11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sitini Na Tano: Suarat At-Talaq. Imeshuka Madina. Ina Aya 12.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu.
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ وَاتَّقُوا اللَّـهَ رَبَّكُمْ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ لَا تَدْرِي لَعَلَّ اللَّـهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَٰلِكَ أَمْرًا ﴿١﴾
1. Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao, na fanyeni hisabu ya eda, na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu msiikiuke; na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake Hujui; pengine Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya.
فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَأَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّـهِ ذَٰلِكُمْ يُوعَظُ بِهِ مَن كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا ﴿٢﴾
2. Basi wanapofikia muda wao, muwashike kwa wema, au farakianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyoagizwa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا ﴿٣﴾
3. Na humruzuku kwa upande asiotazamia. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu amejaalia kila kitu na kipimo chake.
وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا ﴿٤﴾
4. Na wale waliokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayoshaka, basi eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao hawakupata hedhi. Na wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa. Na anayemcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake
kuwa mepesi.
ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُعْظِمْ لَهُ أَجْرًا ﴿٥﴾
5. Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amewateremshia. Na anayemcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.
TALAKA KWA WAKATI WA EDA
Aya 1 – 5
MAANA
Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amewateremshia. Na anayemcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.
Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja hukumu za talaka, kama ifuatavyo:
1.Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.
w
)
, lakini wanakusdiwa wenye kukalifiwa na sharia wote. Kwa sababu sharia inawahusu wote.
Maana ni kuwa mwislamu akitaka kumpa talaka mkewe, anatakikana angoje wakati mnasaba wa kuingia kwenye eda; kiasi amabacho wakati wa talaka utakuwa ni sehemu ya eda. Madhehebu yote ya kiislamu yamekongamana kwenye hilo.
Lakini Sunni wanasema uharamu huu hauharibu talaka kwa kukosekana sharti hilo; bali talaka itakuwa sahihi na mtaliki atapata dhambi.
Shia Imamiya wamesema talaka itakuwa ni upuzi tu, kwa sababu liliokatazwa ni tendo; sawa na kukatazwa kuuza pombe, lengo lake ni kukataza tendo lenyewe sio kukataza tamko lake.
Miongoni mwa waliyoyatolea dalili Shia ni yaliyoelezwa kwenye Sahih Bukhar na Sahii Muslim kwamba Ibn Umar alimpa talaka mkewe akiwa katika hedhi, basi Umar akamuuliza Mtume(s.a.w.
w
)
kuhusu hilo, akasema Mtume: Mwamrishe amrejee, kisha amwache mpaka atwaharike kisha aingie hedhini tena atwaharike. Hapo sasa akipenda ataamzuia na akipenda atampa talaka kabla ya kumgusa. Hiyo ndio eda alioyoiamuru Mwenyezi Mungu Mtukufu apewe talaka kwayo.
Kauli yake Mtume(s.a.w.
w
)
“Akitaka amzuie na akitaka amwache kabla ya kumgusa,” ni ubainifu na tafsiri ya kauli yake: “Amrejee.” Kwamba yaani bado ni mkewe, kwa hiyo amzuie kwa hali yoyote ile wala hakuna hiyari isipokuwa akimpa talaka kwa masharti yake.
Haya ndio maana ya amrejee. Si sahihi kuwa hiyo ni amri ya kumrejea kitalaka; kama walivyosema wanafiqh wa madhehebu mengine. Kwa sababu kumrejea kwa talaka ni kumzuia mke ambako ni natija ya kauli yake ‘Na amrejee!’ na kimsigi jambo haliwezi kuwa hilo lenyewe ndio natija.
Zaidi ya hayo kurejea kwa talaka hakuondoi dhambi iliyotangulia ili kuamruwe na Mtume(s.a.w.
w
)
. Madhehbu yote yameafikiana kwa kauli moja kuwa mke ambaye hajaingiliwa na mumewe anaweza kuachika hata akiwa kwenye hedhi, kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Kwa eda yao, na asiyeingiliwa hana eda kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Enyi ambao mmeamini! Mkiwaoa wanawake waumini kisha mkawaacha kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayoihisabu.” Juz. 22 (33:49).
2.Na fanyeni hisabu ya eda.
Mjue mwanzo wa eda na mwisho wake, kwa sababu ina hukumu zinazohusiana nayo; kama posho ya aliye kwenye eda, haki ya kurejelewa ikiwa ni talaka rejea, haki yake ya kurudia alichokitoa, ikiwa ni talaka ya kujivua (Khul’u), uharamu wa kuolewa mpaka amalize eda na mengineyo waliyoyataja wana fiqh katika vitabu vyao…
Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu katika yale aliyowawajibishia katika hukumu za eda.
3.Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe.
Makusudio ya nyumba zao ni nyumba wanazokaa, sio nyumba za kumiliki; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na kaeni majumbani mwenu…Na kumbukeni yanayosomwa majumbani mwenu” Juz. 22 (33:33-34).
Wameafikiana mafaqihi kuwa mwenye kuachwa talaka rejea anastahki posho, pamoja na makazi muda ule atakaokaa eda. Wametofautiana katika posho ya aliyeachwa talaka baini.
Hanafi wamesema anastahiki posho, awe ana mimba au la. Malik akasema akiwa hana mimba anastahiki makazi tu na akiwa na mimba basi anastahiki posho kamili. Shafii, Shia Imamiya na Hambali wamesema hana posho akiwa hana mimba, lakini akiwa nayo basi anastahiki posho.
Ikiwa wajibu posho basi ni wajibu kwa mtalikiwa kubakia kwenye nyumba aliyotalikiwa mpaka uishe muda wa eda na ni haramu kutoka au kumtoa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: ‘Wasitoke …. Wala msiwatoe.’Ila wakifanya uchafu ulio wazi
; yaani utakaothibitika kisharia.
Wameafikiana kwamba zina ni uchafu unapelekea kutolewa nyumbani. Lakini wametofautina katika isiyokuwa zina. Tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ya uchafu hapa, (Fahisha), ni zina tu, kwa sababu neno hili likinasibishwa kwa wanawake basi fahamu inayokuja haraka akilini ni zina.
Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu msiikiuke.
Yaani masharti ya talaka na hukumu za eda. Nazo ni hukumu za Mwenyezi Mungu na mipaka yake aliyoibainisha katika Kitabu chake na kupitia kwa Mtume wake.
Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake
, kwa sababu ameipeleka kwenye ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Aya nyingine inasema:
وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾
“Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akapetuka mipaka yake, atamtia katika moto; ni mwenye kudumu humo, na atapata adhabu idhalilishayo.” Juz. 4 (4:14).
Hujui; pengine Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya.
Hujui wewe mtaliki labda Mwenyezi Mungu anaweza kuunganisha nyoyo mbili zilizotengana na mambo yakarudi kama zamani. Hapa kuna ishara kwamba nyoyo zina wakati, na inatikakana mtu asiseme jambo kuwa nitalifanya kesho ila kwa kusema inshallah. Ndio maana Imam Ali
akasema:“Nimemjua Mwenyezi Mungu kwa kuvurugika maazimio.’
Yaani kuharibika maazimio ni dalili wazi kuwa kwenye mipango ya mtu kuna mipango ya juu na yenye nguvu zaidi.
4.Basi wanapofikia muda wao, muwashike kwa wema, au farakianeni nao kwa wema.
Ikiwa muda wa eda unakurubia kwisha basi, mtaliki ana hiyari, akitaka atabadilisha azma yake na kumrudisha mtalikiwa kwenye hifadhi yake na akipenda atabakia kwenye hukumu ya kufarikiana na kukatika mfungamano baina yao. katika hali zote mbili anatakikana asimdhuru mke, bali amtekelezee haki yake kwa ukamilifu. Haya ndio makusudio ya kumweka kwa wema au kufarikiana naye kwa wema. Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:231).
Mtalikiwa anaweza kuwa amekoma kutoka hedhi, ana mimba au hana mimba. Kuhusu wawili wa mwanzo maelezo yao yatakuja.
Ama muda wa eda ya asiyekuwa na mimba ni twahara tatu zikiwa ni pamoja na ile aliyepewa talaka. Hii ni kwa Shia Imamiya, Malik na Shafii. Ama kwa Hanafi na Hambali eda yake ni hedhi tatu. Tazama Juz. 2 (2:228).
5.Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu.
Mafaqihi wa madhehebu wameafikana kuweko ushahidi wa waadilifu wawili kwa mujibu wa Aya hii, lakini wakatofautiana ushahidi uwe kwenye nini? Kwenye kurejea au kwenye talaka? Mafakihi wa kisunni wamesema, unazingatiwa kwenye kurejea, lakini wengine wakasema ni wajib; kama Shafii na wengine wakasema ni sunna; kama Hanafi.
Shia imamiya wanasema kuwa si wajibu ushahidi kwenye kurejea, isipokuwa kwenye talaka. Dkt. Muhammad Yusuf Musa, mhadhiri na raisi wa kitengo cha shariya ya Kiislamu, kitivo cha haki katika chuo Kikuu cha Azhar, anasema katika kitabu chake: Al-ahawalu shakhsiyya Uk. 271, chapa ya 1958:
Shia Imammiya wanaona kuwa miongoni mwa masharti muhimu ya talaka ni kuhudhuria mashahidi wawili waadilifu, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu.”
Na katika hilo anasema mmoja wa ulama wao: Hii ni nyenzo nzuri zaidi ya muungano wa wanandoa, kwa sababu watu wema wana athari katika nafsi kuweza kutuliza mawimbi yawe sawa. Ikiwa nasaha zao hazitafaulu, lakini angalau talaka zitapungua kwa kuweko sharti la waadilifu wawili.” Dkt. anaongeza kusema: “Hili halitakikani kufumbiwa macho. Kwa kweli kuichukua rai hii kutaandaa njia ya kutengenea mambo mengi.”
Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Maneno yanaelekezwa kwa mashahidi. Maana ni kuwa msigeuze kitu katika ushahidi, bali utekelezeni kwa njia yake kwa kukusudia kuithibitisha haki, sio kuwaridhisha au kukomoa wanaoshudiliwa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:283).
Hivyo ndivyo anavyoagizwa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Ukweli ni kuwa wanaonufaika na ubainifu wa Mwenyezi Mungu na kutumia hukumu zake ni wale wanaomcha Mungu. Lakini wale wasioamini isipokuwa nafsi zao na masilahi yao, hao ni kama wanyama, hamu yao ni matumbo yao na moto ndio makazi yao.
Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.
kwenye haramu yake kwenda kwenye halali yake na kwenye maasi yake kwenda kwenye twaa yake na humtoshea na kuhitajia wengine,na hum
ruzuku kwa upande asiotazamia.
Tunavyofahamu kutokana na Aya hii ni kuwa riziki haina udhibiti maalumu wala kiasi. Inaweza ikaja bila ya kutazamia na inaweza kuondoka bila ya kutazamia. Kuna matukio mangapi mazuri yanamtokea mtu bila ya kutarajia na kuyapanga na ni matukio mangapi mabaya ya kuumiza, yasiyotazamiwa kutokea, yanatokea? Hakuna shaka kuwa baadhi yanatokea kwa kupuuza na mengine ni kwa mipangilio ya mpangiliaji wa viumbe.
Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha.
Kumtegemea Mwenyezi Mungu ni kuchukua desturi yake ya kufanyakazi na kuhangaika kwa kufuata nyenzo: “Basi tembeeni katika pande zake na kuleni katika riziki zake.” (67:15).
Na Hadith inasema:“Tia akili na utawakali.”
Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake
. Analolitaka linakuwa na asilolitaka haliwi.
Mwenyezi Mungu amejaalia kila kitu na kipimo chake
, hakuna mchezo, wala vurugu au sadfa. Katika Aya nyingine anasema: “Na ameumba kila kitu na akikadiria kipimo.” Juz. 18 (25:2). Pia amesema: “Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.” Juz. 13 (13:8).
6.Na wale waliokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayoshaka, basi eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao hawakupata hedhi.
Mafaqihi wa kisunni wametofautiana sana kuhusiana na umri wa kukoma hedhi; kiasi cha kufikia mgongano na kutatizika. Kuna aliyesema ni miaka 50, mwingine akasema ni 55, watatu akasema ni 60, wanne akasema ni 62,watano akatofautisha baina ya wanawake waarabu na wasiokuwa waarabu akasema kuwa waarabu wana nguvu kimaumbile na wa sita akasema, kila mwanamke ataangalia desturi ya ukoo wake. Na wengi katika wao wamenyamaza hawakuweka kiwango cha mwaka wa kukoma hedhi.
Vile vile wametofautiana katika neno ‘ikiwa mnayo shaka.’ Mmoja akasema ni kutia shaka katika hukumu ya eda si katika hali ya mwanamke na kufikia kwake mwaka wa kukoma hedhi. Wengine wakaseam makusudio ni kutia shaka katika hali ya mwanamke na kukoma kwake.
Ama Shia wamesema: Mwaka wa kukoma hedhi kwa mkuraishi ni miaka 60 na kwa asiyekuwa mkuraishi ni miaka 50, wakitegemea riwaya za Ahlulbayt.
Vile vile wamesema kiwango cha chini kuweza kutoka hedhi ni miaka 9. Hii inaafikiana na yaliyoelezwa kwenye kitabu Almughni cha Ibn Quddama, katika sunni: “Uchache wa umri wa kupata hedhi ni miaka 9, kwa sababu marejeo katika hilo ni kupatikana, na amepatikana aliyetoka hedhi katika umri wa miaka 9. Na imepokewa kutoka kwa Shafii kwamba yeye alimuona mwanamke mwenye wajukuu akiwa na miaka 21.”
Nimesoma katika gazeti kuwa kuna msichana aliyepata hedhi kabla ya miaka9.
Wametofautiana Sunni na Shia katika kufasiri Aya hii. Mafaqihi wa kisunni wakasema kuwa makusudio ya waliokoma kupata hedhi ni waliokatikiwa na hedhi kwa sababu ya umri wao mkubwa, na ambao hawakupata hedhi ni wale ambao hawajapata hedhi kwa sababu ya umri wao mdogo. Wote hawa eda yao ni miezi mitatu, wakiwa wameingiliwa na waume zao.
Hii inaafikiana na baadhi ya mafaqihi wakubwa katika Shia imamiya; kama vile Sayyid Almurtadha, Ibn Zuhra, Ibn Samaa na Ibn Shahr Shub. Hata hivyo wengi katika Shia imamiya, wamesema kuwa makusudio ya waliokoma kupata hedhi ni wanaotiliwa shaka kuwa hedhi yao imekatika kwa umri au kwa jambo jingine.
Na wakafasiri kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ikiwa mnayo shaka,” kuwa ni kutia shaka katika hali yao. Ama makusudio ya ambao hawakupata hedhi ni wale walio katika umri wa hedhi, lakini hawapati hedhi kwa sababu nyingine isiyokuwa ya umri mdogo au mkubwa. Wote hawa eda yao ni miezi mitatu. Wametegemea riwaya za Ahlu bayt katika hilo. Kwa hiyo basi Aya haikuelezea eda ya aliyekoma kutoka hedhi kwa umri mkubwa; si kwa kichanya wala kihasi
Na wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa.
Mafaqihi wa kisuni na kishia wameafikiana kuwa eda ya mtalikiwa mwenye mimba ni mpaka azae, wakatofautiana katika eda ya aliyefiwa na mumewe akiwa na mimba. Sunni wamesema ni sawa na eda ya mtalikiwa inamalizika kwa kuzaa.
Shia wanasema ataangalia muda utakaorefuka zaidi baina ya kuzaa na miezi mine na siku kumi (yaani akizaa kabla ya miezi mine na siku kumi basi atangoja hadi muda huo uishe). Kwa kuchukulia Aya hii na ile isemayo: “Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake (hao wake) wangoje miezi minne na siku kumi.” Juz. 2 (2:234). Huko tumefafanua zaidi.
Na anayemcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi.
Huu ni mfano wa Aya ya 2 na 3 ya Sura hii tuliyo nayo. Hatujui lengo la kukaririka huku isipokuwa kuzidi kuhimiza takua. Kwamba kule kumekuja kuhimiza baada ya amri ya kusimamisha ushahidi kwa njia yake. Hapa kumekuja baada ya kubainisha eda ya aliyekoma na mwenye mimba.
Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amewateremshia. Na anayemcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.
Manufaa ya takua hayana idadi; mingoni mwayo ni aliyoyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya hizi; kama ifuatavyo:-kutoka katika dhiki ya dunia na Akhera, riziki bila ya kutazamia, nusra na kinga kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kuwa mepesi mambo na kufutiwa maovu. Fauka ya yote ni ziada ya malipo. Lakini
أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ أَوْ تَهْدِي الْعُمْيَ وَمَن كَانَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٤٠﴾
“Je, unaweza kumsikilizisha kiziwi, au kumwongoza kipofu na aliyemo katika upotofu ulio wazi?” Juz. 25 (43:40).