13
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
وَقَالَ قَرِينُهُ هَـٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ ﴿٢٣﴾
23. Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.
أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ ﴿٢٤﴾
24. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi.
مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ ﴿٢٥﴾
25. Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka.
الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ ﴿٢٦﴾
26. Ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.
قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ ﴿٢٧﴾
27. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.
قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ ﴿٢٨﴾
28. Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.
مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٢٩﴾
29. Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.
يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ ﴿٣٠﴾
30. Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?
وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ ﴿٣١﴾
31. Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.
هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ ﴿٣٢﴾
32. Haya ndiyo mnayoahidiwa. Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae.
مَّنْ خَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُّنِيبٍ ﴿٣٣﴾
33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.
ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ ﴿٣٤﴾
34. Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima.
لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ ﴿٣٥﴾
35. Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.
ANAYEKATAZA HERI
Aya 23 – 35
MAANA
Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.
Mwenzake ni yule aliyetajwa katika Aya ya 17- Malaika anayeandika matendo ya yule aliye naye. Maana ni kuwa. Mwandishi huyu atamwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t):
Hiki kitabu cha yale uliyonituma. Ndani yake mna mambo yote vile yalivyokuwa: “Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo. Na watasema:
وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا ﴿٤٩﴾
“Ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu? Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa. Na Mola wako hadhulumu yoyote.” Juz. 15 (18:49).
Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi, Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka, ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Katika Aya 21, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema: “Na itakuja kila nafsi pamoja na mpelekaji na shahidi,” na katika Aya tuliyo nayo, anasimulia kuwa atamwambia mpelekaji na shahidi, mchukue kwenye Jahannam aliyenishirikisha, akaikufuru haki na akaifanyia inadi, akaipinga heri na akawazulilia watu nayo.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) atarudia na kusisitiza:Basi mtupeni katika adhabu kali.
Ilivyo ni kuwa hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amempa sifa ya mwenye kuzuia heri yule mwenye kuruka mipaka, anayetia shaka. Na mahali pengine amempa sifa ya mwenye dhambi:
مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾
“Azuiaye heri arukaye mipaka, mwenye dhambi” (68:12).
Tukiunganisha Aya hizi na ile isemayo:
إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ ﴿٤٣﴾ طَعَامُ الْأَثِيمِ ﴿٤٤﴾ كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ ﴿٤٥﴾ كَغَلْيِ الْحَمِيمِ ﴿٤٦﴾
“Hakika Mti wa Zaqqum, Ni chakula cha mwenye dhambi, kama mafuta mazito, hutokota matumboni kama kutokota kwa maji ya moto.” Juz. 25 (44:43-46).
Tukiunganisha zote hizo inatubainikia kuwa kosa la kuzuia heri halina mfano na kosa lolote na kwamba adhabu yake haina kipimo.
Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.
Mwenzake huyu sio yule mwenzake wa kwanza. Yule wa kwanza alikuwa ni katika waandishi wema, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.”
Ama huyu rafiki wa pili ni katika maibilisi ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake: “Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.” Juz. 25 (43:36).
Dalili ya kuwa marafiki ni tofauti ni kauli ya rafiki wa pili: “Sikumpoteza.” Kwa sababu yule rafiki wa kwanza haiwezekani kupoteza, kwa hiyo hawezi kukana, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemchagua kuandika kutokana na uaminifu wake.
Zaidi ya hayo ni kuwa kubishana kesho kutakuwa baina ya wakosefu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Msigombane mbele yangu.” Pia kauli yake: “Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.” Juz. 25 (43:67).
Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.
Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu akiyaelekeza kwa mkosefu na rafiki yake shetani. Maana ni kuwa msianze kuambiana, wewe umenipoteza na mwingine naye aseme sikukupoteza. Kwani leo ni siku ya hisabu na malipo; wala mtu hatanufaika na maneno wala na mengine isipokuwa matendo mema tu; nami niliwawapa mwito wake na nikawahadharisha na siku ya leo kwa atakayehalifu, lakini mkakataa isipokuwa ukafiri.
Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.
Makusudio ya kauli hapa ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mpelekaji na shahidi: “Mtupeni katika Jahannam kila kafiri mwenye inadi.”
Kutupwa huku kutakuwa tu na ni uadilifu. Kutakuwa, kwa vile ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) wala hakuna mabadiliko katika amri yake. Ni uadilifu kwa sababu mkosefu anastahiki hivyo.
Unaweza kuuliza
: maulama wengi wamesema kuwa inawezekana kwa Mwenyezi Mungu kuhalifu kiaga (ahadi ya kuadhibu), lakini haiwezekani kuhalifu ahadi; (ahadi ya mazuri) kama ilivyo katika Hadith, aliposema:“Mwenye kumwahidi yoyote kumlipa uzuri, ni lazima atekeleze, na mwenye kumwahidi ubaya, basi ana hiyari.”
Zaidi ya hayo ni kuwa kiakili ni vizuri kutekeleza ahadi, lakini si vibaya kuhalifu kiaga. Sasa kuna wajihi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Kwangu haibadilishwi kauli?’
Baadhi ya maulama wamejibu kuwa
: Mwenyezi Mungu hasamehi hivi hivi tu, bali ni kwa sababu. Pia kusamehe si kubadilisha kauli. Nasi tunaongezea kwenye jawabu hili kuwa makusudio ya kiaga hapa ni kiaga cha adhabu ya mwenye kuzuia heri, na sio kila kiaga. Kwa sababu mruka mipaka huyu mwenye dhambi, tunavyodhani, ni kuwa hana kafara wala muombezi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?
Hiki ni kinaya cha ukali wa muwako wake na ukali wa adhabu yake, na kwamba haiwi na msongomano wa wenye hatia kwa idadi yoyote watakayokuwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameipa Jahannam sifa kadhaa za kutisha zinazosisimua ngozi za wale wanaomwogopa Mola wao. Ama wale walio na maradhi nyoyoni mwao, wanadharau sifa hizo na wale wanaoziamini.
Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.
Hii ni njia ya Qur’an, inaunganisha malipo ya muovu na mwema. Huko ni shida na machungu na hapa ni raha na nema na Pepo. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Haitakuwa mbali,’ ni kutilia mkazo neno kuletwa karibu.Makusudio ya kuletwa karibu Pepo kwa wenye takua ni kuwa ni yao na wao ni wa hiyo.
Haya ndiyo mnayoahidiwa.
Mlijua enyi wenye takua ahadi ya Mwenyezi Mungu naye ameitekeleza. Basi chukueni neema hii isiyokuwa na mpaka wa sifa wala kufikiwa na akili.
Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.
Sifa hizi nne ni alama za kujulisha mwenye takua: kuwa ni kutubia akijiweka mbali na maasi, kumhofia Mwenyezi Mungu na kudumu kumtii kwa kutumai thawabu zake, akiwa kwenye imani yake na ikhlasi yake kwenye njia moja; ni sawa awe mbele ya watu au akiwa mbali; kinyume na yule mwenye kujionyesha, mwenye ria.
Anakuwa mvivu akiwa peke yake na na anakuwa mchangamfu mbele ya watu. Huyo ndiye mwenye takua ambaye anamwelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo ulio salama.
Kwa maneno mengine ya Imam akimsifu mwenye takua:
“Amemtii anayemwonogoza na akaijiepusha na anayempoteza; akapata njia salama kwa busara ya anayemuonyesha na kutii amri ya anayemwongoza. Akaharakisha kwenye uongofu kabla ya kufungwa milango yake na kuisha nyenzo zake.”
Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima. Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.
Nyinyi wenye takua mtakuwa katika Pepo isiyokatika neema yake, hachoki mkazi wake, hazeeki anayedumu wala hakati tamaa mkazi wake. Mtapata zaidi ya manyoyatamani na kuyapendekeza.
Baada ya hayo, ni kuwa tofauti hii baina ya Pepo na Moto inafichua tofauti iliyopo baina ya wenye takua na wenye hatia na kwamba tofauti yao mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na tofauti ya Pepo na Moto.
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُم بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِن مَّحِيصٍ ﴿٣٦﴾
36. Na karne ngapi tuliziangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Nao walizunguka katika miji. Je, yako makimbilio?
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ ﴿٣٧﴾
37. Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.
وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ ﴿٣٨﴾
38. Na hakika tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita; na wala haukutugusa uchovu.
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ ﴿٣٩﴾
39. Basi vumilia kwa hayo wasemayo na msabihi Mola wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ ﴿٤٠﴾
40. Na katika usiku msabihi na baada ya kusujudu.
وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ ﴿٤١﴾
41. Na sikiliza siku ataponadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.
يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ ﴿٤٢﴾
42. Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.
إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ ﴿٤٣﴾
43. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ ﴿٤٤﴾
44. Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ ﴿٤٥﴾
45. Sisi tunajua sana wayasemayo. Wala wewe si jabari juu yao. Basi mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa kiaga.
SIKU ATAKAPONADI MWENYE KUNADI
Aya 36 – 45
MAANA
Na karne ngapi tuliziangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Nao walizunguka katika miji. Je, yako makimbilio?
Karne ni watu wa zama moja. Maana ni kuwa katika zama zilizopita kulikuwa na uma nyingi zilizokuwa na maendeleo, nguvu na idadi ya watu wengi kuliko wale waliokukadhibisha wewe Muhammad! Pia walikuwa na mawasiliano na miji mingine. Lakini yote hayo hayakuwafaa waliposhukiwa na adhabu, wala hawakupata pa kuikimbia amri ya Mwenyezi Mungu. Je, watu wako hawaogopi kuwasibu yaliyowasibu waliopita?
Maana haya yamekaririka kwenye Aya nyingi; ikiwemo: Juz. 21 (30:9).
Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.
Hayo ni hayo ya kukumbushwa maangamizi ya waliopita. Mwenye moyo ni moyo salama. Kutega sikio ni kusikiliza kwa makini. Shahidi ni yule aliyepo kimoyo na kiakili. Maana ni kuwa yale tuliyoyataja ya maangamizi ni mawaidha tosha kwa mwenye busara na akazingatia.
Na hakika tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita; na wala haukutugusa uchovu
Siku sita ni kinaya cha mikupuo au maendeleo ya kugeuka ulimwengu kutoka hali moja hadi nyingine. Tazama Juz. 8 (7:54).
Basi vumilia kwa hayo wasemayo,
ya ubatilifu na usafihi. Kwa sababu mwisho ni wa wenye kuvumilia uvumilivu wa kiungwana.
Na msabihi Mola wako kabla ya kuchomoza jua.
Hiyo ni ishara ya swala ya Alfajiri.Na kabla ya kuchwa,
ni swala ya adhuhuri na alasiri.
Na katika usiku msabihi,
ni swala ya magharibi na isha. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:130).Na baada ya kusujudu,
ni ishara ya uradi baada ya swala na swala za sunna baada ya kumaliza za wajibu.
Na sikiliza siku ataponadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu. Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.
w
)
. Siku atakayonadi, hapo kuna maneno ya kukadiriwa; yaani sikiliza masimulizi ya siku atakayonadi; na wala sio kusikiliza mnadi. Makusudio ya mahala karibu ni kuwa huo mwito watausikia wote; kama kwamba mnadi yuko karibu nao, ingawaje ukelele unatoka mbinguni.
Hapa ndio inatubainikia njia ya kuchanganya na kuafikiana baina ya Aya hii na ile isemayo:
أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٤٤﴾
“Hao wanaitwa kutoka mahali mbali.” Juz. 24 (41:44).
Maana ni kuwa, sikiza tunayokusimulia ewe Muhammad kuhusiana na ukulele wa ufufuo kwa ajili ya hisabu na malipo. Ukulele huu uko mbali, ukitokea mbinguni na uko karibu kwa kuwa unafika kwenye masikio yote, mpaka ya wafu, watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika:
هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَّا أَسْلَفَتْ وَرُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٣٠﴾
“Huko kila nafsi itajua iliyoyatanguliza na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki, na yote waliyokuwa wakiyazua yatawapotea.” Juz. 11 (10:30)
Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
Uhai na mauti yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye ndio marejeo ya viumbe. Umetangulia mfano wake mara nyingi; kama vile katika Juz. 11(10:56).
Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
Ardhi itawapasukia wa kwanza na wa mwisho, watoke makaburini mwao upesi upesi; wakiwa ni wengi kuliko chunguchungu na machanga. Atakayekuwa na hali nzuri kuliko wengine ni yule atakayepata mahali pa kuweka unyayo wake na pa kuvutia pumzi zake; kama alivyosema Imam Ali
.
Sisi tunajua sana wayasemayo,
ya kumkadhibisha Mtume na kukana ufufuo.Wala wewe si jabari juu yao,
kuwalazimisha kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Wewe ni muonyaji tu.
Basi mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa kiaga
na yule asiyeogopa pia ili utoe hoja. Mwenyezi Mungu amemuhusisha kumtaja anayeogopa kwa kuashiria kuwa yeye ananufaika na ukumbusho zaidi kuliko asiyeogopa:
فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾ سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾ وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى ﴿١١﴾
“Kumbusha ikiwa kutafaa huko kukumbusha. Atakumbuka mwenye kucha na atajiepusha nako muovu.” 87: (9-11).
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Atajiepusha nako muovu,’ ni dalili mkataa kuwa amri ya kukumbusha ni ya ujumla, iwe kutafaa au hakutafaa.
MWISHO WA SURA YA HAMSINI: SURAT QAF