6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُم مِّثْلَ يَوْمِ الْأَحْزَابِ ﴿٣٠﴾
30. Na akasema yule aliyeamini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia mfano wa siku za makundi.
مِثْلَ دَأْبِ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَالَّذِينَ مِن بَعْدِهِمْ وَمَا اللَّـهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِّلْعِبَادِ ﴿٣١﴾
31. Mfano wa hali ya watu wa Nuh na A’di na Thamudi na wale wa baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja.
وَيَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ يَوْمَ التَّنَادِ ﴿٣٢﴾
32. Na enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia Siku ya kunadi.
يَوْمَ تُوَلُّونَ مُدْبِرِينَ مَا لَكُم مِّنَ اللَّـهِ مِنْ عَاصِمٍ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾
33. Siku mtakapogeuka kurudi nyuma, hamtakuwa na wa kuwalinda kwa Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi huyo hana wa kumwongoa.
وَلَقَدْ جَاءَكُمْ يُوسُفُ مِن قَبْلُ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا زِلْتُمْ فِي شَكٍّ مِّمَّا جَاءَكُم بِهِ حَتَّىٰ إِذَا هَلَكَ قُلْتُمْ لَن يَبْعَثَ اللَّـهُ مِن بَعْدِهِ رَسُولًا كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُّرْتَابٌ ﴿٣٤﴾
34. Na alikwishawajia Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyowaletea; mpaka alipokufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta tena Mtume baada yake. Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka.
الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّـهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ وَعِندَ الَّذِينَ آمَنُوا كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ قَلْبِ مُتَكَبِّرٍ جَبَّارٍ ﴿٣٥﴾
35. Wale ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyowafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walioamini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo chapa juu ya kila moyo wa jeuri anayejivuna.
MWENYEZI MUNGU HADHULUMU WAJA
Aya 30 – 35
MAANA
Na akasema yule aliyeamini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia mfano wa siku za makundi. Mfano wa hali ya watu wa Nuh na A’di na Thamudi na wale wa baada yao.
Makusudio ya makundi hapa ni watu waliounda vikundi dhidi ya mitume wao; kwa dalili ya kauli yake: “Mfano wa hali ya watu wa Nuh na A’di na Thamudi na wale wa baada yao.”
Aliposema Firauni: ‘Wala siwaongozi ila kwenye njia ya uongofu’ yule mumin naye akasema: ‘mimi vile vile si kusema niliyowaambia ila kwa kuhofia yasiwapate maangamizi kama yalivyowapata wa mwanzo, pale walipowakadhibisha manabii wao.
Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja,
lakini wao wenyewe wanajidhulumu kwa kuwakadhibisha mitume na kuifanyia jeuri amri ya Mwenyezi Mungu.
Baada ya yule mumin kuwahadharisha na adhabu ya dunia, aliwahadharisha na adhabu ya Akhera kwa kusema:
Na enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia Siku ya kunadi.
Siku ya kunadi ni Siku ya Kiyama, ambapo watu watanadiwa kwa ukulele; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ ﴿٤١﴾
“Siku atakaponadi mwenye kunadi kutoka mahali karibu” (50:41).
Siku mtakapogeuka kurudi nyuma mkijaribu kukimbia adhabu ya moto, lakini wapi! Hamtakuwa na wa kuwalinda kwa Mwenyezi Mungu.
Vipi mtaweza kumkimbia na hali yeye ndiye mwenye nguvu, kwenye jambo lake, hapingwi wala hazuiwi.
Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi huyo hana wa kumwongoa.
Yaani atakayefuata njia ya upotevu basi Mwenyezi Mungu atampoteza; kama vile anayekunywa sumu, Mwenyezi Mungu atamuua tu, wala hutap- ata atakayemponesha na kumpa uhai.
Na alikwishawajia Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyowaletea.
Yaani enyi wamisr! Yusuf aliwajia mababa zenu, wakatia shaka utume wake; kama hivyo nanyi mnatia shaka utume wa Musa. Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu, imeelezwa kuwa Yusuf ni jina la kiibrania (Hebrew) lenye maana ya anayezidisha. Mama yake alimwita hivyo, ili apate ziada ya mtoto mwingine. Naye alikufa akiwa na miaka 110.
Mpaka alipokufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta tena Mtume baada yake.
Hii inaashiria kuwa wao walifurahi kwa kufa Yusuf, kwa vile watakuwa huru na taklifa za Mwenyezi Mungu. Wakasema bila ya kujali, kwa msukumo wa matamanio kwamba Mwenyezi Mungu hatapeleka tena Mtume baada ya Yusuf mpaka Siku ya Mwisho.
Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka
kuhusu Mwenyezi Mungu na haki. Mwenyezi Mungu anampoteza mwenye kupita kiasi, kwa sababu ametoka katika uongofu na akaingia kwenye upotevu kwa uchaguzi wake mbaya na upofu.
Wale ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyowafikia.
Makusudio ya wale wanaojadiliana ni wale wenye kupita kiasi wenye shaka. Ishara za Mwenyezi Mungu ni dalili za umoja wake, unabii wa mananbii wake na hoja wazi. Maana ni kuwa wakosefu wanajibu hoja za Mwenyezi Mungu kwa matamanio yao na kuiga mababa zao.
Ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walioamini kujadili wakosefu bila ya ujuzi wala mwongozo au kitabu.
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo chapa juu ya kila moyo wa jeuri anayejivuna.
Kiburi na kujidai ndio sababu hasa ya kupigwa chapa moyoni. Hilo limetegemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa vile Yeye ndiye aliyejaalia kiburi kuwa ndio sababu ya upofu wa moyo; sawa na alivyoujaalia ujinga kuwa ndio sababu ya kudangana na kuwa mbali na haki na akajaalia kusoma na kufanya utafiti ni sababu ya elimu na mwamko.
وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَّعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ ﴿٣٦﴾
36. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia.
أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَـٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا وَكَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِفِرْعَوْنَ سُوءُ عَمَلِهِ وَصُدَّ عَنِ السَّبِيلِ وَمَا كَيْدُ فِرْعَوْنَ إِلَّا فِي تَبَابٍ ﴿٣٧﴾
37. Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyopambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu.
وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُونِ أَهْدِكُمْ سَبِيلَ الرَّشَادِ ﴿٣٨﴾
38. Na yule ambaye aliamini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni, nitawaongoza njia ya uongofu.
يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ ﴿٣٩﴾
39. Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe yenye kupita tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.
مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَمَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ يُرْزَقُونَ فِيهَا بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٤٠﴾
40. Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo, na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.
NIZIFIKIE NJIA
Aya 36 – 40
MAANA
Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia. Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu.
Firauni alimtaka waziri wake Hamana amjengee mnara mrefu ili apande mbinguni kwenda kumtafuta Mungu wa Musa. Alifanya hivi akiwa anajua kabisa kwamba yeye hawezi kufanya hivyo, lakini vile vile anajua kuwa katika anaowatawala kuna wenye akili fupi wasiokwa na mwamko, watakaomsadiki atakayosema. Kwani kauli yake hii sio kubwa zaidi ya kusema: Mimi ndie Mola wenu mkuuu; na asingejasiri kusema hivyo lau sikuweko watakaomwambia: ndio, wewe ndiye Mola mkuu.
Hivi sasa tukiwa katika karne ya ishirini, karne ya maendeleo hadi mtu kufika mwezini, lakini bado Dalai Lama anapata wanaomwambia: Wewe ni Mungu, na Agha Khan naye anapata wanaomwambia; Wewe ni nusu mungu. “Kila mahali kuna Al-kaaba na imam”
Na hivi ndivyo Firauni alivyopambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa njia.
Mambo mawili yanampambia mtu matendo yake mabaya: Kufuata matamanio na kuendelea na ujinga. Matamanio yalimpambia Firauni kudai ungu na ujinga ukawapambia wanaomtii.
Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu; yaani katika hasara.
Kila aliyejaribu na atakayejaribu kuwahadaa watu na kuwafanyia vitimbi, atakuwa katika hasara; hata kama atakuwa na utawala wa Firauni na mali ya Qaruni.
Na yule ambaye aliamini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni, nitawaongoza njia ya uongofu.
Mumin aliwahadharisha watu wake mara ya kwanza na ya pili. Na hii sasa ni mara ya tatu anawahimiza wakubali nasaha zake, kwa sababu anataka kuwaokoa na wapate kheri. Lakini wengineo wanawaongoza kwenye shari na maangamizi.
Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.
Starehe za dunia zitakwisha tu, hilo halina shaka, lakini maisha ya Akhera yatabakia daima. Basi ni maisha gani kati ya haya mawili yanayofaa kuyafanyia kazi? Katika Nahjul-balagha, imesemwa: “Anafanya nini na dunia aliyeumbiwa Akhera? Na anafanya nini na mali ambaye muda mchache atanyang’anywa na kubakia athari yake mbaya na hisabu yake?” Vile vile imesemwa: “Uchungu wa dunia ni tamu ya Akhera na tamu ya Akhera ni uchungu ya dunia/”
Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo, na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.
Mwenyezi Mungu ni mwadilifu mkarimu. Uadilifu wake unajitokeza kati- ka adhabu ya muovu. Hiyo mbele ya Mwenyezi Mungu inalingana sawa na malipo. Na hupunguza adhabu kwa huruma zake. Ama mwema huzidishiwa ziada nyingi bila ya hisabu, awe mwanamume au mwanamke. Pepo ni malipo tosha kabisa.
Aya inafahamisha wazi kuwa Pepo ni wakf hususi wa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kwa imani isiyokuwa na shaka. Ama yule mwenye kufanya kheri kwa ajili ya kheri tu na huku anamkufuru Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, malipo yake yatakuwa sio Peponi, kwa sababu Pepo si ya makafiri. Tazama Juz. Juz. 4 (3:176 – 178), kifungu: ‘Kafiri na amali njema.’
Kuna mapokezi yanayosema kuwa Mtume(s.a.w.
w
)
amesema: “Hakufanya wema mwislamu au kafiri ila Mwenyezi Mungu humlipa.” Akaulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni yapi malipo ya kafiri? Akasema: mali, watoto, afya nk. Akaulizwa: malipo yake akhera yatakuwa nini? Akasema: Ataadhibiwa adhabu ya chini”
وَيَا قَوْمِ مَا لِي أَدْعُوكُمْ إِلَى النَّجَاةِ وَتَدْعُونَنِي إِلَى النَّارِ ﴿٤١﴾
41. Na Enyi watu wangu! Kwa nini mimi ninawaita kwenye wokovu, nanyi mnaniita kwenye Moto?
تَدْعُونَنِي لِأَكْفُرَ بِاللَّـهِ وَأُشْرِكَ بِهِ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ وَأَنَا أَدْعُوكُمْ إِلَى الْعَزِيزِ الْغَفَّارِ ﴿٤٢﴾
42. Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami ninawaita kwa Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira?
لَا جَرَمَ أَنَّمَا تَدْعُونَنِي إِلَيْهِ لَيْسَ لَهُ دَعْوَةٌ فِي الدُّنْيَا وَلَا فِي الْآخِرَةِ وَأَنَّ مَرَدَّنَا إِلَى اللَّـهِ وَأَنَّ الْمُسْرِفِينَ هُمْ أَصْحَابُ النَّارِ ﴿٤٣﴾
43. Bila ya shaka mnayeniitia, hastahiki wito duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanaopita kiasi basi hao ndio watu wa Motoni!
فَسَتَذْكُرُونَ مَا أَقُولُ لَكُمْ وَأُفَوِّضُ أَمْرِي إِلَى اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ ﴿٤٤﴾
44. Basi mtayakumbuka ninayowaambia. Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja.
فَوَقَاهُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِ مَا مَكَرُوا وَحَاقَ بِآلِ فِرْعَوْنَ سُوءُ الْعَذَابِ ﴿٤٥﴾
45. Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni.
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ ﴿٤٦﴾
46. Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapofika Saa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!.
NINAWAITA KWENYE WOKOVU NYINYI MNANIITA KWENYE MOTO
Aya 41 – 46
MAANA
Na Enyi watu wangu! Kwa nini mimi ninawaita kwenye wokovu, nanyi mnaniita kwenye Moto? Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami ninawaita kwa Mwenye nguvu Mwingi wa maghufira?
Maneno haya na yanayofuatia mpaka Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja, anayasimulia Mwenyezi Mungu kuhusu mumin anayetoa nasaha.
Maana ni, niambieni enyi washirikina kuhusu hali yangu na nyinyi. Mimi nawalingania kwenye kheri itakayowaokoa na adhabu na maangamizi; ambayo ni kumwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu asiyekuwa na mfano na yoyote; na mwenye kumsamehe anayetubia na kurejea Kwake; na nyinyi mananiita kwenye adhabu ya kuungua na kwenye shirki asiyoisamehe Mwenyezi Mungu wala kuingia akilini. Haifuati isipokuwa mwenye kupotea njia.
Bila ya shaka mnayeniitia, hastahiki wito duniani wala Akhera.
Bila shaka yule mnayenitaka nimwabudu, kama Firauni na mwenginewe, hana faida yoyote duniani na Akhera:
إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ﴿١٤﴾
“Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu. Na wakisikia hawajibu. Na Siku ya Kiyama watakataa shirki yenu.” Juz. 22 (35:14).
Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu.
Kila kiumbe kitarudi kwa Mwenyezi Mungu kesho, sio kwa Firauni wala kwa mwenginewe. Watasimama wote mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabuna malipo na wanaopita kiasi basi hao ndio watu wa Motoni!
Amenukuu Tabari na Razi kutoka kwa Mujahid, kwamba makusudio ya wanaopita kiasi hapa ni waliomwaga damu bila ya haki.
Basi mtayakumbuka ninayowaambia yale ya ukweli na nasaha pale mtakapoona adhabu na kuwashukia balaa Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja.
Muhyiddin Bin Arabi anasema katika Futuhatil-makkiyya kuwa neno ufawwidhu (tulilolifasiri kwa maana ya kutegemeza), limechukuliwa kutoka neno fadha lenye maana ya kumimina chombo kikiwa kimejaa na hakiwezi kuchukua ziada.
Kwa hiyo mumin akibebeshwa zaidi ya uwezo wake, huipeleka ile ziada kwa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu (s.w.t) hupokea ziada hiyo na kumpunguzia mzigo mumin. Na yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi na mwenye kumuona mwenye kuamini na akamtegemea na yule anayeelekea kwingine.
Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni.
Firauni alimdhamiria ubaya Musa na mumin mwenye kutoa nasaha, Mwenyezi Mungu akawaokoa na vitimbi vyake, akaangamia Firauni na watu wake kwenye maji. Namna hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaondolea ubaya wenye ikhlasi, na majanga yanawarudia viongozi wa uhaini. Hii ni kabla ya mauti.
Ama baada ya mauti, basi wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni.
Kuna riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’far Assadiq
akisema:Hiyo itakuwa baada ya mauti na kabla ya Kiyama. Kwa sababu siku hiyo haitakuwa na asubuhi wala jioni. Lau angeliadhibiwa mwenye hatia asubihi na jioni tu, basi ingelikuwa afadhali kwake.
Na itapofika Saa ya Kiyama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!
Kila mkosefu ataambiwa Siku ya Kiyama: Ingia Jahannam na ni marejeo mabaya; ni sawa awe ni katika watu wa Firauni au wengineo. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusu kutaja Firauni kwa sababu mazungumzo yanamuhusu yeye hivi sasa.