7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sitini Na Mmoja: Surat As – Saff. Imeshuka Madina. Ina ya 14.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١﴾
1. Vinamsabihi Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ ﴿٢﴾
2. Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda?
كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ ﴿٣﴾
3. Ni chukizo kubwa kwa Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda.
إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِهِ صَفًّا كَأَنَّهُم بُنْيَانٌ مَّرْصُوصٌ ﴿٤﴾
4. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaopigana katika Njia yake kwa safu kama kwamba wao ni jengo lililojengwa kwa risasi.
وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ لِمَ تُؤْذُونَنِي وَقَد تَّعْلَمُونَ أَنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٥﴾
5. Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliyetumwa kwenu? Walipopotoka, Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki
وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُم مُّصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ فَلَمَّا جَاءَهُم بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَـٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٦﴾
6. Na Isa bin Maryam aliposema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat, na mwenye kubashiria Mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad. Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhahiri!
KAMA KWAMBA WAO NI JENGO
Aya 1 – 6
MAANA
Vinamsabihi Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Kila kilichoko kinashuhudia uwezo wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na hikima yake, kwa lugha ya maneno au ya hali. Imetangulia kwa herufi zake. Katika Juz. 27 (57:1) na katika Juzuu hii tuliyo nayo mwanzo wa sura 59. na tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 15 (17:44).
Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda?
Watu wengi wanakusudia uwongo; wanafanya kwa kujificha yale ambayo hawezi kuyadhihirisha. Hakuna mwenye shaka kwamba hawa ni wanafiki kwa kila maana ya neno unafiki.
Basi haifai kuitwa enyi waumini! Hata kama watadhihirisha imani.
Kuna watu wengine wanasema na wanajiandaa kwa nia ya ukweli na kutekeleza, lakini wanapata matatizo yasiyoweza kuzuilika na kushindwa kutekeleza pamoja na juhudi walizofanya. Hawa wanasamehewa, hilo halina shaka.
Na kuna wengine wanasema na wanakuwa na nia ya kutekeleza, lakini ukifika wakati wananaza kuwa wavivu, waoga au mabakhili. Hawa ni waumini lakini ni wapuuzaji, wadhaifu kwenye utashi wao na mbele ya nafsi zao zinazoamrisha sana uovu. Aina hii ya watu ndio wanaokusudiwa kwenye Aya hii.
Ni chukizo kubwa kwa Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda.
Na mwenye kuchukiwa na Mwenyezi Mungu ameanguka kwenye adhabu ya moto. Wafasiri wengi wamesema kuwa jamaa katika maswahaba walikuwa wakitamani kupigana kabla ya vita havijaanza, lakini vikija vita na kuwajibishiwa kupigana, basi wanakuwa wazito. Ndio ikashuka aya hii.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaopigana katika Njia yake kwa safu kama kwamba wao ni jengo lililojengwa kwa risasi.
Yaani lililojengwa kwa mpangilio na lililothabiti. Imenukuliwa kutoka kwa wanaaikolgia, kuwa wao wamegundua majengo ya zamani yaliyojengwa kwa madini ya risasi. Mwenyezi Mungu amesema akimsimulia Dhulqarnain:
آتُونِي أُفْرِغْ عَلَيْهِ قِطْرًا ﴿٩٦﴾
“Nileteeni shaba iliyoyeyuka nimwagie juu yake.” Juz. 16 (18:96).
Ziyada ya maneno ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapenda mshikamano wa watu katika kila lililo na heri na masilahi.
Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye tumwa kwenu?
Swali hili liko pamoja na jawabu lake. Kwa sababu Waisrail ndio wauaji wa manabii kwa nukuu ya kitabu chao kitakatifu; kama ilivyo katika Nehemia (9:26), inasema: “Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.”
Qur’an imesajili Aya kadhaa kuhusiana na kuuwa kwao manabii.
Kama muulizajai atauliza: hakuna chochote kinachojulisha kuwa Waisrail walimuudhi Nabii Musa, hasa kwakuwa alikuwa mwokozi na mhisani wao, nasi tutamjibu hivi: Maudhi ya Waisrail kwa Nabii Musa ni mengi; miongoni mwayo ni kumwambia: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu waziwazi, tufanyie Mungu kama wao walivyo na Mungu, hatuwezi kuvumilia chakula kimoja na mengineyo.
Walipopotoka, Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo zao.
Aya hii inaeleza waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hampotoi mtu mpaka apotoke yeye mwenyewe kwa uchaguzi wake mbaya, wala hamtwezi mtu na kumwangamiza ila akijiangamiza yeye mwenyewe na kujidharau. Aya hii haina tofauti na kauli ya anayesema: “ mwenye kuwa na tamaa ya haramu Mwenyezi Mungu humdhalilisha na kumfedhehsha, na mwenye kukinai na halali, Mwenyezi Mungu humtukuza na kumtajirisha.
Vile vile Aya hii ni tafsiri ya Aya zinazoonyesha kwa dhahiri kuwa Mwenyezi Mungu ndiye ampotezaye mtu; kama ile isemayo: “Humpoteza Mwenyezi Mungu amtakaye na humwongoza amtakaye.” Yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaka kumpoteza anayefuata njia ya upotevu na humwangamiza mwenye kujitia kwenye maangamizi yeye mwenyewe.
Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki maadamu wanang’ang’ania ufuska.
Na Isa bin Maryam aliposema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat, na mwenye kubashiria Mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad.
Aya ya pili katika maudhui haya inasema:
الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ ﴿١٥٧﴾
“Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili.” Juz. 9 (7:157)
Ya tatu inasema:
الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٤٦﴾
“Wale tuliowapa Kitabu wanamjua yeye kama wanavyowajua watoto wao. Na hakika kundi katika wao wanaificha haki na hali wanaijua. Juz. 2 (2:146)
Qur’an imeeleza waziwazi kuwa Tawrat ilyoteremshiwa Musa na Injili iliyoteremshiwa Isa, zimetoa bishara ya unabii wa Muhammad(s.a.w.w)
. Na imewakabili kwa hakika hii, ulama wa kiyahudi na kinaswara, na ikashindana nao, kupinga hilo. Lakini Historia haijataja yeyote katika hawa, aliyekana; bali wamethibitisha wale wachunga haki katika wao, wakakiri na wakasilimu; kama vile Abadallh bin Salaam na wengineo; ingawaje walikuwa ni maadui wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.
KUPOTOLEWA TAWRAT
Unaweza
kuuliza
: Mwislamu atamjibu nini Yahudi au Mkristo akisema: Qur’an yenu imesema kuwa Tawrat na Injil imetoa bishara ya Muhammad na hakuna athari yoyote ya bishara hii kwenye nakala ya Tawrat na Injil tuliyo nayo?
Jibu
: Atakayeuliza hivi, basi Mwislamu anatakiwa amjibu: Swali hili wamelijibu ulama wa kiyahudi na kinaswara wao wenyewe, pale walipokiri waziwazi kuwa Tawrat ya asili iliyoteremshwa kwa Musa imepotea na baada ya kupita miaka akaja mmoja akadai kuwa ameihifadhi moyoni na akaandika madai yake haya; kisha akasema: na iwe ni Tawrat ya Musa, basi ikawa. Hivyo hivyo ikatokea kwa Injil.
Jambo la kushangaza ni kuwa Injil ya Bwana Masih
, baada ya kupotea, yamezaliwa makumi ya Injil zaidi ya hamsini. Mnamo mwaka 325 walikongamana viongozi wa kikiristo na wakakubali injil nne, na hali Isa alikuwa na Injil moja tu, kama wanavyokubaliana manaswara wote. Ni nani basi aliyefanya moja kuwa nne? Lau wangelikubali tatu tungelisema kila mmoja katika watatu (baba mwana na roho mtakatifu) ana yake.
Kinachofahamisha zaidi kuwa Injil hii inatokana na watu wa kanisa, na sio na Masih, ni kuwa ilizuka baada ya kusulubiwa kwake, kuzikwa kwake na kupaa kwake mbinguni. Je alishukiwa na wahyi baada ya kusulubiwa na kuzikwa?
Ikiwa hilo linawezekana, je inawezekana katika hukumu ya kiakili na uhalisia kushukiwa na wahyi ulioandikwa kwenye Injil baada ya yeye kupaa mbinguni?
Swali la pili
: Je, kukiri huku kunapatikana wapi kwa ulama wa kiyahudi na kinaswara?
Jibu
: Kwenye vitabu vyao kadhaa vya kiarabu na vya lugha nyinginezo. Katika vya kiarabu ni Qamusul kitabulmuqaddas (Kamusi ya Kitabu kitakatifu), ambayo walishiriki wataalamu 27 kuitengeneza. Katika mada ya Yoshua, inasema: “Ni jambo lisilo na shaka kwamba sehemu kubwa ya kitabu kitakatifu iliharibiwa au ilikosekana wakati wa kumritadi Mwenyezi Mungu na vikwazo.” Katika mada ya Vitabu inasema: “Kuna rai inayosema kuwa walioongeza sifa ya kanuni ya agano la kale ni waandishi wenyewe wa kitabu, na rai nyingine inasema ni waandishi wanaosaidiwa na roho mtakatifu, wakiwemo viongozi wa kidini wa kiyahudi na wa kimasihi ambao walikubali kitabu hiki kwa kuongozwa na roho mtakatifu vile vile.”
Huku ni kukiri kusiko na shaka kwamba vitabu vya asili vimepotea na kwamba jamaa waliandika vitabu na kuongeza sifa ya utakatifu wao wenyewe. Na kauli nyingine ni kwa kuongozwa na roho mtakatifu. Tukichukua kauli ya kwanza au ya pili yote ni sawa, natija ni moja tu, kwamba wanakubali kuwa vitabu vilivyoko hivi sasa sio vitabu vya asili vya Musa na Isa; isipokuwa ni vitabu vipya vilivyoandikwa na wale wanaodai ni watakatifu au wanaodaiwa ni watakatifu kwa kupewa nguvu na roho mtakatifu.
Roho mtakatifu, kwao, ni roho wa Mungu katika wale watatu. Mwenyezi Mungu amemwita roho, kwa vile analeta uhai, na mtakatifu kwa vile anazitakasa roho za waumini.
Maulama wa Kiislamu wametunga makumi ya vitabu vinavyofahamisha kupotolewa Tawrat na Injil; miongoni mwavyo ni Idh-harulhaqq cha Sheikh Rahmatullah Al-Hindiy.
Ndani yake mna ushahidi 100 wa kuthibitisha upotofu wa Tawrat na Injil, kimatamshi na kimaana. Mwenye Tafsir Al-manar amemwashiria mwandishi huyu alipofasiri sura Annisa aya 46.
Vitabu vingine ni: Arrihlatulmadrasiya cha Sheikh Jawad Albalaghi, Muhammad rasulullah fi bisharatil-anbiya cha Muhammad Abdulghaffar, Muhammad hakadha basharat al-anajil cha Bushra Zachary Michael Kitabu cha mwisho kukisoma katika maudhui haya ni Bisharat walmuqaranat cha Sheikh Muhammad Assadiq Tehraniy, kilichotoka hivi karibuni. Kimejaa ushahidi mkataa kutoka kwenye vitabu vya kiyahudi na kinaswara, kuhusu kupotolewa Tawrat na Injil zilizoko hivi sasa.
Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhahiri!
Mayahudi hawakutosheka kumwambia Bwana Masih
kuwa ni mchawi, bali walithubutu kusema kuwa ni mtoto wa seremala; kama ilivyosemwa kwenya Injil ya Mathayo (13:55) na Injil Marko (6:3). ikinukuu kuwa Mayahudi walimtusi Bibi bikira kuwa alizini.
Lakini pamoja na yote hayo tunawaona wakirsto wengi wanaungana na uzayuni, ulio adui wa dini na utu, hasa kwa Bwana Masihi. Wanaungana dhidi ya Uislamu uliosema:
مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ﴿٧٥﴾
“Masih mwana wa Maryam hakuwa ila ni Mtume. Wamepita kabla yake Mitume, na mama yake ni mkweli.” Juz. 6 (5:75).
Hii inafahamisha tu kuwa umasihi, kwa wale wanaowasaidia waisrail, ni kiasi cha nembo tu ya makusudio mengine na kwamba dini yao na dhamiri zao ni kutawala na kuchokoza; sawa na uzayuni ulivyo.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ وَهُوَ يُدْعَىٰ إِلَى الْإِسْلَامِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٧﴾
7. Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
يُرِيدُونَ لِيُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَاللَّـهُ مُتِمُّ نُورِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٨﴾
8. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapokuwa makafiri watachukia.
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٩﴾
9. Yeye ndiye Aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina watachukia.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿١٠﴾
10. Enyi mlioamini! Je, niwajulishe biashara itakayowaokoa na adhabu iliyo chungu?
تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١﴾
11. Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.
يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٢﴾
12. Atawasamehe dhambi zenu, na atawatia katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.
وَأُخْرَىٰ تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِّنَ اللَّـهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٣﴾
13. Na kinginecho mkipendacho nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu na ushindi uliokaribu. Na wabashirieni Waumini!
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا أَنصَارَ اللَّـهِ كَمَا قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ لِلْحَوَارِيِّينَ مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنصَارُ اللَّـهِ فَآمَنَت طَّائِفَةٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ وَكَفَرَت طَّائِفَةٌ فَأَيَّدْنَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَىٰ عَدُوِّهِمْ فَأَصْبَحُوا ظَاهِرِينَ ﴿١٤﴾
14. Enyi mlioamini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Isa bin Maryam kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Ndipo tukawaunga mkono walioamini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.
MWENYEZI MUNGU ANAKAMILISHA NURU YAKE
Aya 7 – 14
MAANA
Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu?
Mtume(s.a.w.w)
aliwalingania watu wake watupilie mbali ushirikina na kumwamini Mwenyezi Mungu peke yake. Wakaona dhiki, wakampangia njama, wakatengenezea shaka juu yake na wakamzushia. Hivi ndivyo alivyo mbatilifu mwenye inadi, huwa anatengeneza uwongo na kuzua ubatilfiu kila anapolinganiwa kwenye haki; ni sawa mlinganiaji awe Nabii au la.Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu,
wale wanaomzushia Mwenyezi Mungu uwongo. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُم بِعَذَابٍ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ ﴿٦١﴾
“Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.” Juz. 16 (20:61).
Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapokuwa makafiri watachukia
Walijaribu kuumaliza Uislamu kwa uwongo na kusingizia, wakawa ni sawa na anayepingana na Mwenyezi Mungu katika ufalme wake. Mwenyezi Mungu hashindwi na jambo lake, lakini watu wengi hawajui.
Yeye ndiye Aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.
Makusudio ya Mtume hapa ni Muhammad(s.a.w.w)
. Uwongofu ni Qur’an na dini ya haki ni Uislamu. Aya hii na ile iliyo kabla yake zimepita kwa herufi zake katika Juz. 10 (32-33).
Enyi mlioamini! Je, niwajulishe biashara itakayowaokoa na adhabu iliyo chungu?
Dunia ni biashara ya kila mtu. Hakuna yeyote katika maisha haya ila anakusudia masilahi na faida katika matendo yake na matumizi yake. Lakini kuna masilahi mabaya; kama yule anayefanya kwa ajili ya umashuhuri na kurundika mali kwa njia yoyote ile. Masilahi mengine ni mazuri na ya heri; kama yule anayefanya kwa ajili ya haja yake na haja ya wengine.
Kwa kuwa faida ndio msukumo wa kwanza wa kufanya amali, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaonyesha waja wake biashara itakayowaokoa na ghadhabu na adhabu yake na kufuzu kwa kupata radhi na thawabu zake. Hakuna faida kama amani na kupata Pepo. Mwenyezi Mungu ameweka masharti ya kupata faida hii, kwa kauli yake:
Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu.
Hii ndio thamani ‧ imani isiyokuwa na shaka, kujitolea mhanga na kujitolea mali. Likishahakika hilo itatimia kandarasi na Mwenyezi Mungu. Na ninani mwenye kutekeleza ahadi zaidi kuliko Mwenyezi Mungu? Imesemwa katika Nahjulbalagha:“Hakuna thamani ya nafsi zenu isipokuwa Pepo, basi msiiuze ila kwenye hiyo.”
Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.
Kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kufuzu kupata thawabu zake ni bora kuliko nafsi, mali na watoto.
Atawasamehe dhambi zenu, na atawatia katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri katika Bustani za milele.
Huu ni ubainifu na ufafanuzi wa faida inayopatikana kutokana na biashara hii. Faida ya kwanza ni kughufiriwa dhambi. Hakuna uhuru zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kuwa huru na dhambi zake. Faida ya pili, ni makazi ya kudumu na neema ya milele.
Huko ndio kufuzu kukubwa
ambako hakuna kufuzu kwingine zaidi yake.Na kinginecho mkipendacho nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu na ushindi uliokaribu. Na wabashirieni Waumini!
Makusudio ya nusura hapa ni ushindi wa kuiteka Makka; kama inavyokuja haraka akilini. Maswahaba walikuwa wakitamani sana ushindi huu kutokana na adha waliyokuwa wakiipata kutoka kwa washirikina wa Makka. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia Mtume wake awabashirie ushindi huu na kuwa uko karibu, baada ya kuwabashiria maghufira na Pepo.
Enyi mlioamini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!
Maneno yanaelekezwa kwa mswahaba, Mwenyezi Mungu akiwaamuru, wawe na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
, kama vile walivyokuwa wanafunzi wa Isa kwa kauli na vitendo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:52). Katika kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa: “Yesu anaitwa Mnazareti (mnaswara)… jina hilo linarudia mji wa Nazareti (Naswiriy).
Ama masia (masih) ni msimbo wake. Ameitwa hivyo kwa kujitolea kwake. Waumini wake wameitwa wamasia mwaka 42 au 43. Mwanzoni jina hili lilikuwa ni tusi. Baina ya Isa na Musa kuna miaka si chini ya 1200 na si zaidi ya 1491. kwa sababu wanahistoria wana kauli nyingi juu ya hilo.
Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Ndipo tukawaunga mkono walioamini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.
Makusudio ya kushinda hapa ni kushinda kwa hoja na dalili. Maana ni kuwa wana wa Israil walitofautiana kuhusiana na Isa akiwa anatokana na wao. Kuna waliosema ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wengine wakasema ni Mungu na mayahudi wakasema ni mchawi na mtoto wa zina. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawapa nguvu waliosema ni Mtume wa Mwenyezi Mungu dhidi ya wale waliosema ni Mungu.
Katika Waraka wa Yohana imeelezwa kuwa, aliye dhidi ya Masih ni yule anayekana kuwa na mwili na kuungana umungu wa masih na ubinadamu wake. Ama Qur’an inasema kuwa maadui wa Masih ni wale waliozama sana kuhusu yeye na waliosema dhidi yake.
MWISHO WA SURA YA SITINI NA MOJA: SURAT AS – SAFF