TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 28304
Pakua: 3893


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 28304 / Pakua: 3893
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

27

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

يَوْمَ تَرَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ يَسْعَىٰ نُورُهُم بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِم بُشْرَاكُمُ الْيَوْمَ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٢﴾

12. Siku utakapowaona waumini wanaume na waumini wanawake, nuru yao inakwenda mbele yao, na kuume kwao: Furaha yenu leo ni Bustani zipitiwazo na mito chini yake kukaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

يَوْمَ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ لِلَّذِينَ آمَنُوا انظُرُونَا نَقْتَبِسْ مِن نُّورِكُمْ قِيلَ ارْجِعُوا وَرَاءَكُمْ فَالْتَمِسُوا نُورًا فَضُرِبَ بَيْنَهُم بِسُورٍ لَّهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِن قِبَلِهِ الْعَذَابُ ﴿١٣﴾

13. Siku wanafiki wanaume na wanafiki wanawake watapowaambia walioamini: Tuangalieni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na upande wake wa nje kuna adhabu.

يُنَادُونَهُمْ أَلَمْ نَكُن مَّعَكُمْ قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنَّكُمْ فَتَنتُمْ أَنفُسَكُمْ وَتَرَبَّصْتُمْ وَارْتَبْتُمْ وَغَرَّتْكُمُ الْأَمَانِيُّ حَتَّىٰ جَاءَ أَمْرُ اللَّـهِ وَغَرَّكُم بِاللَّـهِ الْغَرُورُ ﴿١٤﴾

14. Watawaita wawaambie: Kwani hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkangojea, na mkatia shaka na matamanio yakawadanganya, Mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu ya na mdanganyifu akawadanganya katika Mwenyezi Mungu.

فَالْيَوْمَ لَا يُؤْخَذُ مِنكُمْ فِدْيَةٌ وَلَا مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مَأْوَاكُمُ النَّارُ هِيَ مَوْلَاكُمْ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٥﴾

15. Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, Wala kwa wale walio kufuru. Makaazi yenu ni Motoni; na ni marejeo maovu yalioje!

NDANI YAKE NI REHMA NA NJE YAKE NI ADHABU

Aya 12 – 15

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema kuwa mwenye kuamini na akatoa sabili kwa ajili ya radhi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, atakuwa na ujira mzuri. Sasa hapa anaubainisha ujira huo kwa kusema:

Siku utakapowaona waumini wanaume na waumini wanawake, nuru yao inakwenda mbele yao, na kuume kwao:

Wenye takuwa waliojitolea, dunini walikuwa wakienda kwa mwongozo wa Mola wao. Siku ya hisabu na malipo mwongozo huu wa Mwenyezi Mungu utawaangazia mwanga hasa wa kuhisiwa, kama inavyoashiria Aya kwa neno utawaona na neno kuume kwao; yaani utaona nuru yao kwa macho yako; kama unavyoona taa anavyoichukuwa mtu mkononi na kuifanya anavyotaka.

Kwa maneno mengine ni kuwa, waliifanyia kazi nuru hii duniani kwa bidii na ikhlasi, wakaikuta Akhera iko mbele yao ikiwangazia masafa.

Furaha yenu leo ni Bustani zipitiwazo na mito chini yake kukaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Kesho waongofu watatoka makaburini mwao na kutembea kwenye mwangaza utakaowafichulia njia ya amani. Na kabla ya kufika mwisho utawajia mwito: Furahini kwa Pepo. Kuna furaha gani zaidi inayoweza kulingana na Pepo ya milele na neema yake? Na ni kufuzu gani kukubwa kuliko huku?

Siku wanafiki wanaume na wanafiki wanawake watapowaambia walioamini: Tuangalieni ili tupate mwangaza katika nuru yenu.

Neno kuangalia tulilolifasiri kutokana na neno la kiarabu nadhr lina maana ya kuona kwa macho, kutaamali au kuhurumia [11] 1. Sio mbali kuwa maana ya kuangalia hapa ni hii ya kuhurumia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelitumia neno hili kwa maana haya ya kuhurumia aliposema:

وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ﴿٧٧﴾

“Wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawaangalia.” Juz. 3 (3:77).

Waongofu duniani walikuwa kwenye nuru ya Mola wao na Akhera watakuwa hivyo hivyo:

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ ﴿١٧﴾

“Na ambao wameongoka anawazidishia uongofu wao na anawapa takua yao” Juz.26 (47:17).

Na wanafiki duniani walikuwa katika viza vya hawaa na mtamanio, basi wao siku ya kiyama watakuwa kwenye giza juu ya giza:

وَمَن كَانَ فِي هَـٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٧٢﴾

“Na aliyekuwa kipofu katika hii, basi Akhera atakuwa kipofu zaidi na aliyepotea njia.”

Juz. 15 (17:72).

Hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu imetaka wanafiki waone nuru ya waongofu ikiwaangazia mbele yao, ili wazidi uchungu juu ya uchungu; kisha uchungu utazidi pale watakapotaka usaidizi kwa waumini kuwa waende kwenye njia yaowaambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru!

Hili ndilo jawabu lao: rudini kwa rafiki yenu shetani na mtafute nuru kutoka kwake. Yuko nyuma yenu leo kama alivyokuwa nyuma yenu jana.

Nuru hii ni ya yule aliyeifanyia kazi duniani na katika Akhera yake. Mwenye kuyanunua maisha ya dunia kwa Akhera, basi hatatoka katika giza isipokuwa kwenye ubaya zaidi.

Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na upande wake wa nje kuna adhabu.

Makusudio ya ukuta ni kizuizi na rehema ni Pepo. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa Pepo na akawaadhibu wanafiki kwa adhabu ya Moto. Baina ya Pepo na Moto kuna kizuizi kilicho na pande mbili.

Watawaita wawaambie: Kwani hatukuwa pamoja nanyi?

Wanafiki watazungumza kwa lugha ya maneno au lugha ya hali kuwa sisi duniani tulikuwa tukifunga na kuswali na kufanya mliyokuwa mkiyafanya nyinyi, kwanini nyinyi mmeingia Peponi na sisi tukaingia motoni?

Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe.

Makusudio ya kujifitini ni kujiangamiza. Waumini watawajibu, ndio mlikuwa pamoja na sisi mkifunga na kuswali, lakini mliziangamiza nafsi zenu kwa uwongo na unafikina mkangojea balaa iwafike waumini,na mkatia shaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kauli zake,na matamanio yakawadanganya , pale mlipodhani kwamba hadaa yenu na unafi- ki wenu utawavusha salama bila ya hisabu na adhabu.

Mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kukutana naye kwa hisabu na malipo,na mdanganyifu akawadanganya katika Mwenyezi Mungu na mkamsadiki shetani na ahadi yake kuwa mtasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, wala kukubaliwa toba wala hamtaweza kuikimbia adhabu:

فَلَن يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِم مِّلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٩١﴾

“Basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidia ya dhahabu kwa kujaza ardhi lau angelitoa. Hao watapata adhabu iumizayo, wala hawatakua na wasaidizi.” Juz. 3 (3:91).

Wala kwa wale walio kufuru.

Vile vile haitakubaliwa fidia na toba kutoka kwa wale waliodhihirisha kufuru bila ya kufanya hadaa na unafiki kama nyinyi.

Makaazi yenu ni Motoni . Hakuna kukimbia wala usaidizi isipokuwa Jahannam ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿١٦﴾

16. Je, bado haujafika wakati kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka? Wala wasiwe kama waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikasusuwaa, na wengi wao ni mafasiki.

اعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿١٧﴾

17. Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Tumewabainishia Ishara ili mpate kutia akili.

إِنَّ الْمُصَّدِّقِينَ وَالْمُصَّدِّقَاتِ وَأَقْرَضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعَفُ لَهُمْ وَلَهُمْ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١٨﴾

18. Kwa hakika wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, watazidishiwa maradufu na watapata ujira mzuri.

وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصِّدِّيقُونَ وَالشُّهَدَاءُ عِندَ رَبِّهِمْ لَهُمْ أَجْرُهُمْ وَنُورُهُمْ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ﴿١٩﴾

19. Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio wakweli hasa; Na Mashahidi mbele ya Mola wao, watapata ujira wao na nuru yao. Na waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.

JE, BADO HAUJAFIKA WAKATI KWA WALIOAMINI

Aya 16 – 19

MAANA

Je, bado haujafika wakati kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka?

Kuunganisha haki iliyoteremka juu ya kumbuka Mwenyezi Mungu ni kwa kitafsiri; kwamba hakuna tofauti baina ya kinachounganishwa na kinachounganisha isipokuwa matamshi tu. Makusudio ya walioamini ni kundi katika wao.

Kabla ya kuleta ubainifu wa Aya, tunatanguliza maelezo kuwa imani inatofautiana kwa nguvu na udhaifu. Kuanzia imani inayomwajibisha aliye nayo kuwa maasumu; kama manabii; hadi imani ya uaminifu; kama vile baadhi ya maswahaba, hadi walio na daraja ya chini na kuendela chini zaidi.

Makusudio ya walioamini hapa ni wale waliotosheka na imani ya juu juu sio ya ndani na kwa dhahiri sio kwa hali halisi, wala haliwashughulishi jambo lolote la watu na masilahi ya umma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelizindua kundi hili la waumini kwenye Aya za jihadi alizoziteremsha katika Kitabu chake na kuhimiza kufanya uadilifu, kuinusuru haki na watu wake na kuwasuluhishia watu. Amewazindua kwenye hakika ya dini kwa mfumo huu wa upole ‘Je, bado haujafika wakati,’ ili waweze kusikia na kuwa na akili?

Wala wasiwe kama waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikasusuwaa.

Watu wa Kitabu ni wayahudi na wanaswara. Kususuwaa nyoyo zao ni kinaya cha kugeuka kwao baada ya Musa. Vile vile wanaswara baada ya Isa, basi nanyi waislamu msigeuke baada ya Muhammad(s.a.w.w) ; kama walivyogeuka watu wa Kitab hapo mwanzo. Mfano wa Aya ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ﴿١٤٤﴾

“Hakuwa Muhammad ila ni Mtume; wamekwishapita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma? Juz. 4 (3:144)

Na wengi wao ni mafasiki.

Makusudio ya ya wengi ni viongozi wa kiyahudi na kinaswara (kikiristo) walioipotoa Tawrat na Injil kwa kupupia vyeo na chumo.

Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake.

Wafasiri wengi wamesema kuwa huku ni kufananisha nyoyo zilizosusuwaa na ardhi iliyokufa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu anaipa uhai ardhi kwa mvua vile vile ataziongoza nyoyo zilizosusuwaa kwa mawaidha.

Tuonavyo sisi ni kuwa huu ni utisho na onyo kwa wale watakaogeuka baada ya Muhammad(s.a.w. w ) – kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafufua; sawa na anavyoifufua ardhi, na atawalipa kuritadi kwao baada ya nabii wao.

Maana haya yanatiwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyokuja moja kwa moja inayosema:Tumewabainishia Ishara ili mpate kutia akili. Hakika nyinyi mtaulizwa siku ya Kiyama yale mliyoyazusha baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) .

Kwa hakika wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, watazidishiwa maradufu na watapata ujira mzuri.

Husomwa bila ya shadda katika herufi swad kwa maana ya waumini na husomwa kwa shadda kwa maana ya wanaotoa sadaka.

Makusudio ya mkopo mwema ni kutoa sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hiyo hakuna kukaririka. Makusudio ya ujira mzuri ni kuwa nuru yao iko mbele yao siku ya Kiyama kuongezea mahurilaini makasri n.k.

Umetangulia mfano wake katika Aya 11 ya sura hii na Juz. 2 (2:245)

Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda kwa mujibu wa imani yao,hao ndio wakweli hasa ; yaani waliodumu na ukweli katika imani yao kwa kauli na vitendo, na ukweli ni njia ya uokovu kwa kila maangamizi.

Na Mashahidi mbele ya Mola wao, watapata ujira wao na nuru yao.

Mashahidi ni wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ama ujira wao mbele ya Mola wao, ameibainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kauli yake: “Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na kuuawa. Ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injil na Qur’an.”Juz. 11 (9:111).

Ama nuru yao ameiashiria katika Aya ya 12 ya sura hii. Mtume(s.a.w.w) anasema: “Hakuna yeyote atayeingia Peponi kisha akapenda kutoka kwenda duniani, hata kama atakuwa na ardhi na vilivyomo ndani yake, isipokuwa shahidi. Atatamani arudi duniani auawe mara kumi, kutokana na karama aliyoiona kwa Mwenyezi Mungu.

Na waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.

Hii ni desturi ya Qur’an kulinganisha wenye takuwa na wakosefu na thawabu zao na adhabu zao kwa kusudia kupendekeza na kuhadharisha.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; ikiwemo ile iliyo katika Juz.7 (6:32). Dunia inayoshutumiwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kupitia kwa mitume wake, ni ile dunia inayotafutiwa matamanio, starehe, mchezo, upuzi, kiburi na kujifaharisha. Ama dunia ambayo haja za wahitaji zinatekelezwa, udhalimu unapingwa na kunufaika ndani ya dunia hiyo na Akhera, basi hiyo haishutumiwi.

28

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿٢٠﴾

20. Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na upuzi, na pambo, na kujifaharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Ni kama mfano wa mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yana rangi ya njano kisha yakawa makapi. Na akhera kuna adhabu kali na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

سَابِقُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا كَعَرْضِ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أُعِدَّتْ لِلَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴿٢١﴾

21. Kimbilieni maghufira ya Mola wenu, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٢٢﴾

22. Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujaziumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾

23. Ili msihuzunike kwa kilicho wapotea, wala msifurahi kwa alichowapa. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna, anayejifaharisha.

الَّذِينَ يَبْخَلُونَ وَيَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبُخْلِ وَمَن يَتَوَلَّ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٤﴾

24. Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili. Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

MAISHA YA DUNIA NI MCHEZO NA UPUZI

Aya 20 – 24

MAANA

Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na upuzi, na pambo, na kujifaharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hikima, ataona kuwa thawabu za Mwenyezi Mungu zimewekewa wanaoamini, wakatenda mema duniani na wakatekeleza haki na wajibu; na kwamba hakuna nyenzo ya kufikia wema wa Akhera isipokuwa kazi ya manufaa katika maisha ya dunia.

Ni kama mfano wa mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yana rangi ya njano kisha yakawa makapi.

Sifa hii inalingana na dunia kwa sababu haiudumu kwenye hali moja. Inakuwa kijani kisha manjano, inakuwa ngumu kisha laini na inatoa na kuzuia. Lau itampa mtu kila analolipenda, basi muda mchache tu inamnyang’anya kila kitu mpaka maisha yake yeye mwenyewe na ya watu wake.

Vile vile mfano unaendana na sifa za mtu duniani. Anakuwa kijana mwenye nguvu ya mifupa, kushupaa nyama yake na kuwa nyororo ngozi; kisha anazeeka na kuwa mnyonge, nyama zinasinyaa, mifupa inakuwa dhaifu na ngozi kuwa manjano. Kila siku zinavyoendelea ndivyo anavyozidi kuwa katika hali mbaya mpaka anakuwa kama makapi na kumalizika.

Ikiwa dunia iko hivi na mtu naye anakuwa hivyo, basi lililo bora kwake ni kuyafanyia kazi maisha ya daima isiyokwisha neema yake wala kuzeeka mkazi wake.

Na akhera kuna adhabu kali na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa dunia haidumu raha yake wala tabu yake, sasa anataja kuwa Akhera ni thabiti kwenye hali moja tu. Neema yake ni ya kudumu na adhabu yake pia ni ya kudumu. Kwa vile inayosababisha neema ni radhi ya Mwenyezi Mungu na sababu ya moto ni ghadhabu zake na zote hizo ziko.

Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

Razi anamnukuu sahaba mtukufu Said bin Jubayr, kwamba amesema katika kufasiri Aya hii: “Dunia ni starehe ya udanganyifu kama ikikufanya upuuze kuitafuta Akhera, lakini kama itakupa mwito wa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kuitafuta Akhera, basi itakuwa ni starehe nzuri na nyenzo bora.”

Sahaba huyu mtukufu ni katika wanafunzi wa Mtume(s.a.w. w ) waliokuwa karibu naye.

Kimbilieni maghufira ya Mola wenu, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake.

Makusudio ya maghufira hapa ni sababu zake; kama vile toba na matendo mema. Baadhi ya wafasiri wamesema, ikiwa upana ni hivyo je, urefu? Wengine wakasema: imegunduliwa kuwa umbali wa ulimwengu hauna mwisho. Kwa hiyo basi upana utakuwa ni wa uhakika sio majazi.

Sisi hatufahamu upana isipokuwa ni ibara ya utukufu wa Pepo na upana wake usiokuwa na kiwango. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:133).

Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu kwa watu, lakini watu wengi hawashukuru.

Hakuna mwenye shaka kwamba utiifu ni sababu ya kuzidishiwa fadhila, bali ndio sababu ya fadhila ya Mwenyezi Mungu na radhi yake siku ya hukumu.

Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujaziumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Maana ya dhahiri ya Aya hii yanaonyesha kuwa masaibu yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu; ni sawa yawe ni katika aina ya majanga ya maumbile; kama matetemeko na mafuriko, au yawe ya kijamii; kama vile vita ufukara na uadui.

Lakini haya siyo makusudio yake moja kwa moja kwa hukumu ya wahyi na akili. Ufafunuzi ni kama ufuatavyo:-

MASAIBU NA MWENYE IDHLAL

Mwenye Idhlal katika kufasiri Aya hii anasema: “Tamko kwa kuliachia kilugha halihusiani na heri au shari. Kila msiba unaotokea kwenye ardhi yote au kwenye nafsi ya mtu au wanaoambiwa, utakua uko katika kitabu tangu azali kabla ya kudhihiri ardhi na kudhihiri nafsi.”

Tunamuuliza mwenye Idhlal: ukiwa kweli unategemea dhahiri ya tamko na kuliachia kilugha, mbona hukufanya hivyo ulipokuwa unafasiri Aya hii: “Na misiba iliyowasibu ni kwa sababu ya ilivyotenda mikono yenu.” Juz. 25 (42:30). Je, umesahau katika tafsiri yako kuwa ulisema ninanunukuu: “Kila msiba uliomsibu mtu una sababu zake kutokana na ilivyofanya mikono yake.” Jalada la 7, uk.38, Juzuu ya 25.

Je, utakuwa unategemea dhahiri ya tamko na kuliachia kilugha hata kama hilo litafanya Aya mbili zigongane?

Je, pia utategemea dhahiri ya tamko likiwa litagongana na hukumu ya akili na uhalisia, na kufahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ana mkono, uso, usikizi na macho?

Je, uzayuni na ukoloni ambao ni chimbuko la masaibu na mabalaa yanayopatikana hivi sasa yanatokana na wao au yanotokana na Mwenyezi Mungu?

Ni jambo lisilowezekana kutokea mgongano baina ya Aya mbili kiuhakika ni kiuhalisi. Pia ni jambo lisilowezekana kugongana Aya na hukumu ya akili. Itakuwaje hivyo na hali imetokea kwa mwenye hikima mwenye ujuzi?

Ikitokea dhahiri ya Aya kugongana na Aya nyingine au kugongana na hukumu ya kiakili, tutajua dhahiri hii siyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu; isipokuwa ameliachia tamko kutegemea desturi yake ya kuleta ibara; kama kuleta ibara ya watu wa Kitabu kwa maana ya mayahudi na wanaswara. Au kuleta ibara kutokana na ilivyozoeleka kiakili; kama uweza wa Mwenyezi Mungu kuuletea ibara ya mkono. Au kuleta ibara kutegema Aya nyingine; kama Aya hizi zifuatazo:-

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ ﴿٣٠﴾

“Na misiba iliyowasibu ni kwa sababu ya ilivyotenda mikono yenu.” Juz. 25 (42:30).

وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِنْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٧﴾

“Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe.” Juz. 4 (3:117).

ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ ﴿٤١﴾

“Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa sababu ya iliyoyafanya mikono ya watu.”

Juz.21 (30:41).

Aya zote hizi na maana yake ni dalili mkataa kwamba makusudio ya Aya tuliyonayo siyo ya kidhahiri ya lugha na kwamba Mwenyezi Mungu ameiacha hivyo kwa kutegema aliyoyasema katika Aya hizo nyingine.

Kwa hiyo basi makusudio ya misiba ya ardhi, katika Aya tuliyonayo, ni majanga ya kimaumbile; kama vile matetemeko n.k. Na makusudio ya masaibu ya nafsi ni baadhi ya magonjwa yasiyokuwa na kinga wala hadhari n.k.

Ama makusudio ya misiba katika Aya zile tatu ni masaibu yanayotokana na binadamu mwenyewe; kama vile dhulma vita njaa n.k.

Ili msihuzunike kwa kilichowapotea, wala msifurahi kwa alichowapa.

Imam Aliy(a.s ) anasema:“Zuhudi yote iko katika matamshi mawili katika Qur’an; kisha akasoma Aya hii na akaendelea kusema: “Asiyekata tamaa kwa yaliyopita wala asifurahi kwa yanayokuja atakuwa ameichukua zuhudi kwa pande zake mbili.”

Hakuna asiyehuzunika na kufurahi; hata mitume pia. Isipokuwa makusu- dio ni furaha isimwingize mtu kwenye batili na huzuni isimtoe kwenye haki. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) kwamba yeye alisema wakati wa mauti ya mwanawe Ibrahim:“Jicho linalia na moyo unahuzunika wala hatusemi isipokuwa yanayomridhisha Mola wetu. Nasi tunakuhuzunikia ewe Ibrahim.”

Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna, anayejifaharisha.

Hakuna kitu kinachofahamisha ujinga kuliko kiburi na kujiona. Imam Aliy(a.s ) anasema: “Ana nini binadamu na kujifaharisha? Mwanzo wake ni tone la manii na mwisho wake ni mzoga. Hawezi kujipa riziki wala kujikinga na mauti.”

Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili.

Anayefanya ubakhili na akawaamuru wengine wafanye ubakhili, ndiye aliyekusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾ عُتُلٍّ بَعْدَ ذَٰلِكَ زَنِيمٍ ﴿١٣﴾

“Mwenye kuzuia heri arukaye mipaka mwenye dhambi, mgumu, juu ya hayo ni mshenzi.”

(68:12-13).

Razi anasema hizi ni sifa za mayahudi. Ikumbukwe kuwa Razi alifariki mwaka 606 AH.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:37).

Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

Bakhili hajidhuru ila yeye mwenyewe, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi wala haumnufaishi utiifu wa mwenye kutii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (47:37).

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ وَأَنزَلْنَا الْحَدِيدَ فِيهِ بَأْسٌ شَدِيدٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ وَرُسُلَهُ بِالْغَيْبِ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢٥﴾

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili wazi wazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا وَإِبْرَاهِيمَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِمَا النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ فَمِنْهُم مُّهْتَدٍ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿٢٦﴾

26. Na hakika tulimtuma Nuh na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walioongoka, na wengi katika wao ni mafasiki.

ثُمَّ قَفَّيْنَا عَلَىٰ آثَارِهِم بِرُسُلِنَا وَقَفَّيْنَا بِعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَآتَيْنَاهُ الْإِنجِيلَ وَجَعَلْنَا فِي قُلُوبِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ رَأْفَةً وَرَحْمَةً وَرَهْبَانِيَّةً ابْتَدَعُوهَا مَا كَتَبْنَاهَا عَلَيْهِمْ إِلَّا ابْتِغَاءَ رِضْوَانِ اللَّـهِ فَمَا رَعَوْهَا حَقَّ رِعَايَتِهَا فَآتَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا مِنْهُمْ أَجْرَهُمْ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿٢٧﴾

27. Kisha tukafuatisha nyuma yao Mitume wetu, na tukamfuatisha Isa bin Maryam, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema. Na utawa wameuzua wao. Hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni mafasiki.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٨﴾

28. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atawapa sehemu mbili katika rehema yake, na atawajaalia muwe na nuru ya kwenda nayo, na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

لِّئَلَّا يَعْلَمَ أَهْلُ الْكِتَابِ أَلَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِّن فَضْلِ اللَّـهِ وَأَنَّ الْفَضْلَ بِيَدِ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴿٢٩﴾

29. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.

CHUMA KINA NGUVU NYINGI

Aya 25 – 29

MAANA

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu.

Kila ambalo unajulikana uhakika kwalo basi hilo ni mizani, ni sawa uwe ni wahyi, akili au hisia; kama vile majaribio na ushuhuda. kwa hiyo basi kuunganisha mizani kwenye Kitabu ni kuunganisha mahsusi kwenye ujumla; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na alichopewa Musa na Isa na manabii kutoka kwa Mola wao.”

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume kwa hoja zinazojulisha juu ya utume wao na risala yao na kwa lile litakalowaongoza watu kwenye haki na uadilifu, ili wawe katika njia iliyonyooka.

Na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu.

Wafasiri wa kale walisema katika kufasiri Aya hii kuwa chuma ni nguvu katika vita, watu wanatengeneza panga na diraya. Pia wanatengeneza visu shoka na sindano. Mifano hii ilikuja kuakisi zama zao na maisha yao. Sisi tungelikuwa wakati wao, nasi tungelisema kama walivyosema. Na wao wangelikuwa zama zetu wangelisema: Chuma ni uti wa mgongo wa maisha katika nyanja zote.

Nyenzo za mawasiliano ya nchi kavu angani na baharini zinatokana nacho. Pia vyombo kadha anavyovihitaji mtu tajiri au fukara, madaraja, majengo, kuta na maghala, vyote vinahitajia chuma. Lau si chuma mtu asingelijua umeme na petrol. Chuma ni msingi wa ilimu nyinyi za kisasa, bali ndio kila kitu cha maendeleo ya karne ya ishirini.

Na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu.

Yaani atakayenusuru mafunzo ya mitume wa Mwenyezi Mungu hata kama hakuwaona.

Kila kitu katika maisha haya kina pande mbili: chanya na hasi; manufaa na madhara. Ikiwa chuma kina manufaa hayo, ya kumhudumia mtu, tuliyoyataja, basi vie vile kina madhara ya kumwangamiza mtu. Kabla ya kugunduliwa chuma mauji yalikuwa ni kwa makumi, lakini baada ya kugunduliwa mauji yamekuwa kwa mamilioni.

Hofu na utisho wanaoishi nao wa magharibi na wa mashariki, damu inayomwagika kama mito huko Cambodia, Laos, Vietnam, Guatemala na mashariki ya kati[12] , maangamizi yote haya na mengineyo ni natija ya nguvu ya silaha ya shari ya chuma dhidi ya wananchi na harakati za ukombozi.

Hapa ndio tunatambua siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu. Na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu.”

Yaani ameumba chuma ili awatie mtihani waja wake kwa yaliyomo ndani ya nyoyo zao ya heri na shari, na kudhihirisha wazi kwenye ulimwengu, ili apambanuke muovu ambaye anaifanya nguvu ni nyenzo ya kutekeleza matamanio yake na malengo yake, na apambanuke mwema ambaye anaona nguvu ni neema ya Mwenyezi Mungu na kuitumia kwa manufaa ya watu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema yake.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.

Atawaadhibu mataghuti madhalimu kwa mikono ya wenye haki ambao hawataki katika maisha haya isipokuwa uhuru, uadilifu na kuishi wote kwa utulivu na amani.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mapinduzi dhidi ya dhulma yanayotokea leo kila pembe ya ardhi. Hakuna mwenye shaka kwamba mapinduzi haya yana nguvu za Mwenyezi Mungu, hayatazuilika maadamu yanatafuta haki na uadilifu. Ama malipo ya mataghuti huko Akhera ni Jahannam, makao mabaya kabisa.

Na hakika tulimtuma Nuh na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu.

Mwenyezi Mungu alimtuma Nuh na Ibrahim kulingania kwenye haki, kila mmoja akafikisha risala ya Mola wake akapigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu; kama ilivyo habari ya Nuh katika Juz. 12 (11:25-49) na kuhusu Ibrahim katika Juz. 17 (21:51-74).

Basi wapo miongoni mwao walioongoka, na wengi katika wao ni wapotovu.

Yaani katika kizazi chao kuna baadhi ni wema, lakini wengi wao walikuwa bila dini wala dhamiri; kama walivyo watoto wa ulama wa dini.

Kisha tukafuatisha nyuma yao Mitume wetu, wengine wengi.

Baada ya Nuh na Ibrahim, Mwenyezi Mungu (s.w.t) alituma mitume wengi; kama vile Hud, Swaleh, Musa n.k.

Na tukamfuatisha Isa bin Maryam, na tukampa Injili.

Waliendelea kufuatana mitume hadi Isa(a.s) akiwa na Injil. Wakati huo ilikuwa ni mwongozo na nuru.

Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema.

Hao ni wale waliomfuta Bwana Masih na wakayatumia mafunzo yake kwa nukuu na kwa kiroho bila ya kugeuza yale yanayotamaniwa na nafsi zao. Hilo linaashiriwa na neno wakamfuata. Tazama mwanzo wa Juzuu ya saba.

Na utawa wameuzua wao. Hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata.

‘Ila’ hapa ni kwa maana ya lakini. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaelezea utawa, isipokuwa viongozi wa kinaswara ndio waliouanzisha kwa madai kuwa unawakurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa vile unawaweka mbali na dunia na starehe zake.

Pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaamuru utawa, bali amewahalalishia riziki njema; hata hivyo bado wao hawakujilazimisha na zuhudi ya utawa, bali waliufanya ni nyenzo ya matamanio na kutawala. Aya hii inafahamisha kuwa hakuna utawa katika Uislamu wala katika dini aliyokuja nayo Bwana Masih.

Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao.

Hao ni wale waliokuwa wafuasi wa Isa halisi na ukweli, waliokuwa wakiamini kwa kauli na vitendo kwamba umasihi ni upendo na huruma, ni usafi na ubinadamu, sio ubaguzi na chuki, dhulma na unyanyasaji, vita na mapinduzi, kuanzisha vita na vurugu wala sio silaha za maangamizi. Pia wakaamini kuwa Umasihi sio nembo za uongo kuzuia uhuru, kueneza hofu na wasiwasi katika nyoyo za waja wa Mwenyezi Mungu.

Na wengi wao ni mafasiki wakiongozwa na kambi ya ukoloni mambo leo na maadui nambari moja wa ubinadamu ambao wana sifa zote zinazowatoa kwenye umasihi wa kihaki na ukweli.

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu.

Yaani enyi ambao mmemkubali Mwenyezi Mungu, fanyeni kwa mujibu wa kuuamini kwenu. wala matendo yenu yasiende kinyume na kauli zenu.

Na muaminini Mtume wake . Mtiini Muhammad(s.a.w.w) na mfuate sera yake na mwongozo wake.

Atawapa sehemu mbili katika rehema yake.

Makusudio ya rehema hapa ni thawabu. Maana ni kuwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akatenda kwa mujibu wa imani yake atakuwa na aina mbili ya tahawabu: thawabu za imani na thawabu za matendo.

Na atawajalia muwe na nuru ya kwenda nayo siku ya Kiyama.

Ambaye Mwenyezi Mungu hatamjalia nuru siku hii atahangaika kwenye giza na atatokeza kwenye machungu.

Na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Atawasamehe maasi yaliyopita, kwa vile Yeye ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu. Ibn Al-arabi anasema katika Futuhat: “Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutanishi maghufira na toba wala na matendo mema, kwa hiyo hapana budi rehema na maghufira imwendee kwenye kuifanyia israf nafsi yake.” Na rehema yake imekienea kila kitu.

Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya kuwa hawana uweza ni kuwa wao hawatapata chcochote katika fadhila za Mwenyezi Mungu siku ya kiyama.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kesho atawaghufiria waliomwamini Muhammad(s.a.w.w) . Na mwenye kufanya mema atampa ujira wake mara mbili, kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu ni mkarimu. Vile vile wajue mayahudi kuwa na manaswara waliokataa kumwamini Muhammad(s.a.w.w) kwamba wao hawana fungu la maghufira na rehema yake, kwa vile wamejizuia kumsadiki Muhammad(s.a.w.w) .

Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.

Anayowafadhili wale ambao wamemwamini Muhammad(s.a.w.w) , wala hakuna wa kuzuia alilolitaka, kwa sababu kila kitu kiko mikononi mwake naye ni muweza wa kila kitu.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA ISHIRINI NA TATU