TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 28300
Pakua: 3893


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 28300 / Pakua: 3893
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Ya Hamsini Na Sita: Surat Al-Waaqia. Imeshuka Makka. Ina Aya 96.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

إِذَا وَقَعَتِ الْوَاقِعَةُ ﴿١﴾

1. Litakapotukia hilo Tukio.

لَيْسَ لِوَقْعَتِهَا كَاذِبَةٌ ﴿٢﴾

2. Hapana cha kukanusha kutukia kwake.

خَافِضَةٌ رَّافِعَةٌ ﴿٣﴾

3. Literemshalo linyanyualo.

ذَا رُجَّتِ الْأَرْضُ رَجًّا ﴿٤﴾

4. Itakapotikiswa ardhi kwa mtikiso,

وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا ﴿٥﴾

5. Na milima itaposagwasagwa,

فَكَانَتْ هَبَاءً مُّنبَثًّا ﴿٦﴾

6. Iwe mavumbi yanayopeperushwa.

وَكُنتُمْ أَزْوَاجًا ثَلَاثَةً ﴿٧﴾

7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu.

فَأَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ مَا أَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ ﴿٨﴾

8. Basi watakuwepo wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

وَأَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ مَا أَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ ﴿٩﴾

9. Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto?

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾

10. Na waliotangulia ndio waliotangulia.

أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾

11. Hao ndio watakaokaribishwa

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿١٢﴾

12. Katika Bustani zenye neema

ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾

13. Fungu kubwa katika wa mwanzo,

وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿١٤﴾

14. Na wachache katika wa mwisho.

عَلَىٰ سُرُرٍ مَّوْضُونَةٍ ﴿١٥﴾

15. Watakuwa juu ya viti vya fahari vilivyodariziwa.

مُّتَّكِئِينَ عَلَيْهَا مُتَقَابِلِينَ ﴿١٦﴾

16. Wakiviegemea wakielekeana.

يَطُوفُ عَلَيْهِمْ وِلْدَانٌ مُّخَلَّدُونَ ﴿١٧﴾

17. Watawazunguukia vijana wa milele.

بِأَكْوَابٍ وَأَبَارِيقَ وَكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ ﴿١٨﴾

18. Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.

لَّا يُصَدَّعُونَ عَنْهَا وَلَا يُنزِفُونَ ﴿١٩﴾

19. Hawataumwa kichwa kwa hivyo wala hawataleweshwa.

وَفَاكِهَةٍ مِّمَّا يَتَخَيَّرُونَ ﴿٢٠﴾

20. Na matunda wayapendayo,

وَلَحْمِ طَيْرٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢١﴾

21. Na nyama ya ndege kama wanavyotamani.

وَحُورٌ عِينٌ ﴿٢٢﴾

22. Na Mahurulaini.

كَأَمْثَالِ اللُّؤْلُؤِ الْمَكْنُونِ ﴿٢٣﴾

23. Walio kama mfano wa lulu zilizohifadhiwa.

جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

24. Ni malipo kwa waliyokuwa wakiyatenda.

لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا تَأْثِيمًا ﴿٢٥﴾

25. Humo hawatasikia upuzi wala maneno ya dhambi.

إِلَّا قِيلًا سَلَامًا سَلَامًا ﴿٢٦﴾

26. Isipokuwa maneno ya Salama, Salama.

LITAKAPOTUKIA TUKIO

Aya 1 – 26

MAANA

Litakapotukia hilo Tukio. Hapana cha kukanusha kutukia kwake.

Makusudio ya tukio hapa ni Kiyama. Katika maisha ya duniani kuna wanaoisadiki Akhera na wanaoikanusha. Lakini ikashafikia wakati wake na kutekelezewa kila nafsi iliyoyachuma, hapo ndio wataikubali na kukiri.

Kwanini? Kwa vile tukio lake ndiloLiteremshalo linyanyualo . Linawainamisha wakosefu na kuwainua wenye takua.

Itakapotikiswa ardhi kwa mtikiso, Na milima itaposagwasagwa, Iwe mavumbi yanayopeperushwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria kuharibika ulimwengu. Ardhi itavunjwavunjwa na tetemeko na majabali yatageuka vumbi.

Na nyinyi mtakuwa namna tatu:

Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawakusanya watu na kuwafanya makundi matatu:

Basi watakuwepo wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

Ni ambao kesho watapewa vitabu vyao kwa mikono yao ya kuume. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

“Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kuume, atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua kuwa nitapokea hisabu yangu.

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ ﴿١٩﴾ إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ ﴿٢٠﴾ فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ ﴿٢١﴾

Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhiwa.” (69:19-21).

Kundi, hata kama ni katika watakaookoka, lakini sio kama kundi la tatu.

Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto?

Hawa ni wale watakopewa vitabu vyao kwa mikono yao ya kushoto. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ ﴿٢٥﴾ وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ ﴿٢٦﴾ يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ ﴿٢٧﴾

“Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, atasema: laiti nisingelipewa kitabu changu wala nisijue nini hisabu yangu. Laiti mauti yangelikuwa ni ya kumaliza.”

(69:25-27).

Na waliotangulia ndio waliotangulia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema waliotangulia, lakini hakubainisha wametangulia kwenye jambo gani; hata hivyo amebainisha mahali pengine: “Hakika wale ambao humwogopa Mola wao wanamnyenyekea. Na wale ambao wanaamini ishara za Mola wao. Na wale ambao hawamshirikishi Mola wao.

Na wale ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao. Hao ndio wanokimbilia kwenye kheri na ndio watakaotangulia kuzifikia.” Juz. 18 (23: 57-61).

Kwa hiyo basi waliotangulia ni wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu peke yake bila ya kuwa na mshirika, na wakaamini siku ya mwisho, wala wasipuuze kumtii kwa kuhofia ghadhabu na adhabu yake, na wakawa wanajitolea mhanga ulio ghali kwa kutaka radhi na thawabu zake.

Hao ndio watakaokaribishwa katika Bustani zenye neema.

Wana hadhi kubwa ya kukaribishwa kwenye utukufu wake mtukuka na wana fungu kubwa la neema yake.

Fungu kubwa katika wa mwanzo, Na wachache katika wa mwisho.

Wametofautiana wafasiri kuwa ni nani hao wa mwanzo, wa mwisho na wachache? Kuna waliosema kuwa makusudio ya wa kwanza ni walioami- ni na wakatangulia kwenye heri kabla ya Muhammad(s.a.w. w ) . Wengine wakasema wote wa kwanza na wa mwisho ni katika umma wa Muhammad(s.a.w. w ) .

Tuonavyo sisi ni kwamba wa kwanza ni ishara ya zama za uislamu wa dhahabu, pale ulipokuwa na nguvu na madaraka na waislamu wakawa wanauamini kwa kauli na vitendo wakiupigania kwa roho na mali. Na wengine ni ishara ya waumini wachache katika zama za baadae. Kauli hii inasadikishwa na kauli ya Imam Ali(a.s ) :

“Zitakuja zama kwa watu haitabakia Qur’an isipokuwa maandishi tu, na Uislamu isipokuwa jina lake. Misikiti yao itajengwa vizuri, lakini itakuwa mibovu ya uongofu. Wakazi wake na waamirishaji wake ndio watakuwa washari zaidi katika watu wa ardhi.

Kutoka kwao itatokea fitna na kwao itaishia hatia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Ninaapa nitawapelekea hawa fitna nimwache mpole hana la kufanya.”

Watakuwa juu ya viti vya fahari vilivyodariziwa.

Vitakuwa vimefuwa kulingana na mili ya watu wa Peponi iliyo myororo na nyuso zenye kunyinyirika.

Wakiviegemea wakielekeana.

Hawana shughuli wala fikra ya familia.

Watawazunguukia vijana wa milele Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.

Vikombe vyenye asali safi, pombe ya ladha kwa wanywaji, mvinyo wenye kusiliwa. Katika kuyapata basi nawashindane wenye kushindana.

Hawataumwa kichwa kwa hivyo wala hawataleweshwa.

Vinywaji hivyo havimwondolei mnywaji akili yake wala hataumwa na kichwa.

Na matunda wayapendayo, na nyama ya ndege kama wanavyotamani. Na Mahurulaini, walio kama mfano wa lulu zilizohifadhiwa.

Kinywaji safi, nyama freshi, matunda aina kwa aina, wanawake wazuri, matandiko na viti. Ni raha na utulivu. Yote hayoni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda ya heri na masilahi ya umma bila ya riya wala kupigiwa ngoma au nzumari.

Humo hawatasikia upuzi wala maneno ya dhambi. Isipokuwa maneno ya Salama, Salama.

Watasikia wapi upuzi na porojo na peponi hakuna matamshi isipokuwa heri tu. Yote haya ni ya wale waliotangulia. Ama watu wa kuume Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha fungu lao, katika Aya zifuatazo.

وَأَصْحَابُ الْيَمِينِ مَا أَصْحَابُ الْيَمِينِ ﴿٢٧﴾

27. Na wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

فِي سِدْرٍ مَّخْضُودٍ ﴿٢٨﴾

28. Katika mikunazi isiyo na miba,

وَطَلْحٍ مَّنضُودٍ ﴿٢٩﴾

29. Na migomba iliyopangiliwa,

وَظِلٍّ مَّمْدُودٍ ﴿٣٠﴾

30. Na kivuli kilichotanda,

وَمَاءٍ مَّسْكُوبٍ ﴿٣١﴾

31. Na maji yanayomiminika,

وَفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ ﴿٣٢﴾

32. Na matunda mengi;

لَّا مَقْطُوعَةٍ وَلَا مَمْنُوعَةٍ ﴿٣٣﴾

33. Hayakatiki wala hayakatazwi,

وَفُرُشٍ مَّرْفُوعَةٍ ﴿٣٤﴾

34. Na matandiko yaliyonyanyuliwa.

إِنَّا أَنشَأْنَاهُنَّ إِنشَاءً ﴿٣٥﴾

35. Hakika Sisi tumewaumba upya.

فَجَعَلْنَاهُنَّ أَبْكَارًا ﴿٣٦﴾

36. Na tutawafanya bikira,

عُرُبًا أَتْرَابًا ﴿٣٧﴾

37. Wanaopenda, walio marika.

لِّأَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٣٨﴾

38. Kwa ajili ya watu wa kuume.

ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿٣٩﴾

39. Fungu kubwa katika wa mwanzo.

وَثُلَّةٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿٤٠﴾

40. Na fungu kubwa katika wa mwisho.

WA KUUME

Aya 27– 40

MAANA

Na wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja karama na neema aliyowaandalia waliotangulia, sasa anataja aliyowaandalia wale walio chini yao kuume. Amewaita wa kuume, kwa vile watapewa vitabu vyao kwa mikono yao ya kuume, kama ilivyotangulia kuelezwa. Hili lifutalo ndilo fungu lao katika Pepo.

Katika mikunazi isiyo na miba, na migomba iliyopangiliwa; yaani ndizi zilizopandanaNa kivuli kilichotanda kisichokuwa na muda.Na maji yanayomiminika bila ya kukatika.Na matunda mengi kwa idadi na aina.

Hayakatiki wala hayakatazwi,

Miti ya duniani inazaa kwa msimu na mtunda yanakuwa ni ya mwenye mti tu, akimpa anayemtaka. Lakini miti ya Akhera matunda yake ni ya kudumu na yanatumiwa na kila mtu.

Na matandiko yaliyonyanyuliwa.

Yaani vitanda vya juu. Ajabu ni kauli ya mfasiri mmoja aliyesema urefu wa kitanda kwenda juu ni masafa ya miaka mia tano.

Hakika Sisi tumewaumba Mahurulainiupya, Na tutawafanya bikira wanaopenda waume zao,walio marika.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaandalia watu wa kuume wanawake bikra, wanaowapenda waume zao na wote wakiwa na umri mmoja.

Mfasiri mmoja amekadiria umri wao kuwa miaka 33. na kimo cha dhiraa sitini kwa dhiraa saba; sawa na alivyokuwa Adam, kulingana na kauli yake mfasiri huyo.

Lengo la kuashiria haya ni kutanabahisha kuwa baadhi ya tafsiri haifai kuzitegemea, kwa sababu ni kusema bila ya ujuzi.

Kwa ajili ya watu wa kuume.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekariri kwa kiasi cha kusisitiza kwamba aliyoyataja ni ya watu wa kuume.

Fungu kubwa katika wa mwanzo na fungu kubwa katika wa mwisho.

Maneno yanaanza tena, kwamba watu wa kuumeni kuna waliokuwa katika zama zilizotangulia na wengine wa zama zitakazokuja; nao kwa kawaida watakuwa ni wachache kuliko watu wa kushoto:

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ ﴿١٣﴾

“Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru.” Juz. 22 (34:13).

وَأَصْحَابُ الشِّمَالِ مَا أَصْحَابُ الشِّمَالِ ﴿٤١﴾

41. Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto.

فِي سَمُومٍ وَحَمِيمٍ ﴿٤٢﴾

42. Katika upepo wa moto, na maji yanayochemka.

وَظِلٍّ مِّن يَحْمُومٍ ﴿٤٣﴾

43. Na kivuli cha moshi mweusi.

لَّا بَارِدٍ وَلَا كَرِيمٍ ﴿٤٤﴾

44. Si baridi wala starehe.

إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُتْرَفِينَ ﴿٤٥﴾

45. Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.

وَكَانُوا يُصِرُّونَ عَلَى الْحِنثِ الْعَظِيمِ ﴿٤٦﴾

46. Na walikuwa wakishikilia kiapo kikubwa.

وَكَانُوا يَقُولُونَ أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na walikuwa wakisema: Tutakapokufa na tukawa udongo na mifupa, ati ndio tutafufuliwa?

أَوَآبَاؤُنَا الْأَوَّلُونَ ﴿٤٨﴾

48. Au baba zetu wa zamani?

قُلْ إِنَّ الْأَوَّلِينَ وَالْآخِرِينَ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho,

لَمَجْمُوعُونَ إِلَىٰ مِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿٥٠﴾

50. Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.

ثُمَّ إِنَّكُمْ أَيُّهَا الضَّالُّونَ الْمُكَذِّبُونَ ﴿٥١﴾

51. Kisha nyinyi, mliopotea, mnaokadhibisha,

لَآكِلُونَ مِن شَجَرٍ مِّن زَقُّومٍ ﴿٥٢﴾

52. Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqum.

فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٥٣﴾

53. Na kwa huo mtajaza matumbo.

فَشَارِبُونَ عَلَيْهِ مِنَ الْحَمِيمِ ﴿٥٤﴾

54. Na juu yake mtakunywa maji yanayochemka.

فَشَارِبُونَ شُرْبَ الْهِيمِ ﴿٥٥﴾

55. Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu.

هَـٰذَا نُزُلُهُمْ يَوْمَ الدِّينِ ﴿٥٦﴾

56. Hii ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.

NA WA KUSHOTO

Aya 41 – 56

MAANA

Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto.

Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwanza, ametaja malipo makubwa aliyowandalia waliotangulia, kisha rehema na thawabu alizowaandalia wa kuume. Sasa, katika Aya hizi tulizo nazo anataja aina kwa aina ya adhabu itakayowapata watu wa kushoto; miongoni mwazo ni kuwa wao watakuakatika upepo wa moto, na maji yanayochemka . Upepo wa moto utavutwa ndani ya mwili na kuchemsha nyama na damu na watakunywa maji yanayochemka tumboni.

Na kivuli cha moshi mweusi.

Neno moshi mweusi tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu yahmum ambalo pia lina maana ya weusi tititi wa kitu chochote na pia moshi mwingi. Maana yanafaa kwa moja wapo au yote pamoja

Si baridi wala starehe.

Ni kivuli lakini hakileti baridi wala kukinga joto, sawa na anayekimbilia kwenye mchanga wa kuchoma.

Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.

Walipetuka mipaka wakawafanyia uovu waja wa Mwenyezi Mungu na miji yao; wakapora riziki za viumbe na wakastarehe kadiri walivyotaka, kuanzia mavazi ya gharama, chakula kitamu, kinywaji kinachoshuka hadi makazi ya fahari. Basi malipo mbele ya Mwenyezi Mungu yamekuwa ni adhabu ya kuungua, kinywaji cha moto, chakula cha zaqqum, upepo wa kuunguza na kivuli ni moshi.

Na walikuwa wakishikilia kiapo kikubwa.

Imesemekana kuwa ni madhambi makubwa. Lakini kauli ya kiapo chao cha uongo kuwa hakuna ufufuo wala malipo, ndiyo iliyo karibu; kama alivyowasimulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) pale aliposema: Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu (kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu.” Juz. 14 (16:38).

Kiapo chao hiki ni matokeo ya shirki yao, kwa hiyo basi inafaa kufasiri Aya tuliyo nayo kwa maana ya shirki.

Na walikuwa wakisema: Tutakapokufa na tukawa udongo na mifupa, ati ndio tutafufuliwa? Au baba zetu wa zamani?

Walisema, kwa madharau, kuwa kweli mchanga unaweza kugeuka kuwa mtu? Wamesahau kuwa Mungu aliwaumba kutokana na mchanga kisha tone la manii.

Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho, bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.

Waambie ewe Muhammad! Ndio, Mwenyezi Mungu atawakusanya kesho viumbe ili kuchambua hisabu na malipo ya matendo. Au kama Mwenyezi Mungu angeliwaacha tu hivi hivi bila ya makemeo wala maswali, angelikuwa ni dhalimu na anayefanya mchezo. Ametukuka sana Mwenyezi Mungu na wanayoyasema madhalimu.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; zikiwemo: Juz. 13 (13:5), Juz. 15 (17:49) na Juz. 18 (23:81-83).

Kisha nyinyi, mliopotea, mnaokadhibisha, Mmepotea mkaacha njia ya haki, mkaikanusha haki na mkabishana kijinga, basi malipo yenukwa yakini mtakula mti wa Zaqqum. Na kwa huo mtajaza matumbo.

Sisi hatujui mti huu na kuna mengi tusiyoyajua, lakini tuna uhakika kuwa unaashiria, adhabu mbaya. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefananisha mashada yake na vichwa vya shetani. Tazama Juz. 22 (37:62).

Na juu yake mtakunywa maji yanayochemka.

Chakula chao ni kichungu kuliko shubiri, kinanuka kuliko mzoga na kinywaji chao ni chumvi.

Tena mtakunywa kama wanavyokunywa ngamia wenye kiu.

Neno kiu tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu him ambalo lina maana ya ngamia mwenye kiu au ugonjwa wa kiu kisichokwisha.

Hii ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.

Hii ni ishara ya hali ya watu wa kushoto. Siku ya malipo ni siku ya kiyama. Karamu ni chakula na kinywaji anachoandaliwa anayekuja. Ni karamu mbaya ya kinywaji, kivazi na hata malazi. Fauka ya hayo mikono itafungwa shingoni na kukutanishwa utosi na nyayo. Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu na mwisho mbaya.