TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 28296
Pakua: 3893


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 28296 / Pakua: 3893
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Ya Arubaini Na Nane: Surat Al-Fath. Imeshuka Makka. Ina Aya 29.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا ﴿١﴾

1. Hakika tumekupa ushindi wa dhahiri

لِّيَغْفِرَ لَكَ اللَّـهُ مَا تَقَدَّمَ مِن ذَنبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ وَيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَيَهْدِيَكَ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا ﴿٢﴾

2. Ili Mwenyezi Mungu akughufirie dhambi yako iliyotangulia na ijayo, na akutimizie neema zake, na akuongoze katika njia iliyonyooka.

وَيَنصُرَكَ اللَّـهُ نَصْرًا عَزِيزًا ﴿٣﴾

3. Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu.

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ وَلِلَّـهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿٤﴾

4. Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili wazidi imani juu ya imani yao. Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima.

لِّيُدْخِلَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَيُكَفِّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَكَانَ ذَٰلِكَ عِندَ اللَّـهِ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٥﴾

5. Ili awaingize waumini wanaume na waumini wanawake katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake, wadumu humo, na awafutie maovu yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

TUMEKUPA USHINDI

Aya 1 – 5

MAANA

Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri.

Neno ‘ushindi’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ‘Fat-h’ ambalo lina maana nyingine zaidi ya hiyo. Lakini Makusudio yake hapa ni ushindi, kwa sababu ndiyo yanayokuja akilini mwanzo, na pia kwamba Nabii(s.a.w. w ) alisema:“Nimeteremshiwa Aya inayopendeza zaidi kwangu kuliko dunia na yaliyomo . Kisha akasoma: “Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri”. Maana ni kuwa tumekupa ushindi ewe Muhammad ushindi wa dhahiri.

Wametofautiana wafasiri kuhusu aina ya ushindi wenyewe. Tabariy ameishilia na kauli nne na Razi akaishilia na tano. Wafasiri wengi wamesema kuwa Makusudio ya ushindi hapa ni ushindi wa Suluhu ya Hudaybiya. Kwa sababu sura hii ilishuka baada ya mkataba wa amani aliowekeana Mtume na watu wa Makka, sehemu ya Hudaybiya.

Hata hivyo kauli iliyo na nguvu kwetu ni kuwa Makusudio ya ushindi hapa ni kuwa juu Uislamu, kuwa na nguvu waislamu na kudhalilika maadui wake wanafiki na washirikina. Kwa sababu ushindi katika Aya ni wa kiujmla haukufungwa na Hudaybiya, kuiteka Makka, kuwashinda waroma na wafursi au kwengineko.

Kwa hiyo basi Aya hii itakuwa inarudufu ile isemayo:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾

“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki, ili ipate kushinda dini zote, ijapokuwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33).

Kwa maneno mengine ni kuwa ushindi ni wa kiujmla sio wa kiaina.

Ili Mwenyezi Mungu akughufirie dhambi yako iliyotangulia na ijayo.

Unaweza kuuliza : lini Nabii alifanya dhambi mpaka asamehewe na Mwenyezi Mungu? Iko wapi isma ya manabii ya kuepukana na dhambi? Itakuwaje ushindi ndio iwe sababu ya maghufira? Kuna uhusiano gani baina ya ushindi na maghufira?

Jibu : Makusudio ya dhambi hapa sio dhambi ya Mtume kiuhakika na kiuhalisi. Itakuwaje na hali yeye ni mwenye kuhifadhiwa na madhambi na makosa. Makusudio ni kuwa washirikina wlikuwa wakiamini kuwa Mtume ana dhambi kutokana na mwito wake wa Tawhid, mwito wa kutupiliwa mbali ushirikina na kupiga vita kuiga waliopita.

Ama Makusudio ya maghufira ni kuwa washirikina hawa walikuja kugundua kuwa Muhammad(s.a.w. w ) hana dhambi na kwamba yeye ni Mtume wa kweli na wa haki na wao ndio waliokuwa na dhambi kwa kumtuhumu na risala yake.

Yaani Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alitoa mwito wa Tawhid akikosoa ibada ya masanamu na kupiga vita dhulma na unyanyasaji na mengine ya ufisadi wa kijahilia na maigizo yake. Ni dhambi gani iliyokubwa zaidi kwa jahili na wengineo kuliko kumkosoa na kumtia ila na vitu vyake vitakatifu vya kidini na ada ya mababu zake ambayo ndio desturi yake?

Lakini baada Mwenyezi Mungu kuidhihirisha dini yake na kumnusuru Nabii wake kwa dalili na hoja na kuingia watu kwenye dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi, wakiwemo washirikina waliokuwa wakimuona Mtume ni mwenye hatia kwao na kwa miungu yao, iliwabainikia kuwa Muhammad(s.a.w. w ) ni mkweli na wao ni wakosefu.

Kwa ufupi ni kuwa makusudio ya dhambi ya Mtume ni dhambi yake kwa madai ya maadui zake washirikina, sio dhambi halisi. Na makusudio ya msamaha ni msamaha wao kwa lile walilodai kuwa ni dhambi; yaani toba yao kwa walivyomdhania Mtume.

Ama kuinasibisha dhambi kwa Mtume, katika dhahiri ya maneno, na kunasibisha msamaha kwa Mwenyezi Mungu, hilo ni jambo sahali, kwamba majazi yanatoa upeo wa hilo na zaidi.

Kuhusu uhusiano wa ushindi na maghufira, uko wazi – kwamba ushindi ndio sababu ya kufichuka ukweli wa Mtume na kuepuka kwake dhambi – iliyodaiwa - waliyomtuhumu nayo washirikina kabla ya ushindi.

Na akutimizie neema zake kwa kukupa ushindi dhidi ya madui zako na kuinua shani yako duniani.

Na akuongoze katika njia iliyonyooka ambayo ni sharia ya Mwenyezi Mungu inayodhamini heri ya watu na masilahi yao, kila wakati na kila mahali.

Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu.

Nusura yenye nguvu ni ile inayokuwa kwa haki na kwa ajili ya haki na kwa jihadi iliyowekewa sharia sio kwa njama au mapinduzi wala kwa msaada wa waovu.

Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za waumini ili wazidi imani juu ya imani yao.

Makusudio ya utulivu ni kuridhia na kutulia kimwamko. Kwa sababu matukio yametuonyesha kuwa utulivu wa kijahili unaishia pabaya. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameipa nguvu dini yake akampa ushindi Nabii wake ili wafurahi waumini, nyoyo zao zitulie, wazidi kuwa na yakini na Mola wao, wamtegemee Nabii wao na kuwa na nguvu katika dini yao.

Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi.

Hii ni kinaya cha ukuu wa uweza; vinginevyo Mwenyezi Mungu hahitajii walimwengu, kwa sababu Yeye ni kukiambia kitu kuwa kinakuwa.

Hapa kuna ishara kwamba lau Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaangamiza washirikina bila jihadi na vita, lakini ni kwa ajili ya kuwajaribu waja ili ajulikane nani mzuri zaidi wa matendo.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima katika kuumba kwake na kupangilia kwake.

Ili awaingize waumini wanaume na waumini wanawake katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake, wadumu humo, na awafutie maovu yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tabari anasema: iliposhuka “Hakika tumekupa Ushindi wa dhahiri,” waumini walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) : Pongezi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu amekwishakubainishia atakavyokufanyia, je na sisi? Ndio ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ili awaingize waumini wananume na waumini wanawake…” mpaka mwisho.

Hata kama riwaya itakuwa si sahihi, lakini hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu anasamehe maovu ya wanaoutubia na kuwangiza waumini katika rehema yake na pepo yake. Na atakayeingia Peponi atakuwa amefuzu fungu lenye kutosheleza.

وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ الظَّانِّينَ بِاللَّـهِ ظَنَّ السَّوْءِ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَلَعَنَهُمْ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَهَنَّمَ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿٦﴾

6. Na awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.

وَلِلَّـهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿٧﴾

7. Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima.

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿٨﴾

8. Hakika tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji.

لِّتُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُعَزِّرُوهُ وَتُوَقِّرُوهُ وَتُسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٩﴾

9. Ili mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mumsaidie, na mumhishimu, na mumsabihi asubuhi na jioni.

NA AWAADHIBU WANAFIKI

Aya 6 – 9

MAANA

Na awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.

Ubaya ni shari na ufisadi. Makusudio ya dhana mbaya kwa Mwenyezi Mungu ni kudhani kuwa, ambaye imetukuka hekima yake, hatafufua walio katika makaburi na kwamba hataunusuru uislamu na Nabii wa uislamu na mengineyo wanayoyadhania wanafiki na washirikina.

Maana kwa ujumla ni kuwa Mwenyezi Mungu, kama alivyowaandalia watu wa imani Peo yenye neema, vile vile amewaandalia wale waliomdhania vibaya, kama waanafiki na washirikana, shari itakayowazunguka kila upande, hasira, laana na mwisho mbaya – moto wa Jahannam usiokwisha wakafa wala hautapunguzwa.

Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliitaja Aya hii alipowaashiria watu wa imani na malipo yao katika Aya iliyotangulia. Hapa tena ameitaja akiwaashiria wanafiki na washirikina. Lengo la kukaririka huku ni kutanabahisha kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muweza wa kuwaneemesha na kuwaadhibu, ili mja amtii Mwenyezi Mungu kwa kutarajia thawabu zake na ajiepushe na kumuasi kuhofia adhabu yake.

Hakika tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji.

Kesho Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) atashuhudia mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba yeye amewafikishia waja yale aliyopewa wahyi, akawabashiria watiifu kuokoka na akawaonya waasi na maangamizi.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 22 (33:45).

Ili mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mumsaidie, na mumhishimu, na mumsabihi asubuhi na jioni.

Mumsaidie na mumhishimu ni Mtume. Imesemekana kuwa ni Muisaidie na muihishimu dini, lakini maana yote ni sawa. Mumsabihi Mwenyezi Mungu. Makusudio ya tasbihi ya asubuhi na jioni ni swala tano.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad kwa viumbe ili wamwamini Mwenyezi Mungu na risala ya Muhammad(s.a.w. w ) wamsaidie kwa kupigana jihadi katika njia yake Mwenyezi Mungu na wamuhishimu kwa kuhishimu hukumu za Mwenyezi Mungu kwa kuzitii na kuzitumia na pia wadumu kwenye Swala tano.

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّـهَ يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّـهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿١٠﴾

10. Hakika wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hakika anaivunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anayetekeleza aliyomuahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atampa ujira mkubwa.

سَيَقُولُ لَكَ الْمُخَلَّفُونَ مِنَ الْأَعْرَابِ شَغَلَتْنَا أَمْوَالُنَا وَأَهْلُونَا فَاسْتَغْفِرْ لَنَا يَقُولُونَ بِأَلْسِنَتِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ قُلْ فَمَن يَمْلِكُ لَكُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا إِنْ أَرَادَ بِكُمْ ضَرًّا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ نَفْعًا بَلْ كَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١١﴾

11. Watakuambia mabedui waliobaki nyuma: imetushughulisha mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha. Wanasema kwa ndimi zao yasiyokuwamo nyoyoni mwao. Sema: Ni nani awezaye kuwasaidia na chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka kuwadhuru au akitaka kuwanufaisha? Bali Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

بَلْ ظَنَنتُمْ أَن لَّن يَنقَلِبَ الرَّسُولُ وَالْمُؤْمِنُونَ إِلَىٰ أَهْلِيهِمْ أَبَدًا وَزُيِّنَ ذَٰلِكَ فِي قُلُوبِكُمْ وَظَنَنتُمْ ظَنَّ السَّوْءِ وَكُنتُمْ قَوْمًا بُورًا ﴿١٢﴾

12. Lakini mlidhani kwamba Mtume na waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mkadhania dhana mbaya, na mmekuwa watu wanaoangamia.

وَمَن لَّمْ يُؤْمِن بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ فَإِنَّا أَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ سَعِيرًا ﴿١٣﴾

13. Na asiyemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa hakika tumewaandalia makafiri Moto mkali.

وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١٤﴾

14. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi. Humsamehe amtakaye, na humwadhibu amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu.

BAIA YA RIDHWAN CHINI YA MTI

Aya 10 – 14

KISA KWA UFUPI

Hakika wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hakika anaivunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anayetekeleza aliyomuahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atampa ujira mkubwa.

Aya hii inaashiria Baiatur-ridhwan Baia iliyoridhiwa iliyokuwa chini ya mti. Kisa chake ni kama ifuatavyo:

Hadi kufikia mwaka wa sita wa Hijra, washirikina ndio waliokuwa wakitawala Makka na Nyumba takatifu. Mwishoni mwa mwaka huo Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alitoka Madina Munawwara pamoja na waislamu 1400 kuelekea Makka Mukkarrama kufanya Umra wakiwa hawana fikra yoyote ya vita.

Walipofika sehemu inayoitwa Hudaybiyya, Abu Sufyani alipata taarifa ya kufika kwao. Kwa hiyo akawakusanya makuraishi na wakapitisha azimio la kuwazuia waislamu wasiingie Nyumba takatifu (Al-Ka’aba) kwa nguvu ya silaha. Wakawakusanya wapanda farasi wakiongozwa na Khalid Bin Al- Walid.

Wakapishana wajumbe baina ya Mtume(s.a.w. w ) na wao. Ujumbe wa makuraishi ulimtaka Mtume arudi Madina wala asiingie Makka, Mtume naye akawajibu kuwa sisi hatukuja kupigana na yoyote, tumekuja kuzuru Nyumba takatifu tu na atakayetuzuia tutapigana naye.

Urwa Bin Mas’ud alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa makuraishi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) , akaona maswahaba wakionyesha aina kwa aina ya mapenzi kwa Mtume, hakutawadha ila waligombania mabaki ya udhu wake na hakutema mate ila waliyachukua mate yake; hata unywele wake ukianguka tu walikuwa wakiugombania.

Basi akarudi akiwa ameshangaa sana kwa aliyoyaona akasema: “Enyi makuraishi jamani! Mimi nilimuona Kisra kwenye Ufalme, Kaizari na Najashi, lakini sikuona kwao ufalme kwa watu wao unaonafana na Muhammad kwa sahaba zake. Mimewaona hawawezi kumwacha kwa jambo lolote. Hebu fikirieni vizuri!”

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alimtuma Uthman kwa Makuraishi kwa vile yuko karibu na Abu sufyan na akamwambia: ‘’Waambie sisi hatukuja kwa vita; tumekuja kuzuru hii nyumba tukitukuza heshima na miko yake. Tuna wanyama tutawachinja kisha twende zetu.’’

Uthman alipowapelekea habari hii wakasema: ‘’Haiwezekani kabisa.’’ Ikawa hakuna habari za Uthman, ukatokea uvumi kuwa ameuawa. Mtume aliposikia uvumi huu akasema: Hatuondoki mpaka tupigane na watu hawa.

Akatoa mwito wa kuungwa mkono akiwa amekaa chini ya mti. Basi saha- ba zake wakambai (kiapo cha utii) haraka sana kwamba watamtii na wako tayari kufa katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliisifu baia hii kuwa ni bai yake hasa, na kwamba ameichukua kwa mkono wake, atakayevunja ahadi hii atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu na kujiletea hasira zake na atayeiteleza kikamilifu atakuwa karibu na Mola na mwisho mzuri.

Jina maarufu la baia hii ni Baia iliyoridhiwa (Baiatur-ridhwan) au Baia ya mti (Bai’atu-shajara). Pia inaitwa Baia iliyoridhiwa chini ya mti kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya sura hii tuliyo nayo: “Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti.”

Makuraishi walipoona ukakamavu wa Mtume walikuja chini kufanya suluhu. Wakakakubaliana kwamba waislamu wasiingie Makka mwaka ule mpaka mwaka unaofuatia wakaingia kufanya Umra na kukaa siku tatu bila ya kuwa na silaha isipokuwa panga kwenye ala zake.

Mtume(s.a.w. w ) akamwita Ali bin Abi Twalib na akamwambia: ‘’Andika Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.’’ Mjumbe wa makuraishi akapinga ana akesema: Andika kwa jina lako ewe Mola wangu. Akakubali Mtume na Ali akaandika. Nabii akaendelea kusema: Andika, haya ndiyo waliyokubaliana Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mjumbe wa makuraishi akapinga tena, na kusema: Andika jina lako na la baba yako. Ali akasita.

Mtume akamwambia na wewe yatakupata mfano wake; akiwa anamwashiria suala la mahakimu wawli katika vita vya Siffin. Na hiyo ni miongoni mwa ilimu ya ghaibu aliyompa wahyi Mwenyezi Mungu Mtume wake mtukufu, ambayo ni miongoni mwa nguvu ya hoja ya utume wake na ukweli katika utume wake.

Walipomaliza kutiliana sahii mkataba wa Hudaybiyya, Mtume na maswahaba walitoa Ihramu zao, wakachinja na wakanyoa vichwa vyao. wakabaki siku kadhaa pale Hudaybiyya kisha wakarudi zao Madina.

Mwaka uliofuatia Nabii na Maswahaba walieleka Makka kufanya Umra. Wakaingia huku wakipiga Takbira hii kwa sauti: la ilaha illa Allah, nasara abdah, waazza jundah, wakhadhalal-ahazaba wahdah (hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa pekee yake, amemnusuru mja wake, amelipa nguvu jeshi lake, na amevidhalilisha vikosi hali ya kuwa peke yake).

Wakabakia Makka siku tatu wakitufu na kuchinja. Umra huu unaitwa Umra wa kulipa, kwa sababu unachukua nafasi ya umra ule waliozuiliwa na washirikina. Ilishuka Aya kwa umra huo kama ilivyoelezwa katika Aya ya 28 ya sura hii tuliyo nayo: “Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya ya haki. Bila ya shaka mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza. Hamtakuwa na hofu.”

MABEDUI WALIOBAKI NYUMA

Watakuambia mabedui waliobaki nyuma: Imetushughulisha mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha.

Mtume(s.a.w. w ) alipotaka kutoka kwenda Makka mwaka ule wa Hudaybiyya. Waislamu walimhimiza wasafiri naye, lakini baadhi ya mabedui wanaoishi kando kando ya Madina na wanafiki wengine walikataa kutoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) , wakidhania kuwa Makuraishi hawatamruhusu Muhammad(s.a.w. w ) kuingia Makka. Wakaambiana: Hatuna haja ya kujiingiza kwenye hatari hii.

Bada ya kutimia mkataba, Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake: utakaporudi Madina wale waliobaki nyuma watatoa visababu, kuwa kuangalia familia zao na mali zao ndiko kulikowazuia kufuatana nawe na watakuomba msamaha wa uongo na wakinafiki. Pia watakutaka uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu awaridhie na kuwasamehe yaliyopita.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawakadhibisha kwa kusema:Wanasema kwa ndimi zao yasiyokuwamo nyoyoni mwao; kama ilivyo kawaida ya wanafiki.

Sema: Ni nani awezaye kuwasaidia na chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka kuwadhuru au akitaka kuwanufaisha?

Mnamwambia uwongo Mwenyezi Mungu na hali Yeye anajua siri zenu na dhahiri zenu? Tena heri yenu na shari yenu iko mikononi mwake. Ni nani atakayemzuia akiwatakia heri au shari?

Bali Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda na tena anamjulisha Mtume wake kuwa nyinyi mnadhihirisha yasiyokuwa nyoyoni mwenu.

Lakini mlidhani kwamba Mtume na waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu.

Mlimwacha Mtume mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hatamnusuru Nabii wake na wale waliokuwa pamoja naye na kwamba ushindi utakuwa wa maadui wa Mwenyezi Mungu dhidi ya vipenzi vyake.

Na mkadhania dhana mbaya kuwa waislamu wanakwenda kwenye mauti tu. Wala hakuna tegemeo la dhana isipokuwa wasiwasi wa shetani tu, kwamba Mwenyezi Mungu hataitia nguvu dini yake na kumnusuru Mtume wake.Na mmekuwa watu wanaoangamia. Kila mwenye kukubali uongozi wa shetani basi ataongozwa kwenye maangamizi.

Na asiyemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa hakika tumewaandalia makafiri Moto mkali. watadumu humo wala hawatapata wa kuwasaidia.

Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi.

Hakuna mfalme mwingine asiyekuwa Yeye wala hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwake. Mwenye kumfanyia ikhlasi na akamtegemea Yeye basi atamtoshea. Na mwenye kuelekea kwa mwinginewe basi atamwachia huyo.

Humsamehe amtakaye yule anayestahiki maghufira, kwa sababu ni hakimu, ni muhali kwake kumsamehe anayemwga damu kidhulma, akavunja mashule ya watoto wadogo na akapora vyakula vya wenye njaa. Na humwadhibu amtakaye anayestahiki adhabu; wala Mola wako si mwenye kuwadhulumu waja.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, Mwenye kurehemu yule anayejihurumia yeye na mwingine; vinginevyo asiye na huruma naye hahurummiwi. Na madhalimu hawana wa kuwanusuru.

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

سَيَقُولُ الْمُخَلَّفُونَ إِذَا انطَلَقْتُمْ إِلَىٰ مَغَانِمَ لِتَأْخُذُوهَا ذَرُونَا نَتَّبِعْكُمْ يُرِيدُونَ أَن يُبَدِّلُوا كَلَامَ اللَّـهِ قُل لَّن تَتَّبِعُونَا كَذَٰلِكُمْ قَالَ اللَّـهُ مِن قَبْلُ فَسَيَقُولُونَ بَلْ تَحْسُدُونَنَا بَلْ كَانُوا لَا يَفْقَهُونَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٥﴾

15. Waliobaki nyuma watasema: Mtapokwenda kuchukua ngawira, tuacheni tuwafuate! Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu. Sema: Hamtatufuata kabisa! Mwenyezi Mungu alikwishasema hivi zamani. Hapo watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu. Bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.

قُل لِّلْمُخَلَّفِينَ مِنَ الْأَعْرَابِ سَتُدْعَوْنَ إِلَىٰ قَوْمٍ أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ تُقَاتِلُونَهُمْ أَوْ يُسْلِمُونَ فَإِن تُطِيعُوا يُؤْتِكُمُ اللَّـهُ أَجْرًا حَسَنًا وَإِن تَتَوَلَّوْا كَمَا تَوَلَّيْتُم مِّن قَبْلُ يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٦﴾

16. Waambie walioachwa nyuma katika mabedui: Mtakujaitwa kwenda pigana na watu wakali kwa vita; mpigane nao au wasalimu amri. Basi mkimtii, Mwenyezi Mungu atawapa ujira mzuri; na mkigeuka kama mlivyogeuka kwanza, atawaadhibu kwa adhabu chungu.

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَن يَتَوَلَّ يُعَذِّبْهُ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٧﴾

17. Kipofu hana tabu, wala kiguru hana tabu, wala mgonjwa hana tabu. Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitiwayo na mito chini yake. Na atakayegeuka atamuadhibu kwa adhabu chungu.

TUACHENI TUWAFUATE

Aya 15 – 17

MAANA

Waliobaki nyuma watasema: Mtapokwenda kuchukua ngawira, tuacheni tuwafuate!

Ni wale wale waliokataa kutoka na Mtume alipoelekea Makka mwishoni mwa mwaka wa sita, ambao amewakusudia Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia. Mtume aliwahimiza wafuatane naye, lakini wakawahofia makuraishi kwa visingizio vya familia na mali.

Baada ya Mtume kurudi Hudaybiyya alikaa Madina hadi mwanzo mwanzo wa mwaka wa saba, akaenda kupigana Khaybara. Huko waislamu walipata ngawira nyingi sana, zilzioamsha tamaa ya waliobaki nyuma. Wakamwambia Mtume na wale aliokuwa nao: tuchukueni na sisi kwenye ngawira hizo. Leo wanataka kutoka na jana walipoitwa walijitia kushughulika na watu wao na mali wakihofia jihadi. Haya ndiyo mantiki ya kila aliyetekwa na tamaa na asione jingine ila hiyo tu.

Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu.

Wanaotaka ni hao hao waliobaki nyuma. Makusudio ya maneno ya Mwenyezi Mungu hapa ni ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwanyima ngawira waliobaki nyuma, ambayo ameiashiria kwa kusema: “Mtapo kwenda kuchukua ngawira.”

Lakini Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hikima yake, hakutubain- ishia ngawira yenyewe.

Je, ni ngawira za Khaybara au yinginezo. Hata hivyo wafasiri wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi watu wa Baia iliyoridhiwa kuwa ngawira ya Khaybara itawahusu wao tu. Razi anasema: Hii ndio kauli mashuhuri kwa wafasiri. Maraghi naye akasema: “ni habari sahaihi.” Hili haliko mbali, kwa sababu vita vya Khaybar ndivyo vya kwanza baada ya mkataba wa Hudaybiyya.

Vyovyote iwavyo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Nabii wake awaambie waliobaki nyuma:Sema: Hamtatufuata kabisa kuchukua ngawira kwa sababu nyinyi mlikataa kufuatana nasi Makka mkihofia vita.Mwenyezi Mungu alikwishasema hivi zamani kuwa hamna fungu la ngawira.

Hapo watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu.

Hapana, sivyo kabisa! Mwenyezi Mungu hakutunyima ngawira bali nyinyi ndio mnaotunyima kwa chuki na husuda kwetu.

Bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.

Hili ni jawabu la Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na kauli yao ‘bali mnatuhusudu.’ Sio kama mlivyodai, ni kutojua kwenu na uasi wenu kwenye hukumu nyingi.

Waambie walioachwa nyuma katika mabedui ambao walikataa kutoka na Mtume kwenda Makka:Mtakujaitwa kwenda pigana na watu wakali kwa vita.

Aliyewaita ni Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) . Baada ya vita vya Khaybar, Mtume aliwaita kwenye vita vya Hunayn, Taif na Tabuk.

Mpigane nao au wasalimu amri.

Yaani wakali ambao mtaitwa mkapigane nao watahiyarishwa mambo mawili na Mtume: Upanga au Uislamu. Basi je, mtaitikia mwito wa Mtume au mtarudi kwenye visigino vyenu kama mlivyofanya hapo mwanzo? Kwa maneno mengine ni kuwa kupambana kwenu na wakali wa vita ndio uthibitisho wa ukweli wenu sio kuchukua ngawira.

Basi mkimtii, Mwenyezi Mungu atawapa ujira mzuri; ngawira duniani na Pepo Akhera. Au Pepo na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yule atakayeuawa.

Na mkigeuka kama mlivyogeuka kwanza, atawaadhibu kwa adhabu iliyo chungu.

Kuna adhabu gani chungu zaidi kuliko adhabu ya Jahannam?

Kipofu hana tabu, wala kiguru hana tabu, wala mgonjwa hana tabu.

Makusudio ya tabu hapa ni dhambi. Maana ni kuwa hakuna dhambi kwa watu wa aina zote hizi tatu kama wakibaki nyuma ikiwa ni vita vya kutoa mwito wa uislamu.

Ama jihadi ya kujikinga na adui na kumzuia na uchokozi wake, hivyo ni lazima kwa wote wanaume kwa wanawake, watu wazima kwa watoto, na wazima na walemavu. Kila mtu ni kwa kadiri ya nguvu zake.

Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitiwayo na mito chini yake. Na atakayegeuka atamuadhibu kwa adhabu chungu.

Maana yako wazi – ni Pepo kwa mtiifu na Moto kwa muasi.

Maana haya yamekaririka kwenye makumi ya Aya, kwa mnasaba wa kutaja heri na shari, kutanabahisha kwamba Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, kwamba mtu hataachwa bure na kwamba yeye atakutana na Mwenyezi Mungu kwa matendo yake. Ni matendo tu ndio yatakua maudhui ya hisabu na kipimo cha malipo.

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا ﴿١٨﴾

18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa ushindi wa karibu.

وَمَغَانِمَ كَثِيرَةً يَأْخُذُونَهَا وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴿١٩﴾

19. Na ngawira nyingi watakazozichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

وَعَدَكُمُ اللَّـهُ مَغَانِمَ كَثِيرَةً تَأْخُذُونَهَا فَعَجَّلَ لَكُمْ هَـٰذِهِ وَكَفَّ أَيْدِيَ النَّاسِ عَنكُمْ وَلِتَكُونَ آيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ وَيَهْدِيَكُمْ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا ﴿٢٠﴾

20. Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira nyingi mtakazozichukua, basi amewatangulizia hii, na akaizuia mikono ya watu isiwafikie. Na ili hiyo iwe ni Ishara kwa waumini, na akawaongoza njia iliyonyooka.

وَأُخْرَىٰ لَمْ تَقْدِرُوا عَلَيْهَا قَدْ أَحَاطَ اللَّـهُ بِهَا وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا ﴿٢١﴾

21. Na nyingine hamjaweza kuzipata, Mwenyezi Mungu amekwishazizingira. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

وَلَوْ قَاتَلَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوَلَّوُا الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿٢٢﴾

22. Na lau makafiri wangelipigana nanyi basi bila ya shaka wangeligeuza migongo, kisha wasingelipata mlinzi wala msaidizi.

سُنَّةَ اللَّـهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلُ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٢٣﴾

23. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokwishapita zamani, hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

وَهُوَ الَّذِي كَفَّ أَيْدِيَهُمْ عَنكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ عَنْهُم بِبَطْنِ مَكَّةَ مِن بَعْدِ أَنْ أَظْفَرَكُمْ عَلَيْهِمْ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا ﴿٢٤﴾

24. Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kuwapa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.

WALIPOKUBAI CHINI YAMTI

Aya 18 – 24

MAANA

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia waumini walipokubai chini ya mti.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashira Baia iliyoridhiwai chini ya mti, kwamba Yeye yuko radhi nayo na watu wake. Yamekwishatangulia maelezo ya Baia hii katika Aya 10 ya Sura hii.

Na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa

Wanaelezewa watu wa baia. Nyoyo zao zilijaa ukweli na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Makusudio ya utulivu ni raha na utulivu wa moyo. Ushindi wa karibu ni mkataba wa Hudaybiyya ambao miongoni mwa athari zake ni kuingia waislamu Makka kufanya umra, pamoja na kuchukia makuraishi. Kuna riwaya isemayo kuwa Umar bin Al- khattwab alimuuliza Nabii(s.a.w. w ) :“Ni ushindi huu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Mtume akasema: “Ndio.”

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya ngawira nyingi, ni ngawira za Khaybara. Kwa sababu Khaybara ilikuwa mashuhuri kwa ngawira nyingi na mashamba. Lakini kauli yenye nguvu ni kila ngawira walizopata watu wa Baia iliyoridhiwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema ngawira kiujumla bila ya kuifunga na jambo maalum.

Maana yake kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaneemesha watu wa Baia iliyoridhiwa kwa utulivu na neema nyingi, kwa sababu Yeye alijua kuwa wao wana ikhlasi katika dini yao na ukweli wa azma yao ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Kila mafanikio waliyoyapata waislamu na kuwapeleka mbele ni katika Athari za nguvu za Mwenyezi Mungu, uweza wake na hekima yake katika mipangilio.

Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira nyingi mtakazozichukua.

Ngawira nyingi hapa ni kila nyara walizozipata waislamu zama za Mtume(s.a.w. w ) . Kwa hiyo basi tofauti ya ngawira zilizotajwa kwenye Aya iliy- otangulia ni kuwa zile zilizowahusu watu wa Baia iliyoridhiwa na hizi ni za waislamu wote kila mahali na kila wakati.

Basi amewatangulizia hii.

Hii ni ishara ya suluhu ya Hudaybiyya. Kwa sababu suluhu hii ndiyo iliy- otangulia. Ama ngawira za Khaybara zilikuwa baada ya suluhu. Lau si neno hii, tungelisema iliyotangulia ni suluhu pamoja na Khaybar.

Na akaizuia mikono ya watu isiwafikie.

Tabari anasema, wametofautiana watu wa taawili kuhusu neno ‘watu’ hapa. Ikasemekana ni mayahudi wengine wakasema ni makuraishi. Tuonavyo sisi makusudio ni maadui wa Uislamu waliojaribu kuumaliza na kuwamaliza Waislamu. Hakuna lililowazuia isipokuwa udhahifu.

Na ili hiyo iwe ni Ishara kwa Waumini.

‘Hiyo’ ni suluhu ya Hudaybiyya. Mwenyezi Mungu ameifanya ni alama kwa waumini kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao na anawanusuru na maadui zao. Hazikupita siku ila ikawabainikia waumini kuwa mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa ni heri kwao na shari kwa washirikina.

Na akawaongoza njia iliyonyooka kwenye kila yaliyo na manufaa yenu ya dunia na Akhera.

Na nyingine hamjaweza kuzipata, Mwenyezi Mungu amekwishazizingira.

Yaani Mwenyezi Mungu amewaahidi ngawira mnazoweza kuzipata hivi sasa, vile vile amewaahidi nyingine msizoweza kuzipata hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu amewahifadhia, na mtazipata baadae, iwe karibu au mbali.

Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hashindwi kuwapa nyara zaidi ya mnavyofikiria na kutegemea.

Na lau makafiri wangelipigana nanyi basi bila ya shaka wangeligeuza migongo, kisha wasingelipata mlinzi wala msaidizi.

Kama kwamba muulizaji aliuliza itawezekana vipi waislamu wapate nyara za makafiri, na hali wao wana nguvu na ni wengi wanaopigania nafsi zao?

Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu kuwa Yeye yuko pamoja na wau- mini na anawakinga. Mwenyezi Mungu hashindwi na jambo. Ama makafiri hawana kimbilio isipokuwa upanga au kukimbia.

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokwishapita zamani, hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mitume waliopita kuwashin- da maadui zao. Kama muulizajai atauliza, mbona hii haiafikiani na Aya zinazoelezea waziwazi kuwa mayahudi walikuwa wakiwaua manabii bila ya haki? Majibu yake yako kwenye Juz. 17 22: (38 – 41).

Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kuwapa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.

‘Yeye’ ni Mwenyezi Mungu. Waliozuiwa mikono ni makafiri. Imesemekana kuwa Makusudio ya bonde la Makka ni Hudaybiyya, kwa vile mji huo uko karibu na Makka.

Wengine wakasema ni Makka yenyewe. Maana haya ndiyo yanayokuja haraka kwenye fahamu, kutokana na neno bonde.

Maana ni kuwa enyi waislamu mmeingia Makka, uliokuwa mji mkuu wa shirki na kitovu cha washirikina mkiwa washindi bila ya vita.

Hii ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu na neema yake kubwa kwenu. Kwa sababu Yeye ndiye aliyewazuia kupigana kwa kuwatia hofu katika nyoyo zao na akawazuia nyinyi kupigana nao kwa kuwakataza.

Suluhu ya Hudaybiyya ilikuwa mwaka wa sita wa Hijra, Umra ya kulipa ukawa mwaka wa saba na kuiteka Makka kukawa katika mwaka wa nane.