19
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾
100. Ewe Mola wangu! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿١٠١﴾
101. Basi tukambashiria mwana aliye mpole.
فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿١٠٢﴾
102. Basi alipofika makamo ya kuhangaika pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa. Utanikuta mimi, Inshallah, katika wanaosubiri.
فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿١٠٣﴾
103. Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.
وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿١٠٤﴾
104. Tulimwita: Ewe Ibrahim!
قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١٠٥﴾
105. Umekwishaisadikisha ndoto. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْبَلَاءُ الْمُبِينُ ﴿١٠٦﴾
106. Hakika haya ni majaribio yaliyo dhahiri.
وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾
107. Na tukamfidia kwa dhabihu adhimu.
وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿١٠٨﴾
108. Na tukamwachia kwa walio baadaye.
سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿١٠٩﴾
109. Amani kwa Ibrahim.
كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١١٠﴾
110. Hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١١﴾
111. Hakika yeye ni katika waja wetu waumini.
وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَاقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١١٢﴾
112. Na tukambashiria Is-haq, Nabii miongoni mwa watu wema.
وَبَارَكْنَا عَلَيْهِ وَعَلَىٰ إِسْحَاقَ وَمِن ذُرِّيَّتِهِمَا مُحْسِنٌ وَظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ مُبِينٌ ﴿١١٣﴾
113. Na tukambarikia yeye na Is-haq na miongoni mwa dhuriya zao yuko mwema na mwenye kudhulumu nafsi yake waziwazi.
NIMEONA USINGIZINI KUWA NINAKUCHINJA
Aya 100 – 113
MAANA
Ewe Mola wangu! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
Ibrahim alifikia uzee sana, wala hakuruzukiwa mtoto. Akamuomba Mola wake ampe kizazi cha waumini na warithi wema.
Basi tukambashiria mwana aliye mpole
ambaye ni Ismail, hilo halina shaka, kwa ushahidi wa Qur’an. Ufafanuzi utakuja baada ya tafsiri ya Aya hizi tulizo nazo.
Basi alipofika makamo ya kuhangaika pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchin- ja. Basi angalia, waonaje?
Yaani alipofikia Ismail umri wa kuhangaika pamoja na baba yake. Ibrahim aliota kuwa anamchinja mwanawe. Kafahamu kutokana na ndoto hii kuwa amchinje au amlete machinjioni mwanawe. Na fahamu ya manabii ni yakini. Ndio maana akaamua kuitekeleza ndoto yake. Akampa habari mwanawe na kumtaka maoni yake.
Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa.
Alimjibu bila ya kusita kuwa mimi sina maoni wala amri yoyote kwenye amri ya Mwenyezi Mungu na amri yako. Nichinje tu maisha yangu hayana thamani yoyote mbele ya radhi za Mwenyezi Mungu na rdhi zako. Nikate kichwa na bado wewe utakuwa unanihurumia, maadamu unatekeleza radhi za Mwenyezi Mungu na kuitikia mwito wake.
Kisha Ismail akawa anampoza baba yake na kumwambia:Utanikuta mimi, Inshallah, katika wanaosubiri
na kuwa mvumilivu kuweza kukabili kuchinjwa.
Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji, tulimwita: Ewe Ibrahim! Umekwishaisadikisha ndoto. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Ismail aliponyoosha shingo yake na Ibrahim akapeleka kisu chake, kila mmoja wao akimwachia Mungu, ulikuja mlingano kutoka amri ya juu kwamba hii ndio tafsiri ya ndoto yako - azimio la kujitolea kwako kuchinja kwa ajili ya ikhalasi ya Mwenyezi Mungu na Ismail kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu kwa moyo safi. Kwa hiyo kuchinja halikuwa ndio lengo.
Unaweza kuuliza
: Ikiwa lengo halikuwa kuchinja, basi kulikuwa na haja gani ya kuamrishwa?
Jibu
: baadhi wanasema kuwa lengo la hilo ni kudhihirisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa watu na vizazi vitakvyokuja, utukufu wa Ibrahim na mwanawe Ismail walivyojitolea muhanga na ikhlasi yao.
Wawe ni sehemu ya kutukuzwa na tukufu hadi ufufuo. Wengine wakasema ni kwa ajili ya kuugeuza wivu wa Sara kwa Hajar, mama wa Ismail na kuzuia ugumu wake kwa Ibrahim.
Nasi tunaongeza kwenye kauli mbili hizo, kuwa vile vile Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alitaka kutoa mfano wa mumin wa haki, kwamba ni yule anayemtii Mwenyezi Mungu katika kila jambo, hata ikibidi kumchinja mwanawe aliye nyongo mkalia ini. Hili linaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):
Hakika haya ni majaribio yaliyo dhahiri.
Yaani azimio hili la kujitolea muhanga kwa hali na mali kwa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio uthibitisho wa kweli wa mumin na ndio msitari unaogawanya baina ya mumin wa kweli na yule mwenye kuleta njozi za kuwa ni mumin, kumbe si chochote.
Na tukamfidia kwa dhabihu adhimu.
Makusudio ya dhabihu hapa ni mnyama wa kuchinjwa. Inasemkana alikuwa kondoo, wengine wakasema ni mbuzi. Sisi hatuna majukumu ya kujua aina ya fidia ilivyokuwa, wala jambo hilo halina uhusiano wa mbali au karibu na maisha yetu.
La kushangaza zaidi ni kauli ya aliyesema kuwa alikuwa ni kondoo aliyelisha Peponi miaka arubaini na kwamba Ibrahim
alimpa Ibilisi wengu na kordani zake. Ikiwa alichunga Peponi miaka arubaini, basi uzito wake utakuwaje?
Na tukamwachia kwa walio baadaye. Amani kwa Ibrahim. Hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema. Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.
Zimetangulia Aya hizi kwa herufi zake kwenye sura hii Aya (78 – 81).
Na tukambashiria Is-haq, Nabii miongoni mwa watu wema. Na tukambarikia yeye na Is-haq.
Bishara hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim kupata mtoto wa pili, ni malipo ya subira yake na kumtoa mtoto wake kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu.
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa kuwa Sara alimzaa Is-haq akiwa na mika 90 na Ibrahim akiwa na miaka mia, na kwamba maana ya neno Is-haq katika Lugha ya Kiebrania ni kucheka. Ama Hajar alimzaa Ismail na umri wa Ibrahim ni miaka 86.
Na miongoni mwa dhuriya zao yuko mwema na mwenye kudhulumu nafsi yake waziwazi.
Mwema katika kizazi hiki ni yule anayefuata mila ya Ibrahim na mwenye kujidhulumu ni yule aliyeiwacha mila hiyo.
JE, DHABIHU ALIKUWA ISMAIL AU IS-HAQ?
Baadhi wamesema kuwa mtoto wa Ibrahim aliyetakiwa kuchinjwa ni Is-haq na wala siye Ismail. Kauli hii haina rejea isipokuwa Hadith za kiisrail za Ka’bul-ahbar na hasadi ya mayahudi kwa watoto wa Ismail. Hili si la kushangaza kwa waisrail. Ama dalili za kuwa aliyetaka kuchinjwa ni Ismail ni kama zifuatazo:-
Kwanza
: Kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Basi tukambashiria mwana aliye mpole. Basi alipofika makamo ya kuhangaika pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja,’ inafahamisha waziwazi kuwa aliyebashiriwa, aliyehangaika naye na aliyetaka kuchinjwa ni mtu mmoja tu ambaye ni mtoto wa kwanza wa Ibrahim. Na mtoto wa kwanza ni Ismail, kwa maafikano ya waislamu, wanaswara na wayahudi.
Biblia inasema: “Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajir alipomzalia Abramu Ishmael”
Mwanzo 16:16. Pia inasema: “Ndipo Ibrahim akaanguka kifudifidi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? Tukiunganisha vifungu viwili hivi, maana yanayopatikana ni kuwa Ismail ni mkubwa wa Is-haq kwa mika 14.
Pili
: Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na tukambashiria Is-haq, Nabii miongoni mwa watu wema,’ ambapo bishara hii ilikuwa ni malipo ya utiifu wake Ibrahim kwa Mungu kumchinja mwanawe. Bila shaka malipo yanakuja baada ya kazi. Kwa hiyo Is-haq alipatikana baada ya Ismail.
Tatu
: Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.” Juz. 12 (11: 71). Vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) atoe bishara ya Is-haq kumzaa Ya’qub kisha wakati huohuo aamr- ishwe achinjwe, kabla ya kupatikana Ya’qub?
Nne
: Kama aliyetaka kuchinjwa alikuwa ni Is-haq basi ingelazimika kuchinja, kufanya sa’yi na kupiga vikuta vya shetani kuwe kwenye ardhi ya Sham alipokuwa Sara na mwanawe Is-haq na wala kusingekuwa Makka alipokuwepo Hajar na mwanawe Ismail.
وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿١١٤﴾
114. Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Harun.
وَنَجَّيْنَاهُمَا وَقَوْمَهُمَا مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ ﴿١١٥﴾
115. Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na tabu kubwa.
وَنَصَرْنَاهُمْ فَكَانُوا هُمُ الْغَالِبِينَ ﴿١١٦﴾
116. Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio washindi.
وَآتَيْنَاهُمَا الْكِتَابَ الْمُسْتَبِينَ ﴿١١٧﴾
117. Na tukawapa wawili hao Kitabu kinachobainisha.
وَهَدَيْنَاهُمَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿١١٨﴾
118. Na tukawaongoza kwenye njia Iliyonyooka.
وَتَرَكْنَا عَلَيْهِمَا فِي الْآخِرِينَ ﴿١١٩﴾
119. Na tukawachia kwa walio baadaye.
سَلَامٌ عَلَىٰ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿١٢٠﴾
120. Amani kwa Musa na Harun.
إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١٢١﴾
121. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
إِنَّهُمَا مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٢٢﴾
122. Hakika hao ni katika waja wetu walio waumini.
وَإِنَّ إِلْيَاسَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٢٣﴾
123. Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٢٤﴾
124. Alipowaambia watu wake: Hamna takua?
أَتَدْعُونَ بَعْلًا وَتَذَرُونَ أَحْسَنَ الْخَالِقِينَ ﴿١٢٥﴾
125. Mnamwomba Baa’li na mnamwacha Mbora wa waumbaji.
اللَّـهَ رَبَّكُمْ وَرَبَّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٢٦﴾
126. Mwenyezi Mungu, Mola wenu na Mola wa baba zenu wa zamani?
فَكَذَّبُوهُ فَإِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ ﴿١٢٧﴾
127. Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa.
إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ ﴿١٢٨﴾
128. Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa.
وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿١٢٩﴾
129. Na tukamwachia kwa walio baadaye.
سَلَامٌ عَلَىٰ إِلْ يَاسِينَ ﴿١٣٠﴾
130. Amani kwa Ilyasin.
إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣١﴾
131. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٣٢﴾
132. Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.
MUSA NA ILYAS
Aya 114 – 132
MAANA
Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Harun.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfanyia hisani Musa na Harun kwa utume, utajo wa kudumu na kuwashinda maadui. Utume hauwi kwa bidii ya mtu au kazi yake; isipokuwa unatokana na uteuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake.” Juz. 8 (6:124).
Ndio maana utume haufungamani na taklifa yoyote. Kwa hiyo mtu haambiwi kuwa Mtume; kama anavyoambiwa kuwa na takua.
Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na tabu kubwa.
Tabia ya mayahudi ni kukubali kila kitu kwa ajili ya mali; ikibidi hata udhalili na aibu. Hivi ndivyo ilivyowazungumzia historia yao.
Firauni aliwafanya watumwa na hawakufanya lolote mpaka Mwenyezi Mungu alipowapa msaada wa Musa kuwatoa kwenye tabu na shida na kupata faraja.
Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio washindi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwangamiza Firauni na askari wake, waisrail wakakomboka na utumwa na udhalili.
Na tukawapa wawili hao Kitabu kinachobainisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimteremshia Musa na Harun Tawrat ndani yake mkiwa na hukumu zilizo waziwazi.
Na tukawaongoza kwenye njia Iliyonyooka,
njia ya haki na uadilifu.Na tukawachia kwa walio baadaye,
utajo mzuri na sifa njema.Amani kwa Musa na Harun
kutoka kwa Mwenyezi Mungu hapa duniani na akhera.
Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema. Hakika hao ni katika waja wetu walio waumini.
Yaani malipo ya wema ni wema tu. Yamepita maelezo kuhusu Musa na Harun katika Aya nyingi.
Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
Wafasiri wanasema kwamba Ilyas ni mmoja wa manabii wa Bani Israil na kwamba nasabu yake inakomea kwa Harun. Kwenye Tafsiri nyingi imeelezwa kuwa Ilyas huyu ndiye Idris aliyetajwa kwenye Juz. 16 (19:56) na Juz. 17 (21:85).
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeelezwa kuwa neno Iliy ni la kiebrania lenye maana ya Mungu wangu na neno la Kigiriki lenye maana hii ni Ilyas. Pia mara nyingine hutumika katika lugha ya Kiarabu.
Alipowaambia watu wake: Hamna takua?
Aliwaongoza watu wake kwenye tawhidi na kuwahadharisha na shirki, kama walivyofanya mitume wengine.
Mnamwomba Baa’li na mnamwacha Mbora wa waumbaji, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?
Baa’ali ni jina la sanamu, kama unavyofahamisha mfumo wa Aya. Kwenye Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa: “Baa’ali ni jina la Kikanaa’ni na maana yake ni Mola wa ahadi.”
Watu wa Ilyas waliabudu Baa’al, kama walivyoabudu masanamu waliokuwa kabla yao; ndio akawalingania kwenye tawhid; kama alivyofanya Nuh, Ibrahim, Musa na mitume wengineo.
Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa.
Yaani walokadhibisha mwito wake, watahudhurishwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na adhabu.
Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa
ambao waliitika mwito wa Ilyas. Hakika wao wataokoka na adhabu na wana wao malipo mema.
Na tukamwachia kwa walio baadaye utajo mwema.
Amani kwa Ilyasin. Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema. Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa jina la baba yake Ilyas ni Yasin na kwamba makusudio ya Ilyasin ni Ilyas hasa, kwa sababu mtoto ni katika watu wa baba.
Vyoyvote iwavyo, makusudio ya Ilyasin hapa ni Ilyas kutokana na mfumo wa mtiririko wa Aya. Kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwenye Aya za nyuma amamtaja Nuh kisha akasema: ‘Amani kwa Nuh,’ akamtaja Ibrahim, akasema: ‘Amani kwa Ibrahim.
Vile vile alipomtaja Musa na Harun. Kisha alipomtaja Ilyas kuwa ni katika Mitume alifuatishia kwa kusema: ‘Amani kwa Ilyasin’ ikajulikna kwamba makusudio ni Ilyas tu.