15
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ ﴿٢٧﴾
27. Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia, lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.
وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٨﴾
28. Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Walii Mwenye kuhimidiwa.
وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ ﴿٢٩﴾
29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.
وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ ﴿٣٠﴾
30. Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi.
وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٣١﴾
31. Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.
وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ ﴿٣٢﴾
32. Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.
إِن يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ ﴿٣٣﴾
33. Akitaka, huutuliza upepo navyo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَن كَثِيرٍ ﴿٣٤﴾
34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda. Naye husamehe mengi.
وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ ﴿٣٥﴾
35. Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.
RIZIKI NI KWA KUFANYA KAZI SIO KWA DUA
Aya 27 – 35
MAANA
Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameitegemeza riziki kwa waja wake kwa kuchuma kwao na kufanya kazi si kwa matakwa yao na matamanio; vinginevyo ingelienea vurugu na kufanya ufisadi katika ardhi.
Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho.
Yaani anamrukuzu kwa kadiri ya utendaji wake wa kazi. Mara nyingine Mwenyezi Mungu hutoa riziki nyingi kwa kazi chache au riziki chache kwa kazi nyingi kulingana na hekima anayoijua Yeye zaidi. Ama utajiri unaotokana na haramu; kama vile kughushi na kupora, hiyo ni riziki ya shetani sio ya kutokana na kutoa kwa Mwingi wa rehema; vipi isiwe hivyo na hali mwenye riziki hiyo amepewa kiaga cha adhabu chungu?
Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.
Anamjua anayeishi kwa hisabu ya kupora na anayeishi kwa jasho lake. Wa kwanza amemwahidi hizaya na adhabu na wa pili ni heshima na thawabu.
Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja riziki, anasema kuwa sababu za hizo riziki, kama vile mvua, ziko mikononi mwake. Huipeleka anapotaka na huizuia anapotaka. Basi ikichelewa kidogo, wao hukata tamaa, lakini anawawahi kwa rehema yake iliyoenea katika kila kitu.
Naye ndiye Walii
anayewasimamia waja wake kwa wemaMwenye kuhimidiwa
anyestahiki sifa njema na kushukuriwa.Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo.
Makusudio ya mbingu ni kilicho juu, iwe sayari au anga; na makusudio ya wanyama hapa ni kila mwenye uhai wakiwemo malaika ndege au yoyote mwenye uhai anayeishi nchi kavu au baharini na kwenye anga au kwenye nyota. Wote hao wanaonyesha kuweko mtengenezaji wake na mtia sura wake.Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo;
sawa na alivyoweza kuwaumba na kuwaeneza mbinguni na ardhini.
Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu.
Aya hii inafahamisha waziwazi, wala haikubali taawili yoyote, kuwa dhulma na ufukara unatokana na watu sio Mwenyezi Mungu na wala hautokani na hukumu ya Mwenyezi Mungu na sharia yake; hata kahati na kuzuilika mvua, sababu yake ni dhulma na ufisadi; kama ilivyoelezwa katika Hadith na katika kitabu cha Mwenyezi Mungu: “Lau wangelisimamisha Tawrat na Injil na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, kwa hakika wangelikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. ‘Juz. 6 (5:66), kifungu cha ‘Riziki na ufisadi’
Naye anasamehe mengi katika madhambi isipokuwa shirki na dhulma, kwa sababu Yeye ndiye aliyesema:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ﴿٤٨﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo.” Juz. 5 (4:48).
Na akasema:
يَوْمَ لَا يَنفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٥٢﴾
“Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makazi mabaya kabisa.” Juz. 24 (40:52).
Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 20 (29:22)
Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.
Ikiwa jahazi limetengenezwa na mtu lakini maji linayoyapitia na upepo unaolisukuma ni katika matengenezo yake Mwenyezi Mungu na hata miti iliyotengenezewa nk. Pia ndege zinazopaa kwenye anga ya Mwenyezi Mungu, magari yanayotembea kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu na vingenevyo hata mtu mwenyewe pia. Vyote hivyo vinadhihirisha uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na rehema zake.
Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari.
Akizuia upepo au akiyagandisha maji basi majahazi yatasimama tu.
Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
Mwenye kuwa na subira ya tafakuri na kuutazama ulimwengu na maajabu ya siri zake, hana budi kuishia kwenye imani ya Mwenyezi Mungu na utukufu wake, na atamshukuru kwa fadhila zake na mwongozo wake.
Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda
hao watu.Naye husamehe mengi;
yaani hawaharakishi pamoja na dhambi zao nyingi.
Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.
Wanaojadiliana katika ishara za Mwenyezi Mungu ni wale wanaosema kuwa hakuna kitu kinachofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu yuko. Maana ni kuwa makafiri hawamuamini Mwenyezi Mungu na kupinga kila dalili inayotamka kuweko kwake.
Hata hivyo iko njia moja ya kuamini na kukiri kwao ambayo ni kuona maangamizi kwa macho yao na kujua kuwa hakuna pa kukimbilia; mfano jahazi likisimama baharini au upepo mkali. Kwa maneno mengine hawaamini mpaka waone adhabu.
فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٣٦﴾
36. Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi. Kwa ajili ya walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao.
وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu na wanapokasirika wao husamehe.
وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na wanaomwitikia Mola wao na wakasimamisha Swala. Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao na wanatoa katika yale tuliyowapa.
وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ ﴿٣٩﴾
39. Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.
وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴿٤٠﴾
40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.
وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ ﴿٤١﴾
41. Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.
إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٤٢﴾
42. Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿٤٣﴾
Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
KILICHOKO KWA MWENYEZI NI BORA NA KITABAKIA
Aya 36 – 43
MAANA
Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu,
Starehe za dunia ni kila kinachostarehesha katika maisha haya; kama vile afya cheo, mali, wanawake, watoto, majengo, samani na mengineyo. Anasa za dunia hata zikiwa nyingi, zinaondoka na kuisha. Ama neema za Akhera zinabaki kwa kubakia kwake:
مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ﴿٩٦﴾
“Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobakia.”
Juz. 14 (16:96).
Anaendelea kusema Mwenyezi Mungu:lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi.
Kila amali itakayotekeleza haja yoyote katika maisha basi hiyo ni akiba mbele ya Mwenyezi Mungu kwa Masharti yafuatayo:-
1.Kwa ajili ya walioamini Mwenyezi Mungu.
Ama wale waliomkufuru hawana chochote mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa adhabu, kwa vile wao hawakiri isipokuwa kuweko kwake. Kuna Hadithi inayosema: “Mwenye kumfanyia amali asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamwachia aliyemfanyia amali, na kesho ataambiwa: chukua malipo yako kwa uliyemfanyia.”
2.Na wakawa wanamtegemea Mola wao
katika mambo yao yote, wala hawajienzi isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu na radhi yake.
3.Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu,
ikiwemo dhulma, uongo na ufisadi. Tazama Juz. 5 (4:31) na Juz. 8 (6:151)
4.Na wanapokasirika wao husamehe;
yaani si wepesi wa kukasirika na wasiokasirika isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu.
5.Na wanaomwitikia Mola wao,
hawamuasi katika amri yake wala makatazo yake.
6.Na wakasimamis
ha Swala.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameihusisha kuitaja hapa kwa vile ndio nguzo ya dini, na Mtume(s.a.w.
w
)
alikuwa akiita ‘kitulizo cha jicho.’ Baadhi ya wataalamu wameiita ‘Uhakika wa Mwislamu’
7.Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao.
Kauli ‘mambo yao’ inaashiria mambo mema ya uma na kwamba wao wanasaidiana kuufanyia kazi uma. Kushauriana huku si katika halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, kwa sababu zinatokana na Mwenyezi Mungu tu peke yake. Tazama Juz. 4 (3:159). Katika Nahjul-balagha amesema: “Kutaka ushauri ni jicho la mwongozo na amejiingiza kwenye hatari anayetosheka na rai yake.”
8.Na wanatoa katika yale tuliyowapa, katika mali.
9.Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.
Unaweza kuuliza
: Tutaichanganya vipi Aya hii na ile isemayo: ‘Na wanapokasirika wao husamehe?’
Jibu
: Kusamehe uovu ni vizuri ikiwa kutasababisha muovu kujirekebisha na kutubia au ikiwa ni kukinga ugomvi na fitina, lakini si kuzuri ikiwa kutasababisha ujeuri na usafihi kwa muasi. Imam Ali
anasema:“Kuwatekelezea ahadi wavunja ahadi ni kuvunja ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu na kuvunja ahadi kwa wavunja ahadi ni kutekeleza ahadi.”
Tumeelezea hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 24 (41:34).
Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ ﴿١٩٤﴾
“Anayewachokoza nanyi mchokozeni kwa kadiri alivyowachokoza.” Juz.2 (2:194).
Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu.
Mfano wake ni
وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿٢٣٧﴾
“Na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua” Juz. 2 (2:237).
Vile vile:
فَمَن تَصَدَّقَ بِهِ فَهُوَ كَفَّارَةٌ لَّهُ ﴿٤٥﴾
“Lakini atakayesamehe itakuwa kafara kwake.” Juz. 6 (5:45).
Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.
Makusudio ya madhalimu hapa ni wale wanaopita mpaka wa kisasi.
Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu
kabisa wala hakuna kuadhibiwa, kwa sababu mwenye kuanza ndiye dhalimu, na mwenye kudhulimiwa anayo haki ya kujitetea; bali akimnyamazia aliyemdhulumu basi atakuwa ni mshirika katika dhulma, kwa sababu kumnyamazia dhalimu kunamtia mori. Na lau dhalimu atajua kuwa mdhulumiwa ataitetea heshima yake basi atajizuia.
Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
Huko nyuma tumewahi kueleza kuwa dhalimu anahukumiwa kuwa ni kafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, ajapotamka shahada mbili. Ndio! Hapa duniani atachukuliwa kama Mwislamu, lakini Akhera atakuwa pamoja na madhalimu. Hilo ni kwa ushahidi wa Aya kadhaa, zinazomwita kafiri kuwa ni dhalimu na dhalimu kuwa ni kafiri. Tazama Juz. 3 (2:254) na Juz. 9 (25:55-62).
Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa;
yaani ni mambo mazuri ya kuazimiwa kufanywa. Aina bora ya subira ni kuvumilia udhia katika kuithibitisha haki na kuitangaza. Na aina bora zaidi ya kusamehe ni kule kutakakosababisha kuondoa fitina na ufisadi.