5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sitini: Surat Al – Mumtahina. Imeshuka Madina. Ina Aya 13.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَقَدْ كَفَرُوا بِمَا جَاءَكُم مِّنَ الْحَقِّ يُخْرِجُونَ الرَّسُولَ وَإِيَّاكُمْ أَن تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ رَبِّكُمْ إِن كُنتُمْ خَرَجْتُمْ جِهَادًا فِي سَبِيلِي وَابْتِغَاءَ مَرْضَاتِي تُسِرُّونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَأَنَا أَعْلَمُ بِمَا أَخْفَيْتُمْ وَمَا أَعْلَنتُمْ وَمَن يَفْعَلْهُ مِنكُمْ فَقَدْ ضَلَّ سَوَاءَ السَّبِيلِ ﴿١﴾
1. Enyi mlioamini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki, mkiwapa mapenzi, na wao wamekwishaikataa haki iliyowajia, wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu mnamwamini Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu, mnafanya upenzi nao kwa siri, na Mimi nayajua mnayoyaficha na mnayodhihirisha. Na mwenye kufanya hayo kati yenu basi amepotea njia ya sawa.
إِن يَثْقَفُوكُمْ يَكُونُوا لَكُمْ أَعْدَاءً وَيَبْسُطُوا إِلَيْكُمْ أَيْدِيَهُمْ وَأَلْسِنَتَهُم بِالسُّوءِ وَوَدُّوا لَوْ تَكْفُرُونَ ﴿٢﴾
2. Wakiwakuta wanakuwa maadui zenu, na wanawakunjulia mikono yao na ndimi zao kwa uovu. Na wanapenda muwe makafiri.
لَن تَنفَعَكُمْ أَرْحَامُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَفْصِلُ بَيْنَكُمْ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٣﴾
3. Hawatawafaa jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
MSIMFANYE RAFIKI ADUI WANGU NA WENU
Aya 1 – 3
KISA KWA UFUPI
Imetangaa kuwa Aya hizi zilishuka kwa Hatab bin Abi Balta’a ambaye alipata mtihani mkali siku ya Badr. Kwa ufupi wamesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
aliaanda jeshi kuipiga Makka. Hatab alipojua hivyo akawaandikia barua Makuraishi kuwahadharisha, akampa mwanamke kuipeleka. Mwenyezi Mungu akampa wahyi Mtume wake habari ya Hatab.
Basi Mtume akawatuma swahaba zake, akiwemo Imam Ali
, wakampata njiani. Walipomuuliza kuhusu barua akakataa, baadhi wakamuamini, lakini Ali akamkatalia na akamtishia kumuua, ndipo akaitoa barua kwenye kucha zake.
Wakaja naye kwa Mtume(s.a.w.
w
)
. Akamuuliza Hatab: ni nani aliyeandika hii? Hatab akasema: “Ni mimi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wallah, sijakufuru tangu niliposilimu, wala sijadanganya tangu nilipoamini, lakini nimefanya hivi kwa makuraishi kuwahami watu wangu na shari yao, na nimejua kuwa Mwenyezi Mungu amewafedhehesha.”
Basi Mtume alimwamini na akamkubalia udhuru wake.
MAANA
Enyi mlioamini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki, mkiwapa mapenzi.
Kuna baadhi ya wafasiri wamefasiri: ‘mkiwapeleka (habari) kwa ajili ya mapenzi.’ Lakini tafsiri ya kwanza ndiyo waliyoisema wengi.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha waumini wasiwe na muungano wowote wa mapenzi na maadui wa haki, wala wasiwe na mwasiliano nao yoyote kwa sababu zozote ziwazo. Kwa sababu wao ni maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui wa waliomwamini.
Na wao wamekwishaikataa haki iliyowajia, wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu mnamwamini Mwenyezi Mungu, Mola wenu.
Aya hii inaashiria sababu za kukataza mapenzi na maadui wa haki, kuwa ni: kwanza, waliikataa Qur’an na Muhammad(s.a.w.
w
)
kwa inadi. Pili, wao walimtoa Mtume nyumbani kwake na wale walioamini pamoja naye. kwa kuwa walimwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuyatupilia mbali masanamu.
Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu.
Maadamu mmeacha watu wenu na mji wenu kwa ajili ya kuliinua neno la Mwenyezi Mungu vipi muwafanye marafiki maadui wa Mwenyezi Mungu? Je, yanaweza kuwa pamoja mapenzi ya Mwenyezi Mungu na mapenzi ya maadui zake katika moyo mmoja? Mnapelekwa wapi?
Mnafanya upenzi nao kwa siri, na Mimi nayajua mnayoyaficha na mnayodhihirisha.
Mnafanya siri mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kujua siri yenu. Vipi iwe hivyo na hali kila siri kwake ni wazi na kila ghaibu kwake ni dhahiri?
Na mwenye kufanya hayo kati yenu basi amepotea njia ya sawa.
Hiili ni onyo na hadhari kwa kila mwenye kuiacha njia ya uongofu na haki; hasa wahaini na wenye njama.
Wakiwakuta wanakuwa maadui zenu, na wanawakunjulia mikono yao na ndimi zao kwa uovu. Na wanapenda muwe makafiri.
Lau maadui wa haki wangepata fursa wangeliwatukana na kuwaua waumini.
Hawatawafaa jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
Sio mali wala watoto, elimu au nasaba itakayoweza kufaa siku ya hisabu isipokuwa amali njema. Maana haya yamekaririka kwenye Aya kadhaa; ikiwemo Juz. 4 (3:116).
قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ إِلَّا قَوْلَ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ لَأَسْتَغْفِرَنَّ لَكَ وَمَا أَمْلِكُ لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ رَّبَّنَا عَلَيْكَ تَوَكَّلْنَا وَإِلَيْكَ أَنَبْنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٤﴾
4. Hakika nyinyi mna kigezo kizuri kwa Ibrahim na wale waliokuwa pamoja naye, walipowaambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunawakataa; na umekwisha dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomwamini Mwenyezi Mungu peke yake. Isipokuwa kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika nitakuombea maghufira, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi Mungu. Mola wetu! Juu yako tumetegemea, na kwako tumerudi, na kwako ndio marejeo.
رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلَّذِينَ كَفَرُوا وَاغْفِرْ لَنَا رَبَّنَا إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٥﴾
5. Mola wetu! Usitufanyie mtihani kwa waliokufuru; Na tughufirie, Mola wetu! Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِيهِمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَمَن يَتَوَلَّ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٦﴾
6. Kwa yakini kimekuwa kigezo kizuri kwenu katika mwendo wao, kwa anayemtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kugeuka basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
عَسَى اللَّـهُ أَن يَجْعَلَ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَ الَّذِينَ عَادَيْتُم مِّنْهُم مَّوَدَّةً وَاللَّـهُ قَدِيرٌ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٧﴾
7. Asaa Mwenyezi Mungu akatia mapenzi baina yenu na wale mliofanya nao uadui. Na Mwenyezi Mungu ni muweza, na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.
KIGEZO CHEMA
Aya 4 – 7
MAANA
Hakika nyinyi mna kigezo kizuri kwa Ibrahim na wale waliokuwa pamoja naye.
Maneno yanaelekezwa kwa maswahab; hasa Hatab Bin abi Balta’a, ambaye aliwapa mapenzi washirikina. Makusudio ya yaliokuwa pamoja na Ibrahim ni kila mwenye kufuata sera; ni sawa awe wakati wake au baada yake. Inavyojulikana ni kuwa hakuamini katika watu wa Ibrahim isipokuwa Lut.
Maana ni kuwa kipenzi cha mwingi wa rehema (Khalilurrahman), Ibrahim
na aliyeamini pamoja naye walipata tabu sana kutoka kwa washirikina, mpaka wakaihama miji yao wakaacha wake na watoto; sawa na yaliyompata Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na maswahaba.
Ibrahim na waliokuwa pamoja naye walifanya subira na wakavumilia wala mali na watoto waliowaacha hawakuwafadhaisha. Basi ni juu yenu enyi maswahaba wa Mtume muwaige wale walioamini pamoja na Ibrahim, wala msisumbuke kwa mali na watoto, na mkaungana na washirikina kwa ajili ya hilo.
Walipowaambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunawakataa; na umekwisha dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomwamini Mwenyezi Mungu peke yake.
Walioamini pamoja na Ibrahim waliwaambia makafiri: Sisi hatuna uhusiano wowote na nyinyi, ni maadui zetu mpaka siku ya mwisho, maadamu ni maadui wa Mwenyezi Mungu mkiabudu masanamu na nyota.
Isipokuwa kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika nitakuombea maghufira, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kama kwamba muulizaji aliuliza: Vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kuwa Ibrahim na walioamini pamoja naye walijitenga na washirikina pamoja na kuwa Ibrahim mwenyewe alisema:
قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾
“Amani iwe juu yako (salamun alayka)! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu. Hakika yeye ananihurumia sana.” Juz. 16 (19:47).
Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba Ibrahim alitaka kumwombea msamaha baba yake kwa vile alikuwa amemwahidi kuwa ataamini. Ilipombainikia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijitenga naye; kama ilvyokuja katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ ﴿١١٤﴾
“Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipompambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa Mpole sana wa moyo, mvumilivu.” Juz. 11 (9:114).
Zaidi ya hayo ni kuwa Ibrahim alimwambia baba yake: “Wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi Mungu.” Mambo yote yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu.”
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha jinsi Ibrahim na wale walioamini pamoja naye jinsi walivyoachana na watu wao na miji yao na kukimbilia kwa Mwenyezi Mungu, wakasema:
Mola wetu! Juu yako tumetegemea
. Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu anamtosha.Na kwako tumerudi
. Tumerudi kwako katika yale yaliyotushughulisha duniani.Na kwako ndio marejeo
kwa ajili ya hisabu na malipo.
Mola wetu! Usitufanyie mtihani kwa waliokufuru
; yaani usitusalitie viumbe wako washari wakatutia kwenye mtihani tusiouweza.Na tughufirie,
madhambi yetu yaliyopita.
Mola wetu. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu,
hukosewi wala hakosewi anayekimbilia kwako.Mwenye hikima
katika kuupeleka ulimwengu na kuupangilia.
Kwa yakini kimekuwa kigezo kizuri kwenu katika mwendo wao, kwa anayemtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazidisha kusisitiza kufuata mfano wa Ibrahim na alioamini pamoja naye. Amerudia Mwenyezi Mungu na kuukariri mfano huu, ili akumbuke au awe na matarajio mwenye kutaraji thawabu na akahofia adhabu yake.
Na mwenye kugeuka basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
Mwenye kuacha kufuata vigezo vya watu wema, basi Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na viumbe wake, mstahiki wa sifa njema katika dhati yake, sifa zake na vitendo vyake vyote. Namna hii Mwenyezi Mungu anawaamuru waovu wapate funzo na mawaidha kwa mwisho mbaya wa waliopita na kuwaamuru waumini kuiga uongofu wa waliopita.
Asaa Mwenyezi Mungu akatia mapenzi baina yenu na wale mliofanya nao uadui.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa hili anaashiria ushindi wa Makka na kwamba wengi wa washirikina ambao Mwenyezi Mungu amekataza kufanya urafiki nao, wataingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi. Hapo mtachanganyika na kuwa na mapenzi na waislamu wapya.
Na Mwenyezi Mungu ni Muweza
wa kuondoa uadui na sababu zake na mahali pake kuweka mapenzi na yanayopelekea hayo.Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Maghufira Mwenye kurehemu,
anawaghufiria madhambi waja wake wenye kutubia na kuwafunika kwa rehema yake.
Ndio! Mwenyezi Mungu alitekelza ahadi yake, akamnusuru mja wake, Bara Arabu yote ikawa chini yake, Makka ikasalimu amri, wakaingia watu katika dini ya Mwenyezi Mungu makundimakundi na yakapatikana mapenzi baina ya wale waliokuwa maadui jana.
لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٨﴾
8. Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakuwapiga vita, wala hawakuwatoa makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.
إِنَّمَا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ قَاتَلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَأَخْرَجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ وَظَاهَرُوا عَلَىٰ إِخْرَاجِكُمْ أَن تَوَلَّوْهُمْ وَمَن يَتَوَلَّهُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٩﴾
9. Hakika Mwenyezi Mungu anawakataza kufanya urafiki na wale tu waliowapiga vita, na wakawatoa makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu. Na wanaowafanya hao marafiki basi hao ndio madhalimu.
MUNGU HAWAKATAZI WASIOWAPIGA VITA
Aya 8 – 9
MAANA
Dola Rafiki Na Dola Adui
Uislamu umetoa mwito wa usalama na ukakataza vita isipokuwa kwa kujikinga au kumsaidia mwenye kudhulumiwa.
Kwenye hili la kwanza Qur’an imeashiria kwa kusema:
وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿١٩٠﴾
“Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga, wala msichokoze. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaochokoza.” Juz. 2 (2:190).
Sababu ya pili imeashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ﴿٩﴾
“Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hayo linadhulumu jingine, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu.” Juz. 26 (49:9).
Qur’an imepinga na kukana vita vya kuharibu na kutaka kutawala vyakula na vyanzo vya mali za watu, ikasema: “Wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.”Juz. 12 (11:85)
Ikasema tena Qur’an:
تِلْكَ الدَّارُ الْآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لَا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الْأَرْضِ وَلَا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٨٣﴾
“Hayo ndiyo makazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasiotaka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho ni wa wenye takua.” Juz. 20 (28:83).
Aya hizi ni miongoni mwa Aya zinazounganisha dunia na Akhera na ufufuo wa kwanza na wa pili. Tazama Juz. 4 (3:182-183) kifungu cha ‘Thamani ya Pepo.’
Ama kwenye usalama, kuna Aya kadhaa zilizouhimiza; miongoni mwazo ni:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً ﴿٢٠٨﴾
“Enyi mlioamini! Ingieni katika usalama nyote.” Juz. 2 (2:208).
Nyngine ni:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ﴿١٢٥﴾
“Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.” Juz. 14 (16:125).
Aya hizi zinathibitisha misingi ya maelewano na na jinsi ya kutatua matatizo ya serikali na mengineyo kwa njia ya amani. Bali Qur’an imetoa mwito wa udugu wa kimataifa, unasimama kwenye misingi ya kujuana, mapenzi, wema na uadilifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Na tumewafanya mataifa na makabila ili mjuane.” Juz. 26 (49:13).
Kwa hiyo kujuana na kuzoeana ndio sababu ya kuweko makabila na mataifa. Ama wema na uadilifu ndio maudhui ya Aya mbili hizi tulizo nazo. Tumwachie Ustadh Khalid bin Khali, aliyesema:
“Hakika msingi unaotuchorea mwongozo wa mfungamno wetu na vita leo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:“Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakuwapiga vita, wala hawakuwatoa makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawakataza kufanya urafiki na wale tu waliowapiga vita, na wakawatoa makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu. Na wanaowafanya hao marafiki basi hao ndio madhalimu.”
Hebu tujiulize na tuwaulize wakazi wote wa duniani: Ni dola ipi inayopiga vita dini yetu, ikatutoa makwetu? Ni nani aliyewafukuza waarabu kutoka Palestina, wakapora mali zao, ardhi zao na majumba yao? Ni akina nani waliowapa silaha Israil, wakawapa mali na kuwaambia kuweni mwiba kwa waarabu? Ni nani aliyetuzuilia silaha zetu na akaiba vyakula vyetu? Ni nani wanaosimama kwenye mikutano ya kimataifa dhidi ya haki yetu na kuwasaidia maadui zetu?”
“Hawa wote, enyi mabwana, ndio wale aliotukataza Mwenyezi Mungu kufanya urafiki nao. Kuna Aya nyingine inatufichulia njia nyingine ya kuishi na hawa, inayosema:
وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَكُمْ ﴿١٩٠﴾
“Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga.” Juz. 2 (2:190)”
“Hawa ndio walioungana dhidi yetu. Mwenyezi Mungu anatuhimiza kupigana nao kwa vile ndio walioanza na ni madhalimu.
“Hivi ni dini gani waliyoitegemea? Au ni hulka gani waliyoitegemea wakosefu hawa ambao wanataka tuungane na magharibi na kuelewana nao? Mimi sijui sura yoyote ya ulahidi wa dini na kuivunjia heshima haki na wajibu, inayofedhesha kuliko mwito huu. Je, tupigane na walio na amani na sisi na tuwape amani wale wanatupiga na kutuchinja kama kondoo?
“Itakuwaje na wao walisherehekea kwenye usiku mweusi harusi ya mashariki ya kati na wakazidisha kukalia miji yetu, wakaua nafsi zetu na uhuru wetu na wakaondoa umoja wetu? Basi mwenye akili na anufaike na majaribio na mwenye dini asome kauli ya Mwenyezi Mungu: Piganeni na wale wanaopigana nanyi.”
Naam! Nimedokoa maneno haya kutoka kitabu Addin fi khidmatisha’ab (Dini katika kuwatumikia wananchi) kilichochapishwa 1963.
Lau Ustadh Khalid angekiandika leo asingelizidisha hata herufi moja ya alioyaandika miaka hiyo. Kwa sababu ana uhakika kuwa yaliyotokea mwezi wa Juni 1967 na yanayotokea hivi sasa ni sehemu ya yaliopangwa na wakoloni wazayuni waliopita na wakawasaidia wale wanaopigana katika njia ya wachinjaji wa watu wao, na wachinjaji nao wakiwategemea waarabu wanaopupia maslahi yao.
Wameafikiana mafakihi wa madhehebu kuwa inafaa, dhimmiy (asiyekuwa na vita na waislamu) katika watu Kitabu, kupewa sadaka, isiyokuwa ya wajibu, kutoka kwa Mwislamu. Abu Hanifa akasema, pia inafaa kupewa Zaka ya fitr na kafara.
Vile vile wameafikiana kufaa kumuusia wasiya wa mali na waqf. Hayo wameyatolea dalili kwa Aya hizi tulizo nazo: “Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakuwapiga vita…”.