12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
Sura Ya Thelathini na Sita: Surat Yasin. Imeshuka Makka isipokuwa Aya moja. Ina Aya 83.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
يس ﴿١﴾
1. Yasin.
وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
2. Naapa kwa Qur’an yenye hekima.
إِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٣﴾
3. Hakika wewe bila shaka ni miongoni mwa waliotumwa.
عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤﴾
4. Juu ya njia iliyonyooka.
تَنزِيلَ الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٥﴾
26. Ni uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أُنذِرَ آبَاؤُهُمْ فَهُمْ غَافِلُونَ ﴿٦﴾
6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi ni wenye kughafilika.
لَقَدْ حَقَّ الْقَوْلُ عَلَىٰ أَكْثَرِهِمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٧﴾
7. Imekwishathibiti kauli juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.
إِنَّا جَعَلْنَا فِي أَعْنَاقِهِمْ أَغْلَالًا فَهِيَ إِلَى الْأَذْقَانِ فَهُم مُّقْمَحُونَ ﴿٨﴾
8. Hakika tumeweka minyororo shingoni mwao, nayo inafika videvuni, kwa hiyo vichwa vyao viko juu.
وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ ﴿٩﴾
9. Na tumeweka kizuizi mbele yao na kizuizi nyuma yao na tumewafunika, kwa hiyo hawaoni.
وَسَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠﴾
10. Ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
إِنَّمَا تُنذِرُ مَنِ اتَّبَعَ الذِّكْرَ وَخَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ فَبَشِّرْهُ بِمَغْفِرَةٍ وَأَجْرٍ كَرِيمٍ ﴿١١﴾
11. Hakika unamuonya yule tu anayefuata ukumbusho na akamcha Mwingi wa rehema kwa ghaibu. Basi mbashirie maghufira na ujira wa heshima.
إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾
12. Hakika sisi tunawahuisha wafu na tunayaandika wanayoyatanguliza na athari zao. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari linalobainisha.
WEWE NI KATIKA MITUME
Aya 1 – 12
MAANA
Yasin
Wafasiri wengi wamesema kuwa tamko hili lina maana kama mianzo mingine ya Sura yenye herufi za mkato; kama ilivyo katika Juz.1 (2:1). Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Amani kwa Ilyasin” (37:130), makusudio yake ni Ilyas.
Naapa kwa Qur’an yenye hekima. Hakika wewe bila shaka ni miongoni mwa waliotumwa juu ya njia iliyonyooka.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameapa, kwa Qur’an yenye hekima, kwamba Muhammad(s.a.w.w)
yuko kwenye dini ya ya sawasawa. Kuapa kwa Mwenyezi Mungu kwa Qur’an pamoja na kuisifu kuwa ina hekima, kunaashiria kwenye utukufu wa Qur’an na ukuu wake na kwamba ni dalili yenye nguvu zaidi juu ya ukweli wa Muhammad(s.a.w.w)
katika mwito wake.
Ama kujisifu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa nguvu na rehema, katika kauli yake:
Ni uteremsho wa Mwenye nguvu Mwenye kurehemu,
ni ishara kuwa anawachukulia waasi kwa namna ya Mwenye uwezo na anawahurumia waumini na wenye kutubia.
Imam Ali
anasema:“Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na rehema, wala rehema haimshughulishi (asiwe) na mateso.”
MDUNDO WA NDANI KATIKA QUR’AN
Mnamo mwaka 1959 Mustafa Mahmud, Mmisri, alitunga kitabu Allahu wal-insan (Mungu na mtu). Katika kitabu hicho alikana Mungu na ufufuo, nami nikamjibu kwa kutunga kitabu Allahu wal-Aqli (Mungu na Akili).
Kisha nikafuatilia makala zake na tungo zake. Nikasoma makala yake katika jarida linaloitwa Ruzil-yusf la tarehe 10-4-1967 akikiri kuweko ufufuo. Hayo nimeyaashiria katika Juz. 1 (2:28 – 29) kifungu cha ‘Ufufuo.’
Mustafa Mahmud ni mwana fasihi, mwenye akili inayogundua undani na siri za lugha. Ushahidi wa hayo ni aliyoyaandika kuhusu Qur’an katika jarida la Sabahul-khayr la tarehe 1-1-1970 kwa anuani ya “Usanifu wa Qur’an” Tunadokoa machache katika makala hiyo, kama yafuatavyo:
“Sijui niseme nini kuelezea hisia niliyoipata katika ibara ya kwanza ya Qur’an... Basi matamshi yake yalikuwa yakiingia kwenye nafsi yangu, kama kwamba ni kiumbe hai chenye maisha ya aina ya peke yake... Nikagundua simulizi za mdundo wa kindani katika ibara za Qur’an Hii ni siri ya ndani sana katika mpangilio wa Qur’an...
Yenyewe sio mashairi wala nathari au lugha ya mjazo; isipokuwa ni ubainifu maalum wa maneno yaliyoundwa kwa njia inayogundua mdundo wa kindani. Mdundo uliozoeleka unakuja kutoka nje na kufika masikioni, na sio ndani bali unatokana na mahadhi, wizani na kina.
Mdundo wa Qur’an hauna wizani wala kina au mahadhi, lakini pamoja na hayo, unashuka kwa kila herufi yake... kutoka wapi na vipi, hiyo ndiyo siri katika siri za Qur’an zisizofanana na mfumo wowote wa kifasihi. Inashangaza na wala hatuwezi kuujua mfumo wake. Ni mfumo wa kipekee haujapatakina katika kila kilichoandikwa kwa lugha ya kiarabu ya zamani na ya sasa. Haiwezekani kuuiga mfumo huu.”
Ndio haiwezekani kuuiga. Na hapa ndio inapatikana siri ya muujiza wa Qur’an. Baada ya mwandishi huyu kuleta ushahidi mwingi wa hakika hii katika maneno ya Mwenyezi Mungu na Aya zake, aliendelea kusema:
“Na sio mdundo wa kindani tu ndio kitu cha aina yake katika Qur’an, bali kuna sifa nyingine inayokutambulisha kuwa hii ni sanaa ya muumba sio ya muumbwa... Hebu isikilize Qur’an ikisifia mfungamano wa maingiliano ya kijinsia baina ya mume na mke, kwa tamako laini na la heshima, jambo ambalo huwezi kulipata kwenye lugha yoyote: “Alipomkurubia [5]
1 alishika mimba nyepesi.” Juz. 9 (7:189).
Tamko hili taghashaha alimfunika (kwa maana ya kumkurubia) linamchanganya mume na mke kama vinavyochanganyika vivuli viwili au kama rangi inavyofunika rangi nyingine. Tamko hili la ajabu linalofahamisha muingiliano mkamilifu wa mume na mke, ni ukomo wa ibara.
Hakika Qur’an ina hali ya kipekee na ya ajabu, inayoleta unyenyekevu katika nafsi na kuathiri moyo, pale tu matamshi yake yanapogusa masikio, kabla ya akili kuanza kuyafanyia kazi. Na ikianza kufanya uchambuzi na kutaamali, inagundua vitu vipya vinavyomzidisha unyenyekevu. Lakini hii ni hatua ya pili; inaweza kutokea na isitokee, inaweza kugundua siri za Aya na inaweza isigundue, na inaweza kuleta busara au isilete, lakini unyenyekevu upo.”
Hii nayo ni aina mojawapo ya muujiza wa Qur’an. Mwandishi huyu wa kitabu Allahu wal insan alimaliza makala yake ndefu kwa kusema: “Hakika Qur’an ni matamshi na maana kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye amekizunguuka kila kitu kwa ujuzi.”
Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi ni wenye kughafilika.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa Muhammad(s.a.w.w)
ni Mtume wa haki na kwamba Qur’an imetoka kwake, sasa anabainisha umuhimu wa Qur’an kuwa inakataza aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, kwenye masikio ya waarabu, walioghafilika na Mwenyezi Mungu na haki, bila ya kufikiwa na muonyaji kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
.
Huko nyuma kwenye Juzuu hii, kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na hakuna uma wowote ila alipita humo muonyaji (35:24),” tumesema kuwa makusudio ya muonyaji hapo ni kila linalosimamia hoja, iwe ni akili au nakili na kwamba makusudio ya muonyaji kwenye Aya hii tuliyo nayo ni Mtume hasa.
Imekwishathibiti kauli juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.
Makusudio ya kauli hapa ni kiaga cha adhabu, na wengi wao ni hao maba- ba zao; yaani mababa za waarabu waliokuwa wakati wa Muhammad(s.a.w.w)
, waliokufa kwenye ushirikina. Ni wachache sana waliokuwa kwenye dini ya Tawhid. Tazama Juz. 15 (17:105–111) kifungu ‘Wanyoofu.’
Hakika tumeweka minyororo shingoni mwao, nayo inafika videvuni, kwa hiyo vichwa vyao viko juu.
Mikono ikifungwa kwa minyororo mpaka shingoni kichwa huinuka juu, na aliyefungwa anakuwa hawezi kugeuka kuume wala kushoto au kuangalia mbele; atakuwa anaangalia juu tu.
Na tumeweka kizuizi mbele yao na kizuizi nyuma yao na tumewafunika, kwa hiyo hawaoni.
Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaweka kwenye vizuizi viwili vya moto. Kimoja mbele yao na kingine nyuma yao, hawawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma; wala hawezi kuona mbingu, kwa sababu vizuizi viwili vimefunika macho yao.
Sio mbali kuwa hiki ni kinaya cha ukali na uchungu wa adhabu. Kwa vyovyote iwavyo, adhabu haihusiki na washirikina tu, bali itaenea kwa kila mwenye hatia na dhalimu.
Imam Ali
anasema:“Ama watu wa maasia atawaweka mahali pa baya, atawafunga mikono kwa minyororo hadi videvuni, utosi utafungwa na nyayo, na atawavisha kanzu za lami na nguo za moto. Watu wake watafungiwa mlango katika Moto mkali wenye kuvuma.”
Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (34:33).
Ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye hawataamini.
Ni sawa kwao ewe Muhammad, uwape mawawidha au usiwape, basi hakika wao, hawatafanya lolote isipokuwa kwa hawaa zao na masilahi yao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:6).
Hakika unamuonya yule tu anayefuata ukumbusho na akamcha Mwingi wa rehema kwa ghaibu. Basi mbashirie maghufira na ujira wa heshima.
Anayekusikiliza ni yule anayeitafuta haki kwa ajili ya haki na kwenda nayo kwa matokeo yoyote yatakayokuwa. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (35: 18).
Hakika sisi tunawahuisha wafu na tunayaandika wanayoyatanguliza na athari zao. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari linalobainisha.
Daftari linalobainisha ni kinaya cha elimu ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa, Mwenyezi Mungu atawafufua, na ameyahifadhi wanayoyafanya ya kheri na ya shari na athari walizoziacha za manufaa au madhara, na kwamba Yeye atamlipa kila mmoja alilolifanya, nao hawatadhulumiwa.
وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا أَصْحَابَ الْقَرْيَةِ إِذْ جَاءَهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿١٣﴾
13. Na wapigie mfano wenyeji wa mji Mitume walipowafikia.
إِذْ أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمُ اثْنَيْنِ فَكَذَّبُوهُمَا فَعَزَّزْنَا بِثَالِثٍ فَقَالُوا إِنَّا إِلَيْكُم مُّرْسَلُونَ ﴿١٤﴾
14. Tulipowatuma wawili wakawakadhibisha. Basi tukawaongezea nguvu kwa (mwingine) wa tatu Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
قَالُوا مَا أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَمَا أَنزَلَ الرَّحْمَـٰنُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَكْذِبُونَ ﴿١٥﴾
15. Wakasema nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na mwingi wa rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
قَالُوا رَبُّنَا يَعْلَمُ إِنَّا إِلَيْكُمْ لَمُرْسَلُونَ ﴿١٦﴾
16. Wakasema: Mola wetu anajua kwamba sisi tumetumwa kwenu.
وَمَا عَلَيْنَا إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٧﴾
17. Wala si juu yetu ila kufikisha waziwazi.
قَالُوا إِنَّا تَطَيَّرْنَا بِكُمْ لَئِن لَّمْ تَنتَهُوا لَنَرْجُمَنَّكُمْ وَلَيَمَسَّنَّكُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٨﴾
18. Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu. Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu.
قَالُوا طَائِرُكُم مَّعَكُمْ أَئِن ذُكِّرْتُم بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ مُّسْرِفُونَ ﴿١٩﴾
19. Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe. Je, ni kwa kuwa mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu mnaopituka mipaka.
وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na akaja mtu mbio kutoka upande wa mbali wa mjini akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni Mitume.
اتَّبِعُوا مَن لَّا يَسْأَلُكُمْ أَجْرًا وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٢١﴾
21. Wafuateni wasiowaomba ujira nao wameongoka.
وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٢﴾
22. Na kwa nini nisimwabudu yule aliyeniumba na kwake mtarejeshwa?
أَأَتَّخِذُ مِن دُونِهِ آلِهَةً إِن يُرِدْنِ الرَّحْمَـٰنُ بِضُرٍّ لَّا تُغْنِ عَنِّي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا وَلَا يُنقِذُونِ ﴿٢٣﴾
23. Je, nishike miungu mingine badala yake? Mwingi wa rehema akinitakia madhara, uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
إِنِّي إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٤﴾
24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotofu ulio dhahiri.
إِنِّي آمَنتُ بِرَبِّكُمْ فَاسْمَعُونِ ﴿٢٥﴾
25. Hakika mimi nimemwamini Mola wenu, basi nisikilizeni.
قِيلَ ادْخُلِ الْجَنَّةَ قَالَ يَا لَيْتَ قَوْمِي يَعْلَمُونَ ﴿٢٦﴾
26. Ikasemwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti watu wangu wangejua.
بِمَا غَفَرَ لِي رَبِّي وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُكْرَمِينَ ﴿٢٧﴾
27. Jinsi Mola wangu alivyonighufiria na akanifanya katika waheshimwa.
WAJUMBE WAWILIA WALIOWAONGEZEWA NGUVU KWA WA TATU
Aya 13 – 27
MAANA
Na wapigie mfano wenyeji wa mji Mitume walipowafikia.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume awaambie washirikina wa Kiarabu. Ama mji, wafasiri wengi wamesema ni Antiokia, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuelezea. Kwa sababu makusudio ya kupiga mfano ni kupata mawaidha na mazingatio, sio jina la mji na sehemu yake.
Dhana kubwa ni kuwa wafasiri wametegemea vitabu vya kinaswara; ambapo imeelezwa kwenye Matendo ya mitume 11:19 – 26, kwamba Barnaba na Sauli walikwenda Antiokia na kuwafundisha watu wengi. Na kwamba mitume ni wanafunzi 12 aliowachagua Bwana Masih
ili wamsaidie na wamwone atakapotoka kaburini, waelezee walimwengu; kama ilivyoelezwa kwenye Mathayo na Matendo ya mitume.
Barnaba alikuwa ni Mkupro (Cyprus) akaingia kwenye ukiristo katika zama za mitume na akawa ni mhubiri; kama ilivyoelezwa katika ‘Kamusi ya Kitabu kitakatifu’
Tulipowatuma wawili wakawakadhibisha. Basi tukawaongezea nguvu kwa (mwingine) wa tatu.
Katika tafsiri nyingi imeelezwa kuwa mitume walikuwa ni wanafunzi wa Isa
na kwamba yeye ndiye aliyewatuma wawili mjini kisha akawaongezea nguvu kwa mwingine wa tatu.
Lakini neno mitume likitegemezwa kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyo katika neno ‘tulipowatuma’ na ‘tukawaongezea nguvu,’ huwa linafahamisha kuwa wao walitumwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja sio kwa kwa amri ya Isa
.
Vyovyote iwavyo, la kuzingatia ni utendaji si majina. Zaidi ya hayo sisi hatutaulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hilo halina uhusiano wowote na maisha yetu kwa karibu au mbali. Maana yaliyo wazi, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwatuma mitume watatu kwenye mji huo, watoe mwito wa haki.
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu. Wakasema; nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na mwingi wa rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
Hii ndio nembo ya wapinzani siku zote. Tazama Juz. 13 ( 14:10), Juz. 15 (17:94), Juz. 17 (21:3), Juz. 18 (23:24) na Juz. 19 (26:154).
Wakasema: Mola wetu anajua kwamba sisi tumetumwa kwenu. Wala si juu yetu ila kufikisha waziwazi.
Baada ya mitume kusimamisha hoja za kusadikisha ukweli wao, waliwaambia wakadhibishaji kuwa sisi tumetumwa kwenu na Mwenyezi Mungu, akatupa ubainifu, kama mnavyouona, na tumetekeleza ujumbe wake, kama inavyotakikana. Basi si juu yetu tena hisabu yenu wala si juu yenu nyinyi hisabu yetu. Yeye ni mjuzi mwenye kuhisabu.
Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu. Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu. Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe. Je, ni kwa kuwa mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu mnaopituka mipaka.
Mkosi wenu mnao wenyewe; yaani hakuna mkosi, bali hizo ni dhana zenu tu. Kuna Hadith mashuhuri isemayo:“Hakuna kuambukiza, wala mkosi
wala nyuni”
Imam As-Sadiq
anasema:“Mkosi unaufanya wewe, ukiupuuza utakupuuza, ukiutilia mkazo utakutilia mkazo na ukiufanya si chochote nao hautakuwa ni chochote”
Yaani hakuna kitu kama kisirani, ndege au mkosi; wala hauna athari yoyote kwa mtu; isipokuwa unaathiri nafsi ya mtu na mishipa yake, kwa vile anavyouwazia tu; kama mtoto anavyotishika na zimwi.
Maana ni kuwa wakadhibishaji waliwaambia mitume kuwa mmetuletea mkosi, kwa hiyo tunahofia tutagawanyika; sasa bora mnyamaze, la sivyo tutawanyamazisha kwa kuwapiga mawe na adhabu kali. Ndio Mitume wakawaambia, chimbuko la hofu ya mkosi linatokana na wasiwasi wenu nyinyi wenyewe, kwamba mwito wetu ni mkosi na shari; na hali yakuwa shari inatoka kwenu kwa kufanya shirki, ujahili na ufisadi.
Na akaja mtu mbio kutoka upande wa mbali wa mjini.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuashiria jina la mtu huyu, lakini wafasiri wengi wakasema jina lake ni Habib An-Najar, na kwamba nyumba yake ilikuwa kandoni mwa mji. Alikuwa mumin. Aliposikia kuwa watu wake wanaazimia kuwaua mitume, alifanya haraka kuja kuwaokoa na kuwasaidia.
Sijui wafasiri wamelitoa wapi jina hili. Mimi nimetafuta mpaka katika Biblia ukurasa wa yaliyomo na kamusi ya Kitabu kitakatifu pia sikulipata.
Vyovyote iwavyo, jina la huyo mtu halina mfungamano wowote na sisi. Wala hakuna linalotushughulisha isipokuwa lile lililofahamishwa na Aya. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsifu kuwa na imani na wema, kwa sababu alisema:
Enyi watu wangu! Wafuateni Mitume. Wafuateni wasiowaomba ujira nao wameongoka.
Aliwapa nasaha watu wake wakubali mwito wa Mitume wala wasiwapinge, kwa sababu ni kwa masilahi yao. Wanatoa mwito na hawataki malipo wala shukrani; wala uluwa au ufisadi katika ardhi.
Na kwa nini nisimwabudu yule aliyeniumba na kwake mtarejeshwa?
Kauli hii ni ya yule mumin anayetoa nasaha. Maana yake ni kuwa, ni kizuizi gani kitakachonizuia na ibada ya ambaye amenifanya niweko baada ya kutokuweko, kisha atatufufua sote baada ya mauti kwa ajili ya hisabu na malipo?
Hapa anawapinga watu wake walioacha ibada ya Mungu mmoja wa pekee. Anaendelea kuwagonga na kusema:
Je, nishike miungu mingine badala yake? Mwingi wa rehema akinitakia madhara, uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotofu ulio dhahiri.
Vipi niabaudu masanamu yasiyodhuru wala kunufaisha? Hayaokoi wala hayaombei? Nikifanya hivyo nitakuwa nimepotea, wala sitakuwa katika walioongoka. Hapana!
Hakika mimi nimemwamini Mola wenu, basi nisikilizeni.
Hawi jasiri wa maneno haya isipokuwa yule asiyeogopa mauti katika njia ya haki na kuinusuru. Kuna mapokezi yanayoeleza kuwa alipowajia watu wake na hakika hii, walimuua kwa kumpiga mawe na hakupata wa kumhami. Hili haliko mbali kulingana na sera ya mataghuti na wafisadi. Linalotia nguvu ukweli wa risala hii ni ile kauli ya washirikina kwa mitume: “Kama hamtakoma basi hakika tutawapiga mawe na itawafika adhabu chungu kutoka kwetu.”
Katika Tafsiri ya Zamakhshari na Tha’labi imesemwa: Watangulizi wa umma ni watatu, hawakukufuru hata kwa kupepesa jicho: Ali bin Abu Twalib, Mtu wa Yasin na Mumin wa watu wa Firauni.
Ikasemwa: Ingia Peponi!
Aliiuza nafsi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na thamani ya bei yake ikawa ni Pepo. Hiyo ni tosha kuwa ni thawabu na malipo.
Akasema: Laiti watu wangu wangejua jinsi Mola wangu alivyonighufiria na akanifanya katika waheshimiwa.
Hakusema hivi kwa kuwacheka watu, ingawaje walimkadhibisha, hapana! Watu wema hawawi hivi; bali alisema hivi kuwasikitikia na yaliyowapita, akitamani lau wangelijua kwamba yeye alikuwa akiwapa nasaha na kwamba zilikuwa ni njozi na ujinga kuwa yeye na mitume wana mikosi.