TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 28299
Pakua: 3893


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 28299 / Pakua: 3893
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Ya Arubaini Na Tisa: Surat Al- Hujurat. Imeshuka Madina. Ina Aya 18.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure-hemu

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١﴾

1. Enyi ambao mmeamini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ ﴿٢﴾

2. Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaanguka, na hali hamtambui.

إِنَّ الَّذِينَ يَغُضُّونَ أَصْوَاتَهُمْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ امْتَحَنَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ لِلتَّقْوَىٰ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿٣﴾

3. Kwa hakika ambao wanateremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amezitia mtihani nyoyo zao kwa takua. Hao watakuwa na maghufira na ujira mkubwa.

إِنَّ الَّذِينَ يُنَادُونَكَ مِن وَرَاءِ الْحُجُرَاتِ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾

4. Hakika ambao wanakuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawana akili.

وَلَوْ أَنَّهُمْ صَبَرُوا حَتَّىٰ تَخْرُجَ إِلَيْهِمْ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥﴾

5. Na lau wao wangelingojea mpaka uwatokee ingelikuwa kheri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

MSINYANYUE SAUTI ZENU KULIKO SAUTI YA NABII

Aya 1 – 5

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakumbusha waumini mambo haya yafutayo:-

1.Enyi ambao mmeamini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Msifanye haraka kusema au kufanya tendo lolote linaoamabatana na dini na masilahi ya uma, mpaka alipitishe Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake mtukufu.

Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Katika Nahjul-balagha imeandikwa: “Mche Mwenyezi Mungu kwa baad- hi ya takua hata kama ni kidogo. Na weka sitara baina yako na Mwenyezi Mungu hata kama ni nyembamba.”

Kwa uchache kabisa wa mtu kumcha Muumba wake ni kujizuia kusema: Lau Mwenyezi Mungu angelihalalisha hili ambalo ameliharamisha au angeliharamisha lile alilolilihalalisha. Au kusema afadhali Nabii angeli- fanya hivi au asingelifanya vile alivyofanya na mengineyo ya ujeuri na ujinga.

2.Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii.

Si jambo zuri kuinua sauti bila ya dharura. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: “Na uinamishe sauti yako. Hakika sauti mbaya zaidi ni ya punda.” Juz. 21 (31:19). Sikwambii tena ikiwa ni kuinua sauti mbele ya wakubwa na kwenye vikao vyao. Na Mtume mtukufu(s.a.w. w ) ni bwana wa manabii na mtukufu wa viumbe wote.

3.Wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaanguka, na hali hamtambui.

Mnapozungumza na Nabii msizungumze kama mnavyozungumza nyinyi. Mwenye kufanya hivyo atakuwa amebatilisha imani yake bila ya kutaka wala kujua. Na mwenye kubatilika imani yake ndio vimebatilika vitendo vyake na atakuwa mikononi mwa waliopata hasara.

Kwa hakika ambao wanateremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amezitia mtihani nyoyo zao kwa takua – yaani amezisafisha nyoyo zao kwa matendo mema -Hao watakuwa na maghufira na ujira mkubwa.

Mwenyezi Mungu huwajaribu waja wake kwa aina mbalimbali ya mitihani, ili apate mawaidha mwenye kuwaidhika na ajikanye mwenye kukanyika. Mwenye kuwaidhika na akawa na subira Mwenyezi Mungu humtakasa, humuongoza njia ya usawa na humneemesha kwa maghufira na ujira wa wenye kuwa na subira.

Aya inaashiria kwamba kuzungumza kwa adabu na kwa inavyotakikana ni katika imani. Imam Ali(a . s) anasema:“Imani ya mja hainyooki mpaka unyooke moyo wake na moyo haunyooki mpaka unyooke ulimi wake.

Hakika ambao wanakuita nyuma ya vyumba, wengi wao hawana akili.

Mtume(s.a.w. w ) alikuwa na wake tisa, kila mmoja alikuwa na chumba chake kilichojengwa kwa makuti ya mtende, mlangoni kukiwa na pazia ya manyoya.

Wafasiri wanasema kuwa mabedui walikuja Madina na wakasimama nyuma ya vyumba vya Mtume wakaanza kuita kwa sauti: Ewe Muhammad(s.a.w. w ) tutokee! Mtume akangoja kidogo; kisha akawatokea. Mwenyezi Mungu amewataja kuwa wengi wao hawakujua walichokuwa wakikifanya, kutokana na ubedui na ushamba.

Na lau wao wangelingojea mpaka uwatokee ingelikuwa kheri kwao, kwa sababu kungoja na kutofanya haraka kuna malipo na thawabu, kumwdhimisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuchunga adabu.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu. Rehema yake inaenea kwa washamba, walalahoi n.k.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ ﴿٦﴾

6. Enyi mlioamini! Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda.

AKIWAJIA FASIKI NA HABARI YOYOTE, ICHUNGUZENI

Aya 6

MAANA

Enyi mlioamini! Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda.

Imekuwa mashuhuri kwa wafasiri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alimtuma Walid bin Uqba bin Abu Muit kwa Bani Mustaliq kuchukua Zaka, wakampokea kwa shangwe ya kumzunguka, lakini akadhania kuwa wanataka kumzuia.

Akarudi kwa Mtume(s.a.w. w ) na kumwambia: wamenizuia na kunifukuza. Basi Mtume(s.a.w. w ) akakasirika na baadhi ya swahaba zake wakamwambia tuwashambulie? Ndio ikashuka Aya hii kuwaondolea tuhuma Bani Mustaliq. Kuna sababu nyingine ya kushuka Aya hii.

Sisi hatutegemei lolote katika sababu za kushuka Aya ila ikithibiti kwa nukuu ya Qur’an au Hadith mutawatir. Zaidi ya hayo ni kuwa kudhania Walid shari hakuwezi kusababisha ufasiki; isipokuwa ni kukosea na kutatizika. Mwenye kukosea haitwi fasiki.

Vyovyote itakavyokuwa sababu za kushuka, lakini Aya haishilii kwenye sababu hiyo, bali inaenda mbali zaidi, kwa vile sababu haiwezi kuhusisha isipokuwa inaenea. Itakuwa sababu inatajwa kwa ajili ya jambo fulani ambalo halihusishi tamko. Kwa hiyo niwajibu kuichukulia dhahiri ya Aya, ambayo inafahamisha uharamu wa kuyachukulia maneno ya fasiki bila ya kuchunguza na kuthibitisha habari yake, kuhofia kuingia kwenye hatari; kama kuwadhuru wengine na kujuta, na majuto ni mjukuu.

Tunapata tafsiri ya Aya hii katika kauli ya Imam Ali(a . s) :“Mwenye kufuata njia iliyo wazi atakunywa maji, na mwenye kuacha atahangaika.”

Kundi la masheikh wa kisunni na kishia wameitumia Aya hii kuwa ni dalili ya wajibu wa kuchukulia kauli ya mwenye kutegemewa bila ya sharti la kuchunguza ukweli wake. Baadhi yao wameitolea dalili kwa maneno ya undani yaliyojifungafunga.

Iko wazi kuwa Aya imechukua msingi wa kiujumla wa kupima habari ambayo haifai kuitegema ila baada ya uthibitisho na hiyo ni habari ya fasiki. Vile vile habari inayotegemwa bila ya uthibitisho ambayo ni habari ya mwenye kutegemewa.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameshartiza kuitegemea habari ya fasiki kwa ubainifu na uthibitisho, lakini hakuitaja habari ya mwenye kutegemewa. Lau ingelikuwa ni wajib kuichunguza habari ya mwenye kuaminika basi angeliitaja. Kwa kuwa haikutajwa basi sharti hiyo haipo.

Tuanavyo sisi ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Akiwajia fasiki na habari yoyote, ichunguzeni,” inafahamisha tu wajibu wa kuichunguza na kuithibitisha habari ya fasiki wala haifahimishi wajibu huo kwa habri ya mwenye kuaminika. Sisi tuko na wale wasemao kuwa kuitegemea habari ya mwenye kuaminika bila ya uchunguzi ni njia wanayoitumia wenye akili wa kale na wa sasa.

Hata hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyoyatenda,” inafahamisha kuwa habari yoyote ambayo hatuna wasiwasi nayo kuingia katika matatizo na haramu, basi inafaa kuitumia bila ya kumwangalia mtoaji habari.

Kimsingi ni kuwa tusiamini habari ila ikiwa inatoka kwa mwenye kuaminika au tuithibitishe na kuichunguza ikiwa inatoka kwa fasiki.

وَاعْلَمُوا أَنَّ فِيكُمْ رَسُولَ اللَّـهِ لَوْ يُطِيعُكُمْ فِي كَثِيرٍ مِّنَ الْأَمْرِ لَعَنِتُّمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ ﴿٧﴾

7. Na jueni kuwa yuko kati yenu Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lau angeliwatii katika mambo mengi, bila ya shaka mngelitaabika. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akauchukiza kwenu ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka.

فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَنِعْمَةً وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٨﴾

8. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

MWENYEZI MUNGU AMEWAPENDEKEZEA IMANI

Aya 7 – 8

MAANA

Na jueni kuwa yuko kati yenu Mtume wa Mwenyezi Mungu na mtukufu wa wa mwanzo na wa mwisho. Basi ni juu yenu kumwadhimisha wala msimpe habari isipokuwa ya ukweli.

Lau angeliwatii katika mambo mengi, bila ya shaka mngelitaabika.

Hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ikielekezwa kwa wau- mini kuwa wamsikilize Mtume na wamtii, wala wasimshauri lile analolijua kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambalo wao hawalijui. Lau angeliwaitikia kwenye mambo mengi wanayomwambia wangelitaabika na kuingia kwenye tabu na dhambi.

Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akauchukiza kwenu ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka.

Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake wamwamini Yeye na wamtii, akawabainishia uzuri wa imani na utiifu, akatumia kila njia kuwahimiza hilo na akamwahidi malipo na thawabu kubwa mwenye kuamini na akatenda mema. Vile vile amewakataza ukafiri na uasi, akabainisha hasara zake na akamtishia kwa adhabu mwenye kukufuru na kuasi na akazisifia adhabu hizo kwa namna ambayo haiwezi kufikirika akilini ila baada ya kubainishwa. Ni mtu gani anayeweza kufikiria adhabu ambayo si mauti wala uhai.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatuma Mitume wake kwa watu ili wafikishe amri, makatazo ahadi na kiaga chake. Kuna wale wanaoitikia kihaki na kiukweli, wengine wakapinga na kufanya inadi na kuna wale waliotikia kuhofia masilahi yao na tamaa ya ngawira.

Wale waliomwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume kihaki na kiukweli ndio aliowakusudia katika kauli yake: “Amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu.” Yaani ameipendekeza na kuipamba kutokana na kueleza uzuri wa imani na kivutio cha thawabu nyingi. Akauchukiza ukafiri kwa kueleza mabaya yake na tishio la adhabu chungu.

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelibainisha hilo kwa waumini na makafiri, kwanini amehusisha kuwataja waumini, kinyume na wengineo?

Jibu : Ndio, lakini sio kila mwenye kusikia ubainifu wa Mwenyezi Mungu anauamini na kunufaika nao, wala sio kila mwenye kunasihiwa na Mwenyezi Mungu anakubali nasaha zake. Bali wema wamekubali na waovu wakakataa. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamtaja na kumsifu mwenye kusikia maneno akafuata mazuri yake na akampuuza mwenye kupinga na akaachana nayo.

Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kuchagua uongofu badala ya upotevu ana fadhila na malipo, lakini fadhila kubwa ni ya yule aliyemwandalia njia ya uongofu, akamwongoza na akampa uweza wa kuifuata. Walisema wakale: “Kama si sababu asingelifaulu msababishaji”

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٩﴾

9. Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hayo linadhulumu jingine, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirejea basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٠﴾

10. Hakika Waumini tu ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemiwe.

NA IKIWA MAKUNDI MAWILI KATIKA WAUMINI YANAPIGANA

Aya 9 – 10

MAANA

Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni.

Uaislamu una mafunzo na miongozo ya kujenga jamii na kuitengeneza; miongoni mwayo ni wajibu wa kumlinda binadamu damu yake, mali yake, hadhi yake na uhuru wake wa kusema na kutenda. Hakuna yeyote mwenye utawala wa hayo isipokuwa haki. Akitoka kwenye haki na akaingilia haki ya wengine, basi hapo atakuwa amejiondolea kinga ya hayo yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ ﴿٧٠﴾

“Na hakika tumewatukuza wanadamau.” Juz. 15 (17:70).

Amesema tena kumwambia Mtume wake:

لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ ﴿٢٢﴾

“Wewe si mwenye kuwatawalia” (88:22).

Akasema tena:

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ﴿٤٢﴾

“Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki.” Juz. 25 (42:42).

Mafunzo mengine ya Uaislamu ni kuhurumiana na kusaidiana katika yale yaliyo na heri na masilahi kwa wote. Ikiwa itatokea uhasama baina ya makundi mawili ya waumini, basi wajibu wa waumini ni kusuluhisha kwenye misingi ya haki na uadilifu na kuchunga umoja usivunjike.

Kuna Hadith tukufu inayosema: “Je, niwaambie jambo lililo na daraja kubwa zaidi kuliko kufunga, kuswali na kutoa sadaka? Wakasema: Naam! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Ni kuwaunganisha waliotengana”

Na likiwa moja la hayo linadhulumu jingine, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu.

Ikiwa kundi moja litakataa kurudi kwenye haki na likang’ang’ania uchokozi, basi ni juu ya waumini wengine kulihami na dhulma lile kundi linaloonewa, kwa hekima na mawaidha mazuri. Ikiwa lile kundi ovu halitakoma ila kwa vita, basi lipigeni katika mipaka ya sharia inayohakikisha amani ya wote.

Na likirejea basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.

Likitubia lile kundi linaloonea na likaacha kabisa, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu, na hakuna atakayeruhusiwa kulifanyia lolote. Lililobaki ni wajibu wa waumini, kwa juhudi zao waondoe, yaliyotokea kwenye nafsi za pande mbili.

Al-Jassas Al-Hanafi, anasema katika Kitabu Ahkamul-Qur’an akiwa anazungumzia Aya hii: “Ali Bin Abi Twalib alipigana na kundi ovu kwa upanga akiwa pamoja na maswahaba wakubwa wa Badr (Ahlu Badr) waliojulikana. Na alikuwa ni mwenye haki. Hakuna aliyehalifu katika kundi kabisa isipokuwa kundi ovu na wafuaisi wake aliokuwa akipigana nao.”

Na akasema Abu Bakr Al-Malik, Maaruf kwa jina la Ibn –Al-Arabi Al- Muafiri, katika Ahkamul - Qur’an: “Imethibiti kwa maulama wa Kiislamu na imethibiti kwa dalili ya dini kwamba Ali Bin Abu Twalib alikuwa Imam na kwamba kila mwenye kupigana naye ni muovu na kupambana na mtu huyo ni wajibu mpaka arudi kwenye haki.”

UDUGU WA KIDINI NA UDUGU WA KIBINADAMU

Hakika Waumini tu ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.

Hii ni kusisitiza kuleta suluhu baina ya pande mbili zilzigombana, pamoja na kuashiria kuwa upatanishi huu ni lazima kwa mfungamano wa udugu. Kuna Hadith isemayo: mwislamu ni ndugu wa mwislamu, hamdhulumu, hamtelekezi wala hamtii aibu.

Unaweza kuuliza: Kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema: Hakika waumini tu ni ndugu, na asiseme: Hakika watu wote tu ni ndugu. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) naye akasema:

“Mwislamu ni ndugu wa mwislamu.” Na asiseme: Mtu ni ndugu wa mtu? Tunajua kuwa Mola ni mmoja, asili ni moja, umbile ni moja na usawa baina ya watu ni wajibu. Kwa hiyo upendo unatakikana uwe ni wa jumla sio mahsusi; sawa na rehe- ma ambayo imekienea kila kitu?

Basi mgawanyo huu utakuwa na tofauti gani na ule unaowagawanya binadamu kwa misingi ya kiuchumi; walivyofanya wamarksi, au kuwagawanya kwa misingi ya kijinsia; kama walivyofanya wanazi au kwa misingi ya vita na silaha kama ilivyo siasa ya kimarekani?

Kisha nini kilichosababisha matatizo na maangamizi haya yanayomkabili binadamu leo, hadi kufikia kumalizana, baada ya binadmu kuweza kumiliki nguvu mbaya ya silaha za maangamizi? Je, hii imesabishwa na binadamu kama binadamu au imesabishwa na aina kwa aina za migawanyo?

Hatimaye sasa binadamu wasaidiane kwa misingi ya dini au asasi za kibanadamu?

Jibu : Maswali yote haya ni haki, na jibu lake ni moja tu litakoloweza kutosheleza maswali yote haya; nalo ni: Kusaidiana ni wajibu baina ya binadamu wote bila ya kubagua. Huu ndio mwito wa uaislamu hasa, unaofahamishwa na makumi ya Aya na riwaya. Tutatosheka kutaja Aya moja na riwaya moja.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 13 ya sura hii: “Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane. Hakika mtukufu zaidi yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi yenu.

Kwa hiyo mwito wake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Enyi watu!’ pamoja na kusema kwake: ‘Kutokana na mwanmmke na mwanamume’ na ‘aliye na takua zaidi’ ni dalili mkataa na wazi kuwa mwito wa Qur’an ni wa kiutu na wa mataifa, unamzingatia mtu ni ndugu wa mtu kwa namna yoyote itakvyokuwa itikadi yake, utaifa wake na jinsia yake.

Mfano wa Aya hii na ufafanuzi wake ni kauli yake Mtume mtukufu(s.a.w. w ) : “Watu wote wako sawa kama chane za shanuo. Jueni kuwa hakuna ubora wa mwarabu kwa mwajemi wala wa mwajemi kwa mwarabu, wala wa mwekundu kwa mweusi wala wa mweusi kwa mwekundu isipokuwa kwa takua … nyote mnatokana na Adamu na Adam ametokana na mchanga.”

Zaidi ya hayo katika Juz.21 (30:30) kuna Aya inayosema kuwa uislamu ni dini ya maumbile na katika Juz. 9 (8:24) kuna Aya inayofahamisha kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni dini ya maisha.

Kwa hali hiyo basi inatubainikia kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake zinazingatia kuamini utu ni sehemu inayokamilisha kumwamini Mwenyezi Mungu, mitume wake na Vitabu vyake.

Kwa hiyo Makusudio ya mumin katika Aya na mwislamu katika Hadith ni yule anayeamwamini Mwenyezi Mungu na mtu kwa kuwa ni mtu.

Kwa maneno mengine ni kuwa hakuna mzozo wala kupingana baina ya udugu wa kibinadamu na udugu wa kiislamu; huu wa kiislamu unauongeza nguvu ule wa kibinadamu.

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿١١﴾

11. Enyi ambao mmeamini! Kaumu isidharau kaumu nyingine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake kwa wanawake wengine, huenda wakawa bora kuliko wao. Wala msitiane kasoro, wala msiitane majina ya kejeli. Na wasiotubu, hao ndio madhalimu.

KAUMU ISIDHARAU KAUMU NYINGINE

Aya 11

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Kaumu isidharau kaumu nyingine, huenda wakawa bora kuliko wao; wala wanawake kwa wanawake wengine, huenda wakawa bora kuliko wao.

Imesemekana kuwa neno Qawm, tulililofasiri kwa maana ya kaumu, kwa maana yake ya kiarabu huwa halitajwi ila kwa wanaume tu, kwa dalili ya kuunganishwa wanawake baada ya neno hilo.

Katika Juz. 19 (25:55-62) tulisema kuwa dhalimu kesho atachukuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni kafiri ingawaje duniani anachukuliwa kuwa ni mwislamu kama akitamka shahada mbili.

Na mwenye kuwadharau wema atakuwa ni dhalimu na safihi.

Hili Mwenyezi Mungu amelikemea kwa ukali sana; kama aliposema:

فَيَسْخَرُونَ مِنْهُمْ سَخِرَ اللَّـهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٩﴾

“…Wakawafanyia maskhara; Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo. “ Juz. 10 (9:79).

Pia kauli yake:

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ ﴿٢٩﴾ وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ ﴿٣٠﴾ وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَ ﴿٣١﴾ وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ ﴿٣٢﴾ وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ ﴿٣٣﴾ فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ ﴿٣٤﴾

“Hakika wale walio na hatia walikuwa wakiwacheka wale ambao wameamini. Wakiwapitia wanakonyezana na wakirudi kwa watu wao walirudi wakishangilia. Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea. Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. Basi leo wale ambao wameamini wanawacheka makafiri” (83: 29-34).

Vile vile amesema:

وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ ﴿١﴾

“Ole wake kila mtia kasoro mwenye kusengenya.” (104:1).

VIPI UTAPATA MARAFIKI?

Nimekumbuka, wakati nikifasiri Aya hii, kwamba kiasi cha mika 16 au zaidi iliyopita nilisoma tarjuma ya kitabu: How to win friends and influence people (vipi utapata marafiki na kuathiri nafsi) cha Dayl Karengi.

Vile vile nimekumbuka hekima ya hali ya juu ya Imam Zainul’abidin, inayohusiana na maudhui hii ambayo ina athari zaidi ya kitabu nilichokitaja pamoja na kuwa kimeenea sana na kufasiriwa kwenye lugha nyingi.

Imam, kwenye hekima yake, alikuwa akikusudia kauli yake Mwenyezi Mungu: “Kaumu isidharau kaumu nyingine, huenda wakawa bora kuliko wao.” Hekima yenyewe ni hii:

“Jihadhari na kuzungumza ambayo moyo unayakanya hata kama una udhuru. Kwani sio kila utakayemwambia shari unaweza kumfafanulia udhuru. Aliye mkubwa kuliko wewe muweke daraja ya mzazi, mdogo daraja ya mtoto, na aliye marika daraja ya kaka. Ni nani katika hawa unapenda kumvunjia heshima yake?

“Ikiwa shetani atakuingilia kujiona kuwa u mbora zaidi ya mwingine, angalia haya yafutayo: Ikiwa ni mkubwa zaidi yako, sema: amenitangulia kwa imani na matendo mema, kwa hiyo ni bora kuliko mimi. Ikiwa ni mdogo kuliko wewe, sema: nimemtangulia kwa maasi, kwa hiyo yeye ni bora kuliko mimi. Akiwa ni marika yako sema: mimi nina uhakika nimefanya dhambi, lakini nina shaka kuwa yeye amefanya dhambi, basi kwanini niache uhakika nichukue shaka?

“Ukiwaona watu wanakutukuza, sema: wamechukulia wema, na ikiwa wanakutenga, sema: kuna makosa nimefanya.”

Imam anaendelea kusema:“Ukiyafanya haya maisha yako yatakuwa mepesi, utakuwa na marafiki wengi na utakuwa na maadui kidogo, na utafurahi kwa wema wao wala hutasikitika kukutenga.”

Vyovyote watavyosema maulama na wenye hekima kuhisiana na maudhui haya, hawatazidisha kitu kwenye hekima hii fasaha ya hali juu.

Hilo si ajabu kwa vile aliyeisema ni mtoto wa wahyi, hazina ya ilimu ya wahyi na aliyekulia kwenye malezi yake.

Wala msitiane kasoro.

Msitiane ila wala msiwambie wengine lile ambalo hampendi kuambiwa.

Wala msiitane majina ya kejeli.

Mtu asimwite mwenzake kwa jina analolichukia. Mafaqihi wamesema kuwa ikiwa jina halikukusudiwa kasoro wala dharau na ni mashuhuri wa hilo, basi halina ubaya; kama vile Hassan Madafu, n.k.

Ni uovu kutumia jina baya baada ya imani.

Hapa kuna tafsiri mbili: Ya kwanza ni msimwite mumin ewe kafiri! Ya pili, ni uovu huko kumwita mwingine kwa jina asilolipenda. Tafsiri hii ina ngvuvu, kwa wafasiri wengi kuliko ile ya kwanza.

Na wasiotubu, hao ndio madhalimu.

Mwenye kutubia ni kama asiye na dhambi na mwenye kung’ang’ania dhambi atakuwa ameidhulumu nafsi yake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu atawaadhibu wenye dhambi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢﴾

12. Enyi ambao mmeamini! Jiepusheni na dhana nyingi. Hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipeleleze, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.

DHANA, UJASUSI NA KUSENGENYA

Aya 12

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza dharau, kutia ila, kubeza na kuitana majina ya kuchukiza. Na akamkemea mwenye kufanya moja katika hayo. Katika Aya hii anakataza dhana mbaya, ujasusi na kusengenya. Ufafanuzi ndio huu ufuatao:-

DHANA

Enyi ambao mmeamini! Jiepusheni na dhana nyingi. Hakika baadhi ya dhana ni dhambi.

Sehemu hii ya Aya inawezekana kufanyiwa muhtasari kwa jumla moja tu: “Kila mtu hana hatia mpaka lithibitike kosa lake.”

Inawezekana jumla hii kuifafanua kwa urefu, tuweke mpaka wa linalopelekea asili ya dhana, kuwa je, inafaa kuichulia dhana au kuna wajibu wa kujieupusha wakati wote au wakati wa kuweko udhuru na wa kutokuweko ilimu? Na je, kuna udhuru wa kutojua au hakuna?

Ikiwa inafaa kuichukulia dhana, je, tuichukulie dhana vyovyote ilivyo sababu yake na mfungamano wake? Na ikiwa haifai kuichukulia dhana kwa namna yote ile, je ni nyenzo gani za ilimu kwenye hukumu ya sharia na mengineyo katika ilimu ya usul (misingi ya sharia) ambayo tumeimalizia miaka si kidogo kuisoma?

Ni vizuri tuchuke tafsiri ya wastani si kurefusha wala kufupiliza. Kabla ya lolote ni lazima tufanye maandalizi ya kujua toafauti baina ya shaka, dhana na ilimu. Shaka ni kuwa sawa uthibitisho na ukanusho. Dhana ni kuwa na nguvu upande mmoja baina ya hizo mbili, lakini bado kunakuwa na uwezekano kwa upande ule usio na nguvu. Ilimu ni kubainika upande mmoja unaofunga kabisa njia ya upande mwingine.

Unaweza kumdhania mtu heri au shari, ukawa umepatia au umekosea katika dhana yako. Hakuna ubaya kabisa ikiwa utamdhania mwenzako heri, iwe umepatia au umekosea; au iwe litajitokeza hilo kwenye kauli yako na vitendo vyako au lisijitokeze.

Mtume mtukufu(s.a.w. w ) anasema:“Wadhanieni waumini heri.” Imam Ali(a . s) anasema:“Liweke jambo la nduguyo kwenye heri.” Tazama Juz. 1 (2:83) kifungu cha ‘Kuchukia usahihi.’

Kwa hiyo basi inatubainikia maana ya kuwa kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema:“Jiepusheni na dhana nyingi,” na wala asisema ‘jiepusheni na kila dhana.’

Neno wingi huwa pia linatumiwa kwa maana ya baadhi; na haya ndiyo Makusudio yake kwenye Aya hii; yaani jiepusheni na dhana mbaya.

Dhana mbaya yenyewe sio haramu ikiwa haitajitokeza kwenye kauli au kitendo, wala mwenye dhana hiyo hana majukumu yoyote. Lakini ni lazima asiitolee maamuzi yoyote na aifanye kama haiko. Akiitolea uamuzi na ikajitokeza athari yake kwenye kauli au kitendo, basi atawajibika na atastahili lawama na adhabu.

Hii ndio dhana aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema: “Hakika baadhi ya dhana ni dhambi.”

Mtume mtukufu(s.a.w.w) anasema:“Mambo matatu hasalimiki nayo yeyote: Kisirani, hasadi na dhana: Ukiona kisirani endelea, ukiona husda usiitake, na ukidhania hakikisha. Kwa hiyo basi maana ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Jiepusheni na dhana nyingi’ nikuwa msizitolee maamuzi wala msizitumie; sawa na kauli yake “Asiwafitini shetani.”

UJASUSI

Wala msipeleleze.

Kupeleleza ni kuchunguza siri na makosa kwa njia ya kujificha. Ni haramu kwa Kitabu, Sunna, Ijmai (kongamano la maulama) na kiakili. Na kauli yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا ﴿٢٧﴾ فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ... ﴿٢٨﴾

“Enyi ambao mmeamini! Msiingie nyumba zisizo nyumba zenu mpaka muombe ruhusa… na msipomkuta yeyote humo msiingie mpaka mpewe ruhusa.” Juz. 18 (24:27-28).

Katika Sunna ni Hadith ya Mtume mtukufu(s.a.w. w ) :“Mwenye kukuchungulia ukamtupia kijiwe na ukamtoboa macho yake, basi huna lawama.” Mafaqihi wamekubaliana kwa pamoja kuitumia Hadith hii. Ama akili inauona ujajusi ni vita dhidi ya maisha ya watu na kuingilia uhuru wao na mambo yao yanayowahusu katika mila na desturi.

Nimekumbuka, wakati nikiandika maneno haya, makala ndefu kuhusu maudhui haya, iliyotolewa na gazeti Al-Ahram la 27-6-1969, nililisoma wakati huo, kisha nikalihifadhi katika mafaili ya magazeti. Nililihifadhi na kuliweka akiba ya kulitumia nikilihitajia. Basi nikalisoma tena, mara nikaona mambo ambayo hata kuyawaza tu ni muhali; baadhi yake ni haya yafuatayo:

“Wamarekani hivi sasa wanajua kuwa sio kuwa kuta zao zina masikio tu, bali zina macho na mboni vile vile, kama lilivyosema gazeti la Times. USA wametengeneza kifaa kidogo cha ukubwa wa milimita, kinachoweza kusajili mazungumzo; na mtu anaweza kukiweka kwenye jaketi kama kifungo. Kila mtu anaweza kukitumia na kinagharimu kati ya dola 10 na 15.

Huko New York, wafanyabiashara wameweka matangazo ya biashara kwenye magazeti kuuza vifaa vya kurikodi mazungumzo ya watu majumbani mwao na wanaviuza madukani kama michezo ya watoto. Bei yake haizidi dola 18.

Mtu akiweka kifaa hiki kwenye gari kikielekezwa kwenye jengo basi kitarikodi kila neno linalosemwa kwenye jengo lile. Bali kuna kifaa cha kusikilizia maneno kisichozidi ukubwa wa punje ya choroko, kinachoweza kuwekwa kwenye kalamu nk, kinatumia betrii ya masaa 18 hadi 50.

Pia wametengeneza kifaa kidogo cha kutuma, kinachoweza kutangaza yanayopita kwenye majumba kwa umbali wa futi 50 na bei yake ni dola 400.

Ajabu ya yote ni kamera zinazopenya ukutani na kupiga picha mambo yote anayoyafanya mtu chooni na hata kwenye giza. Vile vile inawezekana kuchora chale (tattoo) katika mwili wa mtoto wakati anapozaliwa ambayo itafuatilia harakati zake katika maisha yake yote.

Kuna shirika katika Marekani yote linalokusanya habari na harakati binafsi za watu mashuhuri wa siasa, elimu, uandishi uchumi na wengineo na kurikodi maneno yao, na kupiga picha ya vitendo vyao, hata wanapofanya tendo la ndoa na wake zao na wengineo. Mtu anaweza kupata habari hizi kwa dola moja tu. Shirika hili linaitwa Benki ya habari.

Yote hayo yanatokea ikiwa serikali inajua kila kitu, bila ya kufanya lolote, kwa sababu imekuwa ni jambo la kawaida kama vile kuuza magazeti tu.” Mwisho wa nukuu ya gazeti.

Haya ni machache katika mengi. Watunzi wameandika vitabu maalum kuhusiana na maudhui haya. Lau wamarekani wangeliyafanya haya kwao tu wenyewe kwa wenyewe, tungeliwaambia wao na wanowatawala: “shauri yenu, kila mji una uhuru wa kujichagulia unavyotaka.” Lakini wamarekani wamevuka mipaka, wanafanya ujasusi kwenye nchi nyingine kwa ndege na satalaiti.

Usishangae msomaji. Marekani ni nchi ya maendeleo, demokarasia, bwana mkubwa wa uhuru, na polisi wa ulimwengu.

Tena zaidi ya hayo wanaamini Mwenyezi Mungu… Dalili kubwa kuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ni mauaji ya kinyama waliyoyafanya kwenye kijiji kimoja katika Vietnam ya kusini[6] , na kuwasheheneza silaha za kisasa mayahudi ili kuwamaliza wananchi wa Palestina, kuwaua watoto kwa ujumla na kutupa mabomu kwa kutumi ndege za Phantoum kwa watoto wa shule wa Misr! Kweli kabisa USA ni dola kubwa kwenye uwanja huu wa mauaji!

KUSENGENYA

Wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.

Kusengenya ni kumtaja mtu kwa jambo asilolipenda. Mtume mtukufu(s.a.w. w ) anasema:“Kusengenya ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia. Ikiwa jambo hilo analo huko ni kusengenya na ikiwa hana itakuwa ni kumsingizia.” Na kusingizia ni kukubwa zaidi kuliko kusengenya na kumeharamishwa kwa Kitabu Sunna na Ijmai (kongamano la maulama).

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemfananisha mwenye kusengenywa na maiti kwa vile anakuwa hayupo na akaifananisha hishima yake na nyama yake na kumtaja kwa uovu kuwa ndio kula.

Maana ya mnalichukia hilo ni kuwa ikiwa mnaona kinyaa kula nyama ya maiti basi pia muone kinyaa kumsengenya asiyekuwepo, kwa sababu yote mawili hayo yako sawa.

Hakuna jambo linalofahamisha kupungukiwa na udhalili kuliko kusengnya. Imam Ali(a . s) anasema:“Kusengenya ni juhudi ya asiyejiweza.” Na Mwenyezi Mungu hasamehi kusengenya mpaka asamehe aliyesengenywa. Mafaqihi wameuvua uharamu wa kusengenya kwa wafuatao:-

Mpagani, hakimu dhalimu, mwenye kuudhihirisha ufuska wake, kwa sababu mwenye kulitupa joho la haya hana cha kuficha, kumpa ushauri mwenye kutaka ushauri katika kushirikiana na mtu au kumwakilisha kwenye jambo muhimu, kumtengua shahidi kwa kadhi, na mwenye kudhulumiwa kwa yule aliyemdhulumu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

لَّا يُحِبُّ اللَّـهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَن ظُلِمَ وَكَانَ اللَّـهُ سَمِيعًا عَلِيمًا ﴿١٤٨﴾

“Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa aliyedhulumiwa.”

Juz. 6 (4:148).

Katika Kitabu Al-Makasib cha Sheikh Ansari, imesemwa kuwa sehemu zinazoondolewa uharamu wa kusengenya hazina idadi. Kwa sababu kusengenya kunakuwa haramu ikiwa kutangaza huko hakuna masilahi yenye nguvu. Vinginevyo, basi itakuwa wajibu kutangaza na kueneza kwa kuangalia masilahi yenye nguvu zaidi, kama ilivyo katika kila maasi ya haki za Mwenyezi Mungu na haki za binadamu.Tazama mwanzo wa Juz. 6.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿١٣﴾

13. Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane. Hakika mtukufu zaidi yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari.

قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَـٰكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ وَإِن تُطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤﴾

14. Mabedui walisema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatawapunguzia chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ ﴿١٥﴾

15. Hakika Waumini ni wale tu waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasiwe na shaka, na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.

قُلْ أَتُعَلِّمُونَ اللَّـهَ بِدِينِكُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٦﴾

16. Sema: Je, mnamjulisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu?

يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا قُل لَّا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُم بَلِ اللَّـهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٧﴾

17. Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye anayewasimbulia kwa kuwaongoza kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.

إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٨﴾

18. Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

MTUKUFU ZAIDI YENU NI MWENYE TAKUA ZAIDI

Aya 13 – 18

MAANA

Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane. Hakika mtukufu zaidi yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye na takua zaidi yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari.

Watu wanajua kuwa baba yao ni Adam na mama yao ni Hawa, lakini lengo la kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Tuewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke, ni kuwa watu wote wajue kwamba wao ni ndugu ni udugu wa usawa katika haki na wajibu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu; “Ili mjuane,” ni kuwa Makusudio ya kutofautiana kwenu katika miji, nasaba na rangi, sio kuwa muwe vikundi, mchinjane na mjifaharishe kwa mataifa yenu, baba zenu na jinsi zenu, hapana! Sivyo kabisa.

Lengo ni muhurumiane na msaidiane katika yale yaliyo na heri yenu na masilahi yenu. Na mbora kabisa atakuwa yule anayemuogopa Mwenyezi Mungu zaidi na akawanufaisha waja wake.

Aya hii ni mwito kutoka kwenye Qur’an kuwa watu wawe umma mmoja wa kiutu na ulimwengu mmoja unaokusanywa na uadilifu na upendo. Ulimwengu huu ni tegemeo la wenye fikra safi na ni ndoto ya walio wema.

Tuna uhakika kuwa makubaliano ya haki za binadamu, yatabakia kwenye karatasi na yatakuwa ni nadharia tu, ikiwa hautapatikana umoja wa ubinadamu uliotolewa mwito na Qur’an, zaidi ya mika 1300 liliyopita. Amerika na Israil zilitia saini makubaliano ya haki za binadamu, lakini bado ndio za kwanza kuangamiza watu Vietnam na Palestina.

Leo ninapoandika maneno haya 22 April 1970, kamati ya umoja wa mataifa imehakikisha kuwa Israil imevunja haki za binadamu, ikasema waziwazi kuwa Israil imevunja majumba ya wakazi ikaacha miili ya wanaume, wanawake na watoto kwenye kifusi na ikakataa isizikwe. Pia imevunja sehemu takatifu na mahospitali[7] na kuwaadhibu wenyeji kwa umeme. Watu wazima wanawang’oa viungo, watoto wanawakata mikono na kupasua matumbo yao mbele ya baba zao na mama zao na mengineyo ya kinyama na mauji ya maangamizi.

Mabedui walisema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatawapunguzia chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Makusudio ya uaislamu hapa ni kutamka shahada mbili. Katika Juz. 1 (2:82), tumetaja tofauti baina ya mumin na mwislamu. Hapa tutamnukuu Dkt Twaha Hussein katika kitabu Mir’atul-islama (Kioo cha uaislamu).

Yeye ni mwanafasihi anayefahamika kwa siri za fasihi, ninamnukuu: “Wakati wa Mtume kulikuweko waumini na waislamu. Basi, niipi tofauti baina imani na Uislamu? Imani kwa dhahiri ya Aya hii ni jambo lilio moyoni ambalo mihimili yake ni ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na kusadikisha, kwa kina ndani ya dhamiri, kila aliloletewa wahyi Mtume.

Natija ya imani hii ni kumwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume katika kila wanalolitolea mwito, bila ya kigugumizi, kugwazagwaza, wala kutaradadi, kwa hali yoyote ile itakavyokuwa; iwe kuna matukio au majanga. Mhimili mwingine wa imani hii ni kumwogopa Mwenyezi Mungu kiundani kabisa likitajwa jina lake na kumtegemea kwa undani zinaposomwa Aya zake.

“Ama Uislamu ni twaa ya dhahiri ya kutekeleza wajibu na kujiepusha na yaliyokatwaza; hata kama haitafikia imani ya kweli. Kuna watu wanaosilimu kuhofia ubaya; kama walivyosilimu makuraishi walioachwa bila ya kutekwa nyara siku ya kutekwa Makka. Wengine walasilimu kwa hofu na tamaa; kama walivyofanya mabedui aliowataja Mwenyezi Mungu katika Aya hii.”

Hakika Waumini ni wale tu waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasiwe na shaka, na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.

Waumini wa kwelikweli kabisa ni wale wasiokuwa na shaka yoyote kwenye itikadi zao na wanaojitolea kihali na mali, kuihakikisha haki na kuibatilisha batili. Umetangulia mfano wake mara kadhaa; miongoni mwazo ni Juz. 10 (9:88).

Sema: Je, mnamjulisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu?

Mabedui walisema tumeamini, ndio Mwenyezi Mungu anawajibu, kuwa hivi mnamjulisha Mwenyezi Mungu imani yenu na hali Yeye anajua siri na yaliyofichika; kila kitu amekizunguka. Tena je imani inakuwa kwa kudai? Inatosha kuwa mtu ni mjinga kuwa hajui uweza wake Mwenyezi Mungu.

Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye anayewasimbulia kwa kuwaongoza kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.

Makusudio ya kusimbulia kwake Mwenyezi Mungu ni kuwafanyia hisani, kwa sababu Yeye amekataza masimbulizi, na hawezi kukataza jambo kisha alifanye. Makusudio ya kuongoza kwake kwenye imani ni kutoa mwongozo wa haki na kuipendekeza.

Maana ni kuwa mabedui na walio mfano wao wanaona kuwa wamemfanyia hisani Mola wao na mtume wao kwa dini yao na wanataka walipwe; hali yakuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewafanyia hisani wao, pale alipowaongoza kwenye haki na kuwahimiza kupitia Mtume wake.

Kwa hiyo wao ndio wamshukuru kwa alivyowafanyia hisani na kuwaneemesha; sio wao wasimbulie na kutaka kulipwa; ikiwa kweli wameamini dini yao na wakafanya ikhlasi kwenye imani yao. Vinginevyo watakuwa wanastahili kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale aliyowaandalia waongo na wahaini.

Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua imani ya kweli na ya uwongo na kuzipamabanua amali zilizokusudiwa dunia na zile zilizokusudiwa radhi ya Mwenyezi Mungu. Aina zote za amali pamoja na imani au kufuru ndio kipimo cha uadilifu wa hisabu na malipo.

MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA TISA: SURAT AL- HUJURAT