HIDAYA YA RAMADHANI
YANAYOHARIBU SAUMU
Kwa kuwa Mwislamu huwa na hamu kubwa ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhani, kadhalika anatakiwa kuwa na hamu ya kujichunga na mambo ambayo huenda yakamharibia saumu yake. Na mambo yenyewe ni haya:
1. Kula japo kitu kidogo sana;
2. Kunywa hata kama ni tone moja;
3. Kumwingilia mwanamke mchana hata kama manii hayakutoka;
4. Kujitoa manii kwa kujichezesha, au kwa kumchezesha mwanamke hata kama ni mkeo pia kunatengua;
5. Kutooga Janaba, Hedhi, au Nifasi hadi alfajiri pasina sababu ya udhuru maalumu pia kunabatilisha Saumu;
6. Kujifikisha vumbi - zito - kooni makusudi na kadhalika moshi wa sigara pia hubatilisha;
7. Enema-Kupigwa bomba yenye kitu cha majimaji (dawa) kwenye tundu ya nyuma pia kutaharibu;
8. Kujitapisha makusudi;
9. Kumkadhibisha Mwenyezi Mungu au Mtume wake Mohammad(s.a.w.w)
au Maimamu watakatifu kuwa katika jambo fulani walisema hivi hali ni uongo kunabatilisha Saumu;
10. Kujitosa majini makusudi kwa kupiga mbizi, au kukitumbukiza tu kichwa pekee majini pia kunaharibu Saumu.
MASWALA TOFAUTI
Ingawa kula kunabatilisha Saumu lakini kunasamehewa kwa mtu yeyote aliyekula kwa kusahau, vile vile kunywa. Ama kuyameza mate yaliyojaa kinywani, hakuna makosa.
Kuyameza mabaki yaliyaliyosalia menoni wakati wa kula ama kunywa, kunabatilisha.
Kukiangalia chakula kwa hali ya kukitamani na hali umefunga hakubatilishi Saumu. Lakini ni vizuri zaidi kutokiangalia ukiwa wakitamani.
Kudungwa sindano si makosa kwa mtu aliyefunga. Naam, ni vizuri kutumia Ihtiyat (yaani kujitoa mashakani) kwa kutodungwa sindano iliyo na chakula.
Kumbuka kwamba nia ni muhimu sana na Saumu haisihi pasina kutia nia. Kunuia huku ni kusema moyoni. "Nia yangu ni kufunga kesho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu". Kadhalika amali zote za ibada hazisihi pasina nia maalum kama alivyosema Mtume(s.a.w
.w
)
:"Matendo yote hufanywa kwa nia"
. Na hivyo basi nia ni muhimu sana.
Mwenye Saumu akiazimia usiku kwamba mimi kesho sito funga basi Saumu ya siku hiyo haitasihi hata kama atabadili dhamira na kufunga tena hivyo basi atalazimika kuilipa siku hiyo. Na tukumbuke tena kwamba, mtu yeyote aliyeitengua Saumu haimfalii kula au kuendelea na vitendo vilivyokatazwa, bali analazimika kujizuia.
Kusukutua wakati wa kutawadha hakukatazwi lakini ni bora kukuepuka maana huenda maji yakakutangulia pasina kutegemea. Ama kule kupiga mswaki nako ni hivyo hivyo.
Mtume(s.a.w.
w
)
alisema "Harufu ya mdomoni wa mwenye kufunga ni bora na yenye manukato zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko marashi yoyote yale".
Ukimlazimisha mkeo kumwingilia na hali yeye mwenyewe hayuko radhi utalazimika kulipa na kutoa kafara, na pia kuaziriwa kwa kupigwa viboko 50. Na lau nyote mtaridhiana mtalazimika kulipa, kutoa kafara na kuaziriwa kwa kupigwa viboko 25 kila mmoja.
Ingawa tulieleza kwamba kutoka manii kwa kujimai (kuingiliana mke na mume) kunabatilisha Saumu na wanaohusika na kitendo hivyo huwa na janaba, hukumu hii haimhusu aliyetoka manii mchana wa Ramadhani kwa kuota usingizini, bali ataoga tu na Saumu yake haina dosari.
Udhuru wa kutokwa damu ya hedhi ukitokea japo bado kidogo tu magharibi kuingia Saumu yako itakuwa batili, na hivyo basi utalazimika kuirudia.
Kuteta katika mchana wa Saumu na hatimaye kupigana ni jambo baya sana na hasa kwa kuwa mwezi huu ni wa kusameheana, kuhurumiana n.k. Pindi ufungapo unapomuona mtu yeyote akikukabili na upuzi wowote ule, sema: "Innii Saaim", yaani:
“Hakika yangu mimi nimefunga” na ukifanya hivyo utakuwa umeukimbia uovu wote ambao huletwa na shetani.
Kutengua Saumu kwa jambo lolote la haramu kama kuzini, kulewa, na kadhalika, adhabu yake ni:
a. Kulipa siku 60 kwa siku mmoja iliyotenguliwa;
b. Kuwalisha maskini 60;
c. Kumwacha huru mtumwa.
HESHIMA YA RAMADHANI
"Mwezi wa Ramadhani ni ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu..."
(Qur'ani: 2:185)
Waislamu kote ulimwenguni hufunga mwezi ambao ni mwema kuliko miezi yote, ulio na masiku bora kuliko masiku yote, wenye masaa ya baraka kuliko masaa yote na amali zifanyikazo katika mwezi huo ni makbuli kuliko baki ya maombi. Nao ni mwezi wa Ramadhani.
Mwezi huu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa tisa wa miezi wa Kiislamu, ni mwezi wa pekee wa aina yake kwa utukufu. Ni mwezi wa kusameheana, kuombeana heri na hata kufanya ibada kwa wingi na kwa usahali kabisa.
Mwezi huu una matukio mbali mbali ya kihistoria ambayo hayatasahaulika, na ambayo vile vile hupambanua wazi utukufu wake.
Imam Ja'far As-sadiq
alisema kutoka kwa Babuye, Mtume(s.a.w.
w
)
"Taurati ilishuka na kumfikia Nabii Musa
tarehe 6 Ramadhani, nayo Injili iIiteremshiwa Nabii Isa
tarehe 12 za Ramadhani, kadhalika Zaburi ya Nabii Daud
iliteremshwa mnamo tarehe 18 za Ramadhani, vile vile Qur'ani Takatifu iliteremka katika usiku wa Laylatul Qadri ambao kwa kawaida huwa katika mwezi huu wa Ramadhani."
Bila shaka hiyo ni heshima kuu kabisa. Na umejionea mwenyewe, hakuna kitabu kati ya vitabu vitukufu vinne kutoka kwa Mungu kilichoshuka ila kilishuka mwezi huu wa Ramadhani, na hayo yote ni kuonyesha utukufu wa mwezi huu. Kwa hivyo lazima vitendo vyetu katika mwezi huu viwe vitukufu kama mwezi wenyewe ulivyo.
Na katika Historia, tunasimuliwa baadhi ya matukio ya mwezi huu huu wa Ramadhani, kwa mfano:
1. Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib
mwanawe Sayyidna Ali
wa kwanza, na Mjukuu wa Mtume(s.a.w.
w
)
alizaliwa mwezi huu wa Ramadhani tarehe 15 mwaka wa 3 wa tangu Mtume kugura toka Makkah kuja Madina. Mtume mwenyewe ndiyo aliyemfanyia Akiki kwa kumchinjia mbuzi alipotimiza siku 7. Sayyidna Hasan
, kama ilivyokuja katika Historia, alimfanana sana Babuye, Mtume(s.a.w.
w
)
sehemu ya juu. Naye Mtume(s.a.w.
w
)
alimnbashiria kuwa"Bwana wa vijana wa peponi".
2. Vita vya Badr vinavyojulikana zaidi (vita vikuu vya Badr, au Ghazwatul Badr) vilitukia siku ya Ijumaa mwezi wa Ramadhani tarehe 17 mwaka wa 624 A.D. Vita hivi ndivyo vilivyopambanua baina ya wakweli na waongo. Mushirikina (waabudu masanamu) waliharibikiwa sana na Waislamu ndio walioibuka na ushindi.
3. Katika mwezi huu huu, Mtume(s.a.w.
w
)
aliirudisha Makkah chini ya himaya ya Kiislamu tarehe 10 mwaka wa 630 A.D. Baada ya kuiteka Makkah, dini ya Islamu ilizidi mno nguvu na makafiri kuharibikiwa.
4. Imam, Sayyidna Ali bin Abi Talib
, bin Ami yake Mtume(s.a.w.
w
)
aliyezaliwa katika Kaaba, alipigwa upanga na adui wa Uislamu, Abdu Rahmani bin Muljim tarehe 19 ya mwezi huu wa Ramadhani mwaka wa 40 Hijria.
Alipigwa upanga msikitini huko Kufa, Iraq alipokuwa amekwenda kusali sala ya Alfajiri, na alifariki siku ya tatu yake, yaani tarehe 21 Ramadhani.
Sayyidna Ali(a.s.)
, Simba wa Mungu alishirikiana sana na Mtume(s.a.w.
w
)
na kuhudhuria vita vyote pasina kukimbia na ndiye aliyebaki kitandani cha Mtume(s.a.w.
w
)
alipokuwa akihamia Madina.
NASAHA KWA VIJANA
Vijana wa Kiislamu! Mwezi wa Ramadhani umetuwadia, hatuna wakati mwengine tuutarajiao tena na kuutumaini katika kufuzu kwetu usio huu. Balaa zote za kutuletea maafa hapo kesho (Akhera) tuziepuke na tuwe mbali kabisa nazo.
Katika mwezi huu hakuna masingizio yoyote, ambayo tunaweza kujisingizia nayo kama vile kudai kwamba 'O'..... Shetani ametushika sana! Kwani Mtume(s.a.w.
w
)
ametudokezea kwamba, "Mwezi wa Ramadhani unapoingia, milango yote ya rehema huwa wazi (kuwapokea wanaotaka kuingia), milango yote ya Jahannam hufungwa na Mashetani wote hutiwa minyororo ili wasiwahangaishe."
Ajabu kubwa zaidi ni kijana wa Kiislamu kuvaa ushanga, mikufu na bangili namna wafanyavyo wanawake. Ni hadi lini watajisitahi na kuwa na haya juu ya haya wayafanyayo?
Ni aibu kubwa kwa vijana wa Kiislamu kuhalifu sheria za dini yao hasa katika mwezi huu. Kwa kila aliye na uchunguzi, atastaajabu sana kumwona mtu aliyekuwa mnyenyekevu mchana kutwa, msalihina, kubadili hali hiyo na kuufanya usiku kuwa sitara ili kumdumishia maasi yake.
Ikiwa hawatajinasihi katika muda huu wa rehma na maghfira wakumbuke kuwa wamo hatarini ya kupoteza imani.
Badala ya kuketi mabarazani kusengenyana na kufitiniana, tunahimizwa kuingia misikitini na kuendesha ibada mbali mbali na tukisome kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa wingi yaani Qur'ani. Kwani pasi na kufanya hivyo, tutakuwa tunaupoteza wakati wetu ambao ni wa thamani sana kama ilivyopokelewa katika kauli za wahenga wa kiarabu kwamba: 'Wakati ni kama upanga, usipouvunja, (mwishowe) utakukata.'
KWA AKINA DADA
Dada wapendwa wa Kiislamu, mwezi mtukufu wa Ramadhani hutujia mara moja tu kwa mwaka. Tunapokaribia kuumaliza mwezi wa Sha’bani, huwa na furaha tele nyoyoni mwetu ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhani. Na kwa wakati huu hatunalo ila kumshukuru Mumba wetu aliyetuongoza kwenye njia yake nyofu (ya Kusilimu), maana lau si Yeye, kamwe hatungeongoka.
Dada wapendwa, tunapaswa kukumbuka kwamba, kufunga siyo kutozingatia kula na kunywa tu na hatimaye kutayarisha futari, bali kufunga kunakotakikana ni kuzingatia maamrisho yake Sub'haanuhu Wata’ala na Mtumewe(s.a.w.
w
).
Miongoni mwa maamrisho yake kwetu ni kuwatii waume zetu kwani Mwenyezi Mungu hako tayari kuzipokea Saumu zetu tukiwa na ufidhuli kwa waume zetu kwani Mola wetu Anatuambia katika Qur'ani:"Waume ndio wasimamizi wa wanawake."
Naye Mtume(s.a.w.
w
)
anasema kutufunza namna ya kutunza nyumba zetu kwamba"Mwanamke akifunga Saumu yake ya wajibu, asali sala zake fardhi na amtii mumewe, bila shaka ataingia peponi."
Huo ndio wajibu wetu. Ama mtindo wa kuwasengenya wenzetu, majirani zetu, waume zetu, au waume wa wenzetu ni kinyume cha dini ya Islam, na wakati wowote ule haitakikani kuendesha mikutano ya namna hii, na hasa katika Ramadhani, maana yanaweza kukuharibia Saumu yako.
Pia kujifahiri kubughudhiana, kukaripiana, kunyimana vifaa vya nyumbani kama shoka, chumvi, mwiko n.k. na kujiunga katika makundi ya karata hasa na waume ni dhambi isiyosameheka ila kwa kutubia hasa wakati kama huu wa Ramadhani.
JICHAGULIE MWENYEWE
Sote tukiwa Waislamu halisi na walio na gheri juu ya dini yetu tunapaswa kujihifadhi na kuutambua umuhimu wa uwajibu wetu. Katika Saumu hii ambayo huendelea nayo kila mwaka, tunapaswa kutambua kwamba wafungao wako makundi tofauti kadha wa kadha.
1. Wako watu ambao wao ni vijana wa Kiislamu, lakini kwa bahati mbaya wao hawajali na wala hawafungi kamwe wakidai eti kufunga kulianzishwa na Masheikh waliokuwa hawana chakula, na kwamba mtu aliye na chakula kufunga ni kama upumbavu.
2. Wapo watu wafungao lakini wao hufungana kujizuia chakula tu na kutotangamana na wake michana ya Ramadhani, ama katika mambo mengine wao huwa hawajali; kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika, huku wakiwa wamejisahaulisha kuwa hayo ni miongoni mwa yafuturishayo.
3. Kundi jengine hufunga na kufanya baadhi ya yatakikanayo, lakini huwa wao ni wenye kukereka na Saumu, na huwa wao ni wenye kuomba na kutaka Saumu imalizike haraka.
4. Kundi hili hufunga tena kwa unyenyekevu na hushinda misikitini, lakini ufikapo usiku ama Ramadhani imalizikapo, huanza vioja na kuanza upya kuyarejelea yaliyokuwa marufuku nyakati za Ramadhani, basi watu wa namna hii, ni sawa na mtu aliyeweka akiba ya Sh. 5000/- asubuhi, ili zimfae baadaye atakapopatwa na dhiki ya ghafla, na ufikapo usiku huzitumia zote katika starehe zisizo za lazima na kutobakisha kitu.
5. Wa mwisho, ni wale wafungao kwa Imani kamili na baada ya Ramadhani kumalizika wanaendelea na majonzi ya kusikitika kwani hawajui kama watajaaliwa tena kuifikia Ramadhani nyengine. Kundi hili ndilo la wafungao kikweli wajulikanao kama "Mo’ominoon" - yaani waumini halisi.
Ndugu mpendwa, unatakiwa kujikagua ili ujuwe kundi ulimo hivi sasa, la sivyo, kiri kutojitambua wewe mwenyewe.
Tunawatakieni nyinyi na sisi mwisho mwema ili tufungapo, tuimalize Saumu kwa baraka na amani ili iishapo tuwe kuendelea na utu wetu.
'SAUMU' KATIKA BIBLIA
Saumu kama ilivyopokewa katika Qur'ani kadhalika imepokewa katika vitabu vya dini mbali mbali.
Kulingana na ushahidi wa Aya tuliyoitaja huko nyuma inayosema "Enyi mlioamini, mmefaradhiwa kufunga kama walivyofaradhiwa wa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu! Ulazima wa Saumu kwa watu wote wa leo na wa kale umethibiti”
Ingawa katika Aya hiyo Mwenyezi Mungu atujulisha kama, jee Saumu tuliyofaradhiwa sisi ndiyo ile ile na kwa namna ile ile na kwa idadi zile zile walizofaradhiwa wa kabla yetu ama kwa namna iliyo tofauti? Hata hivyo si lazima juu yetu kujua.
Na Mwenyezi Mungu alitujulisha hili ili tusiwe na malalamiko (kama ilivyo ada ya mwanadamu) kuwa, kwa nini sisi tulazimishwe Saumu na hali wa kabla yetu hawakufunga na hali wao ni waja kama sisi? Ndiyo maana Akatujulisha mapema kabla ya nyudhuru zetu kutolewa. Ingawa ndugu zetu Wakristo wanatambua wazi Fardhi hii, kwa bahati mbaya wao hawakuijali bali wameyashughulikia mengine.
Hebu na tuangalie katika kitabu chao (Biblia - Agano jipya).
Katika Mathayo 6, kifungu cha 16 hadi 18 kumeandikwa hivi: "Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana, maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo jipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini na Baba yako aonaye sirini atakujazi."
Pia katika Mathayo 4, kifungu cha 1-2 imeandikwa hivi: "Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Iblisi. Akafunga siku Arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa."
Ndugu mpendwa, jee pana udhuru wowote tena wa kutofunga kwa Wakristo baada ya ushahidi huu? Jee inafaa kutumia mbinu zozote zile za ulaghai ili kuupuza maamrisho ya Allah? Jee inasihi mtu kutangatanga mabarabarani akinadi kwa kila namna ya vishindo eti "Mimi nimeokoka.....Mimi nimeokoka..." Na hali anaihepa Saumu? Hasha Wakalla.......hilo haliwi.