TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 27990
Pakua: 4503


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 27990 / Pakua: 4503
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

25

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sabini Na Tano: Al-Qiyama. Imeshuka Makka. Ina aya 40.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

لَا أُقْسِمُ بِيَوْمِ الْقِيَامَةِ ﴿١﴾

1. Ninaapa kwa Siku ya Kiyama!

وَلَا أُقْسِمُ بِالنَّفْسِ اللَّوَّامَةِ ﴿٢﴾

2. Na ninaapa kwa nafsi inayoji­laumu!

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَلَّن نَّجْمَعَ عِظَامَهُ ﴿٣﴾

3. Hivi anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake?

بَلَىٰ قَادِرِينَ عَلَىٰ أَن نُّسَوِّيَ بَنَانَهُ ﴿٤﴾

4. Kwanini! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake!

بَلْ يُرِيدُ الْإِنسَانُ لِيَفْجُرَ أَمَامَهُ ﴿٥﴾

5. Lakini mtu anataka afanye maovu mbele yake.

يَسْأَلُ أَيَّانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ ﴿٦﴾

6. Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?

فَإِذَا بَرِقَ الْبَصَرُ ﴿٧﴾

7. Basi jicho litakapofanya kiwi.

وَخَسَفَ الْقَمَرُ ﴿٨﴾

8. Na mwezi utapopatwa.

وَجُمِعَ الشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ﴿٩﴾

9. Na likakusanywa jua na mwezi.

يَقُولُ الْإِنسَانُ يَوْمَئِذٍ أَيْنَ الْمَفَرُّ ﴿١٠﴾

10. Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio?

كَلَّا لَا وَزَرَ ﴿١١﴾

11. Sivyo! Hapana pa kukimbilia!

إِلَىٰ رَبِّكَ يَوْمَئِذٍ الْمُسْتَقَرُّ ﴿١٢﴾

12. Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako.

يُنَبَّأُ الْإِنسَانُ يَوْمَئِذٍ بِمَا قَدَّمَ وَأَخَّرَ ﴿١٣﴾

13. Siku hiyo ataambiwa mtu aliy­oyatanguliza na aliyoy­aakhirisha.

بَلِ الْإِنسَانُ عَلَىٰ نَفْسِهِ بَصِيرَةٌ ﴿١٤﴾

14. Bali mtu anajiona mwenyewe.

وَلَوْ أَلْقَىٰ مَعَاذِيرَهُ ﴿١٥﴾

15. Ingawa atatoa nyudhuru zake.

لَا تُحَرِّكْ بِهِ لِسَانَكَ لِتَعْجَلَ بِهِ ﴿١٦﴾

16. Usiitikisie ulimi wako kwa kuifanyia haraka.

إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ ﴿١٧﴾

17. Hakika ni juu yetu kuiku­sanya na kuisoma.

فَإِذَا قَرَأْنَاهُ فَاتَّبِعْ قُرْآنَهُ ﴿١٨﴾

18. Hivyo tunapoisoma, basi fuatiliza kusoma kwake.

ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ ﴿١٩﴾

19. Kisha ni juu yetu kuibainisha.

KIAPO KWA SIKU YA KIYAMA

Aya 1 - 19

MAANA

Ninaapa kwa Siku ya Kiyama!

Yaani ninaapa kwa hiyo siku. Tafsiri hii ni ikiwa herufi la` ni ziada kiirabu ya nahw, kama walivyosema wafasiri wengi. Lakini ikiwa ni ya kukanusha kama walivyoona wengine, basi tafsiri yake itakuwa: Siapi kwa siku ya Kiyama; yaani hakuna haja kamwe ya kufanya hivyo, kwa sababu inaeleweka wazi. Kwa tafsiri zote mbili kuna maneno ya kukadiriwa ambayo ni hakika nyinyi mtafufuliwa kwa umbo jipya.

Na ninaapa kwa nafsi inayojilaumu!

Wafasiri wana kauli nyingi kuhusiana na maana ya nafsi inayojilaumu. Tuonavyo sisi ni kuwa mara nyingi sana mtu hujilaumu kutokana na matendo aliyoyafanya au kuyaacha yeye mwenyewe, baada ya kum­bainikia kuwa kufanya au kuacha kunamletea madhara ya kiafya, kama vile kula chakula alichokatazwa; au hasara aliyoipata kutokana na bei aliy­oifanya na mengineyo katika madhara ambayo hayana uhusiano na dini au muumba wake kwa namna yoyote ile. Haya sio maana yaliyokusudiwa hapa katika nafsi inayojilaumu.

Mara nyingine mtu anaweza kuhisi majuto na masikitiko kutokana na kuk­iuka miko ya haki na kupuuza kufanya heri; ni sawa awe amefanya hivyo kwa makusudi na kujua au amefanya bila ya kujua na kutokusudia; kisha ikambainikia hakika, kama itakavyokuwa hali ya kafiri Siku ya Kiyama. Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa kuhusu nafsi yenye kujilaumu.

Hivi anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake? Kwanini! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake!

Wanaokanusha ufufuo wanasema ni muhali kupata uhai mifupa iliyokuwa mchanga. Wameyasema hayo kwa mifumo mbali mbali, na Mwenyezi Mungu naye akawajibu kwa aina mbali mbali ya mifumo; miongoni mwayo ni Aya hii tunayoifasiri.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye atakayeikusanya na kuipa uhai, wala hakuna ajabu katika uweza wake Mtukufu asiyeshindwa na chochote. Fauka ya hayo Yeye atairudisha mifupa kwa ukamilifu, kama ilivyokuwa, hata ile midogo na myembamba; kama vile mifupa ya vidole vya mkono, itarudi kama ilivyokuwa, pamoja na ngozi yake, rangi yake na nywele; bali hata alama za vidole zilizokuwako.

Hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi. Kwa sababu yule aliyepangilia mwanzo na kuzifanya alama za vidole zitofautiane kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kuanzia binadamu wa kwanza hadi wa mwisho, ni wepesi zaidi kwake kuzirudisha kama zilivyokuwa kwa sifa zake zote. Kwa sababu kutofautiana alama za vidole kwa mfano huu ni dalili ya nguvu zaidi juu ya uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu kuliko kuirudisha mifupa na wafu.

Lakini mtu anataka afanye maovu mbele yake.

Maovu ni madhambi, mbele yake ni kuendelea. Kwa hiyo basi makusudio ya mtu hapa yatakuwa ni muovu mwenye dhambi. Ujumla wa maana ni kuwa mwenye dhambi huyu anataka kuendelea na dhambi zake mpaka siku yake ya mwisho. Ndio maanaanauliza kwa madharau:Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama ni mbali au karibu?

Basi jicho litakapofanya kiwi, Na mwezi utapopatwa, na likakusany­wa jua na mwezi.

Mwenye inadi aliuliza ni lini Kiyama? Ndio Mwenyezi Mungu akazitaja sifa zake, jicho litaduwaa mwanga wa mwezi utaondoka na kugongana na mwezi kutokana na kuharibika nidhamu ya ulimwengu.

Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio kulikimbia janga hili? Sivyo! Hapana pa kukimbilia! Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako. Yeye peke yake ndiye marejeo ya waja siku hiyo na viumbe wote watanyenyekea kwenye hukumu yake.

Siku hiyo ataambiwa aliyoyatanguliza na aliyoyaakhirisha.

Makusudio ya aliyoyatanguliza ni aliyoyafanya katika heri na shari, na aliyoyaahirisha ni aliyoyaacha katika wajibu uliofaradhishwa kwake, maana ni kuwa mtu atakaposimama mbele ya Mola wake kesho kwa his­abu, yatamfunukia matendo yake yote ya heri na shari kuanzia mwanzo hadi mwisho wake. vile vile yata mfunukia majukumu aliyoyaacha.

Bali mtu anajiona mwenyewe, ingawa atatoa nyudhuru zake.

Kila mtu anajijua, anayajua aliyoyafanya na aliyoyaacha wala haihitajii kuambiwa. Yeye anajua tu hata kama atajaribu kutoa vijisababu.

Usiitikisie ulimi wako kwa kuifanyia haraka. Hakika ni juu yetu kuikusanya na kuisoma. Hivyo tunapoisoma, basi fuatiliza kusoma kwake. Kisha ni juu yetu kuibainisha.

Maneno yanaaza upya, kama ilivyo kawaida ya Qur’an kutoka kwenye maudhui moja hadi nyingine; iwe kuna jambo la kunasibiana au hakuna. Imam Ja’far As-Sadiq(a.s ) anasema: “Aya moja inaweza kuwa na jambo mwanzo wake na mwisho wake ni jambo jingine.”

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) . Ni juu yetu kuikusanya yaani kuikusanya kwenye moyo wako. Tunapoisoma, yaani tunapoimaliza kuisoma.

Ujumla wa maana ni kuwa Jibril anapokusomea Qur’an, ewe Muhammad, usiwe na haraka ya kusoma kwa kuhofia kukupita kitu, sisi tutaifanya kamili katika moyo wako, mpaka akimaliza Jibril nawe anza kusoma. Ni juu yetu kukulinda usisahau wala kukosea kuisoma, au kubainisha hukumu yake na pia kuitumia.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:114).

كَلَّا بَلْ تُحِبُّونَ الْعَاجِلَةَ ﴿٢٠﴾

20. Sivyo! Bali nyinyi mnapenda ya sasa.

وَتَذَرُونَ الْآخِرَةَ ﴿٢١﴾

21. Na mnaacha Akhera.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ ﴿٢٢﴾

22. Nyuso siku hiyo zitang’ara.

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ ﴿٢٣﴾

23. Zinamtazama Mola wake.

وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ بَاسِرَةٌ ﴿٢٤﴾

24. Na nyuso nyingine siku hiyo zitakunjamana.

تَظُنُّ أَن يُفْعَلَ بِهَا فَاقِرَةٌ ﴿٢٥﴾

25. Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo.

كَلَّا إِذَا بَلَغَتِ التَّرَاقِيَ ﴿٢٦﴾

26. Sivyo! Itakapofikia kwenye mitulinga.

وَقِيلَ مَنْ رَاقٍ ﴿٢٧﴾

27. Na pakasemwa: Nani wa kum­ganga?

وَظَنَّ أَنَّهُ الْفِرَاقُ ﴿٢٨﴾

28. Na akajua kuwa huko ndiko kufariki.

وَالْتَفَّتِ السَّاقُ بِالسَّاقِ ﴿٢٩﴾

29. Na utapoambatishwa muundi kwa muundi.

إِلَىٰ رَبِّكَ يَوْمَئِذٍ الْمَسَاقُ ﴿٣٠﴾

30. Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako!

فَلَا صَدَّقَ وَلَا صَلَّىٰ ﴿٣١﴾

31. Basi hakusadiki, wala hakuswali.

وَلَـٰكِن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿٣٢﴾

32. Bali alikanusha, na akageuka.

ثُمَّ ذَهَبَ إِلَىٰ أَهْلِهِ يَتَمَطَّىٰ ﴿٣٣﴾

33. Kisha akenda kwa watu wake kwa matao.

أَوْلَىٰ لَكَ فَأَوْلَىٰ ﴿٣٤﴾

34. Ole wako, tena ole wako!

ثُمَّ أَوْلَىٰ لَكَ فَأَوْلَىٰ ﴿٣٥﴾

35. Kisha Ole wako, tena ole wako!

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى ﴿٣٦﴾

36. Hivi anadhani mtu kuwa ataachwa bure?

أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِّن مَّنِيٍّ يُمْنَىٰ ﴿٣٧﴾

Je, hakuwa ni tone la manii lililoshushwa?

ثُمَّ كَانَ عَلَقَةً فَخَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٣٨﴾

38. Kisha akawa pande la damu, tena akamuumba na akam­linganisha sawa?

فَجَعَلَ مِنْهُ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ ﴿٣٩﴾

39. Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke?

أَلَيْسَ ذَٰلِكَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ﴿٤٠﴾

40. Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu?

MNAPENDA YA SASA

Aya 20 - 40

MAANA

Sivyo! Bali nyinyi mnapenda ya sasa, na mnaacha Akhera.

Ya sasa ni maisha ya dunia. Maneno yanaelekezwa kwa yule mwenye kuiuza dini yake kwa dunia yake na kuathirika na maisha yanayoisha badala ya yanayobakia, awe mwislamu au sio mwislamu. Aya iko wazi kwa hilo, haikubali taawili.

Nyuso siku hiyo zita ng’ara, zinamtazama Mola wake.

Shia Imamiya na Mu’tazila wamesema haiwezekeani Mungu kuonekana duniani wala Akhera, na wakasema vile vile kuwa kutazama hapa ni kwa akili sio kwa macho au ni kungoja, kwa maana ya kuwa zitangojea na kutazamia neema ya Mwenyezi Mungu na karama yake.

Ashaira wamejuzisha kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho. Hayo tumeyazungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 1 (54-57) kifungu cha ‘Kumuona Mungu.’ Kwamba utafiti wa maudhui haya hauna faida, kiu­jumla wala kimahsusi na huenda ukaongeza mpasuko baina ya Waislam, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumkalifisha nayo yeyote.

Vyovyote iwavyo ni kuwa wenye takua kesho watafufuliwa katika hali ya uso mwangavu wakiwa na furaha kwa fadhila aliyozowapa Mwenyezi Mungu.

Na nyuso nyingine siku hiyo zitakunjamana. Zitajua ya kuwa zitafiki­wa na livunjalo uti wa mgongo.

Wakosefu watakuwa kinyume kabisa na wenye takua; watafufuliwa waki­wa na nyuso zilizokunjana na kusinyaa na nyoyo zao zinazotetemeka kwa hofu ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:106).

Sivyo! Itakapofikia rohokwenye mitulinga, Na pakasemwa: Nani wa kumganga? Na mwenyeweakajua kuwa huko ndiko kufariki.

Aya hizi zinaelezea hali ya kukata roho na kufikiwa na mauti ambayo hataokoka nayo yeyote; awe Nabii, muovu, mdogo au mkubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameanza na neno sivyo, baada ya kutangulia maneno bali nyinyi mnapenda dunia na kuiacha Akhera, kwa hiyo ikanasabiana kuyakemea hayo. Maana ni, ewe mkosefu acha kuathirika na ulimwengu unaoisha badala ya ule wa kubakia, na ukumbuke mauti yanay­ovunja dhati na kukata matamanio, kumbuka pumzi za mwisho wakati roho inapofika kooni, huku watu wako, baada ya kushindwa kukutibu wak­iuliza ni nani tabibu mzuri wa kukutibu, na wewe mwenyewe ukiwa na uhakika kuwa unayafikia mauti yasiyokuwa na tiba wala dawa

Na utapoambatishwa muundi kwa muundi.

Muundi mmoja wa anayekata roho utakuwa juu ya mwingine kutokana na shida ya kukata roho. Imesemekana kuwa ni kinaya cha kuelezea jambo gumu, kwa waarabu, wanasema kuhusina na jambo gumu: ‘limepandiwa na muundi.’

Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako.

Mwenye kufa hana kwengine kwa kwenda isipokuwa kwa Mungu tu. Miongoni mwa maneno ya Imam Ali(a.s ) , akisifia hali ya mwenye kuka­ta roho, anasema:

“Wakati yeye akiicheka dunia na dunia nayo inamcheka kutokana na kujisahau kwake. Mara wakati unamkanyaga kama mwiba, na siku zikaanza kudhoofisha nguvu zake na mauti yakianza kumkodolea macho kwa karibu, na huzuni ambayo hajawahi kuwa nayo ikaanza kumshika, na ugonjwa ukamshika… Muuguzaji akachoka na watu wake wakashindwa kuelezea ugonjwa wake…Hakika mauti yana uchungu usioweza kusifika au kuingia kwenye akili za watu wa dunia.”

Basi hakusadiki, wala hakuswali, bali alikanusha, na akageuka, kisha akenda kwa watu wake kwa matao.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Aya hii ilishuka kwa Abu Jahl, nayo ni picha inayofuata asili ya sifa zake, kwa sababu hakumsadiki Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) wala hakuwahi kuswali hata kwa kupepesa jicho, bali alikadhibisha haki, akaivuruga, akaipinga na akaidharau. alikuwa akienda kwenye vikao vya Mtume(s.a.w.w) na kusikiliza Qur’an, kisha anarudi kwa watu wake kwa maringo.

Vyovyote itakavyokuwa sababu ya kushuka Aya ni kuwa dhahiri ya Aya inaenea kwa kila mwenye kuifanyia inadi haki na kuikalia juu, kwa sababu linalozingatiwa ni kuenea Aya, sio kuhusisha sababu.

Ole wako, tena ole wako! Kisha Ole wako, tena ole wako!

Lengo la kukaririka huku ni kuzidisha kuhadharisha na kiaga. Maana ni maangamizi na adhabu inakustahili wewe ewe mwenye dhambi.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alimshika mkono Abu Jahl na kumwambia:“Ole wako tena ole wako!” Mja wa laana huyu akasema: Unanitisha ewe Muhammad! Wallahi wewe huwezi kunifanya kitu wala Mola wako! Wallahi tena, hakuna anayenishinda katika bonde hili…”

Mtume alikuwa akasema: ‘Kila umma una Firauni wake na Firauni wa umma huu ni Abu Jahl.’ Naye aliuliwa kifo kibaya sana kwenye vita vya Badr.

Hivi anadhani mtu kuwa ataachwa bure?

Hatumjui yeyote anayefikiri na kudhania kuwa hana majukumu yoyote, kwa namna yoyote ile atakavyokuwa mjinga na mpotevu. Kama yuko mwenye kudhania hivi basi atakuwa amejishusha chini kufikia daraja ya wadudu na wanyama.

Lau Mwenyezi Mungu (s.w.t) angelimwacha bure bure angelikuwa Mwenyezi Mungu amefanya mchezo katika vitendo vyake. Ametakata Mwenyezi Mungu Mtukufu na hayo kabisa: “Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.” Juz. 17 (21:16).

Je, hakuwa ni tone la manii lililoshushwa?

Huyu anayekanusha ufufuo, hakuwa ni maji tu yaliyomininwa kwenye mfuko wa uzazi,kisha akawa pande la damu, tena akamuumba na akamlinganisha sawa? Tone la manii lilikuwa umbo baada ya umbo ndani ya viza vitatu, kisha akatoka humo akiwa mtu kamili baada ya kuwa chini ya walio chini.

Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kulifanya tone la manii ni binadamu kamili, ametoa humo watoto wa kike na wa kiume.

Je! Huyo Mungu aliyyeyafanya maji hafifu kuwa ni mtu wa ajabu katika sura yake, akili yake na vipawa vyake na akatoa humo wanawake na watoto,hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu?

Kwanini! Yeye ana uweza wa kila kitu na hakuna chochote kilichopo ila kinatamka uweza wake na kumsifu kwa sifa sifa zake. Wala kuumbwa mtu si kitu kulinganisha na kuumbwa ulimwengu:

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾

“Hakika umbo la mbingu na ardhi ni kubwa zaidi kuliko umbo la watu. Lakini watu wengi hawajui.” Juz. 24 (40:57).

Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).

MWISHO WA SURA YA SABINI NA TANO: AL-QIYAMA

26

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sabini Na Sita: Al-Insan. Imeshuka Makka Ina 31. Imesemekana isiyokuwa hivyo.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا ﴿١﴾

1. Je, kilimpitia binaadamu kipin­di katika zama ambacho hakuwa kitu kinachotajwa?

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٢﴾

2. Hakika tumemuumba mtu kutokana na tone la manii lililochanganyika, tumfanyie mtihani. Tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾

3. Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushuku­ru, au mwenye kukufuru.

إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ سَلَاسِلَ وَأَغْلَالًا وَسَعِيرًا ﴿٤﴾

4. Hakika tumewaandalia makafiri silsili na pingu na Moto mkali.

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا ﴿٥﴾

5. Hakika watu wema watakuny­wa katika glasi zilizochanganyi­ka na kafuri.

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا ﴿٦﴾

6. Ni chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiitiririsha mtiririko.

JE, KILIMPITIA BINADAMU KIPNDI

Aya 1 – 6

MAANA

Je, kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho hakuwa kitu kinacho tajwa?

Wamesema wafasiri kuwa herfi hal, tuliyoifasiri kwa maana ya je, ni ya uhakika, kwa maana ya hakika kilimpitia…

Aya hii iko katika picha ya swali na maana yake ni kusisitiza na kuhakik­isha. Lengo la Aya ni kuwa mtu anatakikana afikirie akilini mwake na kuji­uliza kuhusu uweza uliyomfanya yeye aweko baada ya kutokuweko. Ni kitu gani kimemfanya apatikane? Amepita vipi kutoka hali moja hadi nyingine? Je, anakwenda wapi?

Katika hili Imam Ali(a.s) anasema:“Amrehemu Mwenyezi Mungu mja aliyejua ametoka wapi, yuko wapi na anakwenda wapi.” Hili ndilo lengo la Aya hii. Ufuatao ni ufupi wa ufafanuzi wa yaliyoashiriwa na Aya hii na nyingine zinazofuatia katika hali ya kutoka mtu kwenye ngazi moja hadi nyingine mpaka kukamilika kwake. Ama kuhusu yuko wapi na anakwenda wapi tumekwisha fafanua huko nyuma katika kufasiri Aya za dunia na Akhera:­

1.Je, kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho hakuwa kitu kinachotajwa?

Ulipita muda mrefu sana ambao mtu hakuwa na atahari yoyote ya kuweko: “Je hakumbuki mtu ya kwamba tulimuumba kabla na hali hakuwa cho­chote?” Juz. 16 (19:67). Wataalamu wanasema kuwa mtu alipatikana hapa ardhini tangu miaka milioni 5: ” Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini.” Juz. 15 (17:55).

2.Kisha Mwenyezi Mungu akamuumba Adam, baba wa watu, kutokana na udongo:

“Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo.” Juz. 3 (3:59). Hapa aligura mtu kutoka hali ya kukosekana hadi kupatikana akiwa mchanga usiokuwa na uhai.

3.Hakika tumemuumba mtu kutokana na tone la manii lililochanganyika, tumfanyie mtihani.

Hii ni ishara ya kugura mtu kutoka udongo hadi kuwa majimaji, ambayo ni tone la manii lililokuwa kutokana na mfungamano wa aina mbali mbali ali­zoziashiria Imam Ali(a.s) kwa kauli yake:“Na jinsi yenye mchanganyiko wa udongo wa rangi tofauti, na vitu vyenye kufanana na kuafikiana, na vitu vilivyo kinyume visivyoafikiana, na viliyochanganyika vinavyobainika.”

Mingoni mwa atahari za udongo wa rangi tofauti ni tunavyomuona mtu akiwa na macho meusi na uso mweupe, katika vyenye kufanana na kuafikiana ni mifupa ya mikono na miundi na katika athari ya vilivyo kinyume visivyoafikiana ni mapenzi na chuki, tamaa na kukinai, kunyenyekea na kutakabari, mapambano ya akili na matamanio n.k. Hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Tumfanyie mtihani,’ pale anapopata mapambano makali mtu baina ya dhamiri yake na matamanio yake.

4.Tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

Hii ni ishara ya kugura mtu kutoka tone la manii lililopata uhai ndani ya tumbo lake baada ya kupita siku kadhaa akiwa kwenye giza lisilokuwa na usikizi wala uoni hadi kwenye mng’ao pamoja na usikizi na uoni, lakini bila ya akili wala utambuzi, sawa na mnyama.

5.Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria kugura mtu kutoka kwenye maisha ya mnyama hadi kwenye maisha ya ubinadamu; yaani baada ya kutimia kwake kuwa mwili ulio na hisia, Mwenyezi Mungu akampa akili na utambuzi ili aweze kupambanua baina ya haki na batili na uongofu na upotevu. Vile vile amempa uhuru ili kwa akili yake na uhuru wake aweze kubeba majukumu na kustahiki thawabu na adhabu, baada ya kubainishiwa na kupewa hoja.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameuletea ibara ya shukrani, uongofu, kwa sababu ni kumtii Mwenyezi Mungu, na uovu akauita ukafiri kwa sababu ni kumuasi yeye.

Kwa ufafanuzi zaidi wa hayo tutaashiria hali ya uwiano baina ya mtu na viumbe vingine wa ardhini kwa ujumla: Viumbe hivi vinagawanyika kwenye viumbe vilivyotulia, vizisivyokuwa na uhai wala kukua; kama vile mchanga, miamba na madini, na viumbe vingine vyenye uhai. Vyenye uhai navyo vinagawanyika mafungu matatu:

1. Uhai wa mimea; hii ina harakati na kukua bila ya kuwa na hisia wala utambuzi. Kwa hiyo mimea haisikii wala haioni, pia haina akili.

2. Ni maisha ya wanyama; miongoni mwa sifa za wanyama ni kuwa na harakati, kukua, kuhisi, kusikia na kuona, lakini bila ya kuwa na akili wala utambuzi kwa aghlab, au utambuzi wa kimafungu sio wa kiujumla

3. Ni maisha ya kiutu; miongoni mwa sifa za mtu ni kuwa na harakati, kukua, kusikia kuona, fauka ya hayo anakuwa na utambuzi wa kimafungu na wa kiujumla; kwa hiyo anajua mengi yaliyokuwa na yatakayokuwa. Ni kwa utambuzi huu na maarifa haya ndio akawa tofauti na viumbe wengine wote wa ardhini.

Kwa hiyo basi mtu anakuwa na uwiano na vitu vilivyotulia, kwa vile yeye alikuwa mchanga, anaoana na mimea kwa vile alikuwa tumboni mwa mama yake akikua pole pole na kutaharaki bila ya kusikia wala kuona, na anawiana na wanyama kwa sababu alipokuwa mtoto alikuwa na hisia, kusikia na kuona, lakini bila ya utambuzi na akili. Kisha akatofautiana na vyote kwa akili na utambuzi. Kuanzia hapa ndio akawa anabeba majuku­mu na kustahiki thawabu na adhabu, kinyume na viumbe wengine.

Hapa inatakikana kujiuliza: Ni nani aliyemgurisha mtu kutoka kipindi cha kutokuwepo, hadi kwenye mchanga uliotulia, na kutoka hapo hadi mmea unaotaharaki, hadi kufikia mnyama mwenye usikizi na hatimae binadamu kamili mwenye akili inayompa habari ya yaliyopita na yatakayokuja, akaweza kutengeneza maendeleo, na kutawala viumbe vingi, hata mnyama mwenye usikizi na uoni? Je, hali hii na mengineyo yasiyokuwa na idadi yana tafsiri nyingine zaidi ya kuweko muumba mwenye uwezo ambaye akili zinashindwa kumuwazia na ndimi haziwezi kumsifia?

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria majukumu ya mtu kwa kauli yake: “Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru,” amefuatilia kutaja aliyowaandalia makafiri kwa kusema:

Hakika tumewaandalia makafiri silsili na pingu na Moto mkali.

Silisili ni za miguu na pingu ni za mikono na moto ni wa mwili.

Hakika watu wema watakunywa katika glasi zilizochanganyika na kafuri.

Glasi ni chombo cha kioo cha kunywea. Pia neno hili hutumika kwa kiny­waji chenyewe, na haya ndiyo maana yaliyokusudiwa hapa. Wafsiri wengi wamesema kuwa kinywaji cha watu wa peponi kina harufu nzuri, kama harufu ya kafuri, na sisi tunasema kuwa mchanganyiko wa kafuri ni uhakika, kama inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Ikiwa ladha ya kafuri duniani inachukiza, basi sio lazima ya Peponi nayo iwe hivyo hivyo. Pombe ya dunia inaleta uzito kichwani na maumivu, lakini kinywaji cha pombe ya Peponi:

لَا فِيهَا غَوْلٌ وَلَا هُمْ عَنْهَا يُنزَفُونَ ﴿٤٧﴾

“Hakina madhara, wala hakiwamalizikii.” Juz. 23 (37:47).

Ibn Abbas anasema: “Kila lilichotajwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an kuhusu vilivyo Peponi, hakiko duniani isipokuwa jina tu.”

Ni chemchem watakayoinywa waja wa Mwenyezi Mungu, waki­itiririsha mtiririko.

Yaani itapita kadiri watakavyo, ni kiasi cha kutaka tu. Aya kadhaa zimekwishapita zinazosifia aliyowaandalia Mwenyezi Mungu waja wake wenye takua, na kwamba wao watastarehe humo starehe ambazo hakuna jicho lililowahi kuona wala siko lilowahi kusikia au kuwaziwa na moyo wa mtu. Na wakosefu nao wataadhibiwa kwa namna isiyosemeka wala kuwazika.

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا ﴿٧﴾

7. Wanatimiza nadhiri, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea.

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا ﴿٨﴾

8. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na mateka.

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا ﴿٩﴾

9. Hakika tunawalisha kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ﴿١٠﴾

10. Hakika tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku ya kukunja uso yenye giza kali.

فَوَقَاهُمُ اللَّـهُ شَرَّ ذَٰلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا ﴿١١﴾

11. Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.

وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا ﴿١٢﴾

12. Na atawalipa Bustani za hariri kwa vile walivyosubiri.

مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ لَا يَرَوْنَ فِيهَا شَمْسًا زَمْهَرِيرًا وَلَا ﴿١٣﴾

13. Humo wataegemea juu makochi, hawataona humo jua kali wala baridi kali.

وَدَانِيَةً عَلَيْهِمْ ظِلَالُهَا وَذُلِّلَتْ قُطُوفُهَا تَذْلِيلًا ﴿١٤﴾

14. Na vivuli vyake vitanawiri juu yao, na mashada ya matunda yake yataning’inia chini chini.

وَيُطَافُ عَلَيْهِم بِآنِيَةٍ مِّن فِضَّةٍ وَأَكْوَابٍ كَانَتْ قَوَارِيرَا ﴿١٥﴾

15. Na watapitishiwa vyombo vya fedha na bilauri za kioo.

قَوَارِيرَ مِن فِضَّةٍ قَدَّرُوهَا تَقْدِيرًا ﴿١٦﴾

16. Kioo kinachotokana na fedha, wamezikadiria kwa vipimo.

وَيُسْقَوْنَ فِيهَا كَأْسًا كَانَ مِزَاجُهَا زَنجَبِيلًا ﴿١٧﴾

17. Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.

عَيْنًا فِيهَا تُسَمَّىٰ سَلْسَبِيلًا ﴿١٨﴾

18. Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil.

وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ وِلْدَانٌ مُّخَلَّدُونَ إِذَا رَأَيْتَهُمْ حَسِبْتَهُمْ لُؤْلُؤًا مَّنثُورًا ﴿١٩﴾

19. Na watawazungukia wavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.

وَإِذَا رَأَيْتَ ثَمَّ رَأَيْتَ نَعِيمًا وَمُلْكًا كَبِيرًا ﴿٢٠﴾

20. Na utakapoyaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.

عَالِيَهُمْ ثِيَابُ سُندُسٍ خُضْرٌ وَإِسْتَبْرَقٌ وَحُلُّوا أَسَاوِرَ مِن فِضَّةٍ وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا ﴿٢١﴾

21. Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao atawanywesha kinywaji safi.

إِنَّ هَـٰذَا كَانَ لَكُمْ جَزَاءً وَكَانَ سَعْيُكُم مَّشْكُورًا ﴿٢٢﴾

22. Hakika haya ni malipo yenu; na mahangaiko yenu yameshukuriwa.

HUWALISHA CHAKULA JUU YA KUKIPENDA KWAKE

Aya 7 – 22

MAANA

Baada ya kuashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) baadhi ya yale aliyowaan­dalia watu wema kesho, hapa anasema wanastahiki hayo kutokana na sifa tatu:

1.Wanatimiza nadhiri.

Nadhiri kilugha ni ahadi, na kisharia ni kujilazimishaa mtu, aliyebaleghe na kuwa na akili timamu, kufanya jambo au kuliacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; kutenda au kuacha kuwe kunamridhisha Mwenyezi Mungu; vinginevyo itakuwa sio nadhiri, kama wanavyosema wahakiki.

Tamko la nadhiri ni kusema mwenye kuweka nadhiri: Nimejilazimisha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, au nimeweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Haiwezi kuwa nadhiri ikiwa hakuna mojawapo ya majina ya Mwenyezi Mungu; kama vile Mwingi wa rehema, Muumba, Muhuyishaji, Mfishaji n.k. Lau atasema: nimeweka nadhiri kuwa nitafanya jambo kadhaa, basi itakuwa ni mchezo.

Ahadi katika istilahi ya wanafiqh wengi, ni kusema yule mwenye kuweka ahadi: Ninamuahidi Mwenyezi Mungu, au nimejilazimisha kumwahidi Mwenyezi Mungu jambo fulani. Yamini ni kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu (kiapo). Yametangulia maelezo kuhusu Viapo katika Juz. 7 (5:59). Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapenda na anamlipa thawabu kila mwenye kusadikisha na kufanya vizuri katika kitendo au kauli; ni sawa iwe ni kauli, ahadi, nad­hiri, kiapo, ushahidi au habari yoyote.

2.Na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea.

Wanamtii Mwenyezi Mungu katika kila kitu kuhofia siku ambayo shari yake inaenea kwa kila mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na akamhali­fu katika hukumu miongoni mwa hukumu zake.

3.Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yati­ma, na mateka.

Wanajitolea kila kizuri tena wakiwa wanakihitajia sana; mfano wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu:

وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ﴿٩﴾

“Na wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.” Juz. 28 (59:9).

Mateka hapa, imesemekana ni mateka aliyetekwa na waislamu katika vita na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa Uislamu. Imepokewa riwaya kuwa maswahaba walikuwa wakimpeleka mtu waliyemteka, basi mtume humk­abidhi kwa mmoja wa waislamu na kumwambia kaa naye vizuri. Akimchukua nyumbani kwake na kumtunza kuliko yeye mwenyewe na familia yake.

Hakika tunawalisha kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. Hakika tunaogopa kutoka kwa Mola wetu siku ya kukunja uso yenye giza kali.

Hatutaki malipo kutoka kwenu wala kwa mwingine; isipokuwa tunawal­isha na kujitolea kwa msukumo wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuhofia siku ya kuchunguzwa matendo na yenye vituko vingi. Waliyasema haya kwa lugha ya maneno na ya matendo au amewasemea Mwenyezi Mungu kwa kujua imani na ikhlasi iliyo nyoyoni mwao.

Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.

Walihofia siku ya mkusanyiko wakapata kinga ya shari yake kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi, wakabadilishiwa hofu yao kuwa amani, nyuso zao zikaangaza nuru ya furaha.

Na atawalipa Bustani za hariri kwa vile walivyosubiri.

Walivumilia njaa ili wamshibishe mwingine, malipo yao yamekuwa Bustani iliyo na kila kinachotamaniwa na nafsi na kuburudika na macho. Katika tafsiri nyingi imeelezwa kuwa Aya hizi zilimshukia Imam Ali bin Abi Twalib; miongoni mwazo ni ibara ya Ar -Razi, ninamnuku: “Ametaja Al-Wahidi, katika watu wetu ‧ yaani Sunni ‧ na mwenye Al­kashaf katika Mu’tazila, kwamba Hasan na Husein(a.s) walikuwa wagonjwa, Mtume(s.a.w.w) na watu wengine wakaenda kuwaamkia, wakasema: “Ewe Abul-Hasan, unaonaje lau utaweka nadhiri kwa ajili ya wanao. Basi akaweka nadhiri Ali, Fatima na Mtumishi wao Fidha, kufunga siku tatu ikiwa watapona.

Basi wakapona. Ali akakopa pishi tatu za shairi. Fatima akasaga pishi moja na kutengeneza mikate mitano kulingana na idadi yao. Wakaiweka ili wafuturu, akaja muombaji, akasema: As-salamu alaykum, enyi watu wa nyumba ya Muhammad! Maskini jamani, nilisheni atawalisha Mwenyezi Mungu Peponi. Basi wakampa bila ya kuonja kitu isipokuwa maji, wakaamkia saumu.

Ilipofika jioni na kuleta chakula aliwasimamia yatima wakampa. Akaja mateka usiku wa tatu, wakafanya hivyo hivyo. Ilipofika asubuhi Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaona wanatetemeka kama vifaranga, akasema: “Ni huzuni kubwa iliyoje kuwaona katika hali hii! Jibril akashuka na kusema:“Chukua ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu anakupongeza kwa watu wa nyumba yako, soma Sura hii.”

Humo wataegemea juu makochi, hawataona humo jua kali wala bari­di kali.

Humo ni humo Peponi. Jua kali ni kinaya cha joto. Maana yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:31).

Na vivuli vyake vitanawiri juu yao, na mashada ya matunda yake yataning’inia chini chini.

Neno kunawiri tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu daniU ambalo lina maana ya kuwa karibu, kama walivyofasiri hivyo wafasiri wengi. Lakini pia lina maana hiyo tuliyoitumia. Tumetumia maana hiyo kwa vile inaendana na kivuli, pia inaendana na herufi alayhim, (jua yao); kama inge­likuwa na maana ya karibu ingelitumika herufi ilayihim. Kuwa chini matunda maana yake ni kuweza kuchumwa bila ya kizuizi chochote. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (69:23)

Na watapitishiwa vyombo vya fedha na bilauri za kioo; kioo kinachotokana na fedha, wamezikadiria kwa vipimo.

Ni watu wa Peponi hao, na ndio watakaokadiria. Maana ni kuwa rangi na ukubwa wa vikumbe utakua vile wanavyotaka watu wa Peponi, vile watakavyokadiria kwenye nafsi zao na kuleta picha kwenye akili zao. Wafasiri wameleta swali kuhusu Aya hii, kwamba chombo cha kioo kinawezaje kuwa cha fedha, je, ni sawa kusema kioo kinatokana na fedha na maji yanatokana na udongo? Wamejibu kuwa madini ya bilauri yametokana na fedha, lakini ni nyem­bamba zinaonesha kama kioo[10] .

Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi.

Wafasiri wanasema kuwa waarabu walikuwa wakipenda kuweka tangaw­izi kwenye vinywaji, ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akakisifia kinywaji cha Peponi kwayo.

Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil ambayo ni tamu mno, kinywaji chake kinashuka vizuri,Na watawazungukia kuwatumikiawavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa.

Wao ni kama lulu kwa uzuri wao na kunyinyirika kwao. Waliotawanywa ni ishara ya wingi wao na kuweko huku na huko.

Na utakapoyaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.

Ukiingia Peponi utaona ambayo hayajaonekana wala kusikiwa na kuwaziwa.

Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao atawanywesha kinywaji safi kabisa.

Watavaa Hariri nyembamba na nzito, vile vile mikononi mwao mtakuwa na bangili na watakunywa kinywaji safi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:31). Hakika haya ni malipo yenu; na mahangaiko yenu yameshukuriwa. Baada ya takrima yote hiyo wataaambiwa huu ndio mshahara wenu wa matendo yenu mliyoyafanyia juhudi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:19).

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ تَنزِيلًا ﴿٢٣﴾

23. Hakika Sisi tumekuteremshia Qur’an kidogo kidogo.

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تُطِعْ مِنْهُمْ آثِمًا أَوْ كَفُورًا ﴿٢٤﴾

24. Basi subiri hukumu ya Mola wako wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au

mwenye kufuru.

وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٢٥﴾

25. Na lidhukuru jina la Mola wako asubuhi na jioni.

وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا ﴿٢٦﴾

26. Na usiku msujudie Yeye, na umsabihi usiku mrefu.

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ يُحِبُّونَ الْعَاجِلَةَ وَيَذَرُونَ وَرَاءَهُمْ يَوْمًا ثَقِيلًا ﴿٢٧﴾

27. Kwa hakika watu hawa wanapenda ya sasa, na wana­iacha nyuma yao siku nzito.

نَّحْنُ خَلَقْنَاهُمْ وَشَدَدْنَا أَسْرَهُمْ وَإِذَا شِئْنَا بَدَّلْنَا أَمْثَالَهُمْ تَبْدِيلًا ﴿٢٨﴾

28. Sisi tumewaumba, na tukavi­imarisha viungo vyao. Na tuk­itaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.

إِنَّ هَـٰذِهِ تَذْكِرَةٌ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا ﴿٢٩﴾

29. Hakika haya ni mawaidha; basi anayetaka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake.

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿٣٠﴾

30. Wala hamuwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hiki­ma.

يُدْخِلُ مَن يَشَاءُ فِي رَحْمَتِهِ وَالظَّالِمِينَ أَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٣١﴾

31. Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kud­hulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.

WANAPENDA YA SASA

Aya 23 – 31

MAANA

Hakika Sisi tumekuteremshia - ewe Muhammad(s.a.w.w) -Qur’an kidogo kidogo.

Ni haki isiyokuwa na shaka na tumekuahidi kukunusuru, kwa sharti la kuvumila maudhi kutoka kwa wenye inadi na upinzani.

Basi subiri hukumu ya Mola wako.

Hukumu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kupita mambo kwa desturi yake ya maumbile na kupatikana kwa wakati wake maalum. Njia ya uon­gofu kwa mwenye kuipendelea ni nasaha na uongofu, na njia ya nusra ni kuwa na subira katika jihadi.

Wala usimtii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru.

katika yale wanayokuzuwia nayo na wanayokuvutia nayo. Washirikina walimwekea mtume mali, wanawake na uongozi ili aache mwito wake wa kumlingania Mwenyezi Mungu, akawa anakataa. Hilo linaashiriwa na kukatazwa kumtii mwenye dhambi na mwenye kufuru. Makusudio ya mwenye kufuru ni kila mpinzani.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya mwenye dhambi hapa ni Utba bin Rabia, kwa sababu alikuwa amezama kwenye starehe, mwenye kufuru ni Abu Jahl au Walid bin Mughira. Vyovyote iwavyo sababu ya kushuka, lakini haihusishi tamko.

Na lidhukuru jina la Mola wako asubuhi na jioni.

Yaani kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu katika mambo yako yote na wakati wako wote wala usiogope lawama. Umetangulia mfano wake katika Juz. 23 (33:42).

Na usiku msujudie Yeye, na umsabihi usiku mrefu.

Fanya tahajudi usiku muda kiasi. Amri hii ni ya Sunna sio ya wajib kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ ﴿٧٩﴾

“Na katika usiku amka kwayo, ni ziada kwa ajili yako.” Juz. 15 (17:79).

Kwa hakika watu hawa wanapenda ya sasa, na wanaiacha nyuma yao siku nzito.

Hawa ni ishara ya washirikina na kila mwenye kuipenda dunia, ikamtawala na kuichukia akhera na kuifanyia uadui. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameita siku nzito kwa vile itakuwa ngumu kwa makafiri.

Sisi tumewaumba, na tukaviimarisha viungo vyao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyewaleta kutoka kutokuwepo, akawatia sura na kuzifanya nzuri sura zao, vipi wanamkana na kuasi amri zake na makatazo yake?

Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.

Huu ni ukemeo kwa wale wanokadhibisha kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuwangamiza na kuwaleta watu wengine bora kuliko wao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (47:38)

Hakika haya ni mawaidha.

Haya ni haya yaliyo katika Sura hii tuliyo nayo, ndani yake mkiwa na maonyo na mapendekezo, yakiwa ni mawaidha kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.

Basi anayetaka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake; wala hamuwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha njia mbili ya kheri na shari. Akakataza hii na akaamrisha ile, akamwacha mtu ajichagulie mwenyewe, lakini mwenye inadi hawezi kufanya heri ila akifanyishwa kwa nguvu na Mwenyezi Mungu, na hili haliwezi kuwa kwa sababu litakwenda kinyume na uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, hikima yake na desturi yake kwa viumbe wake. Tazama Juzuu hii tuliyo nayo (74:56), tumefafanua zaidi huko.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima.

Mwenye kujua hali za waja wake, ana hikima kwa sababu hatoi amri ila kwa lenye heri na masilahi, wala hakatazi ila lenye shari na ufisadi.

Humuingiza amtakaye katika rehema yake.

Makusudio ya rehema hapa ni Pepo na matakwa yake ni kuwa hamwingizi Peponi yoyote yule ila kwa juhudi na kuifanyia kazi; hivyo ndivyo anavyotaka.

Aya zinazofahamisha hivyo ziko nyingi na wazi; miongoni mwazo ni: “Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira? Juz. 4 (3:142). Vipi atataka Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwingiza Peponi asiyestahiki na hali alimtoa humo Adam alipoasi.

Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.

Wenye takua watapata rehema ya Mwenyezi Mungu na wakosefu watapa­ta ghadhabu na adhabu yake.

MWISHO WA SURA YA SABINI NA SITA: AL-INSAN