17
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٧﴾
27. Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.
قَالُوا إِنَّكُمْ كُنتُمْ تَأْتُونَنَا عَنِ الْيَمِينِ ﴿٢٨﴾
28. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kuume.
قَالُوا بَل لَّمْ تَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٢٩﴾
29. Watasema: Bali nyinyi wenyewe hamkuwa waumini.
وَمَا كَانَ لَنَا عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ بَلْ كُنتُمْ قَوْمًا طَاغِينَ ﴿٣٠﴾
30. Na hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi mlikuwa waasi.
فَحَقَّ عَلَيْنَا قَوْلُ رَبِّنَا إِنَّا لَذَائِقُونَ ﴿٣١﴾
31. Basi kauli ya Mola wetu imekwishatuthibitika. Hakika bila ya shaka tutaonja.
فَأَغْوَيْنَاكُمْ إِنَّا كُنَّا غَاوِينَ ﴿٣٢﴾
32. Tuliwapoteza kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
فَإِنَّهُمْ يَوْمَئِذٍ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ ﴿٣٣﴾
33. Basi hakika wao siku hiyo watashirikiana katika adhabu.
إِنَّا كَذَٰلِكَ نَفْعَلُ بِالْمُجْرِمِينَ ﴿٣٤﴾
34. Hivyo ndivyo tutakavyowafanyia wakosefu.
إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٣٥﴾
35. Wao walipokuwa wakiambiwa: Hapana Mola ila Mwenyezi Mungu (La ilaha illa Llahu) tu, wakijivuna.
وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ ﴿٣٦﴾
36. Na wakisema: Hivi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?
بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٣٧﴾
37. Bali ameleta haki, na amewasadikisha Mitume.
WATAKABILANA WAO KWA WAO
Aya 27 – 37
MAANA
Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kuume.
Neno yamin, tulilolifasiri kwa maana ya kuume, huwa lina maana nyingi; miongoni mwazo ni: mkono, upande usiokuwa wa kushoto na baraka na nguvu. Makusudo hapa ni kupoteza.
Wahalifu wataulizana na kulaumiana wakati watakapoiona adhabu. Wanyonge watawatupia lawama viongozi kuwa kama si nyinyi tunge- likuwa waumini. Hadaa hii wameiletea ibara ya kuume. Kwa sababu waarabu wanakiona kitu kinachokuja kwa upande wa kuume kuwa ni kizuri. Kwa hiyo kusema kwao mkitujia kwa upande wa kuume ni sawa na anayesema umenilenga hasa au umeniwahi kweli. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:38).
Watasema: Bali nyinyi wenyewe hamkuwa waumini. Na hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi mlikuwa waasi. Basi kauli ya Mola wetu imekwishatuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja. Tuliwapoteza kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
Hii ni kauli ya viongozi wakiwajibu wale wanyonge, kwamba sisi kazi yetu ilikuwa ni kutoa mwito na kuupamba, nanyi mkauitikia. Nasi tuliwaita kwenye kufuru mkaitikia na mtume akawaita kwenye imani mkamkimbia, kwa sababu ya uhabithi na upotevu wenu. Vinginevyo sisi tuna uwezo gani juu yenu lau mngeliamua kumwamini Mwenyezi Mungu; kama walivyoamini wengine?
Kwa hiyo basi natija ya ukafiri wetu na upotevu wenu na kutuitikia ni kustahiki kauli ya adhabu kwetu na kwenu; kama muonavyo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 20 (29:25) na Juz. 22 (33:67).
Basi hakika wao siku hiyo watashirikiana katika adhabu.
Haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). Maana yake ni kuwa adhabu itawaangukia wote siku hiyo watakayolaumiana.
Hivyo ndivyo tutakavyowafanyia wakosefu.
Adhabu ya daima bila ya kutofautisha mfuasi na mwenye kufuatwa.
Wao walipokuwa wakiambiwa:Hapana Mola ila Mwenyezi Mungu (La ilaha illa Llahu) tu, wakijivuna.
Walijivuna na wajifanya wakubwa kuliko haki, ndio yakawapata yaliyowapata wajivuni waliokuwa kabla yao.
Na wakisema: Hivi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?
Wafasiri wamesema kuwa washirikina walijichanganya kwenye maneno yao; pale walipomsifu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
kuwa ni mshairi na mwenda wazimu, ambapo mshairi huwa anatumia akili kupangilia maneno yake kwa usanifu wa hali ya juu. Sasa mwendawazimu anaweza kweli kazi hii.
Bali ameleta haki, na amewasadikisha Mitume.
Hapana! Huyo si mshairi wala mwendawazimu isipokuwa ni Mtume mtukufu, ameleta haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na amewasadikisha Mitume waliomtangulia na vitabu vyao.
Baada ya hayo. Kwa hakika mwendawazimu ni bora kuliko yule aliyemsifu Muhammad,(s.a.w.
w
)
aliyeteulia na Mwenyezi Mungu na kumchagua kwa ujumbe wake na kumjaalia ni bwana na mwisho wa Mitume, kuwa ni mwendawazimu. Tazama tafsri ya (36:69) katika Juzuu hii tuliyo nayo.
إِنَّكُمْ لَذَائِقُو الْعَذَابِ الْأَلِيمِ ﴿٣٨﴾
38. Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.
وَمَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٣٩﴾
39. Wala hamtalipwa ila mliyokuwa mkiyafanya.
إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ ﴿٤٠﴾
40. Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliotakaswa.
أُولَـٰئِكَ لَهُمْ رِزْقٌ مَّعْلُومٌ ﴿٤١﴾
41. Hao ndio watakaopata riziki maalum.
فَوَاكِهُ وَهُم مُّكْرَمُونَ ﴿٤٢﴾
42. Matunda, nao watahishimiwa.
فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٤٣﴾
43. Katika Bustani za neema.
عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٤٤﴾
44. Wako juu ya viti wameelekeana.
يُطَافُ عَلَيْهِم بِكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ ﴿٤٥﴾
45. Wakizungushiwa kikombe cha chemchem.
بَيْضَاءَ لَذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ ﴿٤٦﴾
46. Cheupe kitamu kwa wanywao.
لَا فِيهَا غَوْلٌ وَلَا هُمْ عَنْهَا يُنزَفُونَ ﴿٤٧﴾
47. Hakina madhara, wala hakimaliziki.
وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ عِينٌ ﴿٤٨﴾
48. Na watakuwa nao wanawake wenye macho makunjufu.
كَأَنَّهُنَّ بَيْضٌ مَّكْنُونٌ ﴿٤٩﴾
49. Kama kwamba wao ni mayai yaliyohifadhika.
JUU YA VITANDA WAMEELEKEANA
Aya 38 – 49
MAANA
Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.Wala hamtalipwa ila mliyo kuwa mkiyafanya.
Baada ya Mwenyezi Mungu kusema kuwa wakosefu watashirikiana katika adhabu, sasa anawaambia kuwa adhabu yao ni malipo ya yaliyochumwa na mikonoi yao, wala hawatadhulumia hata chembe.
Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliotakaswa. Hao ndio watakaopata riziki maalumu.
Hii ni desturi ya Qur’an, kuwataja wakosefu na adhabu yao kisha kufuatia kuwataja wema na malipo yao. Malipo yenyewe kwa ujumla ni riziki maalum ya Mwenyezi Mungu kwa ajili yao.
Ama ufafanuzi wa riziki hiyo ni kama ifuatavyo:
Matunda,
wanayoyatamani,nao watahishimiwa.
Kwa sababu matunda na kudharauliwa ni sumu na huzuni. Kuna mithali isemayo: “Niheshimu wala usinilishe”
Katika Bustani za neema,
zinazopitiwa na mito.Wako juu ya viti wamekabiliana,
wakiangaliana kwa raha na furaha
Wakizungushiwa kikombe cha chemchem.
Vijana watawapatia kinywajicheupe kitamu kwa wanywao,
chenye rangi na ladha nzuri.Hakina madhara,
Hakiumizi kichwawala kuleta maumivu wala hakimaliziki.
Neno nazaf likitumika kwenye kinywaji lina maaana ya kumalizika na likitumika kwa mtu lina maana ya kuisha akili yake; ndio maana baadhi ya wafasiri wakasema “Hakiwaleweshi;” yaani kinywaji hakimalizi akili yao.
Na watakuwa nao wanawake wenye macho makunjufu
Matunda, heshima, furaha, watumishi na zaidi ya hayo ni wanawake safi warembo wenye macho makunjufu na mazuri,kama kwamba wao ni mayai yaliyohifadhika.
Kuwa kama mayai ni kinaya cha usafi wao na kuwa hawajaguswa na mikono wala kutazamwa na mcho.
WANAWAKE NA WATUMISHI
Hivi karibuni nilipata barua kutoka kwa mwananfunzi mmoja wa kike wa Kuwait, ikisema kuwa alikuwa na mazungumzo na rika lake. Yeye akasema kuwa Uislamu haumtofautishi mwanamume na mwanamke.
Wenzake wakampinga na kumwambia kuwa Qur’an imeelezea wazi kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawalipa wanaume wema mahurulaini na hakusema vile atakavyowalipa wanawake wema. Kama haki ingelikuwa sawa, basi malipo yangelikuwa ya aina moja. Msichana anasema alishindwa kujibu na akataka nimwandikie ili awakinaishe wenzake.
Majibishano haya mazuri yanatufahamisha kuwa mwanamke ni sawa na mwanamume katika mataminio yake ya kimwili na mapendeleo yake. Na kwamba kupata mume ndio malipo bora zaidi, kama ilivyo kwa mwana- mume kupata mke. Vile vile inatufahamisha kuwa wivu wa mwanamke kwa mwanamume ni kama wa mwanamume.
Basi nikamjibu hivi: “Qur’an imeelezea waziwazi usawa baina ya mwanamume na mwanamke kama msingi wa ujumla. Kwenye hilo inasema:
أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ ﴿١٩٥﴾
“ …kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke” Juz. 4 (3:195).
“Mwenye kufanya mema - mwanamume au mwanamke - hali ya kuwa ni mwenye kuamini, basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kitobwe cha kokwa ya tende.” Juz. 5 (4:124).
Hakuna mwenye shaka kwamba atakayeingia Peponi atapata kila kinachotamaniwa na nafsi na kuburudisha macho awe mwanamume au mwanamke, kama ilivyoelezwa kwenye (43:71).
Vile vile Qur’an imewataja watumishi kama ilivyowataja Hurulaini. Ilipowasifu Hurulaini kuwa ni kama mayai yaliyohifadhika, pia imewataja watumishi kuwa ni lulu iliyotawanywa, kama iliyosemwa kwenye. (76:19)
Sio mbali kuwa kunyamazia kutaja kuwa mwanamke atalipwa kwa kijana mzuri kumefuata ada na desturi iliyozoeleka kwa watu ya kumzungumzia kijana kuoa na kumuuliza, kwa nini huoi? Lakini hawamuulizi msichana, kwa nini huolewi; kwa vile wanakuwa na haya sana. Wakale walisema: “Ana haya kama msichana.”
Vile vile imesemekana kuwa ladha za Peponi zote ni za kiroho si za kimaada au jinsia, na kwamba kutaja hurilaini, matunda na vikombe ni kama ishara na alama ya ladha ya kimwili kwenye ladha ya kiroho na kwamba viti na vitanda ni kinaya cha cheo na daraja.
فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٥٠﴾
50. Tena watakabiliana wao kwa wao wakiulizana.
قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ إِنِّي كَانَ لِي قَرِينٌ ﴿٥١﴾
51. Aseme msemaji miongoni mwao: Hakika mimi nilikuwa na rafiki.
يَقُولُ أَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُصَدِّقِينَ ﴿٥٢﴾
52. Aliyekuwa akiniambia: Hivyo wewe ni katika wanaosadiki.
أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَدِينُونَ ﴿٥٣﴾
53. Ati tukishakufa tukawa udongo na mifupa, ndio tutahisabiwa?
قَالَ هَلْ أَنتُم مُّطَّلِعُونَ ﴿٥٤﴾
54. Atasema: Je! Nyie mtachungulia?
فَاطَّلَعَ فَرَآهُ فِي سَوَاءِ الْجَحِيمِ ﴿٥٥﴾
55. Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
قَالَ تَاللَّـهِ إِن كِدتَّ لَتُرْدِينِ ﴿٥٦﴾
56. Aseme Wallahi! Ulikaribia kuniangamiza.
وَلَوْلَا نِعْمَةُ رَبِّي لَكُنتُ مِنَ الْمُحْضَرِينَ ﴿٥٧﴾
57. Na lau si neema ya Mola wangu bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa waliohudhurishwa.
أَفَمَا نَحْنُ بِمَيِّتِينَ ﴿٥٨﴾
58. Je! Sisi hatutakufa?
إِلَّا مَوْتَتَنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿٥٩﴾
59. Isipokuwa kifo chetu cha kwanza; wala sisi hatutaadhibiwa.
إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٦٠﴾
60. Hakika huku, bila ya shaka, ndiko kufuzu kukubwa.
لِمِثْلِ هَـٰذَا فَلْيَعْمَلِ الْعَامِلُونَ ﴿٦١﴾
61. Kwa mfano wa haya nawafanye wafanyao.
أَذَٰلِكَ خَيْرٌ نُّزُلًا أَمْ شَجَرَةُ الزَّقُّومِ ﴿٦٢﴾
62. Je! Kukaribishwa hivi ni bora, au mti wa Zaqum?
إِنَّا جَعَلْنَاهَا فِتْنَةً لِّلظَّالِمِينَ ﴿٦٣﴾
63. Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni fitna kwa waliodhulumu.
إِنَّهَا شَجَرَةٌ تَخْرُجُ فِي أَصْلِ الْجَحِيمِ ﴿٦٤﴾
64. Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Moto.
طَلْعُهَا كَأَنَّهُ رُءُوسُ الشَّيَاطِينِ ﴿٦٥﴾
65. Mashada yake ni kama vichwa vya mashetani.
فَإِنَّهُمْ لَآكِلُونَ مِنْهَا فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٦٦﴾
66. Basi hakika hao bila ya shaka watakula katika huo, na wajaze matumbo kwa huo.
ثُمَّ إِنَّ لَهُمْ عَلَيْهَا لَشَوْبًا مِّنْ حَمِيمٍ ﴿٦٧﴾
67. Kisha juu yake wapewe mchanganyiko wa maji ya moto.
ثُمَّ إِنَّ مَرْجِعَهُمْ لَإِلَى الْجَحِيمِ ﴿٦٨﴾
68. Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
KWA MFANO WA HAYA NAWAFANYE WAFANYAO
Aya 50 – 68
MAANA
Tena watakabilaiana wao kwa wao wakiulizana.
Bado maneno yanaendelea kuhusu watu wa Peponi. Katika Aya iliyotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema kuwa watu wa Peponi watakuwa na aina mbali mbali za starehe.
Katika Aya hii anasema kuwa watazungumziana wao kwa wao, huku wakiwa na furaha, kuhusiana na maisha yao ya duniani. Miongoni mwayo ni:
Aseme msemaji miongoni mwao: Hakika mimi nilikuwa na rafiki aliyekuwa akiniambia: Hivyo wewe ni katika wanaosadiki ati tukishakufa tukawa udongo na mifupa, ndio tutahisabiwa?
Mumin huyu atawazungumzia wenzake na jirani zake kuhusiana na vile waumini wa malipo ya kiyama walivyokuwa wakifanyiwa masikhara wakisema wasioamini, ati mamake fulani, kweli tukishakufa na kuisha kabisa tutafufuliwa tuwe hai?
Hivi ndivyo alivyo kila mlahidi. Na hiyo hasa inatokana na kuwa kuamini ufufuo ni sehemu ya kuamini wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa yule aliyemteua katika waja wake. Ikiwa mlahidi haamini wahyi huu, ataweza kweli kuamini ufufuo baada ya mauti? Kwa maneno mengine ni kuwa ufufuo ni katika mambo ya ghaibu ambayo kwa mlahidi ni vigano tu.
Atasema: Je! Nyie mtachungulia?
Mumin ataendelea kuwaambia wenzake akiwaomba waangalie Jahnnam ili waone mwisho wa aliyekuwa na dharau.
Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
Akishawaambia wenzake atachungulia kwenye Jahannam amwone jamaa yuko katikati ya Jahannam.Aseme
- kwa kumtahayariza-Wallahi! Ulikaribia kuniangamiza.
Yaani kunitia kwenye shaka kwa wasiwasi wako na shaka zako.Na lau si neema ya Mola wangu bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa waliohudhurishwa
pamoja nawe katika moto.
Kisha mumin atawageukia wenzake awaambie:
Je! Sisi hatutakufa, isipokuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. Hakika huku, bila ya shaka, ndiko kufuzu kukubwa.
Atazungumza haya kwa furaha kutokana na aliyoyapata huku akisema alhamudulillah, tumepita mtihani vizuri, hakuna mauti tena wala tabu. Hakuna isipokuwa radhi za Mwenyezi Mungu na neema zake. Katika maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hawataonja humo isipokuwa mauti ya kwanza na atawakinga na adhabu ya moto” (44:57).
Kwa mfano wa haya nawafanye wafanyao na washindane wanaoshindana.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaachia waja matendo na amali, akawajibishia kufanya yale yaliyo na kheri nao na masilahi kwao; na akawakataza yale yaliyo na shari yao na ufisadi. Kisha akwaachia hiyari ya kufanya na kuacha. Mwenye kutii akamwahidi Pepo na mwenye kuasi akamwahidi adhabu ya kuunguza.
Hakuna mwenye shaka kuwa mwenye akili atajihurumia na kuchagua lililo na masilahi zaidi. Imeelezwa kwenye Nahjul-balagha: “Hakuna thamani ya nafsi zenu ispokuwa Pepo. Basi msiziuze ila kwayo.”
Je! Kukaribishwa hivi ni bora, au mti wa Zaqum? Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni fitna kwa waliodhulumu.
Kukaribishwa hivi ni kukaribishwa kwenye neema. Makusudio ya fitna hapa ni adhabu. Ama mti wa Zaqum ameubanisha Mwenyezi Mungu kwa kusema:
Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Moto. Mashada yake ni kama vichwa vya mashetani. Basi hakika hao bila ya shaka wataku- la katika huo, na wajaze matumbo kwa huo.
Zaqqum ni kauli ya waarabu kwa chakula kinachochukiza kukila. Kwenye Tafsir Tabari kuna maelezo Haya: “Iliposhuka Aya hii Abu Jahl alisema kwa madharau: “Mimi nitawaletea Zaqqum.” Akaleta siagi na tende kisha akasema: Haya! Nyinyi kuleni Zaqqum. Basi hii ndio Zaqqum anayowatisha nayo Muhammad.
Vichwa vya mashetani, ni kinaya cha ubaya na mandhari ya kutisha ya huo mti. Yule anayesema kuwa Zaqqum ni nembo ya ubaya wa adhabu, hatuwezi kumpinga.
Kisha juu yake wapewe mchanganyiko wa maji ya moto.
Yaani watakula zaqqum na wanywe maji ya usaha; kama anavyosema Mwenyezi Mungu: “Nyuma yake iko Jahannam na atanyeshwa maji ya usaha uliochanganyika na damu” Juz.13 (14: 16).
Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
Makusudio ya marejeo ni makazi ya mwisho na makao yao ya kudumu. Maana ni kuwa chakula chao ni Zaqqum na kinywaji chao ni maji moto. Ama kivazi chao, Mwenyezi Mungu amekiashiria kwa kusema:
سَرَابِيلُهُم مِّن قَطِرَانٍ ﴿٥٠﴾
“Nguo zao zitakuwa za lami” Juz. 13 (14:50).