15
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE
Sura Ya Sitini Na Nane: Surat Al- Qalam. Imeshuka Makka. Imesemekana kuwa baadhi imeshuka Madina. Ina Aya 52.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
ن وَالْقَلَمِ وَمَا يَسْطُرُونَ ﴿١﴾
1. Nun. Naapa kwa kalamu na yale wanayoandika.
مَا أَنتَ بِنِعْمَةِ رَبِّكَ بِمَجْنُونٍ ﴿٢﴾
2. Kwa neema ya Mola wako wewe si mwendawazimu.
وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ ﴿٣﴾
3. Na kwa hakika wewe una ujira usiokatika.
وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ ﴿٤﴾
4. Na hakika wewe una tabia tukufu.
فَسَتُبْصِرُ وَيُبْصِرُونَ ﴿٥﴾
5. Karibu utaona, na wao wataona.
بِأَييِّكُمُ الْمَفْتُونُ ﴿٦﴾
6. Ni nani kati yenu aliyepandwa na wazimu.
إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿٧﴾
7. Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
فَلَا تُطِعِ الْمُكَذِّبِينَ ﴿٨﴾
8. Basi usiwatii wanaokadhibisha.
وَدُّوا لَوْ تُدْهِنُ فَيُدْهِنُونَ ﴿٩﴾
9. Wanatamani lau ungelainisha ili nao wakulainishie.
وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ ﴿١٠﴾
10. Wala usimtii kila mwingi wa kuapa aliye dhalili.
هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ ﴿١١﴾
11. Msingiziaji, apitae akifitini.
مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾
12. Mwenye kuzuia heri, mwenye kudhulumu, mwingi wa madhambi.
عُتُلٍّ بَعْدَ ذَٰلِكَ زَنِيمٍ ﴿١٣﴾
13. Mwenye roho ngumu, juu ya hayo, ni mwanaharamu.
أَن كَانَ ذَا مَالٍ وَبَنِينَ ﴿١٤﴾
14. Ati kwa kuwa ana mali na watoto!
إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا قَالَ أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٥﴾
15. Anaposomewa Aya zetu, husema: Hizi ni ngano za watu wa kale!
سَنَسِمُهُ عَلَى الْخُرْطُومِ ﴿١٦﴾
16. Tutamtia doa juu ya pua.
WEWE SI MWENDAWAZIMU
Aya 1- 16
MAANA
Nun
. kwa kukadiria maneno ya kuwa hii ni sura ya Nun. Hii sio kama mianzo mingineyo ya herufi zinazoanziwa sura, tulizozizungumzia katika Juz. 1 (2:1).
Kuna aliyesema kuwa ni samaki, mwingine akasema ni chombo cha wino, watatu akasema ni wino, wa nne akasema ni nun ya neno rahman, na jamaa wa kisufi wakasema kuwa ni nafsi. Kauli zote hizi zinahitajia dalili.
Naapa kwa kalamu na yale wanayoandika.
Wametofautiana kuhusu kalamu: Kuna waliosema ni kalamu iliyotumika kwenye lawh mahfud[ (ubao maalum uliohifadhiwa). Mwingne akasema ni kila kalamu, na kwamba herufi aliY na la` kwenye neno hili ni ya jinsi, ambayo inamaanisha kuenea.
Hii ndio kauli iliyo dhahiri; kwamba makusudio sio kalamu hasa, bali ni nyenzo yoyote ya kuandikia; kama inavyoashiria kauli inayofuatia inayosema: “Na yale wanayoyaandika.”
Kwa hiyo basi kalamu itakuwa ni kinaya cha chombo cha kuandikia, vyovyote kitakavyokuwa, kilichopo au kitakachogunduliwa karibuni au baadaye. Tumedokeza faida za ubainifu katika Juz. 27 (55:4), kwamba manufaa ya ubainifu ni sawa na manufaa ya maji na hewa.
Kwa neema ya Mola wako wewe si mwendawazimu.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
. Hakuna yeyote anayedhania kuwa Muhammad(s.a.w.w)
ni mwenda wazimu. Wale waliompa sifa hiyo walikusudia kuwa ana jinni linalompa wahyi; kama wanavyodai kwamba kila mshairi ana jinni linalomfundisha ushairi.
Hilo linaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwasimulia:
وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ ﴿٣٦﴾
“Na wakisema: Hivi tuiache miungu miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?” Juz. 23 (37:36).
Na kwa hakika wewe una ujira usiokatika.
Neno ‘usiokatika’ tumelifasiri kutokana na neno mamnun, ambalo pia lina maana ya kusimbuliwa au maana zote mbili pamoja (kukatika na kusimbuliwa).
Kimsingi ni kuwa malipo yanapimwa kwa natija ya kazi na athari yake. Bado athari za Muhammad(s.a.w.w)
, mwito wake na ukuu wake unaendela hadi leo, kuanzia mashariki mwa ardhi hadi magharibi yake na utaendelea hadi siku ya mwisho. Kwa hiyo si kioja kupata karama ya milele kutoka kwa Mola wake.
Na hakika wewe una tabia tukufu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumsifu yeyote katika mitume wake na wasifa huu isipokuwa Muhammad.
Maana yake yanafupilizwa na kauli yake Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: “Mola wangu amenifunza maadili akayafanya mazuri mafunzo yangu,” yaani Mwenyezi Mungu ameelekeza kwa Muhammad(s.a.w.w)
maadili yale yale aliyoumba kwa ajli ya nafsi.
Vile vile Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwahi kuapa kwa maisha ya mtu isipokuwa kwa maisha ya Muhammad(s.a.w.w)
; pale aliposema:
لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِي سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٢﴾
“Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao wakimangamanga.”
Juz. 14 (15:72).
Ama wasifu wa Muhammad(s.a.w.w)
kuwa ni mwisho wa manabii, Maana yake ni kuwa Muhammad alifikia ukomo wa sifa za mtu zisizofikiwa na yeyote kwa ukamilifu. Ni muhali kuja baada yake atakayekuwa bora zaidi kuliko yeye au kuja na sharia bora zaidi ya sharia zake; bali hakuna kiumbe yeyote kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho anayefanana naye. Hilo linaashiriwa na kauli yake Mtume(s.a.w.w)
: “Mimi ni bwana wa watu wote, wala sisemi kwa kujifaharisha.”
Hii ni kwa kuwa sharia na utume umeishilizwa kwake. Ibn Al-arabiy anasema, katika Futuhat: kuwa Mwenyezi Mungu ameumba viumbe aina kwa aina, akafanya walio bora. Walio bora katika viumbe ni mitume, na katika mitume kuna wateule ambao ni ulul-az` na katika wao kuna mteule zaidi naye ni Muhammad(s.a.w.w)
.
Karibu utaona, na wao wataona, ni nani kati yenu aliyepandwa na wazimu.
Hili ni onyo na kiaga, kwamba hivi karibuni itakubainikia wewe na maadui zako kwamba wao ndio wajinga, wapotevu na wendawazimu zaidi katika watu, na kwamba wewe ndiwe ulie juu, mwenye akili na mtukufu wa maadili zaidi ya watu wengine na kwamba ndiwe mtukufu wao zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
Mwenyezi Mungu anajua cheo chako ewe Muhammad(s.a.w.w)
na uongofu na anajua nafasi ya wahasimu wake ya upotevu na mbele yao kuna hisabu na malipo. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 14 (16:125).
Basi usiwatii wanaokadhibisha.
Washirikina walijaribu kila njia kumzuia Mtume(s.a.w.w)
na mwito wake, wakajaribu kumbembeleza kwa cheo na mali, akakataa. Wakatamani lau watakubaliana naye kufanya vile watakavyo, Mwenyezi Mungu akamkataza hilo. Lengo la kumkataza ni kuwakatisha tamaa na wajue kuwa hakuna mjadala wala makubaliano katika twaa ya Mwenyezi Mungu na amri yake. Katazo hili linafanana na anayekutaka mkubaliane naye kwenye dini yako, ukiwa unataka kumkatisha tamaa kabisa, na kumwambia: Mwenyezi Mungu amenikataza hilo.
Wanatamani lau ungelainisha ili nao wakulainishie.
Washirikina walitamani Mtume(s.a.w.w)
apunguze baadhi ya yale anayowalingania na wao waache baadhi ya yale aliyowakataza, ijapokuwa ni kwa njia ya kupakaka mafuta kwa mgongo wa chupa ili kusiwe na mvutano baina ya pande mbili.
Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa aliyetoa maoni hayo anasifika na sifa aliyoiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kusema:Wala usimtii kila mwingi wa kuapa aliye dhalili
. Anakithirisha viapo bila ya sababu jambo linalomsababisha kuwa dhalili anayedharauliwa.Msingiziaji
anawatia ila sana watu.Apitaye akifitini
. Anajaribu kuwavuruga watu kwa kunukuuu ya huku akiyapeleka kule.
Mwenye kuzuia heri
, yeye haifanyi na anazuia wengine wasiifanye.Mwenye kudhulumu
, haki za watu.Mwingi wa madhambi
na makosa.Mwenye roho ngumu, juu ya hayo, ni mwanaharamu,
asiyejua nasaba yake. Hii ni sifa mbaya zaidi ya zote zinazofikiriwa na akili.
Wafasiri wengi wamesema kuwa aliyekusudiwa na ushenzi huu ni Walid bin Al-mughira, aliyekuwa ni miongoni mwa vigogo wa kikuraishi, mwenye mali nyingi na watoto; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:Ati kwa kuwa ana mali na watoto! Anaposomewa Aya zetu, husema: Hizi ni ngano
za uwongoza watu wa kale!
Wafasiri wamesema kuwa Aya hii ni ya kukataza kumtii mshenzi huyu. Lakini lililo karibu zaidi na usawa ni kuwa huko kuwa na mali na watoto kumemfanya athubutu kusema Qur’an ni simulizi za watu wa zamani; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾
“Hakika mtu hupituka mipaka kwa kujiona ametajirika.” (96:6-7).
Sikwambii tena akiwa na nguvu na watu.Tutamtia doa juu ya pua
yake. Waarabu wanatumia kutaja pua kwa ajili ya utukufu na udhalii. Wanasema kwa utukufu: ana pua ya kunusa. Kwenye udhalili wanasema: pua yake ikio mchangani.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamfedhehesha mjeuri huyu ambaye amejitukuza kwa mali na watoto, atamdhalilisha muda wote, atam laani kwa lugha iliyosajiliwa kwenye Kitabu chake na atamfedhehesha Akhera mbele ya ushuhuda, kwa kusawijika uso na alama nyinginezo za kuakisi madhambi yake.
إِنَّا بَلَوْنَاهُمْ كَمَا بَلَوْنَا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ إِذْ أَقْسَمُوا لَيَصْرِمُنَّهَا مُصْبِحِينَ ﴿١٧﴾
17. Hakika tumewajaribu kama tulivyowajaribu wenye shamba, walipoapa kwamba watalivuna itakapokuwa asubuhi.
وَلَا يَسْتَثْنُونَ ﴿١٨﴾
18. Wala hawakusema: Inshaallah!
فَطَافَ عَلَيْهَا طَائِفٌ مِّن رَّبِّكَ وَهُمْ نَائِمُونَ ﴿١٩﴾
19. Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako, nao wamelala!
فَأَصْبَحَتْ كَالصَّرِيمِ ﴿٢٠﴾
20. Likawa kama limefyekwa.
فَتَنَادَوْا مُصْبِحِينَ ﴿٢١﴾
21. Wakaitana asubuhi.
أَنِ اغْدُوا عَلَىٰ حَرْثِكُمْ إِن كُنتُمْ صَارِمِينَ ﴿٢٢﴾
22. Ya kwamba raukeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna.
فَانطَلَقُوا وَهُمْ يَتَخَافَتُونَ ﴿٢٣﴾
23. Basi walikwenda na huku wakinong’onezana.
أَن لَّا يَدْخُلَنَّهَا الْيَوْمَ عَلَيْكُم مِّسْكِينٌ ﴿٢٤﴾
24. Ya kuwa leo asiliingie hata maskini mmoja.
وَغَدَوْا عَلَىٰ حَرْدٍ قَادِرِينَ ﴿٢٥﴾
25. Na walirauka, nao wana nguvu za kunyima.
فَلَمَّا رَأَوْهَا قَالُوا إِنَّا لَضَالُّونَ ﴿٢٦﴾
26. Basi walipoliona, wakasema: Hakika tumepotea!
بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ ﴿٢٧﴾
27. Bali tumenyimwa!
قَالَ أَوْسَطُهُمْ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ لَوْلَا تُسَبِّحُونَ ﴿٢٨﴾
28. Akasema Mbora wao: Je, Sikuwambia, kwa nini hamumsabihi Mwenyezi Mungu?
قَالُوا سُبْحَانَ رَبِّنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٢٩﴾
29. Wakasema: Ametakasika Mola wetu! Hakika tulikuwa madhalimu.
فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَلَاوَمُونَ ﴿٣٠﴾
30. Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao.
قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا طَاغِينَ ﴿٣١﴾
31. Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka!
عَسَىٰ رَبُّنَا أَن يُبْدِلَنَا خَيْرًا مِّنْهَا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا رَاغِبُونَ ﴿٣٢﴾
32. Asaa Mola wetu akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.
كَذَٰلِكَ الْعَذَابُ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٣٣﴾
Kama hivyo inakuwa adhabu, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi, laiti wangelijua!
LIKAWA KAMA LIMEFYEKWA
Aya 17 – 33
MAANA
Hakika tumewajaribu kama tulivyowajaribu wenye shamba.
Waliojaribiwa ‧ katika neno tumewajaribu - ni washirikina wa kikuraishi waliomkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria katika Aya ya nane ya surua hii. ‘Basi usiwatii wanaokadhibisha.’ Akiwemo yule mwenye kupituka mipaka mwenye dhambi ambaye, kama walivyosema wafasri, ni Walid bin Almughira, kigogo wa makuraishi msemaji wa wakadhibishaji akielezea ufidhuli na jeuri yao juu ya haki.
Aya hizi tulizo nazo zinampigia mfano yeye na wao, kwamba kulikuwa na watu waliokuwa na shamba lililojaa mazao, lakini wao walikuwa mabahili kwa mafukara na masikini.
Mazao yalipokomaa na kukurubia kuvunwa walipanga njama na kuapa kuwa wavune shamba asubuhi na mapema, mafukara wakiwa hawana habari. Waliazimia hivyo bila ya kuyaunganisha maazimio yao na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Waliambiana kuwa wawanyime wahitaji kile walichopewa na Mwenyezi Mungu, wakiwa wamesahau mipangilio ya Mwenyezi Mungu na uweza wake.
Usiku huo huo walioazimia kuvuna, Mwenyezi Mungu alilitermshia shamba janga la mbinguni lilioharibu mazao yote kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Walipoamka asubuhi na kwenda shambani walipigwa na butwaa, wakaanza kulaumiana wenyewe kwa wenyewe, kila mmoja akimwambia mwenzake: “Wewe ndiye sababu ya haya.” Miongoni mwao alikuwako mtu mwema aliyewapa nasaha kabla, lakini hawakumsikiliza, ndio akawaambia: Kwani sikuwaaambia, lakini mkakataa. Basi tubieni kwa Mola ili mpate kufaulu. Wakatubia kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wakamwomba msamaha na kutaka wahurumiwe na kuneemeshwa kutoka shambani mwao.
Lengo la kupiga mfano huu, ni kupata funzo kila aliyeneemeshwa na Mwenyezi Mungu; hasa watu wa Makka akiwemo yule mshenzi. Wapokezi wa Hadith wanasema watu wa Makka walipatwa na kahati na njaa kwa vile walimkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
, ndipo akawaombea majanga na Mwenyezi Mungu akaitikia maombi yake. Kahati iliendelea kiasi cha miaka saba mpaka wakawa wanakula mizoga na mifupa. Pia wapokezi wanasema Mwenyezi Mungu aliingamiza mali ya Walid.
Haya ndio makusudio ya Aya kwa ujumla wake. Ufuatao ni ufufanuzi wa Aya moja moja:-
Walipoapa kwamba watalivuna itakapokuwa asubuhi.
Wenye shamba waliapa kuwa watalivuna mafukara wakiwa hawana habari.
Wala hawakusema: Inshaallah!
Yaani hawakusema tutavuna asubuhi Mungu akipenda.
Tumefasiri wala hawakusema inshaallah! Kutokana na maneno ya kiarabu yastathnuua ambayo tafsiri yake ya moja kwa moja ni ‘hawakutenga au hawakutoa.’ Kwa hiyo baadhi ya wafasiri wakasema maana ni hawakutenga kitu kwa ajili ya masikini. Kila moja kati ya tafsiri mbili hizi inafaa. Vile vile zinaweza kwenda kwa pamoja.
Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako, nao wamelala! Likawa kama limefyekwa.
Wenye shamba walilala raha mustarehe wakiwa na imani ya kulivuna shamba lao asubuhi na mapema, lakini usiku huo likafikwa na janga.
Neno kufyekwa, tumelifasiri kutokana na neno Asswarim, ambalo maana yake nyingine ni weusi, kwa maana ya kuungua na kuwa jeusi kama usiku wa giza
Wakaitana asubuhi, ya kwamba raukeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna.
Ilipofika asubuhi waliitana ili wawahi kwenda shamba bila ya masikini kujua.
Basi walikwenda na huku wakinong’onezana. Ya kuwa leo asiliingie hata masikini mmoja.
Walifanya haraka wakidhamiria kwa siri kuwa masikini asionje hata chembe ya mazao.
Hakuna mwenye shaka kuwa huu ni uchoyo. Ikiwa hawa shamba lilikuwa lao na mazao ni yao hawakuiba, lakini pamoja na hayo Mwenyezi Mungu aliwaghadhabikia na kuwaandalia adhabu; je, itakuwaje kwa yule aliyepituka mipaka kwenye maisha ya watu akawanyang’anya vyakula vyao, akawaua na kuwafukuza kwenye miji, kama wanavyofanya wakoloni hivi sasa katika mashariki ya dunia na magharibi yake?
Na walirauka, nao wana nguvu za kunyima.
Waliingia shambani mwao wakiwa na dhamira kabisa ya kuwanyima mafukara, wakiwa na mawazo kwamba shamba na mazao yake yako mikononi mwao. Hawakujua kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao.
Basi walipoliona, wakasema: Hakika tumepotea! Bali tumenyimwa!
Walipofika shamba yaliwashangaza waliyoyaona na wakakubali kuwa wamepotea na kusema: sisi ndio tuliokosa fadhila za Mwenyezi Mungu na thawabu zake, na tunastahili ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake na sio mafukara na masikini.
Miongoni mwao alikuwa mtu mwema aliyekuwa akiaamrisha mema na kuwakataza maovu, lakini hawakusikiliza nasaha zake. alipoona yaliyowafika:
Akasema Mbora wao: Je, Sikuwambia, kwa nini hamumsabihi Mwenyezi Mungu?
Yaani hamumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kauli wala kwa vitendo kwa kutoa. alisema hivi kwa kuwahurumia. Kisha akawaamuru kutubia:Wakasema: Ametakasika Mola wetu! Hakika tulikuwa madhalimu
wa nafsi zetu kwa kumuasi Mwenyezi Mungu.
Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao.
Kila mmoja anamtupia lawama mwinziwe; kama ilivyo hali ya washirikina, wanapofikwa na yale yaliyofanywa na mikono yao.
Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka!
Walirudia akili zao na wakacha kulaumiana, wakakiri dhambi zao kwamba wao walikuwa katika upotevu, wakijiombea kufa kwa kusema ‘Ole wetu’ na kumwomba msamaha Mwenyezi Mungu, wakasema:Asaa Mola wetu akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.
Hii ni dua na matarajio yao kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) awasamehe yaliyopita na awabadilishie yaliyo bora kuliko yaliyopita. Na Mwenyezi Mungu anakubali toba kutoka kwa waja wake, anawasamehe mengi na anaitikia maombi ya anayemuomba kwa ukweli na ikhlasi.
Kama hivyo inakuwa adhabu, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi, laiti wangelijua!
Razi anasema hii iko wazi haihitaji tafsir, lakini sheikh Maraghi amekataa isipokuwa kuifasiri kwa kusema: “Yaani adhabu ya Akhera ni kali na inaumiza zaidi kuliko adhabu ya duniani.”