19
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنثَىٰ ﴿٢٧﴾
27. Hakika wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.
وَمَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا ﴿٢٨﴾
28. Nao hawana ujuzi wowote wa hayo isipokuwa wanafuata dhana tu, na hakika dhana haifai kitu mbele ya haki.
فَأَعْرِضْ عَن مَّن تَوَلَّىٰ عَن ذِكْرِنَا وَلَمْ يُرِدْ إِلَّا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٢٩﴾
29. Basi mwachilie mbali anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.
ذَٰلِكَ مَبْلَغُهُم مِّنَ الْعِلْمِ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اهْتَدَىٰ ﴿٣٠﴾
30. Huo ndio mwisho wao wa ujuzi. Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anayemjua zaidi mwenye kuongoka.
وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى ﴿٣١﴾
31. Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo katika ardhi, ili awalipe waliotenda ubaya kwa waliyoyatenda, na waliotenda mema awalipe mema.
الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ إِنَّ رَبَّكَ وَاسِعُ الْمَغْفِرَةِ هُوَ أَعْلَمُ بِكُمْ إِذْ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَإِذْ أَنتُمْ أَجِنَّةٌ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ ﴿٣٢﴾
32. Ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na vitendo vichafu, isipokuwa makosa madogo. Hakika Mola wako ni Mkunjufu Naye anawajua sana tangu alipowaumba kutoka kwenye ardhi, na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijitakase nafsi zenu, Yeye anamjua sana mwenye takua.
DHANA HAISAIDI KITU MBELE YA HAIFAI
Aya 27 – 32
MAANA
Hakika wasioamini Akhera wanawaita Malaika kwa majina ya kike.
Waliikadhibisha haki kwa ujinga na inadi. Kila moja kati ya mawili hayo linatosha kuwa ni tafsiri na sababu ya uzushi wao kwa Mwenyezi Mungu kwamba ana washirika, mke na watoto wa kike. Hawakutosheka kusema ana watoto mpaka wakawapa majina maalum.
Nao hawana ujuzi wowote wa hayo isipokuwa wanafuata dhana tu,
ndio wakathibitisha vitu visivyokuwako wala kuwa na dalili yoyote isipokuwa njozi tu zinazopita vichwani mwao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwarudi kwa kuwaambia kuwa hajui yeye kama ana mabinti aliposema:
قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١٨﴾
“Sema je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? Ametakasika na ametukuka na hao wanaomshirikisha naye.” Juz. 11 (10:18).
Na hakika dhana haifai kitu mbele ya haki.
Lau watu wangelifuata dhana, mambo yasingelikwenda sawa katika maisha haya. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 11 (10:36).
Basi mwachilie mbali anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.
Maneno yaaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
lakini yanakusudiwa kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Maana ni kuwa usiwajadili wale ambao wamezama kwenye uasi na upotevu, wasioamini kitu wala kuona kima chochote isipokuwa nafsi zao na chumo lao:
وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا ﴿٢٥﴾
“Na wakiona kila ishara hawaiamini.” Juz. 7 (6:25).
Basi kuna haja gani ya kubishana nao. Tazama kifungu: ‘Haki na manufaa’ katika Juz. 3 (3:52-54) na kifungu: ‘Mjadala wa kijinga na upotevu.’ Juz.17 (22: 1-7).
Huo ndio mwisho wao wa ujuzi
na haki. Hawana ujuzi, dini dhamiri, haki na msimamo isipokuwa anasa na kutukuza mali. Tazama Juz. 18 (25:7-16). Kifungu: ‘Mantiki ya watu wa pesa ni benki na ardhi.’
Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anayemjua zaidi mwenye kuongoka.
Ewe Muhammad! Mola wako anajua kuwa wale walioukadhibisha unabii wako hawakataziki na upotevu. Vile vile anajua kuwa wewe uko kwenye uongofu na wale wanaokufuata katika waumini. Kwa sababu Yeye amekizunguka kila kitu na ni muweza wa kumlipa mwenye kuamini na kuongoka na adhabu ya mwenye kupotea.
Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo katika ardhi, ili awalipe waliotenda ubaya kwa waliyoyatenda, na waliotenda mema awalipe mema.
Aya hii ni kemeo na kiaga kwa yule aliyemwashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: “Anayeupa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia.”
Njia ya ukemeo ni kuwa dunia na Akhera ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye peke yake ndiye mmiliki wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.
Kwa hiyo atakayeiacha Akhera na akaitafuta dunia na akaihangaikia, tutampa hiyo dunia na katika Akhera hana isipokuwa adhabu; ambapo kila mtu atapata malipo ya matendo yake, ikiwa ni heri basi ni heri na ikiwa ni shari basi ni shari.
Ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na vitendo vichafu, isipokuwa makosa madogo. Hakika Mola wako ni Mkunjufu wa maghufira.
Madhambi makubwa ni kama kufru, shirk na dhulma. Na kila linalopituka mpaka kwenye uovu ni katika vitendo vichafu na ni dhambi kubwa pia; kama vile zina na ulawiti. Ama madhambi madogo ni yale ambayo mara nyingi yanampitia mtu; isipokuwa wale maasumu; kama kuangalia na kukaa kwenye meza ya pombe. Tumezungumza kwa ufafanuzi katika Juz.5 (4:31).
Maana ya Aya ni kuwa mwenye kujing’oa kwenye madhambi makubwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) huumpa msamaha na hisani yake hata kama aki- fanya madhambi madogo. Lakini hii haimaanishi kwamba mtu anaruhusiwa kufanya madhambi madogo; hapana! Vinginevyo itakuwa ni halali; isipokuwa ni kwamba mwenye kujiepusha na madhambi makubwa awe na matumaini ya kusamehewa madogo kutoka kwa Mola wake. Vinginevyo ingelikuwa Pepo ni ya maasumu tu.
Imeelezwa katika Nahju-Bbalagha: “Dhambi kubwa ni ile aliyoidharau mtendaji… Na kuyakuza mtu maasi ya mwingine na kuadharau yake na kujiona ana twaa nyingi kuliko mwingine.”
Naye anawajua sana tangu alipowaumba kutoka kwenye ardhi, na mlipokuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijitakase nafsi zenu, Yeye anamjua sana mwenye takua.
Ndio! Mwenyezi Mungu anamjua zaidi mtu kuliko anavyojijua yeye mwenyewe vyovyote atakavyokua na ilimu. Haiwezekani mtu kujijua kuliko anavyojuliwa na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyemfanya aweko na kumpa uhai, akamficha na atamfufua. Yuko naye akimjua tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake mpaka pumzi yake ya mwisho.
Zaidi ya hayo ni kuwa viungo vya mtu hata moyo wake ni shahidi wake mbele ya muumba wake. Shahidi mkali zaidi atakayetamka kumtakasa mtu na kufanya awe katika wenye ikhlasi ni matendo yake mema. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:49) na Juz. 18 (24:21).
أَفَرَأَيْتَ الَّذِي تَوَلَّىٰ ﴿٣٣﴾
33. Je, Umemwona yule aliyegeuka?
وَأَعْطَىٰ قَلِيلًا وَأَكْدَىٰ ﴿٣٤﴾
34. Na akatoa kidogo, kisha akajizuia?
أَعِندَهُ عِلْمُ الْغَيْبِ فَهُوَ يَرَىٰ ﴿٣٥﴾
35. Je, anayo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona?
أَمْ لَمْ يُنَبَّأْ بِمَا فِي صُحُفِ مُوسَىٰ ﴿٣٦﴾
36. Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?
وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ ﴿٣٧﴾
37. Na vya Ibrahim aliyetimiza ahadi?
أَلَّا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ﴿٣٨﴾
38. Kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine?
وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾
39. Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyahangaikia.
وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾
40. Na kwamba mahangaiko yake yataonekana.
ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴿٤١﴾
41. Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu.
MTU HATAPATA ILA ALIYOYAFANYA
Aya 33 – 41
MAANA
Je, Umemwona yule aliyegeuka? Na akatoa kidogo, kisha akajizuia?
Yaani akazuia kutoa. Maana ni kuwa hebu niambie ewe Muhammad kuhusu mtu ambaye ameupa kisogo utajo wa Mwenyezi Mungu, na akawa ametoa kitu kidogo katika mali yake au nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha akajizuia kutoa!
Hii ndivyo inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Kisha linakuja swali, kuwa je, Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimkusudia mtu maalum aliyemjua Nabii(s.a.w.
w
)
, au alikusudia mfano wa jumla kwa kila atakayekuwa na sifa hizi? Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilimshukia Walid bin Al- Mughira, wengine wakasema ni Uthman Bin Affan. Kauli zote mbili zinahitajia dalili. Kwa hiyo basi Aya inabakia na ujumla wake na kuenea kwa kila mwenye sifa hizo.
Je, anayo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona?
Je, huyu mpingaji anayejizuia kutoa anajua kuwa yeye yuko kwenye amani ya adhabu ya siku ya kiyama mpaka akajasiri kupinga na kujizuia? Na atakuwa ameitoa wapi ilimu hii na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameteremsha katika Kitabu yanayokadhibisha madai yake kama atadai hivyo?
Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa? Na vya Ibrahimu aliyetimiza ahadi?
Hakusikia mpinzani huyu aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Tawrat na maandishi ya Ibrahim ambaye alitimiza ahadi kwa njia ya ukamilifu. Hakusikia kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha katika vitabu viwili hivi,kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwingine?
Yaani kila mtu ataadhibiwa kwa dhambi zake na hakuna atakayembebea madhambi yake.
Aya hii imekaririka katika Juz. 8 (6:164), Juz. 15 (17:15), Juz. 22 (35:18) na Juz. 23 (39:7).
Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyahangaikia.
Makusudio ya kuhangaika hapa ni kufanya amali na harakati katika maisha haya. Aya hii inafahamisha wazi kuwa dini ya Uislamu ni dini ya maisha, kwa sababu inaelezea waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu anawangalia waja wake kupitia matendo yao katika maisha ya dunia na anaamiliana nao kwa mujibu wake.
Maana yake ni kuwa kila atakavyofanya mtu kwa ajili ya heri yake na akatatua matatizo yake atakuwa amekuwa karibu na Mwenyezi Mungu na dini ya Mwenyezi Mungu na atastahiki rehema na karama.
Na kadiri atavyoyakimbia maisha akajiweka mbali na matatizo yake kwa kutosheka na takbira, tahalili, kufunga na kuswali, basi atakuwa amejiweka mbali na Mwenyezi Mungu na dini yake na rehema yake.
Na kwamba mahangaiko yake yataonekana.
Yaani Mweneyzi Mungu atamuhisabu kwa mujibu wa matendo yake Siku ya Kiyama. Makusudio ya kuonekana hapa ni kuhisabiwa; vinginevyo ni kuwa Mweneyzi Mungu (s.w.t) anajua kila kitu hata mawazo na wasiwasi.
Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu.
Iko wazi haihitaji tafsiri, ni sawa na kauli yake Mweneyzi Mungu Mtukufu:
أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَى ﴿١٩٥﴾
“Kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke.” Juz. 4 (3:195).
وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ ﴿٤٢﴾
42. Na kwamba kwa Mola wako ndio mwisho.
وَأَنَّهُ هُوَ أَضْحَكَ وَأَبْكَىٰ ﴿٤٣﴾
43. Na kwamba Yeye ndiye anayeleta kicheko na kilio.
وَأَنَّهُ هُوَ أَمَاتَ وَأَحْيَا ﴿٤٤﴾
44. Na kwamba Yeye ndiye anayefisha na kuhuisha.
وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ ﴿٤٥﴾
45. Na kwamba Yeye ndiye aliyeumba jozi, dume na jike,
مِن نُّطْفَةٍ إِذَا تُمْنَىٰ ﴿٤٦﴾
46. Kutokana tone la manii linapomiminwa.
وَأَنَّ عَلَيْهِ النَّشْأَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٤٧﴾
47. Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine.
وَأَنَّهُ هُوَ أَغْنَىٰ وَأَقْنَىٰ ﴿٤٨﴾
48. Na kwamba ni Yeye ndiye anayetosheleza na anayetajirisha.
وَأَنَّهُ هُوَ رَبُّ الشِّعْرَىٰ ﴿٤٩﴾
49. Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola wa Shii’ra.
وَأَنَّهُ أَهْلَكَ عَادًا الْأُولَىٰ ﴿٥٠﴾
50. Na kwamba Yeye ndiye aliyewaangamiza A’di wa kwanza.
وَثَمُودَ فَمَا أَبْقَىٰ ﴿٥١﴾
51. Na Thamudi hakuwabakisha.
وَقَوْمَ نُوحٍ مِّن قَبْلُ إِنَّهُمْ كَانُوا هُمْ أَظْلَمَ وَأَطْغَىٰ ﴿٥٢﴾
52. Na kabla yao kaumu ya Nuh. Na hao hakika walikuwa ni madhalimu zaidi, na waasi zaidi.
وَالْمُؤْتَفِكَةَ أَهْوَىٰ ﴿٥٣﴾
53. Na miji iliyopinduliwa, ni Yeye aliyeipindua.
فَغَشَّاهَا مَا غَشَّىٰ ﴿٥٤﴾
54. Vikaifunika vilivyofunika.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكَ تَتَمَارَىٰ ﴿٥٥﴾
55. Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?
هَـٰذَا نَذِيرٌ مِّنَ النُّذُرِ الْأُولَىٰ ﴿٥٦﴾
56. Hili ni Onyo katika maonyo yale yale ya zamani.
أَزِفَتِ الْآزِفَةُ ﴿٥٧﴾
57. Tukio la karibu limekurubia.
لَيْسَ لَهَا مِن دُونِ اللَّـهِ كَاشِفَةٌ ﴿٥٨﴾
58. Hapana wa kulifichua isipokuwa Mwenyezi Mungu.
أَفَمِنْ هَـٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ ﴿٥٩﴾
59. Je, mnayastaajabia maneno haya?
وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na mnacheka wala hamlii?
وَأَنتُمْ سَامِدُونَ ﴿٦١﴾
61. Nanyi mmeghafilika?
فَاسْجُدُوا لِلَّـهِ وَاعْبُدُوا ﴿٦٢﴾
62. Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumwabudu.
KWA MOLA WAKO NDIO MWISHO
Aya 42 – 62
MAANA
Na kwamba kwa Mola wako ndio mwisho.
Aya hii na zinazofuatia bado zinaungana na zile alizosema Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa ziko katika vitabu vya Musa na Ibrahim. Makusudio ya mwisho ni kusimama mtu mbele ya Mola wake kwa ajili ya hisabu ambayo hataepukana nayo.
Na kwamba Yeye ndiye anayeleta kicheko na kilio.
Kicheko ni ishara ya furaha ya watu wa Peponi na kilio ni huzuni ya watu wa motoni. Inawezekana kuwa ni ishara ya silika ya ladha, uchungu, huzuni na furaha aliyompa Mwenyezi Mungu mtu.
Watu wa falsafa wanasema kuwa mtu hawezi kutaharaki isipokuwa kwa mvuto wa ladha; kama vile tendo la ndoa au kwa kuhofia maumivu; kama vile njaa.
MAADA NA MAISHA
Na kwamba Yeye ndiye anayefisha na kuhuisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye anayetoa uhai na kuuchukua. Ama kauli ya mwenye kusema maada ndio asili ya uhai na ndiyo iliyousababisha, hayo ni madai tu yanayokataliwa na msingi wa akili. Kwa sababu maada haina harakati kwa maumbile yake mpaka ipate sababu ya kuibadilisha.
Ni nani mwenye akili anayeweza kukubali kuwa maada pofu imejitengenezea yenyewe macho, masikio na moyo? Ikiwa uhai ni sifa ya maada kwanini kukatokea kukua, harakati, hisia na kufikiri katika baadhi tu, na kwingine kusitokee?
Ikiwa mtu atajibu kuwa baadhi ya maada zina maandalizi ya uhai na nyingine hazina, tutamuuliza: Je, tofauti hii imetoka wapi? Kutoka ndani ya maada yenyewe au kutoka nje? Ikiwa imetoka ndani basi ni lazima kila maada iwe na uhai; vinginevyo itakuwa kitu kimoja kimesababisha kupatikana na kukosekana kwa wakati mmoja. Na ikiwa imesabishwa na sababu ya nje, basi hivyo ndivyo tusemavyo.
Na kwamba Yeye ndiye aliyeumba jozi, dume na jike kutokana tone la manii linapomiminwa.
Mwanamume anashusha manii yake katika mfuko wa uzazi, mimba inatungwa na anapatikana mtoto wa kike au wa kiume. Ni nani basi aliyeleta maandalizi ya mbegu hii mwilini? Ni nani aliyeleta mamilioni ya chembe hai? Je, wataalamu wanaweza kutengeneza chembe moja itakayotoa mtoto wa kike au wa kiume? Bali je, wanaweza kutofautisha chembe itakayotengeneza mtoto wa kiume au wa kike? Ikiwa mbegu za uzazi zinategemea sababu za maumbile, basi sababu hizi zinaishia kwa yule aliyetengeneza maumbile.
Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine.
Juu yake ni juu ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa ufufuo hauna budi kuweko.
Na kwamba ni Yeye ndiye anayetosheleza na anayetajirisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa waja wake na akawafanya wajitosheleze bila ya kuwa na haja ya kuomba wengine na wengine akawapa ya kuwatosheleza na ziada ya kuweka akiba. Mmoja wa wataalamu anasema: “Mwenye kuonja ladha ya kujitosheleza atakuwa amepata fungu la kujitosheleza na kwamba hilo lina utukufu.’’
Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola wa Shii’ra.
Shiira (Sirius) ni nyota inayoangaza. Mwenyezi Mungu amehusisha kuitaja hapa kwa sababu watu wa wakati wa jahilia walikuwa wakiiabudu. Imesemekana kuwa ni kubwa kuliko Jua kwa mara ishirini na kwamba iko mbali na jua kwa mara milioni zaidi ya sisi tulivyo mbali na Jua.
Na kwamba Yeye ndiye aliyewaangamiza A’di wa kwanza.
Hao ni watu wa Hud. Mazungumzo kuwahusu yamekwishapita huko nyuma mara kadhaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu kuwa wa kwanza kutokana na wale waliokuja baada yao katika umma. Mwenye Majmaulbayan anasema ni kwa sababu walikuja A’di wengine.
Na Thamudi hakuwabakisha,
yeyote katika wao.
Hao ni watu wa Swaleh. Vile vile yametangulia maelezo yao na ya watu wa Nuh ambao amewaashiri Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kusema:Na kabla yao kaumu ya Nuh. Na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waasi zaidi
kuliko A’di na Thamud.
Na miji
ya kaumu ya Lutiliyopinduliwa, ni Yeye aliyeipindua
akaizamisha ndani ya ardhi.
Vikaifunika vilivyofunika
kwa adhabu.
Basi neema gani ya Mola wako unayoifanyia shaka?
Maneno yanaelekzwa kwa kila mtu.
Hili ni onyo katika maonyo yale yale ya zamani.
Wafasiri wengi wamesema kuwa ‘Ishara’ hapa ni ya Qur’an au Muhammad(s.a.w.
w
)
, kwa hiyo isemwe Hii au Huyu.
Hakuna mwenye shaka kuwa Qur’an na Muhammad(s.a.w.
w
)
ni katika maonyo ya mwanzo, lakini pamoja na hayo, tunavyofahamu ni kuwa Mwenyezi Mungu ameashiria yale aliyoyataja miongoni mwa dalili na mawaidha yaliyokusanya mambo muhimu yanayotakikana kuchunguzwa na kuwa ni mafunzo; kama maswala ya kuwa kila mtu peke yake ndiye mwenye majukumu ya makosa yake, kwamba Mwenyezi Mungu anamwangalia kupitia matendo yake, kuwa hakuna chimbuko la uhai isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu tu peke yake na mwisho wa waasi ni maangamizi.
Haya na mengineyo mfano wake ni miongoni mwa maudhui muhimu ya ulimwengu na binadamu. Anapoyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t), ili kumfahamisha mtu kuwa Mwenyezi Mungu yuko na ni mkuu, itakuwa kutajwa kwake hasa kunaashiria kuwa maana yake na malengo yake yanajitokeza kwa wataalamu na kwamba wao ndio wana haki zaidi ya kumjua Mwenyezi Mungu, kumwamini na kumcha:
إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ﴿٢٨﴾
“Hakika si mengineyo, wanaomcha Mwenyezi Mungu katika waja wake ni wale wajuzi.”
Juz. 22 (35:28).
Tukio la karibu limekurubia.
Makusudio ya tukio hapa ni Kiyama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameliisifu kuwa linasogea, kwa vile linakuja na kila linalokuja liko karibu na kila lililopita ni kama halikuwako.
Hapana wa kulifichua isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Kulifichua ni hilo tukio la karibu; yaani Kiyama. Unaweza kufasiri kufichua kwa maana ya ilimu; kama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ﴿١٨٧﴾
“Wanauliza hiyo Saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.” Juz. 9 (7:187).
Pia unaweza kufasiri kwa kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:
مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّـهِ ﴿٤٣﴾
“Kabla ya kufika siku isiyozuilika inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.” Juz.21 (30:43).
Je, mnayastaajabia maneno haya na mnacheka?
Mananeno haya ni haya mazungumzo ya Kiyama. Imesemkana ni Qur’an. Tafsri zote mbili ni sawa, kwa sabau makafiri walistahajabu ufufuo:
فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ ﴿٢﴾ أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ ﴿٣﴾
“Na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu! Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!” Juz. 26 (50:2-3).
Pia waliistaajabu Qur’an:
أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ ﴿٦٣﴾
“ Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola? Juz. 8 (7:63).
Wala hamlii? Nanyi mmeghafilika?
Ilikuwa bora mzililie nafsi zenu ambazo mmezidhulumu kwa ukafiri na dhulma:
فَلْيَضْحَكُوا قَلِيلًا وَلْيَبْكُوا كَثِيرًا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨٢﴾
“Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.”
Juz. 10 (9:82)
Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumuabudu.
Hanafi, Shafi, Shia Imamia na Hambali wamesema ni wajibu kusujudi wakati wa kusomwa Aya hii, kwa sababu Mtume(s.a.w.
w
)
alisujudi wakati wa kusomwa kwake na walisujudi waliokuwa pamoja naye, lakini Maliki wakasema kuwa siwajibu.
MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA TATU: SURAT AN-NAJM