3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ ﴿٦٠﴾
60. Na Siku ya Kiyama utawaona wale ambao wamemsingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makazi ya wanaotakabari?
وَيُنَجِّي اللَّـهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦١﴾
61. Na Mwenyezi Mungu atawaokoa walio na takua kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utao wagusa, wala hawatahuzunika.
اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ ﴿٦٢﴾
62. Mwenyezi Mungu Mungu ndiye Muumba wa kila kitu; na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.
لَّهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٦٣﴾
63. Anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale ambao wamezikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye hasara.
قُلْ أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَأْمُرُونِّي أَعْبُدُ أَيُّهَا الْجَاهِلُونَ ﴿٦٤﴾
64. Sema: Je! Mnaniamrisha nimwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi majahili?
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٦٥﴾
65. Na kwa hakika umepewa wahyi na waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukishirikisha amali zako zitapomoka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.
بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ ﴿٦٦﴾
66. Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٧﴾
67. Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu haki ya kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Ametakasika na Ametukuka na wanayomshirikisha nayo.
WALIOMSINGIZIA UWONGO MWENYEZI MUNGU
Aya 60 – 67
MAANA
Na Siku ya Kiyama utawaona wale ambao wamemsingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makazi ya wanaotakabari?
Kila anayemnasibishia Mwenyezi Mungu yale asiyokuwa na ujuzi nayo basi atakuwa amemsingizia Mwenyezi Mungu; iwe amemnasibishia kuwa na washirika, mke na mtoto, au kazi za Mwenyezi Mungu; kama kuingilia utume ukhalifa, hukumu au kutoa fatwa kwa jina la dini.
Aliulizwa Imam Ja’far As-sadiq
kuhusiana na maana ya Aya hii, akasema:“Mwenye kudai uimamu usiotokana na Mwenyezi Mungu, atakuwa amemsingizia uongo Mwenyezi Mungu”
Muulizaji akasema: Hata kama ni Alawi. Imam akasema: hata kama ni Alawi. Muulizaji akaendelea kuuliza: Hata kama ni Fatimi, Imam akasema:Hata kam ni Fatimi.”
Malipo ya mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kufufuliwa akiwa na uso uliosawijika, katika kundi lililoandaliwa Jahannam na Mwenyezi Mungu, makazi mabaya kabisa.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wanotakabari’ baada ya kauli yake ‘wale ambao wamemsingizia Mwenyezi Mungu,’ inaashiria kuwa kumsingizia Mwenyezi Mungu ni kiburi.
Na Mwenyezi Mungu atawaokoa waliona takua kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utaowagusa, wala hawatahuzunika.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahadharisha wasingiziaji na moto wa Jahannam, sasa anawabashiria wakweli na wenye takua, kuokoka na moto na kila ubaya. Zaidi ya hayo hawatakuwa na huzuni wala majuto kwa yale waliyoyakosa duniani.
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu.
Kila kilichoko akiwemo mtu, mnyama mimea na mawe, kinafahamisha kuweko kwa Mwenyezi Mungu kwa sura ya ufundi wa mjengaji kutokana na jengo lenyewe na aliyekitengeneza na kila jingo
Na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.
Yaani ni mwenye kusimamia, kwa sababu kila kitu kimepatikana kwa uweza wa Mwenyezi Mungu na kitabaki chini ya uangalizi wake mpaka atakapotaka, vinginevyo itakua hakina maana.
Anazo funguo za mbingu na ardhi.
Funguo ni kinaya cha kuwa Mwenyezi Mungu ni mzingatiaji wa ulimwen- gu na ni mjuzi wa yote yanayopita humo kuanzia chembe ndogo hadi sayari kubwa: “Na ziko kwake funguo za ghaibu” Juz. 7 (6:59).
Na wale ambao wamezikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye hasara.
Makusudio ya ishara za Mwenyezi Mungu ni ulimwengu na nidhamu yake ya ajabu ambayo lau itakoseka kwa kiasi cha unywele tu, basi utaharabika.
Maana ya kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu ni kutozikubali dalili za nidhamu hii kuwa kuna aliyezipanga na uhandisi na mhandisi wake.
Wakadhibishaji wamezitia hasara akili zao na dalili hizi, kwa sababu zimepofuka na hisia. Vile vile wamezitia hasara nafasi zao na akhera, kwa vile wamezichagulia ukafiri na inadi; na Jahannam yatakuwa ndio makazi ya kila kafiri mwenye inadi.
Sema: Je! Mnaniamrisha nimwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi majahili?
Kuna mapokezi yanayosema kuwa washirikina walimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
na kusema: Tutakupa mali itakayokufanya uwe tajiri zaidi ya wote katika Makka na tutakuoza msichana unayemtaka, kwa sharti ya kuwa uache mwito wako. Ndio ikashuka Aya hii.
Iwe riwaya hii ni sahihi au la lakini inafafanua zaidi na Aya hii. Ni vizuri tudokoe maneno yafuatayo kutoka katika makala ya marehemu Mustafa Sadiq Ar-rafii, yenye kichwa cha maneno ‘Dirhamu na dinari’: “Nimewaona baadhi ya mafakihi wakitoa mawaidha na kuwaambia watu halali na haramu, lakini hakika wanawafanyia maskhara vile anavyomfanyia maskhara mwizi anayempa mawaidha mwizi mwingine na kumwambia usiibe.”
Hali hii pia iko kwa waandishi wanasiasa na wengineo wanaobeba nembo za uzalendo na ubinadamu. Ar-rafii anaendelea kusema: “Mwenye kutukuza dirhamu na dinari (pesa) huwa anautukuza unafiki, tamaa na uwongo… Hakika haiba ya Uislamu ni kujitolea maisha sio kupupia maisha, na kuwasaidia waumini sio kuwafanyia uadui. Na utajiri unapimwa kwa inavyofanya kazi mali sio kukusanya mali.”
Na kwa hakika umepewa wahyi na waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukishirikisha amali zako zitapomoka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.
Makusudio ya kupomoka (kuanguka) amali ni kukosa thawabu. Kushirikisha ni muhali kwa mitume, lakini kukadiria muhali sio muhali. Zaidi ya hayo ni kuwa kutahadharishwa kitu hakufahamishi kuwa aliyehadharishwa anadhaniwa kuwa atafanya alilohadharishwa.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hakubali ibada ya yeyote ila ikiwa imetakata na kuwa safi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Mwenye kumwabudu Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine, basi hastahiki thawabu; hata akiwa ni kama mtume. Tumefafanua kuanguka amali katika Juz. 2 (2:216 – 218), kifungu cha ‘Kupomoka.’
Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
Kwa dhahiri hii ni amri, lakini kwa hakika ni kuelezea kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
haabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu wala hamshukuru yeyote asiyekuwa yeye. Imekuja kwa tamko la amri kutanabahisha waja kuwa ibada na shukrani ni lazima iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mmoja tu.
Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) mara nyinyi huwaambia wote kwa kumtuma Mtume wake mtukufu: “Na kwamba elekeza uso wako kwenye dini safi, wala usiwe miongoni mwa washirikina.” Juz. 11 (10:105), “Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe...” Juz. 12 (11:112) na “Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana...” Juz. 12 (11:114).
Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu haki ya kadiri yake
kwa sababu wao wamemkataa na kuamini masanamu na pesa.
Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume.
Hiki ni kinaya cha ukuu wa Mwenyezi Mungu na uweza wake; na kwamba mbingu na ardhi na vyote viliomo baina yake vinanyenyekea amri yake.
Ametakasika na Ametukuka na wanayomshirikisha nayo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametakasika na kila shirki na wanayoyasema kuwa ana mkono wa kuume. Na pia ametakasika na ufananisho wanaomsifu nao majahili.
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ ﴿٦٨﴾
68. Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka. Kisha itapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاءِ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٦٩﴾
69. Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Mola wake, na Kitabu kitawekwa, Na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.
وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٧٠﴾
70. Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyafanya, na Yeye anayajua sana wanayoyatenda.
وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧١﴾
71. Na wale ambao wamekufuru watasukumwa kwenye Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu wakiwasomea Aya za Mola wenu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii? Watasema: Ndio! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.
قِيلَ ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ ﴿٧٢﴾
72. Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari.
WALIOKUFURU WATASUKUMWA
Aya 68 – 72
MAANA
Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka.
Kupuziwa parapanda ni kinaya cha ukelele. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ ﴿٤٢﴾
“Siku watakaposikia ukelele kwa haki, hiyo ndiyo siku ya kutoka.” (50:42).
Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa ukelele au mpulizo huu utakaririka mara tatu: Wa kwanza ni ule ilioelezwa katika Aya isemayo:
وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ ﴿٨٧﴾
“Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu.” Juz. 20 (27:87).
Ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka ni yule mwenye takua ambaye umemtangulia wema.
Mpulizo wa pili ni wa mauti ulioashiriwa kwenye Aya hii tuliyo nayo. Na makusudio ya ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka ni kuwa watu wa ardhini watakufa wote na wa mbinguni hawatabaki isipokuwa ambaye Mwenyezi Mungu atamtaka.
Wafasiri wametofautiana kuhusiana na huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtaka katika wa mbinguni. Ikasemekana kuwa ni Jibril na Israfil. Wengine wakasema ni mashahidi. Mwingine hata akathubutu kusema ni Mwenyezi Mungu – Tunamuomba msamaha Mwenyezi Mungu na tunatubu kwake.
Sio mbali kuwa kusema ila ambaye Mwenyezi Mungu amemtaka, sio hakika bali ni majazi ya kuwa amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾
“Kila kilichoko juu yake kitatoweka na itabaki dhati ya Mola wako mwenye utukufu na heshima” (55:26-27).
Mpulizo wa tatu ni wa ufufuo amabao amaeuashiria Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kusema:Kisha itapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea
hukumu ya Mwenyezi Mungu kwao.
Kwenye Nahajul-balagha imeelezwa: “Na itapulizwa parapanda, kila chenye uhai kitakufa na kila sauti itakuwa bubu, milima na majabali yataporomoka na mawe yageuke mchanga na iwe tamabarare. Hakutakuwa na muombezi wa kuombea wala ndugu wa kutetea wala udhuru utakaonufaisha.
”
Na ardhi itang’ara kwa Nuru ya Mola wake.
Makusudio ya ardhi hapa ni ardhi ya ufufuo na mkusanyiko. Nayo itang’arishwa na nuru ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu yenyewe ni twahara isyokuwa na aina yoyote ya upotevu na ufisadi; haku- na isipokuwa haki na uadilifu.
Na Kitabu kitawekwa, yaani mandishi ya matendo yote:
وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ﴿١٣﴾
“Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.” Juz. 15 (17:13).
Mulla Sadra anasema katika Al-asfar: “Mwenye kutenda kitendo au kusema kauli, athari yake inajitokeza kwenye nafsi yake na moyo wake.
Athari hii inayopatikana kwenye moyo na roho iko kama nakshi na maandishi katika vitabu na mbao. Nyoyo na roho hizo, ambazo zina athari ya vitendo na kauli, kwa lugha ya sharia zinaitwa kurasa za matendo.”
Na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa. Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyafanya, na Yeye anayajua sana wanayoyatenda.
Makusudio ya mashahidi hapa ni manaibu wa mitume katika kufikisha ujumbe wao na desturi zao kwa watu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawafufua watu kwa ajili ya hisabu. Atawaleta manabii wawe mashahidi kwa manaibu wao kuwa wao walichukua ujumbe kwa manabii ili waufikishe kwa watu.
Kisha manaibu nao watatoa ushahidi kuwa wao waliwafundisha watu na waliufikisha ujumbe kwa ukamilifu. Baada ya kupatikana ushahidi wa manabii kwa manaibu na wa manibu kwa watu, hapo Mwenyezi Mungu atawahukumu wote kwa uadilifu bila ya kumpunguzia thawabu mtiifu wala kumzidishia adhabu Muasi.
Yeye anawajua zaidi wote, wakiwemo manabii na mashahidi, kuliko nafsi zao. Amewaita hapa kwa ushahidi kukamilisha hoja na kuondoa visababu vyote.
Tazama Juz. 2 (2:143).
Na wale ambao wamekufuru watasukumwa kwenye Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia itafunguliwa milango yake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja, katika Kitabu aina kwa aina ya dhabu ya wakosefu; kama vile: udhalili na utwevu, upofu na kusawijika uso, minyororo na nguo za moto, chakula cha Zaqqum na kinywaji cha usaha na kusukumwa na malaika kupelekwa kwenye Jahannam ili wawe kuni zake. Hao malaika wana miadi nao ya kuwangoja, ndio maana watakuta milango tayari iko wazi.
Na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu wakiwasomea Aya za Mola wenu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii?
Makusudio ya swali hili ni kutahayariza na kwamba wao ndio waliojichagulia mwisho huu mbaya.
Watasema: Ndio! Lakini limekwishathibiti neno la adhabu juu ya makafiri.
Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾ فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١١﴾
“Na watasema: lau tungelikuwa tunasikia au kutia akilini, tusingelikuwa katika watu wa Motoni! Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa motoni!” (67:10-11).
Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo.
Basi ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari kwenye haki na kutoka kwenye uadilifu.
Lau kusingelikuwa na dalili nyingine ya kuandaliwa Jahannam isipokuwa kwa wenye kiburi, mataghuti, wafisadi na wapotevu tu, ingelitosha. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ ﴿١٤٥﴾
“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini motoni. Juz. 5 (4:145)
Akasema tena:
إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا ﴿٢١﴾ لِّلطَّاغِينَ مَآبًا ﴿٢٢﴾
“Hakika Jahannam inangojea. Ni marejeo kwa wenye kupetuka mipaka” (78:21-22).
Huko nyuma tumewahi kusema kuwa lau kusingeliku na mahakama, huko akhera, ya kisasi cha aliyedhulimiwa kwa dhalimu, basi ingelikuwa aliyeuliwa kidhulma ana hali mbaya zaidi ya aliyemuua.
Tazama Juz. 11 (10:3-4) kifungu cha: ‘malipo ni lazima.’
وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ ﴿٧٣﴾
73. Na waliomcha Mola wao watapelekwa Peponi kwa makundi, mpaka watakapoifikia, nayo milango yake imekwishafunguliwa, walinzi wake watawaambia: Salaamun Alaikum, (Amani iwe juu yenu!) Mmekua wema. Basi ingieni humu mkae milele.
وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿٧٤﴾
74. Na watasema: Alhamdulillah, (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
وَتَرَى الْمَلَائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَقِيلَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٧٥﴾
75. Na utawaona Malaika wak- izunguka pembeni mwa Arshi ya Mwenyezi Mungu, wakimsabihi na kumsifu Mola wao. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote!
WALIOMCHA MOLA WAO WATAPELEKWA PEPONI
Aya 73 – 75
MAANA
Na waliomcha Mola wao watapelekwa Peponi kwa makundi, mpaka watakapoifikia, nayo milango yake imekwishafunguliwa, walinzi wake watawaambia: Salaamun Alaikum, (Amani iwe juu yenu!) Mmekua wema. Basi ingieni humu mkae milele.
Wakosefu watapelekwa kwenye Jahannam huku Malaika wa adhabu wakiwasukuma kwa nguvu na kwa udhalili. Wenye takua wanaingia Peponi wakiwa wamezungukwa na Malaika kwa taadhima na takrima na watasema:
Alhamdulillah, (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
Wanaosema hayo ni waumini. Makusudio ya ardhi hapa ni ardhi ya Peponi. Wataitumia kama vile anavyotumia mrithi, mali aliyoachiwa. Kule duniani waliifanyia kazi Pepo wakitegemea na kuamini aliyoahidi Mwenyezi Mungu kwa wenye takua na subira. Watapoiona watafurahia na kumsifu Mwenyezi Mungu wakijua kuwa ahadi yake ni ya kweli na haki.
Imeelezwa kwenye Nahajul-balagha: “Malaika watawazunguka watu Peponi, watawashukia kwa upole, na watawafungulia milango ya mbingu. Watawaandalia sehemu za heshima alizowafahamisha Mwenyezi Mungu, akaridhia mahangaiko na kusifia makazi yao”
.
Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Arshi ya Mwenyezi Mungu, wakimsabihi na kumsifu Mola wao.
Katika Juz. 8 (7:53), tumebainisha, kwa ushahidi wa Qur’ani, kuwa Makusudio ya Arshi ni kuwa amri yote ni ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo maana yake hapa ni kuwa Malaika hawafanyi lolote ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu; kama ulivyokuja wasifu wao katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ ﴿٢٦﴾ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ ﴿٢٧﴾
“Bali hao ni waja waliotukuzwa. Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.”
Juz. 17 (21:26-27)
Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote!
Yaani muasi hatazidishiwa adhabu, wala mtiifu hatapunguziwa thawabu. Kuna tafsiri nyingine zinazasema kuwa Mwenyezi Mungu alipoanza kuumba alisema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.
Baada ya kufa viumbe na kuwafufua na kutulia watu wa peponi atasema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote, ili awafundishe waja wake adabu yake ya kuanza kila jambo kwa sifa njema na kumalizia kwa sifa njema.
MWISHO WA SURA YA THELATHINI NA TISA: SURAT AZ-ZUMAR