina nyingi ya adhabu kwa waasi; miongoni mwazo ni aina hii: Uchungu wa adhabu, kudumu kwake na kuendelea kwake. Hakuna mauti ya kumaliza adhabu wala sababu ya kupelekea kupunguziwa adhabu.

Hivyo ndivyo tunavyomlipa kila mwenye kuzidi ukafiri.

Ni malipo yanayolingana na kosa lake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:56 – 57).

Na humo watapiga makelele: Mola wetu! Tutoe tufanye mema, sio yale tuliyokuwa tukiyafanya.

Watapiga kelele na kutaka usaidizi, lakini hakuna wa kuwaokoa. Watatubia, lakini baada ya kupita muda. Umetangulia mfano wake katika Juz. 18 (23:99 – 100,107).

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٢٨﴾

“Na kama wangelirudishwa, bila shaka wangeyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo.” Juz. 7 (6:28).

Watapiga kelele na kutaka usaidizi, lakini hakuna wa kuwaokoa. Na watataka kutubia, lakini baada ya kupita muda. Umetangulia mfano wake katika Juz. 18 (23: 99-100, 107).

Je, hatukuwapa umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka, na akawajia mwonyaji?

Wanamtaka Mwenyezi Mungu awaruidishe duniani ili wawahi yale yaliyowapita katika imani na matendo mema.

Mwenyezi Mungu naye anawajibu kuwa mlikuwako duniani hapo mwanzo, mkakaa muda mwingi, akawajia mbashiri na muonyaji, mkafahamishwa njia ya uwongofu, lakini mkakataa.

Basi onjeni adhabu, hivi sasa, kutokana na vile mlivyokuwa mkikufuru.Na madhalimu hawana wa kuwanusuru, kwa sababu wao ndio waliojidhulumu wenyewe kwa uchaguzi wao mbaya. Kwani Mwenyezi Mungu aliwapa hoja na ubainifu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa siri za mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

Anajua siri na dhahiri, na yanayofichikana machoni ardhini na mbinguni, wala hakuna chochote kilichokuwa na kitakachokuwa kinachofichikana kwake.

Yeye ndiye aliyewafanya nyinyi makhalifa katika ardhi. Na anayekufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila hasara.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ardhi katika muundo wa kuweza kuishi watu, wakirithishana vizazi na vizazi. Akawapa akili na uwezo wa kuweza kuitumia kadiri wanavyotaka. Akawaamrisha wamwabudu Yeye peke yake bila ya kumshirikisha na jambo; akawawekea mipaka na kuwakataza wasiikiuke.

Mwenye kusikiliza na akawa na utii basi atapata malipo mema na mwenye kupinga basi atapata adhabu ya moto itakayozidi, na kuzidi kila wanavyozidisha uasi na kupituka mipaka. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا ﴿١٧٨﴾

“Hakika tunawapa muda ili wazidi katika dhambi.” Juz. 4 (3:178).

قُلْ أَرَأَيْتُمْ شُرَكَاءَكُمُ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا فَهُمْ عَلَىٰ بَيِّنَتٍ مِّنْهُ بَلْ إِن يَعِدُ الظَّالِمُونَ بَعْضُهُم بَعْضًا إِلَّا غُرُورًا ﴿٤٠﴾

40. Sema mnaona hawa washirika wenu mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, nionyesheni wameumba nini katika ardhi? Au wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu, nao kwa hicho, wakawa na hoja, lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu.

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤١﴾

41. Kwa hakika Mwenyezi Mungu huzuia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipokuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole, Mwingi wa maghufira.

وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِن جَاءَهُمْ نَذِيرٌ لَّيَكُونُنَّ أَهْدَىٰ مِنْ إِحْدَى الْأُمَمِ فَلَمَّا جَاءَهُمْ نَذِيرٌ مَّا زَادَهُمْ إِلَّا نُفُورًا ﴿٤٢﴾

42. Na waliapa kwa ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwafikia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipowajia muonyaji hakuwazidishia ila kukimbia.

اسْتِكْبَارًا فِي الْأَرْضِ وَمَكْرَ السَّيِّئِ وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا ﴿٤٣﴾

43. Kwa kutakabari kwao katika ardhi na kufanya vitimbi viovu. Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe. Basi hawangoji ila desturi ya wa zamani. Hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu wala hutapata mageuzi katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

ANAZIZUIA MBINGU NA ARDHI

Aya 40 – 43

MAANA

Katika Aya hii ya kwanza hapa, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa hoja tatu washirikina:

Sema mnaona hawa washirika wenu mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, nionyesheni wameumba nini katika ardhi?

Niambieni enyi washirikina! Ni jambo gani lililowafanya mumfanye Mwenyezi Mungu ana washirika? Je, ardhini kuna kitu chochote kinachofahamisha kuwa kimetengenezwa na wengi? Hapana! Vitu vyote vina- julisha kuweko Mungu mmoja tu, na mpangilio wake ni ushahidi wa utukufu wake na hekima yake.

Au wana ushirika wowote katika mbingu?

Yaani hao mnaowaabudu wana athari yoyote mbinguni kujulisha kuwa wao ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba?

Au tumewapa Kitabu, nao kwa hicho, wakawa na hoja.

Tuliowapa ni hao washirikina sio washirika wanaoabudiwa. Maana ni kuwa au mumewafanya washirika wa Mungu hao mnaowabudu kwa kutegemea Kitabu kilichoteremshwa au Nabii aliyetumwa? Kwa ujumla ni kuwa hakuna hoja yoyote ya kiakili na kinakili kwa wanavyovishirikisha; bali wao wanamangamanga tu.

Lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu.

Makusudio ya udanganyifu hapa ni ubatilifu. Viongozi wa washirikina walikuwa wakiwaambi wafuasi wao kuwa masanamu yatawaombea kesho. Hakuna mwenye shaka kuwa ahadi hii ni uwongo, uzushi na ubatilifu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu huzuia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipokuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole, Mwingi wa maghufira.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezizuwia sayari kwa nguvu ya mvutano; sawa na anavyowazuia ndege angani kwa mbawa zao. Mwenyezi Mungu ametegemeza kwake, kwa sababu yeye ni muumba wa ulimwengu na msababishi wa sababu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:65).

Na waliapa kwa ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwafikia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote.

Walioapa ni washirikina. Katika Bahrul-Muhit imesemwa kuwa watakuwa waongofu ambao hawana mfano. Makuraishi walikuwa wakiwapinga Mayahudi kwa kupotoka kwao na dini yao na kuwaua mitume wao. Wakaapa viapo vya nguvu kwamba akiwajia Mtume kutoka kwa kwa Mwenyezi Mungu watakuwa watiifu zaidi.

Lakini alipowajia muonyaji hakuwazidishia ila kukimbia kwa kutak- abari kwao katika ardhi na kufanya vitimbi viovu.

Hatimaye mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliwajia na hoja na ubainifu, lakini wao walimkadhibisha na wakamkimbia na wakamfanyia kiburi yeye na mwito wake. Vile vile walimfanyia vitimbi yeye na wafuasi wake na wakawazuia watu kuamini utume wake. Hata hivyo mwisho walishindwa na wakasalimu amri wakiwa dhalili na wanyonge.

Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe.

Vitimbi viovu ni kumdhamiria ubaya ndugu yako na kumpangia njama, bila ya yeye kujua, ili atumbukie. Hata hivyo, akiwa hajui yaliyodhamiri- wa na kupangwa, basi Mwenyezi Mungu anajua na atamlipa mpanga njama malipo ya muongo mwenye hadaa na balaa litamrudia yeye.

Basi hawangoji ila desturi ya wa zamani. Hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutapata mageuzi katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Desturi ya wa zamani ni desturi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wa zamani ambayo ni kuangamia waliowakadhibisha mitume wa Mwenyezi Mungu. Maana ni je, hawajui wanaomkadhibisha Mtume wetu Muhammad, kwamba Mwenyezi Mungu aliangamiza kaumu ya Nuh, A’ad, Thamud na mfano wao waliowakadhibisha mitume? Na kwamba hii ni desturi yake Mwenyezi Mungu isiyobadilika wala kugeuka? Je, hawapati funzo kwa wengine?

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا ﴿٤٤﴾

44. Je, hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa waliokuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Na hakuna kitu kiwezacho kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala ardhini. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye kuweza.

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا ﴿٤٥﴾

45. Na lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, basi asingeliwacha katika ardhi hata mnyama mmoja, lakini yeye anawaakhirisha mpaka muda maalum. Ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.

ASINGELIMUACHA HATA MNYAMA MMOJA

Aya 44 – 45

MAANA

Je, hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa waliokuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao.

Aya hii inaungana na ile ya kabla yake. Ile inasema kuwa desturi ya Mwenyezi Mungu kwa waliowakadhibisha hapo mwanzo ni kuangamizwa na kung’olewa kabisa, na hii inawambia wale wanaomkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) kuwa athari ile ya waliokadhibisha kabla yenu iko wazi na wala sio mbali na nyinyi. Hebu safirini kidogo katika ardhi muone. Pengine mnaweza kuzingatia na mkapata funzo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 ( 22:46).

Na hakuna kitu kiwezacho kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala ardhini. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye kuweza.

Hampiti aliyepo wala hamshindi mwenye kukimbia. Kila kitu kinanyenyekea uweza wake na kinanyenyekea ukuu wake. Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa viumbe wote wanahusika na dhambi; hata wanyama, ndege na chembe chembe. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawateremshia adhabu, na akiiteremsha inawaenea wote; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ﴿٢٥﴾

“Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu miongoni mwenu peke yao”

Juz. 9 (8:25).

Na lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, basi asingeliwacha katika ardhi hata mnyma mmoja, lakini yeye anawaakhirisha mpaka muda maalum. Ukifika muda wao basi haki- ka Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.

Jambo linalofahamisha zaidi maudhi ya mtu kwa muumba wake, ni kuwa yeye anakula riziki yake na anamwabudi mwingine. Hii peke yake inatosha kuadhibiwa. Lakini kila kitu, mbele ya Mwenyezi Mungu, kina muda maalum.

MWISHO WA SURA YA THELATHINI NA TANO: SURAT FATIR