23
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
سَنَفْرُغُ لَكُمْ أَيُّهَ الثَّقَلَانِ ﴿٣١﴾
31. Tutawakusudia enyi wazito wawili.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٢﴾
32. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ ﴿٣٣﴾
33. Enyi makundi ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni! Hamtapenya ila kwa madaraka.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٤﴾
34. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
يُرْسَلُ عَلَيْكُمَا شُوَاظٌ مِّن نَّارٍ وَنُحَاسٌ فَلَا تَنتَصِرَانِ ﴿٣٥﴾
35. Mtapelekewa muwako wa moto na ufukizo; wala hamtanusurika.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٦﴾
36. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فَإِذَا انشَقَّتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ وَرْدَةً كَالدِّهَانِ ﴿٣٧﴾
37. Itakapopasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٨﴾
38. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُسْأَلُ عَن ذَنبِهِ إِنسٌ وَلَا جَانٌّ ﴿٣٩﴾
39. Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٠﴾
40. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ ﴿٤١﴾
41. Watajulikana wakosefu kwa alama zao, basi watakamatwa kwa nywele zao za utosi na kwa miguu.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٢﴾
42. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي يُكَذِّبُ بِهَا الْمُجْرِمُونَ ﴿٤٣﴾
43. Hii ndiyo Jahannamu ambayo wakosefu wakiikadhibisha.
يَطُوفُونَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ حَمِيمٍ آنٍ ﴿٤٤﴾
44. Watakuwa wakizunguka baina ya hiyo na maji ya moto yanayochemka.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٥﴾
45. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
HAMTAPENYA ILA KWA MADARAKA
Aya 31 – 45
MAANA
Tutawakusudia enyi wazito wawili.
Makusudio ya kuwakusudia hapa ni kuwahisabu, na hicho ni kiaga kwa kila mwenye kufanya dhambi katika wazito wawili ambao ni watu na majini.
Katika Bahru Al-muhit cha Abu hayan Al-andalusi imeelezwa: “Wameitwa watu na majini kuwa ni wazito kwa sababu ya uzito wao juu ya ardhi. Katika Hadith limetumika neno hilo pale iliposemwa: ‘Hakika mimi ninawachia vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, Ahlu bayt wangu,’ vimeitwa hivyo kwa sababu ya utukufu wao.”
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ni uweza wake wa kufufua na kuhisabu au ni nini? Hisabu na malipo ni katika neema kubwa kwa viumbe; vinginevyo mwenye kudhulumiwa angelikuwa na hali mbaya zaidi kuliko aliyedhulumu.
Enyi makundi ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni! Hamtapenya ila kwa madaraka.
Kabisa hakuna kuokoka na kukutana na Mwenyezi Mungu ila kwa tawfiki inayotoka kwake kwenye toba na kujing’oa kwenye dhambi.
Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Ila kwa madaraka.’ Kwa sababu toba ni ngome inayomkinga mwenye kutubia kwa ikhlasi na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ni uweza wake kwenu au ni hadhari yake au mengine?
Mtapelekewa muwako wa moto na ufukizo; wala hamtanusurika.
Wamesema kuwa muwako hapa, lililofasiriwa kutokana na neno shuwadh, ni muwako wa moto bila ya moshi. Na ufukizo, lililotokana na nuhas ni moshi bila ya moto. Vyovyote iwavyo, maana yanayopatikana kutokana na Aya ni kuashiria vituko vya kiyama na machngu yake, na kwamba mkosefu hataokoka na machungu na vituko hivi kwa uombezi wala usaidizi.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ni adhabu ya mwenye kupituka mipaka au ni nini?
Itakapopasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta.
Mbingu na vilivyomo ndani yake miongoni mwa sayari vitayeyuka kama yanavyoyeyuka mafuta kwenye moto na rangi ya myeyuko huu itakuwa kama wekundu wa waridi.
Lengo la kufananisha huku na mengineyo yaliyokuja katika Aya nyingine ni kuashiria kuharibika ulimwengu na kubomoka kwake Siku ya Kiyama.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ninani dhalimu mkubwa na muovu zaidi kuliko yule mwenye kukadhibisha ukweli na akaikalia juu haki?
Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.
Tukiunganisha Aya hii na ile isemayo: “Na wasimamisheni. Hakika hao wataulizwa” Juz. 23 (37:24), inatubainikia kuwa Siku ya Kiyama kuna sehemu watu wataulizwa yale waliyokuwa wakiyafanya na sehemu nyingine hakutakuwa na maswali wala majibu, bali ni kungoja maswali na hisabu. Tazama Juz. 22 (36:55-68).
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ni kwa kusimama kuonyeshwa hisabu au ni kusimama kuingoja? Yote hayo ni dhiki na uchungu, hilo halina shaka, lakini malipo ni katika neema itokayo kwa Mwenyezi Mungu kwa vileWatajulikana wakosefu kwa alama zao, basi watakamatwa kwa nywele zao za utosi na kwa miguu.
Yaani wakosefu watakuwa na alama za kuwatambulisha na kuwapambanua na watu wema, zaidi ya hayo Malaika wa adhabu watawafunga utosi na miguu pamoja na kuwatupa Motoni kifudifudi.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Katika mawaidha na makanyo?
Hii ndiyo Jahannamu ambayo wakosefu wakiikadhibisha.
Hili ni jawabu sahihi zaidi kwa mwenye kukadhibisha adhabu ya Mwenyezi Mungu, nalo ni kutumbukizwa ndani yake:
وَنَقُولُ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿٤٢﴾
“Na tutawaambia wale ambao wamedhulumu: onjeni adhabu ya moto wa Jahannam mliokuwa mkiukadhibisha.” Juz. 22 (34:42).
Watakuwa wakizunguka baina ya hiyo na maji ya moto yanayochemka.
Hiyo ni Jahannam. Maji ya moto ni kinywaji.
Kukisifia kuwa kinachemka ni kuonyesha kuwa kinywaji hiki kitafikia kiwango cha joto kiasi ambacho mnywaji atahisi kama kwamba kiko motoni.
Maana ni kuwa hakuna kazi kwa wakosefu isipokuwa kuzunguka baina ya Moto au kunywa kinywaji cha Moto.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, ni adhabu ya Moto au ni kinywaji cha Moto? Yote hayo mawili ni katika neema ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu ni hukumu ya uadlifu na upanga wa haki.
وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ ﴿٤٦﴾
46. Na mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake atapata Bustani mbili.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٧﴾
47. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
ذَوَاتَا أَفْنَانٍ ﴿٤٨﴾
48. Zenye matawi yaliyotanda.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٩﴾
49. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِمَا عَيْنَانِ تَجْرِيَانِ ﴿٥٠﴾
50. Ndani yake zimo chemchem mbili zinazopita.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥١﴾
51. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِمَا مِن كُلِّ فَاكِهَةٍ زَوْجَانِ ﴿٥٢﴾
52. Humo katika kila matunda zimo namna mbili.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٣﴾
53. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ فُرُشٍ بَطَائِنُهَا مِنْ إِسْتَبْرَقٍ وَجَنَى الْجَنَّتَيْنِ دَانٍ ﴿٥٤﴾
54. Wakiegemea matandiko yenye vitambaa vya hariri nzito; na matunda ya Bustani hizo
yapo karibu.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٥﴾
55. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِنَّ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٥٦﴾
56. Humo watakuwamo wanawake watulizao macho; hajawagusa mtu kabla yao wala jini.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٧﴾
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
كَأَنَّهُنَّ الْيَاقُوتُ وَالْمَرْجَانُ ﴿٥٨﴾
58. Kama kwamba wao ni yakuti na marijani.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٩﴾
59. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ ﴿٦٠﴾
60. Hakuna malipo ya ihsani ila ihsani?
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦١﴾
61. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
وَمِن دُونِهِمَا جَنَّتَانِ ﴿٦٢﴾
62. Zaidi ya hizo mbili ziko Bustani mbili nyingine.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٣﴾
63. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
مُدْهَامَّتَانِ ﴿٦٤﴾
64. Za kijani kibivu.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٥﴾
65. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِمَا عَيْنَانِ نَضَّاخَتَانِ ﴿٦٦﴾
66. Mna chemchem mbili zinazofurika.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٧﴾
67. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِمَا فَاكِهَةٌ وَنَخْلٌ وَرُمَّانٌ ﴿٦٨﴾
68. Mna humo matunda, na mitende na komamanga.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٩﴾
69. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
فِيهِنَّ خَيْرَاتٌ حِسَانٌ ﴿٧٠﴾
70. Wamo wanawake wema wazuri.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧١﴾
71. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
حُورٌ مَّقْصُورَاتٌ فِي الْخِيَامِ ﴿٧٢﴾
72. Wanawake wazuri wanaotawishwa katika mahema.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٣﴾
73. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٧٤﴾
74. Hajawagusa mtu kabla yao wala jini.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٥﴾
75. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ رَفْرَفٍ خُضْرٍ وَعَبْقَرِيٍّ حِسَانٍ ﴿٧٦﴾
76. Wameegemea juu ya matakia ya kijani na mazulia mazuri.
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٧﴾
77. Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
تَبَارَكَ اسْمُ رَبِّكَ ذِي الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٧٨﴾
78. Limekuwa na baraka jina la Mola wako, Mwenye utukufu na ukarimu.
HAKUNA MALIPO YA HISANI ILA HISANI
Aya 46 – 78
MAANA
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuhofisha na kumpa kiaga yule mwenye kupetuka mipaka na akafanya uovu, sasa anamtuliza yule mwenye takua na akalisadikisha tamko jema, na kumwahidi Pepo iliyo na sifa kubwa kwa chakula chake, kinywaji chake, huri laini wake, miti yake, mito yake, samani zake na vipambo vyake kwa namna ambayo haina mfano wala hatuijui.
Nyingi katika Aya hizi ziko wazi hazihitajii tafsiri; mbali ya kuwa ni kukariri yaliyotangulia. Kwa hiyo tutafupiliza tafsiri ila kukiwa na haja ya kurefusha.
Na mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake atapata Bustani mbili.
Makusudio ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuwa yeye ni msimamizi wa kila nafsi akijua siri yake na dhahiri yake. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far Assadiq
amesema:“Mwenye kujua kuwa Mwenyezi Mungu anamuona na kusikia anayoyasema, na likamzuia hilo kufanya maovu, atakuwa ameogopa kusimama mbele ya Mola wake.”
Wafasiri wana kauli kadhaa kuhusu maana ya Bustani mbili. Iliyo karibu zaidi na ufahamu ni bustani katika Pepo, kwa sababu neno Pepo limefasiriwa kutoka neno la kiarabu janna lenye maana ya bustani. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika wasifu wakezenye matawi yaliyotanda
; yaani matawi yenye majani na matunda.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Je, nyinyi majini na watu mnakanusha neema hizi tulizozitaja. Kila swali linalokuja kwa tamko hili, basi inayoulizwa ni neema aliyoitaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) kabla ya swali; kwa hiyo hakuna haja ya kutaja na kubainisha kinachouliziwa.
Ndani yake zimo chemchem mbili zinazopita.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Maana yako wazi, lakini pamoja na hayo mfasiri mmoja amesema: kupita maana yake ni kutawanyika. Mwingine akasema: yaani zinapita baina ya miti. Wa tatu akasema chemchem moja inaitwa tasnim na nyingine inaitwa salsabil.
Wanne naye akasema: zinapita ni kwa ambaye macho yake yanatiririka machozi kwa kumhofia Mwenyezi Mungu.
Hakuna chimbuko la tafsiri hizi isipokuwa hamu ya kusema tu. Kwa nini wana hamu ya kusema? Ni kwa vile tu wao ni wafasiri.
Humo katika kila matunda zimo namna mbili.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Tunda moja linaweza kuwa na aina mbili; kama zabibu kavu na mbichi, tende mbichi na za kuiva
na matofaha ya tamu na yasiyokuwa tamu.
Wakiegemea matandiko yenye vitambaa vya hariri nzito; na matunda ya Bustani hizo yapo karibu.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Mfano wake ni Aya isemayo: “Vishada vyake viko karibu.” (69:23).
Humo watakuwamo wanawake watulizao macho; hajawagusa mtu kabla yao wala jini.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Humo, ni humo Peponi; na kabla yao, ni kabla ya hao waume wa Hurilaini. Maana ni kuwa Hurilaini hawataangalia isipokuwa waume zao, pia watakuwa ni bikra kama walivyumbwa.
Kama kwamba wao ni yakuti na marijani kwa urembo na uzuri.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
UJIRA NI HAKI NA ZIADA NI FADHILA
Hakuna malipo ya ihsani ila ihsani?
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Kila wanaloliona watu kuwa ni hisani au wema basi kwa Mwenyezi ni hivyo hivyo, kwa Sharti yakuwa lisikataliwe na akili iliyo salama wala kukatazwa na sharia; kama ilivyokuwa wakati wa jahilia, walikuwa wakiona ni wema na jambo zuri kuabudu masanamu na kuwadhulumu wanyonge, hasa wanawake.
Mpaka leo hii bado kuna mamilioni ya watu wanaoona ni hisani kuabudu masanamu na watu wakimfanya Mwenyezi Mungu ana watoto na washirika. Hakuna mwenye shaka kuwa hii ni desturi mbaya sana.
Ikiwa mtu atafanya jambo na watu wakaliona ni zuri na lisikataliwe na akili na sharia, basi mwenye kuilifanya anastahiki ujira na karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu na atamzidisha ziada ya anayostahiki:
لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ﴿٢٦﴾
“Kwa wafanyao wema ni wema na ziyada.” Juz. 11(10:26).
Kundi katika wanatiolojia wamesema kuwa thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa tendo la wajibu ni fadhila sio malipo wala haki. Wengine wakasema, bali ni malipo na haki.
Imam Ali
anasema:“Ingelikuwa kuna yeyote mwenye haki lakini wengine hawana haki juu yake, ingelikuwa hivyo kwa Mwenyezi Mungu tu peke yake, sio kwa viumbe wake, kutokana na uwezo wake kwa waja wake na kwa uadilifu kwa kila linalopita katika hukumu yake.
Lakini amejaalia haki yake kwa waja wake ni kumtii na akajalia malipo yao yawe juu yake, kwa kuwaongezea malipo kwa fadhila na kupanua ile ziyada kwa wanaostahiki.”
Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu ana haki yake naye anayo haki ya wengine. Hakuna linalofahamisha hivyo kuliko kauli hiyo ya Imama Ali
.
Kwa hiyo haki ya Mwenyezi Mungu ni kutiiwa na waja wake na haki ya watiifu kwake, Yeye ambaye imetukuka hikima yake, ni malipo kulingana na matendo. Zaidi ya hayo ni fadhila kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Hii inaafikiana na hukumu ya kiakili na maumbile, kwani watu wote wanaona ni fadhila na hisani ukimlipa aliyekufanyia kazi zaidi ya malipo yake na stahiki yake. Lakini ukimlipa bila ya ziada wala upungufu basi wewe ni mtekelezaji, lakini sio mhisani wala makarimu.
Zaidi ya hayo Uislamu, kwa misingi yake na matawi yake, unajengeka kwenye fikra ya uadilifu. Na ujira wa kazi ni haki ya wajibu kuitekeleza katika mantiki ya uadilifu na hukumu yake.
Zaidi ya hizo mbili ziko Bustani mbili nyingine.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani katika Pepo kuna kuzidiana kulingana na imani za waumini na kutofautiana na matendo yao. Haya ndiyo yanayopelekea mantiki ya haki na misingi ya uadilifu. Kwa hiyo inatubainikia kuwa Bustani mbili zilizotajwa mwanzo ni za wale wenye imani ya nguvu, wenye kazi iliyo na manufaa zaidi na wenye juhudi zaidi ya wengine, na hizi mbili zilizotajwa sasa ni za walio chini ya hapo.
Za kijani kibivu.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani rangi yake inaeleka weusi kutokana na kuiva sana.
Mna chemchem mbili zinazofurika.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani zinachimbuka maji. Ama zile zilizotajwa mwanzo maji yake yanapita. Kama ambavyo bustani mbili zilozitajwa mwanzo ni tofauti na zilizotajwa baadae vile vile chemchem.
Mna humo matunda, na mitende na komamanga.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa tende na komamanga sio matunda ndio maana kukawa na maunganisho. Razi anasema kuwa katika matunda kuna ya Ardhini, kama vile matango n.k. na kuna yaliyo kwenye miti, kama vile tende n.k. Kwa hiyo kuunganisha kunakuwa kwa mahususi kwenye jumla.
Wamo wanawake wema wazuri.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani wazuri wa umbo na tabia.
Wanawake wazuri wanaotawishwa katika mahema.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Mwenye Majmaul’bayan anasema maana yake ni kutwawishwa kwenye makuba wanayojengewa wanawake wanaotawa nyumbani. Wengine wakasema kuwa makusudio ni mahema hasa; kwani yako mengine yanashinda majumba kwa uzuri. Kauli hii ndio iliyo karibu na dhahiri ya Aya.
Hajawagusa mtu kabla yao wala jini.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani bado ni bikra. Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 56 ya Sura hii. Wameegemea juu ya matakia ya kijani na mazulia mazuri.
Basi ni ipi katika neema ya Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Yaani kwenye mito ya kuegemea.
limekuwa na baraka jina la Mola wako, Mwenye utukufu na ukarimu.
Mwenyezi Mungu ana utukufu na ukubwa, ikiwa ni pamoja na ukarimu na fadhila kwa viumbe wake. Tazama kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu na mtu na Ibn A-arabi’.
Katika Aya 27 ya sura hii tuliyo nayo.
MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA TANO: SURAT AR-RAHMAN