8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
اللَّـهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ قَرَارًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٤﴾
64. Ni Mwenyezi Mungu aliyewafanyia ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa jengo. Na akawatia sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akawaruzuku vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Basi amekuwa na baraka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.
هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٥﴾
65. Yeye yuko hai - hapana mungu isipokuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَمَّا جَاءَنِيَ الْبَيِّنَاتُ مِن رَّبِّي وَأُمِرْتُ أَنْ أُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٦﴾
66. Sema: Hakika nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ziliponijia hoja zilizo wazi kutokana na Mola wangu. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ يُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ ثُمَّ لِتَكُونُوا شُيُوخًا وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ مِن قَبْلُ وَلِتَبْلُغُوا أَجَلًا مُّسَمًّى وَلَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾
67. Yeye ndiye ambaye amewaumba kwa udongo, kisha kwa tone, kisha kwa pande la damu, kisha akawatoa katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanaokufa kabla, na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kutia akili.
هُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ فَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٦٨﴾
Yeye ndiye ambaye anahuisha na anafisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa.
AMEWATIA SURA NA AKAZIFANYA NZURI
Aya 64 – 68
MAANA
Ni Mwenyezi Mungu aliyewafanyia ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa jengo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t), hapa, ameisifu ardhi kuwa ni mahali pa kukaa, mahali pengine ameipa sifa ya tandiko na pengine kitanda. Maana yote hayo ni mamoja. Na ameisifu mbingu hapa kuwa ni jengo na mahali pengine kuwa ni sakafu na yenye buruji na yenye mpangilio.
Makusudio ya sakafu ni kufananisha, kwa sababu inaonekana kama hivyo kwenye macho. Kundi la wafasiri limesema kuwa makusudio ya buruji ni nyota na mpangilio. ni njia. Ama makusudio ya jengo ni kuwa aliiumba kwa mpangilio mzuri na akaipamba kwa pambo la nyota; kama ilivyo katika Juz. 23 (37:6).
Na akawatia sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akawaruzuku vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Basi amekuwa na baraka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mtu, akalifanya vizuri umbile lake, kimo na viungo, kwa mpangilio wa hali ya juu; kuongezea ubainifu, utambuzi, na mengineyo, kama vile utambuzi n.k. Hali hii ya uwiano wa ajabu baina ya mtu na ulimwengu; kiasi ambacho muundo wake umekuja kwa namna ambayo mtu anaweza kutumia nishati na heri zote zilizo ulimwenguni kulingana na haja na masilahi yake, huenda ndiyo inayomfanya mtu awe kiumbe wa aina yake.
Lau kusingelikuwa na dalili yoyote inayofahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, isipokuwa kiumbe huyu wa ajabu (mtu), basi ingelitosha. Hapa ndio tunapokuta tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na katika ardhi zimo Ishara na katika nafsi zenu, je hamuoni?” (51:20-21). Tumeyazungumzia hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:70).
Yeye yuko hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
Yeye yuko hai kwa sababu Ndiye anayetoa uhai na ni Mmoja wa peke Yake kwa sababu ni Mungu. Kwani uungu unapelekea kuwa wa pekee mmoja tu. Maana ya kumsafia dini ni kumwamini na kumwelekea Yeye tu peke Yake, katika kauli zote na vitendo vyote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:29) na Aya ya 14 ya sura hii tuliyo nayo.
Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema kuwa Yeye ndiye aliyewatia sura, anaashiria kuwa inatakikana mtu amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema yake ya kuumba na kuruzuku.
Sema: Hakika nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ziliponijia hoja zilizo wazi kutokana kwa Mola wangu. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
Huu ni mfumo mzuri wa kujadili na kudadisi. Washirikina walipomwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: abudu masanamu tunayoyaabudu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake waambie kuwa vipi niabudu masanamu na hali Mwenyezi Mungu amenikataza kuyaabudu na akaniamuru kusalimu amri Kwake Yeye peke yake.
Pia amenifahamisha dalili za kutosha kwamba mnavyoviabudu hav- istahiki kuabudiwa kabisa, kwa sababu ni mawe tu, yasiyodhuru wala kunufaisha. Umetangulia mfano wake katika Aya 41 ya sura hii tuliyo nayo.
Yeye ndiye ambaye amewaumba kwa udongo, kisha kwa tone, kisha kwa pande la damu, kisha akawatoa katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanaokufa kabla, na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kutia akili
Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (16:70), Juz. 17 (22:70), Juz. 18 (23:14) na Juz. 22 (35:11).
MWANAFALSAFA RUSSEL NA MUDA ULIOWEKWA
Yeye ndiye ambaye anahuisha na anafisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye anayeleta mauti na uhai katika vitu vya asili ya maumbile na Ndiye aliyeleta maumbile yote, zikiwemo sayari zake, kwa neno ‘kuwa’ kutokana na kutokuweko chochote. Sio kutokana na ukungu; wala mengineyo. Kama muulizaji atauliza: Ni nani basi aliyemuumba Mwenyezi Mungu? Tutajibu: maana ya neno Allah (Mwenyezi Mungu) ni kuwa Yeye ni muumba asiyeumbwa na kwamba dhati yake inapelekea kupatikana wala haihitaji mwenye kuipatisha.
Akisema mara ya pili kuwa hayo ni madai tu yanyohitaji uthibitisho, na kwamba huo ukungu huuhitaji mwenye kuupatisha, tutamjibu hivi: Maisha haya na nidhamu hii haiwezi kufasiriwa na ukungu wala na kitu chochote kisichokuwa na uhai wala utambuzi. Kwa sababu asiyenacho haiwezi kuitoa.
Kwa hiyo basi haitabakia kwa mwenye akili kufasiri uhai na nidhamu katika maumbile isipokuwa kukubali kuweko Mwenye uwezo, Mpangiliaji aliyemuumba wa kila kitu na asiyehitajia chochote. Makadirio yoyote yasiyokuwa haya hayakubaliki kiakili.
Na mwenye kupinga basi na alete lililo bora kuliko hili na amwachie mtu kufuata atakalo nasi tutakuwa pamoja naye.
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemumba mtu katika umbile zuri, akamgurisha kutoka hali moja hadi nyingine mpaka kufikia muda wake uliowekwa. Ikiwa hatujamuona muumba basi tumeona athari na dalili zinazofahamisha kuwa Yeye ni Mkuu katika uumbaji Wake.
Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kufahamu.’ Tunakumbuka tukio lililomtokea mwanafalsafa mkubwa Bretrand Russel, alipokuwa na umri wa miaka 76.
Mnamo mwaka 1948, alisafiri kwa ndege kutoka Oslow hadi London. Ndege ilipokuwa inakurubia ufukwe wa Norway, mhudumu mmoja wa ndege alimuuliza kama ni lazima avute sigara? Alikuwa amekaa kwenye viti vya mbele, akamjibu: “Nisipovuta nitakufa.”
Basi akamuonyesha viti vya nyuma aende akakae huko, ataruhusiwa kuvuta sigara. Mara tu baada ya kukaa, ndege ikaanguka baharini, watu waliokuwa viti vya mbele wakafariki na waliokuwa vya nyuma wakapona.
Hatuwezi kupata tafsiri ya hili ispokuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kufahamu.’ Mwenyezi Mungu ametanabisha kufika muda uliowekwa na kufahamu, ili awaeleze walahidi wanaofasiri tukio kama hili na mfano wake kuwa ni sadfa.
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّـهِ أَنَّىٰ يُصْرَفُونَ ﴿٦٩﴾
69. Je, Huwaoni wale ambao wanabishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu wanageuziwa wapi?
الَّذِينَ كَذَّبُوا بِالْكِتَابِ وَبِمَا أَرْسَلْنَا بِهِ رُسُلَنَا فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٧٠﴾
70. Ambao wamekadhibisha Kitabu na yale tuliyowatuma nayo Mitume wetu. Basi watakuja jua.
إِذِ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ وَالسَّلَاسِلُ يُسْحَبُونَ ﴿٧١﴾
71. Zitakapokuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa.
فِي الْحَمِيمِ ثُمَّ فِي النَّارِ يُسْجَرُونَ ﴿٧٢﴾
72. Katika maji ya moto, kisha wataunguzwa Motoni.
ثُمَّ قِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ تُشْرِكُونَ ﴿٧٣﴾
73. Tena wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwashirikisha.
مِن دُونِ اللَّـهِ قَالُوا ضَلُّوا عَنَّا بَل لَّمْ نَكُن نَّدْعُو مِن قَبْلُ شَيْئًا كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ الْكَافِرِينَ ﴿٧٤﴾
74. Badala ya Mwenyezi Mungu Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu huwapoteza makafiri.
ذَٰلِكُم بِمَا كُنتُمْ تَفْرَحُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنتُمْ تَمْرَحُونَ ﴿٧٥﴾
75. Haya ni kwa sababu mlikuwa mkifurahi katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ ﴿٧٦﴾
76. Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo. Basi ni maovu yaliyoje makazi ya wanaotakabari!
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ فَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ ﴿٧٧﴾
77. Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyowaahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ فَإِذَا جَاءَ أَمْرُ اللَّـهِ قُضِيَ بِالْحَقِّ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْمُبْطِلُونَ ﴿٧٨﴾
78. Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa haki, na hapo wapotofu watapata hasara.
MLIKUWA MKIFURAHI
Aya 69 – 78
MAANA
Je, Huwaoni wale ambao wanabishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu wanageuziwa wapi?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake mtukufu akipinga ubishi wa kibatili wa washirikina, kuwa umeona ewe Muhammad jinsi washirikina na wapenda anasa wanavyozifumbia macho hoja mkataa na ubainifu ulio wazi juu ya ukuu wa Mwenyezi Mungu na utume wako? Na pia vile wanavyoikimbia haki na kwenda kwenye ujinga na upotevu wa kuabudu mawe?
Ufafanuzi zaidi wa Aya hii na ufupisho wake ni kauli ya Imam Ali
:“Mwenye kukithirisha mzozo wake kwa ujinga hudumu upofu wake na haki.”
Ambao wamekadhibisha Kitabu
yaani Qur’anina yale tuliyowatuma nayo Mitume wetu. Basi watakuja jua.
Siku hiyo uhakika utadhihirika na wakosefu wataiona adhabu yao,zitakapokuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa katika maji ya moto, kisha wataunguzwa Motoni.
Wataburuzwa kupelekwa motoni wakiwa wamefungwa minyororo, kinywaji chao kitakuwa maji ya moto na mikono itafungwa shingoni na utosi utakutanishwa na nyayo:
يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ ﴿٤١﴾
“Watajulikana wakosefu kwa alama zao, watakamatwa kwa nywele za utosi na kwa miguu” (55-41).
Tena wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwashirikisha badala ya Mwenyezi Mungu
na mkiwaweka akiba ya wakati wa shida? Basi waiteni wawaitikie ikiwa nyinyi ni wakweli.
Watasema: Wametupotea,
wala hatuwaoni hata athari yao.bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu!
Kumbe walikuwa ni mangati tu.
Hivyo ndivyo Mwenyezi huwapoteza makafiri,
kwa sababu wameamua kufuata njia mbaya kwa hiyari yao, baada ya kukatazwa na wakafa kwenye uovu na kufuru na hali wameamriwa kutubia na kurejea kwa Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu. Mwenye kuingia mlango wa uovu, ajilaumu mwenyewe tu.
TUNATAFUTA DUNIA KWA DINI
Haya ni kwa sababu mlikuwa mkifurahi katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
Wakifurahi kwa mambo duni ya dunia yanayoisha wala hawatilii umuhimu neema za daima za akhera zinazowapita. Lakini wasifa huu hauwahusu washirikina tu; bali unatuhusu sisi pia. Tofauti ni kuwa wao wanaikabili dunia wakiwa wanikana Akhera waziwazi na kwa ndani, lakini sisi tunaikabili dunia na kuipupia kwa kutumia imani ya Mwenyezi Mungu na Siku ya mwisho. Sasa ni lipi kati haya mawili linastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu?
Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo. Basi ni maovu yaliyoje makazi ya wanaotakabari!
Ataambiwa haya mwenye kutakabari na kila mwenye kuitumia dini na nchi kujinufaisha na akachezea akili za watu wasio na hatia; ni sawa ameyafanya hayo kwa makusudi au kutojua hakika na hali halisi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾ الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾
“Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo? Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri? Juz. 16 (18:103 – 104).
Ulama wameafikana kwa kauli moja kwamba mjinga (asiyejua) kwa uzembe hana udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu.
Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli.
Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 55 katika sura hii tuliyo nayo.
Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyowaahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.
Maneno yanelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
kuhusiana na washirikina. Maana ni kuwa tunaweza tukawaadhibu duniani wale wanaokukadhibisha na kukuudhi wewe ukiwaona na tunaweza tukakuhitari ukaja kwetu kabla ya hayo. Katika hali zote hizo, marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Aya inashiria kwamba mumin wa kweli anatakikana afurahi kwa yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu, awe na yakini na dini yake na afanye juhudi kadiri atakavyoweza kupiga vita ubatilifu na upotevu, kisha malipo amwachie Mwenyezi Mungu:
وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٣٢﴾
“Na Mola wako si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda” Juz. 8 (6:132)
Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia na wengine hatukukusimulia.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 6 (4:164). Tazama kifungu ‘Je, mitume wote ni wa mashariki?
Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya ishara hapa ni muujiza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hudhihirisha muujiza mikononi mwa mitume, kulingana na inavyotaka hekima na masilahi; sio kama wanavyotaka wenye kiburi na inadi.
Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa haki, na hapo wapotofu watapata hasara.
Hapo ni hapo Siku ya Kiyama; nayo ni siku mbaya sana kwa wabatilifu na siku njema sana kwa wenye haki.
اللَّـهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَنْعَامَ لِتَرْكَبُوا مِنْهَا وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٧٩﴾
79. Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewajaalia wanyamahowa ili muwapande baadhi yao na wengine muwale.
وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَلِتَبْلُغُوا عَلَيْهَا حَاجَةً فِي صُدُورِكُمْ وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ ﴿٨٠﴾
80. Na katika hao mna manufaa Na manapata kwao haja zilizo vifuani mwenu; Na mnachukuliwa juu yao na juu ya majahazi.
وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَأَيَّ آيَاتِ اللَّـهِ تُنكِرُونَ ﴿٨١﴾
81. Na anawaonyesha ishara zake, basi ni ipi katika ishara za Mwenyezi Mungu mtaikataa?
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَانُوا أَكْثَرَ مِنْهُمْ وَأَشَدَّ قُوَّةً وَآثَارًا فِي الْأَرْضِ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨٢﴾
82. Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٨٣﴾
83. Basi walipowajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walifurahia elimu waliyokuwa nayo na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia sti- hzai.
فَلَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا قَالُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ وَكَفَرْنَا بِمَا كُنَّا بِهِ مُشْرِكِينَ ﴿٨٤﴾
84. Walipoiona adhabu yetu wakasema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu peke yake na tumekataa tuliyokuwa tukimshirikisha naye.
فَلَمْ يَكُ يَنفَعُهُمْ إِيمَانُهُمْ لَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا سُنَّتَ اللَّـهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ فِي عِبَادِهِ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْكَافِرُونَ ﴿٨٥﴾
85. Lakini imani yao haikuwa ni yenye kuwafaa walipoiona adhabu yetu. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyopita kwa waja wake. Na hapo waliokufuru watapata hasara.
MWENYEZI MUNGU AMEWAJAALIA WANYAMAHOWA
Aya 79 – 85
MAANA
Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewajaalia wanyamahowa ili muwapande baadhi yao na wengine muwale.
Wanyamahowa ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatumikisha kwa ajili ya manufaa ya binadamu; kama vile kula na kupanda.
Amewahusu kuwataja, pamoja na kuwa neema zake hazina idadi, kwa kuungana kwake na maisha ya waarabu wakati huo, na mpaka sasa bado wana mahitaji mengi sana katika baadhi ya miji.
Na katika hao mna manufaa mengine; kama vile kunufaika na manyoya yake na ngozi zake. Na manapata kwao haja zilizo vifuani mwenu;
kama vile kubeba mizigo mizito na bidhaa mbalimbali kutoka mji mmoja hadi mwingine.Na mnachukuliwa juu yao na juu ya majahazi.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:142) na Juz. 14 (16:66).
Na anawaonyesha ishara zake, basi ni ipi katika ishara za Mwenyezi Mungu mtaikataa?
Yaani mtaikataa pamoja na hoja na dalili? Ndio walikata kwa vitendo ishara za Mwenyezi Mungu na hukumu zake. Kwa sababu mema kwao ni maovu na maovu kwao ni mema.
Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi.
Historia ya watu wa ardhi imejaa mazingatio na mawaidha kwa mwenye kuzingatia na kupata somo. Ni uma ngapi zilifikia ukomo wa starehe na maendeleo, lakini walipopetuka mipaka, Mwenyezi Mungu aliwakamata kwa dhulma zao kwa mshiko wa Mwenye nguvu na uweza.Basi hayakufaa waliyokuwa wakiyachuma;
kama vile utawala, mali na makasri na ngome walizozijenga. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (12:109), Juz. 17 (22:46) na Juz 21 (30:9).
Basi walipowajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi wakifurahia elimu waliyokuwa nayo.
Makusudio ya furaha hapa ni kughurika. Na makusudio ya elimu ni sababu za utajiri, yaani elimu ya kuzalisha chakula na mavazi. Hilo linaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi.’ Qarun naye alipoambiwa: “Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya Akhera” Alijibu: “Nimepewa haya kwa sababu ya elimu” Juz 20 (28:77-78)
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume, kwa hoja mkataa, wakati uliopita kwenye umma zilizokuwa na utajiri; kama vile viwanda n.k. Wakaghurika kwa sababu hizi au kwa elimu na wakawafanyia maskhara manabii wa Mwenyezi Mungu na vitabu; sawa na mashirika ya leo yanayohodhi kila kitu ambayo yanaikataa haki na ubinadamu na kudharau thamani yake na amani ya mataifa
Na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.
Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa kupituka kwao mipaka na yakawasibu yale waliyokuwa wakiyadharau. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kupituka mipaka na kuasi, hata kama muda utarefuka kiasi gani.
Walipoiona adhabu yetu wakasema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu peke yake na tumekataa tuliyokuwa tukimshirikisha naye.
Walipokuwa katika amani ya Mwenyezi Mungu walimkufuru, lakini walipoiona adhabu yetu wakasema tumeamini,lakini imani yao haikuwa ni yenye kuwafaa walipoiona adhabu yetu.
Kwa sababu hii sio imani yoyote ispokuwa ni kukimbia adhabu, lakini watakimbia wapi?
Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyopita kwa waja wake,
ambayo ni kuwa Mwenyezi Mungu anasikiliza toba na kuzikubali katika nyumba ya taklifa na matendo sio katika nyumba ya hisabu na malipo.
Na hapo waliokufuru watapata hasara.
Kila mkosefu ni mwenye hasara na mtupu.
MWISHO WA SURA YA ARUBAINI: SURAT AL-GHAAFIR