2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
قُلِ اللَّـهُمَّ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِي مَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٤٦﴾
46. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyokuwa wakikhitalifiana.
وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَبَدَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مَا لَمْ يَكُونُوا يَحْتَسِبُونَ ﴿٤٧﴾
47. Na lau kuwa waliodhulumu wangelikuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikomboa katika adhabu mbaya Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyokuwa wakiyatazamia.
وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na utawadhihirikia ubaya wa waliyoyachuma, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
فَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَانَا ثُمَّ إِذَا خَوَّلْنَاهُ نِعْمَةً مِّنَّا قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ بَلْ هِيَ فِتْنَةٌ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na dhara inapomgusa mtu hutuomba. Kisha tunapompa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui.
قَدْ قَالَهَا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٥٠﴾
50. Walikwishayasema haya waliokuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَالَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ هَـٰؤُلَاءِ سَيُصِيبُهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٥١﴾
51. Basi ukawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Na wale ambao wamedhulumu miongoni mwa hawa utawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Nao si wenye kushinda.
أَوَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٢﴾
52. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaoamini.
UTAHUKUMU BAINA YAO
Aya 46 – 52
MAANA
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyokuwa wakikhitalifiana.
Aya hii inafungamana na ile iliyotangulia: ‘Na wewe si mlinzi juu yao.’ Maana yake yako wazi. Kwa ufupi ni, sema ewe Muhammad, baada ya kufikisha ujumbe na kutoa nasaha: ewe Mwenyezi Mungu wewe ni muumba wa ulimwengu, Mfalme wa wafalme, Mjuzi wa yaliyoko kwangu na kwa wakadhibishaji. Hukumu ni yako peke yako katika kila kuhitalifiana na kuzozana baina ya waja wako kwenye maisha haya.
Na lau kuwa waliodhulumu wangelikuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikomboa katika adhabu mbaya Siku ya Kiyama. Na yatawadhi- hirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyokuwa wakiyatazamia.
Walikuwa wakipupia dunia na wakikusanya mali juu mali, wakiwa wameghafilika na kukutana na Mwenyezi Mungu na hisabu yake. Wakati watakaposimima mbele yake kwa ajili ya hisabu na kuwafunukia waliyokuwa wakiyapuuza, basi watauma mikono wakijuta. Lakini wapi!
Jahannam haiwezi kukombolewa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:91), Juz. 11 (10: 54) na Juz. 13 (13:18)
Na utawadhihirikia ubaya wa waliyoyachuma, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
Walikuwa wanapoambiwa iogoponi siku ambayo mtarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu, walikuwa wakiifanyia masikhara kauli hii na yule aliyeisema.
Lakini watakapohudhurishwa siku iliyoagwa, hapo ndio haki- ka itawadhihirikia na adhabu itawashukia kulingana na msimamo wao wa madharau na kumdharau yule aliyewaonya.
UDHURU MBAYA KULIKO DHAMBI
Na dhara inapomgusa mtu hutuomba. Kisha tunapompa neema zitokazo kwetu, husema: ‘Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu.’
Makusudio ya mtu hapa ni kila mwenye sifa hiyo iliyotajwa ambaye anamtaka msaada Mwenyezi Mungu wakati wa shida na kumsahau wakati wa raha huku akisema kwa kujidai: ‘Neema hii ni kwa mipango na ufundi wangu.’
Wakati nikiandika maneno haya, nimekumbuka siasa ya Marekani aliyoitangaza Rusk, alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, alisema: “Hapana budi kwa Marekani kuonyesha umuhimu wake katika dunia nzima, ikiwemo anga yake, maji yake na pambizo zake zinazoizunguka.”
Anamaanisha kuwa ni lazima Amerika itawale dunia yote na vilivyomo ndani yake.
Tangazo hili lilikuwa mnamo mwaka 1966, kabla ya Marekani kupeleka chombo chake mwezini. Kwa hiyo ingelikuwa leo angeuanganisha mwezi na sayari nyinginezo.
Baada ya magazetu ya kimataifa kutangaza siasa hii ya kikoloni, aliyoitangaza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Amerika, kibaraka mmoja aliandika makala ya kutetea siasa hii, kwa kusema:
“Marekani ndio dola kubwa kielimu na kiutajiri. Imeonyesha ushindi mkubwa katika uwanja wa elimu na viwanda. Kwa hiyo basi inayo haki ya kuingilia ulimwengu kwa sura mbalimbali, kutawala kila inachokitaka, kugeuza kanuni za nchi yoyote, vile inavyotaka, na kuielekeza kiuchumi, kuiwekea bajeti yake na kuipangia nchi hiyo itakachouza nje na itakochonunua.
Vile vile Marekani inayo haki ya kutumia siasa kwenye nchi yoyote kwa mfumo wowote, hata ikibidi kutumia nguvu, kwa mapinduzi ya kijeshi na kuunga mkono harakati za upinzani, ili kuleta utulivu.
Marekani inayo haki hii na zaidi, kwa sababu:
kwanza
: Haki hii ni ya kielimu.
Pili
: Marekani inamiliki silaha za maangamizi, na kila mwenye kumilki silaha hizi ana haki ya kutawala dunia nzima na vilivyomo ndani yake.”
Yote yaliyoandikwa kwenye makala hii kupitia mwandishi huyu ni ubainifu wa siasa halisi ya Marekani kama ilivyo. Mwenye kutaka kuhakikisha haya naangalie siasa ya Marekani katika Vietnam, Asia, Afrika na Latin Amerika.
Vile vile msimamo wake wa kiadui kwa nchi za kiarabu, jinsi inavyotoa msaada usiokuwa na mpaka kwa adui Israil na inavyopinga jaribio lolote la amani katika tatizo la Palestina na mahali popote penye tatizo mashariki na magaharibi.
Mzandiki huyu aliyejitolea kuitetea Marekani, kubariki siasa zake na kusema kuwa inayo haki ya kushibisha matamanio yake ya kiuadui, kwa kuwa eti inamiliki viwanda vya silaha, tunamuuliza hivi: Ikiwa elimu inaruhusu kuua, kubomoa na kupora, maana yake ni kuwa elimu ni ya shari sio ya heri na ni ya ufisadi wala sio ya utengenezaji?
Na kwamba mwenye elimu anayoruhusa kuitumia elimu yake kuiba, kudanganya na kuzua? Na mwizi atakuwa ni mwenye kushukuriwa na kulipwa; na kila anavyozidi kuwa hodari wa hatia na kuwa na ufisadi mwingi na upotevu basi atakuwa anastahiki heshima?
Ikiwa elimu inaboresha uadui, kwanini basi Marekani inainua nembo za haki za binadamu na kujaribu kila juhudi kuwakinaisha watu kwamba wao wanafanya ibada wana zuhudi na wanupiga vita ukomonisti kwa jina la imani ya Mungu na siku ya mwisho?
Zaidi ya hayo mzushi huyu mwenye dhambi amaesahau kuwa anafichua hiyana yake na upotevu wake, huku akiwa anatetea matamanio ya Marekani kwa mantiki yake ya kufedhehesha akitoa udhuru kwa yaliyo mabaya zaidi ya dhambi yake.
Sio! Huo ni mtihani!
Makusudio ya mtihani hapa ni neema. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamneemesha mja wake ili amjaribu kuwa atashukuru au atakufuru. Akishukuru humzidishia neema duniani na malipo akhera, na akikufuru basi Jahannam imeandaliwa makafiri.
Lakini wengi wao hawajui
kuwa Mwenyezi Mungu anawapa mtihani waja wake ili vidhihirike vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu.
Walikwishayasema haya waliokuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
Yaani haya ya kusema kuwa nimepewa kwa elimu yangu. Maana ni kuwa msemaji huyu mjinga ana wanaofanana naye katika historia, lakini mali haikuwazuia na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake iliyotolewa kiaga. Tazama Juz. 20 (28:76-82).
Basi ukawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Na wale ambao wamedhulumu miongoni mwa hawa - waliomkadhibisha Muhammad – utawasibu ubaya wa waliyoyachuma.
Mwenye kufanya wema atalipwa nao wala hatapata msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hii imethibiti kwa wote bila ya kuvua wala kuhusika na uma zilizotangulia au zijazo. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.
Nao si wenye kushinda.
Kwani inawezekana muumbwa kumshinda muumba wake?
Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaoamini.
Umetangulia mfano wake katika Juzuu zifuatazo: Juz.13 (13:27), Juz.15 (17:30), Juz.20 (28:82), Juz.21(29:62), Juz.21 (30:37) na Juz.22 (34:36,39).
Na tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hili katika Juzuu zifuatazo: Juz. 6 (5:64-66), kifungu cha ‘Riziki na ufisadi,’ Juz. 7 (5:100) kifungu ‘Je riziki ni bahati au majaliwa?’ Juz. 13 (13:26-29) kifungu ‘Mtu na riziki’ na Juz. 20 (29:56-63) kifungu ‘Riziki na kumtegemea Muumba si kiumbe.’
قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾
53. Sema: Enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ ﴿٥٤﴾
54. Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni kwake, kabla ya kuwajia adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.
وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ ﴿٥٥﴾
55. Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijawajia adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ ﴿٥٦﴾
56. Isije ikasema nafsi: Ee masikitiko yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu; na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!
أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴿٥٧﴾
57. Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye takua.
أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٨﴾
58. Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.
بَلَىٰ قَدْ جَاءَتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٥٩﴾
59. Wapi! zilikwishakujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!
MWENYEZI MUNGU ANASAMEHE MADHAMBI YOTE
Aya 53 – 59
MAANA
Sema: Enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Huu ni mwito wa wazi, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa wale waliodhulumu nafsi zao kwa kufanya madhambi na maasi. Akaahidi msamaha kwa kila dhambi kadiri itakavyokuwa kubwa. Kwa hiyo amefungua mlango kwa yule mwenye kutaka kufuta maovu yake yeye mwenyewe na kutengeneza yaliyoharibika.
Kuna Hadith inayosema:“Hakika Mwenyezi Mungu hachoki mpaka mchoke. Mkiacha naye anaacha.”
yaani mkiacha toba naye anaacha maghufira. Katika Hadith nyingine Mtume(s.a.w.
w
)
anasema:“Hakuna ninachopenda zaidi katika dunia na vilivyomo kuliko Aya hii.”
Imekua mashuhuri kauli ya kuwa hii ni Aya yenye matarajio zaidi katika Qur’ani.
Miongoni mwa madhambi makubwa zaidi ni kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu:
قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ ﴿٥٦﴾
“Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.” Juz. 14 (15:56).
Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 5 (4:56). Pia tumeweka kifungu maalum cha toba ’Toba na umbile’ katika Juz. 4 (4:17-18).
Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni kwake, kabla ya kuwajia adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.
Chukueni fursa enyi wenye dhambi wala msiipoteze. Tubieni kwake na mumfanyie ikhlasi kwa kauli na vitendo.
Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijawajia adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
Hakuna kitu, katika alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kilicho bora zaidi ya kingine kwake. Kila alichokisema ni kizuri zaidi na adhimu. Ama kwa wenye dhambi basi kitu bora zaidi walichoteremshiwa ni mwito wa toba na kukubaliwa hata ikiwa dhambi ni kubwa kiasi gani. Na yasiyokuwa hayo ni kiaga na hadhari.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha matokeo ya atakayepuuza toba; kama ifuatavyo:
Isije ikasema nafsi: Ee masikitiko yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu
katika kumtii. Masikitiko ni miongoni mwa adhabu kubwa ya nafsi. Hasa ikiwa hakuna kimbilio wala pa kutokea.
Na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!
Kesho mwenye madhambi atasema kwa majuto na masikitiko: Sikutosheka na kumwasi Mwenyezi Mungu na kupuuza toba mpaka nikawafanyia masihara wanaomtii Mwenyezi Mungu na wenye kuogopa adhabu yake.
Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye takua.
Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelishirikisha” Juz. 8 (6:148).
Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.
Mfano wake ni:
قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ﴿١٠٠﴾
“Husema Mola wangu nirudishe ili nitende mema badala ya yale niliyoacha” Juz. 18 (23:99-100).
Wapi! Mambo hayako kama unavyotaka zilikwishakujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!
Zilimjia ishara za Mwenyezi Mungu akazikanusha na akasema hazitoki kwa Mwenyezi Mungu. Akafanya kiburi na imani na akamkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha akakadhibisha na akasema: hakuna chochote kilichonijia kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake.
Kwa hiyo akachanganya maovu ya kufuru, uwongo na kiburi. Lau angelichukua fursa ya kutubia ingelikuwa hana haja na malalamiko yote haya; na angelikuwa kwenye raha bila ya kuwa na hizaya.