2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قِيلَ لَكُمْ تَفَسَّحُوا فِي الْمَجَالِسِ فَافْسَحُوا يَفْسَحِ اللَّـهُ لَكُمْ وَإِذَا قِيلَ انشُزُوا فَانشُزُوا يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١١﴾
11. Enyi mlioamini! Mkiambiwa: fanyeni nafasi katika vikao, basi fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atawafanyia nafasi. Na mkiambiwa: ondokeni, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua daraja walioamini miongoni mwenu, na waliopewa ilimu. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyatenda anazo habari.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَاجَيْتُمُ الرَّسُولَ فَقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَةً ذَٰلِكَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَأَطْهَرُ فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢﴾
12. Enyi mlioamini! Mnaponong’onezana na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya kunong’ona kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
أَأَشْفَقْتُمْ أَن تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَاتٍ فَإِذْ لَمْ تَفْعَلُوا وَتَابَ اللَّـهُ عَلَيْكُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٣﴾
13. Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kunong’ona kwenu? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi simamisheni Swala, na toeni Zaka, na mtiiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu ana habari kwa mnayoyatenda.
FANYENI NAFASI MWENYEZI MUNGU ATAWAFANYIA NAFASI
Aya 11 – 13
MAANA
Enyi mlioamini! Mkiambiwa: fanyeni nafasi katika vikao, basi fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atawafanyia nafasi.
Maswahaba walikuwa wakiwahi kwenye vikao vya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
na wakipupia kuwa karibu naye. Mara nyingi vikao vilikuwa na msongamano wa watu. Aliyewahi hakuwa akimpa nafasi anayekuja, basi analazimika kurudi au kukalia nyayo zake. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawafundisha adabu ya kiislamu; Akawaamuru kuwapa nafasi wengine kwenye vikao na akawaahidi kuwapa nafasi Peponi.
Na mkiambiwa: ondokeni, basi ondokeni.
Kwanza Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamuru waliokaa wawatengenezee nafasi wengine; kisha akawaamuru kumsikiliza Mtume(s.a.w.
w
)
akiwataka kuachia nafasi wengine ikiwa nafasi haitoshi.
Kuna riwaya inayosema kuwa Mtume(s.a.w.
w
)
alikuwa akiwasimamisha baadhi ili wakae wale waliotangulia kwenye mambo mema, na ikawa wengine wanaonyesha kuchukia kwenye nyuso zao. Lakini baada ya kushuka Aya hii walifanya heshima na kuwapisha ndugu zao kwa moyo safi kabla ya kuamuriwa na Mtume(s.a.w.
w
)
.
Kuna tafsiri nyingine zinazosema kuwa maana ni: mkiambiwa ondokeni kwenda kwenye mambo ya heri basi itikieni. Hili haliko mbali, kwa sababu amri inaenea kwenye maana yote; iwe ni kutoa nafasi, kufanya jihadi au mengineyo.
Ndio! Katika adabu za Qur’an ni mtu kumfanyia nafasi ndugu yake au kumpisha pale alipokaa yeye, lakini sio adabu wala maadili mema kwa yule aliyekuja kumwondoa mahali pake yule aliyekaa.
Mtume(s.a.w.
w
)
alikuwa akikaa mwisho walipokaa watu, ila ikiwa mwenye kikao atamtaka mtu ampishe ndio anamwitikia, lakini vile vile haitakikani kwa mwenye kikao kumwondoa mtu isipokuwa kwa sababu ya maana; kama vile aliyekaa kukikosea adabu kikao au ikiwa aliyekuja ana shani na daraja mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
Mwenyezi Mungu atawainua daraja walioamini miongoni mwenu, na waliopewa ilimu. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyatenda ana habari.
Mwenyezi Mungu anawajua watu bora na anajua daraja za ubora naye anampa kila mwenye fadhila haki yake. Bora zaidi katika watu ni yule aliye zaidi kujichunga na aliyoyaharimisha Mwenyezi Mungu. Ikiwa pamoja na kujichunga hivi ana mwamko na ilimu basi atakuwa juu ya walio juu.
Hakuna mwenye shaka kwamba kumwadhimisha aliyeadhimishwa na Mwenyezi Mungu ni faradhi ya lazima. Kuna Hadith inayosema kuwa Mtume alikuwa akiwatukuza watu wa Badr na kuwatanguliza juu ya wengine. Siku moja waliingia baadhi yao kwenye majilisi yake wakakuta watu wamesongamana kwake wala hakuna yeyote aliyewapisha.
Mtume(s.a.w.
w
)
akawaambia wale waliokaribu yake: ni nani ambaye si katika watu wa Badr. Simama ewe fulani na wewe ewe fulani, na akawakalisha watu wa Badr.
Riwaya hii inaafikiana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Mwenyezi Mungu atawainua daraja walioamini miongoni mwenu…”
KUKAA MBELE KWENYE KIKAO
Mimi ninaposoma makala ya gazeti inayofungamana na maudhui ya Aya yoyote katika Qur’an Tukufu huwa ninaiweka kwenye faili maalum, mpaka nikifikia kuifasiri basi ninairudia ile makala na kuitolea ushahidi.
Pia huwa ninaashiria jina la gazeti na tarehe yake, kwa sababu kizazi kipya wanakinaika na magazeti zaidi kuliko rejea nyingine; kwa mfano kama kwenye Juz. 13 (13:5-7) kifungu cha ‘wanaoamini maada na maisha baada ya mauti.’ Juz. 15 (17: 82-85), kfungu cha: ‘Mwenyezi Mungu na ilimu ya chembe hai,’ Juz. 23 (38: 65-88), kifungu cha: Uislamu na msichana wa kiingereza,’ na Juz. 24 (41:37-46) kifungu cha ‘safari ya mwezini.’
Basi siku moja nilisoma mojawapo ya majarida ya wanasiasa wakubwa kuhusu meza ya maelewano kuwa ni nani atakayekaa mbele, ni nani atakayekuwa nyuma na ni ujumbe upi utatangulia kwenye chumba cha mkutano kabla ya mwingine.
Katika mfano alioutoa mwandishi ni ule wa mwaka 1945 baada ya vita ya pili ya dunia: Waliafikiana Churchill, Stalin na Roosevelt kukutana kwa majadiliano ya mapatano mjini Budabest, lakini wakatofautiana kuwa ni nani atakayeingia kwanza kwenye ukumbi wa mkutano. Ubishi huu uliendelea kwa muda kisha suluhisho likawa wakutane kwenye ukumbi wenye milango mitatu ili wote waingie kwa wakati mmoja.
Nimeikumbuka makala hiyo na kuileta hapa ili aone msomaji kuwa Uislamu unaipa kipaumbele ilimu na ikhlasi. Haya ndio maendeleo ya haki na uadilifu kwa maana yake sahihi, lakini kuwatukuza wanaotengeneza mauti, wanaomiliki makombora ya Menotman na CC, na silaha nyinginezo za maangamizi, hakuna uzito wowote isipokuwa katika sharia ya shetani na maendeleo ya vita na uchokozi.
Enyi mlioamini! Mnaponong’onezana na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya kunong’ona kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Sioni tafsiri nzuri zaidi ya Aya hii kuliko ile ya Muqatil bin Hayan, aliposema: “Matajiri waliwazidi mafukara kwenye vikao vya Mtume(s.a.w.
w
)
- hii ndio hali yao kila mahali na kila wakati - wakazidisha kumnong’oneza Mtume mpaka akachukia kukaa kwao sana, ndio Mwenyezi Mungu akaamuru sadaka.
Basi matajiri wakajizuia kutoa na mafukara wakakosa cha kutoa, wakamlilia hali Mtume na kutamani kutoa lau wangelikua nacho na kukifikisha kwenye vikao vya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
. Hapo daraja ya mafukara ikazidi, mbele ya Mwenyezi
Mungu na daraja ya matajiri ikaanguka.” Katika tafsiri kadhaa ikiwemo Tafsiru ttabari na Tafsiru rrazi imeelezwa kuwa hakuifanyia kazi Aya hii isipokuwa Ali bin Abu Twalib
. Alikuwa na dinar moja akaivunja zikawa dirham 10, akawa kila anapotaka kusemezana na Mtume hutoa sadaka dirhamu moja. Kisha hukumu hiyo ikaondolewa kabla ya kuitekeleze mwingine asiyekuwa Ali.
Mwenye Tafsir Ruhulbayan anasema: “Imepokewa kutoka kwa Imran kuwa Yeye amesema: Imepokewa kutoka kwa Abdallah bin Imran kuwa amesema: Ali alikuwa na mambo matatu, lau ningelikuwa na mojawapo kati ya hayo ingelikuwa bora kwangu kuliko wanyama wekundu: Kumuoa Fatima, kupewa bendera siku ya Khaybar na Aya ya mnong’ono.”
Mnachelea ufukara kuwa hamtaweza kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kunong’ona kwenu? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi simamisheni Swala, na toeni Zaka, na mtiiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Ilipokuwa uzito kwa matajiri kutoa sadaka kwa kuhofia kuisha mali yao, na Mwenyezi Mungu akalijua hilo, na wakajua kuwa wakati wa Mtume sio wao peke yao tu, ni wakufikisha ujumbe na kupanga mambo ya Waislamu, ndio Mwenyezi Mungu akaruhusu kunong’ona na Mtume bila ya kutoa sadaka na akawasamehe wale wasiotoa, lakini wasizembee swala, Zaka na mengineyo.
Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
Haufichiki kwake wema wa mwenye kufanya wema na uovu wa mwenye kufanya uovu na atamlipa kila mmoja stahiki yake.
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ تَوَلَّوْا قَوْمًا غَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مَّا هُم مِّنكُمْ وَلَا مِنْهُمْ وَيَحْلِفُونَ عَلَى الْكَذِبِ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٤﴾
14. Huwaoni wale waliofanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo, na hali ya kuwa wanajua.
أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾
15. Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda ni maovu kabisa.
اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٦﴾
16. Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watapata adhabu ifedheheshayo.
لَّن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١٧﴾
17. Haitawafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio watu wa motoni, wao watadumu humo.
يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيَحْلِفُونَ لَهُ كَمَا يَحْلِفُونَ لَكُمْ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ عَلَىٰ شَيْءٍ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٨﴾
18. Siku atakayowafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuapie kama wanavyowaapia nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Ehe! Kwa hakika hao ndio waongo.
اسْتَحْوَذَ عَلَيْهِمُ الشَّيْطَانُ فَأَنسَاهُمْ ذِكْرَ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ الشَّيْطَانِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ الشَّيْطَانِ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٩﴾
19. Shetani amewatawala na akawasahaulisha dhikr ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi la Shetani. Ehe! hakika kundi la Shetani ndilo lenye kuhasirika.
WAMEFANYA VIAPO VYAO NI NGAO
Aya 14 – 19
MAANA
Huwaoni wale waliofanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo, na hali ya kuwa wanajua.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
. Waliofanya urafikki ni wanafiki, waliokasirikiwa na Mwenyezi Mungu ni mayahudi na nyinyi, ni nyinyi waislamu. Maana ni kuwa hebu niambie ewe Muhammad kuhusu wanafiki! Wamefanya urafiki na mayahudi na wakapanga njama nao dhidi ya waislamu na uislamu; wakiwa na uhakika kuwa wao si waisalamu wala si katika mayahudi, ni vizabizabina, huku hawako wala kule hawako.
Wameapa kwa kukusudia uwongo kuwa ni waislmu na kwamba hawakusema kitu wala kupanga njama na mayahudi. Kwa ajili ya unafiki wao na viapo vyao vya uwongo,Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda ni maovu kabisa
. Kila mwenye kudhihirisha kinyume na yaliyo kwenye dhamiri yake basi ni muovu kwa kauli yake na vitndo vyake, kwa sababu amejitoa kwenye dhati yake na hakika yake.
Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watapata adhabu ifedheheshayo.
Yaani wanafiki wanajaribu kufanya njama zao kwa viapo vya uwongo na kujikinga navyo; huku wakiwahadaa wale wanaotaka uongofu na kuwazuia na malengo yao, lakini Mwenyezi Mungu hafichwi na kinga yoyote wala dhamiri zozote. Basi ameipasua sitara yao duniani, na Akhera watapata adhabu ya kufedhehesha.
Haitawafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio watu wa motoni, wao humo watadumu.
Walipata fursa katika maisha ya duniani, lakini wakaichezea, wala hakuna kitu kwa yule mwenye kuvuta muda na kupuuza isipokuwa adhabu. Na si mali wala watoto inayoweza kurudisha yaliyopita.
Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 4 (3:116).
Siku atakayowafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuapie kama wanavyowaapia nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Ehe! Kwa hakika hao ndio waongo.
Siku ya Kiyama, waja watakuwa na hali mbalimbali; kuna wengine watahurusiwa kuzungumza. Basi Mwenyezi Mungu atakapowapa fursa ya kuzungumza, wakosefu, watamuapia kwa uwongo, kama walivyokuwa wakimwapia Nabii na waislamu duniani; wakiamini kuwa viapo vyao vitawakinga na adhabu. Vipi iwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu anajua kuwa wao ni waongo katika imani zao na itikadi zao?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:22).
Shetani amewatawala na akawasahaulisha dhikr ya Mwenyezi Mungu.
Shetani wa matamanio aliwaita kwenye upotevu na ufisadi nao wakamwitikia, basi wakapofuka na uwongofu.
Hao ndio kundi la Shetani. Ehe! hakika kundi la Shetani ndilo lenye kuhasirika.
Kwa sababu, vyovyote vile iwavyo, mwenye kumfanya shetani ni kiongozi wake, atamwongoza kwenye kila uovu na maangamizi, iwe kesho au kesho kutwa; hata kama atajisheheni mabomu na makombora.
إِنَّ الَّذِينَ يُحَادُّونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ فِي الْأَذَلِّينَ ﴿٢٠﴾
20. Hakika wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho.
كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾
21. Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mitume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.
لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٢٢﴾
22. Hupati watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanapendana na wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika mabustani yapitiwayo na mito chini yake. Humo watadumu. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu. Ehe! Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.
BILA SHAKA NITASHINDA MIMI NA MITUME WANGU
Aya 20 – 22
MAANA
Hakika wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho.
Aya hii ina mshabaha wa jibu la swali la kukisiwa, kwamba maadui wa Mwenyezi Mungu wanaishi wakiwa na nguvu ya maandalizi na idadi, wakiendelea kuwatesa watu wa Mwenyezi Mungu kwa mauaji na kuwatorosha, vipi Mwenyezi Mungu anawapa muda na kuwapa nguvu?
Aya inajibu kuwa washari ndio viumbe dhalili zaidi kuanzia mwanzo hadi mwisho, kwa sababu mwisho wao ni hizaya na udhalili duniani na Akhera. Hapa duniani ni kuwa Mwenyezi Mungu anawaadhibu kwa mikono ya waliowema:
قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُّؤْمِنِينَ ﴿١٤﴾
“Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin.” Juz. 10 (9:14).
Ama adhabu ya Akhera hiyo ni kali na ni kubwa zaidi.
Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mitume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.
Ushindi utakuwa Akhera, na vile vile utakuwa duniani kwa upanga, adhabu ya kutoka mbinguni, hoja na dalili au kwa kudumu utajo.
Tazama Juz. 17 (38-41) kifungu cha: “Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini.” Vile vile Juz. 26 (47:7).
Hupati watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanapendana na wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao.
Haiwezekani kabisa imani ichanganyike na mahaba ya makafiri. Itakuwaje hivyo na hali Mwenyezi Mungu ndiye Aliyesema:
مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ﴿٤﴾
“Mwenyezi Mungu hakumwekea mwanamume nyoyo mbili ndani yake.” Juz. 21 (33:4).
Kuna kauli mashuhuri kutoka kwa Imam Ali
kuwa rafiki wa adui ni adui. Pia akasema: “Tulikuwa pamoja na Mtume(s.a.w.w)
mapigano yakiendela kwa mababa, watoto, ndugu na jamaa. Kila msiba na shida haukutuzidisha isipokuwa imani na kuendelea kwenye haki na kusalimu amri.” Hayo tumeyazungumzia kwa ufafanuzi zaidi kwenye Juz.4 (3:28).
Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake.
‘Hao’ ni ni wale ambao imani yao haiathiriki hata kwa mababa na mama zao. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amethibitishia imani katika nyoyo za wenye ikhlasi na akawapa nguvu kwa hoja: “Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera.” Juz. 13 (14:27).
Na atawaingiza katika Mabustani yapitiwayo na mito chini yake. Humo watadumu. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye.
Maana ya Mwenyezi Mungu kumridhia mja wake ni kumpa fadhila zake, na maana ya mja kumridhia Mola wake ni kuridhia aliyompa. Ibn Al-arabiy, anasema katika Futuhat: “Mwenyezi Mungu huridhia amali chache ya mja wake na wao wanaridhia thawabu chache walizopata kutoka kwa Mola wao, kwani kadiri Mwenyezi Mungu anavyotoa ni vichache kulingana na vilivyoko kwake.”
Lakini hivi alivyoviita vichache Ibn al-arabiy, ni vichache kwa Mwenyezi Mungu Mtufu na ni vingi kwa waja. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Ili amzidishie ziada nyingi.” Juz. 2 (2:245).
Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu. Ehe! Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.
Aya hii ni mkabala wa Aya 19 ya Sura hii tuliyo nayo inayosema: “Hao ndio kundi la Shetani. Ehe! hakika kundi la Shetani ndilo lenye kukhasirika.”
Kwa ufupi ni kuwa mtu kadiri atakavyokuwa na uwezo, lakini hawezi kuchanganya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kuwaridhisha maadui wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akiwaridhisha atakuwa amemghadhabisha Mwenyezi Mungu na akimridhisha Mungu atakuwa amewaghadhibisha maadui. Wao hawaridhii isipokuwa yule aliye katika hali yao, kwa ushahidi wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu:
وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ﴿١٢٠﴾
“Hawatakuwa radhi nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila yao.” Juz. 1 (2:120).
Katika Hadith Mtume(s.a.w.w)
anasema:“Ewe Mwenyezi Mungu usinijaalie muovu wala fasiki kwangu, kwani nimekuta katika yale uliyatolea wahyi kuwa: “Hupati watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanapendana na wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”
MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA NANE: AL–MUJADALA