TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 27988
Pakua: 4503


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 27988 / Pakua: 4503
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sitini Na Sita: Surat At –Tahrim. Imeshuka Madina. Ina Aya 12.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١﴾

1. Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha alichokuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta radhi za wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

قَدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ وَاللَّـهُ مَوْلَاكُمْ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

2. Hakika Mwenyezi Mungu amewapa Sharia ya kufungua viapo vyenu. na Mwenyezi Mungu ni Mola wenu. Na Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

وَإِذْ أَسَرَّ النَّبِيُّ إِلَىٰ بَعْضِ أَزْوَاجِهِ حَدِيثًا فَلَمَّا نَبَّأَتْ بِهِ وَأَظْهَرَهُ اللَّـهُ عَلَيْهِ عَرَّفَ بَعْضَهُ وَأَعْرَضَ عَن بَعْضٍ فَلَمَّا نَبَّأَهَا بِهِ قَالَتْ مَنْ أَنبَأَكَ هَـٰذَا قَالَ نَبَّأَنِيَ الْعَلِيمُ الْخَبِيرُ ﴿٣﴾

3. Na Nabii alipomwambia mmoja wa wake zake jambo la siri. Basi alipolitangaza yule mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjulisha sehemu na akaacha sehemu nyengine. Alipomwambia hayo, huyo mke akasema: Nani aliyek­wambia haya? Mtume akase­ma: Kaniambia Mjuzi Mwenye habari!

إِن تَتُوبَا إِلَى اللَّـهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ ﴿٤﴾

4. Kama nyinyi wawili mtatubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwishaelekea kwenye haki. Na mkisaidiana dhidi yake Mtume, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wake, na Jibrili, na waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia.

عَسَىٰ رَبُّهُ إِن طَلَّقَكُنَّ أَن يُبْدِلَهُ أَزْوَاجًا خَيْرًا مِّنكُنَّ مُسْلِمَاتٍ مُّؤْمِنَاتٍ قَانِتَاتٍ تَائِبَاتٍ عَابِدَاتٍ سَائِحَاتٍ ثَيِّبَاتٍ وَأَبْكَارًا ﴿٥﴾

5. Akiwapa talaka, asaa Mola wake akampa wake wengine badala yenu nyinyi, walio bora kuliko nyinyi, wanyenyekevu, waumini, watiifu, walio tubu, wenye kushika ibada, wafanyao kheri, wajane na wanawali.

KWA NINI UNAHARIMISHA ALICHOKUHALILISHIA MWENYEZI MUNGU?

Aya 1 - 5

KISA KWA UFUPI

Wametofautiana wafasiri na wapokezi wa Hadith kuhusu sababu ya kushu­ka Aya hizi. Kwenye Sahih Bukhar na Sahihu Muslim, kuna Hadith iliy­opokewa kutoka kwa Aisha, amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alikuwa akipenda haluwa na asali. Siku moja akanywa asali kwa mkewe Zaynab bint Jahsh. Tukakubaliana mimi na Hafsa, kuwa akiingia kwa mmoja wetu amwambie: Nasikia harufu ya mughafiri[3] .”

Na ikawa hivyo. basi Mtume akasema:“hapana nimekunywa asali kwa Zaynab na sitarudia tena kunywa, lakini usimwambie mtu.”

Katika tafsiri ya Sheikh Al-Maraghi ni kuwa Mtume(s.a.w.w) aliingia kwa Hafsa, kisha akamjulisha Aisha pamoja na kuwa Mtume alimwambia iwe siri. Sheikh anaendelea kusema: Aisha na Hafsa walikuwa wakielewana kuwa dhidi ya wake wengine wa Mtume(s.a.w.w) .

Vyovyote inavyosemwa kuhusu sababu za kushuka Aya hizi, ni kuwa dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Mtume(s.a.w.w) alijizuia kutumia kitu alichohalalishiwa na Mwenyezi Mungu kutokana na sababu fulani. Na kwamba hilo alilifanya siri na mmoja wa wakeze na kumwamuru asilidhihirishe, lakini mke akakhalifu na kulitoa. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamnasihi Nabii wake kutojinyima alivyohalalishiwa na Mwenyezi Mungu na akawakemea wakeze wasiosikiliza amri yake.

MAANA

Ewe Nabii! Kwa nini unaharamisha alichokuhalalishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta radhi za wake zako.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) . Makusudio ya uharamu hapa ni kiasi cha kujizuila tu kuacha halali kwa kumridhisha mwingine; kama vile kuacha kuvuta sigara kwa sababu ya kumridhisha mke ambaye anachukia hilo.

Kwa hiyo makusudio hapa sio kuharamisha kisharia. Ni muhali hilo. Vipi iwe hivyo na Kitabu cha Mwenyezi Mungu alichokiteremsha katika moyo wa Muhammad(s.a.w.w) kinasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحَرِّمُوا طَيِّبَاتِ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٨٧﴾

“Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” Juz. 7 (5:87).

Anasema tena;

قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ لَكُم مِّن رِّزْقٍ فَجَعَلْتُم مِّنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّـهُ أَذِنَ لَكُمْ أَمْ عَلَى اللَّـهِ تَفْتَرُونَ ﴿٥٩﴾

“Sema: Je, mwaonaje zile riziki alizowateremshia Mwenyezi Mungu, kisha mkafanya katika hizo nyingine haramu na nyingine halali? Sema: Je, Mwenyezi Mungu amewaruhusu au mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo?” Juz.11 (10:59).

Inasemekana kitu alichojiharamishia ni asali na kwamba alikusudia kum­ridhisha mkewe Hafsa kwa sababu aliona vibaya kunywa asali kwa mkewe Zaynab bint Jahsh. Basi moyo wa Hafsa ukafurahi kwa hilo

Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Msamaha na maghufira haumaanishi kuwa kuna dhambi. Mara nyingi inakuwa ni ibara ya thawabu zake na rehema zake. Manabii walikuwa wakiomba msamaha na maghufira kwa Mwenyezi Mungu; mfano: “Juz. 10: (9:43).

Hakika Mwenyezi Mungu amewapa Sharia ya kufungua viapo vyenu.

Inasemekana kuwa Mtume(s.a.w.w) aliapa kuacha kitu alichohalalishiwa na Mwenyezi Mungu, ndio akamwamuru aache kiapo chake na atoe kafara.

Tuonavyo sisi - Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi - ni kuwa Mtume(s.a.w.w) hakuapa, lakini aliahidi kuacha; na ahadi ya maasumu ni wajibu kuitekeleza kwa hali yoyote itakavyokua, ni sawa aliloliahidi liwe ni sunna au halali. Kwa sababu ahadi yake ina nguvu na ni kubwa zaidi kuliko kiapo cha mwingine. Kwa hiyo inafaa kuitwa kiapo.

Na Mwenyezi Mungu ni Mola wenu. Na Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.

Mwenyezi Mungu ndiye mtawala wa mambo ya Nabii na waumini, ndiye anayewanusuru dhidi ya wanaotaka kuwafanyia njama na anajua hikima aliyoifanyia shariya ya hukumu ya viapo na mengineyo.

Na Nabii alipomwambia mmoja wa wake zake jambo la siri.

Hii inafahamisha kuwa Nabii ni mtu kama watu wengine; anafanya siri na wake zake kama wafanyavyo siri watu wengine. Hatofautiani nao isipokuwa kwa kushukiwa na wahyi, na umaasumu unakuwa katika aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu na kila mambo ya aibu. Tazama Juz. 16 (20-17) kifungu cha ‘Hakika ya utume.’

Basi alipolitangaza yule mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjulisha sehemu na akaacha sehemu nyengine.

Yaani baada ya yule kulitangaza lile aliloambiwa aliweke ni siri, Mwenyezi Mungu alimjulisha Mtume wake mtukufu, naye Mtume akamwambia yule mke baadhi ya mambo aliyoyafichua. Hakumwambia yote kwa kumhurumia. Hapa kuna ishara kuwa huyo alipituka mipaka ya kufichua mambo ya siri.

Alipomwambia hayo, huyo mke akasema: Nani aliyekwambia haya? Mke alimuuuliza Mtume amepata wapi habari hizo,Mtume akasema: Kaniambia Mjuzi Mwenye habari! Ambaye anajua hiyana ya macho na yanayofichwa na vifua.

Kama nyinyi wawili mtatubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwishaelekea kwenye haki.Na mkisaidiana dhidi yake Mtume,basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia.

Dhamiri ya nyinyi wawili inamrudia Aisha na Hafsa; kama ilivyoandikwa katika vitabu vya Tafsiri na Hadith. Tutaonyesha vine; viwili vikiwa vya tafsir na viwili vya Hadith:

Kwenye Tafsir Attabari kuna maelezo haya, ninanukuu: “Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Na mkisaidiaana dhidi yake , ni yule aliyepewa siri na Mtume(s.a.w.w ) na yule aliyemfichulia siri hiyo, ambao ni Hafsa na Aisha. Watu wa taawili wamesema kama tulivyosema sisi.”

Razi naye akasema: ninamnukuu: “Kama nyinyi wawili mkitubia,” maneno yanaelekezwa kwa Aisha na Hafsa. Bukhari anasema katika Sahih yake Juz. 6 kwa anuani ya ‘Sura Attahrim.” Ibn Abbas alimuuliza Umar Bin Al-khattab: Ni nani hao wawili waliosaidiana dhidi ya Mtume(s.a.w.w) katika wake zake? Akasema: hao ni Hafsa na Aisha. Na mfano wake katika sehemu ya pili ya Juzuu ya pili ya Sahih Muslim kwa anuani ‘Mlango wa kuapa na kujitenga na wanawake.’

Kuna swali pia kuhusu neno ‘Kama nyinyi wawili mkitubia,’ amesema Muslim: Ibn Abbas alimuuliza Umar: Ni nani hao wake wawili katika wakeze Mtume(s.a.w.w) ambao wameambiwa; kama mkitubia? Akasema Umar: ‘’Ni Hafsa na Aisha.’’

Maana ya Aya ni kuwa Aisha na Hafsa walisaidiana dhidi ya Mtume(s.a.w.w) na wakafichua siri yake pamoja na kutaka isitolewe, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawamuru kutubia kosa hili. Kwamba wakitubuia na kutengemaa, basi nyoyo zao zitakuwa zimeelekea kwa Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlas, lakini kama waking’ang’ania kusaidiana dhidi ya Mtume, basi Mwenyezi Mungu atamlinda. Vile vile Jibril, malaika wote, waumini na watu wema.

Unaweza kuuliza : Kwa nini vitisho vyote. kwani Aisha na Hafsa wana nini mpaka wachanganyiwe nguvu ya Mwenyezi Mungu, nguvu ya Jibril pamoja na malaika wengine na walio wema katika waumini?

Jibu : Aisha na Hafsa sio wanaokusudiwa kuhusishwa wao tu na makemeo haya; isipokuwa makusudio kwanza ni kueleza cheo na heshima ya Mtume; kisha kuwafahamisha wote akiwemo Hafsa na Aisha na kila mwenye kumdhamiria kumfanyia ubaya Nabii(s.a.w.w) , kuwa Nabii(s.a.w.w) yuko kwenye ngome imara ya nguvu ya Mwenyezi Mungu, malaika na mawalii wake.

Akiwapa talaka, asaa Mola wake akampa wake wengine badala yenu nyinyi, walio bora kuliko nyinyi, wanyenyekevu, waumini, watiifu, walio tubu, wenye kushika ibada, wafanyao kheri, wajane na wanawali.

Ni jambo gani mnalojidai nalo enyi wake wa Mtume mpaka mkawa dhidi yake? Je, umewahadaa uzuri wenu, dini yenu, utiifu wenu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake au ni kwa nini?

Basi na ajue kila mmoja wenu kwamba lau Mtume(s.a.w.w) atawapa talaka nyote, basi Mwenyezi Mungu atambadilishia walio bora kuliko nyinyi kwa uzuri, ukamilifu, dini na ikhlasi; tena akipenda wajane akitaka au bikra au wote.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٦﴾

6. Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu. Hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَعْتَذِرُوا الْيَوْمَ إِنَّمَا تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٧﴾

7. Enyi mliokufuru! Msilete udhuru leo. Hakika tu mnalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٨﴾

8. Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli! Asaa Mola wenu akawafutia maovu yenu na akawaingiza katika Pepo zipitiwazo na mito chini yake. Siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii. Na walioamini pamoja naye, nuru yao inakwenda mbele yao na kuumeni, na huku wanasema: Mola wetu! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٩﴾

9. Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na uwawekee ngumu! Na makazi yao ni Jahannamu. Na hayo ni marejeo mabaya.

KUNI ZAKE NI WATU NA MAWE

Aya 6 – 9

MAANA

Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe.

Makusudio ya mawe ni masanamu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtafika.” Juz. 17 (21:98).

Maana ni ikiwa mumin anahisi majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa anayoyasema na anayoyafanya na kuhofia ghadhabu yake na adhabu yake, basi ni juu yake kuona kuwa ana jukumu kwa watu wake na watoto wake na kwamba ni wajibu wake kunyoosha mkono wake kwa kazi kwa ajili ya masilahi yao na kunyooka kwao.

Ikiwa baba anafanya kila awezalo kwa ajili ya watoto wake kwa ajili ya mustakbali wao katika maisha haya yanayoisha, basi ingekuwa bora kwake kufanya bidii kwa ajili ya wema wao katika maisha yanayobakia na kuwakinga na jambo kubwa zaidi kuliko misukosuko yote. Lakini baba atafanya nini katika kizazi hiki ambacho kinawataka wazazi wawanyenye­kee watoto?

Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu ya ukakamavu kwa wasiokuwa na maana waliopituka mipaka na kufanya uovu duniani kwa waja wa Mwenyezi Mungu.

Hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa.

Yaani hao malaika wakali, wanaharakisha kumtii Mwenyezi Mungu bila ya kusita, naye anawaambia kwa kila muovu mwenye dhambi:

خُذُوهُ فَغُلُّوهُ ﴿٣٠﴾

“Mshikeni na mumtie pingu.” (69:30).

Enyi mliokufuru! Msilete udhuru leo. Hakika tu mnalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

Siku hii ya leo ni siku ya hisabu na malipo ya matendo, sio siku ya toba na kutoa udhuru. Watatubia kitu gani wale ambao viwanda vyao vinafanyakazi usiku na mchana kutengeneza mauti na kuboa?

Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli! Asaa Mola wenu akawafutia maovu yenu na akawaingiza katika Pepo zipi­tiwazo na mito chini yake.

Asaa ikitoka kwa Mwenyezi Mungu basi maana yake ni kuwa tu. Toba ya kweli ni ile ya kujing’oa kabisa kwenye uovu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke Yake. Nayo iko wazi kwa kila mwenye kufanya madhambi na akaasi. Vile vile ni wema mkubwa unaofuta yaliyo maovu yaliyo kabla yake na inaleta thawabu za Mwenyezi Mungu na Pepo yake.

Siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii.

Hii ni kuwapinga maadui wa Nabii, kwamba wao ndio watakaodhalilika duniani na Akhera; vinginevyo ni nani anayefikiria kuwa Mwenyezi Mungu atamdahalilisha Muhammad(s.a.w.w) siku ya Kiyama, na yeye maisha yake duniani yalikuwa ni rehema kwa viumbe wote?

Na walioamini pamoja naye, nuru yao inakwenda mbele yao na kuumeni, na huku wanasema: Mola wetu! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Umetangulia mfano wake katika Juz.27 (57:12).

Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na uwawekee ngumu! Na makazi yao ni Jahannamu. Na hayo ni marejeo mabaya.

Kabisa! Hakuna upole wala huruma kwa mataghuti, wala hakuna cha kuwafanyia mbele ya haki na uadilifu isipokuwa upanga. Ni sharia gani au kanuni gani inayohurumia na kuwapuuza wanaodharau maisha ya watu na kueneza hofu nyoyoni mwao, huku wakisema: asiyekuwa pamoja na sisi na kuwa mtumwa wetu basi huyo ni adui yetu naye hatapata kutoka kwetu isipokuwa silaha za maangamizi?

Hapo huruma na upole itakuwa ni kuuumaliza uadui na watu wake. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma katika moto wake kama alivyo na huruma katika Pepo yake.

ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ كَفَرُوا امْرَأَتَ نُوحٍ وَامْرَأَتَ لُوطٍ كَانَتَا تَحْتَ عَبْدَيْنِ مِنْ عِبَادِنَا صَالِحَيْنِ فَخَانَتَاهُمَا فَلَمْ يُغْنِيَا عَنْهُمَا مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا وَقِيلَ ادْخُلَا النَّارَ مَعَ الدَّاخِلِينَ ﴿١٠﴾

10. Mwenyezi Mungu amewapi­gia mfano waliokufuru-mke wa Nuhu na mke wa Luti. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini wakawafanyia hiyana, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoja na wanaoingia!

وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿١١﴾

11. Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walioamini mke wa Firauni, aliposema: Mola wangu! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhalimu.

وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا وَصَدَّقَتْ بِكَلِمَاتِ رَبِّهَا وَكُتُبِهِ وَكَانَتْ مِنَ الْقَانِتِينَ ﴿١٢﴾

12. Na Maryam binti Imrani, aliyeilinda tupu yake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa watiifu.

MKE WA NUH NA MKE WA LUT

Aya 10 – 12

MAANA

Mwenyezi Mungu amewapigia mfano waliokufuru-mke wa Nuhu na mke wa Luti. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini wakawafanyia hiyana, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoja na wanaoingia!

Hakuna tofauti baina ya mwanamume na mwanamke kiasili na kimajukumu. Kila mmoja ni sehemu ya mwingine. Kila mmoja hawezi kujitosha peke yake. Kuna wanaume wema na waovu na kuna wanawake wema na waovu.

Aya iko mbali kabisa na kutofautisha baina ya mwanamke na mwanamume. Imepigia mfano mwanamke kwa sababu tu ya kuwaonyesha baadhi ya mama wa waumin waliokuwa dhidi ya Mtume(s.a.w.w) ; kama ilivyokuja katika Aya ya nne ya Sura hii tuliyo nayo.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa baadhi ya wakeze walikuwa dhidi yake, na kuwakemea, sasa anasema kuwa aliye karibu na Mwenyezi Mungu ni yule anayejikurubisha kwake kwa maadili na matendo mema, hata kama yuko karibu na muovu wa waovu.

Na aliye mbali na Mwenyezi Mungu ni yule anayejibaadisha kwa maovu na madhambi, hata kama yuko karibu na mwenye takuwa zaidi ya wenye takua. Hakuna udugu katika hilo. Hakuna kitu kabisa kitakachofaa siku ya Kiyama isipokuwa takua na ikhlasi.

Amepiga mfano Mwenyezi Mungu kwa mke wa Nuh, kwa vile alikuwa akimuudhi mumewe na kumwambia ni mwenda wazimu na alikuwa akifichua siri zake kwa washirikina. Na mke wa Lut alikuwa akiwasaidia mahabithi kwa kuwajulisha juu ya wageni wake. Ndio maana akawapa wasifu wa hiyana ambayo ni kinyume na amana; na wala sio kwa maana ya zina. Kwa sababu waislamu wanaitakidi kuwa mke yeyote wa Nabii hakuwahi kuzini.

Kwa ufupi ni kuwa: Mwenyezi Mungu atamwingiza motoni mke wa Nuh na wa Lut kwa sababu ya ukafiri na unafiki wao, ingawaje walikuwa ni wake wa manabii wakubwa. Basi hivyo hivyo atawaingiza motoni wakeze Mtume mtukufu(s.a.w.w) waliokuwa dhidi yake, iwapo hawatatubia kwa Mwenyezi Mungu na kwake.

Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walioamini mke wa Firauni, aliposema: Mola wangu! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhalimu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kupiga mfano kuwa ukaribu wa muovu kwa mwema haumfai kitu, sasa analeta mfano wa kuwa pia ukaribu wa mwema kwa kwa muovu haumdhuru kitu. Akapiga mfano wa mke wa Firauni; uhusiano wake na Firauni haukumdhuru. Asiya bint Muzahim alimwamini Mwenyezi Mungu na vitabu na mitume yake na akamkufuru mumewe Firauni.

Basi akamtishia kumuua. Akaathirika na radhi za Mwenyezi Mungu na neema zake kuliko ufalme wa Firauni na usultani wake, akajitenga naye na amali yake; akamwomba Mola wake ampe rehema yake na amneemeshe kwa fadhila yake.

Katika Tafsir Attabariy kuna maelezo kuwa: Firauni alipompelekea watu wake aliwaambia: Muonyesheni jiwe kubwa zaidi mtakalolipata. Akibakia na imani yake ya Mwenyezi Mungu basi mtupieni jiwe na akirejea na kuachana nayo basi atakuwa ni mke wangu.

Basi walipomletea alinyanyua macho yake mbinguni akaona nyumba yake Peponi akasema yale maneno yake na roho yake ikatoka. Wale wakaangusha jiwe kwenye mwili usiokuwa na roho.

Tafsiri nyingine zinasema kuwa: maombi yake ya kujengewa nyumba Peponi, ni kama kusema: Jirani kwanza kabla ya nyumba.

Na Maryam binti Imrani, aliyeilinda tupu yake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa watiifu.

Kuhifadhi tupu yake ni kinaya cha usafi wake kutokana na waliyomzulia mayahudi kuwa ni mzinfu muovu. Makusudio ya kupulizia ni kutiwa uhai wa mtoto wake, Bwana Masih; sawa na alivyotia uhai kwa Adam:

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٢٩﴾

“Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kumsujudia.”

Juz. 14 (15:29).

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amepiga mfano wa waumini wanawake kwa Bibi Maryam mtakatifu aliyemwamini Mwenyezi Mungu, mitume wake na vitabu vyake na akabeba mimba ya mwanawe kwa neno lake Mwenyezi Mungu.

Umetangulia mfano wake mara nyingi. Tazama Juz. 6 (4:171).

MWISHO WA SURA YA SITINI NA SITA: SURAT AT –TAHRIM