20
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ ﴿٥٧﴾
57. Na alipopigiwa mfano Mwana wa Maryam, watu wako waliupigia ukelele.
وَقَالُوا أَآلِهَتُنَا خَيْرٌ أَمْ هُوَ مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا بَلْ هُمْ قَوْمٌ خَصِمُونَ ﴿٥٨﴾
58. Wakasema: Miungu yetu kwani ni bora au Yeye? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٥٩﴾
59. Hakuwa yeye Isa ila ni mja tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.
وَلَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَا مِنكُم مَّلَائِكَةً فِي الْأَرْضِ يَخْلُفُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na tungelipenda tungeliwafanya badala yenu Malaika katika ardhi kuwa makhalifa.
وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا وَاتَّبِعُونِ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦١﴾
61. Na kwa hakika hiyo ni elimu ya Saa. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo njia iliyonyooka.
وَلَا يَصُدَّنَّكُمُ الشَّيْطَانُ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٦٢﴾
62. Wala asiwazuie Shetani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhahiri.
وَلَمَّا جَاءَ عِيسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ قَالَ قَدْ جِئْتُكُم بِالْحِكْمَةِ وَلِأُبَيِّنَ لَكُم بَعْضَ الَّذِي تَخْتَلِفُونَ فِيهِ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿٦٣﴾
63. Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimewajia na hikima, na ili niwaeleze baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii.
إِنَّ اللَّـهَ هُوَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦٤﴾
64. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, na Mola wenu. Basi Mwabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia iliyonyooka.
فَاخْتَلَفَ الْأَحْزَابُ مِن بَيْنِهِمْ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ عَذَابِ يَوْمٍ أَلِيمٍ ﴿٦٥﴾
65. Lakini makundi yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٦٦﴾
66. Hawangoji ila Saa iwajie ghafla na hali wao hawatambui?.
ALIPOPIGIWA MFANO MWANA WA MARYAM
Aya 57 – 66
MAANA
Na alipopigiwa mfano Mwana wa Maryam, watu wako waliupigia ukelele. Wakasema: Miungu yetu kwani ni bora au Yeye?
Anaambiwa Mtume(s.a.w.
w
)
. Wafasiri wamesema kuwa aliyempigia mfano mwana wa Maryam ni Abdallah bin Ziba’ara. Aya inaashiria tukio lililotokea baina ya Mtume(s.a.w.
w
)
na makafiri wa kikuraishi; kwa ufupi ni kama ifuatavyo:
Iliposhuka Aya: “Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam mtaifikia” Juz. 17 (21:98), makuraishi waliona vibaya sana, wakamwendea Abdallah bin Ziba’ara, kabla ya kusilimu, naye akamwambia Mtume: “Manaswara wanamwabudu Masih, ikiwa Masih atakuwa katika Moto sisi tutakuwa radhi kuwa miungu yetu iko pamoja naye kwa sababu yeye ni bora kuliko hiyo au hiyo siyo bora kuliko yeye” Makuraishi waliposikia walilipuka kwa makelele ili wamnyamazishe Mtume asiweze kujibu na watu wafikirie kuwa ameshindwa kujibu.”
Mapokezi mengine yanasema kuwa Mtume(s.a.w.w)
alimwambia Bin Zab’ara: “Ni ujinga ulioje wako kutojua lugha ya watu wako? Hujui kuwa herufi ‘ma’ ni ya wasio na akili?” yaani ‘hayo mnayoyaabudu.’
Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu.
Kukupinga kwako makuraishi kwa kumtolea mfano Masih sio kwa makusudio ya kuihakiksha haki na kuidhihirisha, isipokuwa ni kwa makusudio ya kuikimbia haki na kuvungavunga tu. Wao wanajua wazi kuwa makusudio ya hayo mnayoyaabudu ni masanamu yao hasa.
Bali hao ni watu wagomvi!
Wanazidisha ugomvi na uhasama ili kulinda masilahi yao.
Hakuwa yeye Isa ila ni mja tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.
Isa ni mja katika waja wa Mwenyezi Mungu, aliyeneemeshwa kwa utume na kaumbwa bila ya baba, kama Adam, ili awe ni ishara kuwafahamisha Wana wa Israil uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake, waweze kuongoka na kuwa na takua. Lakini wao walizidi inadi na ujeuri, wakasema kuhusu Bwana Masih na mama yake mambo ambayo yanaweza kuitingisha Arshi.
Na tungelipenda tungeliwafanya badala yenu Malaika katika ardhi kuwa makhalifa.
Hili ni kemeo na karipio kwa washirikina. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu hana haja na nyinyi wala ibada yenu. Kama angelitaka anageliwaangamiza na mahala penu pakachukuliwa na Malaika watakomtakasa na kumsifu kwa sifa njema bila ya kumuasi na jambo lolote.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم ﴿٣٨﴾
“Na mkigeuka atawaleta watu wengine na hawatakuwa mfano wenu.” (47:38).
Na kwa hakika hiyo ni elimu ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia iliyonyooka.
‘Hiyo’ ni hiyo Qur’an. Maana ni kuwa Qur’an inawaelimisha watu siku ya Kiyama na kuwapa uhakika wake na pia kuwahadharisha na vituko vyake; wala haifai kukitilia shaka. Na hii Qur’an ni njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ ﴿٩﴾
“Hakika hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa.” 15 (17:9).
Iliyonyooka kabisa ndio hiyo njia iliyonyooka.
Unaweza kuuliza
: kwanini isiwe hakika huyo, yaani Isa, kwa vile Isa ndiye aliyetajwa na Qur’an haikutajwa kwenye Aya?
Jibu
: maudhui ya Aya ni mjadala kuhusiana na Isa, na masimulizi yake yamesimuliwa na Qur’an. Kwa hiyo kutajwa Bwana Masih ni kutajwa Qur’an. Hili linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye Aya hiyo hiyo: “Hii ndiyo njia iliyonyooka” ambayo makusudio yake ni Qur’an kama tulivyoeleza. La kushangaza ni mfasiri mmoja aliyeirudisha dhamir kwa Isa na kufasiri njia iliyonyooka kuwa ni mwito wa Muhammad(s.a.w.w)
na Qur’an.
Wala asiwazuie Shetani na haki na kuitumia. Hakika yeye ni adui yenu wa dhahiri.
Uadui wa wazi na chuki inamfanya awaghuri kwa mambo machafu. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ ﴿٢٧﴾
“Shetani asiwatie katika fitna, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo).”
Juz. 8 (7:27).
Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimewajia na hikima, na ili niwaeleze baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii.
Makusudio ya dalili hapa ni miujiza inayofahamisha utume wa Isa; kama vile kuponesha upofu na ukoma. Na makusudio ya hikima ni elimu ya dini ya Mwenyezi Mungu na sharia yake.
Maana ni kuwa Isa, ambaye utume wake umethibiti kwa dalili wazi, aliwaambia Wana wa Israili: Nimewajia na hukumu zote za dini, kiitikadi na kisharia na kwazo mtamjua mwenye haki na mbatilifu, basi mcheni Mwenyezi Mungu mtaongoka.
Unaweza kuuliza
: Kwa nini amesema baadhi ya mnayohitalifiana na asiseme yote?
Wamejibu
kundi katika wafasiri kwamba Makusudio yake ni kuwa Isa
, kwa wasifu wake kama Mtume, huwa anawabainishia mambo ya dini tu, lakini haingilii mambo ya dunia.
Kuna riwaya ya maulama wa kisunni kutoka kwenye sahihi zao kwamba Mtume(s.a.w.w)
amesema:“Nyinyi ni wajuzi zaidi wa mambo ya dunia yenu na mimi ni mjuzi zaidi wa mambo ya dini yenu.”
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, na Mola wenu. Basi mwabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia iliyonyooka.
‘Hii’ ni ishara ya Tawhid na kukataza shirki. Maana yako wazi, kama alivyosema Razi.
Lakini makundi yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
Makusudio ya makundi ni mayahudi na manaswara kwa upande mmoja, na manaswara wenyewe kwa upande wa pili. Mayahudi walisema kuwa Isa ni mtoto wa zina (mwanaharamu), wakipingana katika hilo na manaswara wote na waislamu wote. Na hao manaswara wenyewe nao walikhitalifiana, baada ya Masihi, makundi mbali mabli. Kuna waliosema Isa ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wengine wakasema ni mwana wa Mungu na wengine wakasema kuwa yeye ni mungu hasa. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanayomsifia.
Hawangoji ila Saa iwajie ghafla na hali wao hawatambui?
Hili ni karipio na kemeo kwa yule anayemfanya Isa kuwa ni Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (12:107).
الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ ﴿٦٧﴾
67. Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.
يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ ﴿٦٨﴾
68. Enyi waja wangu! Leo hamtakuwa na khofu, wala hamtahuzunika.
الَّذِينَ آمَنُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا مُسْلِمِينَ ﴿٦٩﴾
69. Ambao waliziamini Ishara zetu na wakawa Waislamu.
ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ ﴿٧٠﴾
70. Ingieni kwenye Bustani (Pepo), nyinyi na wake zenu katika hali ya kufurahishwa.
يُطَافُ عَلَيْهِم بِصِحَافٍ مِّن ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ وَأَنتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٧١﴾
71. Watapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; Na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda, na macho yanavifurahia. Na nyinyi mtakaa humo milele.
وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٧٢﴾
72. Na hiyo ni Bustani (Pepo) mliyorithishwa kwa hayo mliyokuwa mkiyafanya.
لَكُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ كَثِيرَةٌ مِّنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٧٣﴾
73. Mnayo humo matunda mengi mtakayoyala.
إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي عَذَابِ جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿٧٤﴾
74. Hakika wakosefu watakaa milele katika adhabu ya Jahannamu.
لَا يُفَتَّرُ عَنْهُمْ وَهُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ ﴿٧٥﴾
75. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا هُمُ الظَّالِمِينَ ﴿٧٦﴾
Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio waliokuwa madhalimu.
وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ ﴿٧٧﴾
77. Na watapiga kelele: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako! Atasema: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
لَقَدْ جِئْنَاكُم بِالْحَقِّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَكُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٨﴾
78. Kwa yakini tuliwaletea Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.
أَمْ أَبْرَمُوا أَمْرًا فَإِنَّا مُبْرِمُونَ ﴿٧٩﴾
79. Au wamekata shauri? Bali ni Sisi ndio tunaopitisha.
أَمْ يَحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُم بَلَىٰ وَرُسُلُنَا لَدَيْهِمْ يَكْتُبُونَ ﴿٨٠﴾
80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong’ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
SIKU HIYO MARAFIKI WATAKUWA NI MAADUI
Aya 67 – 80
MAANA
Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.
Makusudio ya maadui ni kukatika muungano; iwe ni kwa chuki na kulaaniana au bila chuki. Maana ni kuwa muungano wa mapenzi na urafiki uliokuwa duniani, baina ya watu, siku ya kiyama utaondoka na kukatika; ila ukiwa chimbuko lake ni udugu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kusaidiana kwenye twaa yake.
Kwani huo utadumu bila ya kuwa na kikomo, bali unazidi na kukua kila muda unavyorefuka, kwa sababu yaliyoko kwa ajili ya Mwenyezi Mungu yanazidi.
Zaidi ya hayo ni kwamba watu wa Peponi watakuwa ni familia moja, hata kama walikuwa wanatofautiana duniani: Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٤٧﴾
“Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.”
Juz.14 (15:47).
Enyi waja wangu! Leo hamtakuwa na khofu, wala hamtahuzunika.
Hii ni amani ya Mwenyezi Mungu kesho kwa wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wakawa na takua.
Ambao waliziamini Ishara zetu na wakawa Waislamu: Ingieni kwenye Bustani (Pepo), nyinyi na wake zenu katika hali ya kufurahishwa.
Huu ni ubainifu na tafsiri ya waja wa Mwenyezi Mungu na kwamba wao ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wakanyenyekea twaa yake na malipo yao mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuwaingiza Peponi pamoja na wake zao walio wema.
Maana ya ‘kufurahishwa’ ni kuwa thawabu zao haziishii kwenye amani na kukosa hofu tu; bali zinavuka hadi kwenye shangwe na furaha. Vile vileWatapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe;
sahani ni za chakula na vikombe ni vya kinywaji.
Na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda
katika starehehe za kimaada na za kiroho,na macho yanavifurahia,
katika mandhari mazuri.Na nyinyi mtakaa humo milele
bila ya kuwa na mwisho.
Na hiyo ni Bustani (Pepo) mliyorithishwa kwa hayo mliyokuwa mkiyafanya.
Pepo ni haki yenu enyi waumini mlioifanyia kazi; sawa na mirathi. Kwa sababu nyinyi mliifanyia kazi duniani.
Mnayo humo matunda mengi mtakayoyala.
Chakula, kinywaji na matunda pia. Vinavyotamaniwa na nafsi havina idadi, kwa sababu matamanio ya nafsi hayana udhibiti. Vile vile ladha ya jicho.
Hakika wakosefu watakaa milele katika adhabu ya Jahannamu. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja walioongoka, sasa anataja waliopotea na kwamba wao watakuwa katika adhabu ya daima wakiwa hawana matumaini yoyote ya kwisha wala kupungua.
Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio waliokuwa madhalimu.
Kwa sababu Allah (s.w.t) aliwahadharisha na kawaonya, lakini wakakataa isipokuwa kufuru.Na watapiga kelele
waseme:Ewe Malika! Na atufishe Mola wako! Naye atasema: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
Watamuomba Malik, mtunzaji wa Moto, awaombee kwa Mwenyezi Mungu awape mauti, ili waepukane na adhabu. Naye Malik atawajibu kuwa hakuna kuokoka, nyinyi mtakua humo humo tu. Haya ndiyo mliyozifanyia nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyafanya.
Unaweza kuuliza
: Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya iliyotangulia amewaelezea kuwa wao watakata tamaa hata ya kupunguziwa adhabu, sikwambii kukatika. Vipi hapa anawatolea habari kwamba wao watataka mauti ili waondokewe na adhabu? Hii inafahamisha matarajio ambayo yanapingana na kukata tamaa.
Jibu
: Watu wa motoni watakuwa na hali ya kukata tamaa na mara nyingine kuwa na matumaini. Zaidi ya hayo inawezekana kuwa mwito wao kwa Malik ni kiasi cha kuelezea shida yao tu.
Kwa yakini tuliwaletea Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.
Wanaoipinga haki wako aina mbili: Kwanza, ni wale wanaopinga kwa kutoijua. Pili, ni wale wanaoipinga kwa vile inagongana na masilahi yao na matamanio. Aina hii ndio nyingi zaidi.
Kila atakayeingia motoni kesho atauingia kwa sababu aliipinga haki na kutoitumia, lakini wachache miongoni mwao watastahiki adhabu kwa vile wamezembea kuijua haki. Na wengi watastahiki adhabu kwa vile wameiacha kwa kuwa inagongana na matamanio yao; sio kwa kutoijua.
Au wamekata shauri? Bali ni Sisi ndio tunaopitisha.
Yaani hao makuraishi. Maana ni kuwa washirikina hawakufanya njama zozote kwa Mtume ila Mwenyezi Mungu huvunja njama zao; kama alivyowafanyia makuraishi, pale walipopanga njama ya kumuua mtume akiwa amelala kitandani mwake.
Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong’ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
Wao wanapanga njama kwa siri wakidhani kuwa hilo linafichika kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini Yeye anajua siri na yaliyofichika, naye haviongozi vitimbi vya wahaini.
قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ ﴿٨١﴾
81. Sema: Ingelikuwa Mwingi wa rehema ana mwana, basi mimi ningelikuwa wa kwanza kumwabudu.
سُبْحَانَ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٨٢﴾
82. Ametakasika Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa Arshi, na hayo wanayomsifia.
فَذَرْهُمْ يَخُوضُوا وَيَلْعَبُوا حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي يُوعَدُونَ ﴿٨٣﴾
83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayoahidiwa.
وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ ﴿٨٤﴾
84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
وَتَبَارَكَ الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَعِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٥﴾
85. Na amekuwa na baraka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo kati yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa Na kwake Yeye mtarudishwa.
وَلَا يَمْلِكُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الشَّفَاعَةَ إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿٨٦﴾
86. Wala hao wanoaomba badala yake Yeye hawana uweza wa uombezi, isipokuwa anayeshuhudia kwa haki, na wao wanajua.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٨٧﴾
87. Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi wanageuzwa wapi?
وَقِيلِهِ يَا رَبِّ إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ قَوْمٌ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٨٨﴾
88. Na usemi wake ni: Ewe Mola wangu! Hakika hawa ni watu wasioamini.
فَاصْفَحْ عَنْهُمْ وَقُلْ سَلَامٌ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٨٩﴾
89. Basi wasamehe, na uwaambie salama. Watakuja jua.
INGELIKUWA MWINGI WA REHEMA ANA MWANA
Aya 81 – 89
MAANA
Sema: Ingelikuwa Mwingi wa rehema ana mwana, basi mimi ningelikuwa wa kwanza kumwabudu.
Mwenye Majamaul-abayan, ameitajia Aya hii ktk njia tano na akarefusha maneno bila ya kuwa na haja ya kufanya hivyo, kwa sababu maana yako wazi nayo ni sema: ewe Muhammad(s.a.w.
w
)
kumwambia yule anayedai kuwa Mwenyezi Mungu ana mwana kwamba mimi nitakuwa na wewe lakini kwa sharti ya kunithibitishia dalili mkataa ya hilo.
Lakini hakuna dalili ya madai haya; bali kuna dali ya kinyume chake. Kwa hiyo mimi ni katika wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa kuamini kuwa Mwenyezi Mungu hakuzaa wala hakuzaliwa.
Kwa ufupi ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
alikufunga kukubali kwake na jambo lilio muhali. Hakuna mwenye shaka kuwa kuli- funga jambo na muhali ni sawa na muhali. Mfumo huu ni maarufu kwa maulama katika kujadiliana, na ni wa kumnyamazisha mbishi.
Ametakasika Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa Arshi, na hayo wanayomsifia
ya kumnasibishia mtoto na mshirika.Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayoahidiwa.
Makusudio ya porojo na kucheza ni kusema kuhusu Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi. Siku yao ni Siku ya Kiyama.
Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
Mwenyezi Mungu pekee ndiye muumba wa ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, ndiye mpangiliaji wake kwa ujuzi wake na hekima yake; hakuna yoyote asiyekuwa Yeye anayestahiki ibada.
Na amekuwa na baraka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama.
Kaulia yake ‘na viliomo kati yake’ inaashiria kuwa katika anga kuna vitu tusivyovijua uhakika wake, na hakuna anayejua Kiyama kitakuwa lini isipokuwa Mwenyezi Mungu tu.
Na kwake Yeye mtarudishwa kwa ajili ya hisabu na malipo.
Wala hao wanoaomba badala yake Yeye hawana uweza wa uombezi, isipokuwa anayeshuhudia kwa haki, na wao wanajua.
Wao wanaabudu masanamu kwa kudai kuwa yatawaombea kwa Mwenyezi Mungu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia, hapana, hakuna anayeweza kuombea kwake isipokuwa yule anayemtamkia neno la Tawhid, akaliamini kwa ujuzi, na lazima anayeombewa awe anastahiki uombezi na msamaha
Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi wanageuzwa wapi?
Wao wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Aliewaumba, lakini bado wanaacha kumwabudu na kuayendea masanamu. Umetangulia mfano wake katika Aya 9 ya sura hii tuliyo nayo.
Na usemi wake Mtume ni: Ewe Mola wangu! Hakika hawa ni watu wasioamini. Basi wasamehe, na uwaambie maneno ya salama. Watakuja jua.
Maana ni kuwa Mtume alimwambia Mola wake kuwa wale ulionituma kwao hawakuniitikia. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamwambia usijali na upinzani wao, kwani mwisho ni wako sio wao. Makusudio ya salama hapa ni kama makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا ﴿٦٣﴾
“Na wajinga wakiwasemesha husema: Salama” Juz. 19 (25:63).
MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA TATU: SURAT AZ-ZUKHRUF