19
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sabini Na Mmoja: Surat Nuh. Imeshuka Makka Ina Aya 28.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
إِنَّا أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ أَنْ أَنذِرْ قَوْمَكَ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١﴾
1. Hakika Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake: Uwaonye kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu.
قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢﴾
2. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa dhahiri kwenu,
أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاتَّقُوهُ وَأَطِيعُونِ ﴿٣﴾
3. Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche, na munitii.
يَغْفِرْ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُؤَخِّرْكُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى إِنَّ أَجَلَ اللَّـهِ إِذَا جَاءَ لَا يُؤَخَّرُ لَوْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤﴾
4. Atawaghufiria miongoni mwa madhambi yenu, na atawaakhirisha mpaka muda uliowekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapofika haucheleweshwi. Laiti mngejua!
قَالَ رَبِّ إِنِّي دَعَوْتُ قَوْمِي لَيْلًا وَنَهَارًا ﴿٥﴾
5. Akasema: Ee Mola wangu! Hakika mimi nimewalingania watu wangu usiku na mchana.
فَلَمْ يَزِدْهُمْ دُعَائِي إِلَّا فِرَارًا ﴿٦﴾
6. Lakini mlingano wangu haukuwazidisha ila kukimbia.
وَإِنِّي كُلَّمَا دَعَوْتُهُمْ لِتَغْفِرَ لَهُمْ جَعَلُوا أَصَابِعَهُمْ فِي آذَانِهِمْ وَاسْتَغْشَوْا ثِيَابَهُمْ وَأَصَرُّوا وَاسْتَكْبَرُوا اسْتِكْبَارًا ﴿٧﴾
7. Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakafanya kiburi kingi!
ثُمَّ إِنِّي دَعَوْتُهُمْ جِهَارًا ﴿٨﴾
8. Tena niliwalingania kwa uwazi,
ثُمَّ إِنِّي أَعْلَنتُ لَهُمْ وَأَسْرَرْتُ لَهُمْ إِسْرَارًا ﴿٩﴾
9. Kisha nikawatangazia, tena nikasema nao kwa siri.
فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا ﴿١٠﴾
10. Nikasema: Ombeni maghufira kwa Mola wenu; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe.
يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا ﴿١١﴾
11. Atawaletea mvua nyingi.
وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا ﴿١٢﴾
Na atawapa mali na wana, na atawapa mabustani na atawafanyia mito.
NILIWALINGANIA WATU WANGU
Aya 1 - 12
MAANA
Hakika Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake: Uwaonye kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu.
Sheikh Abdul-qadir Al-Maghrib, akifasiri Aya hizi alinukuu vitabu vya mwanzo mwanzo kwamba Historia ya kuabudu masanamu inaanzia zama za Anush bin Shith bin Adam, na kwamba wakati wa Nuh shirki ilifikia ukomo, ndio akachaguliwa na Mwenyezi Mungu kupambana na shiriki hii na kuwaonya washirikina na maangamizi kama watanga’ang’ania upotevu.
Jina halisi la Nuh ni Raha, na baina ya Nuh na babu yake mkubwa Adam, kuna miaka 1056. Ilipotokea tufani umri wake ulikuwa ni miaka 600, na aliishi miaka 350 baada ya hapo. alimuwahi mjukuu wake Ibrahim na akaishi naye zaidi ya nusu karne. Baada ya Nuh kuokoka na tufani alilima na kupanda kwenye ardhi.
Huu ni muhtasari wa aliyoyanukuu Al-Maghribi kutoka kwenye vitabu hivyo, Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi.
Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa dhahiri kwenu. Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche, na munitii.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtuma Nuhu kwa watu kwa mambo matatu: Kwanza, Waache kuabudu masanamu na kumwabudu Mungu mmoja. Pili, wafanye kheri na wajiepushe na shari. Tatu, wamtii katika yale aliyowaamrisha na kuwakataza. Akawadhaminia mambo mawili kwa Mwenyezi Mungu, kama wataitikia:
La kwanza:Atawaghufiria miongoni mwa madhambi yenu,
mliyoyafanya kabla ya imani, kwa sababu imani inafuta yaliyo kabla yake, lakini yale madhambi mtakayoyafanya baada ya imani mtakua na majukumu nayo. Haya yanashiriwa na neno ‘miongoni mwa dhambi yenu.’
La pili:Na atawaakhirisha mpaka muda uliowekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapofika haucheleweshwi.
Mkimwamini Mwenyezi Mungu peke yake atawaondolea adhabu ya kuangamizwa na tufani nk, atawapa muda wa kumaliza umri wa kawaida na mwenye dhambi atampa muda hadi siku ya Kiyama; vinginevyo atawaharakishia adhabu ya kuangamia duniani.
Laiti mngejua
, kuwa Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na wanayoyafanya madhalimu.Akasema: Ee Mola wangu! Hakika mimi nimewalingania watu wangu usiku na mchana, Lakini mlingano wangu haukuwazidisha ila kukimbia.
Maana ya usiku na mchana ni daima. Nuhu aliwaita kwenye haki na akawasisitiza, mpaka: “Wakasema: Ewe Nuh! Umejadiliana nasi na umezidishi kutujadili.” Juz. 12 (11:32), lakini yeye aliendelea na mwito wake na wao wakaendelea na inadi yao.
Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakafanya kiburi kingi!
Walijiziba masikio kwa vidole ili wasisikie mwito wa haki, na walijifunika nguo ili wasiuone uso wa mwenye kulingania. Hii inaweza kuwa ni hakika hasa, na pia inaweza kuwa ni kwa majazi ya inadi yao. Vyovyote iwavyo, maana ni moja tu, nayo ni kuikataa haki kwa kiburi. Nuh walimuona ana daraja ya chini kuliko wao, kwa hiyo wakaona vipi wanaweza kuwa wafuasi wake? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwasimulia wao:
وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ وَمَا نَرَىٰ لَكُمْ عَلَيْنَا مِن فَضْلٍ ﴿٢٧﴾
“Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu.” Juz. 12 (11:27).
Tena niliwalingania kwa uwazi, Kisha nikawatangazia, tena nikasema nao kwa siri.
Kundi la wafasiri wamesema kauli ya Nuh ya kwanza: Nimewalingia watu wangu usiku na mchana, na kauli ya pili: Tena niliwalingania kwa uwazi na kauli ya tatu: kisha nikawatangazia na nikasema nao kwa siri, zinajulisha kuwa mwito wake ulikuwa na daraja tatu: aliuanza kwa siri, kisha akaufanya wazi, tena mara ya tatu akautangaza na kuufanya siri pamoja.
Kauli hii haiko mbali na dhahiri ya Aya, lakini inawezekana pia kuwa makusudio ya maunganishi haya na kukaririka huku ni kuwa yeye aliwalingania kwa kila mfumo bila ya kuchoka, lakini pia haikufaa kitu.
Nikasema: Ombeni maghufira kwa Mola wenu; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Atawaletea mvua nyingi. Na atawapa mali na wana, na atawapa mabustani na atawafanyia mito.
Ikiwa watamwamini Mwenyezi Mungu peke yake na wakamfanyia ikhlasi kwa kauli na vitendo, basi Nuhu atawadhaminia kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) awasamehe maovu yao yaliyoopita na awatoshelezee katika fadhila zake kwa mali na watoto; mbingu zimimine heri zake na ardhi nayo itoe mazao yake na wawe na siha, amani, raha pamoja na kuzidi kizazi.
IMANI NA RAHA
Aya hizi zimeifunga raha na amani kuwa lazima ziwe pamoja na imani na takua, lakini inavyoonekana ni kinyume na hivyo. hai ni Marekani (U.S.A.). Inajulikana kuwa hiyo ndio dola iliyo na ubabe kuliko yoyote duniani, ndiyo yenye ufisadi na uadui zaidi; mpaka ikajiwekea msingi kuwa asiyekuwa mtumwa wake basi huyo ni adui yake. Sote tunajua siasa yao hiyo jinsi ilivyoleta majanga - hakuna damu inayomwagika au ufisadi unajitokeza mashariki mwa dunia na magharibi ila Marekani ina mkono wake, kwa namna moja au nyingine. Hakuna mhaini yeyote wa nchi yake ila wanamtukuza.
Pamoja na haya yote hiyo ndio dola tajiri na yenye nguvu zaidi ulimwenguni. Ushahidi wa hilo ni kuwa pato lake ni asilimia 43 ya pato lote la ulimwengu na hali wakazi wake ni asilimia 6 tu ya wakazi wote waulimwengu
.
Sasa kuna wajihi wa kuunganisha haya na dhahiri ya Aya inayoifunga raha na imani?
Jibu
:kwanza
, Aya hizi zilihusiana na watu wa Nuh, na hakuna dalili ya kuwa zinaenea, ili zihusaiane na wengine. Kuongezea kuwa Mwenyezi Mungu ana muamala maalum na umma unaoonywa na mitume wake moja kwa moja.
Pili
, utajiri wa U.S.A. unatokana na shetani sio na Mwenyezi Mungu, kwa sababu zaidi sana umetokana na uporaji na unyang’anyi.
Tatu
, Aya hizi zimeunganisha baina ya imani na raha ya dunia na Akhera kwa pamoja. Sio imani na raha ya dunia peke yake: “Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa, ni heri kwa nafsi zao. Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika (kufanya) dhambi na wana wao adhabu idhalilishayo.” Juz. 4 (3:178).
Nne
, umejuaje kuwa Amerika na dola nyingine dhalimu ziko kwenye amani? Ni nani mwenye akili anayejiaminisha na majanga? Je, himaya ya Roma ilidumu? Au ya uingereza na himaya nyinginezo zilidumu mpaka udumu ufidhuli wa USA?
Hizi hapa dalili za kuanguka zinaanza kujitokeza, kuanzia mawimbi ya ukombozi ulimwenguni kote hadi kwenye mapinduzi ya watu weusi wapatao milioni thalathini ndani ya USA. Na kuanzia utawala wa ujasusi wakuua na kuanzisha vita hadi kwenye bangi na madawa ya kulevya, na kuanzia ugomvi na uadui pamoja na watu wa mabara yote matano hadi kwa raisi anayewalinda wezi na wamwagaji damu na mengine yasiyokuwa na kikomo.
Ni muhali kudumu amani na raha kwa mfumo huu wa kushangaza.
Ajabu ni sadfa iliyotokea wakati nikandika maneno haya nikasoma gazeti la Aljumhuriya la Misr la tarehe 10 ‧ 7- 1970, likinukuu magazeti ya New York, kwamba mashoga wapatao elfu tano wazee kwa vijana wameandamana kwenye barabara za New York, wakibeba mabango wakitaka serikali ihalalishe ulawiti, kwa kuiga wanawake waaliohalalishiwa kujiuza miili yao (umalaya).
Kwenye gazeti la News wee^ la tarehe 12 -7-1970, kuna maelezo kuwa kasisi Barry ambaye ni mashuhuri kwa ulawiti alitoa mwito wa kueneza ulawiti na usagaji, kwa sababu mambo hayo mawili ni katika upendo wa Mungu. Mwito wake huu umeenea na kuwa na wafuasi wengi katika pembe zote za USA.
Hakuna mwenye shaka kwamba katika mashoga na mabasha hawa watatokea viongozi watakaotawala siasa za usalama na vita, mambo ya elimu na kazi katika jamii ya Marekani. Hapo ndio itakuwa USA ni duni kuliko nyumba ya buibui.
مَّا لَكُمْ لَا تَرْجُونَ لِلَّـهِ وَقَارًا ﴿١٣﴾
13. Mna nini hamumwekei heshima Mwenyezi Mungu?
وَقَدْ خَلَقَكُمْ أَطْوَارًا ﴿١٤﴾
14. Na hali Yeye amewaumba katika hali mbalimbali?
أَلَمْ تَرَوْا كَيْفَ خَلَقَ اللَّـهُ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ﴿١٥﴾
15. Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka?
وَجَعَلَ الْقَمَرَ فِيهِنَّ نُورًا وَجَعَلَ الشَّمْسَ سِرَاجًا ﴿١٦﴾
16. Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa?
وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ﴿١٧﴾
17. Na Mwenyezi Mungu amewaotesha katika ardhi kama mimea.
ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا ﴿١٨﴾
18. Kisha atawarudisha humo na atawatoa tena.
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ بِسَاطًا ﴿١٩﴾
19. Na Mwenyezi Mungu amewafanyia ardhi kuwa busati.
لِّتَسْلُكُوا مِنْهَا سُبُلًا فِجَاجًا ﴿٢٠﴾
Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.
AMEWAUMBA KATIKA HALI MBALIMBALI
Aya 13 - 20
MAANA
Mna nini hamumwekei heshima Mwenyezi Mungu? Na hali Yeye ame waumba katika hali mbalimbali?
Nuhu anawakana watu wake huku akiwashangaa, vipi hawamwogopi Mwenyezi Mungu pamoja na utukufu wake, na hali wanajua kwamba Yeye amewaumba kwa mchanga, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu. Anaendela hivi hadi kuwa mkongwe.
Vile vile anawaelekeza kuuangalia uwezo wa Mwenyezi Mungu katika kuumba mbingu na ardhi na sayari, akasema:
Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka?
Chunguzeni na mzingatie umbile la mbingu na nidhamu yake inayojulisha kupatikana mtengenezaji mwenye hikima. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo kwenye sura (67:3). Pia tumeifafanua kidogo katika Juz. 28 (66:12).
Kauli ya Nuh inafahamisha kuwa watu wake walikuwa pia wakiamini kuwa mbingu ni saba na kwamba itikadi hii ilianzia zamani za kale.
Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa?
Ndani yake ni ndani ya mkusanyiko wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelipa Jua sifa ya taa na mwezi kuwa ni nuru, kwa sababu taa ndio chimbuko la nuru na Jua nalo ni chimbuko la mwezi na mwanga wake unaenea na una manufaa zaidi kuliko wa mwezi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11(10:5).
Na Mwenyezi Mungu amewaotesha katika ardhi kama mimea. Kisha atawarudisha humo na atawatoa tena.
Huyu ndiye mwanadamu. Ameumbwa kutokana na ardhi, kisha arudishwe humo, tena atolewe humo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:55).
Na Mwenyezi Mungu amewafanyia ardhi kuwa busati ili mtembee humo katika njia zilizo pana.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefanya njia pana katika ardhi ili watu wayaendee makusudio yao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (21:32).
قَالَ نُوحٌ رَّبِّ إِنَّهُمْ عَصَوْنِي وَاتَّبَعُوا مَن لَّمْ يَزِدْهُ مَالُهُ وَوَلَدُهُ إِلَّا خَسَارًا ﴿٢١﴾
21. Nuh akasema: Mola wangu! Hakika hao wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila hasara.
وَمَكَرُوا مَكْرًا كُبَّارًا ﴿٢٢﴾
22. Na wakapanga vitimbi vikubwa.
وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا ﴿٢٣﴾
23. Na wakasema: Msiwaache miungu yenu; msimwache Wadda wala Suwaa wala Yaghutha, wala Yau’qa, wala Nasra.
وَقَدْ أَضَلُّوا كَثِيرًا وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا ضَلَالًا ﴿٢٤﴾
24. Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala usiwazidishie waliodhulumu ila kupotea.
مِّمَّا خَطِيئَاتِهِمْ أُغْرِقُوا فَأُدْخِلُوا نَارًا فَلَمْ يَجِدُوا لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ أَنصَارًا ﴿٢٥﴾
25. Basi kwa ajili ya makosa yao kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
وَقَالَ نُوحٌ رَّبِّ لَا تَذَرْ عَلَى الْأَرْضِ مِنَ الْكَافِرِينَ دَيَّارًا ﴿٢٦﴾
26. Na Nuh akasema: Mola wangu! Usimwache juu ya ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri!
إِنَّكَ إِن تَذَرْهُمْ يُضِلُّوا عِبَادَكَ وَلَا يَلِدُوا إِلَّا فَاجِرًا كَفَّارًا ﴿٢٧﴾
27. Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao hawatazaa ila waovu makafiri.
رَّبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَن دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا تَبَارًا ﴿٢٨﴾
28. Mola wangu! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na kila aliyeingia nyumbani mwangu kuwa ni mumin, na waumini wanaume, na waumini wanawake; na wala usiwazidishie waliodhulumu
ila kuangamia.
WALA MSIMWACHE WADDA WALA SUWAA
Aya 21 - 28
MAANA
Nuhu akasema: Mola wangu! Hakika hao wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila hasara.
Hii ni ripoti au mashtaka kutoka kwa Nuh kwenda kwa Mola wake, akimwambia Mola wangu na Bwana wangu! Umenituma kuwaongoza waja wako washirikina, nimetekeleza ujumbe kwa njia yake, lakini wao wamenipinga, wakawaitikia viongozi walioingiwa na kiburi kutokana na mali na watoto. Kila wanavyozidi mali na watoto, basi wanazidi kufuru, inadi na kuwa na nguvu ya kupiga vita haki na watu wake, kwa kupupia jaha na chumo lao.
Na wakapanga vitimbi vikubwa.
Yaani hao viongozi waliopituka mipaka. Makusudio ya vitimbi vyao, ni mifumo waliyookuwa wakiitumia kuwazuia wanyonge kuwa na imani; miongoni mwayo ni kusema kwao:Na wakasema: Msiwaache miungu yenu;
yaani msiache kuabudu masanamu kwa ibada ya Mungu mmoja.
Walikuwa na masanamu mengi; yaliyokuwa muhimu na shani kwao ni matano, ndio maana wakayahusisha kuyataja na wakasema:msimwache Wadda wala Suwaa wala Yaghutha, wala Yau’qa, wala Nasra.
Nuh alikuwa akitilia mkazo sana kukataza ibada ya haya masanamu matano, kwa sababu ndiyo yaliyokuwa makubwa.
Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa haya matano yaliabudiwa wakati wa jahilia hadi wakati wa Mtume Mtukufu(s.a.w.w)
, na Wadda alikuwa wa kabila la Kalb, Suwaa ni wa Hudhayl, Yaghutha ni wa Ghatwif, Yau’qa ni wa Hamadan na Nasra ni wa Himyar. Pia kuna masanamu mengine ya watu wengine; kama vile Lata, Uzza, Hubal na Manat.
Na hao walikwishawapoteza wengi, wala usiwazidishie waliodhulumu ila kupotea.
Viongozi waliopituka mipaka wamewapoteza. Makusudio ya kupotea ni kuangamia; mfano kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٤٧﴾
“Hakika wakosefu wamo katika upotofu na mioto.” Juz. 27 (54:47).
Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
Aya hii ni maneno yaliyooingilia kati maneno ya Nuh na dua yake, lakini yameyakamilisha. Maana yake ni kuwa watu wa Nuh waling’ang’ania ukafiri na upotevu, ndio Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa tufani, na adhabu ya Akhera ni kali na yenye kubaki, wala hakuna yoyote atakayeokoka nayo.
Na Nuh akasema: Mola wangu! Usimwache juu ya ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri!
Yaani usimbakishe yeyote. Nuh hakuomba dua hii ila baada ya kupata wahyi usemao:
وَأُوحِيَ إِلَىٰ نُوحٍ أَنَّهُ لَن يُؤْمِنَ مِن قَوْمِكَ إِلَّا مَن قَدْ آمَنَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٣٦﴾
“Akaletewa wahyi Nuh kuwa hataamini katika watu wako isipokuwa yule aliyoekwishaamini.
Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda.” Juz. 12 (11:36).
Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao hawatazaa ila waovu makafiri.
Hii inafahamisha kwamba ukafiri na uovu umepituka mipaka kwenye jamii ya watu wa Nuh, kiasi ambacho kila anayeinukia anakuwa ni kafiri muovu. Inajulikana kwamba nafsi ya mtoto ni kama kioo, inaakisi kila linalomzunguka.
Kuna riwaya inayosema kuwa mtu alikuwa anamchukua mtoto wake hadi kwa Nuh na kumwambia jihadhari na huyu - yaani Nuh - kwa sababu ni muongo, na baba yangu aliniusia kama ninavyokuusia wewe. Basi mkubwa anakufa akiwa na hilo na mtoto naye anainukia nalo.
Mola wangu! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na kila aliyoeingia nyumbani mwangu kuwa ni mumin, na waumini wanaume, na waumini wanawake.
Baada ya kuwaduilia makafiri, alimuomba Mwenyezi Mungu maghufira yeye na wazazi wake wawili, na kila aliyeamani katika watu wake na watoto wake aliowakusudia katika kauli yake: ‘aliyeingia nyumbani mwangu.’ Vile vile alimuombea kila mumin mwanamume na mwanamke kuanzia Adam hadi siku ya ufufuo Na wala usiwazidishie waliodhulumu ila kuangamia, kwa yule aliyekataa maangamizi na Moto.
Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu imeelezwa: “Athari zilizofukuliwa zimedhihirisha kuwa tukio la gharika lilikuwa tukio halisi, na kwamba kisa hiki kilianza kuandikwa baina ya miaka 1590 ‧ 1595 BC (kabla ya kuzalia Nabii Isa). Tazama Juz. 12 (11:45-49) kifungu cha “Tufani imethibiti kwa umma nyinginezo.”
Hapa kuna swali linajitokeza: Je, tufani iliyofahamishwa na athari zilizofukuliwa na ikaelezwa kwenye vitabu vya kale ni ya Nuh au ni nyingine?
Jibu
: vyovyote iwavyo, ni kuwa Tufani ya Nuh haiwezi kuzuia tufani nyingine kutokea. Kila wakati kunatokea tufani moja au zaidi katika sehemu yoyote katika ardhi. Inawezekena kuwa Tufani ya Nuh ilienea, au ilihusu sehemu fulani katika ardhi. Hakuna nukuu wazi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu inayofahamisha kuwa ilikuwa hiyo tu.
MWISHO WA SURA YA SABINI NA MMOJA: SURAT NUH