23
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sabini Na Nne: Surat Al- Muddathir. Imeshuka Makka Ina Aya 56.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ ﴿١﴾
1. Ewe uliyejigubika!
قُمْ فَأَنذِرْ ﴿٢﴾
2. Simama uonye!
وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ ﴿٣﴾
3. Na Mola wako mfanyie takbira!
وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ ﴿٤﴾
4. Na nguo zako zitwaharishe.
وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ ﴿٥﴾
5. Na mabaya yaambae!
وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ ﴿٦﴾
6. Wala usitoe kwa kutaka kingi.
وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ ﴿٧﴾
7. Na kwa ajili ya Mola wako, fanya subira!
فَإِذَا نُقِرَ فِي النَّاقُورِ ﴿٨﴾
8. Basi litapopulizwa barugumu.
فَذَٰلِكَ يَوْمَئِذٍ يَوْمٌ عَسِيرٌ ﴿٩﴾
9. Siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu.
عَلَى الْكَافِرِينَ غَيْرُ يَسِيرٍ ﴿١٠﴾
10. Kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
EWE ULIYEJIGUBIKA
Aya 1 - 10
MAANA
Aya hizi zinaashiria wadhifa wa Muhammad(s.a.w.w)
kama mjumbe wa haki kwa viumbe. Pia kuna ishara kuwa watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu wako sawa; ufafanuzi ni kama ufufatavyo:
Ewe uliyejigubika!
Huyo ni Mtume mtukufu(s.a.w.w)
. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwita kwa sifa hii kwa sababu wakati huo alikuwa katika hali hiyo kutokana na sababu fulani; kama tulivyosema mwanzo wa Sura iliyopita.
Simama uonye!
Neno linaweza kuwa na maana moja ya kilugha, lakini maana hayo, mara nyingi, yanatofautiana kulingana na msemaji na anayeambiwa. Mfano neno ‘onya,’ maana yake katika kamusi za lugha lina maana ya kuhofisha na kuhadharisha.
Kwa mfano ukimuona mtu anachimba shimo njiani na kumwambia toa onyo, utakuwa unamaanisha atangaze na kuwaonya wapita njia wasiingie shimoni. Ukimwambia mwana fakihi katika kijiji: ‘onya.’ Utakuwa unamaanisha awafundishe watu wa hapo hukumu za dini na kuwahofisha kuzihalifu.
Ama kauli ya Mtukufu kwa Nabii wake; ‘simama uonye,’ Maana yake ni pambana na waasi wenye nguvu na kiburi kwa neno la haki na uwambie: nyinyi ni wapotevu wafisadi na mtajua kesho hizaya na udhalili utakaowapata, kama hamtarudi kuuacha upotevu wenu. Ukiwambia hivi uvumilie yatakayokupata kutoka kwao na umsabihi Mola wako na kumshukuru.
Tukiona jinsi Muhammad(s.a.w.w)
alivyopambana na makuraishi wakiwa na nguvu na kauli na yeye hana chochote zaidi ya ikhlasi na imani, hapo ndio tunabainikiwa na yaliyomsibu kutoka kwao: walimpa sifa ya uchawi, uwongo, ushairi na hata wendawazimu. Walimshakizia watoto wamfanyie masikhara na kumtupia mawe; wakawaambia wanawake waweke miba kwenye njia atakayopita na wasafihi wamwekee uchafu na najisi njiani; hata kuna mmoja wao aliyewahi kumvua kilemba Mtume na kukifunga shingoni mwake. Fauka ya yote hayo makuraishi waliweka azimio la kumwekea vikwazo Mtume na watu wake na kumzuia asiwe na mahusiano na jamii.
Pamoja na yote hayo Nabii(s.a.w.w)
alivumilia na kuendelea na mwito wake bila ya kujali hali ngumu waliyompa makuraishi, wakaunda vikosi na majeshi. Akavumilia, akawa imara na subira na kuitikia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ewe uliyejigubika! Simama uonye.”
Haya yanatuwekea wazi kuwa wadhifa wa Mtume ni kuonya pamoja na uvumilivu wa tabu na mashaka. Hili ndilo jambo la kwanza. Ama la pili, ni usawa baina ya watu, linalofahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na Mola wako mfanyie takbira!
Ukimwambia mtu wa kawaida: Mfanyie takbira Mwenyezi Mungu, tutafahamu kuwa unataka asema Allahf akbar; kama vile ukisema: mswalie Mtume.
Lakini kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Nabii wake: ‘Na Mola wako mfanyie takbira, ina maana kubwa na nzito zaidi, ambayo ni: Ewe Muhammad(s.a.w.w)
waambie usoni mwao wale wanojifanya majabari wenye kiburi kuwa enzi ni ya Mwenyezi Mungu na Yeye pekee ndiye mkubwa aliye juu, na kwamba nguvu, utukufu na utawala ni wa mmoja aliye pekee asiyekuwa na mshirika kutoka kwenye miungu wenu au nyinyi wenyewe au kutoka kwa wengine; na kwamba watu wote wako sawa katika kumwabudu Mwenyezi Mungu; hakuna tofauti baina ya mweusi na mweupe wala baina ya tajiri na fukara.
Muhammad aliitikia mwito wa Mola na kuwaambia mataghuti mengi tu; miongoni mwayo ni: “Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.” Juz. 17 (21:98).
Na nguo zako zitwaharishe.
Vile vile hii inafungamana na kulingania na kuonya. Hakuna anayetia shaka kuwa usafi wa mwili na nguo ni katika imani, lakini makusudio hapa ni zaidi ya hivyo; kwamba Mtume(s.a.w.w)
atoe mwito wa usafi wa nje, kama vile uchafu, na usafi wa ndani, kama vile udanganyifu na hiyana, ria na unafiki, ujinga na kuhadaika na madhambi mengineyo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hayo ameyatolea ibara ya usafi wa nguo, kwa kutumia desturi ya waarabu; wanaposema: Fulani ni msafi wa mapindo ya nguo yake, wakimaanisha kuwa ni msafi wa moyo na dhati.
Na mabaya yaambae!
Hii inakuwa ni tafsiri na ufafanuzi wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na nguo zako zitwaharishe,’ kama ilivyosemekana. Pia imesemekana makusudio ni ushirikina na kuabudu masanamu.
Wala usitoe kwa kutaka kingi.
Makusudio ya kutaka kingi hapa ni kujiona umefanya mengi. Maana ni kuwa Ewe Muhammad! umewafanyia watu mema mengi na fadhila nyingi, lakini usimsimbulie yeyote kwa hilo ukajiona kuwa umefanya mengi, ukasema mimi nimefanya hili ni kawafadhili lile. Kwani kila ulilojitolea ni fadhila yako kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna fadhila gani na tukufu zaidi kuliko kuafikiwa kufanya kheri?
Mara nyingi huko nyuma tumeeleza kuwa makatazo yanafaa hata ikiwa anayeambiwa hana azma ya kufanya hilo linalokatazwa, mbali ya kuwa amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake yanawahusu waja wake wote, hata wale wenye takua.
Imesemwa katika Nahjul-balagha: “Kutekeleza haja hakuwezi kuendelea ila kwa mambo matatu: Kwa kuifanya ndogo itakuwa kubwa, kwa kuificha itajitokeza na kwa kuiharakisha itasifika.”
Na kwa ajili ya Mola wako, fanya subira!
Mwenyezi Mungu hakumwamrisha Nabii wake mtukufu jambo lolote la taklifa ya kufikisha na utume ila analikutanisha na subira, kama ilivyosemekana, kwa sababu ya kujua kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu maudhi atakayopambana nayo kutoka kwa wenye inadi.
Basi litapopulizwa barugumu; siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu; kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
Ni kama mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ ﴿١٠١﴾
“Basi itakapopuziwa parapanda, Juz. 18 (23:101).
Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamuru Mtume wake kuwa na uvumilivu kutokana na adha ya wakadhibishaji, sasa anawahadharisha na Siku ya Kiyama ambayo itakuwa ngumu na kali sana kwao; itakuwa nzito isiyofuatiwa na wepesi. Yametangulia makumi ya Aya kuhusiana na aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu kwa wakosefu; yakiwemo chakula, kinywaji na adhabu kali.
ذَرْنِي وَمَنْ خَلَقْتُ وَحِيدًا ﴿١١﴾
11. Niache peke yangu na niliye muumba.
وَجَعَلْتُ لَهُ مَالًا مَّمْدُودًا ﴿١٢﴾
12. Na nikamjaalia kuwa na mali mengi.
وَبَنِينَ شُهُودًا ﴿١٣﴾
13. Na wana wanaoonekana.
وَمَهَّدتُّ لَهُ تَمْهِيدًا ﴿١٤﴾
14. Na nikamtengenezea mipango.
ثُمَّ يَطْمَعُ أَنْ أَزِيدَ ﴿١٥﴾
15. Kisha anatumai nimzidishie!
كَلَّا إِنَّهُ كَانَ لِآيَاتِنَا عَنِيدًا ﴿١٦﴾
16. Sivyo! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu!
سَأُرْهِقُهُ صَعُودًا ﴿١٧﴾
17. Nitamtesa kwa mateso ya hali ya juu.
إِنَّهُ فَكَّرَ وَقَدَّرَ ﴿١٨﴾
18. Hakika yeye alifikiri na akapima.
فَقُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ﴿١٩﴾
19. Basi amelaaniiwa! Vipi alivyopima!
ثُمَّ قُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ﴿٢٠﴾
20. Tena amelaaniiwa! Vipi alivyo pima!
ثُمَّ نَظَرَ ﴿٢١﴾
21. Kisha akatazama.
ثُمَّ عَبَسَ وَبَسَرَ ﴿٢٢﴾
22. Kisha akakunja uso na akanuna.
ثُمَّ أَدْبَرَ وَاسْتَكْبَرَ ﴿٢٣﴾
23. Kisha akageuka, na akatakabari.
فَقَالَ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ يُؤْثَرُ ﴿٢٤﴾
24. Akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa.
إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ ﴿٢٥﴾
25. Haya si chochote ila ni kauli ya binadamu.
سَأُصْلِيهِ سَقَرَ ﴿٢٦﴾
26. Nitamtia kwenye Saqar.
وَمَا أَدْرَاكَ مَا سَقَرُ ﴿٢٧﴾
27. Na nini kitakujulisha ni nini Saqar?
لَا تُبْقِي وَلَا تَذَرُ ﴿٢٨﴾
28. Haubakishi wala hauachi.
لَوَّاحَةٌ لِّلْبَشَرِ ﴿٢٩﴾
29. Unababua ngozi.
عَلَيْهَا تِسْعَةَ عَشَرَ ﴿٣٠﴾
30. Juu yake wapo kumi na tisa.
وَمَا جَعَلْنَا أَصْحَابَ النَّارِ إِلَّا مَلَائِكَةً وَمَا جَعَلْنَا عِدَّتَهُمْ إِلَّا فِتْنَةً لِّلَّذِينَ كَفَرُوا لِيَسْتَيْقِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا وَلَا يَرْتَابَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَالْمُؤْمِنُونَ وَلِيَقُولَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْكَافِرُونَ مَاذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِهَـٰذَا مَثَلًا كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ وَمَا هِيَ إِلَّا ذِكْرَىٰ لِلْبَشَرِ ﴿٣١﴾
31. Na hatukuwafanya walinzi wa Moto ila Malaika, Wala hatukufanya idadi yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru. Ili wawe na yakini waliopewa Kitabu na wazidi imani wale walioamini, wala wasiwe na shaka wale waliopewa Kitabu na waumini, na wapate kusema walio na maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu? Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoza amtakaye. Na hapana ajuae majeshi ya Mola wako ila Yeye. Na huo si chochote ila ni ukumbusho kwa watu.
NIACHE PEKE YANGU NA NILIYEMUUMBA
Aya 11 - 31
KISA KWA UFUPI
Walid bin Al-Mughira Al-Makhzumi, alikuwa ni miongoni mwa vigogo wa kikuraishi, akiwa na mali nyingi na watoto. Siku moja akamsikia Mtume akisoma Aya mojawapo ya Qur’an, akasema: “Hii sio maneno ya binadamu wala jinni. Wallah, hakika kauli yake ‧ yaani Qur’an ‧ ina utamu na ina mvuto na kwamba juu yake kuna matunda na chini yake kumejaa. Hakika iko juu na haishindwi.”
Basi makuraishi waliposikia hivi wakahofia maneno ya Walid kama yakienea kwa watu, watamwamini Muhammad(s.a.w.w)
. Wakamtaka Walid ampinge Mtume. Akasema nisemeje sasa? Niseme ni mwendawazimu, nani ataamini? Au niseme ni kuhani, naye hakuwahi kuwa kuhani kabisa.
Nikisema ni mshairi, yeye hajawahi kutamka shairi na nikisema ni mwongo, hakuna yeyote aliyewahi kusikia uwongo kwake. Kisha akafiria akaona ampe sifa ya uchawi na kwamba yeye ameichukua Qur’an kutoka kwa wachawi.
MAANA
Niache peke yangu na niliyemuumba.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. Makusudio yake ni kumkemea na kumhadharisha Walid bin Mughira kwa maafikiano ya wafasiri. Maana ni kuwa niachie mimi huyo ewe Muhammad, usijishughulishe naye, wala na yale anayokuzulia. Mimi peke yangu ndiye nitakayempiga vita na kumpa adhabu.
Mwenyezi Mungu alifikia ghadhabu hii kwa Walid, kwa sababu yeye alipituka mipaka na uovu; akakufuru neema ya Mwenyezi Mungu na akaipinga haki na kuifanyia kiburi haki na watu wake. Kila mwenye kuipinga haki basi ni mlengwa wa ghadhabu hii na makemeo haya; kama vile Walid Bin Mughira, kwa vile sababu ya kushuka Aya haihusiki na aliyeteremshiwa tu, bali inaenea, kama tulivyosema mara nyingi.
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Na nikamjaalia kuwa na mali mengi,
inaashiria kuwa linasobabisha na kuleta msukumo wa kufanya uovu ni utajiri na wingi wa mali. Aya kadhaa zianaashria hakika hii, ikiwemo Aya 11 ya sura iliyopita na pia kauli yake Mwenyezi Mungu akimsimulia muasi aliyojifaharisha kwa mtu mwema:
أَنَا أَكْثَرُ مِنكَ مَالًا ﴿٣٤﴾
“Mimi nimekushinda kwa mali” Juz. 15 (18:34).
Inatosha kuwa ni ushahidi wa hayo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾
“Hakika mtu hupituka mipaka, kwa kujiona amejitosheleza.” (96:6-7).
Kwa kutegemea Aya hizi na nyingine zilizo mfano wake, inawezekana kusema, ijapokuwa ni kwa kubuni, kwamba asili ni kuwa kila tajiri ni muasi, mpaka ithibitike kinyume. Imelezwa kwenye Nahjul-balagha: “Ni uzuri ulioje wa matajiri kuwanyenyekea mafukara kwa kutaka yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu! Na uzuri zaidi kuliko huo ni maringo ya mafukara kwa matajiri kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu.”
Kuna Hadith isemayo: “Heri zote ni za aliyesilimu na ikawa maisha yake ni kutosheka.. ewe Mwenyezi Mungu mruzuku Muhammad na kizazi cha Muhammad kujichunga na kutosheka.”
Na wana wanaoonekana
, wakiwa pamoja naye wakishindana kumhudumia.Na nikamtengenezea mipango
. Nimemsahilishia njia ya jaha na mali akiogelea kwenye neema atakavyo.
Kwa mnasaba huu tunaashiria kwamba neema za dunia hazifahamishi kuridhiwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: “Hakika maisha ya dunia ni mchezo na upuzi tu.” Juz. 26 (47:36). Kwenye Hadith amesema: “ Lau dunia mbele ya Mwenyezi Mungu italinganishwa na kheri kwa ubawa wa mbu, basi kafiri asingekunywa hata tama moja la maji.”
Ilijitokeza dunia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, mbora wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, akaikataa, lakini Walid, muovu wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, ilikithiri mali yake,kisha anatumai nimzidishie
! Yaani ana tamaa ya kuzidishiwa mali yake ili azidi uovu na uadui.
Haiwezekani kuchanganyika wema na tamaa katika moyo mmoja. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
anasema: “Tamaa ni ufunguo wa kila maasi na ni msingi wa kila hatia na ni sababu ya kuanguka mambo mema.”
Sivyo! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu!
Tokomea mbali ewe mpinzani mwenye hiyana! Hivi una tamaa kwa Mungu na wewe unaifanyia inadi haki na kuizuia kwa kutangaza vita kwa watu wa haki? Wapokezi wanasema kuwa iliposhuka tu Aya hii Walid alibadilika kutoka kwenye enzi na kuwa dhalili, utajiri kuwa fukara, na akafa na hali mbaya.
Amesema kweli aliyoesema: “Hawakusema watu kwa jambo lolote kuwa lina heri ila kuna shari iliyofichwa na nyakati.” Hii ni duniani, ama malipo yake huko Akhera yanaelezwa na Aya hii:
Nitamtesa kwa mateso ya hali ya juu.
Hali ya juu inaweza kuwa ni ukali na mashaka na inaweza kuwa ni zaidi. Mfumo wa maneno unajulisha maana zote mbili na kwamba adhabu siku hiyo itazidi kiwango na kiaina, muda baada ya muda.
Hakika yeye alifikiri na akapima.
alifikiria kuhusu Qur’an na akaandaa kauli ya uzushi kwamba Qur’an ni uchawi ulionukuliwa, kama itakavyokuja mbele.
Basi amelaaniwa! Vipi alivyopima! Tena amelaaniwa! Vipi alivyopima!
Amelaaaniwa kisha akalaaniwa katika kufikiria kwake na kupanga kwake kauli, vitendo na makusudio yake yote. Hakuna kitu kinachofahamisha ufasaha zaidi kuliko kukaririka laana kwa waovu.
Kisha akatazama
. Baadaa ya kufikiria aliinua jicho lake kwa vigogo wa kikuraishi,kisha akakunja uso
, kwa kukunja nyusi zakena akanuna
; uso ukamuiva.
Kisha akageuka, na akatakabari.
Alihakikisha alipofikiria kuwa Qur’an ni haki isiyokuwa na shaka, lakini pamoja na hayo aliipinga na akaitukukiaakasema: “Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa. Haya si chochote ila kauli ya binaadamu
,” aliyoichukua Muhammad kutoka kwa makuhani wa kichawi.
Picha hii ya Walid iliyopigwa na Qur’an, ya kufikiri, kupima, kukunja uso na kununa, inatujulisha kuwa yeye alikuwa hana la kufanya katika kupanga uwongo kwenye jambo analoliamini kuwa ni haki na kweli.
Nitamtia kwenye
Moto waSaqar
. Atakayetiwa ni huyo huyo Walid. Saqar ni miongoni mwa majina ya Jahannam.Na nini kitakujuulisha ni nini
huo Moto waSaqar
? Kwani umefika kikomo cha kutisha; miongoni mwayo ni kwamba huohaubakishi
yeyote katika wakosefuwala hauachi
aina yoyote ya adhabu ila inawashushia naunababua ngozi
.
Makusudio ya kubabua hapa ni kuiva, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا ﴿٥٦﴾
“Kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilisha ngozi nyingine.” Juz. 5 (4:56).
Juu yake wapo kumi na tisa.
Yaani juu ya hiyo Saqar. Kumi na tisa ni walinzi wa Jahannam. Je, kumi na tisa ni idadi, au aina au ni viongozi? Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.
Kuna riwaya isemayo kuwa Abu Jahl, aliwaambia makuraishi: ‘’Hamna maana ninyi! Hivi watu kumi katika nyinyi wanashindwa kumshika mmoja katika hao 19?”
Mmoja alieyitwa Abul-Mushid alisema: “Mimi peke yangu nitawatoshea na 17, nyinyi shikeni wawili tu.” Huyu alisema kwa madharau kama alivyosema Abu Jahl.
Na hatukuwafanya walinzi wa Moto ila Malaika.
Walinzi wa moto si katika aina ya binadamu; bali ni malaika wakali wenye nguvu; hakuna anayewazidi nguvu isipokuwa aliye pekee, Mwenye nguvu ambaye ameumba kila kitu.
Kama kwamba muulizaji ameuliza: Nini makusudio ya kutajwa idadi, jambo ambalo linafungua mlango wa madharau kwa wapinzani? Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba kutaja kwake kuna faida tatu:
1.Wala hatukufanya idadi yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru.
Ndio! Mwenyezi Mungu anajua kwamba washirikina watakaposikia idadi watacheka na kufanya stihizai, lakini pamoja na hayo ametaja, kwa sababu haki inapaswa itangazwe, hata kama natija yake ni madharau ya wanaodharau. Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawajaribu waja, naye ni mjuzi zaidi kuliko nafsi zao. Anawajaribu kwa raha na dhiki. Vile vile anasema haki ili vijitokeze vitendo vyao vinavyostahiki thawabu na adhabu.
Kutajwa idadi kumedhihirisha hakika ya washirikina ya kudharau ghaibu, hivyo wakastahiki ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu; kama kulivyodhihirisha hakika ya waumini wakastahiki radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake, kama yatakavyokuja maelezo. Zaidi ya hayo ni kuwa kutangaza Mtume neno la haki bila ya kuangalia yatakayompata kwa ajili yake, ni dalili mkataa kwamba hana jingine analolitaka isipokuwa kuihakikisha haki na kuibatilisha batili.
2.Ili wawe na yakini waliopewa Kitabu.
Ulama wa kiyahudi na wa kinaswara wakati huo walishuhudia kwa imani na yakini kwamba walinzi idadi yao ni 19, kwa sababu hilo linaafikiana na waliyoyasoma katika Tawrat na Injil.
3.Na wazidi imani wale walioamini.
Wahyi wa mambo ya ghaibu unawazidisha makafiri upinzani na jeuri na waumini wanazidi imani. Imesemekana kuwa waumini huzidi yakini wakiambiwa na watu wa Kitabu kuwa idadi imo kwenye vitabu vyao. Usawa ni kuwa kila Aya katika Aya zake Mwenyezi Mungu Mtukufu inawazidisha waumini yakini kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake; ni sawa watu wa Kitabu wakubali au wapinge. Ni kweli kwamba kukubali kwao ni hoja kwa wapinzani.
Wala wasiwe na shaka wale waliopewa Kitabu na waumini.
Huu ni ufafanuzi na msisitizo wa yaliyokuwa kabla yake, kwa sababu kutokuweko shaka ni kuwa na yakini na kuzidi imani.
Na wapate kusema walio na maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu?
Vile vile huu ni ufafanuzi na msisitizo wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Wala hatukufanya idadi yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru,” pamoja na kufafanua aina ya makafiri ambao ni wanafiki walio na maradhi katika nyoyo zao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:26).
Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoza amtakaye.
Mwenye kufuata njia ya upotevu Mwenyezi Mungu humpoteza:
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ ﴿٥﴾
“Walipopotoka, Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo zao.” Juz. 28 (61:5).
فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ﴿١٠﴾
“Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi.” Juz. 1 (2:10).
Na mwenye kufuata njia ya uongofu Mwenyezi Mungu humuongoza: “Na ambao wameongoka anawazidishia uongofu.” Juz. 26: (47:17).
Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (35:8).
Na hapana ajuae majeshi ya Mola wako ila Yeye.
Askari wa Mwenyezi Mungu sio wale 19 tu, viumbe wote wanatii matakwa hata wanyama, wadudu, ndege, upepo, matetemeko, matufani na mengineyo ambayo hakuna anayejua isipokuwa mwanzishaji wa viumbe na mrudishaji.
Na huo si chochote ila ni ukumbusho kwa watu.
Huo ni huo moto wa Saqar. aliyoumba Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kuwahadharisha nao ili wayaogope maasi kwa ndani na nje.