TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 21351
Pakua: 3395


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 21351 / Pakua: 3395
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

Mwendelezo wa Sura Ya Thelathini Na Tisa: Surat Az-Zumar.

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَبَ عَلَى اللَّـهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ ﴿٣٢﴾

32. Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na kuikadhibisha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makazi ya makafiri?

وَالَّذِي جَاءَ بِالصِّدْقِ وَصَدَّقَ بِهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na aliyeleta ukweli na aliyeusadikisha, hao ndio wenye takua.

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٤﴾

34. Watapata watakachotaka kwa Mola wao. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.

لِيُكَفِّرَ اللَّـهُ عَنْهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي عَمِلُوا وَيَجْزِيَهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٣٥﴾

35. Ili Mwenyezi Mungu awafutie uovu zaidi walioufanya na awalipe ujira wao kwa wema zaidi ya waliokuwa wakiufanya.

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٦﴾

36. Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtoshea mja wake? Na wanakutishia kwa wasiokuwa Yeye! Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumwongoza.

وَمَن يَهْدِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّضِلٍّ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِعَزِيزٍ ذِي انتِقَامٍ ﴿٣٧﴾

37. Na anayeongozwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumpoteza. Je! Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu anayeweza kulipiza.

JE, MWENYEZI MUNGU SI WA KUMTOSHEA MJA WAKE?

Aya 32 – 37

MAANA

Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu, akamfanyia washirika au mtoto?

Kauli mbaya zaidi ni uwongo na uwongo mbaya zaidi ni kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Na kuikadhibisha kweli imfikiapo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia ulimi wa Mtume wake.

Hivi ndivyo walivyo watu wa masilahi na manufaa, mahali popote na wakati wowote, wanaukana ukweli na kuusadikisha uwongo. Kwa sababu masilahi yao yanakuwa kwa uzushi na ubatilifu. Miongoni mwa niliyoyasoma kuhusiana na haya ni kuwa uwongo mkubwa zaidi ni kusema mwongo: “Mwenyezi Mungu anajua kuwa mimi ni mkweli.”

Je! Siyo katika Jahannamu makazi ya makafiri ? Bila shaka ndio makazi yao na makazi ya kila taghuti muovu.

Na aliyeleta ukweli na aliyeusadikisha, hao ndio wenye takua.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alikuja na ukweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu na waislamu wakausadikihsa. Hao mbele ya Mwenyezi Mungu ndio watu wema ikiwa watayaogopa aliyoyakataza; vinginevyo kusadikisha bila matendo hakuna maana yoyote.

Watapata watakachotaka kwa Mola wao. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.

Yaani wale wanaogopa aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu. Kwa sababu bado mazungumzo yanawahusu wao. Mwenyezi Mungu hakuanisha malipo, bali amewaachia vile watakavyo.

Ili Mwenyezi Mungu awafutie uovu zaidi walioufanya na awalipe ujira wao kwa wema zaidi ya waliokuwa wakiufanya.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasamehe madhambi yote, makubwa na madogo, kwa yule mwenye kutubia, akaamini na akatenda mema; na atawalipa wale wanaomtii na kushukuru neema zake kwa wema mkubwa kuliko vile walivyokuwa wakitii na kushukuru.

Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtoshea mja wake? Na wanakutishia kwa wasio kuwa Yeye!

Makusudio ya mja wake hapa ni Muhammad(s.a.w. w ) . Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamkinga na shari ya anayemkusudia shari. Makusudio ya wale wasiokuwa yeye ni masanamu. Kundi la wafasiri wamesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alipoyataja masanamu kwa ubaya, makuraishi walisema: Muhammad asipokoma kuwataja vibaya miungu wetu, basi tutamshtakia kwao apatwe na majanga.”

Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii. Hili haliko mbali na akili za wajinga na wapumbavu. Hakuna mwenye shaka kuwa Mwenyezi Mungu anamtoshea na kumkinga mja wake na mtume wake.

Na anayepotezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumwongoza. Na anayeongozwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumpoteza.

Wakati tukifasiri Aya ya 23 ya Sura hii tuliyo nayo, kwenye Juz. 23, na kwengineko, tulisema kuwa: Mwenyezi Mungu, anampoteza yule mwenye kufuata njia ya upotevu kwa hiyari yake, na anamwongoza mwenye kuchagua uongofu kwa hiyari yake na akafuata njia yake.

Je! Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu anayeweza kulipiza anayekufuru na akadhulumu kwa hiyari yake tena baada ya kupewa hoja?

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ قُلْ أَفَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَنِيَ اللَّـهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ أَوْ أَرَادَنِي بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ قُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ عَلَيْهِ يَتَوَكَّلُ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿٣٨﴾

38. Na ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Tosha yangu ni Mwenyezi Mungu. Kwake wategemee wanaotegemea.

قُلْ يَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٣٩﴾

39. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi pia nafanya. Basi punde mtajua.

مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na itakayemshukia adhabu ya kuendelea.

إِنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ لِلنَّاسِ بِالْحَقِّ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَلِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ ﴿٤١﴾

41. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka amepotoka kwa nafsi yake. Na wewe si mlinzi juu yao.

اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٤٢﴾

42. Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake. Huzishika zilizohuku- miwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ شُفَعَاءَ قُلْ أَوَلَوْ كَانُوا لَا يَمْلِكُونَ شَيْئًا وَلَا يَعْقِلُونَ ﴿٤٣﴾

43. Au ndio wamejifanyia waombezi badala ya Mwenyezi Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui?

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٤٤﴾

44. Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake Yeye ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.

وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿٤٥﴾

45. Na anapotajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za wasioiamini Akhera huchafuka. Na wanapotajwa walio kinyume naye basi wao hufurahi.

SEMA, TOSHA YANGU NI MWENYEZI MUNGU

Aya 38 – 45

MAANA

Na ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu.

Jawabu lao hili linatokana na ufahamu wa kimaumbile aliowaumbia watu Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hakuna tafsiri ya kupatikana ulimwengu isipokuwa kuweko Mwenyezi Mungu. Lakini walahidi wanasema: “Sisi hatuamini isipokuwa kwa kujaribu.” Ama maumbile hayo ni maneno ya upuzi. Nasi kwa upande wetu tunawauliza: ikiwa hamuamini isipokuwa majaribio, basi tuonyesheni majaribio yaliyowafahamisha kuwa hakuna Mungu.

Sisi hatuna shaka kuwa mwenye kupinga maumbile haya au kupinga mantiki yake, ndio ameupinga ubinadamu na kupinga yaliyo na thamani zaidi ndani ya binadamu; ukiwemo utashi na uwezo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (29:66) na (31:25).

Sema: Je! Mnawaonaje wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake?

Washirikina walimtishia Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa masanamu, ndio Mwenyezi Mungu akamwamrisha mtume wake awaambie kuwa masanamu yana uwezo gani kwangu na kwa mwengine? Je, yanaweza kunikinga ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kunidhuru? Au yanaweza kuzuia heri anazonitakia Mwenyezi Mungu? Hapana! Masanamu hayawezi kujikinga hata hayo yenyewe ikiwa binadamu anataka kuyavunja kwa shoka au kuyakanyaga kwa kiatu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:17) na Juz. 11 (10:107).

Sema: Tosha yangu ni Mwenyezi Mungu. Kwake wategemee wanaotegemea.

Ewe Muhammad! Mwambie anayekadhibisha risala yako kuwa mimi nataka msaada kwa Mwenyezi Mungu na kumtaka mwongozo; naye kwangu ni tosha kabisa! Na yeyote mwenye dhiki basi akimbilie kwake. Yeye ana tosha kuwa walii na msaidizi.

Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi pia nafanya. Basi punde mtajua Ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na itakayemshukia adhabu ya kuendelea.

Yaani kila mtu abaki kama alivyo, kisha tungoje mwisho utakuwaje. Bila shaka itakuwa ni hasara na moto kwenu nyinyi na baraka na neema kwetu sisi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:104) na Juz. 11 (10:93).

Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa haki.

Basi fikisha bishara na maonyo, kwa niaba ya Mola wako, kwa kutumia Aya zake; wala usimwachie yoyote udhuru.

Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka amepotoka kwa nafsi yake. Na wewe si mlinzi juu yao.

Kila mtu ana majukumu yake na hisabu yake kwa muumba wake, wewe huna majukumu yoyote kwake baada ya kumfikishia na kumpa nasaha.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:104) na Juz. 11 (10:108).

Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa.

Wanaoamini maada wanasema: Mtu ni huu mwili tu, wala hakuna kitu kingine nyuma yake. Tazama kifungu ‘Wanaoamini maada na maisha baada ya mauti’ katika Juz. 13 (13:5-7). Na ‘Pamoja na wanaoamini maada’ katika Juz. 14 (16:78-83).

Waumini wanasema: Mtu ni mwili na roho, na kwamba roho ndiyo inayouendesha mwili na kuupangilia kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mauti ni kukatika mfungamano wa roho na mwili na roho kwenda kwa Mola wake: “Ewe nafsi iliyotua! Rejea kwa Mola wako hali ya kuwa uradhi mwenye kuridhiwa” (89:27-28).

Na hii ndio maana ya kuwa ‘Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapoku- fa,’ ni kuwa anazishika wakati wa kufa miili.

Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake.

Usingizi ni aina ya mauti au ni mauti kimajazi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ ﴿٦٠﴾

“Naye ndiye anayewafisha usiku.” Juz. 7 (6:60).

Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Inayokufa wakati wa kulala ni nafsi ya upambanuzi na akili ambayo inafarikiana na mwenye kulala, kwa hiyo hawi na akili. Ama ile inayokufa wakati wa mauti ni nafsi ya uhai ambayo inaondoka na pumzi na mwenye kulala huwa anapumua. Kwa hiyo tofauti baina ya kushikwa usingizini na kwisha kwenye mauti ni kuwa usingizi ni kutokuwa macho na mauti ni kutokuwa hai. Na kushikwa usingizini roho inakuwa mwilini na kushikwa kwenye mauti ni roho kuondoka mwilini.”

Huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.

Mwenyezi Mungu kuzishika roho wakati wa kufa mwili na wakati wa kulala. Zile zilizohukumiwa kufa zinabaki kwake na zile nyingine anaziachia zirudi mpaka muda maalum.

Umar bin Al-Khattab alisema: “Ajabu ni kuwa mtu anaota ndoto inakuwa kama kuchukua kwa mkono na anaota ndoto nyingine, lakini haiwi kitu.” Imam Ali bin Abi Twalib akamwambia: “Hakika Mwenyezi Mungu anazifisha nafsi zote. Ile unayoiona iko mbele yake basi ni ya ukweli na unayoiona baada ya kuiachia basi ni ya uwongo.” Akastaajabu Umar kutokana na kauli ya Imam.

Haya ameyanukuu Sheikh Al-Maraghi katika tafsiri yake kutoka kwa Abi Hatim na Ibn Mardawayh.

Au ndio wamejifanyia waombezi badala ya Mwenyezi Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui?

Masanamu hayatambui kitu, wala hayawezi kujikinga na madhara, lakini pamoja na hayo washirikina wanawatarajia wawaombee mbele ya Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo wanavyofanya wajinga. Muombezi bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu kwa wale wenye madhambi ni toba na kurejea kwa Mwenyezi Mungu.

Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu.

Yaani hakuna yoyote anayemiliki uombezi wowote isipokuwa yule aliyemilikishwa na Mwenyezi Mungu:

قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّـهِ ﴿١٥٤﴾

“Hakika mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu” Juz.4 (3:154).

Ni wake Yeye ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.

Mfano wake ni

وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ﴿١٧﴾

“ Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na vilivyomo baina yake.” Juz. 6 (5:17).

Na anapotajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za wasioiamini Akhera huchafuka. Na wanapotajwa wenginewe asiye kuwa Yeye basi wao hufurahi.

Washirikina walipokuwa wakisikia kauli ya hapana mola ispokuwa Mwenyezi Mungu (Lailaha illa llah) wanakimbia, na wanaposikia kusifiwa masanamu wanafurahi.

Hivi ndivyo walivyo wabatilifu wa zamani na wa sasa. Haiwapumbazi isipokuwa batili wala haiwatishi isipokuwa haki. Kwenye Nahjulbalagha, amesema: “Ambaye inakuwa uzito kwake kuambiwa haki au kuonyeshwa uadilifu, basi kuyatumia mawili hayo inakuwa uzito zaidi.”

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

قُلِ اللَّـهُمَّ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِي مَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٤٦﴾

46. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyokuwa wakikhitalifiana.

وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَبَدَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مَا لَمْ يَكُونُوا يَحْتَسِبُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na lau kuwa waliodhulumu wangelikuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikomboa katika adhabu mbaya Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyokuwa wakiyatazamia.

وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٤٨﴾

48. Na utawadhihirikia ubaya wa waliyoyachuma, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

فَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَانَا ثُمَّ إِذَا خَوَّلْنَاهُ نِعْمَةً مِّنَّا قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ بَلْ هِيَ فِتْنَةٌ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na dhara inapomgusa mtu hutuomba. Kisha tunapompa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui.

قَدْ قَالَهَا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٥٠﴾

50. Walikwishayasema haya waliokuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.

فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَالَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ هَـٰؤُلَاءِ سَيُصِيبُهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٥١﴾

51. Basi ukawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Na wale ambao wamedhulumu miongoni mwa hawa utawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Nao si wenye kushinda.

أَوَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٢﴾

52. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaoamini.

UTAHUKUMU BAINA YAO

Aya 46 – 52

MAANA

Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyokuwa wakikhitalifiana.

Aya hii inafungamana na ile iliyotangulia: ‘Na wewe si mlinzi juu yao.’ Maana yake yako wazi. Kwa ufupi ni, sema ewe Muhammad, baada ya kufikisha ujumbe na kutoa nasaha: ewe Mwenyezi Mungu wewe ni muumba wa ulimwengu, Mfalme wa wafalme, Mjuzi wa yaliyoko kwangu na kwa wakadhibishaji. Hukumu ni yako peke yako katika kila kuhitalifiana na kuzozana baina ya waja wako kwenye maisha haya.

Na lau kuwa waliodhulumu wangelikuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikomboa katika adhabu mbaya Siku ya Kiyama. Na yatawadhi- hirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyokuwa wakiyatazamia.

Walikuwa wakipupia dunia na wakikusanya mali juu mali, wakiwa wameghafilika na kukutana na Mwenyezi Mungu na hisabu yake. Wakati watakaposimima mbele yake kwa ajili ya hisabu na kuwafunukia waliyokuwa wakiyapuuza, basi watauma mikono wakijuta. Lakini wapi!

Jahannam haiwezi kukombolewa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:91), Juz. 11 (10: 54) na Juz. 13 (13:18)

Na utawadhihirikia ubaya wa waliyoyachuma, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Walikuwa wanapoambiwa iogoponi siku ambayo mtarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu, walikuwa wakiifanyia masikhara kauli hii na yule aliyeisema.

Lakini watakapohudhurishwa siku iliyoagwa, hapo ndio haki- ka itawadhihirikia na adhabu itawashukia kulingana na msimamo wao wa madharau na kumdharau yule aliyewaonya.

UDHURU MBAYA KULIKO DHAMBI

Na dhara inapomgusa mtu hutuomba. Kisha tunapompa neema zitokazo kwetu, husema: ‘Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu.’

Makusudio ya mtu hapa ni kila mwenye sifa hiyo iliyotajwa ambaye anamtaka msaada Mwenyezi Mungu wakati wa shida na kumsahau wakati wa raha huku akisema kwa kujidai: ‘Neema hii ni kwa mipango na ufundi wangu.’

Wakati nikiandika maneno haya, nimekumbuka siasa ya Marekani aliyoitangaza Rusk, alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, alisema: “Hapana budi kwa Marekani kuonyesha umuhimu wake katika dunia nzima, ikiwemo anga yake, maji yake na pambizo zake zinazoizunguka.”

Anamaanisha kuwa ni lazima Amerika itawale dunia yote na vilivyomo ndani yake.

Tangazo hili lilikuwa mnamo mwaka 1966, kabla ya Marekani kupeleka chombo chake mwezini. Kwa hiyo ingelikuwa leo angeuanganisha mwezi na sayari nyinginezo.

Baada ya magazetu ya kimataifa kutangaza siasa hii ya kikoloni, aliyoitangaza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Amerika, kibaraka mmoja aliandika makala ya kutetea siasa hii, kwa kusema:

“Marekani ndio dola kubwa kielimu na kiutajiri. Imeonyesha ushindi mkubwa katika uwanja wa elimu na viwanda. Kwa hiyo basi inayo haki ya kuingilia ulimwengu kwa sura mbalimbali, kutawala kila inachokitaka, kugeuza kanuni za nchi yoyote, vile inavyotaka, na kuielekeza kiuchumi, kuiwekea bajeti yake na kuipangia nchi hiyo itakachouza nje na itakochonunua.

Vile vile Marekani inayo haki ya kutumia siasa kwenye nchi yoyote kwa mfumo wowote, hata ikibidi kutumia nguvu, kwa mapinduzi ya kijeshi na kuunga mkono harakati za upinzani, ili kuleta utulivu.

Marekani inayo haki hii na zaidi, kwa sababu:

kwanza : Haki hii ni ya kielimu.

Pili : Marekani inamiliki silaha za maangamizi, na kila mwenye kumilki silaha hizi ana haki ya kutawala dunia nzima na vilivyomo ndani yake.”

Yote yaliyoandikwa kwenye makala hii kupitia mwandishi huyu ni ubainifu wa siasa halisi ya Marekani kama ilivyo. Mwenye kutaka kuhakikisha haya naangalie siasa ya Marekani katika Vietnam, Asia, Afrika na Latin Amerika.

Vile vile msimamo wake wa kiadui kwa nchi za kiarabu, jinsi inavyotoa msaada usiokuwa na mpaka kwa adui Israil na inavyopinga jaribio lolote la amani katika tatizo la Palestina na mahali popote penye tatizo mashariki na magaharibi.

Mzandiki huyu aliyejitolea kuitetea Marekani, kubariki siasa zake na kusema kuwa inayo haki ya kushibisha matamanio yake ya kiuadui, kwa kuwa eti inamiliki viwanda vya silaha, tunamuuliza hivi: Ikiwa elimu inaruhusu kuua, kubomoa na kupora, maana yake ni kuwa elimu ni ya shari sio ya heri na ni ya ufisadi wala sio ya utengenezaji?

Na kwamba mwenye elimu anayoruhusa kuitumia elimu yake kuiba, kudanganya na kuzua? Na mwizi atakuwa ni mwenye kushukuriwa na kulipwa; na kila anavyozidi kuwa hodari wa hatia na kuwa na ufisadi mwingi na upotevu basi atakuwa anastahiki heshima?

Ikiwa elimu inaboresha uadui, kwanini basi Marekani inainua nembo za haki za binadamu na kujaribu kila juhudi kuwakinaisha watu kwamba wao wanafanya ibada wana zuhudi na wanupiga vita ukomonisti kwa jina la imani ya Mungu na siku ya mwisho?

Zaidi ya hayo mzushi huyu mwenye dhambi amaesahau kuwa anafichua hiyana yake na upotevu wake, huku akiwa anatetea matamanio ya Marekani kwa mantiki yake ya kufedhehesha akitoa udhuru kwa yaliyo mabaya zaidi ya dhambi yake.

Sio! Huo ni mtihani!

Makusudio ya mtihani hapa ni neema. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamneemesha mja wake ili amjaribu kuwa atashukuru au atakufuru. Akishukuru humzidishia neema duniani na malipo akhera, na akikufuru basi Jahannam imeandaliwa makafiri.

Lakini wengi wao hawajui kuwa Mwenyezi Mungu anawapa mtihani waja wake ili vidhihirike vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu.

Walikwishayasema haya waliokuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.

Yaani haya ya kusema kuwa nimepewa kwa elimu yangu. Maana ni kuwa msemaji huyu mjinga ana wanaofanana naye katika historia, lakini mali haikuwazuia na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake iliyotolewa kiaga. Tazama Juz. 20 (28:76-82).

Basi ukawasibu ubaya wa waliyoyachuma. Na wale ambao wamedhulumu miongoni mwa hawa - waliomkadhibisha Muhammad – utawasibu ubaya wa waliyoyachuma.

Mwenye kufanya wema atalipwa nao wala hatapata msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hii imethibiti kwa wote bila ya kuvua wala kuhusika na uma zilizotangulia au zijazo. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Nao si wenye kushinda.

Kwani inawezekana muumbwa kumshinda muumba wake?

Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaoamini.

Umetangulia mfano wake katika Juzuu zifuatazo: Juz.13 (13:27), Juz.15 (17:30), Juz.20 (28:82), Juz.21(29:62), Juz.21 (30:37) na Juz.22 (34:36,39).

Na tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hili katika Juzuu zifuatazo: Juz. 6 (5:64-66), kifungu cha ‘Riziki na ufisadi,’ Juz. 7 (5:100) kifungu ‘Je riziki ni bahati au majaliwa?’ Juz. 13 (13:26-29) kifungu ‘Mtu na riziki’ na Juz. 20 (29:56-63) kifungu ‘Riziki na kumtegemea Muumba si kiumbe.’

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾

53. Sema: Enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni kwake, kabla ya kuwajia adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.

وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ ﴿٥٥﴾

55. Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijawajia adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.

أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ ﴿٥٦﴾

56. Isije ikasema nafsi: Ee masikitiko yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu; na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!

أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴿٥٧﴾

57. Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye takua.

أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٨﴾

58. Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.

بَلَىٰ قَدْ جَاءَتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٥٩﴾

59. Wapi! zilikwishakujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!

MWENYEZI MUNGU ANASAMEHE MADHAMBI YOTE

Aya 53 – 59

MAANA

Sema: Enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Huu ni mwito wa wazi, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa wale waliodhulumu nafsi zao kwa kufanya madhambi na maasi. Akaahidi msamaha kwa kila dhambi kadiri itakavyokuwa kubwa. Kwa hiyo amefungua mlango kwa yule mwenye kutaka kufuta maovu yake yeye mwenyewe na kutengeneza yaliyoharibika.

Kuna Hadith inayosema:“Hakika Mwenyezi Mungu hachoki mpaka mchoke. Mkiacha naye anaacha.” yaani mkiacha toba naye anaacha maghufira. Katika Hadith nyingine Mtume(s.a.w. w ) anasema:“Hakuna ninachopenda zaidi katika dunia na vilivyomo kuliko Aya hii.” Imekua mashuhuri kauli ya kuwa hii ni Aya yenye matarajio zaidi katika Qur’ani.

Miongoni mwa madhambi makubwa zaidi ni kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu:

قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ ﴿٥٦﴾

“Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.” Juz. 14 (15:56).

Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 5 (4:56). Pia tumeweka kifungu maalum cha toba ’Toba na umbile’ katika Juz. 4 (4:17-18).

Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni kwake, kabla ya kuwajia adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.

Chukueni fursa enyi wenye dhambi wala msiipoteze. Tubieni kwake na mumfanyie ikhlasi kwa kauli na vitendo.

Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijawajia adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.

Hakuna kitu, katika alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kilicho bora zaidi ya kingine kwake. Kila alichokisema ni kizuri zaidi na adhimu. Ama kwa wenye dhambi basi kitu bora zaidi walichoteremshiwa ni mwito wa toba na kukubaliwa hata ikiwa dhambi ni kubwa kiasi gani. Na yasiyokuwa hayo ni kiaga na hadhari.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha matokeo ya atakayepuuza toba; kama ifuatavyo:

Isije ikasema nafsi: Ee masikitiko yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu katika kumtii. Masikitiko ni miongoni mwa adhabu kubwa ya nafsi. Hasa ikiwa hakuna kimbilio wala pa kutokea.

Na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!

Kesho mwenye madhambi atasema kwa majuto na masikitiko: Sikutosheka na kumwasi Mwenyezi Mungu na kupuuza toba mpaka nikawafanyia masihara wanaomtii Mwenyezi Mungu na wenye kuogopa adhabu yake.

Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye takua.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelishirikisha” Juz. 8 (6:148).

Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.

Mfano wake ni:

قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ﴿١٠٠﴾

“Husema Mola wangu nirudishe ili nitende mema badala ya yale niliyoacha” Juz. 18 (23:99-100).

Wapi! Mambo hayako kama unavyotaka zilikwishakujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!

Zilimjia ishara za Mwenyezi Mungu akazikanusha na akasema hazitoki kwa Mwenyezi Mungu. Akafanya kiburi na imani na akamkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha akakadhibisha na akasema: hakuna chochote kilichonijia kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake.

Kwa hiyo akachanganya maovu ya kufuru, uwongo na kiburi. Lau angelichukua fursa ya kutubia ingelikuwa hana haja na malalamiko yote haya; na angelikuwa kwenye raha bila ya kuwa na hizaya.