16
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
Sura Ya Thelathini Na Saba: Surat As-Saffat. Imeshuka Makka ina Aya 182.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
وَالصَّافَّاتِ صَفًّا ﴿١﴾
1. Naapa kwa wanaojipanga safu-safu.
فَالزَّاجِرَاتِ زَجْرًا ﴿٢﴾
2. Na kwa wenye kuzuia sana.
فَالتَّالِيَاتِ ذِكْرًا ﴿٣﴾
3. Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
إِنَّ إِلَـٰهَكُمْ لَوَاحِدٌ ﴿٤﴾
4. Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja.
رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَرَبُّ الْمَشَارِقِ ﴿٥﴾
5. Mola wa mbingu na ardhi, na vilivyomo kati yake, na ni Mola wa mashariki zote.
إِنَّا زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِزِينَةٍ الْكَوَاكِبِ ﴿٦﴾
6. Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya dunia (karibu) kwa pambo la nyota.
وَحِفْظًا مِّن كُلِّ شَيْطَانٍ مَّارِدٍ ﴿٧﴾
7. Na kuilinda na kila shetani muasi.
لَّا يَسَّمَّعُونَ إِلَى الْمَلَإِ الْأَعْلَىٰ وَيُقْذَفُونَ مِن كُلِّ جَانِبٍ ﴿٨﴾
8. Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.
دُحُورًا وَلَهُمْ عَذَابٌ وَاصِبٌ ﴿٩﴾
9. Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.
إِلَّا مَنْ خَطِفَ الْخَطْفَةَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ ثَاقِبٌ ﴿١٠﴾
10. Isipokuwa anayenyakua kitu kidogo, na mara humfuatia kimondo kinachong’ara.
WANAOJIPANGA SAFU
Aya 1 – 10
MAANA
Naapa kwa wanaojipanga safu-safu. Na kwa wenye kuzuia sana. Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
Wametofautiana wafasiri katika maana ya wanaojipanga safu, wenye kuzuia na wenye kusoma ukumbusho. Kuna waliosema kuwa ni Malaika.
Wengine wakasema ni waumini wanaokaa safu katika Swala ya jamaa na katika jihadi. Na wenye kuzuia ni makatazo ya Qur’an na Aya zake. Na wenye kusoma ni wasomaji wa Qur’an kwenye Swala na kwengineko.
Sio mbali kuwa makusudio ni aina tatu alizozitaja Imam Ali
katika khutba ya kwanza kwenye Nahjul-Balagha, katika wasifu wa Malaika: “Miongoni mwao kuna ambao wamesujudu na wala hawarukui, na kuna waliorukuu na wala hawasimami, kuna waliosimama katika safu na wala hawatawanyiki.” Aliposema: ‘Kuna waliosimama katika safu na wala hawatawanyiki’ inawezekana kuwa ni ishara ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa wanao jipanga safu-safu.”
Kisha Imam Ali
akaendelea kusema: “ Miongoni mwao kuna waaminifu wa wahyi wa Mungu, na ni ndimi zitamkazo kwa mitume Wake;” yaani wanaoshuka na wahyi kwa mitume wake; kama vile Jibril
. Kauli hii nayo ina uwezekano wa kuwa ni ishara ya kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.” Kwa sababu wao wanasoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu wakati wanapofikisha kwa Mitume.
Akaendelea kusema: “Na miongoni mwao kuna wahifadhi wa waja wake.” Sheikh Muhammad Abduh, katika kuwaelezea hawa, anasema: “Kama kwamba wao ni nguvu inayotiwa katika miili ya binadamu na katika nafsi zao; akiwahifadhi Mwenyezi Mungu binadamu wasiangamie kwa Malaika. Na lau si hivyo, maangamizi yangelikuwa yanamwandama mtu zaidi kuliko amani.”
Sheikh, katika kuleta picha hii, anakusudia kurahisisha kufahamu jinsi Malaika wanavyohifadhi waja; akisema: “Kama kwamba wao.”
Kwa hiyo basi inawezekana hilo linaashiria kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na kwa wenye kuzuia sana,” ikiwa tutasema kuwa kuzia hapa maana yake ni kuzuia udhia kwa waja.
Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. Mola wa mbingu na ardhi, na vilivyomo kati yake, na ni Mola wa mashariki zote.
Makusudio ya mashariki
zote ni mashariki ya Jua kwa kuangalia kwamba kila siku linatokeza mashariki na kutua magharibi. Mwenyezi Mungu amekata kuwa Yeye ni mmoja hana mshirika katika kuumba na kupangilia.
MWENYEZI MUNGU NA KUAPA NA VIUMBE VYAKE
Unaweza kuuliza
: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameapa kwa Malaika?
Wafasiri wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu ameapa kwa Malaika kujulisha ukuu wa daraja na umuhimu wao. Hili ndio jawabu lao kwa kila alichoapia Mwenyezi Mungu; iwe ni wakati, mahali au chochote kilichoko juu au chini. Hata hivyo mwenye Dhilal ameunganisha kuapa huku na kauli ya watu wa jahiliya waliosema kuwa Malaika ni mabinti wa Mungu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
أَفَأَصْفَاكُمْ رَبُّكُم بِالْبَنِينَ وَاتَّخَذَ مِنَ الْمَلَائِكَةِ إِنَاثًا إِنَّكُمْ لَتَقُولُونَ قَوْلًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾
“Je, Mola wenu amewachagulia waototo wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika? Hakika nyinyi mnasema kauli kubwa.” Juz. 15 (17:40).
Akasema mwenye Dhilal: Lengo la kuapa kwa Malaika ni kuwarudi wenye kuamini upotofu huu alioita Mwenyezi Mungu ‘kauli kubwa.’
Tuanavyo sisi ni kuwa Mwenyezi Mungu anaapa na kitu chochote kile kwa lengo moja tu – kuwa kila kilichopo kwa asili yake kinafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja hana mshirika.
Hakuna mwenye shaka kuwa Malaika wanaopanga safu na wasiopanga safu wanamwabudu Mwenyezi Mungu na kumtii kwa ujuzi na yakini na kwa utumishi wao. Kwa hiyo kujua kwao hivi ni dalili mkataa kuwa Yeye ni mmoja hana mshirika katika kuuumba umiliki na upangiliaji; sawa na kujua wataalamu hakika ya maudhui waliyoyagundua na kuyafanyia majaribio.
Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya dunia (karibu) kwa pambo la nyota.
Makusudio ya mbingu ni anga ya juu na dunia ni dunia yetu sisi binadamu
, sio ulimwengu wote. Makusudio ya nyota ni zile zilizo kwenye anga iliyo karibu zaidi na sisi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejaalia nyota, jinsi ziliyvo na mwanga wake katika anga yetu, kuwa ni pambo na urembo; mbali ya manufaa na faida zake:
وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ النُّجُومَ لِتَهْتَدُوا بِهَا فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ﴿٩٧﴾
“Na yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Juz. 7 (6:97).
Na kuilinda na kila shetani muasi wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande, wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. Isipokuwa anayenyakua kitu kidogo, na mara humfuatia kimondo kinacho ng’ara.
Misamiati ya Aya hii iko wazi, isipokuwa miwili-Shetani asi na viumbe watukufu. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameinyamazia, hawaku- tubainishia. Nasi hatuwezi kufasiri bila ya ujuzi. Kwa hiyo tunasema kuwa Aya hizi ni katika zinazotatiza kwetu, lakini inawezekana kuwa ziko wazi kwa wenzetu.
Sio mbali kuwa sababu ya kunyamazia ni kuwa kumjua shetani huyu na kiumbe mtukufu hakuna uhusiano na maisha yetu au kuwa fahamu zetu zinashindwa kufahamu uhakika wake. Na mwenye elimu kadiri atakavyojitahidi, lakini hawezi kujua kila kitu; bali hawezi hata kujua kitu chochote katika vinavyomzunguka uhakika wake hasa kilivyo.
Kujua kwetu misamiati ya Aya; kama kimondo kinachong’ara, adhabu ya kudumu, kunyakua na kufuatiwa, hakuwezi kutosha kufasiri makusudio ya Aya kwa ujumla wake, maadamu hatujui uhakika wa shetani asi na viumbe watukufu.
Baadhi ya wafasiri wamesema makusudio ya shetani asi ni shetani jini. Wengine wakasema ni binaadamu ambaye hafikiri ukuu na utukufu wa nyota na kufahamisha kwake kuweko Mwenyezi Mungu. Masufi wanase- ma: Makusudio ya shetani ni picha na nguvu ya kuwazia. Yote hiyo ni kutupia kwa mbali. Ni afadhali kunyamaza kuliko kusema bila ya kujua. Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾
“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” Juz. 15 (17:85).
فَاسْتَفْتِهِمْ أَهُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَم مَّنْ خَلَقْنَا إِنَّا خَلَقْنَاهُم مِّن طِينٍ لَّازِبٍ ﴿١١﴾
11. Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tuliowaumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unaonata.
بَلْ عَجِبْتَ وَيَسْخَرُونَ ﴿١٢﴾
12. Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
وَإِذَا ذُكِّرُوا لَا يَذْكُرُونَ ﴿١٣﴾
13. Na wanapokumbushwa hawakumbuki.
وَإِذَا رَأَوْا آيَةً يَسْتَسْخِرُونَ ﴿١٤﴾
14. Na wanapoona Ishara, wanafanya maskhara.
وَقَالُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾
15. Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhahiri.
أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿١٦﴾
16. Ati tukishakufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?
أَوَآبَاؤُنَا الْأَوَّلُونَ ﴿١٧﴾
17. Hata baba zetu wa zamani?
قُلْ نَعَمْ وَأَنتُمْ دَاخِرُونَ ﴿١٨﴾
18. Sema: Naam! Na hali nyinyi ni madhalili.
فَإِنَّمَا هِيَ زَجْرَةٌ وَاحِدَةٌ فَإِذَا هُمْ يَنظُرُونَ ﴿١٩﴾
19. Na hakika ni ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
وَقَالُوا يَا وَيْلَنَا هَـٰذَا يَوْمُ الدِّينِ ﴿٢٠﴾
20. Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.
هَـٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿٢١﴾
21. Hii ndiyo Siku ya upambanuzi mliyokuwa mkiikadhibisha.
احْشُرُوا الَّذِينَ ظَلَمُوا وَأَزْوَاجَهُمْ وَمَا كَانُوا يَعْبُدُونَ ﴿٢٢﴾
22. Wakusanyeni waliodhulumu, na wenzao, na hao waliokuwa wakiwaabudu,
مِن دُونِ اللَّـهِ فَاهْدُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطِ الْجَحِيمِ ﴿٢٣﴾
23. Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!
وَقِفُوهُمْ إِنَّهُم مَّسْئُولُونَ ﴿٢٤﴾
24. Na wasimamisheni. Hakika hao wataulizwa.
مَا لَكُمْ لَا تَنَاصَرُونَ ﴿٢٥﴾
25. Mna nini? Mbona hamsaidiani?
بَلْ هُمُ الْيَوْمَ مُسْتَسْلِمُونَ ﴿٢٦﴾
26. Bali leo, watasalimu amri.
BALI UNASTAAJABU, NA WAO WANAFANYA MASKHARA
Aya 11 – 26
MAANA
Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tuliowaumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unaonata.
Waulize ewe Muhammad, wale wanaokana ufufuo kuwa kuumba mbingu na ardhi bila ya nyenzo yoyote ni kugumu au kumrudisha mtu kwenye uhai baada ya kufa kwake, na hali Mwenyezi Mungu amemuumba kwa udongo tu uanonata?
Hakika yule ambaye ameuumba ulimwengu bila ya nyenzo yoyote, inakuwa wepesi zaidi kurudisha viungo vya mtu kwenye uhai.
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾
“Hakika kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu, lakini watu wengi hawajui.” (40:57)
Unaweza kuuliza
: Kwenye Juz.15 (18: 22) Mwenyezi Mungu anasema: “Wala usiulize habari zao kwa yeyote yule.” Kuna njia gani ya kuafikiana Aya mbili hizi?
Jibu
: maudhui ya Aya ile yanahusiana na watu wa pango; ambapo Mwenyezi Mungu alimkataza Nabii wake mtukufu kutomuuliza yeyote kuhusiana na wao, baada ya kumweleza habari zao. Na hii tuliyo nayo inahusiana na washirikina tu. Na makusudio ni kuwatahayariza na kuwapa hoja.
Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
Wewe Muhammad unawastaajabu washirikina kwa jinsi walivyomfanya Mwenyezi Mungu kuwa na washirika, pamoja na dalili za umoja zilizo wazwazi. Nao vile vile wanakushangaa wewe; bali wanakufanyia maskhara. Kwa sababu dalili za ushirikina ziko wazi kulingana na ufahamu wao na wala sio dalili za tawhid.
Hii inafahamisha kuwa ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili kweli ni jambo la ajabu. (38:5).
Ikiwa mtu atasema pamoja na yule mshairi: “Kila mtu dini yake anaitukuza, laitani usahihi ningejuzwa,” nasi tutajibu:
Kuna misingi na uhakika ulio wazi ambao hawawezi kutofautiana hata watu wawili; ambapo anaweza kuijua mjuzi na asiyekuwa mjuzi; mfano: Elimu ni bora kuliko ujinga, na utajiri ni bora kuliko ufukara.
Ikiwa wawili watatofautiana katika nadharia fulani, yule ambaye kauli yake itaishia kwenye misingi iliyo wazi basi huyo ndiye atakayekuwa na haki.
Na wanapokumbushwa hawakumbuki. Na wanapoona Ishara, wanafanya maskhara.
Kwa sababu mwenye kutii hawaa yake na kuiga mababa zake, huifumbia macho haki: Imam Ali
anasema:“Yeyote anayeiacha haki, mazuri huwa mabaya kwake na mabaya huwa mazuri kwake, na hulewa ulevi wa upotevu.”
Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhahiri.
Haya wameyakari mara nyingi. Miongoni mwayo ni yale yaliyo katika Juz. 7 (6:7).
Ati tukishakufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? Hata baba zetu wa zamani?
Maana yako wazi. umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz. 13 (13:5), Juz. 15 (17: 98), Juz. 18 (23: 82) na Juz. 20 (27:68)
Sema: Naam! Na hali nyinyi ni madhalili. Na hakika ni ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
Yaani sema ewe Muhammad, kuwaambia wale wanaopinga ufufuo: ndio, nyinyi mtafufuliwa kutoka kwenye makaburi yenu kwa neno moja tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mtakusanywa kwake mkiwa madhalili na mtaiona adhabu mliyokuwa mkiikadhibisha kwa macho yenu.
Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. Hii ndiyo Siku ya upambanuzi
-baina ya haki na batili -mliyokuwa mkiikadhibisha.
Haki inapowajia wanapokuwa na fursa ya kuifanyia kazi, wanasema huu ni uwongo na uchawi, hauamini ila mjinga mwenye kuhadaliwa. Na wakati ukipita ukaja wakati wa malipo na kuonja ubaya wa matendo yao, watasema: Ole wetu, sisi tulikuwa kwenye mghafala wa haya, tumejidhulumu wenyewe.
Hali hii mara nyingi inatokea. Mjinga anahangaikia litakalomdhuru, lakini anapopewa nasaha na mwenye akili na kumhadharisha na mwisho mbaya, yeye humdharau na anafura kichwa.
Yakimfika na kutokuwa na pa kukimbilia na kutambua kuwa amehasirika anahangaika na majuto na kusema: laitani nisingelikuwako.
Wakusanyeni waliodhulumu, na wenzao, na hao waliokuwa wakiwaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu.
Aya inaashiria kugawanyika wakosefu; kwamba mshirikina atafufuliwa na washirikina wenzake mahali pamoja kwenye Jahannam wakiwa pamoja na masanamu waliyokuwa wakiyaabudu. Vile vile mwizi pamoja na wezi. Kila aina kwa aina yake; sawa na walivyokuwa duniani.
Waongozeni njia ya Jahannamu!
Ikishamalizika hisabu Malaika wataambiwa: Haya wapelekeni haraka kwenye moto mbaya.
Na wasimamisheni. Hakika hao wataulizwa:
Kabla ya Malaika kuwapeleka kwenye Jahannam watawazuia ili waulizwe yale waliyokuwa wakiyafanya. Katika badhi ya mapokezi imeelezwa kuwa siku hiyo mtu ataulizwa kuhusu alivyomaliza umri wake, mali yake alivyoipata na kuitumia na elimu yake alivyoifanyia kazi.
Ama kulinganisha baina ya Aya hii na ile isemayo:
فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُسْأَلُ عَن ذَنبِهِ إِنسٌ وَلَا جَانٌّ ﴿٣٩﴾
“Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.” (55:39)
Tumekuelezea mara nyingi. Kwa ufupi ni kuwa siku ya mwisho itakuwa na hali ya kuulizwa na ya kutoulizwa. Tazama juzuu hii tuliyo nayo (36:65).
Mna nini? Mbona hamsaidiani?
Yaani kesho wataambiwa wakosefu; kwa nini leo hamsaidiani na kule duniani mlikuwa na mshikamano dhidi ya haki na watu wake. Lengo la swali hili ni kutahayariza.
Bali leo, watasalimu amri.
Watafuata amri ya Mwenyezi Mungu na hawatakuwa na hila yoyote.