12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliyeviumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na ikiwa watafanya kiburi, basi hao walioko kwa Mola wako wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٣٩﴾
39. Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi imetulia, lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inashtuka na kututumka. Bila ya shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.
إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤٠﴾
40. Hakika wale ambao wanaupotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je, Atakayetupwa Motoni ni bora au atakayekuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayoyatenda.
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ ﴿٤١﴾
41. Hakika wale ambao wanakataa dhikiri inapowajia. Na hayo bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu.
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ ﴿٤٢﴾
42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ ﴿٤٣﴾
43. Haambiwi ila yale yale waliyoambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako bila ya shaka ni Mwenye maghufira, na ni Mwenye adhabu chungu.
وَلَوْ جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا أَعْجَمِيًّا لَّقَالُوا لَوْلَا فُصِّلَتْ آيَاتُهُ أَأَعْجَمِيٌّ وَعَرَبِيٌّ قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٤٤﴾
44. Na lau tungeliifanya Qur’ani kwa lugha ya kigeni wangelisema: Kwa nini Aya zake hazikupambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na mwarabu? Sema: Hii Qur’ani ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini. Na wasioamini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako mahali mbali.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ ﴿٤٥﴾
45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea hitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwishatangulia neno la Mola wangelihukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka nayo yenye kuwatia wasiwasi.
مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٤٦﴾
46. Anayetenda mema basi anajitendea mwenyewe, na anayetenda uovu basi ni juu ya yake; na Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja.
HAUTAKIFIKIA UPOTOVU MBELE YAKE WALA NYUMA YAKE
Aya 37 – 46
SAFARI YA MWEZINI
Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja, katika Kitabu chake Kitukufu, Aya kadhaa za kilimwengu na zinavyomfahamisha Muumba na sifa Zake. Miongoni mwa Aya hizo ni zile za kutofautiana usiku na mchana, kuumbwa jua na mwezi n.k. Tazama Juz. 3 (3:27) Juz. 23 (36:37 – 40) na (39:5). Humo mumetajwa usiku, mchana, jua na mwezi.
Kutokana na kutajwa mwezi tutaashiria tukio muhimu lilitokea ulimwenguni la safari ya anga za mbali ya waamerika wawili Neil Amstrong na Edwin kwenda mwezini, katika majira ya kiangazi ya mwaka 1969. Watu walilizungumzia sana tukio hili na wengi wakaniuliza kuhusu maoni ya dini kuhusiana na safari hii. Nikajibu kwa makala iliyosambazwa magazetini, kisha nikaiunganisha na Tafsir Al-kashif kulingana na Aya zinazotaja mwezi. Basi kabla ya kuchapishwa tafsiri, mfanyakazi mmoja wa kiwanda cha uchapishaji akanishauri niiondoe makala hiyo, nami nikakubali bila ya kujua sababu.
Baada ya kupita muda mchache tangu kuchapishwa Tafsir Al-kashif , ikanibainikia kuwa ilikuwa vizuri sikuweka makala hiyo kwenye Tafsiri. Hiyo ilitokana na kuwa nilisoma kwenye gazeti la Al-akhabar la Misr la 6-2-1970, makala, iliyofasiriwa kutoka kwenye gazeti la Pravda la Urusi, ya wanasayansi wawili wa kirusi, Mikhail Vassin na Alexander Cherbakov.
Wataalamu hawa wawili walichunguza matokeo waliyoyatangaza wamarekani katika uchunguzi wao wa mchanga wa mwezini na madini yaliyopatikana kwenye ardhi ya mwezi, wakasema: “Somo hili linakataa nadharia zote zilizoenea kuhusiana na asili ya mwezi, wala halikubali isipokuwa tafsiri moja tu; kwamba mwezi umetengenezwa kwa usanii wa hali ya juu wenye mpangilio. Na iliyoutengeneza ni nguvu ya ajabu yenye uwezo usioweza kufikiwa na chochote.”
Hii inamaanisha kwamba wanavyoamini wamaada kuhusu ulimwengu ni njozi tu. Makala hii inaendelea kusema: “Uchunguzi wa kielimu wa kisasa unakataa nadharia zote na makisio yote kuhusu chanzo cha mwezi na kuan- za fikra mpya ya kutatua kitandawili hiki inayosema: Usanii wa mwezi umetokana na kitu kilichoendelea sana kielimu na kifani, kisha kikaunda harakati ya mwezi kwa vifaa vilivyoendela sana. Ndani ya mwezi kuna mamabo ya ajabu yasiyowezakana kupatikana kwa sadfa.”
Gamba la nje la mwezi liko na tabaka mbili za kimsingi: ya kwanza ni tabaka ya kutenganisha joto lenye unene wa 4 km. La pili lina unene wa 300 km. Juu yake kuna aina mbalimbali ya vifaa vilivyoundwa kuzuia mtingishiko. Kwa hiyo mwezi unaweza kuhimili safari bila ya kuondoka sehemu yake kwa mamilioni ya mamilioni ya miaka.”
Lakini kuna swali linataka majibu: Ikiwa mwezi umetengenezwa na kitu chenye akili iliyoendela, basi kitu hiki kimetoka wapi? Kwa nini kikafanya bidii ya kutengenza sayari hii? Ni kwa ajili ya kuzunguka kwenye sayari tu basi?
Nadharia ya kisasa haiwezi kujibu swali hili. Lakini inaamini kuwa makisio ya karibu zaidi kuliko jambo lolote ni kuwa mwezi umetengenezwa na kwamba mtenegenzaji wake amekuwa na mpangilio wa kiajabu.”
Wakomonisti wawili wanasema: “Akili inakataa makadirio na tafsiri yoyote isipokuwa moja tu, kwamba mwezi umetengenezwa na ilioutengeneza ni nguvu ya ajabu.”
Ndio! Ni kweli umetengenezwa, na mtengenezaji wake hana mshirika wala wa kufanana naye. Uhandisi wake ndio uliotuongoza kujua hilo.
Ama kauli ya wataalamu wawili kuwa umetengenezwa na kitu kilichoendelea sana na mfumo wake ni wa ajabu sana, kauli hii ni kukiri waziwazi kwamba kwenye mwezi kuna mpangilio ambao hauwezi kutokea kwa yeyote isipokuwa kwa aliye Muweza, Mwenye hekima ambaye hana mfano na chochote naye ni Muumba aliye Mjuzi.
Tuna uhakika kwamba hivi karibuni tutasoma kukiri wazi zaidi ya hivi, kutakakovunja kauli za wamaada na nadharia za walahidi. Na itathibitika kwa hisia na majaribio kwamba nyuma ya ulimwengu huu kuna nguvu inayoshinda nguvu zote inayokiamabia kitu kuwa na kikawa.
Hili haliwezi kuepukwa na maendeleo ya elimu na akili huru. Hapa ndio inakuwa siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ ﴿١٨٥﴾
“Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu?”
Juz. 9 (7:185).
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾
“Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanotia akilini (mambo).” Juz. 13 (13:4)
هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾
“Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye?” Juz. 21 (31:11)
Msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye- viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
Aliyeviumba, ni aliyeumba usiku, mchana, jua na mwezi au aliyeumba sayari na nyota zote. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya jua na mwezi, kwa sababu ndivyo vilivyojitokeza zaidi kwa watu.
Mafakihi wameafikiana kwa kauli moja kwamba ni wajibu kusujudu kwa mwenye kuisoma au kuisikia Aya hii. Wengine wakasema, bali hata aliyesikia bila ya kukusudia pia atasujudu.
Aya inawaambia wasabai, walioabudu nyota, kutokana na manufaa yake, kuwa Mwenyezi Mungu ndiye ambaye ameumba sayari na akazifanya ziwe na manufaa kwa waja, nazo ni viumbe tu kama sisi, zinamwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kumsujuduia na kukubali utumishi.
Na ikiwa watafanya kiburi, basi hao walioko kwa Mola wako wanam- takasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
Yaani ikiwa hao waabudu nyota watang’ang’ania ushirikina, basi Mwenyezi Mungu hana haja nao wala ibada yao, kwa sababu anao waja – Malaika – hawaachi kumsabihi Mwenyezi Mungu usiku na mchana.
Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi imetulia, lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inashtuka na kututumka. Bila ya shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.
Maana haya yamekaririka kwenye Aya kadhaa na kwa mifumo mbali mbali; miongoni mwazo ni: Juz. 17 (22:5)
Hakika wale ambao wanaupotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii sisi.
Washirikina waliitia ila Qur’ani wakasema ni uchawi na wakasema ni ngano, lakini Mwenyezi Mungu anajua kauli zao na atawauliza nazo na kuwaadhibu.
Je, Atakayetupwa Motoni ni bora au atakayekuja kwa amani Siku ya Kiyama?
Swali hili linabeba jawabu lake. Ni nani mwenye akili anayeweza kusema moto ni bora kuliko pepo au hofu ni nzuri kuliko amani? Lakini wakosefu wameghafilika na msingi huu, na wao hasa wameathirika na moto kuliko pepo na hofu kuliko amani.
Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayoyatenda.
Hii ni hadhri na onyo kwamba wao watakutana na adhabu baada ya kuifu- ata kwa njia ya kufuru na upotevu.
Hakika wale ambao wanakataa dhikiri inapowajia.
Makusudio ya dhikiri hapa ni Qur’ani. Hapa kuna maneno ya kukadiriwa, kuwa wataadhibiwa.
ISRAIL NA QUR’AN
Na hayo bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameisifu Qur’ani kuwa ina nguvu na kwamba haifikiwi na upotofu wowote. Maana ya kuwa na nguvu ni nguvu za hoja zake na dalili zake zilizo wazi. Ama kuwa haifikiwi na upotovu, wafasiri wametaja njia tano; iliyokaribu zaidi ni ile isemayo kuwa kila itikadi, sharia habari na mengineyo yaliyomo ndani yake ni haki isiyokuwa na shaka.
Yametangulia maelezo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz.14 (15:9). Huko tumeeleza kuwa Israili ilichapisha maelfu ya nakala za Qur’ani na kuziko-roga baadhi ya Aya zake; mfano ile isemayo: “Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake.” Juz. 3 (3:85), wakaandika: “Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislamu itakubaliwa kwake.” Hili lilitokea mwaka 1968. Chuo kiku cha Al-azhar kilikusanya nakala hizi na kuzizuia zisisambae.
Israil ikarudia tena mnamo mwaka 1969 na ikakoroga Aya nyingine: “Walisema Mayahudi: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa waliyoyasema.” Juz. 6 (5:64), wakabadilisha neno ‘wamelaaniwa’ likawa ‘wameamini.’ Nakala hizi za Qur’ani ya kiisrail zikaenea kwenye maduka ya Lebanon na kwenye miji mingi ya Uarabuni. Pia ilisambazwa huko Malesia, Pakistan, India, Indonasia, Guinea, Ivory coast (Cote de vory) Iran n.k.
Leo hii tarehe 25-2-1970. Gazeti la An-nahar la Beirut limeandika kuwa wakili Faruq Sa’d amepeleka mshtaka kwa niaba ya Ofisi na wachapishaji wa Mash-had Alhusayniy ya Cairo ya kumtia hatiani mwenye kuivuruga Qur’ani Takufu, kuiiga, kuipotoa na kuirekebesha. Pia limeandika kwamba nakala za kupotoshwa zimechapisha Ujerumani Magharibi na wachapishaji wa Cologne – Doits.
Israil haikutosheka hapa na vita vyake dhidi ya Uislamu na waislamu, wakaitangaza Qur’ani ya kukorogwa kwenye idhaa yake. Idhaa ya Cairo ilitumia mwezi mzima kurikodi Qur’ani kutoka idhaa ya Israil.
Vile vile Israil imetengeneza radio ya mkono wanayoiuza kwa bei rahisi kabisa, ambayo haishiki idhaa yoyote isipokuwa idhaa yake inayopotosha Qur’ani tu. Israili inafanya yote haya na mengineyo kwa kuitikia msingi wa kizayui alioutangaza mmoja wa viongozi wake, aliposema: “Ni lazima tuifanye Qur’ani ni silaha ya kuwamaliza waislamu.”
Tumeyaeleza yote haya kama mfano wa vita vya Israil dhidi ya Uislam, ili pengine waweze kuzinduka baadhi ya wafalme na maraisi; bali hata baadhi ya masheikh wanaojiita waislamu, lakini wanafanyakazi kwa siri kwa manufaa ya Israil na wasaidizi wake.
Nilishangazwa na kauli ya sheikh mmoja mpotofu akisema: “Israil ina afadhali kuliko wengine kwa sababu inasoma Qur’ani kwenye idhaa yake.” Ndio ewe sheikh! Wacha kutangaza, bali inachapisha na kusambaza pia, lakini ile iliyopotoshwa na kukorogwa ili kumaliza Uislamu; sawa na baadhi ya wenye vilemba vya usheikh vya upotovu.
Huambiwi ila yale yale waliyoambiwa Mitume wa kabla yako.
Washirikina wa uma zilizotangulia waliwaambia mitume na manabii wao: “Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayotuitia…Hayakuwa haya isipokuwa ni vigano vya wakale…Hakuwa huyu isipokuwa ni mchawi mzushi.” Na hivi ndivyo walivyokuambia mataghuti wa watu wako ewe Muhammad! Kwa sababu Mola aliyekutuma wewe na aliyewatuma waliokuwa kabla yako ni mmoja na risala yake ni moja, na masilahi ya mataghuti ambayo yanasigana na wafuasi wa haki ni hayo hayo wakati wowote na mahali popote.
Hakika Mola wako bila ya shaka ni Mwenye maghufira, na ni Mwenye adhabu chungu.
Aya imekusanya vinyume viwili: msamaha wa mwenye dhambi ikiwa atatubia, na adhabu ikiwa ataendelea. Namna hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anafanya katika Aya kadhaa, anakutanisha ahadi na kiaga, kupendekeza na kuhadharisha, ili aogope mja adhabu ya Mungu apate kumcha, na wala asikate tamaa na rehema yake atubie na arejee.
Na lau tungeliifanya Qur’ani kwa lugha ya kigeni wangelisema: Kwa nini Aya zake hazikupambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na mwarabu?
Qur’ani iliwateremkia waarabu kwa lugha yao wanayoipenda na kuitukuza, lakini baadhi ya mataghuti wao waliwaambia wengine: Lau ingeliteremka kwa lugha nyingine wangelitaaradhi na kusema itakuwaje Mtume mwarabu na lugha ya kigeni? Hivi ndivyo wanavyouandalia kila mlango ufunguo na kila usiku na taa. Hakuna lengo isipokuwa kuikimbia haki tu.
Sema: Hii Qur’ani ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini.
Qur’ani ni mwongozo kwa mwenye kutaka uongofu na ni haki kwa njia ya haki na ni ponyo kwa mwenye kutaka kupona maradhi ya ukafiri na unafiki. Imam Ali
anasema:“Hakika katika Qur’ani kuna ponyo la ugonjwa mkubwa zaidi ambao ni unafiki na dhulma.”
Na wasioamini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni.
Qur’ani ni uongofu na mwangaza kwa wenye ikhlasi, lakini ni upofu machoni mwa wanafiki, ni uziwi masikiano mwao na maradhi nyoyoni mwao.
Hao wanaitwa nao wako mahali mbali.
Qur’ani iliwaita duniani kwa mwito wa Mwenyezi Mungu, lakini hawakuitikia kama kwamba hakuna mwito au kwamba uko mbali hausikiki. Vile vile itawaita Siku ya Kiyama: “Ehe! Kila mpanda mbegu ana wasi-wasi na matokeo ya kazi yake; isipokuwa aliyepanda Qur’ani,” kama ilivyo katika Nahajul-balagha. Wafasiri wanasema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘nao wako mahali mbali,’ ni ishara kwamba wao hawasikii wala hawafahamu, sawa anayeitwa kwa sauti ya mbali asiyoisikia wala kuifahamu.
Lakini maana haya yanapingana na lengo la kuita, kwa sababu kutakuwa hakusikiwi. Maana yaliyo na nguvu zaidi ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Nao wako mahali mbali,’ ni ishara yakuwa mwito unatoka mbinguni, lakini unasikiwa na wote. Hilo linafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ ﴿٤١﴾ يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ﴿٤٢﴾
“Siku atakaponadi mwenye kunadi kutoka mahali karibu, siku watakaposikia ukele wa haki.” (50:41-42).
Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea hitilafu kati yake.
Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat. Walihitalifiana kwenye hiyo iliposhuka. Kuna walioisadiki na walioikadhibisha. Kadhalika Qur’ani, iliposhuka, kuna walioisadiki na walioikadhibisha.
Na lau kuwa halikwishatangulia neno la Mola wangelihukumiwa.
Imetaka hekima yake Mtukufu kuiahirisha adhabu ya wakosefu hadi siku ya ufufuo. Vinginevyo asingebakia taghuti wala mwenye dhambi yoyote.
Na hakika wao wamo katika shaka nayo yenye kuwatia wasiwasi.
‘Wao’ ni washirikina wa kiarabu, ‘nayo’ ni hiyo Qur’ani. Makusudio ya shaka hapa ni ubishi bila ya ilimu na haki. Maana ni kuwa wao wanabishana kuhusu Qur’ani, lakini kwa ujinga na upotofu. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 12 (11:110).
Anayetenda mema basi anajitendea mwenyewe, na anayetenda uovu basi ni juu ya yake; na Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja.
Maana ya Aya hii yamekaririka kwenye Aya kadhaa; zikiwemo hizi zifuatazo:
فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٤﴾
“Basi leo nafsi yeyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyokuwa mkiyatenda Juz. 23 (36:54)
Na ile iliyo katika Juz. Hii tuliyo nayo:
الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ﴿١٧﴾
“Leo kila nafsi italipwa kwa iliyochuma. Hapana dhulma leo.” (40:17)
Na nyinginezo zinasema kuwa mtu anakuwa na hiyari halazimishwi.