14
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sitini Na Saba: Surat Al-Mulk. Imeshuka Makka. Ina Aya 30.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾
1. Ametukuka ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.
الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾
2. Ambaye ameumba mauti na uhai ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira.
الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ ﴿٣﴾
3. Aliyeumba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha jicho! Unaona kosa lolote?
ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ ﴿٤﴾
4. Tena rudisha jicho mara mbili, jicho lako litakurudia likiwa dhalili lililochoka.
وَلَقَدْ زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَجَعَلْنَاهَا رُجُومًا لِّلشَّيَاطِينِ وَأَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابَ السَّعِيرِ ﴿٥﴾
5. Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao.
وَلِلَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٦﴾
6. Na kwa waliomkufuru Mola wao ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo!
إِذَا أُلْقُوا فِيهَا سَمِعُوا لَهَا شَهِيقًا وَهِيَ تَفُورُ ﴿٧﴾
7. Watakapotupwa humo watausikia muungurumo wake na huku inafoka.
تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ الْغَيْظِ كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ ﴿٨﴾
8. Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakuwajia mwonyaji?
قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ ﴿٩﴾
9. Watasema: Kwa nini! Alitujia mwonyaji, lakini tukakadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa!
وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾
10. Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikia, au kuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa Motoni!
فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١١﴾
11. Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni!
AMETUKUKA MWENYE UFALME WOTE
Aya 1 – 11
MAANA
Ametukuka ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekitukukia kila kitu kwa uwezo wake na nguvu zake, wala hashindwi na lolote; miongoni mwa athari za utukufu huu ni kuwa Yeye ndiyeAmbaye ameumba mauti na uhai ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikia, au kuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa Motoni!
Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni! Na Yeye ni Mwenye nguvu Mwingi wa maghufira.
Uhai huu umetoka wapi na vipi unatoweka? Hakuna jibu la maswali hayo isipokuwa kuweko aliye hai asiyekufa. Tazama Juz. 7 (6:95) kifungu cha ‘Uhai umetoka wapi?’
Ama hekima ya uhai duniani na umauti kisha ufuufo, ni kudhihirika vitendo vya mtu katika dunia yake, kisha alipwe thawabu au adhabu katika Akhera yake. Imeelezwa katika Hadith kwamba Mtume(s.a.w.
w
)
, aliposoma Aya hii, alifasiri kwa kusema: Ni nani miongoni mwenu mwenye akili nzuri zaidi na mwenye kujichunga zaidi na aliyoyaharimisha Mwenyezi Mungu na aliye mwepesi zaidi wa kumtii?.
Vile vile miongoni wa athari za utukufu Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwamba Yeye ndiyealiyeumba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha jicho! Unaona kosa lolote? Tena rudisha jicho mara mbili, jicho lako litakurudia likiwa dhalili lililochoka.
Kutajwa mbingu saba hakumaanishi kuwa ni hizo tu; Tazama Juz. 28 (65:12). Tabaka Maana yake ni kufuatana katika mpangilio wa kutengenezwa kwake.
Maana ni kuwa hakikisha, uchunguze na utaamali vizuri, tena urudie mara kwa mara, uangalie viumbe, kwa hakika huoni wala hutaona isipokuwa hekima, mpangilio, nidhamu na mfumo wa hali ya juu katika kila kitu; hakuna tofauti kabisa katika mpangilio wa kutengenezwa kwake wala hakuna upungufu au kasoro yoyote, kuanzia kidogo kabisa hadi kikubwa sana.
Ziulize akili zote: Ni nani aliyekipa kila kitu umbo lake na kukikadiria kipimo chake? Je ni sadfa? Ni lini basi sadfa iliweza kushangaza akili? Hakuna jawabu kwa mwenye akili timamu isipokuwa kurejea kwenye nguvu iliyo nyuma ya maumbile ambayo ni vigumu kuijua hakika yake ni ulivyo ukuu wake.
Kuanzia hapa ndio inakuwa siri ya historia ya kumwamini Mwenyezi Mungu aliyekuwako kwa kuwako mtu, bali kwa kila kiumbe. Tuna uhakika kabisa kwamba mpinzani, lau atafikiria vizuri na kuzingatia umbile la mbingu na ardhi, basi angelimwamini Mwenyezi Mungu atake asitake. Anasema Lord Kelvin, mmoja wa wanasayansi wanaojitokeza: “Ukifikiri kwa undani sana basi ilimu itakufanya ulazimike kuamini kuweko Mwenyezi Mungu.”
Hilo limewekwa wazi na Qur’an pale iliposema:
إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ﴿٢٨﴾
“Hakika si mengineyo, wanaomcha Mwenyezi Mungu katika waja wake ni wale wajuzi.”
Juz. 22 (35:28).
Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao.
Makusudio ya mataa ni nyota. Kupiga kunaweza kuwa kwa miali inayounguza - aghlabu - katika anga kabla ya kufika ardhini; au inaweza kuwa ni kwa mawe yanayoanguka kutoka kwenye nyota (vimondo). Kila aliye mfidhuli muasi basi huyo ni shetani; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَإِذَا خَلَوْا إِلَىٰ شَيَاطِينِهِمْ قَالُوا إِنَّا مَعَكُمْ ﴿١٤﴾
“Na wanapokuwa peke yao kwa mashetani wao, husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi.”
Juz. 1 (2:14).
Mmoja wa wafasiri amesema: “Walaghai wanafikiri kwamba wao wanajua ghaibu kwa kuangalia nyota; na Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawavurumishia miali ya Jahannam kwa vile wao walivyokuwa wakivurumishia ghaibu.” Na sisi tunasema: Tafsiri hii vile vile ni kuivurumishia ghaibu.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 23 (37:6-10) na Juz. 24 (41:12).
Na kwa waliomkufuru Mola wao ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! Watakapotupwa humo watausikia muungurumo wake na huku inafoka. Inakaribia kupasuka kwa hasira.
Mwenye Dhila anasema: “Mtu anaweza kudhania kuwa hii ni ibara ya majazi, lakini Jahannam ni kiumbe hai kina hasira na kuchukia. Hata hivyo wafasiri wengi wamesema makusudio ni kuwa Jahannam ina mvumo mkubwa na kalabi. Mwenye kuiona anaidhania kuwa imewakasirikia makafiri.”
Tafsiri hii iko karibu na ufahamu na usadikisho kuliko tafsiri ya idhla inayofanana na tafsiri ya watu wa dhahiri.
Kila likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakuwajia mwonyaji?
Makusudio ya swali la walinzi ni kuwatahayariza wakosefu na kuwalaumu; sawa na kumwambia anayeadhibiwa kwa kosa lake: “Umejitakia mwenyewe haya.”
Watasema: Kwa nini! Alitujia mwonyaji, lakini tukakadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa!
Yaani manabii wamo katika upotevu mkubwa! Kwanini? Kwa vile wao wanatoa mwito wa tawhid na uadilifu. Lakini mataghuti na waasi wanaoabudu mawe na masanamu ndio wenye busara. Haya ndiyo mantiki ya wapotevu na wafisadi kila wakati na kila mahali.
Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikia, au kuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa Motoni! Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni!
Walipowajia mitume kwa hoja wazi wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakiwakadhibisha kwa inadi na kiburi na wakawaambia: Nyinyi ni wapotevu mliopotea. Mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo. Lakini adhabu ilipowazunguka walikuwa dhalili na wakajuta; wakakubali kuwa wao ndio wapotevu. Lakini wapi! Wamekwishachelewa! Malipo yao yamekuwa ni kuungua.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:130) na Juz. 24 (39:71).
إِنَّ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿١٢﴾
12. Hakika wanaomwogopa Mola wao kwa ghaibu, watapata maghufira na ujira mkubwa.
وَأَسِرُّوا قَوْلَكُمْ أَوِ اجْهَرُوا بِهِ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١٣﴾
13. Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٤﴾
14. Hivi asijue aliyeumba, naye ni Mpole, Mwenye habari?
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ ﴿١٥﴾
15. Yeye ndiye aliyeifanya ardhi dhalili kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa.
أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ ﴿١٦﴾
16. Je, mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni kuwa hatawadidimiza kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika?
أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ ﴿١٧﴾
17. Au mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni kuwa Yeye hatawapelekea kimbunga chenye changarawe? Basi mtajua vipi maonyo yangu.
وَلَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿١٨﴾
18. Na walikwishakadhibisha waliokuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu?
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ بَصِيرٌ ﴿١٩﴾
19. Je, hawawaoni ndege walioko juu yao wakizikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu.
TEMEBEENI KATIKA PANDE ZAKE
Aya 12- 19
MAANA
Hakika wanaomwogopa Mola wao kwa ghaibu, watapata maghufira na ujira mkubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja aliyowaandaia wakosefu, sasa anataja aliyowaandalia wenye takua, katika misingi ya kuvutia na kuogopesha. Wenye takua ni wale wanaojichunga na aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu katika hali zote. Hakuna tofauto kwao wajulikane na watu au wasijulikne, kwa sababu wao wanafanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu anayejua yaliyosiri na kujificha.
Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
Yaani yaliyodhamiriwa. Mwenye kujua yaliyodhamiriwa nyoyoni basi atakuwa anajua yanayosemwa.
Aya hii imetangulia katika Juz. 11 (11:5).
Hivi asijue aliyeumba, naye ni Mpole, Mwenye habari?
Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu, kwa sababu Yeye ni muumba wa kila kitu. Sifa ya upole inaashiria kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hamfanyii haraka muovu kumwadhibu kwa kumhurumia, pengine anaweza kutubia na kujing’oa kwenye dhambi zake.
Yeye ndiye aliyeifanya ardhi dhalili kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwenye huruma kwa waja wake, anajua mahitaji yao katika maisha haya. Ndio maana amewaumbia ardhi na akawawekea humo chakula na riziki na akaifanya iitikie matakwa, mahitaji na masilahi yao. Sheikh Abdul qadir Al-maghribi anasema: “Ardhi ni neema kwetu, ni kipando kilichozoeleka, na ni mtumishi mwenye uzoefu.”
Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu hilo ameliwekea desturi ya kulifanyia kazi na kulihangaikia. Hekima yake imetaka kuzifungamanisha sababu na visababishi pamoja na natija kwa utangulizi wake. Atakayetoka kwenye desturi hii basi atakuwa ameifanyia ujeuri desturi ya Mwenyezi Mungu na matakwa yake.
Na kwake Yeye ndio kufufuliwa.
Hii ni hadhari na kiaga kwa anayetafuta riziki bila ya kusumbuka na kuhangaika kisharia:
لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي كَبَدٍ ﴿٤﴾
“Hakika tumemuumba mtu katika tabu.” (90:4).
Yaani asumbuke na kufanya juhudi; kama walivyosema wafasiri wengi.
Je, mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni kuwa hatawadidimiza kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika? Au mnadhani mko salama kwa alioko mbinguni kuwa Yeye hatawapelekea kimbunga chenye changarawe?
Makusudio ya alioko mbinguni ni muumba wa mbingu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameihusisha mbingu ‧ pamoja na kuwa Yeye ni muumba wa kila kitu‧ kwa sababu watu wanazingatia kupangilia kwake kuwa ni kupangilia mbingu.
Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutaja neema ya ardhi na kheri zake, sasa anatoa tahadhari ya mwisho wa dhulma na ufisadi. Kwani neema hii itageuka kuwa shari na balaa kwa wakosefu na wafisadi kwa vile aliyeijaalia kuwa laini kwa waja ana uwezo wa kuwadidimiza kwa matetemeko na kuwameza wao na wanavyovimiliki. Au awaletee kimbunga kitakachowafyeka kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho wao.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:68).
Basi mtajua vipi maonyo yangu.
Mwenyezi Mungu aliwaonya na kuwahadharisha na mwisho mbaya, lakini mkayakadhibisha maonyo na mkamdharau muonyaji. Basi karibuni itawafikia adhabu mliyokuwa mkiikadhibisha na kuidharau.
Na walikwishakadhibisha waliokuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu?
Kukasirika kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni adhabu yake. Maana ni kuwa mmekwishasikia habari za aliowapatiliza Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi zao na mnajua vipi iliwashukia adhabu. Je hamwogopi kuwasibu yaliyowasibu? Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni Juz. 10 (9:69) na Juz. 22 (34:45).
Je, hawawaoni ndege walioko juu yao wakizikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu.
Aya hizi zinawalingania wapinzani wanaomkana Mungu, wafikirie katika kuumba kwa Mwenyezi Mungu na uweza wake Mtukufu. Miongoni mwa athari za uweza huu ni kuumba ndege na kuweko angani. Basi ni nani aliyewaumba kwa umbo linalowawezesha kuruka kiasi cha kukunjua mbawa zake mara nyingi na kuzikunja mara nyingine; kama afanyavyo muogeleji. Je iliyofanya hivyo ni sadfa na maumbile yaliyo mapofu?
“Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi.” Juz. 7 (6:38). Ana utambuzi kama mlivyo nyinyi na anakwenda kulingana na maumbile kama mnavyokwenda nyinyi. Ndege anaruka kwa mbawa zake, na mtu anatembea kwa miguu yake na kusafiri kwa gari, ndege au vyombo vya majini.
Sababu zote hizi ni katika utengenzaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu alizozileta kama nyenzo za kufikia malengo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (14:79).
أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي هُوَ جُندٌ لَّكُمْ يَنصُرُكُم مِّن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ إِنِ الْكَافِرُونَ إِلَّا فِي غُرُورٍ ﴿٢٠﴾
20. Au ni lipi hilo jeshi lenu la kuwanusuru badala ya Mwingi wa Rehema? Hawako makafiri ila katika udanganyifu.
أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي يَرْزُقُكُمْ إِنْ أَمْسَكَ رِزْقَهُ بَل لَّجُّوا فِي عُتُوٍّ وَنُفُورٍ ﴿٢١﴾
21. Au ni nani huyo ambaye atawapa riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki.
أَفَمَن يَمْشِي مُكِبًّا عَلَىٰ وَجْهِهِ أَهْدَىٰ أَمَّن يَمْشِي سَوِيًّا عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٢٢﴾
22. Je, anayekwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anayekwenda sawasawa katika Njia Iliyonyooka?
قُلْ هُوَ الَّذِي أَنشَأَكُمْ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٢٣﴾
23. Sema: Yeye ndiye aliyewaumba, na akawapa masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo tu mnavyoshukuru.
قُلْ هُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٢٤﴾
24. Sema: Yeye ndiye aliyewatawanya katika ardhi, na kwake mtakusanywa.
وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٥﴾
25. Na wanasema: ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
قُلْ إِنَّمَا الْعِلْمُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢٦﴾
26. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha.
فَلَمَّا رَأَوْهُ زُلْفَةً سِيئَتْ وُجُوهُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَقِيلَ هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَدَّعُونَ ﴿٢٧﴾
27. Lakini watakapoiona kwa karibu, nyuso za waliokufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyokuwa mkiyaomba.
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَهْلَكَنِيَ اللَّـهُ وَمَن مَّعِيَ أَوْ رَحِمَنَا فَمَن يُجِيرُ الْكَافِرِينَ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٨﴾
28. Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu ataniangamiza mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakayewalinda makafiri na adhabu chungu?
قُلْ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ آمَنَّا بِهِ وَعَلَيْهِ تَوَكَّلْنَا فَسَتَعْلَمُونَ مَنْ هُوَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٩﴾
29. Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhahiri.
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَصْبَحَ مَاؤُكُمْ غَوْرًا فَمَن يَأْتِيكُم بِمَاءٍ مَّعِينٍ ﴿٣٠﴾
30. Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atawaletea maji yanayotiririka?
ANAYEKWENDA AKISUNUKIA
Aya 20 – 30
MAANA
Au ni lipi hilo jeshi lenu la kuwanusuru badala ya Mwingi wa Rehema?
Aya hii inaungana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya iliyotangulia: “Je, mnadhani mko salama…”
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahofisha na kudidimizwa ardhini na kimbunga. Anawauliza, ambaye imetukuka hekima yake, kwa njia ya kutahayariza na kukaripia mtafanya nini ikiwashukia adhabu? Mtakimbia? Na hakuna atakayeokoka na kukimbia au mtakimbilia masanamu yenu nayo hayawezi hata kujisaidia hayo yenyewe?
Jawabu ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Hawako makafiri ila katika udanganyifu
, na dhana za uwongo kwamba wao wako kwenye amani na kusalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Au ni nani huyo ambaye atawapa riziki kama Yeye akizuia riziki yake?
Hili ni swali jingine kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Maana yake ni: Ikiwa Mwenyezi Mungu atawazuilia sababu za riziki, kama vile mvua, ni nani basi atakayewaletea mvua? Je, ni hayo masanamu yenu mnayoyaabudu au ni ujinga na ghururi yenu?
Jibu ni: Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki.
Wao wanajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuruzuku, lakini pamoja na hayo wanaifanyia inadi haki na wanag’ang’ania kwenye batili, kwa sababu maisha yao yanasimamia batili na kuipiga vita haki na watu wake.
Je, anayekwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anayekwenda sawasawa katika Njia Iliyonyooka?
Huu ni mfano wa tamko la swali; mfano wa kuwatofautisha wapotevu waliozama katika ujeuri na kukataa na wale walioongoka wanaosikiliza maneno na wakafuata mazuri yake. Mfano wa wapotevu ni kama anayekwenda njiani na uso wake umeinamia ardhini huku anajikwaa. Ama walioongoka mfano wao ni kama mfano wa anayekwenda kwenye njia iliyo wazi na mtazamo ulio salama.
Maana ya Aya hii yamekaririka kwenye Aya kadhaa; ikwemo ile isemayo:
مَثَلُ الْفَرِيقَيْنِ كَالْأَعْمَىٰ وَالْأَصَمِّ وَالْبَصِيرِ وَالسَّمِيعِ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾
“Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia. Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Je, hamfikiri?” Juz. 11 (11:24).
Sema: Yeye ndiye aliyewaumba, na akawapa masikio na macho, na nyoyo.
Mwenyezi Mungu amewaumbia masikio, basi waidhikeni kwa mnayoyasikia. Amewajaalia macho, basi zingatieni kwa mnayoyaona, miongoni mwa ishara na miujiza. Amewapa akili, kwanini hamfahamu?
Mmoja wa wafasiri wa zamani alisema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametanguliza usikizi kwa sababu faida zake zina nguvu zaidi kuliko za kuona. Kwa vile usikizi ni wa kuzungumziwa na uoni ni wa kuangalia, na daraja ya kuzungumza ndiyo inayotangulia.”
Mwanafisihi mmoja wa hivi karibuni naye anasema: “Halitangulii neno lolote, katika Qur’an, kulitangulia jingine ila ni kwa sababu fulani, wala halifuati nyuma ila ni kwa sababu; mfano rahisi ni tunavyoona Qur’an ikitanguliza usikizi kuliko uoni katika Aya kadhaa. Jambo hili wanalijua wataalamu wa upasuaji. Wanaona kuwa viungo vya usikizi ni vya hali ya juu, vilivyofungana na laini zaidi kuliko viungo vya uoni.
Mama hawezi kupotewa na sauti ya mtoto wake na anaweza kuitambua hata kukiwa na maelfu ya sauti, lakini anaweza asimuone kukiwa na msongamano.”
Ni kidogo tu mnavyoshukuru
, kwa sababu Mungu ameumba masikio na macho kwa ajili ya heri na wema na nyinyi mnavitumia kwa shari na ufisadi.
Sema: Yeye ndiye aliyewatawanya katika ardhi.
Yaani amewafanya wengi kwenye uzazi ili mshindane katika uwanja wa maisha na uimarishaji wake na kugawana kheri zake kwa mujibu wa uwezo wa mtu. Haya ndiyo waliyoyasema wafasiri, lakini kama wangelikuweko hivi sasa ingeliwabidi kuongeza kauli hii: Lakini madola makubwa yanashindana katika uwanja wa silaha, kuwanyima wenye njaa neema na baraka ya ardhi, ili waweze kulingana na viwanda vya mauti wanavyovimiliki mataghuti walanguzi.
Mahisabu yanaonyesha kuwa matumizi ya silaha ni zaidi ya matumizi ya elimu na afya kwa pamoja.
Na kwake mtakusanywa
, awaadhibu wafisadi kwa hatia na makosa yao.Na wanasema: ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
Swali hili limekaririka mara nyingi sana kutoka kwa wapinzani. Ni ajabu na mshangao, kwa sababu hakuna mwenye akili isipokuwa anataka dalili kwa lile lililo na uwezekano wa kuwa kwa linalofanana na kushabihiana nalo.
Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha.
Hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ﴿١٨٧﴾
“Wanauliza hiyo saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.” Juz. 9 (7:187).
Lakini watakapoiona kwa karibu, nyuso za waliokufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyokuwa mkiyaomba.
Nabii aliwahadharisha na Siku ya Kiyama, lakini wakamwambia kwa dharau: “Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.”
Lakini watakapofufuliwa siku ya Kiyama na kuambiwa: “Haya ndiyo mliyokuwa mkiyahimiza,”
watasema: “Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.”
Hivi ndivyo alivyo kila mjinga anayepanda kichwa na asiyejali yanayosema na yanayofanywa kwa ajili yake.
Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu ataniangamiza mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakayewalinda makafiri na adhabu chungu?
Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hikima ataona kuwa, aghlabu, tofauti iliyokuwako baina ya manabii na washirikina, ilikuwa kwenye ushirikina na ufufuo, na kwamba Aya nyingi zilikuwa zikizunguka kwenye misingi miwili hii, kwa mfumo wa moja kwa moja au isiyokuwa moja kwa moja. Washrikina walikuwa wakitoa hoja ya kuabudu masanamu kuwa ni ibada ya mababa na mababu, na wakiukana ufufuo kwa hoja ya kuwa atakayegeuka kuwa mchanga vipi anaweza kurudi hai tena?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemfundisha Nabii wake mtukufu hoja za kuwarudi na kuwaonya na adhabu ya sasa na ya baadae. Yamekwishatangulia makumi ya Aya juu ya hilo. Basi washirikina walishindwa kuzijibu hoja, wakabaki kukimbilia kwenye inadi, jeuri na dharau. Mara nyingine wakawa wanamduilia Mtume(s.a.w.
w
)
aangamie; kama ilivyoashiria kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “ Au wanasema: mshairi, tunamtazamia kupitilizwa na dahari. Juz. 27 (52:30).
Aya zilizotangulia zimeelezea jinsi Mtume alivyowaambia washirikina kuhusu ufufuo na hadhari ya adhabu ya gharika na vimbunga duniani na adhabu ya Jahannam na marejeo mabaya Akhera.
Kisha ikawa wao wanamuombea dua mbaya Mtume na mwito wake; kiasi cha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwamrisha kuwaambia: Je, mnanitazamia mimi na aliye pamoja nami kuangamia? Hebu niambieni mtapata faida gani ikiwa yatakuwa hayo mnayoyatamani, je, kutawaokoa na adhabu na hali nyinyi mnaendelea kwenye upotevu? Hapana! Hakuna litakalowafaa isipokuwa toba na kurejea, iwe mtakufa kabla yangu au nife kabla yenu.
Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea.
Hii ndio njia ya kuokoka ‧ kumwamini Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye ndiye anayerehemu na kumghufiria mwenye kutubia dhambi zake na akamtegemea katika mambo yake.
Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhahiri.
Baada ya Mtume mtukufu(s.a.w.
w
)
kuwaambia washirikina, kama Mwenyezi Mungu atatuangamiza au kuturehemu, sasa anawaambia: hapana! Nyinyi ndio mtaangamia, kwa sababu ni wapotevu na wapotezaji. Ama sisi tuko katika rehema ya Mwenyezi Mungu na himaya yake na tuna nusura duniani na Akhera, na kesho mtalijua hilo kiuhakika.
Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atawaletea maji yanayotiririka?
Usawa kwenu enyi washirikina ni kutubia kwa Mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa neema zake zisizohisabika; yakiwemo haya maji yenu ambayo ndio chimbuko la maisha yenu. Mwenyezi Mungu angelitaka angeliyadidimiza ndani ya ardhi, na mkafa na njaa na kiu; na wala hakuna mwenye kuzuia matakwa yake.
Kuna mfasiri mmoja aliyesema kuwa Mwenyezi Mungu alikusudia, kwa hili, kulainika nyoyo zao, ili waweze kurudi kwenye uongofu. Hili haliko mbali, kwani mfumo wa kutoa mwito uko namna mbali mbali.
MWISHO WA SURA YA SITINI NA SABA: SURAT AL-MULK