21
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
Sura Ya Arubaini Na Nne: Surat Ad-Dukhan. Imeshuka Makka. Ina Aya 59.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
حم ﴿١﴾
1. Haa Mim.
وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾
2. Naapa kwa Kitabu kinachobainisha.
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ ﴿٣﴾
3. Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni waonyaji.
فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ ﴿٤﴾
4. Katika huo hubainishwa kila jambo la hikima.
أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ ﴿٥﴾
5. Ni amri itokayo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦﴾
6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ ﴿٧﴾
7. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, ikiwa nyinyi mna yakini.
لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨﴾
8. Yeye Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha - Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo.
بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ يَلْعَبُونَ ﴿٩﴾
9. Lakini wao wamo katika shaka wakicheza.
TUMEITEREMSHA USIKU ULIOBARIKIWA
Aya 1 – 9
MAANA
Haa Mim.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1)
Naapa kwa Kitabu kinachobainisha. Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa.
Umebarikiwa kwa kuteremkiwa na Qur’an. Tukiunganisha Aya hii na ile isemayo:
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾
“Hakika tumeiteremsha katika usiku wa heshima (Laylatul-qadr.) (97:1)
Na pia ile isemayo:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ ﴿١٨٥﴾
“Ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qur’an.” Juz.2 (2:185),
Tukiunganisha Aya hizi tatu, tunapata maana kuwa usiku uliobarikiwa ni Laylatul-qadr, na kwamba uko ndani ya mwezi wa Ramadhani uliobarikiwa.
Katika Juz. 2 (2: 183-185), Tumesema kwamba mwanzo wa kushuka Qur’an ulikuwa kwenye Layaltul-qadr, sio kuwa ilishuka Qur’an yote usiku huo. Kwa maelezo zaidi rudia huko.
Hakika Sisi ni Waonyaji
wa adhabu kali kwa atakayeasi na kufanya ufisadi katika ardhi. Onyo hili limekuja katika Qur’an iliyoteremshwa kwenye moyo wa Muhammad(s.a.w.
w
)
.
Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima. Ni amri itokayo kwetu.
Wafasiri wametofautiana kuhusu ‘jambo la hikima.’ wengi wameonelea ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anagawanyia waja wake riziki na muda wa kifo katika usiku huu. Pia anasamehe makosa mengi kwa anayemtaka.
Wengine wakasema kuwa Makusudio ya jambo la hikima ni ubainifu wa kila jambo la dini uliokuja katika Qur’an. Lakini ikumbukwe Mwenyezi Mungu amesema katika huu, na hakusema katika hii. Ubainifu zaidi utaku- ja katika Juz. 30 (97).
Hakika Sisi ndio wenye kutuma. Ni rehema itokayo kwa Mola wako.
Yaani Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad kuwa ni rehema kwa viumbe vyote; kama ilivyoelezwa katika Juz. 17 (21:107).
Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Anasikia kauli na anajua yaliyo kwenye nia.
Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, ikiwa nyinyi mna yakini.
Mwenye akili akiuangalia ulimwengu kwa mtazamo safi na kutilia maanani, atashuhudia kwa ikhlasi na yakini kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mmiliki wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake na kwambaYeye Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha.
Hakuna yeyote anayeleta uhai isipokuwa Yeye. Na muda ukifika hakuna kinachoweza kuusogeza mbali wala karibu.
Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo
. Vipi basi mnaabudu mizimu na kumtii shetani badala ya Mwenyezi Mungu?
Lakini wao wamo katika shaka wakicheza.
Wametia shaka ya kutumwa Muhammad(s.a.w.
w
)
pamoja na dalili na ubainifu na wanafanya mchezo na mwisho wao na yale wanayotakiwa kuyafanya.
فَارْتَقِبْ يَوْمَ تَأْتِي السَّمَاءُ بِدُخَانٍ مُّبِينٍ ﴿١٠﴾
10. Basi ingoje siku ambayo mbingu italeta moshi ulio dhahiri.
يَغْشَى النَّاسَ هَـٰذَا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١١﴾
11. Utakaowafunika watu. Hii ni adhabu chungu!
رَّبَّنَا اكْشِفْ عَنَّا الْعَذَابَ إِنَّا مُؤْمِنُونَ ﴿١٢﴾
12. Mola wetu! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
أَنَّىٰ لَهُمُ الذِّكْرَىٰ وَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مُّبِينٌ ﴿١٣﴾
13. Kutafaa nini kukumbuka kwao? Na alikwishawafikia Mtume mwenye kubainisha.
ثُمَّ تَوَلَّوْا عَنْهُ وَقَالُوا مُعَلَّمٌ مَّجْنُونٌ ﴿١٤﴾
14. Kisha wakamgeuzia uso, na wakasema: Amefunzwa, mwenda wazimu.
إِنَّا كَاشِفُو الْعَذَابِ قَلِيلًا إِنَّكُمْ عَائِدُونَ ﴿١٥﴾
15. Hakika tutaiondoa adhabu kidogo, (lakini) nyinyi kwa yakini mtarudia.
يَوْمَ نَبْطِشُ الْبَطْشَةَ الْكُبْرَىٰ إِنَّا مُنتَقِمُونَ ﴿١٦﴾
16. Siku tutakayowashika kwa mashiko makubwa, hakika sisi ni wenye kutesa.
وَلَقَدْ فَتَنَّا قَبْلَهُمْ قَوْمَ فِرْعَوْنَ وَجَاءَهُمْ رَسُولٌ كَرِيمٌ ﴿١٧﴾
17. Na hakika kabla yao tuliwajaribu watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
أَنْ أَدُّوا إِلَيَّ عِبَادَ اللَّـهِ إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٨﴾
18. Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.
وَأَن لَّا تَعْلُوا عَلَى اللَّـهِ إِنِّي آتِيكُم بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿١٩﴾
19. Na msijitukuze mbele ya Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitawaletea uthibitisho ulio wazi.
وَإِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُمْ أَن تَرْجُمُونِ ﴿٢٠﴾
20. Nami najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu, ili msinirujumu.
وَإِن لَّمْ تُؤْمِنُوا لِي فَاعْتَزِلُونِ ﴿٢١﴾
21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
SIKU AMBAYO MBINGU ITALETA MOSHI
Aya 10 – 21
MAANA
Basi ingoje siku ambayo mbingu italeta moshi ulio dhahiri, utakaowafunika watu.
Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Nabii wake mtukufu Muhammad(s.a.w.
w
)
akimwahidi kumkubalia dua yake. Hiyo ni baada ya Makuraishi kuzidi sana kumuudhi Mtume(s.a.w.
w
)
. Akawaombea dua mbaya, akasema:“Ewe Mola wangu wafanyie miaka kama ya Yusuf.”
Basi mvua ikakatika na ardhi ikawa kame, makuraishi wakapatwa na njaa mpaka wakawa wanakula mifupa na mizoga. Kutokana na njaa mtu alikuwa akiona kama moshi mbinguni.
Wakasema: Hii ni adhabu chungu! Mola wetu! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
Walimjia Mtume(s.a.w.
w
)
na kumwambia: Muombe Mwenyezi Mungu (s.w.t) atuondolee adhabu hii na sisi tutaamini risala yako.
Kutafaa nini kukumbuka kwao? Na alikwishawafikia Mtume mwenye kubainisha. Kisha wakamgeuzia uso, na wakasema: Amefunzwa, mwendawazimu.
Walitoa ahadi ya kuwaidhika na kukumbuka kama Mwenyezi Mungu atawaondolea adhabu, lakini wao hawatubii wala hawatekelezi ahadi. Kwani hawakushuhudia dalili za Tawhid, lakini pamoja na hayo wakamshirikisha Mwenyezi Mungu? Je, hakuwajia Mtume na hoja zilizo wazi wakamkadhibisha? Wakasema ni mwendawazimu, anafundishwa baadhi ya matamshi na jinni au mtu, kisha anakuja kutusomea?
Hakika tutaiondoa adhabu kidogo,
(lakini)nyinyi kwa yakini mtarudia.
Makusudio ya adhabu hapa ni adhabu ya kahati na njaa. Kurudia, ni kuvunja ahadi kwa kurudia makosa. Maana ni kuwa tutawaondolea shida waliyo nayo, katika baadhi ya wakati, lakini sisi tunajua wazi kuwa watavunja ahadi. Lakini hiyo ni katika upande wa kutimiza na kuondoa visababu.
Siku tutakayowashika kwa mashiko makubwa, hakika sisi ni wenye kutesa.
Hili ni tishio kuwa Mwenyezi Mungu siku ya kiyama atawashika kwa adhabu ya kufedhehesha kutokana na uasi na jeuri yao.
Kwa ufupi ni kuwa makuraishi walimuudhi Nabii(s.a.w.
w
)
, naye akawombea dua mbaya. Ilipowapata shida walimkimbilia Mtume na kumwahidi kutubia, lakini walivunja ahadi baada ya kupata faraja, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawatishia kwa Jahannam na makazi mabaya.
Na hakika kabla yao tuliwajaribu watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
Yaani kabla ya makuraishi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwapa mtihani watu wa Firauni kwa neema na kumakinishwa katika ardhi; kama walivyopewa mtihani makuraishi kwa kuondolewa adhabu. Mwenyezi Mungu alimtuma Musa kwa watu wa Firauni; kama alivyomtuma Muhammad kwa makuraishi. Wote wakaasi amri ya Mwenyezi Mungu.
Na Musa akamwambia Firauni na watu wake:Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.
Firauni alikuwa akiwakandamiza wana wa Israil kwa kuwachinja watoto wa kiume na kuwabakisha wa kike kwa ajili ya utumishi. Kwa hiyo Musa akamtaka Firauni amwachie ili aende nao anapotaka. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَأَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَا تُعَذِّبْهُمْ ﴿٤٧﴾
“Basi tuwachie wana wa Israil wala usiwaadhibu.” Juz. 16 (20:47).
Na msijitukuze mbele ya Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitawaletea uthibitisho ulio wazi.
Haya ni maneno ya Musa kwa watu wa Firauni. Maana ni kuwa msijiweke juu ya twaa ya Mwenyezi Mungu, kwani mimi nina hoja za kutosha za kuthibitisha haki.
Nami najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu, ili msinirujumu.
Najilinda na ninakimbilia kwake ikiwa mtanikusudia ubaya.
Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
Achaneni na mimi, kama hamtaki kunisadiki na kuitikia mwito wangu.
فَدَعَا رَبَّهُ أَنَّ هَـٰؤُلَاءِ قَوْمٌ مُّجْرِمُونَ ﴿٢٢﴾
22. Ndipo akamwomba Mola wake kuwa watu hawa ni wakosefu.
فَأَسْرِ بِعِبَادِي لَيْلًا إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ ﴿٢٣﴾
23. Basi nenda na waja wangu usiku. Hakika mtafuatwa.
وَاتْرُكِ الْبَحْرَ رَهْوًا إِنَّهُمْ جُندٌ مُّغْرَقُونَ ﴿٢٤﴾
24. Na iache bahari imetulia, hakika wao ni jeshi litakalozamishwa.
كَمْ تَرَكُوا مِن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٢٥﴾
25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
وَزُرُوعٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ ﴿٢٦﴾
26. Na mimea na mahala pa fahari!
وَنَعْمَةٍ كَانُوا فِيهَا فَاكِهِينَ ﴿٢٧﴾
27. Na neema walizokuwa wakijistareheshea!
كَذَٰلِكَ وَأَوْرَثْنَاهَا قَوْمًا آخَرِينَ ﴿٢٨﴾
28. Ndivyo hivyo! na tukawarithisha haya watu wengine.
فَمَا بَكَتْ عَلَيْهِمُ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ وَمَا كَانُوا مُنظَرِينَ ﴿٢٩﴾
29. Mbingu na ardhi hazikuwalilia; wala hawakupewa muda.
وَلَقَدْ نَجَّيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنَ الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿٣٠﴾
30. Na hakika tuliwaokoa wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha.
مِن فِرْعَوْنَ إِنَّهُ كَانَ عَالِيًا مِّنَ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾
31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupituka mipaka.
وَلَقَدِ اخْتَرْنَاهُمْ عَلَىٰ عِلْمٍ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿٣٢﴾
32. Na hakika tuliwachagua kwa ujuzi kuliko walimwengu wengine.
وَآتَيْنَاهُم مِّنَ الْآيَاتِ مَا فِيهِ بَلَاءٌ مُّبِينٌ ﴿٣٣﴾
33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
WATU HAWA NI WAKOSEFU
Aya 22 – 33
MAANA
Ndipo akamwomba Mola wake kuwa watu hawa ni wakosefu.
Musa alikata tamaa na Firauni na watu wake, ndipo akawaombea mabaya na akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu waharakishie maangamizi duniani kwa sababu ya kufuru yao.” Mwenyezi Mungu akamwitikia dua yake na kumwambia:Basi nenda na waja wangu usiku. Hakika mtafuatwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha atoke Misri yeye na wana wa Israil usiku na akamjulisha kuwa Firauni na watu wake watawafuata.
Na iache bahari imetulia, hakika wao ni jeshi litakalozamishwa.
Fuata njia ya baharini, ukishavuka upande wa pili, wewe iwache kama ilivyo, kwa sababu jeshi la adui litaingia na wataangamia wote.
Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! Na mimea na mahala pa fahari! Na neema walizokuwa wakijistareheshea! Ndivyo hivyo! na tukawarithisha haya watu wengine.
Watu wa Firauni walikuwa katika starehe za vyakula na vinywaji, wana utawala, makasri, mito na matunda. Mwenyezi Mungu akawatumia Musa kuwalingania kwenye uadilifu na kuacha ufisadi katika nchi, lakini hawakumwitikia mlinganiaji wa Mwenyezi Mungu. Basi akawaangamiza na akawarithisha watu ambao hawakuwa na uhusiano wowote na wao.
Sheikh Al-Maraghi anasema akifasiri Aya hii: “Wakati fulani wasyria walichukua Misr na wakati mwingine ikachukuliwa na wababilon na pia wahabeshi. Kisha wafursi, wayunani (wagiriki), waroma, na waarabu. Vile vile utawala wa Altoulenion, Alikhchidip, Fatimid, Ayyubids, Mamluk, Uturuki, Ufaransa na Uingereza. Na sisi hivi sasa tunapigana ili kuwatoa katika nchi yetu ili tuweze kumakinika na uhuru wa chi yetu.”
Sheikh huyu alikuwa katika zama za mfalme Faruk Bin Fuad. Nasi tunaunganisha maneno yake kwa kusema: Hivi sasa Uzayuni umepora Sinai na ukanda wa mashariki katika mfereji wa Suez, kwa msaada U.S.A. kambi mpya ya ukoloni.
Na wamisri wanajitahidi na kupigana kuwatoa wavamizi kwenye ardhi yao. Haya ndio maisha ya jihadi na mapigano. Mtu kufa na bunduki mkononi akipigania nchi yake na heshima yake ni bora zaidi kuliko kuishi maisha ya udhalili na utwevu.
Mbingu na ardhi hazikuwalilia.
Hiki ni kinaya cha kutowapa umuhimu watu wa Firauni pale Mwenyezi Mungu alipowagharikisha baharini,wala hawakupewa muda;
bali Mwenyezi Mungu aliharakisha maangamizi yao duniani.
Na hakika tuliwaokoa wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha
ambayo ni kuuawa watoto wao wa kiume na kutumikishwa wanawake wao na mabinti zao na pia kudhalilishwa wanaume kwa kazi za sulubu
Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupituka mipakaya kila ufisadi, uasi na kiburi. Na hakika tuliwachagua kwa ujuzi kuliko walimwengu wengine.
Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Kitabu chake, amewasifu kwa sifa mbaya wana wa Israil, akasajili
makosa makubwa waliyoyafanya; kama vile usaliti, kuifanyia jeuri haki na kula mali kwa dhulma.
Vile vile amewasifu kwa ukafiri, dhulma na akawalaani katika Aya kadhaa na kuwatishia kwa adhabu kali.
Kwa maana hii ndio wafasiri wakakongamana kuwa makusudio ya walimwengu, katika Aya hii na mfano wake, ni walimwengu wa zama zao si kila zama.
Katika Juz. 1 (2:47-48) tulisema kuwa Mwenyezi Mungu aliwafadhilisha juu ya watu wa zama hizo kwa vile tu Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume wengi kutokana na wao. Hivi sasa tumepata wazo kutokana na Aya tuliyo nayo kuwa makusudio ya walimengu ni Firauni na wale walioukubali uungu wake na wala sio watu wote wa wakati ule. Siri ya kufadhilishwa huko ni kuwa waisrail hawakumwabudu Firauni kama wamisri waliotangulia.
Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
Makusudio ya ishara hapa ni miujiza; kama kupasuka bahari, kufunikwa na kiwingu, kuteremshiwa Manna na Salwa na kububujika maji kutoka kwenye jiwe. Na Makusudio ya majaribio ni neema. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٣٥﴾
“Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na heri na kwetu mtarejeshwa.” Juz. 17 (21:35).