4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٩﴾
9. Na waliofanya maskani na imani yao kabla yao, wanawapenda waliohamia kwao wala hawapati dhiki katika vifua vyao kwa walivyopewa, na wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.
وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٠﴾
10. Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole Mwingi wa rehema.
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ نَافَقُوا يَقُولُونَ لِإِخْوَانِهِمُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَئِنْ أُخْرِجْتُمْ لَنَخْرُجَنَّ مَعَكُمْ وَلَا نُطِيعُ فِيكُمْ أَحَدًا أَبَدًا وَإِن قُوتِلْتُمْ لَنَنصُرَنَّكُمْ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿١١﴾
11. Je, Huwaoni wanaofanya unafiki wanawaambia ndugu zao waliokufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamtii yeyote kabisa dhidi yenu.
Na mkipigwa vita lazima tutawasaidia. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.
لَئِنْ أُخْرِجُوا لَا يَخْرُجُونَ مَعَهُمْ وَلَئِن قُوتِلُوا لَا يَنصُرُونَهُمْ وَلَئِن نَّصَرُوهُمْ لَيُوَلُّنَّ الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يُنصَرُونَ ﴿١٢﴾
12. Wakitolewa hawatatoka pamoja nao na wakipigwa vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo; Kisha hawatanusuriwa.
لَأَنتُمْ أَشَدُّ رَهْبَةً فِي صُدُورِهِم مِّنَ اللَّـهِ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ ﴿١٣﴾
13. Hakika nyinyi ni tishio zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasiofahamu.
لَا يُقَاتِلُونَكُمْ جَمِيعًا إِلَّا فِي قُرًى مُّحَصَّنَةٍ أَوْ مِن وَرَاءِ جُدُرٍ بَأْسُهُم بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْقِلُونَ ﴿١٤﴾
14. Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vilivyozatitiwa kwa ngome au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.
كَمَثَلِ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَرِيبًا ذَاقُوا وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٥﴾
15. Ni kama mfano wa waliokuwa kabla yao hivi karibuni. Walionja ubaya wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.
WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO
Aya 9 – 15
MAANA
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha daraja ya wahajiri katika Aya iliyotangulia, sasa anabainisha daraja ya Answar, kwa kusema, kama ifuatavyo:-
Na waliofanya maskani na Imani yao kabla yao, wanawapenda waliohamia kwao.
Makusudio ya maskani hapa ni Madina. Maana ni kuwa Answar, wenyeji wa Madina, walimsaidia Mtume pamoja na wale waliohama naye. Wakajitolea kwa nafsi zao na mali zao; bali waliwapendela wao kuliko nafsi zao; kama itakavyoashiria Aya.
Miongoni mwa Aya zilizoshuka kwa ajili ya Answar ni:
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٧٤﴾
“Na wale waliokaribisha na kusaidia, hao ndio waumini kweli, wana wao maghufira na riziki njema.” Juz. 10 (8:74).
Wala hawapati dhiki katika vifua vyao kwa walivyopewa Wahajiri.
Mwanzoni Wahajiri walikuwa ni mafukara zaidi katika Madina wakipata tabu. Lau si Answar wangelikufa na njaa. Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akiwapa sadaka mafukara na hawapi matajiri na walio na uwezo wa kuchuma.
Kwa hiyo alikuwa akiwapa kipaumbele Wahajiri; mara nyingine akiwapa ngawira wao tu. Answar walikuwa wakiliridhia hilo bila ya kuona choyo wala dhiki nyoyoni, na wakiona ni haki kabisa. Ndio akasajili Mwenyezi Mungu (s.w.t) sifa zao hizi kwenye Kitabu chake.
Na wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.
Kumpendela mwingine kuliko nafsi yake mtu, akiwa na mahitaji, hakuwezi kulinganihswa na jambo lolote isipokuwa kujitolea mhanga. Imeelezwa katika vitabu vya Tafsir na Historia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
aliwaambia Answar: “Mkipenda ngawira hii iwe baina yenu na Wahajiri, lakini mshirikiane nao katika mali yenu, au muwaachie ngawira na nyinyi mbaki na mali yenu. Answar wakasema: bali tutawaachia ngawira na tutashirikiana nao katika mali yetu ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Hapo Mtume akawaombea dua na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu! Warehemu Answar na watoto wa Answar.”
Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.
Uchoyo ni mama wa maovu. Mwenye kuuitikia utamzuia na kila heri, na mwenye kuushinda kwenye nafsi yake basi atakuwa ameikinga na kila uovu na hatari.
Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani.
Yaani waliokuja baada ya Answar na Wahajiri. Makusudio ya waliokuja baada yao ni kila mwenye kufuata sera mpaka siku ya Kiyama, wala hakuna njia ya kuwahusisha Tabiina (waliowafuatia maswahaba). Kwa sababu linalozingatiwa ni matendo sio mahali fulani wala wakati. Maswahaba hawakufikia walipokuwa ila ni kwakuwa walisikilza kauli wakafuata mazuri yake.
Wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini.
Ni muhali kabisa kuwa pamoja imani na undani. Inawezekana mtu kujiwekea undani?
Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole Mwingi wa rehema
kwa waja wako walioitakasa dini yao na nyoyo zao kutokana undani na unafiki.
Je, Huwaoni wanaofanya unafiki wanawaambia ndugu zao waliokufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamtii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima tutawasaidia.
Makusudio ya watu wa Kitab hapa ni Bani Nadhir, ndugu wa wanafiki katika ukafiri na uadui kwa Mtume. Aya inaashiria tukio maalum. Pale Mtume(s.a.w.w)
alipotangaza vita dhidi ya Bani Nadhir, wanafiki wakiongozwa na Abadallah bin Ubayya waliwaambia: piganeni na Muhammad na sisi tuko na nyinyi, akiwapiga nasi tutampiga na wakiwatoa Madina tutatoka nanyi; hatutamsikiliza Muhammad wala mwenginewe.
Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo
kwenye kauli yao na ahadi yao.
Wakitolewa
Bani Nadhirhawatatoka pamoja nao
wanafiki,na wakipigwa vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo;
Hii ndio hali ya mnafiki, ulimi wake unahalifiwa na moyo wake na dhahiri yake inahalifiwa na siri yake.
Kisha hawatanusuriwa
wala kunufaika na kwa vitimbi na unafiki wao.
Hakika nyinyi ni tishio zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasiofahamu.
Wanafiki wanawaogopa waumini kwa ukali wao wa vita, kwa sababu wao wanatazamia shari ya haraka wala hawatazimii adhabu inayokuja Akhera.
Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta.
Mayahudi hawakabiliani na waumini uso kwa uso katika uwanja wa vita, bali wanajificha kwenye mitaa yao nyuma ya ngome na kuta na kuwarushia waumini mishale na mawe; kama ilivyo hali ya mwoga.
Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali.
Wao wana nguvu kwa maandalizi yao na idadi yao, lakini masilahi na hawa za nafsi zimewatawanyisha. Wao wamechangukana, hata kama wanajionyesha kuwa na umoja na mapenzi.
Lau wangelikuwa na umoja na kupendana wangeliwatokea kupambana nanyi, lakini hawakupigana nanyi. Hili liko kwa wayahudi na wasiokuwa wayahudi, kwani umoja ni nguvu hata kama idadi na nyenzo ni ndogo, na utengano ni udhaifu hata kama kuna nyenzo na wingi wa watu.
Tumeshuhudia ushindi wa watu wasio na haki wachache juu ya walio na haki wengi na wenye nyenzo. Siri ni utengano wa hawa kwenye haki yao na umoja wa wale kwenye batili yao.
Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili
ya kufahamu kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ni kama mfano wa waliokuwa kabla yao hivi karibuni. Walionja ubaya wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.
Mayahudi walijenga uadui na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w
)
; ni sawa na hali ya makafiri wa kikuraishi na wengineo waliompiga vita Mtume; pale walipoishia kwenye fedheha ya duniani na Akhera ni adhabu ya kuungua.
كَمَثَلِ الشَّيْطَانِ إِذْ قَالَ لِلْإِنسَانِ اكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦﴾
16. Ni kama mfano wa Shetani anapomwambia mtu: kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
فَكَانَ عَاقِبَتَهُمَا أَنَّهُمَا فِي النَّارِ خَالِدَيْنِ فِيهَا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الظَّالِمِينَ ﴿١٧﴾
17. Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hayo ndiyo malipo ya madhalimu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٨﴾
18. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿١٩﴾
19. Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio mafasiki.
لَا يَسْتَوِي أَصْحَابُ النَّارِ وَأَصْحَابُ الْجَنَّةِ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٢٠﴾
20. Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.
AKIKUFURU HUMWAMBIA MIMI NIKO MBALI NAWE
Aya 16 – 20
MAANA
Ni kama mfano wa Shetani anapomwambia mtu: kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
Wanafiki waliwaambia Bani Nadhir: “Piganeni na Muhammad na sisi tuko pamoja nanyi katika vita,” lakini yalipowafika yaliowafika, walijificha kwenye viota vyao na hawakuonekana hata athari yao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameifananisha hali ya wanafiki na Bani Nadhir na hali ya shetani na mtu mwenye kutenda dhambi. Huwa anamhadaa kwa ufisadi na upotevu na kumpa tamaa ya amani. Mambo yakichacha humwacha na adhabu na maangamizi na kujitenga naye na kudhihirisha hofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (8:48) na Juz. 13 (14:22).
Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hayo ndiyo malipo ya madhalimu.
Wawili ni shetani na mtu aliyeingia kwenye mtego wake. Maana yako wazi. Kwa ufupi ni kuwa kila mmoja, mwenye kuhadaa na mwenye kuhadaiwa, atakuwa katika Jahannam ambayo ni marejeo mabaya.
Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu,
ambaye nyinyi mko mikononi mwake, na mwenye kumcha Mwenyezi Mungu humfanyia wepesi mambo yake; kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Qur’an (65:4).
Na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho.
Kila analolifanya mtu katika maisha haya huwa amelifanya kwa ajili ya Akhera. Mwenye busara anaangalia kwenye dunia yake kwa mtazamo wa mwenye kuicha kwa wema sio mwenye kuchukua anasa zake.
Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
Mwenyezi Mungu anamjua mwenye kuamini kwa kauli na vitendo na mwenye kumwamini kwa fikra tu anayoisema na kuisahau kwenye vitendo. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelikariri jambo la takua kwa ukomo wa kuhimiza na kupendekeza.
Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao.
Walisahau kufanya kwa amri ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu akawasahaulisha kufanya kwa masilahi ya nafsi zao. na aliyedanganyika zaidi katika watu ni yule aliyejisahau na asifanye kwa ajili ya usalama wake kujiepusha na maangamizi.
Hao ndio mafasiki.
Kwa sababu hawakunufaika na ubainifu wa Mwenyezi Mungu na kupata funzo kwa mawaidha yake.
Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.
Vipi atakuwa sawa mwema na mwovu? Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa miongoni mwazo ni Juz. 21 (32:18).
لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا الْقُرْآنَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُ خَاشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾
21. Lau tungelieiteremsha hii Qur’an juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeliuona ukinyenyekea, ukipasuka kwa hofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu ili wafikiri.
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿٢٢﴾
22. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu, Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٢٣﴾
23. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwangaliaji, Mwenye nguvu, Jabari, Mkubwa; Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayomshirikisha nayo.
هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٤﴾
24. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kinamsabihi kilicho katika mbingu na ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
LAU TUNGELIITERMSHA HII QUR’ANI JUU MLIMA
Aya 21 – 24
MAANA
Lau tungelieiteremsha hii Qur’an juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeliuona ukinyenyekea, ukipasuka kwa hofu ya Mwenyezi Mungu.
Hii ni kiasi cha kukadiria tu, kunakofahamika kutokana na neno ‘Lau.’ Lengo ni kubainisha ukuu wa Qur’an, kwamba ina nguvu na athari; kiasi ambacho lau itateremshwa kwenye jabali basi lingenyenyeka na kulainika pamoja na ugumu wake. Pia lingelipasuka na kuanguka kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu. Basi vipi mtu ambaye anaumizwa na chawa na kufa kwa kusongwa koo na jasho humfanya anuke; kama alivyosema Amirul Muminin, Ali
?
Ana nini mtu huyu mnyonge, “anayesikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anang’ng’ania huku akijivuna, kama kwamba hakuzisikia. ”
Juz. 25 (45:8).
Je, ni kwa kuwa moyo wake ni mgumu kama jabali ambalo limekazana sana, au ni ujinga, inadi na kung’ang’ania upotevu?
Na hiyo ni mifano tunawapigia watu ili wafikiri,
katika hikima ya Qur’an, mawaidha yake, dalili yake, na ubainifu wake, na waongoke, kwa nuru yake, kwenye njia ya usawa, lakini:
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ ﴿٣٧﴾
“Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.”
Juz. 26 (50:37).
Baada ya hayo yote, hakika ukuu wa Qur’an ni ukuu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Walisema wakale: maneno ni sifa ya mwenye kusema; hasa yale yanayorudia ilimu yake.
Ndio maana Mwenyezi Mungu akaisifia Qur’an kwa sifa zake; kama vile nguvu, hekima, utukufu, ukuu, nuru, haki, rehema, ukweli n.k.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajisifu kwa sifa zake tukufu akasema:Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu,
apasaye kuabudiwa kwa haki, anayesifika kwa sifa zote nzuri za ukamilifu; zikiwemo hizi zifuatazo:-
Mwenye kuyajua yaliofichikana na yanayoonekana
. Anayajua yaliyoghaibu kwa watu na yaliyo dhahiri.
Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
. Sifa mbili hizi zimetokana na rehema kwa maana ya hisani. Inawezekana kuwa kuchanganywa matamko mawili ni kuashiria kuwa rehema yake imeenea kila kitu, hata katika hali ya kughadhibika kwake; na kwamba kuikatia tamaa ni kufuru na upotevu.
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu.
Huu ni msisitizo wa tawhid. Yeye niMfalme;
ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, Ndiye anayetoa uhai na kufisha.
Mtakatifu;
yaani ametakasika na yasiyolaikiana na utukufu wake.Mwenye salama
; kwa sababu inatokana na Yeye mtukufu utulivu na amaniMtoaji wa amani
; Anawapa thawabu waumini na anawapa amani ya adhabu ya moto.Mwangaliaji
; Mwenye kuchunga na kuhifadhi.
Mwenye nguvu
; asiyeshindwa wala kuzidiwa nguvu.Jabari
; Aliye juu bila ya kufikiwa.Mkubwa;
Ana ukubwa na utukufu.Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayomshirikisha nayo
, ya kuwa na mshirika, mke na mtoto.Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji
.
Hizi ni sifa mbili tofauti. Neno mtengenezaji tumelifasiri kutokana na neno Bariu ambalo imesemekana kuwa hapa lina maana ya kuwa mbali na upungufu.Mtia sura
; Mwenye kuumba sura na umbo.Mwenye majina mazuri kabisa.
Kila jina lake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni zuri na ni kuu. Tazama Juz. 9 (7:180) Kifungu cha: ‘Je, majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo?’
Kinamsabihi kilicho katika mbingu na ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Tasbihi inakuwa kwa lugha ya maneno na lugha ya hali. Tazama Juz. 15 (15:44) kifungu cha ‘Kila kitu kinamsabihi.
MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA TISA: SURAT AL-HASHR