10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ ﴿١٣﴾
13. Basi wakipuuza, sema: Nawahadharisha ukelele mfano ukelele wa A’di na Thamudi.
إِذْ جَاءَتْهُمُ الرُّسُلُ مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ قَالُوا لَوْ شَاءَ رَبُّنَا لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً فَإِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿١٤﴾
14. Walipowafikia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angelitaka Mola wetu bila ya shaka angeliwateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyotumwa.
فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ ﴿١٥﴾
15. Ama kinaA’di walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ ﴿١٦﴾
16. Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za nuhusi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ فَأَخَذَتْهُمْ صَاعِقَةُ الْعَذَابِ الْهُونِ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿١٧﴾
17. Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua ukelele wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma
وَنَجَّيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿١٨﴾
18. Na tukawaokoa wale ambao wameamini na wakawa na takua.
NAWAHADHARISHA UKELELE
Aya 13 – 18
MAANA
Basi wakipuuza, sema: Nawahadharisha ukelele mfano ukelele wa A’di na Thamudi. Walipowafikia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu!
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
kuhusiana na washirikina wa kiarabu. Mbele yao na nyuma yao ni kinaya cha msisitizo wa mitume na jitihadi zao katika kubashiria na kuonya, na kwamba wao walifuata kila njia kwa ajili ya kuwaongoza wao, lakini shetani akawapambia na akawaingizia dhana yake, pale aliposema:
ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ ﴿١٧﴾
“Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.” Juz. 8 (7:17).
Maana ni kuwa, sema ewe Muhammad kumwambia yule anayekukanusha wewe na risala yako kuwa A’d na Thamud waliwakadhibisha waliowalingania kama haya ninayoyalingania – Tawhid, na wakatoa juhudi zao kwa ajili ya uongofu wao.
Lakini walipong’ang’nia kwenye upotevu, Mwenyezi Mungu aliwakamata kwa adhabu ya dunia na Akhera na kwam- ba mimi nawaonya yasije yakawasibu yale yaliyowasibu wao.
Wakasema: Angelitaka Mola wetu bila ya shaka angeliwateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyotumwa.
A’d na Thamud waliwajibu mitume kwa kuwakadhibisha kwa sababu Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, hatumi ispokuwa Malaika. Kauli yao hii tumeipinga katika kufasiri Juz. 7 (6:9).
Ama kina A’di walitakabari katika ardhi bila ya haki.
Kauli yake Mwenyezi Mungu: bila ya haki ni katika upande wa kufafanua na kusiitiza tu. Kwa sababu hakuna kiburi cha haki; hasa ikiwa ni kumfanyia kiburi Mwenyezi Mungu.
A’di walifanya kiburi wakawadharau wanyonge na wakasema hakuna yoyote anayetuweza.
Na wakasema: Nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao?
Hili ni wazi, halihitaji dalili. Imam Aliy
anasema:“Kila mtukufu asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni dhalili, na kila mwenye nguvu asiyekua yeye Mungu ni dhaifu, na kila mfalme asiyekua Yeye ni mmilikiwa, na kila mjuzi asiyekua yeye ni mwanafunzi na kila muweza asiyekua Yeye ni dhaifu.
Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
Walizikana dalili za ulimwengu zinazofahamisha umoja wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake. Wakasema kila kilichomo ulimwenguni pamoja na mpangilio wake na nidhamu ni kazi ya maumbile.
Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za nuhusi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwadhibu duniani kwa upepo uliokuja na baridi katika siku za mkosi na hizaya, kisha watakamilisha adhabu kali zaidi na ya kufedhehesha huko Akhera kuliko adhabu ya duniani.
Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua ukelele wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
Aya hii ni dalili wazi kwamba mtu ana hiyari wala halazimishwi, kwa sababu inasema Mwenyezi Mungu aliwaongoza Thamud kwenye njia ya uokovu, akawaamrisha kuifuata na akawakataza maasi, akawabainishia njia ya maangamizi akawakataza na kuwahadharisha na mwisho mbaya kama wataifuata, lakini wakaathirika nayo kuliko ya uokovu; ikawa malipo yao ni balaa na hasara.
Na tukawaokoa wale ambao wameamini na wakawa na takua.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaokoa kwa sababu walifuata njia ya uokovu. Yametangulia mazungumzo kuhusu A’di katika Juz.12 (11:50) na kuhusu Thamud katika Juzuu hiyo hiyo na sura hiyo Aya 50.
وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّـهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿١٩﴾
19. Na siku watakapokusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao watazuiliwa.
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٠﴾
20. Hata watakapoufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢١﴾
21. Na wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliyewaumba mara ya kwanza, na kwake Yeye mtarejeshwa.
وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٢٢﴾
22. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisiwashuhudie. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyokuwa mkiyatenda.
وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾
23. Na hiyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Mola wenu, imewaangamiza; na mmekuwa miongoni mwa waliopata hasara.
وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾
23. Basi wakisubiri Moto ndio makazi yao. Na wakitoa udhuru hawakubaliwi.
MASIKIO YAO NA MACHO YAO YATAWASHUHUDIA
Aya 19 – 24
MAANA
Na siku watakapokusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao watazuiliwa.
Aya hizi tulizo nazo zinaungana na Aya iliyopita inayosema: ‘Basi wakipuuza, sema: nawahadharisha ukelele mfano ukulele wa A’di na Thamudi.’ Yaani pia waambie ewe Muhammad kuwa Malaika wa adhabu watawapeleka wakosefu kwenye Jahannam kwa nidhamu.
Atakayechelewa watamkemea na atakayejaribu kukimbia watamzuia. Makusudio ni kuwa hawana pakukimbia.
Hata watakapoufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Hakuna kitu Siku ya Mwisho ispokuwa hisabu na malipo. Baadhi ya Aya za Qur’ani, ikiwemo hii tuliyo nayo,zinafahamisha kwamba Mwenyezi Mungu hatamwaadhibu mkosefu siku hiyo mpaka amkinaishe kuwa ana dhambi na anastahili adhabu.
Hii ni miongoni mwa tofauti zilizoko baina ya hakimu wa duniani anayetoa hukumu yake kwa hali yoyote iwayo; awe mwenye kuhukumiwa amekinai kuwa kweli amekosea au la, na hukumu ya Mwenyezi Mungu huko Akhera; ambapo Mwenyezi Mungu kesho hatatoa hukumu mpaka mhukumiwa akinai kuwa anastahili adhabu.
Kwa ajili hii ndio kutakuwa na ushahidi mwingi dhidi ya mkosefu. Wachukuzi wa dini watashuhudia kuwa walimfikishia halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, Malaika watatoa ushahidi kua aliasi na akafanya jeuri na kitabu cha matendo yake kitasajili kila kauli na kitendo. Ikiwa hatatosheka, ngozi yake itashuhudia kuwa iligusa haramu, kama zina na utangulizi wake, masikio yatatoa ushahidi kuwa yalisikia haki na yakaikataa na macho nayo yatatoa ushahidi kuwa yaliona dalili za umoja wa Mungu yakazikataa na mengineyo.
Aya inaashiria maana ya ndani yakuwa sharti la shahidi ni kutopendelea. Pengine mkosefu anaweza akatuhumu kwamba wafikisha dini na Malaika wanaweza kuwa upande wa Mwenyezi Mungu kwa vile wanafanya mambo kwa amri yake. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaleta ushahidi wa mtu mwenyewe binafsi ili kuondoa tuhuma hii hata kama si ya kweli.
Kuna Hadith isemayo kuwa mja kesho atamwambia Mola wake: Je, hukunikataza dhulma? Atajibiwa: ndio! Basi atasema: Mimi sitakubaliana na ushahidi ispokuwa ushahidi wa nafsi yangu. Basi hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu ataviamuru viungo vitoe ushahidi. Mja mwenye dhambi atasema: Potoleeni mbali! Mara ngapi nimewapinga!
Na wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia?
Kauli yao hii inaonyesha kuwa baadhi wa wakosefu hawatakubali ushahidi wa wafikishaji dini na wa Malaika na kwamba wao watafikiria kuwa kukataa kwao huku kutawafaa, lau si Mwenyezi Mungu kuwawekea ushahidi wao wenyewe.
Zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliyewaumba mara ya kwanza, na kwake Yeye mtarejeshwa.
Viungo vyao duniani vinatamka kwa lugha ya kihali na kushuhudi hekima na mpangilio uliomo duniani kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwanzilishi na mrejeshaji. Na akhera vitatamka hivyo hivyo kwa uwazi kabisa. Wametofautiana wafasiri katika namna ya ushahidi wa viungo kesho.
Kuna wanaosema kuwa kutajitokeza alama za kuonyesha makosa yaliyofanyika. Wengine wakasema kuwa Mwenyezi Mungu atavitamkisha hasa kiuhakika. Hii ndio kauli iliyo wazi, kwa sababu dhahiri ya Aya inaonyesha hivyo, na akili hailikatai hilo.
Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisiwashuhudie. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyokuwa mkiyatenda.
Makusudio ya kudhani hapa ni kuitakidi. Yaani mliamini enyi wakosefu kuwa mnafanya makosa kujificha mkihofia watu na sio kumhofia Mwenyezi Mungu, kwamba hajui mnayoyafanya kwa kujificha, na kwamba viungo vyenu havitawafichua siku ya hisabu.
Na hiyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Mola wenu, ime- waangamiza; na mmekuwa miongoni mwa waliopata hasara.
Itikadi ya ubatilifu ndiyo iliyowapeleka kwenye Jahannam na ni mrejeo mabaya. Hii vile vile inalingana na wale wanaoiamini Akhera kinadharia na kuikana kimatendo; pale wanapojificha na watu na hawajifichi na Mwenyezi Mungu.
Bali hawa ni wabaya zaidi kuliko wale wanaopinga ufufuo na uweza wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu wakiwa na uhakika kuwa yuko nao akisikia na kuona; na kwamba hakifichiki kwake chochote katika mbingu na ardhi.
Basi wakisubiri Moto ndio makazi yao. Na wakitoa udhuru hawakubaliwi.
Wakivumilia moto wakosefu basi ndio sawa na ndio makazi yao wala hawataokoka. Na wakiomba radhi kwa Mwenyezi Mungu hawaridhii.” Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!” Juz. 15 (18:29).
وَقَيَّضْنَا لَهُمْ قُرَنَاءَ فَزَيَّنُوا لَهُم مَّا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ ﴿٢٥﴾
25. Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. na ikawathibitikia kauli wawe pamoja na uma zilizopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kuhasirika.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ ﴿٢٦﴾
26. Na wale ambao wamekufuru walisema: Msiisikilize Qur’ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
فَلَنُذِيقَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا عَذَابًا شَدِيدًا وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٧﴾
27. Basi wale ambao wamekufuru hapana shaka tutawaonjesha adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo ya mabaya zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
ذَٰلِكَ جَزَاءُ أَعْدَاءِ اللَّـهِ النَّارُ لَهُمْ فِيهَا دَارُ الْخُلْدِ جَزَاءً بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ ﴿٢٨﴾
28. Hayo ndiyo malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na nyumba ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ ﴿٢٩﴾
29. Na wale ambao wamekufuru watasema: Mola wetu! Tuonyeshe waliotupoteza miongoni mwa majini na tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
WALIOKUFURU WALISEMA MSISIKILIZE QUR’ANI
Aya 25 – 29
MAANA
Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao.
Makusudio ya yaliyo mbele yao ni dunia na balaa yake, na ya nyuma yao ni Akhera ambayo kwa wapinzani ni uzushi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaandalia mataghuti marafiki wabaya wanaowavutia na maovu na kuwaweka mbali na mema.
Unaweza kuuliza
: ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewapangia watakaowahadaa kwenye upotevu na maasi, basi si itakuwa ni dhulma kuwaadhibu na kusema: ‘Basi ikiwathibitikia kauli;’ yaani adhabu.
Jibu
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewafanyia hivyo baada ya wao wenyewe, kwa uchaguzi wao mbaya, kufuata njia ya upotevu. Hilo amelifafanua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliposema:
وَمَن يَعْشُ عَن ذِكْرِ الرَّحْمَـٰنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ ﴿٣٦﴾
”Anayeyafanyia upofu maneno ya Mwingi wa rehema tunamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.” (43:36)
Pia akasema:
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ ﴿٥﴾
“Walipopotoka Mwenyezi Mungu alizipotosha nyoyo zao” (61:5).
Hayo yamekwishaelezwa huko nyuma mara kadhaa.
Na ikawathibitikia kauli wawe pamoja na uma zilizopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kuhasirika.
Waliasi na wakafanya uovu, wakastahili adhabu, sawa na walivyostahili mfano wao katika umma zilizopita. Aya hii inafahamisha kuwa majini wana umma na vizazi, wana mitume na manabii; na miongoni mwao kuna wema na wengine waovu, sawa na watu.
Na wale ambao wamekufuru walisema: Msiisikilize Qur’ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
Mataghuti walishangaa walipoona athari ya Qur’ani na inavyoatwala kwenye nafsi za watu; wakawa wamedangana hawajui wafanye nini baada ya kushindwa kukabili hoja kwa hoja. Kisha wakaafikiana waipige vita kwa mambo yasiyosawa – waipe sifa ya uchawi na vigano na waifanyie vurugu. Wakaona kuwa hiyo ndiyo njia iliyobaki ya kuishinda.
Hii ya kufanya vurugu inafahamisha kukubali kwao kushindwa, na kwamba Qur’ani ni ngome ya Mwenyezi Mungu iliyoshinda fikra zote za bianadamu, wakati wote.
Basi wale ambao wamekufuru hapana shaka tutawaonjesha adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo ya mabaya zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
Makosa yanagawanyika sehemu mbili: Kuna yale mabaya na yale yaliyo mabaya zaidi. Vile vile malipo kwa sababu:
مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا ﴿٤٠﴾
“Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo,” (40:40).
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja mabaya zaidi waliyoyafanya ili kubainisha kuwa malipo nayo yatakuwa mabaya zaidi, sawa na matendo yao.
Hayo ndiyo malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na nyumba ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
Hayo ni ishara ya hayo malipo ya mtendo mabaya zaidi ambayo ni kudumu katika moto wa Jahannam. Kudumu huku, Mwenyezi Mungu amekufanya ni malipo ya kila mpinzani mwenye inadi na mshirikina, mambo ambayo hayana udhuru wowote kabisa.
Ujinga unaweza kuwa ni udhuru, lakini sio katika shirki na kupinga. Kwa sababu dalili za umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake hazikujificha, ziko waziwazi. Kuzijua kunahitaji kuangalia kusikokuwa kwa kuiga au kufuata mapenzi ya moyo.
Na wale ambao wamekufuru
katika wadhaifuwatasema: Mola wetu! Tuonyeshe waliotupoteza miongoni mwa majini na watu
katika wale waliofuatwa,tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
Walimuomba Mwenyezi Mungu awaletee wale waliowapoteza katika mashetani watu na majini ili wawakanyage na wawe sehemu ya ndani kabisa ya Jahannam, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekwishawafanyia mabaya na mabaya zaidi.pale alipomkamata kila mmoja kwa dhambi yake.