1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
Sura Ya Arubaini Na Sita: Surat Al-Ahqaf. Imeshuka Makka. Ina Aya 35.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
حم ﴿١﴾
1. Haa miim.
تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
مَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾
3. Hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda uliowekwa. Na wale waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa.
قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ ائْتُونِي بِكِتَابٍ مِّن قَبْلِ هَـٰذَا أَوْ أَثَارَةٍ مِّنْ عِلْمٍ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤﴾
4. Sema: Je, mnawaona wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au wana shirika katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki, au athari yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ ﴿٥﴾
5. Na ni nani mpotofu mkubwa kuliko yule anayeomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ambaye hatamjibu mpaka Siku ya Kiyama, Na wala hawatambui maombi yao.
وَإِذَا حُشِرَ النَّاسُ كَانُوا لَهُمْ أَعْدَاءً وَكَانُوا بِعِبَادَتِهِمْ كَافِرِينَ ﴿٦﴾
6. Na watakapokusanywa watu watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.
IKO WAPI DALILI IKIWA NYINYI NI WA KWELI?
Aya 1-6
MAANA
Haamiim. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 25 (45:1) na Juz. 23 (39:1).
Hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda uliowekwa.
Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima, haumbi kitu ila kwa hikima, na ni muhali kuumba kwa mchezo. Ameuumba ulimwengu na yaliyomo ndani yake kwa hikima na malengo sahihi. Akauwekea muda maalum wa kwisha kwake; baada yake ni hisabu na malipo katika nyumba ya pili.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (30:8).
Na wale waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa.
Mwenyezi Mungu anawahofisha wakosefu na siku ya Kiyama na vituko vyake, na akawawekea dalili wazi, lakini wakakataa isipokuwa inadi na jeuri.
Je, mnawaona wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au wana shirika katika mbingu?
Maana ni kuwa nipeni habari enyi waabudu masanamu, ni jambo gani liliowafanya muyafanye masanamu ni miungu na kuyaabudu. Je, ni kwa kuwa yameumba kitu katika ardhi na mbinguni au yalishirikiana na Mwenyezi Mungu katika kuumba mbingu au sehemu yake?
Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki
cha Qur’an; kama vile Tawrat, Injil n.k., kinachosema kuwa masanamu ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake au kuwa yanaweza kuwaombea kwa Mungu au kuwa na utajo wowote.
Au athari yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
Ikiwa hamna dalili ya nukuu yoyote, je mnayo dalili ya kiakili kusadikisha myasemayo na kuyafanya sahihi mnayoyaabudu?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (35:40).
KUABUDU MASANAMU WAKATI MAENDELEO YA KUFIKA ANGANI
Unaweza kuuliza
: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametilia umuhimu sana kuwarudi wenye kuabudu masanamu na mizimu kwenye Aya hii na nyinginezo, na hali hili sio jambo zito sana na liko wazi kabisa? Kuupinga uungu wa masanamu si ni jambo liliowazi; sawa na kuukanusha upofu na uoni na giza na nuru?
Jibu
: Kuyatukuza masanamu na kuyaabudu, kumekua ni sehemu ya maisha ya mtu kuanzia zama na Nuh
mpaka zama za Muhammad(s.a.w.
w
)
, ambapo baina ya wawili hao kuna maelefu ya miaka; bali mpaka hivi sasa kwenye maendeleo ya kufika angani, bado masanamu yameenea mashariki mwa ardhi na magharibi yake.
Masanamu yaliyoko kwenye nyumba za ibada, siku hizi, kwenye njia panda na kwenye vilele vya milima. Pia mapicha kwenye kuta yaliyoenea huku na huko na kwenye vitabu vya kumbukumbu si ni aina ya kuabudu masanamu?
Umetukuka ukuu wa Muhammad(s.a.w.
w
)
katika kumtukuza mtu kwa kumsafisha na ibada ya masanamu yaliyotengenezwa na mikono yake. Mshairi anasema:
Namshangaa insani mchonga jiwe ambaye
Hulifanya rahamani Mungu aabudiwaye
Huku adhani moyoni hudhuru na kumfaaye
Si aabudu mikono ilochonga hilo jiwe
Hayo si ndio maono lau ataka ajuwe
Basi na iwe mikono ya kuabudu si jiwe
Ndiyo imechonga jiwe kama anavyoelewa
Na nani mpotofu mkubwa kuliko hao wanaowaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, ambao hawatawaitikia mpaka Siku ya Kiyama.
Makusudio ya kusema ‘mpaka siku ya Kiyama,’ ni milele na kutowezekana kujibu kabisa. Maana ni kuwa hakuna mjinga aliyepotea zaidi kuliko yule anayeabudu kisichosikia anayeita wala kumjibu anayeomba.
Na wala hawatambui maombi yao.
Washirikina wanaabudu masanamu, lakini masanamu hayana habari nao, wala hayana hisia yoyote.
Na watakapokusanywa watu watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.
Vile vile siku ya Kiyama wakati watu watakapofufuliwa kwa hisabu na malipo, miungu ya washirikina itajitenga nao na kuwakataa. Tazama Juz.11 (10:28).
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ هَـٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٧﴾
7. Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, wale waliokufuru husema juu ya haki inapowajia: Huu ni uchawi ulio wazi.
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ إِنِ افْتَرَيْتُهُ فَلَا تَمْلِكُونَ لِي مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا هُوَ أَعْلَمُ بِمَا تُفِيضُونَ فِيهِ كَفَىٰ بِهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٨﴾
8. Au wanasema: Ameizua! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo mnayoropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ni Mwingi wa Maghufira, Mwenye kurehemu.
قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٩﴾
9. Sema, mimi si kioja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyofanywa mimi wala nyinyi. Mimi nafuata niliyopewa Wahyi tu, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji, mwenye kubainisha.
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَكَفَرْتُم بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٠﴾
10. Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na alishuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا لَوْ كَانَ خَيْرًا مَّا سَبَقُونَا إِلَيْهِ وَإِذْ لَمْ يَهْتَدُوا بِهِ فَسَيَقُولُونَ هَـٰذَا إِفْكٌ قَدِيمٌ ﴿١١﴾
11. Na wale ambao wamekufuru waliwaambia wale ambao wameamini: Lau hii ingelikuwa ni heri, wasingelitutangulia. Na walipokosa kuongoka kwayo basi wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
وَمِن قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً وَهَـٰذَا كِتَابٌ مُّصَدِّقٌ لِّسَانًا عَرَبِيًّا لِّيُنذِرَ الَّذِينَ ظَلَمُوا وَبُشْرَىٰ لِلْمُحْسِنِينَ ﴿١٢﴾
12. Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa kiongozi na chenye rehema. Na hiki ni Kitabu chenye kusadikisha cha lugha ya kiarabu, ili kiwaonye wale waliodhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
AU WANASEMA WAMEYATUNGA?
Aya 7 – 12
MAANA
Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, wale waliokufuru husema juu ya haki inapowajia: Huu ni uchawi ulio wazi.
Makusudio ya ishara zetu na haki ni Qur’an. Maana ya zilizo wazi ni kuwa Aya za Qur’an ziko wazi hazikufunganafungana. Lakini pamoja na kuwa Qur’an iko wazi na kudhihiri dalili kuwa ni haki, bado wazushi, walio mataghuti na wapenda anasa wameipa sifa ya uchawi ulio waziwazi. Si kwa lolote ila ni kwa kuwa imewafanya wao kuwa sawa na watu wengine. Umetangulia mfano wa hayo katika Aya kadhaa huko nyuma.
Au wanasema: Ameizua! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.
Je, washirikina wanadai kuwa umeizua hii Qur’an ewe Muhammad(s.a.w.
w
)
? Waambie: vipi nimzulie Mungu uwongo na hali mimi ndiye ninayemuhofia zaidi? Je, mtanikinga na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake ikiwa nitasema uwongo au kumzulia? Aliyasema haya Mtume kutegemea vile wanavyomjua yeye jinsi anavyochukia uwongo na tabia nyinginezo mbaya.
Yeye anajua zaidi hayo mnayoropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi.
Hakifichiki kitu katika kauli zenu na vitendo vyenu nanyi mtahisabiwa navyo; na Mwenyezi Mungu ananijua mimi na nyinyi, kwa hiyo anashudia ukweli na uaminifu kwangu na anashuhudia uwongo na hiyana kwenu
Na Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Atawasamehe na kuwachanganya kwenye rehema yake ikiwa mtatubia na kurejea.
Sema: mimi si kioja miongoni mwa Mitume.
Mimi si wa kwanza kufikisha ujumbe wa Mungu. Wamenitangulia mitume na manabii wengi
Wala sijui nitakavyofanywa mimi wala nyinyi.
Mtume(s.a.w.
w
)
anajua hali yake na hali ya washirikina huko Akhera. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa habari ya hilo; kama zinavyoeleza Aya kadhaa; mbali ya kuwa ilimu hii ni katika nyenzo za utume. Zimekuja Hadith mutawatir, kwamba Mtume aliwabashiria pepo watu kadhaa.
Kwa hiyo basi Maana ya Aya ni kuwa Mtume hajui yatakayowatokea katika maisha ya duniani na atawatia mtihani gani Mwenyezi Mungu. Vile vile hajui kuwa Mwenyezi Mungu atawaadhibu hapa duniani au ataahirisha adhabu yao mpaka siku ya ufufuo.
Mimi nafuata niliyopewa Wahyi tu, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji mwenye kubainisha.
Sio kazi ya muonyaji kujua ilimu ya ghaibu; isipokuwa yeye anafikisha anayopewa wahyi na Mwenyezi Mungu kuhusiana na yale yatakayowatokea washirikina.
Ieleweke kuwa Aya hii ilishuka kabla ya kushuka Aya inayosema kuwa mwisho ni wa dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wajapochukia washirikina. Au pengine ni miongoni mwa mifumo ya kutoa mwito kwa hikima na mawaidha mazuri.
Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na alishuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.
Sura hii tuliyo nayo imeshuka Makka isipokuwa Aya hii tuliyo nayo, ilishuka Madina kwa ajili ya Abdullah bin Salim, aliposilimu Madina. Yeye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa Wana wa Israil. Haya ndiyo yaliyoelezwa kwenye tafsiri nyingi.
Maana ni sema ewe Muhammad kuwaambia wale wanaodai kuwa Qur’an ni uchawi uliozushwa, hebu niambieni itakuwaje hali yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ikithibiti kuwa Qur’an ni haki na kweli na akaiamini mwana wa chuoni katika wana wa Israil; kama vile Abdullah bin Salam ambaye anatambua siri za wahyi na kushuudia kuwa mafunzo ya Qur’an ni kama mafunzo ya Tawrat iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Musa? Basi mtakuwaje mkibaki na upotevu wenu na inada yenu? Je mjidhulumu kwa hiyari yenu na kujianika kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu?
Na wale ambao wamekufuru waliwaambia wale ambao wameamini: Lau hii ingelikuwa ni heri, wasingelitutangulia.
Watu wengi walioitikia mwito wa Mtume(s.a.w.
w
)
, mwanzo mwanzo wa mwito wa Uislamu, walikuwa ni miongoni mwa wanyonge. Kwa hiyo mamwinyi wakaifanya hiyo ni sababu ya kuituhumu risala ya Mtume. Kwa sababu, wanavyodai, ni kuwa haki ni ile inayokubaliwa na vigogo, wala sio kuwa watu wajulikane kwa kuwa na haki. Kila wanalolilifanya matajiri ndio haki na wanalolilifanya wengine ni batili. Hayo ndiyo madai yao, lakini kila mwenye kuipinga haki itamshinda.
Ndio maana hazikupita siku mtumwa wa kihabeshi akapanda kwenye mgongo wa Al-Ka’aba akinadi Lailaha illallah Muhammadurrasulullah (Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu). Na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
akayavunja masanamu na kuyatupa chini ya nyayo zake huku akisema: “Haki imefika na batili imeondoka, hakika batili ni yenye kuondoka.”
Katika Tafsir Arrazi, imeandikwa kuwa mjakazi wa Amru alisilimu na alikuwa akimpiga mpaka anachoka. Basi makafiri wakasema: “Kama Uislamu ungelikuwa ni kheri asingetutangulia majakazi wa Amru.” Lakini Amru mwenyewe alisilimu badaye, akapigana vita vya Roma na Fursi.
Na walipokosa kuongoka kwayo basi wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
Wanazungumziwa makafiri wa kikuraishi. ‘Kwayo’ ni hiyo Qur’an. Mataghuti waliisifu kuwa ya zamani, kwa vile, kwa madai yao, wanasema ni ngano za watu wa kale zilizopitwa na wakati.
Walisema hivi sio kwa lolote isipokuwa wao hawaamini isipokuwa masilahi yao na chumo lao tu, na Qur’an inapinga na kupiga vita hayo.
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa kiongozi na chenye rehema. Na hiki ni Kitabu chenye kusadikisha cha lugha ya kiarabu, ili kiwaonye wale waliodhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Qur’an ni kama Tawrat iliyomshukia Musa. Vitabu vyote hivyo viwili vinaongoza kwenye haki na ni rehema kwa mwenye kuviamini na avitumia kwa mujibu wake. Tawrat ilitoa habari za kuja Muhammad:
الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ ﴿١٥٧﴾
“Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakatazamaovu.” Juz. 9 (7:157).
Vile vile Qur’an inaisadikisha Tawrat hii na inatamka kwa lugha yenu, enyi waarabu, ikimuonya na adhabu yule atakayefanya uovu na kumpa habari njema za thawabu yule mwenye kufanya wema. Basi vipi mara mnasema ni uchawi na mara nyingine ni ngano za watu wa kale; mbona hamyasemi hayo kwa Tawrat?