16
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU
Sura Ya Hamsini Na Mbili: Surat At-Tur. Imeshuka Makka. Ina Aya 49.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
وَالطُّورِ ﴿١﴾
1. Naapa kwa Mlima,
وَكِتَابٍ مَّسْطُورٍ ﴿٢﴾
2. Na kitabu kilichoandikwa
فِي رَقٍّ مَّنشُورٍ ﴿٣﴾
3. Katika waraka wa ngozi iliyo kunjuliwa,
وَالْبَيْتِ الْمَعْمُورِ ﴿٤﴾
4. Na kwa Nyumba iliyojengwa,
وَالسَّقْفِ الْمَرْفُوعِ ﴿٥﴾
5. Na kwa sakafu iliyonyanyuliwa,
وَالْبَحْرِ الْمَسْجُورِ ﴿٦﴾
6. Na kwa bahari iliyojazwa.
إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ لَوَاقِعٌ ﴿٧﴾
7. Hakika adhabu ya Mola wako hapana shaka itatokea.
مَّا لَهُ مِن دَافِعٍ ﴿٨﴾
8. Hapana wa kuizuia.
يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا ﴿٩﴾
9. Siku zitakapotikisika mbingu kwa mtikiso,
وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا ﴿١٠﴾
10. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
فَوَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ ﴿١١﴾
11. Basi ole wao siku hiyo wanaokadhibisha,
الَّذِينَ هُمْ فِي خَوْضٍ يَلْعَبُونَ ﴿١٢﴾
12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
يَوْمَ يُدَعُّونَ إِلَىٰ نَارِ جَهَنَّمَ دَعًّا ﴿١٣﴾
13. Siku wataposukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu.
هَـٰذِهِ النَّارُ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٤﴾
14. Huu ndio ule Moto mliokuwa mkiukadhibisha!
أَفَسِحْرٌ هَـٰذَا أَمْ أَنتُمْ لَا تُبْصِرُونَ ﴿١٥﴾
15. Je, huu ni uchawi, au hamuoni?
اصْلَوْهَا فَاصْبِرُوا أَوْ لَا تَصْبِرُوا سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ إِنَّمَا تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾
16. Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyokuwa mkiyatenda.
NAAPA KWA MLIMA
Aya 1 – 16
LUGHA
Anasema Fayruzi Abad katika Kamusi yake Al-Muhit: Neno Tur linatumika kwa maana ya uga wa nyumba, kila mlima na mlima ulio karibu na Ayla unaoitwa mlima Sinai. Pia hutumika kwa milima miwili, mmoja uko Qudus na mwingine ulioko Raasul-ayn. Vile vile mlima ulioko Tiberias.
MAANA
Naapa kwa Mlima, na kitabu kilichoandikwa katika waraka wa ngozi iliyo kunjuliwa, na kwa Nyumba iliyojengwa, na kwa sakafu iliyonyanyuliwa, na kwa bahari iliyojazwa.
Mlima hapa ni ule mlima Sinai aliozungumza Mwenyezi Mungu na Musa. Pia Mwenyezi Mungu ameapa na mlima huu katika (95:2).
Makusudio ya kitabu chenye kuandikwa ni kila kitabu cha mbinguni. Kwa sababu neno kitabu hapa limekuja kwa kuenea kwenye jinsia yake (nakra). Kulihusisha neno hilo na kitabu maalum kutahitajia maunganishao. Kule kutajwa mlima sinai tu, hakutoshi kuwa makusuidio yawe ni Tawrat.
Makusudio ya kusema kilichoandikwa katika waraka, ni kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha kitabu ila alikifanya kitumike mikononi mwa watu na kila mtu aweze kukifikia na kukijua kwa ukamilifu. Imam Aliy
anasema:
“Nashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake aliyemtuma kwa dini liliyo mashuhuri na kitabu kilichoandikwa.”
Nyumba iliyojengwa ni Al-Kaa’ba. Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ ﴿١٢٧﴾
“Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile nyumba.” Juz. 1 (2:127).
Sakafu iliyonyanyuliwa ni mbingu:
وَجَعَلْنَا السَّمَاءَ سَقْفًا ﴿٣٢﴾
“Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu.” Juz. 17 (21:32).
Yani iko kama sakafu katika jicho la mwenye kutazama. Bahari iliyojazwa ni kujaa maji:
وَإِذَا الْبِحَارُ سُجِّرَتْ ﴿٦﴾
“Na bahari zitakapojazwa.” (81:6).
Mwenyezi Mungu ameapa na vitu hivi vitano kuashiria uweza wake. Tazama Juz. 23 (37:1) kifungu cha: ‘Mwenyezi Mungu na kuapa na viumbe vyake.’
Hakika adhabu ya Mola wako hapana shaka itatokea
kwa wakosefu. Jumla hii ni jawabu la kiapo. Hapana wa kuizuia; kama yalivyo mauti hakuna wa kuyarudisha ila yule mwenye kuleta uhai na mauti.
Siku zitakapotikisika mbingu kwa mtikiso.
Yaani kani mvutano itaondoka, uzani baina ya sayari utaharibika na kutokea mparaganyo utakaoenea.
Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
Itakapotikisika mbigu ardhi itatetemeka na milima itaondoka sehemu zake.
Aya mbili hizi zinaashiria kusimama kiyama na kuharibika ulimwengu, ambapo viumbe watakusnywa kwa ajili ya hisabu.
Basi ole wao siku hiyo wanaokadhibisha. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
Waliichezea dunia nayo ikawachezea, lakini hawakuiweza, kwa hiyo ikawapiga mweleka na ikawapeleka haraka kwenye Jahannam ambayo ni makazi mabaya.
Siku wataposukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu.
Watasukumwa kwa nguvu na Malaika wa adhabu watawaambia: Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukadhibisha! “Ionjeni adhabu iunguzayo. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu. Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.” Juz. 10 (8:50-51).
Je, huu ni uchawi, au hamuoni.
Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
aliwahofisha na Moto wa Jahannam wakamwambia wewe ni mchawi. Siku ya malipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawafanya ni kuni za Jahannam na awaambie, je mmeona sasa? Je, Muhammad ni mchawi? Je, adhabu ya kuungua ni uchawi? Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu, adhabu ni hiyo hiyo haipungui wala haiishi. Hakika mnalipwa kwa mliyokuwa mkiyatenda ya dhulma na ufisadi.
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ ﴿١٧﴾
17. Hakika wenye takua watakua katika Mabustani na neema,
فَاكِهِينَ بِمَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ وَوَقَاهُمْ رَبُّهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ ﴿١٨﴾
18. Wakifurahi kwa yale aliyowapa Mola wao. Na Mola wao atawalinda na adhabu ya Motoni.
كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾
19. Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.
مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَّصْفُوفَةٍ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ ﴿٢٠﴾
20. Wakiegema viti vya fahari vilivyopangwa safu. Na tutawaoza mahurulaini.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾
21. Na walioamini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja kitu katika vitendo vyao kila mtu ni rehani wa alichokichuma.
وَأَمْدَدْنَاهُم بِفَاكِهَةٍ وَلَحْمٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢٢﴾
22. Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyopenda.
يَتَنَازَعُونَ فِيهَا كَأْسًا لَّا لَغْوٌ فِيهَا وَلَا تَأْثِيمٌ ﴿٢٣﴾
23. Watapeana humo bilauri zisio na (vinywaji) vya upuuzi wala dhambi.
وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ غِلْمَانٌ لَّهُمْ كَأَنَّهُمْ لُؤْلُؤٌ مَّكْنُونٌ ﴿٢٤﴾
24. Na watawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizofichwa.
وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٥﴾
25. Wataelekeana wakiulizana.
قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ ﴿٢٦﴾
26. Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa.
فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾
27. Basi MwenyeziMungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾
28. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
WATU WA PEPONI
Aya 17 – 28
MAANA
Hakika wenye takua watakua katika Mabustani na neema, Wakifurahi kwa yale aliyowapa Mola wao. Na Mola wao atawalinda na adhabu ya Motoni.
Neno ‘wakifurahia’ tumelifasiri kutokana na neno fakihina ambalo pia lina maana ya kuwa njema nafsi. Maana zote mbili zinaendana na Pepo na neema. Lakini maana ya kufurahia inaafikiana zaidi na kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia: Kuleni na kunyweni kwa raha.
Maana ni kuwa walimcha Mwenyezi Mungu duniani, naye amewakinga na adhabu ya Moto na amewafanyia Pepo kuwa ndio malipo yao.
Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.
Nyinyi wacha Mungu, mna haki zaidi ya neema hii, kwa sababu mlifanya kwa ikhlasi. Aya inafahamisha kuwa hakuna heshima yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kiumbe isipokuwa kwa kufanya amali. Ama vyeo nasaba na mali si chochote, ila zikiwa ni nyenzo za heri na masilahi ya umma.
Wakiegema viti vya fahari vilivyopangwa safu.
Kuegema viti pamoja na kuwa faragha, kunafahamisha kutokuwa na matatizo ya maisha na tabu zake.
Na tutawaoza mahurulaini,
wanovutia akili na macho kwa uzuri wao na ukamilifu wao. Neema iliyoje!
Na walioamini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao.
Hakuna mwenye shaka kwamba watoto wadogo hawataadhibiwa kwa hali yoyote ile; ni sawa wazazi wao wawe wema au waovu, kwa sababu hakuna adhabu bila ya uasi, wala hakuna uasi bila taklifa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwondolea kalamu mtoto mdogo mpaka abaleghe.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekariri katika Aya kadhaa kauli yake: “Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.” Juz. 8 (6:164).
Ama kauli ya anayesema kuwa mtoto wa kafiri ataingia motoni, kwa vile kama angeliishi basi angelifuata dini ya baba, kuali hii imeachwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu humuhisabu mtu kwa aliyoyatenda, wala hamuhisabu kwa ambayo angeliyatenda.
Unaweza kuuliza
: Je, watoto wadogo watafufuliwa na kuingia Peponi?
Jibu
: Hakuna njia ya kujua hilo isipokuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Nabii wake. Akili hapa haina nafasi ya kuhukumu; wala hakuna katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu au Hadith mutawatir kwamba watoto wa makafiri watafufuliwa.
Kuna Hadith isemayo: “Hakika waumini wataongozwa kwa baba zao wenye takua siku ya kiyama.” Wafasiri wengi wamesema kuwa watoto wakubwa wa waumini katika kizazi cha wanaomcha Mwenyezi Mungu watakutanishwa na daraja za juu za mababa zao Peponi, hata kama amali zao njema ziko chini, ili wazazi waburudike nao. Wameitolea dalili kauli yao hiyo kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na wala hatutawapunja kitu katika vitendo vyao;
yaani tutawazidisha karama mababa wala hatutawapunguzia mababa kitu chochote katika thawabu zao na daraja zao.
Shia Imamia, Hanafi, Shafii na Hambali wamesema kuwa mtoto atahukumiwa kuwa ni Mwislamu kutokana na mmoja wa wazazi wake. Akiwa mmoja ni mwislamu na mwingine ni kafiri, basi mtoto atahukumiwa kuwa ni Mwislamu, bila ya kuangalia aliye kafiri ni baba au mama. Lakini Malik wamesema unaozingatiwa ni Uislamu wa baba tu, lakini mama hana athari yoyote ya Uislamu kwa mtoto wake.
Kila mtu ni rehani wa alichokichuma.
Yeye peke yake atafuatwa na matendo yake na kwayo ndio atakubaliwa nayo kesho kwa Mungu wala hataulizwa aliyotenda mwingine.
Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyopenda.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kutaja matunda na nyama, kwa sababu ndio vyakula vikuu.
Watapeana humo bilauri zisio na (vinywaji) vya upuuzi wala dhambi.
Watakunywa vinywaji vya kuchangamsha, lakini visivyokuwa na ulevi au vurugu wala kusababisha dhambi na kuchukuliana maneno.
Na watawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizofichwa.
Kusema kwake Mwenyezi Mungu ‘watumishi wao’ ni ishara yakuwa wao watafuata amri zao na makatazo yao.
Wataelekeana wakiulizana.
Wataulizana ilivyokuwa duniani, Vipi wamestahiki heshima hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 23 (37:50).
Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa.
Tulimwogopa Mwenyezi Mungu duniani kwa kuhofia ghadhabu yake na kutumai thawabu zake,Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani
kwa rehema yake, akatuhusisha na neema yakena akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto
unaoambua ngozi na kuunguza nyuso.
Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
Duniani tulikuwa wema wenye huruma, na Mwenyezi Mungu huku Akhera amekuwa mwema kwetu na Mwenye huruma.