6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا ﴿٢٤﴾
24. Je, Hawaizingatii hii Qur’an? Au kwenye nyoyo zipo kufuli?
إِنَّ الَّذِينَ ارْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِهِم مِّن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَى الشَّيْطَانُ سَوَّلَ لَهُمْ وَأَمْلَىٰ لَهُمْ ﴿٢٥﴾
25. Kwa hakika ambao wanarudi kwa migongo yao baada ya kuawabainikia uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewachelewesha.
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لِلَّذِينَ كَرِهُوا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ سَنُطِيعُكُمْ فِي بَعْضِ الْأَمْرِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِسْرَارَهُمْ ﴿٢٦﴾
26. Hayo ni kwa sababu waliwaambia waliochukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu: Tutawatii katika baadhi ya mambo. Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.
فَكَيْفَ إِذَا تَوَفَّتْهُمُ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ ﴿٢٧﴾
27. Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao!
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّـهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ ﴿٢٨﴾
28. Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha. Basi akaviangusha vitendo vyao.
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَن لَّن يُخْرِجَ اللَّـهُ أَضْغَانَهُمْ ﴿٢٩﴾
29. Je, ambao wana maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?
وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُم بِسِيمَاهُمْ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ ﴿٣٠﴾
30. Na lau tungelipenda, tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao. Na bila ya shaka utawajua kwa namna ya usemi Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.
وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ ﴿٣١﴾
31. Na bila ya shaka tutawajribu mpaka tuwajue wapignao jihadi katika nyinyi na wanaosubiri. Nasi tutazijaribu habari zenu.
JE HAWAIZINGATI QUR’AN?
Aya 24 – 31
MAANA
Je, Hawaizingatii hii Qur’an? Au kwenye nyoyo zipo kufuli?
Wanaambiwa wanafiki. Kwa sababu Aya hii na ilie iliyo kabla yake inawazungumzia wao. Dalili zote zilizokuja katika Qur’an, za kuweko Mwenyezi Mungu katika kuumbwa mbingu na ardhi, hoja wazi za utume wa Muhammad(s.a.w.
w
)
.
Ubaya wa shirki, dhulma na ufisadi katika ardhi, yote hayo yako wazi hayakufumbwafumbwa; kuongezea athari ya mfumo wa Qur’an katika moyo wa msomaji na msikilizaji anavyopata hisia. Basi makafiri wananini hawaathiriki na muujiza huu? Je, wamekosa usikizi na macho au nyoyo zao zimefungwa na kufuli na kutu.
Kwa hakika ambao wanarudi kwa migongo yao baada ya kuawabainikia uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewachelewesha.
Neno kurudi tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu Irtaddu (kuritadi) lenye maana ya kuamini haki kisha kuikanusha. Pia kuijua haki kwa dalili mkataa kisha kuikanusha kwa matamanio ya nafsi, kunaingia katika hukumu ya kuritadi, kwa sababu kuijua haki ni sawa na kuiamini na kuichukia ni sawa na kuiritadi.
Ama mwenye kuficha ukafiri na akadhihirisha imani huyo ni mnafiki na murtadi vile vile. Ni mnafiki kwa vile amedhihirisha kinyume na yaliyo moyoni mwake na ni murtadi kwa kuwa duniani anakuwa kama mumin na Akhera anakuwa kafiri; kama kwamba yeye ni mumin na wakati huo huo ni murtadi.
Tamko la Aya limegusia aina zote tatu. Kwa sababu dalili za dhahiri zilizosimaia kwenye Tawhid, ufufuo na utume wa Muhammad(s.a.w.w)
ndio hoja aliyoikusuduia Mwenyezi Mungu kwa kusema: ‘Baada ya kuwabainikia uongofu,’ lakini shetani aliwadanganya kwa unafiki na kuiritadi haki na kuipinga. Akawaahidi ahadi ya uwongo na kuwatia wasiwasi wa tamaa na matamanio.
Hayo ni kwa sababu waliwaambia waliochukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu: Tutawatii katika baadhi ya mambo.
Waliosema ni wanafiki na waliochukia ni mayahudi waliokuwa majirani wa Mtume. Kwa sababu mayahudi ndio watu wanaochukia zaidi kila kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu; hasa Qur’an. Maana ni kuwa wanafiki waliwambia mayahudi: sisi tuko pamoja na nyinyi kuhusu Muhammad na tunashirikiana nanyi katika kumpiga vita; isipokuwa hali haituruhusu kutangaza uadui wetu kwake. Kwa hiyo tuacheni tujionyeshe kuwa ni waislamu na tutakuwa pamoja nanyi kwenye njama dhidi yake.
Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.
Yaani siri za mayahudi na za wanafiki, kwa sababu kwake hakifichiki chochote katika ardhi wala mbinguni.
Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao!
Wamekimbia jihadi kwa kuogopa mauti, je wataweza kuyakimbia mauti na mapigo yake? Na ufufuo na vituko vyake.
Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaadhibu wakati wa mauti na baada yake vile vile, kwa vile waliathirika na yale yanayomchukiza Mwenyezi Mungu kuliko yale yanayomridhisha.
Basi akaviangusha vitendo vyao,
havitawafaa kitu.
Je, ambao wana maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?
Wanafiki walificha chuki na uadui kwa Mtume na maswahaba; wakawadhihirishia upendo na utii; wakadhani kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatadhihirisha wanayoyaficha vifuani mwao.
Na lau tungelipenda tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao.
Kukuonyesha ni kukutambulisha na kutambua ni kuwatambua kwa alama zao. Lengo la kugawanya huku kunakofanana na kukaririka ni kusisitiza kuwa Mtume hapitwi na kitu anachofahamishwa na Mwenyezi Mungu. Lakini asiyekuwa Mtume anaweza kukosea katika kufahamu kwake.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa ilishuka kabla ya Mtume kuwafahamu wanafiki, kutokana na neno ‘lau,’ lakini Mtume(s.a.w.w)
aliwatambua baadae kutoka na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na bila ya shaka utawajua kwa namna ya usemi
wao.
Namna ya usemi ni kule kumaanisha kwake; kama vile udhuru wa uwongo waliokuwa wakiutoa wanafiki na jinsi wanavyowalaumu watu wema na kuwasifu washari na mengineyo yanayojiachia mdomoni yanayaofahamisha ria na unafiki.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Anas: “Hakufichika mnafiki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
, baada ya Aya hii.” Vile vile Nabii(s.a.w.w)
alikuwa akiwajuwa wanafiki kwa vitendo vyao. Walikuwa wakiikimbia jihadi na wakiona uzito kujitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.
Hili ni kemeo kwa kila anayedhihirisha heri na kuficha shari.
Na bila ya shaka tutawajaribu mpaka tuwajue wapignao jihadi katika nyinyi na wanaosubiri. Nasi tutazijaribu habari zenu.
Mwenyezi Mungu anawajua wanaopigana jihadi na walio na subira kabla ya kuwafanyia majaribio, lakini anafanya hivi kwa kuamrisha na kukataza ili amdhihirishe na amtambulishe muovu na mwema kwa vitendo ambavyo vinastahiki adhabu au thawabu.
Imeelezwa katika Nahjul-balagha: “Mwenyezi Mungu anataka mumnusuru na hali yeye ana majeshi ya mbinguni na ardhini na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima. Na anataka mukopeshe na Yeye ana hazina za mbingu na ardhi na Mwenye kujitosha Mwenye kusifiwa…Anataka kuwajaribu ninani wenu mwenye matendo mema zaidi.
Basi harakisheni matendo yenu mtakuwa jirani na Mwenyezi Mungu.”
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَشَاقُّوا الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَىٰ لَن يَضُرُّوا اللَّـهَ شَيْئًا وَسَيُحْبِطُ أَعْمَالَهُمْ ﴿٣٢﴾
32. Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wakakinzana na Mtume baada ya kuwabainikia uwongofu, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote, na ataviangusha vitendo vyao.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ ﴿٣٣﴾
33. Enyi ambao mmeamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume; wala msiviharibu vitendo vyenu.
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ مَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ﴿٣٤﴾
34. Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria.
فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّـهُ مَعَكُمْ وَلَن يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ ﴿٣٥﴾
35. Basi msilegee na kuita kwenye suluhu. Na hali nyinyi ndio mko juu; Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi, Wala hatawanyima malipo ya vitendo vyenu.
إِنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا يُؤْتِكُمْ أُجُورَكُمْ وَلَا يَسْأَلْكُمْ أَمْوَالَكُمْ ﴿٣٦﴾
36. Hakika uhai wa duniani ni mchezo na upuzi. Na mkiamini na mkawa na takua, atawapa ujira wenu, Wala hawaombi mali zenu.
إِن يَسْأَلْكُمُوهَا فَيُحْفِكُمْ تَبْخَلُوا وَيُخْرِجْ أَضْغَانَكُمْ ﴿٣٧﴾
37. Akiwaomba hizo na akiwashikilia mtafanya ubakhili, na atatoa chuki zenu.
هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَمِنكُم مَّن يَبْخَلُ وَمَن يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَن نَّفْسِهِ وَاللَّـهُ الْغَنِيُّ وَأَنتُمُ الْفُقَرَاءُ وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم ﴿٣٨﴾
38. Ehee! Nyinyi mnaitwa mtumie katika njia ya Mwenyezi Mungu, Na wapo katika nyinyi wanaofanya ubakhili. Na anayefanya ubakhili basi anajifanyia ubakhili mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, na nyinyi ndio wahitaji. Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.
MSIBATILISHE AMALI ZENU
Aya 32 – 38
MAANA
Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wakakinzana na Mtume baada ya kuwabainikia uwongofu, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote, na ataviangusha vitendo vyao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
alilingania kwenye Uislamu kwa dalili na ubainifu; wakakaukataa watu wa masilahi na wakawazuia watu wasiukubali Uislamu kwa kutumia nguvu, mali na propaganda za uwongo.
Lakini Mwenyezi Mungu alimpa nguvu Mtume wake, akaidhihirisha dini yake na akaviangusha vitendo vya wahaini.
Hadi leo Uislamu na waislamu wanakabiliana sana na nguvu za shari. Zilizo hatari zaidi ni baadhi ya dola zinazobeba jina la Uislamu huku zikishirikiana na adui mkubwa zaidi, mkoloni wa kizayuni. Umefika wakati, sasa, waislamu waondoe vumbi la chuki na mfarakano ili waweze kuungana pamoja dhidi ya adui yao mwenye ushirikiano na wenzake.
Enyi ambao mmeamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake!Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume;
yaani fanyeni mambo kwa imani yenu.
Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Mtiini Mwenyezi Mungu,’ baada ya kusema: ‘Enyi ambao mmeamini,’ ni sawa na kauli yake:
فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا ﴿١١٠﴾
“Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake basi naatende matendo mema.” Juz. 16: (18:110).
Wala msiviharibu vitendo vyenu
kwa shirki na unafiki wala kwa masimbulizi na udhia au kwa maovu ambayo huondoa mema. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴿٢٧﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu.” Juz. 6 (5:27).
Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu hakubali matendo ila kwatakua.” Imam Ali
anasema:“Kwenye matendo, kuweni ni wenye kujishughulisha zaidi na kukubaliwa matendo.”
Hakika ambao wamekufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria
huko Akhera. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawafufua watu kulingana na walioyofia na atawahisabu kulingana na walivyomaliza uhai wao kwenye ukafiri au imani.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:161) na Juz. 3 (3:91).
QUR’AN NA SIASA YA VITA
Basi msilegee na kuita kwenye suluhu.
Matukio yamethibitisha kwamba mwenye kulegea mbele ya adui yake na akaogopa kumkabili basi ndio amempa silaha atayompigia na kujifanya mnyonge kwake. Imam Ali
anasema:“Kuogopa ni kuvunjika moyo na kuona haya ni kusumbuka.”
Tazama Juz. 22 (33: 59-62) kifungu ‘Vita vya nafsi.’
Siasa nzuri ya vita ni kuwa mkakamavu mtu mbele ya adui yake, vile vile asipuuze nguvu za adui, bali ajiandae vizuri na amkabili kwa uimara kabisa bila ya kujali mashaka na tabu atakayoipata.
Qur’an imeandika siasa hii kwa kusema: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu.” Yaani msilegee mbele ya adui mkasalimu amri kwenye nguvu zao na utaghuti wao.
Pia kauli yake: “Na waandalieni nguvu vile muwezavyo.” Juz. 10 (8:60). Yaani msidharau nguvu zao; mjifunge kibwebwe kwa kila nguvu mliyo nayo ya watu na ya kiuchumi.
Na hali nyinyi ndio mko juu;
yaani mtashinda, lakini mpaka muungune na kuwa safu moja kumkabili adui wenu na adui wa Mwenyezi Mungu; vinginevyo mtashindwa na haitabakia hata harufu yenu; kama inavyosema Qur’an katika Juz. 10 (8:46).
Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi,
mkiitikia mwito wake wa jihadi kwa hali na mali, ili tamko la Mwenyezi Mungu liwe juu ili neno la haki liwe juu na neno la batili liwe chini. Ama yule mwenye kupenda raha na akasalimu amri kwenye nguvu ya upotevu na ufisadi, basi Mwenyezi Mungu ataachana naye na kumwachia aliyejisalimisha naye
Wala hatawanyima
malipo yavitendo vyenu
kuanzia nafsi, watu au mali iliyotoka kwa ajili ya dini, nchi au haki yoyote. Muhanga huu hauwezi kwenda burebure; bali ni heshima ya dini na nchi katika maisha ya duniani na ni akiba Akhera mbele ya Mwenyezi Mungu.
Unaweza kuuliza
: Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu na hali nyinyi ndio mko juu,” si inajulisha waziwazi kwamba mwenye nguvu anafaa kumdhibiti mnyonge bila ya kuwa na huruma naye wala kuwa na suluhu naye? Bila shaka hili linapingana na ubinadamu na uadilifu, wala haliafikiani na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً ﴿٢٠٨﴾
“Enyi ambao mmeamini! Ingieni kwenye usalama nyote” Juz. 2 (2:208)?
Jibu
: kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Basi msilegee na kuita kwenye suluhu na hali nyinyi ndio mko juu,” maana yake ni ikiwa mtapata balaa ya adui aliye mnyama asiyekuwa na kipimo cha haki wala uadilifu wala hajilazimishi na kanuni wala ahadi na pia hafahamu lugha yoyote isipokuwa nguvu. Mkifikiwa na adui wa aina hii basi nilazima mkabiliane; msimwogope wala msiwe na huruma katika haki. Kummaliza adui huyu ni kuimaliza shari na kuleta heri ya wote.
Ajabu ya sadfa! Imetokea wakati nikiandika maneno haya leo hii 8 April 1970, Israil, ikitumia ndege aina Phantoum ya Amerika na makombora yake, imeshambulia shule ya msingi ya Bahrul-baqar katika Jamhuri ya Umoja wa Kiarabu [3]
1, na kuua watoto 47, na kujeruhi kadhaa, wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 12.
Bila shaka U.S.A. ndiyo inayobeba majukumu ya kuuliwa watoto wadogo wasiokuwa na hatia yoyote. Na pia majukumu ya mashambulizi ya mfano huo yaliyotokea katika kiwanda cha Aba Za’abal yaliyowaacha wahanga 33 majeruhi na waliouawa.
Amerika ndio yenye majukumu, kwa vile ndiyo iliyoisheheni Israil kwa silaha na mali na ikaamrisha iwafanyie waarabu; kama hiyo yenyewe inavyoifanyia Vietnam. Vyombo vya habari vimenukuu kuwa jeshi la Amerika limesambaratisha mji mzima katika Vietnam. Hakuokoka katika mji huo mtoto wala mwanamke. Mji huu na mashule yake unahusiana vipi na vita?!
Je, usalama utakuweko na wanyama hawa? Jamani! Pengine labda maana ya usalama yawe ni kusalimu amri kwa madhalimu na waasi!
Hakika uhai wa duniani ni mchezo na upuzi
kwa mwenye kuipondokea na akahadaika na ubatilifu wake; bali ni shari hasa kwa mwenye kuanzisha vita kwa ajili ya dunia. Na ni nyumba ya heri kwa mwenye kuwaidhika nayo na akaifanya ni maandalizi ya Akhera yake.
Na mkiamini na mkawa na takua atawapa ujira wenu.
Kuunganisha takua na imani kunafahamisha kuwa kuamini tu na kusadikisha hakuna malipo mbele ya Mwenyezi Mungu; bali hapana budi kuweko na vitendo pamoja na imani. Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿٣٠﴾
“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri.”Juz. 15 (18:30)
Wala hawaombi mali zenu. Na akiwaomba hizo na akiwashikilia mtafanya ubakhili, na atatoa chuki zenu.
Makusudio ya hawaombi ni hawataki mtoe mali yote wala kutoa mali nyingi ya kuwadhuru. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejaalia fungu la mafukara katika mali ya matajiri na akachunga kiwango cha kutosheleza mahitaji na vile vile masilahi ya watowaji wasidhurike.
Lau kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hekima yake, angeliwataka matajiri zaidi kiwango hiki na akawahimiza kutoa, basi wangelizuia na wangekua na chuki na Uislamu na Nabii.
Ehee! Nyinyi mnaitwa mtumie katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa Makusudio ya njia ya Mwenyezi Mungu ni jihadi. Usahihi ni kuwa inakusanya kila lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi ya watu kwa namna moja au nyingine.
Na wapo katika nyinyi wanaofanya ubakhili. Na anayefanya ubakhili basi anajifanyia ubakhili mwenyewe.
Bakhili anamnyima Mwenyezi Mungu na kujilimbikizia mwenyewe, lakini natija inakuwa kinyume na anavyotaka; pale anapoiweka nafsi yake kwenye ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na kuinyima radhi zake na thawabu zake. Tazama kifungu; ‘Mali ndio sababu ya ugomvi’ mwanzo wa Juz. 4 (3:92).
Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, na nyinyi ndio wahitaji
wa fadhila zake na rehma zake. Hakupata ukwasi mja yeyote ila kwa sababu inayotoka kwake. Ama Yeye Mwenyezi Mungu ni mkwasi kwa dhati yake sio kwa kufaidika, ni mtendaji sio kwa kutumia ala, na ni mkadiriaji sio kwa kufikiria.
Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.
Kama mkiupinga mwito wa Mwenyezi Mungu na mkang’ang’ania uasi na ujeuri basi atawaondoa na awalete wengine watakaomsabihi na kumsifu bila ya kumuasi na lolote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14:19) na Juz. 22 (35:16).
MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA SABA: SURAT MUHAMMAD