17
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI
Sura Ya Arubaini Na Tatu: Surat Az-Zukhruf. Ina aya 89 Imeshuka Makka. Imesemekana isipokuwa Aya moja haikushuka Makka
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
حم ﴿١﴾
1. Haa-miim.
وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾
2. Naapa kwa Kitabu kinachobainisha.
إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٣﴾
3. Hakika tumeifanya Qur’an kwa kiarabu ili mfahamu.
وَإِنَّهُ فِي أُمِّ الْكِتَابِ لَدَيْنَا لَعَلِيٌّ حَكِيمٌ ﴿٤﴾
4. Na hakika hiyo imo katika mama wa Kitabu kilichoko kwetu, ni tukufu na yenye hiki- ma.
أَفَنَضْرِبُ عَنكُمُ الذِّكْرَ صَفْحًا أَن كُنتُمْ قَوْمًا مُّسْرِفِينَ ﴿٥﴾
5. Je, tuache kuwakumbusha kwa kuwa ni watu mliopita mipaka?
وَكَمْ أَرْسَلْنَا مِن نَّبِيٍّ فِي الْأَوَّلِينَ ﴿٦﴾
6. Na manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
وَمَا يَأْتِيهِم مِّن نَّبِيٍّ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٧﴾
7. Na hakuwajia nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
فَأَهْلَكْنَا أَشَدَّ مِنْهُم بَطْشًا وَمَضَىٰ مَثَلُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨﴾
8. Na tuliwaangamiza waliokuwa na nguvu kushinda wao, na mfano wa watu wa zamani umekwishapita.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ ﴿٩﴾
9. Na ukiwauliza: Nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi.
الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَجَعَلَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا لَّعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٠﴾
10. Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko, na akawafanyia ndani yake njia mpate kuongoka.
وَالَّذِي نَزَّلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَنشَرْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا كَذَٰلِكَ تُخْرَجُونَ ﴿١١﴾
11. Na ambaye ameteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyokufa. Na hivyo ndivyo mtakavyotolewa.
وَالَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا وَجَعَلَ لَكُم مِّنَ الْفُلْكِ وَالْأَنْعَامِ مَا تَرْكَبُونَ ﴿١٢﴾
12. Na ambaye ameumba aina zote, na akawafanyia jahazi na wanyamahowa mnaowapanda.
لِتَسْتَوُوا عَلَىٰ ظُهُورِهِ ثُمَّ تَذْكُرُوا نِعْمَةَ رَبِّكُمْ إِذَا اسْتَوَيْتُمْ عَلَيْهِ وَتَقُولُوا سُبْحَانَ الَّذِي سَخَّرَ لَنَا هَـٰذَا وَمَا كُنَّا لَهُ مُقْرِنِينَ ﴿١٣﴾
13. Ili mkae vizuri migongoni mwao. Kisha mkumbuke neema za Mola wenu mnapokaa sawa sawa juu yao hao mnaowapanda na mseme: Ametakasika aliyemfanya huyu atutumikie, na tusingeliweza kufanya haya wenyewe.
وَإِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا لَمُنقَلِبُونَ ﴿١٤﴾
14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
KITABU KINACHOBAINISHA
Aya 1 – 14
MAANA
Haa-miim.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Naapa kwa Kitabu kinachobainisha.
Hiki ni kiapo kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Qur’an ambayo ndani yake mna ubainifu wa uongofu na upotevu, na halali na haramu.
Hakika tumeifanya Qur’an kwa kiarabu ili mfahamu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (12:2), Juz. 16 (20:113), Juz. 24 (41:3) na kwenye Juzuu hii tuliyo nayo (42:7). Tumekwishaizungumzia sana Aya hii, na hivi sasa hatuna la ziada.
Na hakika hiyo imo katika mama wa Kitabu kilichoko kwetu, ni tuku- fu na yenye hikima.
‘Hiyo’ ni hiyo Qur’an na mama ni asili. Hakuna mwenye shaka kwamba ilimu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndio asili ya vitabu vyote mbinguni. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameisifu Qur’an kuwa ni tukufu kwa sababu inainua na kuwatukuza wanayoisikiliza na kuitumia. Tumeona jinsi ilivyowatoa waarabu kwenye ujinga wa wajinga kuwapeleka kwenye maendeleo na jinsi ilivyoeneza utawala wao na lugha mashariki ya ardhi na magharibi yake, pale walipohalalisha halali ya Qur’an na wakaharamisha haramu ya yake.
Vile vile Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameisifu kuwa ina hikima kwa sababu imeweka sawa baina ya watu bila ya kubagua, ikatoa mwito wa kusameheana na ikahimiza kufanya kazi yenye manufaa na kusaidiana kwa masilahi ya watu wote.
Je, tuache kuwakumbusha kwa kuwa ni watu mliopita mipaka?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuitaja Qur’an kwamba ni mtoa nasaha mwaminifu, sasa anawaambia wale walioikadhibisha katika washirikina wa kiarabu: Mnaonaje tuache kuwakumbusha Qur’an kwa vile tu nyinyi mmezipitishia kiasi nafsi zenu na mkazidhulumu kwa ujinga na upotevu? Bali nyinyi ndio mnafaa zaidi kukumbushwa kuliko wengineo.
Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
Ni wengi tu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsimulia Mtume wake habari za manabii kadhaa na akamwambia:
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ ﴿٧٨﴾
“Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia na wengine hatukukusimulia.” Juz. 24 (40:78).
Na hakuwajia nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli,
kama walivyokukejeli wewe ewe Muhammad. Kwa hiyo lisikutie tabu hilo, si mageni hayo. Ni vita baina ya wapotevu na wanaolingania haki na uadilifu, kila mahali na kila wakati.
Na tuliwaangamiza waliokuwa na nguvu kushinda wao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza mataghuti waliokuwa na nguvu katika umma zilizopita kwa kuwanusuru wema walio wanyonge.
Na mfano wa watu wa zamani umekwishapita.
Yaani tumekusimulia katika Qur’an hali ya waongo wa zamani na jinsi walivyoangamia, ili watu wako wapate funzo.
Na ukiwauliza: Nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (29:61), (31:25) na Juz. 24 (39:38)
Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko, na akawafanyia ndani yake njia mpate kuongoka. Na ambaye ameteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyokufa. Na hivyo ndivyo mtakavyotolewa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:99), Juz. 13 (13:3) na Juz. 16 (20:53).
Na ambaye ameumba aina zote.
Yaani aina zote za waanyama, mimea na vitu vigumu.
Na akawafanyia jahazi na wanyamahowa mnaowapanda.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwatajia neema ya maji na ardhi na kwamba wao wanakula, kuvaa na kunywa humo, sasa anawatajia neema ya mawasiliano. Ametaja jahazi na wanyama kwa njia ya mfano tu sio kuwa ndio hayo tu; kwa sababu magari na ndege hayakuwa maarufu wakati huo.
Ili mkae vizuri migongoni mwao.
Yaani migongoni mwa hao mnaowapanda.
Kisha mkumbuke neema za Mola wenu mnapokaa sawa sawa juu yao hao mnaowapanda na mseme: Ametakasika aliyemfanya huyu atutumikie, na tusingeliweza kufanya haya wenyewe. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
Katika Nahjul-balagha amesema: “Ewe Mola wangu! Ninajilinda kwako na mashaka ya safari, na huzuni ya marejeo na ubaya wa mandhari katika watu wa nyumbani na mali.
Ewe Mola wangu! Hakika wewe ni mwenza safarini na wewe ndiwe wa kuachwa nyuma na familia. Wala hawezi kuyakusanya haya mawili isipokuwa wewe. Kwa sababu mwenye kuachwa nyuma hawezi kuwa mwenza na mwenza hawezi kuachwa nyuma.”
Sheikh Muhammad Abduh anaielezea kauli hiyo ya Imam Ali
, kwa kusema:“Mwanzo wa maneno haya umepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na akayatimiza Amirul-muminin kwa kusema Wala hawezi kuyakusanya…mpaka mwisho. Dhati ya Mwenyezi Mungu iko sawa mahali pote na wakati wote. Kwa hiyo kuwa safarini na kuwa mjini kwake ni sawa.”
وَجَعَلُوا لَهُ مِنْ عِبَادِهِ جُزْءًا إِنَّ الْإِنسَانَ لَكَفُورٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾
15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanadamu ni mwenye kukufuru waziwazi.
أَمِ اتَّخَذَ مِمَّا يَخْلُقُ بَنَاتٍ وَأَصْفَاكُم بِالْبَنِينَ ﴿١٦﴾
16. Au amejichukulia watoto wa kike katika vile alivyoviumba, na akawachagulia nyinyi watoto wa kiume?
وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِمَا ضَرَبَ لِلرَّحْمَـٰنِ مَثَلًا ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ ﴿١٧﴾
17. Na mmoja wao akibashiriwa kwa yale aliyompigia mfano Mwingi wa rehema, uso wake husawijika naye amejaa chuki.
أَوَمَن يُنَشَّأُ فِي الْحِلْيَةِ وَهُوَ فِي الْخِصَامِ غَيْرُ مُبِينٍ ﴿١٨﴾
18. Ati aliyelelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema bayana?
وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ ﴿١٩﴾
19. Na wakawafanya malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wataulizwa!
وَقَالُوا لَوْ شَاءَ الرَّحْمَـٰنُ مَا عَبَدْنَاهُم مَّا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ إِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿٢٠﴾
20. Na husema: Angelipenda Mwingi wa Rehema tusingeliwaabudu. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا مِّن قَبْلِهِ فَهُم بِهِ مُسْتَمْسِكُونَ ﴿٢١﴾
21. Au tuliwapa Kitabu kabla ya hiki, wakawa wameshikamana nacho?
بَلْ قَالُوا إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّهْتَدُونَ ﴿٢٢﴾
22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi na tunaongoza nyayo zao.
وَكَذَٰلِكَ مَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّقْتَدُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na kadhalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila wapenda anasa wake walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi na tunafuata nyayo zao.
قَالَ أَوَلَوْ جِئْتُكُم بِأَهْدَىٰ مِمَّا وَجَدتُّمْ عَلَيْهِ آبَاءَكُمْ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٢٤﴾
24. Akasema: Hata nikiwaletea yenye muongozo bora kuliko mliowakuta nayo baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.
فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿٢٥﴾
25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa waliokadhibisha!
AU AMEJICHUKULIA WATOTO WANAWAKE
Aya 15 – 25
MAANA
Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanadamu ni mwenye kukufuru waziwazi. Au amejichukulia watoto wakike katika vile alivyoviumba, na akawachagulia nyinyi watoto wa kiume?
Makusudio ya fungu hapa ni mtoto, kwa sababu ni sehemu ya mzazi wake. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watoto wa kike katika vile alivyoviumba, inaonyesha dalili ya uharibifu wa madai yao kuwa Mwenyezi Mungu ana mtoto, kwa sababu muumbwa hawezi kuwa ni sehemu ya aliyeumba; kama ambavyo nyumba haiwezi kuwa ni sehemu ya mjenzi.
Washirikina hawakutosheka na uzushi huu, mpaka wakamhusisha Mwenyezi Mungu na wale watoto wasiowapenda wao.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:100), Juz. 15 (17:40) na Juz. 23 (37:149-153).
Na mmoja wao akibashiriwa kwa yale aliyompigia mfano Mwingi wa rehema, uso wake husawijika naye amejaa chuki.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwasifu washirikina na ukafiri ulio waziwazi, sasa anawashutumu wale wanaohuzunika na kukasirika wakipata wasichana, wakati huohuo wanamzulia Mwenyezi Mungu na kusema kuwa ana watoto wasichana.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (16:58).
Ati aliyelelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema bayana?
Ewe mshirikina mjinga! Unamnasibishia Mwenyezi Mungu wanawake wanojipamba, na kama ukihojiwa kwenye hilo utashindwa na hoja na dalili? Wafasiri wamesema wamemnasibishia Mwenyezi Mungu wanawake ambao hawawezi hoja na kubishana Dhahiri ya Aya inarudia kwenye tafsiri hii.
Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao?
Vipi wanajasiri washirikina kusema kuwa Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu. Je, walikuwako kwa Mwenyezi Mungu wakati akiwaumba Malaika au aliwapa habari ya hilo? Amesema kweli aliyesema: “Mtu amesema uwongo juu aliye mfano wake, juu ya Mola wake, juu ya Mitume wake na Malaika wake, vile vile amesema uwongo juu ya nafsi yake.”
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
أَمْ خَلَقْنَا الْمَلَائِكَةَ إِنَاثًا وَهُمْ شَاهِدُونَ ﴿١٥٠﴾
“Au tumewaumba malaika kuwa ni wanawake na wao wakashuhudia? Juz. 23 (37:150).
Ushahidi wao utaandikwa na wataulizwa!
Kwa Mwenyezi Mungu hakufichiki chochote, Yeye anajua uzushi wao kwake na kwa Malaika wake na kesho atawauliza na kuwahisabu
Na husema: Angelipenda Mwingi wa Rehema tusingeliwaabudu.
Wanadai kuwa Mwenyezi Mungu yuko radhi wao kuabudu Malaika na masanamu; vinginevyo angeliwazuia kwa nguvu. Wamesahau kama Mwenyezi Mungu angelifanya hivyo, mtu angelikuwa sawa na mawe, asingelistahiki thawabu wala adhabu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:148).
Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
Wamenasibisha shirki yao na upotevu wao kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu! Hawajui kuwa Yeye, ambaye imetukuka enzi yake, anaamrisha na anakataza kitaklifa na kimongozo, akaacha utekelezaji uwe kwa matakwa ya aliyekalifishwa, ili yadhihiri matendo yake yatakayomfanya astahiki thawabu au adhabu.
Au tuliwapa Kitabu kabla ya hiki, wakawa wameshikamana nacho?
Hapana! Hawana dalili ya akili wala ya nakili kwa madaia yao, isipokuwa dalili hii:
Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi na tunaongoza nyayo zao.
Kwa hiyo kuwaiga mababa ndio kimbilio la kwnza na la mwisho. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameisimulia kauli yao hii katika Aya kadha; miongoni mwazo ni: Juz. 2 (2:170), Juz. 7 (5:104), Juz.17 (21:53), Juz.21 (31:21) na nyinginezo. Tumeweka kifungu kuhusu kuiga na mafungu yake katika Juz. 2 (2:170).
Na kadhalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila wapenda anasa wake walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya des- turi na tunafuata nyayo zao.
Haya ndio mantiki ya wanaotaka manufaa yao tu, tangu walipoanza kupatikana hadi siku ya mwisho. Tazama kifungu ‘Fikra ya mataghuti’ katika Juz. 13 (13:30-31), Juz. 15 (17:16-21) na kifungu ‘Mantiki ya watu wa pesa ni benki na ardhi.’ katika Juz. 18 (25:7-16).
Akasema: Hata nikiwaletea yenye muongozo bora kuliko mliowaku- ta nayo baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.
Tunalolifahamu kutokana na kauli yao hii ni kuwa wao wanaikataa haki popote na vyovyote iwavyo; hata kama ingelitoka kwa mababa zao, na kwamba wao hawaamini chochote isipokuwa manufaa na chumo lao tu.
Ama kujiingiza kwenye desturi ya mababa ni visingizio tu, wakihofia kujulikana uhakika wao na watu. Tumewawona wengi wakiwabeza mababa zao, si kwa lolote ila kuwa wanagongana na masilahi na mapendeleo yao. Hakuna malipo kwa mwenye kuipinga haki isipokuwa kumtumilia nguvu:
Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa waliokadhibisha!
Bila shaka ni fedheha na moto wa Jahannam.