TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 28308
Pakua: 3893


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 28308 / Pakua: 3893
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Hamsini Na Nne: Surat Al-Qamar. Imeshuka Makka. Ina Aya 55.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi Mwenye kurehemu.

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ ﴿١﴾

1. Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!

وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ ﴿٢﴾

2. Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Uchawi unaoendelea.

وَكَذَّبُوا وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ وَكُلُّ أَمْرٍ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣﴾

3. Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo lina wakati maalum.

وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّنَ الْأَنبَاءِ مَا فِيهِ مُزْدَجَرٌ ﴿٤﴾

4. Na bila ya shaka zimewajia habari zenye makaripio.

حِكْمَةٌ بَالِغَةٌ فَمَا تُغْنِ النُّذُرُ ﴿٥﴾

5. Hikima kamili, lakini maonyo hayafai.

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ ﴿٦﴾

6. Basi jiepushe nao. Siku atakapoita mwitaji kuliendea jambo linalochusha.

خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ ﴿٧﴾

7. Macho yao yatainama; watatoka makaburini, kama kwamba wao ni nzige waliotawanyika.

مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ يَقُولُ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَسِرٌ ﴿٨﴾

8. Wanamkimbilia mwitaji; makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.

MWEZI UMEPASUKA

Aya 1 – 8

MAANA

Saa imekaribia.

Maana yake ni sawa na Aya 57 ya sura iliyopita: “Tukio la karibu limekurubia.” Nayo ni kuwa siku ya Kiyama itafika tu, hilo halina shaka.

Na mwezi umepasuka!

Wafasiri wengi wamesema kuwa washirikina walimtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu,(s.a.w. w ) aupasue mwezi mara mbili ikiwa yeye ni mkweli. Basi akamwomba Mola wake, na mwezi ukapasuka vipande viwili, kisha ukarudi kwenye hali yake ya kawaida.

Hakuna mwenye shaka kuwa hili linawezekana, lakini kuwezekana ni jambo jingine na kutokea ni jambo jingine.

Kwa sababu kutokea kunahitajia dalili ya kuthibitisha; wala hakuna dalili ya kuthibitisha; bali dalili ziko kinyume na hivyo; kama ifuatavyo:-

Kwanza : Haya hayaafikiani na Aya kadhaa zinazoelezea waziwazi kuwa Mtume(s.a.w. w ) hakuitikia maoni ya wa shirikina kutaka mambo yasiyokuwa ya kawaida, naye akawajibu kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu:

قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنتُ إِلَّا بَشَرًا رَّسُولًا ﴿٩٣﴾

“Sema: ametakasika Mola wangu! Kwani mimi ninani isipokuwa ni mwanadamu Mtume!”

Juz. 15 (17:93).

Pia Mwenyezi Mungu amebainisha kuwa wanotaka muujiza wataendela na ukafiri wao hata wakijibiwa maombi yao:

وَمَا مَنَعَنَا أَن نُّرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَن كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ ﴿٥٩﴾

“Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila nikuwa watu wa zamani waliikanusha.”

Juz. 15 (17:59).

Akasema tena:

وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾

“Na wakiona kila Ishara hawaiamini na wakiona njia ya uongofu hawaishi- ki kuwa ndiyo njia, lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia,. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.” Juz. 9 (7:146).

Zaidi ya hayo ni kuwa mwenye kutaka visababu hana udhuru wowote baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwapa changa moto walimwengu wote na wakashindwa; pale aliposema: “Na mkiwa na shaka kwa (hayo) tuliyomteremshia mtumwa wetu, basi leteni sura moja iliyo mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.” Juz. 1 (2:23).

Pili : kupasuka mwezi ni tukio kubwa la kilimwengu, lau lingetokea wangeliona wa mashariki na wa magharibi, na wangeliliandika ulama na wanahistoria wengineo; kama walivyoandika matukio mengineyo.

Tatu : Kupasuka mwezi ni katika maudhui ambayo hayathibiti isipokuwa kwa khabar mutawatir na maudhui ya kupasuka mwezi yamekuja kwa Khabar Al-ahd. Tofauti ni kuwa katika Mutawatir wapokezi ni wengi na wanatofautiana hali zao na malengo yao, kwa namna ambayo, kwa kawaida, hawawezi kukongamana wakasema uwongo. Na Ahad ni kinyume na hivyo. Kwa hiyo unaweza kutofautisha kwamba mutawatir inategemewa zaidi kuliko Ahad.

Nne : Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Na umepasuka mwezi baada ya kauli yake: ‘Kimekurubia Kiyama.’ Inafahamisha kuwa mwezi utapasuka kitakapokuwa Kiyama na kwamba makusudio ya kupasuka mwezi hapa, ndio yale yaliyo katika kauli yake:

إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾

“Itakapopasuka mbingu.” (84:1).

Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: uchawi unaoendelea usiokuwa na mwisho.

Katika (74:24), Mwenyezi Mungu anamsimulia Walid bin Al-Mughira, kuwa alisema: “Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa.”

Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao.

Ujinga na hawaa umewapofusha na kila hoja na dalili. Kwa hiyo, pamoja na dalili za wazi, lakini wakakikadhibisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukutana naye.

Na kila jambo lina wakati maalum.

Hili ni kemeo kwa anayeiacha Qur’an. Maana ni kuwa kila kitu kimethibiti katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakifichiki kwake jambo lolote likiwamo kuipinga Qur’an na kuachana nayo.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki: Sema nami sikuwakilishwa juu yenu. Kila habari ina wakati maalum na punde mtajua.” Juz. 7 (6:66-67).

Na bila ya shaka zimewajia habari zenye makaripio.

Makusudio ya habari hapa ni kila Aya katika Qur’an yenye mawaidha na mazingatio, mapendekezo na makatazo, au zinazofahamisha njia ya imani, Siku ya Mwisho na wahyi ulioteremshwa kwa Mtume(s.a.w. w ) .

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwabainishia washirikina, kupitia Nabii wake Muhammad(s.a.w. w ) , dalili za kutosha juu ya haki, pia mawaidha ya kutosheleza ya kuikemea batili.

Hikima kamili.

Kila lilioko katika Qur’an ni hekima iliyofikia ukomo wa mawaidha na dalili juu ya haki,lakini maonyo hayafai kitu, kukiwa na inadi na kung’ang’ania ukafiri na upotevu.Basi jiepushe nao, ewe Muhammad, kwa sababu umewafikishia ujumbe wa Mola wako, lakini hawakukuitikia. Na ukafikisha nasaha, lakini hawakukubali.

Siku atakapoita mwitaji kuliendea jambo linalochusha. Macho yao yatainama; watatoka makaburini. Jambo linalochusha ni linalochukiwa na nafsi na kutochukulika. Makusudio yake hapa ni adhabu.

Hii ni kuwahofisha na kuwapa kiaga wale walioipinga haki, na kwamba wao wana siku ngumu isiyokuwa na kimbilio la adhabu yake, nayo ni siku watakayotoka makaburini kuelekea kwa Mola wao na hisabu, wakiwa madhalili wanyenyekevu, waamejawa na mshangao na kuchanganyikiwa.

Kama kwamba wao ni nzige waliotawanyika kutokana na wingi wao pale Mwenyezi Mungu atakapowafufua wafu na kuwausanya, watakapokutana wa mwanzo hadi wa mwisho.

Hapa kuna ishara ya kuwa ufufuo utakuwa kwa roho na mwili pamoja.

Wanamkimbilia mwitaji.

Yaani watakwenda haraka kwenye hisabu na malipo.

Makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu yenye vituko, hatari, maumivu na hofu.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu:

يَوْمَ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ سِرَاعًا كَأَنَّهُمْ إِلَىٰ نُصُبٍ يُوفِضُونَ ﴿٤٣﴾ خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الَّذِي كَانُوا يُوعَدُونَ ﴿٤٤﴾

“Siku watakapotoka makaburini kwa upesi; kama kwamba wao wanakimbilia kwenye mradi. Macho yao yatainama, fedhea itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa.” (70:43-44).

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ ﴿٩﴾

9. Kabla yao kaumu ya Nuh walikadhibisha; wakamkadhibisha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ ﴿١٠﴾

10. Basi akamwomba Mola wake: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!

فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُّنْهَمِرٍ ﴿١١﴾

11. Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika.

وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ ﴿١٢﴾

12. Na tukaipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo liliokadiriwa.

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ ﴿١٣﴾

13. Na tukamchukua kwenye ile ya mbao na misumari.

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِّمَن كَانَ كُفِرَ ﴿١٤﴾

14. Inakwenda kwa macho yetu. Ni malipo kwa alivyokuwa amekanushwa.

وَلَقَد تَّرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٥﴾

15. Na hakika tuliiacha iwe ni Ishara. Basi je, yupo anayekumbuka?

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٦﴾

16. Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo?

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾

17. Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

NUH

Aya 9 – 17

MAANA

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliashiria kwamba Muhammad(s.a.w. w ) aliwaonya watu wake, lakini hayakufaa maonyo. Katika Aya tulizonazo anaashiria kuwa hali ya Muhammad(s.a.w. w ) na watu wake, katika hilo, ni kama hali ya Nuh, na watu wake:

Kabla yao kaumu ya Nuh walikadhibisha; wakamkadhibisha mja wetu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: “wakamkadhibisha ni tafsiri ya kauli yake: “Walikadhibisha.” Kama kwamba muulizaji aliuliza: hawa jamaa walimkadhibisha nani? Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu kuwa wao walimkadhibisha mja wetu Nuh,na wakasema ni mwendawazimu ; sawa na walivyosema makuraishi kumwambia Mtume mtufu(s.a.w. w ) .

Shutuma hii ni ya kawaida kwa wale wanaoshindwa kujibu.

Na akakaripiwa.

Hapa Mwenyezi Mungu anaashiria yale aliyosema katika kauli yake:

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ ﴿١١٦﴾

“Wakasema: kama hutakoma ewe Nuh, bila shaka utapigwa mawe.” Juz.19 (26.116).

Walimkemea, wakamzuia kufikisha na wakamtisha kumpiga mawe na kumuua kama ataendelea.

Basi akamwomba Mola wake Mlezi: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!

Watu wa Nuh walipodhikika naye, naye akadhikika nao, alimkimbilia Mola wake na kusema kuwa nimemaliza mbinu zote na kazi yangu ya tabligh imefika ukomo, sasa iliyobaki ni amri yako kwa watu hawa makafiri waovu, basi waadhibu na uinusuru dini yako na mjumbe wako.

Kwa hakika Nuh hakuwaapiza watu wake ila baada ya kukata tamaa nao. Aliendelea kuwalingania kiasi cha miaka elfu kupungua hamsini bila ya mafanikio; kama ilivyoelezwa katika Juz.20 (29:14).

Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika. Na tukaipasua ardhi kwa chemchem.

Dua ya Nuh iliitikiwa na Mwenyezi Mungu, akawagharikisha kwa maji yanayotoka mbinguni na yanayotoka ardhini, yakakutana maji kwa jambo liliokadiriwa.

Yaani mvua na chemchem zikachanganyika ikawa ni bahari kubwa kila upande. Hakuna aliyesalimika isipokuwa aliyekuwa katika Jahazi (safina).

Tufani na maangamizi haya yalikuwa ni kwa amri iliyokadiriwa. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Kwa jambo lililokadiriwa,’ iko katika maana ya kauli yake:

وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا ﴿٣٨﴾

“Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kadari iliyokadiriwa.” Juz. 22 (33:38).

Na tukamchukua kwenye ile ya mbao na misumari

Aliyechukuliwa ni Nuh. Maana ni kuwa safina ilikuwa kama majahazi mengineyo, ilitengenezwa kwa mbao na misumari,lakini inakwenda kwa macho yetu, kwa hifadhi na kuilinda. Kwa hiyo ikaokoka na hatari; vinginevyo isingeweza kuhimili mikikimikiki ya tufani.

Ni malipo kwa alivyokuwa amekanushwa.

Neno ‘malipo’ linaashiria sababu zilizowajibisha tufani na kuangamia makafiri.

Na hakika tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anayekumbuka?

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliiacha habari ya safina iwe ni somo na mawaidha kwa yule anayewaidhika kwa mazingatio.

Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo?

Ni kweli kabisa tufani iliangamiza. Ama Nuh, mwenye kutoa bishara na maonyo, alikuwa ni mkweli katika aliyoyafikisha na kuyatolea maonyo.

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliiteremsha Qur’an kwa ajili ya ukumbusho na maonyo, na ameyafanya mepesi maana yake kufahamika ili wanufaike nayo, sio watajirike kwa matamshi yake, kuzifanyia dawa Aya zake, au kuzipotoa na kuziuza kwa thamani ndogo.

Basi je yupo anayekumbuka?

Je, watazingatia na kupata onyo, kwa yaliyokuja katika Qur’an, wale wanaoifanyia biashara dini na kuyabadilisha maneno sehemu zake kwa kufuata matamanio yao na malengo yao?

Kisa cha Nuh kimetangulia katika sura Hud, iliyo kwenye Juzuu ya 12, na nyinginezo.

كَذَّبَتْ عَادٌ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٨﴾

18. A’di walikadhibisha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُّسْتَمِرٍّ ﴿١٩﴾

19. Hakika tuliwapelekea upepo mkali katika siku ya Nuhsi iendeleayo.

تَنزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُّنقَعِرٍ ﴿٢٠﴾

20. Ukiwaangusha watu kama vigogo vya mitende vilivyong’olewa.

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٢١﴾

21. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٢٢﴾

22. Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ ﴿٢٣﴾

23. Thamudi waliwakadhibisha waonyaji.

فَقَالُوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٢٤﴾

24. Wakasema: Je tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!

أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ ﴿٢٥﴾

25. Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!

سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ ﴿٢٦﴾

26. Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.

إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ ﴿٢٧﴾

27. Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu. Basi watazame tu na usubiri.

وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ ﴿٢٨﴾

28. Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu itahudhuriwa.

فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ ﴿٢٩﴾

29. Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٠﴾

30. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ ﴿٣١﴾

31. Hakika tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyosagika yaliyo zizini.

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٣٢﴾

32. Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka, Basi je yupo anayekumbuka?

HUD NA SWALEH

Aya 18 – 32

MAANA

A’di walikadhibisha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

A’di ni kaumu ya Hud. Walimkadhibisha Nabii wao, Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa adhabu chungu. Akabainisha aina hii ya adhabu kwa kusema:

Hakika tuliwapelekea upepo mkali katika siku ya Nuhsi iendeleayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku ngumu na hatari. Uliendelea upepo wa adhabu siku hiyo mpaka ukawamaliza wote.

Ukiwaangusha watu kama vigogo vya mitende vilivyong’olewa.

Kimbunga kiliwang’oa kutoka sehemu zao na kuwatupa chini kama vigogo vya mtende vilivyong’olewa ardhini.

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelikariri hilo ili kusisitiza kutoa hadhari na maonyo.

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

Tazama Aya 17 ya sura hii tuliyo nayo, nuku yake na tafsiri yake ni moja tu.

Thamudi waliwakadhibisha waonyaji.

Thamud ni kaumu ya Swaleh. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta tamko la wengi pamoja na kuwa aliyekadhibishwa ni mmoja tu, Swaleh, kwa sababu kumkadhibisha Nabii mmoja ni sawa na kuwakadhibisha manabii wote, kutokana na kuwa risala ni moja na anayewatuma ni mmoja.

Wakasema: Je tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!

Swaleh ni katika sisi na miongoni mwetu, tumemjua tangu utotoni na ukubwani, vipi tumfuate; wala hakuna anayemfuata na kumsadiki isipokuwa mpotevu. Ndio lau angelikuwa na mali, watumishi na wajakazi, ingelifaa kumfuata.

Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu?

Haiwezekani kabisa! Itakuwaje na yeye ni mmoja wetu:

وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾

“Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.” Juz. 18 (23:34).

Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!

Kwa mantiki yao ni kuwa inatosha kuwa ni mwongo kwa vile anatokana nao na ni miongoni mwao. Kwa hiyo suala ni aina ya mtu na wala sio haki na msingi.

Hili si geni! Ndio mantiki ya watu wa chumo na vyeo, kila mahali na kila wakati na vile vile mantiki ya wajinga na waigaji.

Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi, kuwa je, ni Swaleh au wale ambao wamemkadhibisha.

Ndio! Watajua karibu kwamba wao ndio wazushi pale Mwenyezi Mungu atakapowapa mtihani wa ngamia, kisha wamchinje na wapate ghadhabu na adhabu ifedheheshayo.

Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu.

Ni mtihani wa kuwapambanua muovu na mwema.

Basi watazame tu na usubiri.

Ngoja kidogo ewe Swaleh na uvumilie maudhi yao, utaona vile watakavyopatwa na adhabu.

Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu itahudhuriwa na atakayehusika.

Wape habari kuwa maji yatagawanywa baina yao na ngamia. Siku moja itakuwa yao na na nyingine ya ngamia.

Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.

Hawakuwa radhi kugawana maji, ndio wakamwita yule muovu wao zaidi ili amchinje ngamia. Akaitikia yule muovu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Thamud walikadhibisha kwa sababu ya uovu wao. Alipofanya haraka muovu wao zaidi” (91:11-12). Basi walimchinja ngamia na adhabu ikawashukia.

Wametofautiana katika Makusudio ya neno ‘taatwa,’ tulilolifasiri kwa maana ya ‘akaja.’ Kuna waliosema kuwa Makusudio yake ni kuwa yule muovu alikunywa pombe kabla ya kuchinja. Wengine wakasema ni kuchukua ala ya kuchinjia. Sio mbali kuwa Makusudio yake hapa ni kuja bila ya kujali.

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo?

Yalikuwa ni ya kubomoa. Kukaririka ni msisitizo wa kuhadharisha na kuonya

Hakika tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyosagika yaliyo zizini.

Walipigwa na ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyovunjikavunjika yanayopeperushwa na upepo. Mwenye Al-Manar anasema: “Mara nyingi neno Hashim hutumiwa kwa majani yaliyovunjika vunjika.”

Majani haya anayakusanya mwenye zizi kwa ajili ya wanyama wake. Kwa hiyo basi wasifa huu umekuja kwa njia ya majazi, (kufananisha). sio uhakika

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

Huenda akanufaika na kukaririka huku mwenye kupotea njia. Kimetangulia kisa cha Hud na Swaleh katika Sura ya Hud.

21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ بِالنُّذُرِ ﴿٣٣﴾

33. Watu wa Lut waliwakadhibisha waonyaji.

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ نَّجَّيْنَاهُم بِسَحَرٍ ﴿٣٤﴾

34. Hakika tuliwapelekea kimbunga cha vijiwe. Isipokuwa wafuasi wa Lut. Tuliwaokoa karibu na alfajiri.

نِّعْمَةً مِّنْ عِندِنَا كَذَٰلِكَ نَجْزِي مَن شَكَرَ ﴿٣٥﴾

35. Kwa neema inayotoka kwetu. Hivyo ndivyo tunavyomlipa anayeshukuru.

وَلَقَدْ أَنذَرَهُم بَطْشَتَنَا فَتَمَارَوْا بِالنُّذُرِ ﴿٣٦﴾

36. Na hakika yeye aliwaonya mkamato wetu; lakini waliyatilia shaka hayo maonyo.

وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَن ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٧﴾

37. Na walimtaka awape wageni wake, tukayapofua macho yao. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ صَبَّحَهُم بُكْرَةً عَذَابٌ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣٨﴾

38. Na iliwafikia asubuhi adhabu ya kuendelea.

فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٩﴾

39. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٤٠﴾

40. Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ ﴿٤١﴾

41. Na waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.

كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٤٢﴾

42. Walizikadhibisha Ishara zetu zote, tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu, Mwenye uweza.

LUT

Aya 33 – 42

MAANA

Watu wa Lut waliwakadhibisha waonyaji, sawa na walivyokadhibisha watu wa Nuh, A’di Thamud na wengineo. Siri yao ni moja tu, mapambano ya haki na batili na uadilfu na dhulma. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha aina ya adhabu iliyowashukia watu wa Lut kwa kusema:

Hakika tuliwapelekea kimbunga cha vijiwe.

Yaani aliwatupia vijiwe vilivyochukuliwa na upepo. Vijiwe hivi ndivyo alivyovitaja Mwenyezi Mungu katika Juzuu hii tuliyonayo (51:33).

Isipokuwa wafuasi wa Lut. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.

Mwenyezi Mungu alimwokoa Lut na wale waliokuwa pamoja naye, pale alipowatoa usiku kutoka kwenye kijiji ambacho watu wake wamekuwa madhalimu.

Kwa neema inayotoka kwetu. Hivyo ndivyo tunavyomlipa anayeshukuru.

Mwenyezi Mungu alimwadhibu aliyeasi na akamneemesha aliyetii kwa kutumia misingi ya uadilifu. Lakini Razi anasema: “Hata kama wangeliaangamizwa watu wa Lut pia ingelikuwa ni uadilifu.”

Mwenyezi Mungu ndiye mkweli zaidi wa mazungumzo; naye ndiye aliyesema:

وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ صِدْقًا وَعَدْلًا لَّا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ ﴿١١٥﴾

“Na limetimia neno la Mola wako kwa ukweli na uadlifu. Hakuna wa kubadilisha neno lake.”

Juz. 8 (6:115).

Yaani uadilifu ni ule uliokwishatimia; vinginevyo ni dhulma.

Nahakika yeye aliwaonya mkamato wetu; lakini waliyatilia shaka hayo maonyo.

Lut aliwahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu, lakini wakatia shaka na wakadharau; bali hata walitoa vitisho na:

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا لُوطُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمُخْرَجِينَ ﴿١٦٧﴾

“Wakasema: kama hutakoma ewe Lut, bila shaka utakuwa miongoni mwa watakaotolewa.”

Juz. 19 (26:167).

Na walimtaka awape wageni wake.

Walisikia kuwa kuna wageni kwa Lut, kwa hiyo wakaenda kwake haraka na wakamwambia kwa ufidhuli: tupatie wageni wako tuwafanyie uchafu.

Tukayapofua macho yao.

Yaani Mwenyezi Mungu aliyatia upofu macho yao wasiweze kuwaona, kisha akawapelekea adhabu na akawaambia:Basi onjeni adhabu na maonyo yangu ambayo miliyatilia shaka na kuyadharau

Na iliwafikia asubuhi adhabu ya kuendelea.

Iliwafikia adhabu asubuhi, ikaendela hadi ikawamaliza wote.

Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

Haya ameyasema Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya adhabu ya kupofuka, kisha akayakariri baada ya adhabu ya mawe

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?

Ameikariri Aya hii, ambaye imetukuka hikima yake, mara nne: Ya kwanza ni baada ya kuashiria kisa cha Nuh, ya pili ni baada ya kisa cha Hud, ya tatu baada ya kisa cha Swaleh na ya nne ni hapa baada ya kisa cha Lut.

Lengo ni kupata mazingatio na mafunzo katika kila moja ya visa hivi vine. Kwa sababu ni tosha kabisa katika waadhi na ukumbusho.

Kisa cha Lut kimekwisha tangulia katika sura ya 11, katika Juz.12, na nyinginezo.

Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.

Mfano wake ni Aya isemayo:

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ ﴿١٠٣﴾

“Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Firauni na wakuu wake” Juz. 9 (7:103)

Walizikadhibisha Ishara zetu zote; nazo zilikuwa tisa; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَىٰ تِسْعَ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ ﴿١٠١﴾

“Hakika tulimpa Musa Ishara tisa zilizo wazi.” Juz. 15 (17:101).

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezitaja tano pale aliposema:

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ ﴿١٣٣﴾

“Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, Juz. 9 (7:133).

Nyingine nne amezitaja katika Aya mbalimbali; nazo ni mkono, fimbo, kufunguka kifundo katika ulimi wa Musa na kupasuka bahari.

Tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu Mwenye uweza.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwangamiza Firauni na watu wake majini na hapo mwanzo alikuwa akiwaambia watu wake: Mimi ndiye Mola wenu mkuu. Basi Mwenyezi Mungu akamuonjesha adhabu ya hizaya ya dunia na adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi.

أَكُفَّارُكُمْ خَيْرٌ مِّنْ أُولَـٰئِكُمْ أَمْ لَكُم بَرَاءَةٌ فِي الزُّبُرِ ﴿٤٣﴾

43. Je, Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi mtaachwa?

أَمْ يَقُولُونَ نَحْنُ جَمِيعٌ مُّنتَصِرٌ ﴿٤٤﴾

44. Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda?

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ ﴿٤٥﴾

45. Wingi wao huu utashindwa, na watasukumwa nyuma.

بَلِ السَّاعَةُ مَوْعِدُهُمْ وَالسَّاعَةُ أَدْهَىٰ وَأَمَرُّ ﴿٤٦﴾

46. Bali Saa ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito sana na chungu zaidi.

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٤٧﴾

47. Hakika wakosefu wamo katika upotofu na mioto.

يَوْمَ يُسْحَبُونَ فِي النَّارِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ ذُوقُوا مَسَّ سَقَرَ ﴿٤٨﴾

48. Siku watakapokokotwa Motoni kifudifudi: Onjeni mguso wa Jahannamu!

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾

49. Kwa hakika tumekiumba kila kitu kwa kipimo.

وَمَا أَمْرُنَا إِلَّا وَاحِدَةٌ كَلَمْحٍ بِالْبَصَرِ ﴿٥٠﴾

50. Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.

وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا أَشْيَاعَكُمْ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٥١﴾

51. Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Je, yupo anayekumbuka?

وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ ﴿٥٢﴾

52. Na kila kitu walichokifanya kimo vitabuni.

وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُّسْتَطَرٌ ﴿٥٣﴾

53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ ﴿٥٤﴾

54. Hakika wenye takua watakuwa katika Mabustani na mito.

فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِندَ مَلِيكٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٥٥﴾

55. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.

KILA KITU TUMEKIUMBA KWA KIPIMO

Aya 43 – 55

MAANA

Je, Makafiri wenu ni bora kuliko hao?

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w. w ) . Hao ni watu wa uma zili- zotangulia walioangamia kwa sababu ya kufuru na inadi yao. Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu ametaja aina za adhabu zilizowapata.

Maana ni kuwa nyinyi sio bora zaidi ya tuliowaangamiza; bali nyinyi ni waovu zaidi na wenye uasi zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Je, mmejiaminisha yasiwapate yale yaliyowapata wenzenuau yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi mtaachwa? Je, Mwenyezi Mungu ameteremsha katika kitabu chochote miongoni mwa vitabu vyake kuwa nyinyi mtasalimika na adhabu yake?

Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda?

Hivi nyinyi mnadai kwa ni kundi kubwa lilisiloshindwa?

Wingi wao huu utashindwa, na watasukumwa nyuma.

Iliposhuka Aya hii washirikina ndio waliokuwa na nguvu, kwa vile walikuwa wengi. Ama waislamu walikuwa ni mmoja mmoja wadhaifu. Mshirikina yeyote alikuwa na uwezo wa kumuudhi Mwislamu.

Lakini hazikupita siku na mambo yakageuka, washirikina wakasukumwa nyuma, Uislamu na waislamu wakawa juu, na ikabainika kwa ukaribu na umbali kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Wingi wao huu utashindwa,’ kuwa ni kweli. Hii peke yake ni ubainifu mkataa kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anatamka kupitia kwenye ulimi wa Mtume wake mtukufu(s.a.w. w ) .

Bali Saa ya Kiyamandio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito sana na chungu zaidi.

Neno ‘yao,’ linawarudia wote, kuanzia kaumu ya Nuh mpaka makafiri wa Kiarabu ambao walimkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) . Maana ni kuwa kila adhabu iliyowapata makafiri duniani, si chochote kulinganisha na adhabu ya Akhera. Kila balaa isyokuwa Moto hiyo ni salama.

Hakika wakosefu wamo katika upotofu na mioto. Siku watakapokokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu!

Hii ni tafsiri na ubainifu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na Saa hiyo ni nzito sana na chungu zaidi.’ Watu wa motoni hawatatosheka na vituko vyake tu, bali Malaika wa adhabu watawahamishia kwenye adhabu mbalimbali; kama vile kuvutwa kifudifudi, makomeo ya chuma na mengineyo yasiyoelezeka.

Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.

Aya ya pili inasema:

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴿٢﴾

“Na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo.” Juz. 18 (25:2).

Ya tatu inasema:

وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾

“Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.” Juz. 13 (13:8).

Ya nne:

الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾ وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ ﴿٣﴾

“Ambaye ameumba akalinganisha sawa na Ambaye amekadiria na akaongoza.” (87:2-3).

Na kuna Aya nyinginezo nyingi zinazofamisha kuwa hakuna kitu chochte kilichopo ila kimekadiriwa kwa kipimo maalum na sifa zisizozidi wala kupungua vile inavyotakikana na kwamba kila kilichomo ndani yake kitakuwa kimepangwa kwa mpangilio mzuri na kuweka mahali panapolingana na wadhifa na umuhimu wake.

Tukitafuta kilichosababisha hivyo kinachokubalika kiakili, hatupati isipokuwa utashi wa Mwenyezi Mungu ambao uko nyuma ya kila kitu. Anasema Conte: “Maumbile ni kama kazi ya usanii. Kuitolea dalili ya chimbuko lake ni sawa na kutolea dalili athari pale ilipotokea.”

Unaweza kuuliza : Hiwezekani kuwa nidhamu hii imetokana na kazi ya sadfa?

Jibu : Sadfa kama lilivyo jina lake, haiwezekani kukaririka. Kuyafasiri matukio kwa sadfa, itakuwa ni kukimbia. Hayo ni kwa hukumu ya akili na uhalisia. Ndio maana wakasema maulama kuwa, hakimbilii kwenye sadfa ila mwenye kushindwa.

Zaidi ya hayo, kama nadharia hii ingelikuwa sahihi basi ilimu isingelikuwa na maana kabisa. Kwa sababu ilimu ina misingi maalumu; vinginevyo itakuwa si ilimu. Kinyume na sadfa ambayo huwa haina maaudhui maalumu, na kama itakuwa na maaudhui maalum, basi itakuwa nayo siyo sadfa.

Ikiwa sadfa ni batili, basi madhehebu ya wanaosema kuwa maada ndio asilili ya kila kitu nayo yatakuwa ni batili.

Ni nani mwenye akili anayeweza kukubali kuwa ulimwengu umepatikana kwa sadfa, kila kilichomo ndani yake ikiwemo kanunui na nidhamu imepatikana kwa sadfa na maada nayo imepatikana kwa sadfa? Hapa ndio tunakuta tafsiri ya kauli ya msahiri: “Kila kitu ni ishara kwake kutambulisha umoja wake.”

Pia tafsiri ya aliyesema: “Uwezekano si zaidi ya ulivyo.” Yaani kila kitu kimewekwa mahali panaponasibiana nacho, lau kitaepuka hata kiasi cha unywele basi itabainika kasoro na upungufu.

Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.

Hiki ni kinaya cha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) akitaka kukileta kitu ni kiasi cha kutaka tu, wala hahitajii wakati hata ule wa kupepesa jicho au chini yake. Ametaja kupepesa jicho kwa kiasi cha kuleta karibu maana tu.

Kwa maneno ya wanafalsafa ni kuwa mnasaba wa matakwa yake Mwenyezi Mungu kwa anachokitaka ni kama mnasaba wa kupatikana kinachopatikana.

Na bila ya shaka tumekwishawaangamiza wenzenu. Je, yupo anayekumbuka?

Katika wakati uliopita walikuweko wenzenu waliojiona kama mnavyojiona nyinyi enyi washirikina wa kiarabu; wakawakadhibisha mitume wao kama nyinyi mnavyomkadhibisha Muhammad (s.a.w.), Mwenyezi Mungu akawapondaponda kabisa. Basi chukuueni somo kwao kabla ya kuchukuliwa somo nyinyi.

Na kila kitu walichokifanya kimo vitabuni. Na kila kidogo na kikub- wa kimeandikwa.

Si kauli wala kitendo, kiwe kidogo au kikubwa kitakuwa kimethibitishwa, kwa aliyekitenda, katika ilimu ya Mwenyezi Mungu. Mwenye faida ni yule anayejihisabu kabla ya kuhisabiwa.

Hakika wenye takua watakuwa katika Mabustani na mito. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.

Wenye takua ni wale waliojiangalia na wasijiingize kwenye maangamizi kwa kumuasi Mwenyezi Mungu. Wakajihisabu kwa kila dogo na kubwa, wakawa ni wenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu.

MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA NNE: SURAT AL-QAMAR