3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
وَاذْكُرْ أَخَا عَادٍ إِذْ أَنذَرَ قَوْمَهُ بِالْأَحْقَافِ وَقَدْ خَلَتِ النُّذُرُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٢١﴾
21. Na mtaje ndugu wa kina A’di, alipowaonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake: kuwa msimwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.
قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَأْفِكَنَا عَنْ آلِهَتِنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٢٢﴾
22. Wakasema: Je, umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
قَالَ إِنَّمَا الْعِلْمُ عِندَ اللَّـهِ وَأُبَلِّغُكُم مَّا أُرْسِلْتُ بِهِ وَلَـٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ ﴿٢٣﴾
23. Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Mimi ninawafikishia niliyotumwa, lakini ninawaona kuwa nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.
فَلَمَّا رَأَوْهُ عَارِضًا مُّسْتَقْبِلَ أَوْدِيَتِهِمْ قَالُوا هَـٰذَا عَارِضٌ مُّمْطِرُنَا بَلْ هُوَ مَا اسْتَعْجَلْتُم بِهِ رِيحٌ فِيهَا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٤﴾
24. Basi walipoliona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili ni la kutunyeshea mvua! Kumbe, haya ni hayo mliyoyahimiza, ni upepo ndani yake imo adhabu chungu!
تُدَمِّرُ كُلَّ شَيْءٍ بِأَمْرِ رَبِّهَا فَأَصْبَحُوا لَا يُرَىٰ إِلَّا مَسَاكِنُهُمْ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْقَوْمَ الْمُجْرِمِينَ ﴿٢٥﴾
25. Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake. Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tunavyowalipa watu wakosefu.
وَلَقَدْ مَكَّنَّاهُمْ فِيمَا إِن مَّكَّنَّاكُمْ فِيهِ وَجَعَلْنَا لَهُمْ سَمْعًا وَأَبْصَارًا وَأَفْئِدَةً فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ سَمْعُهُمْ وَلَا أَبْصَارُهُمْ وَلَا أَفْئِدَتُهُم مِّن شَيْءٍ إِذْ كَانُوا يَجْحَدُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٢٦﴾
26. Na hakika tuliwamakinisha, sio kama tulivyowamakinisha nyinyi, Na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo; na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao, Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yakawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.
وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا مَا حَوْلَكُم مِّنَ الْقُرَىٰ وَصَرَّفْنَا الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢٧﴾
27. Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tuliziainisha Ishara ili wapate kurejea.
فَلَوْلَا نَصَرَهُمُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ قُرْبَانًا آلِهَةً بَلْ ضَلُّوا عَنْهُمْ وَذَٰلِكَ إِفْكُهُمْ وَمَا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٢٨﴾
28. Basi mbona wale waliowashika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na hivyo ndio uwongo wao na waliyokuwa wakiyazua.
HUD
Aya 21 -28
MAANA
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekitaja kisa cha Hud, katika Juz. 8 (7:65-72), Juz. 12 (11:50 -60), Juz. 19 (26: 123-140) na katika Juzuu nyinginezo zilizopita na zitakazofuatia. Kwa hiyo hapa tutaja kwa ufupi tu, kwa kutegemea yaliyokwishapita.
Na mtaje ndugu wa kina A’di, alipowaonya watu wake kwenye vilima vya mchanga.
Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Hud na watu wake, ili wapate mawaidha na mazingatio. Walikuwa ni waarabu kama watu wako, walikuwa na nguvu zaidi na mali, na nyumba zao zilikuwa karibu na mji wako, kwa vile waliishi kwenye vichuguu vya mchanga – sehemu ya Yemen iliyoshikana na Hijaz; kama ilivyosemekana.
Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake.
Makusudio ya waonyaji ni mitume. Maana ni kuwa waambie ewe Muhammad, kuwa vile vile Hud hakuwa Mtume wa mwanzo wala wa mwisho, bali Mwenyezi Mungu alituma mitume wengi kabla ya Hud na baada yake. Na alikuwa akiwaonya watu wake kwa maneno yale yale ya kila Nabii:
Kuwa msimwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu,
ikiwa mtabakia na upotevu na shirki mliyo nayo.
Wakasema: Je, umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
Yaani wewe Hud unataka tuache kuabudu masanamu na tuabudu Mungu mmoja, si ni jambo la ajabu hili! Tena unatuhofisha na adhabu, si utuletee haraka basi ikiwa vitisho vyako ni vya kweli?
Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Mimi ninawafikishia niliyotumwa, lakini ninawaona kuwa nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.
Mola wangu ameniamarisha niwaonye na adhabu, basi nikatii amri, nikawaonya. Ama kuwa lini itatokea adhabu hiyo, ni ya aina gani au ikoje, anaiujua Mwenyezi Mungu tu, mimi sijui lolote katika hayo. Isipokuwa nina uhakika kabisa kuwa nyinyi ni watu mliozama kwenye ujinga na upotevu.
Basi walipoliona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili ni la kutunyeshea mvua!
Waliidhania adhabu kuwa ni mawingu, wakafurahi kuwa watanyeshewa mvua, Kwa hiyo wakabashiriana kupata rutuba na mavuno.
Basi Hud akawaambia au hali halisi ikaonyesha:
Kumbe, haya ni hayo mliyoyahimiza, ni upepo ndani yake imo adhabu chungu! Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake.
Wakaona mawingu angani ambayo dhahiri yake ni rehema na undani wake ni adhabu, wakadanganyika na dhahiri na wakaghafilika na yanayojificha yanayokuja ghafla. Basi adhabu ikawanyakua wakiwa wamelewa amani na matamanio. Huu ndio mwisho wa mwenye kuyatii matamanio yake.
Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu
amabazo zimekuwa ni makaburi ya miili yao. Mwenye akili ni yule anayepata mawaidha na mfano wa watu hawa, akahofia mashiko ya Mwenyezi Mungu wakati wa nema na raha na akatarajia rehema yake wakati wa shida na karaha.
Hivyo ndivyo tunavyowalipa watu wakosefu
duniani na Akhera au Akhera peke yake kulingana na inavyotaka hikima yake.
Na hakika tuliwamakinisha, sio kama tulivyowamakinisha nyinyi.
Tuliwaangamiza akina A’d walipoasi na kupetuka mipaka, na tulikuwa tumewapa nguvu na mali kwa namna ambayo hatukuwapa nyinyi mfano wake enyi vigogo wa kikuraishi. Hivi hamuogopi kuwapata yaliyowapata A’d na wengineo katika uma zilizopita?
Na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo;
kama tulivyowapa nyinyi,na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao,
kwa sababu hawakunufaika nayo, bali walikuwa kama wendawazimu, viziwi, mabubu na vipofu kwenye ukumbusho na hadhari.
Basi enyi watu wa Makka msighurike na masikio, macho na akili zenu. Kwani yote hayo hayawatafaa kitu itakaposhuka adhabu.
Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yakawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.
Waliipinga haki pamoja na dalili zake na wakaidharau na watu wake. Wakaingia kwenye uovu na upotevu; malipo yao yakawa ni maangamizi na kuvunjika.
Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tuliziainisha Ishara ili wapate kurejea.
Maneno yanaelekezwa kwa washirikina wa Makka. Makusudio ya miji ni watu wa miji hiyo ambao ni akina A’d na Thamud na wanaopakana nao.
Kuzianisha Ishara ni kuwabainishia aina za dalili na mawaidha, na walihadharishwa kwa kauli na vitendo ili wawaidhike na wakome, lakini wakakataa isipokuwa ukafiri, basi ikawathibitikia adhabu na wakabomolewa kabisa.
Basi mbona wale waliowashika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa wawakurubishe,
kwa Mwenyezi Mungu,hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na hivyo ndio uwongo wao na waliyokuwa wakiyazua.
‘Hivyo’ ni hivyo kutookoa masanamu na kwamba hayamsaidii aliyekuwa akiyaabudu wakati wa dhiki. Maana ni kuwa kauli ya washirikina kuwa sanamu ni muombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu na muokozi wetu, ni uzushi.
وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِم مُّنذِرِينَ ﴿٢٩﴾
29. Na tulipokuletea kundi la majini kusikiliza Qur'an. Basi walipoihudhuria walisema: Nyamazeni! Na ilipomalizwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.
قَالُوا يَا قَوْمَنَا إِنَّا سَمِعْنَا كِتَابًا أُنزِلَ مِن بَعْدِ مُوسَىٰ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ وَإِلَىٰ طَرِيقٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٣٠﴾
30. Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinachoongoza kwenye Haki na kwenye Njia iliyonyooka.
يَا قَوْمَنَا أَجِيبُوا دَاعِيَ اللَّـهِ وَآمِنُوا بِهِ يَغْفِرْ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُجِرْكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣١﴾
31. Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na mumwamini, Mwenyezi Mungu atawasamehe, na atawakinga na adhabu chungu.
وَمَن لَّا يُجِبْ دَاعِيَ اللَّـهِ فَلَيْسَ بِمُعْجِزٍ فِي الْأَرْضِ وَلَيْسَ لَهُ مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءُ أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٣٢﴾
32. Na asiyemwitikia mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hatashinda katika ardhi, wala hatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhahiri.
MAJINI WANASIKILZA QUR’AN
Aya 29 – 32
MAANA
Na tulipokuletea kundi la majini kusikiliza Qur’an. Basi walipoihudhuria walisema: Nyamazeni! Na ilipomalizwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.
Miongoni mwa wadhifa wa akili ni kuhukumu uwezekeano wa kuweko kitu au kutokuweko. Ikihukumu uwezekano wa kuweko, basi inakimbilia kuthibitisha kuweko kwake kwa kutumia nyenzo, zinazoafikiana na maumbile ya kitu kinachotakiwa kuthibitishwa, kwa hisia na majaribio.
Kikiwa ni katika mambo ya kiakili, basi njia yake itakuwa ni akili. Na kikiwa ni katika mamabo ya ghaibu –sio kuweko Mungu – basi njia yake itakuwa ni wahyi tu. Ukielezea basi itakuwa ni lazima kukubaliana nao.
Hakuna mwenye shaka kwamba akili haikatai kuweko viumbe vilivyo mbali nasi na vinavyotofautiana na tunayoyajua na tuliyoyazoea. Bali tuna uhakika kuwa tusiyoyajua ni mengi zaidi kuliko tunayoyajua; miongoni mwa hayo ni majini. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyataja katika Aya kadhaa; kama vile:
وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ﴿١١﴾
“Na hakika katika sisi wako wema na wengine katika sisi ni kinyume na hayo.” (72:11).
Mwenyezi Mungu alipeleka kundi katika hao wema kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.
w
)
, wakamsikia akisoma Qur’an, wakaanza kuambiana: ‘Hebu nyamazeni na mzingatie maana yake.’ Basi wakanyamaza na kusikiliza kwa makini. Wakaona uongofu na nuru, wakamwamini Muhammad(s.a.w.
w
)
. Mtume alipomaliza kusoma walirudi haraka kwa watu wao kuwaonya na kuwapa bishara ya Uislamu.
Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinachoongoza kwenye Haki na kwenye Njia iliyonyooka
Waliwaambia watu wao kuwa tumesikia Kitabu kutoka kwa Muhammad(s.a.w.
w
)
kinachofanana na kile alichoteremshiwa Musa, nacho kinasadikisha yale waliyokuja nayo manabii, ya kuamini tawhid na ufufuo. Vile vile kinaongoza kwenye usawa na kufanya heri:
فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا ﴿١﴾ يَهْدِي إِلَى الرُّشْدِ فَآمَنَّا بِهِ وَلَن نُّشْرِكَ بِرَبِّنَا أَحَدًا ﴿٢﴾
“Wakasema: hakika tumesikia Qur’an ya ajabu. Inaongoza kwenye uwongofu kwa hiyo tumeiamini na hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.” (72:1-2).
Ikiwa sisi hatujawaona majini walioathirika na Qur’an na kuiamini, lakini tumewaona wataalamau na watu wenye akili wengi wakiathirika na matamshi ya Qur’an kwa kiasi cha kusikia matamshi yake tu; tena wakaamini imani isiyokuwa na shaka kuwa inatoka kwa Mwenye hekima Mjuzi.
Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na mumwamini, Mwenyezi Mungu atawasamehe, na atawakinga na adhabu chungu.
Itikieni mwito wa haki na mumfuate anayeutoa mwito huo; Mwenyezi Mungu atawasamehe dhambi zenu na atawaingiza katika rehema yake na kuwaokoa na ghadhabu yake na adhabu yake.
Na asiyemwitikia mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hatashinda katika ardhi, wala hatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhahiri.
Hakuna kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa kwake tu wala hakuna kuokoka na adhabu yake isipokuwa kwa ikhlasi na matendo mema.
Hao wamo katika upotevu ulio dhahiri.
‘Hao’ ni hao wasioitikia mwito wa Mwenyezi Mungu, na asiyemwitikia atakuwa ameiacha njia ya haki na uongofu.
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٣٣﴾
33. Je, hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliyeziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwa nini? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَلَيْسَ هَـٰذَا بِالْحَقِّ قَالُوا بَلَىٰ وَرَبِّنَا قَالَ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na siku makafiri watakapoonyeshwa Moto, Je, haya si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyokuwa mkikataa.
فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ وَلَا تَسْتَعْجِل لَّهُمْ كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّن نَّهَارٍ بَلَاغٌ فَهَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٣٥﴾
35. Basi subiri, kama walivyosubiri Mitume wenye azma, Wala usiwahimizie. Siku watakayoyaona waliyoahidiwa, itakuwa kama kwamba hawakukaa ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa isipokuwa walio watu mafasiki?
JE, HAYA SI KWELI?
Aya 33 – 35
MAANA
Je, hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliyeziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwa nini? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Ulimwengu huu wa ajabu unajulisha uweza wa muumba na ukuu wake. Vile vile unajulisha, tena kwa njia bora, kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ana uwezo wa kuwafufa wafu. Kwa vile sabu inayoleta mambo hayo mawili ni moja, ambayo ni uweza wa mwenye kukiambia kitu ‘kuwa’ na kikawa. Imam Ali
anasema:“Namshangaa anayekanusha ufufuo wa pili na hali anaona ufufuo wa kwanza!”
Maana ya Aya hii yametangulia katika makumi ya Aya na yatakuja mengine mengi; miongoni mwayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, tulichoka kwa umbo la kwanza?” (50:15). Basi tutachoka vipi na umbo la pili?
Na siku makafiri watakapoonyeshwa Moto,
yaani watakapoadhibiwa na kuaambiwa:Je, haya,
mliyokuwa mkiyakanusha hapo mwanzo,si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu!
ni kweli.
Walikanusha duniani ambapo kunawadhuru kukana na wamekubali Akhera ambapo hakuwanufaishi chochote kukiri kwao.
Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu mlikuwa mkikataa;
bali mliwadharau wale walioamini hisabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Na ungeliona watakaposimamishwa mbele ya Mola wao, Akasema: Je, si kweli haya? Watasema: Kwa nini? Tunaapa kwa Mola wetu. Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakataa.” Juz. 7 (6:30).
Basi subiri, kama walivyosubiri Mitume wenye azma,
Kwenye tafsiri nyingi imeelezwa kuwa mitume wenye azma (Ululu-azm) ni watano: Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Muhammad. Kila mmoja wao alikuwa na sharia mahususi aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu kutumiwa na viumbe wote wakati wake mpaka afike mtume mwingine kati ya hao watano.
Akija anafuta sharia ya yule aliyemtangulia katika wale watano, mpaka kufikia sharia ya Muhammad(s.a.w.
w
)
, Bwana wa mitume na mwisho wa manabii. Hiyo haiwezi kufutwa hadi siku ya kiyama. Ama manabii wengine wasiokuwa hao ululu-azm, walikuwa wakitumia sharia ya waliyemtangulia katika hao watano.
Kuna riwaya za Ahlul-bayt zinazozungumzia hili na kuashirwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ﴿١٣﴾
“Amewapa sharia ya Dini aliyomuusia Nuhu na tuliyokupa wahyi wewe, na tuliyowausia Ibrahim na Musa na Isa,” Juz. 25 (42:13).
Ambapo amewahusu kuwataja hao watano na kutaja neno sharia. Na ‘wewe’ ni wewe Muhammad.
Wala usiwahimizie adhabu. Siku watakayoyaona waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa ulimwenguni ila saa moja ya mchana.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.
w
)
, na wanaoambiwa ni wale walioikanusha risala yake. Makusudio ya yale mliyoahidiwa ni adhabu ya Jahannam. Maana ni kuwa usifanye haraka ewe Muhammad(s.a.w.
w
)
ya kutaka wale waliokufuru waadhibiwe, kwa sababu itawapata tu huko Akhera. Huku kukaa kwao duniani hata kukirefuka, lakini watapoiona adhabu wataona kama kwamba ni kitambo kidogo tu.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿١٩٧﴾
“Ni starehe ndogo. Kisha makazi yao ni Jahannam ni mahali pabaya pa kushukia.”
Juz. 4 (3:197).
Imam Ali
anasema:“Hakika dunia ni starehe za siku kidogo, zinaondoka kama yanavyoondoka mangati au kama yanavyopotea mawingu.”
Huu ndio ufikisho!
Yaani Qur’an ni ufikisho wa risala za Mwenyezi Mungu Mtukufu, nayo ni hoja tosha ya mawaidha yake na ni ponyo kwa anayetaka mwongozo na uongofu.
Kwani huangamizwa wengine isipokuwa walio watu mafasiki?
Hapana!
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ ﴿٥١﴾ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٥٢﴾
“Hakika wenye takua watakuwa katika mahali pa amani. Katika mabustani na chemchem.”
Juz. (44:51-52).
MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA SITA: SURAT AL-AHQAF