HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU 0%

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU Mwandishi:
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi: Tarehe

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi: Jopo La Waandishi Wa Vitabu Vya Kiada
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi:

Matembeleo: 9802
Pakua: 4352

Maelezo zaidi:

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9802 / Pakua: 4352
Kiwango Kiwango Kiwango
 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi:
Swahili

SOMO LA NANE: URITHI WA MBORA WA MITUME

AKILI NA UKAMILIFU WA MWANADAMU

Mtume(s.a.w.w ) alielezea kuhusu akili, majukumu yake na nafasi yake katika maamrisho na majukumu ya mwanadamu, nafasi yake katika matendo na malipo, hivyo akabainisha sababu za kukua na kukamilika kwa akili akasema: “Hakika akili ni kitanzi dhidi ya ujin- ga na nafsi ni sawa na mnyama mbaya, hivyo iwapo hakufungwa kitanzi hucharuka, basi akili ni kitanzi kuliko ujinga.

“Mwenyezi Mungu aliumba akili kisha akaiambia nenda mbele ikaenda mbele. Rudi nyuma, ikarudi nyuma. Hapo Mwenyezi Mungu akaiambia: Naapa kwa nguvu Zangu na utukufu Wangu, sikuumba kiumbe muhimu kuliko wewe, wala kitiifu kuliko wewe. Kupitia wewe nitaumba na nitarudisha, na kwa ajili yako nitalipa thawabu na nitaadhibu, hivyo uvumilivu ukatokana na akili, na elimu ikatokana na uvumilivu, na uongofu ukatokana na elimu. Utawa ukatokana na uongofu, na kujimiliki kukatokana na utawa, na aibu ikatokana na kujimiliki na heshima hutokana na haya.

“Heshima husababisha kudumu ndani ya heri na kuchukizwa na shari, hivyo kumtii mshauri kunatokana na kuchukizwa na shari. Haya ni makundi kumi katika aina za kheri na katika kila kundi kuna aina kumi za kheri….”[123]

ELIMU NI UHAI WA NYOYO

Mtume(s.a.w.w ) alijali sana elimu na maarifa akabainisha nafasi ya elimu na jukumu lake katika maisha akasema: “Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila mwisilamu. Fuateni elimu toka kila sehemu mnayodhani mtaipata. Jifunzeni toka kwa wenyenayo hakika kujifunza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni wema na kuitafuta ni ibada, kujikumbusha elimu hiyo ni tasbihi na kuitumia ni jihadi, kumfunza yule asiyejua ni sadaka na kuieneza kwa wahusika ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu elimu ndio alama ya halali na haramu, na minara ya watu wa peponi na ndio mfariji wakati wa upweke na rafiki wakati wa ugeni na upweke, na ndio msemeshaji wakati wa siri na upekee. Ni alama ijulishayo mambo ya siri na ya kudhuru, ni silaha dhidi ya maadui, na ni pambo kwa vipenzi.

Mwenyezi Mungu huwainua watu kupitia elimu, hivyo huwafanya viongozi bora ambao athari zao hunufaisha na vitendo vyao hufuatwa, mawazo yao hutegemewa huku malaika wakipenda urafiki wao, huwapangusa kwa mbawa zao na huwabariki katika Swala zao. Kila kibichi na kikavu huwaombea msamaha. Pia viumbe vya baharini na nchi kavu, kuanzia vidogo hadi vikubwa navyo huwaombea msamaha.

Hakika elimu ni uhai wa moyo dhidi ya ujinga na ni nuru ya macho dhidi ya kiza na ni nguvu ya mwili dhidi ya udhaifu. Humfikisha mja nafasi ya wenye heri na vikao vya watu wema na daraja la juu hapa duniani na huko Akhera. Kuitaja tu huwa sawa na kufunga, na kuisoma ni sawa na kusali Swala za usiku. Kupitia elimu Mola hutiiwa na undugu huunganishwa na haramu na halali hujulikana. Elimu huwa mbele ya vitendo na vitendo hufuata elimu.

Mwenyezi Mungu huwapa watu wema na huwanyima waovu, hivyo ni jambo zuri sana kwa yule ambaye hajanyimwa na Mwenyezi Mungu fungu lolote la elimu. Sifa ya mwenye akili ni kumvumilia asiyejua na kumsamehe aliyemdhulumu, kumnyenyekea aliye chini yake na kushindana katika kutafuta wema dhidi ya yule aliye juu yake.

Anapotaka kuzungumza, kwanza hufikiri hivyo kama ni la heri huzungumza na kufaidika, na kama ni la shari hunyamaza na kusal- imika. Iwapo utamfika mtihani hushikamana na Mwenyezi Mungu na huzuia mkono na ulimi wake. Aonapo jambo bora hulichangamkia na hapo aibu haimzuii wala tamaa haimpeleki pupa. Basi hizo ndio sifa kumi hujulikana kwazo mtu mwenye akili.

Sifa ya mjinga ni kumdhulumu anayechanganyikana naye, kumdhulumu aliye chini yake, kumfanyia kiburi aliye juu yake. Huongea bila kufikiri, na akiongea hutenda dhambi na akinyamaza husahau. Iwapo utamfika mtihani basi huuendea pupa na kumcharua.

Huwa mzito aonapo jambo la heri huku akijitenga nalo, hana khofu dhidi ya dhambi zake za mwanzo wala hatetemeki dhidi ya umri wake uliyobaki na dhambi alizonazo. Huwa mzito na mwenye kuchelewa dhidi ya jambo la heri. Hasikitikii heri yoyote iliyompita au aliyoipoteza. Hizo ni sifa kumi za mjinga ambazo akili imenyimwa.”[124]

VIZITO VIWILI: KITABU NA KIZAZI (AHLUL-BAYT)

Mtume(s.a.w.w ) aliwachorea watu njia ya wema wa kweli akawapa dhamana ya kuufikia wema huo iwapo tu watashikamana kwa ukamilifu na mafunzo aliyoyabainisha, hivyo akawapa ufupi wa njia ya wema ambayo inawakilishwa na kitendo cha kushikamana na asili na misingi miwili ambayo hutegemeana nayo ni: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi chake, Akasema:

“Enyi watu, hakika mimi nawatangulia nanyi mtanikuta katika hodhi. Fahamuni kuwa mimi nitawauliza kuhusu vizito viwili, hivyo angalieni jinsi gani mtahusika navyo baada yangu. Hakika Mpole mtoa habari amenipa habari kuwa: Hakika hivyo viwili havitoachana mpaka vinikute. Nilimwomba Mola Wangu hivyo na akanipa. Fahamuni hakika mimi nimewaachieni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-Bayt, hivyo msiwatangulie mtafarikiana, wala msiwaache mtaangamia na wala msiwafunze hakika wao ni wajuzi zaidi yenu. Enyi watu! Msiwe makafiri baada yangu ikawa baadhi yenu wanawauwa wengine hivyo mkanikuta huku mkiwa kundi dogo kama mfereji wa maji uliyoacha njia. Fahamuni kuwa Ali bin Abu Talib ni ndugu yangu na wasii wangu, atapigania tafsiri ya Qur’ani baada yangu kama nilivyopigania uteremkaji wake.”[125]

MAWAIDHA FASAHA

Mtume(s.a.w.w ) ambaye mwenendo wake ni fasaha tupu ana semi fupifupi ambazo ni alama ya ufasaha wake, hivyo miongoni mwa mawaidha yake ni:

“Enyi watu, mazungumzo ya kweli kabisa ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na shikio imara ni neno la uchamungu, na mila bora kabisa ni mila ya Ibrahim, na mwenendo bora kabisa ni mwenendo wa Muhammad, na mazungumzo matukufu kabisa ni kumtaja Mwenyezi Mungu.

“Visa vizuri sana ni visa vya Qur’ani, mambo bora ni maamrisho na mambo mabaya ni bidaa. Uongofu bora kabisa ni uongofu wa manabii, kifo bora ni kifo cha mashahidi, upofu zaidi ni kupotea baada ya kuongoka. Kazi bora ni ile yenye kunufaisha, na uongofu bora ni ule wenye kufuatwa. Upofu mbaya ni upofu wa moyo, na mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Kichache kinachotosheleza ni bora kuliko kingi kisichofaa.

“Msamaha mbaya ni ule uombwao wakati kifo kimefika na majuto mabaya ni majuto ya siku ya Kiyama. Kati ya makosa makubwa ya ulimi ni uongo. Utajiri bora ni utajiri wa nafsi na maandalizi bora ya safari ni uchamungu. Msingi wa busara ni kumwogopa Mwenyezi Mungu na jambo bora uliyopewa moyo ni yakini. Kilevi husababisha moto, na pombe ni mkusanyiko wa mikasa yote. Wanawake ni kamba za ibilisi na ujana ni tawi la uwendawazimu.

“Chumo baya zaidi ni riba, na chakula kibaya zaidi ni kula mali ya yatima. Mwema ni yule anayewaidhika kupitia mwenzake. Hakika kila mmoja wenu atawekwa ndani ya dhiraa nne (Kaburini). Kipimo cha vitendo ni mwisho wake na kila lijalo basi liko karibu. Kumtukana muumini ni ufasiki na kumuua ni ukafiri. Kumla nyama yake (kumsengenya) ni maasi na mali yake imeharamishwa kama ilivyoharamishwa damu yake.

“Atakayemuomba Mwenyezi Mungu msamaha basi Mwenyezi Mungu atamsamehe. Atakayesamehe basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na atakayevumilia katika msiba basi Mwenyezi Mungu atampa badala.”[126]

MUHTASARI

Mtume(s.a.w.w ) ni mfano hai wa ukamilifu wa mwanadamu. Pia urithi wake ndio wenye thamani baada ya Qur’ani. Hakika yeye alikunywa toka chemchemu ya ufunuo mpaka akabubujisha ukamili- fu wake kwa wanadamu kwa kiwango kinachotosheleza kuwapeleka wanadamu mbele upande wa ukamilifu na kuwafikisha kileleni mwa ukamilifu.

Tumechagua mifano ya ufasaha wake na semi zake fasihi kuhusu akili, elimu na njia ya kufikia wema na ukamilifu. Tumechagua kwa kiwango ambacho kitawaangazia wenye kufuata njia yake, hivyo wale watafuta ukweli hawatojizuia kutumia madhumuni ya semi hizo.

SOMO LA TISA: DONDOO ZA MAISHA YA MBORA WA MAWASII

KIONGOZI WA WAUMINI ALI BIN ABU TALIB

Baada ya kifo cha nabii wa mwisho Muhammad(s.a.w.w ) uongozi wa Mwenyezi Mungu unaendelea kwa mawasii kumi na wawili toka kizazi chake. Kizazi ambacho Mwenyezi Mungu alikitakasa na kukiondolea uchafu nao ni Maimam wema waongozaji upande wa haki na makhalifa wema ambao Mtume(s.a.w.w ) aliwaacha pamoja na Qur’ani tukufu. Akauambia umma wake ushikamane navyo pamoja ili wapate mafanikio na wema hapa duniani na kesho Akhera. Imam Ali bin Abu Talib(a.s ) ndiye Imam wa kwanza kati ya Maimam vion- gozi wema na kati ya makhalifa wa Mwenyezi Mungu na watawala Wake katika ardhi Wake.

Mtume(s.a.w.w ) alitoa maelezo juu ya uimamu wake,[127] hiyo ni baada ya kumlea yeye mwenyewe na kumpandikiza elimu yake, sifa zake nzuri na maadili yake mazuri. Akafahamika kwa kufuata haki, jihadi yake, kujitolea kwake, kumwabudu Mwenyezi Mungu na kupenda kuhami ujumbe wa Mola Wake. Hivyo akamkabidhi jukumu baada ya kuubainishia umma jinsi yeye anavyostahiki na kufaa cheo hiki cha uwasii na uongozi. Alibainisha hayo tangu mwanzo wa utume wake uliobarikiwa.

Imam Ali aliwatangulia maswahaba wote katika kuukubali ujumbe wa Mwenyezi Mungu huku akiwatangulia ndugu wote wa karibu wa Mtume(s.a.w.w ) katika kumsaidia Mtume(s.a.w.w ) .[128] Akamhami katika kipindi chote cha zama za Makka.[129] Akalala kitandani kwa Mtume(s.a.w.w ) usiku wa kuhama[130] huku akifidia nafsi yake dhidi ya nafsi ya Mtume(s.a.w.w ) . Aliendelea kuuhami Uislamu kipindi chote cha miaka yote ya matatizo[131] huku akitii amri za Mtume katika kila jambo na kila sehemu.

KUKUA KWA IMAM ALI BIN ABU TALIB NA HATUA ZA MAISHA YAKE

NASABA YAKE ING’AAYO

Imam Ali(a.s ) ametokana na kuzaliwa na wazazi wawili watukufu watakasifu ambao hawajachafuliwa na shirki wala uchafu wa kijahiliya. Imam Ali(a.s ) amesema:

“Naapa kwa Mwenyezi Mungu baba yangu wala babu yangu Abdul Muttalib wala Hashim wala Abdul Manafi katu hawakuabudu sanamu……. Walikuwa wakiswali wakielekea Al-Kaaba kwa kufuata dini ya Ibrahim huku wakishika- mana nayo[132] .Hivyo baba ni Abu Talib na jina lake ni Abdu Manafi. Babu ni Abdul Mutalib na jina lake ni Shaybatul-hamdi. Babu wa baba yake ni Hashim na jina lake ni Amru mtoto wa Abdu Manafi na jina lake ni Al-Mughira mtoto wa Quswayyi mtoto wa Kilabi mtoto wa Murrat mtoto wa Luayyi mtoto wa Ghalib mtoto wa Fahri mtoto wa Malik mtoto wa An-Nadhar mtoto wa Kinanat mtoto wa Khuzaymat mtoto wa Mudrikat, mtoto wa Iliyasa, mtoto wa Mudhar, mtoto wa Nazar, mtoto wa Maaddi, mtoto wa Adinan. Adinan ana- tokana na Ismail mtoto wa Ibrahim kipenzi cha Mwenyezi Mungu.”

Abu Talib ni mdogo wa Abdullah mzazi wa Mtume(s.a.w.w ) kwa baba na mama. Alimlea Mtume(s.a.w.w ) utotoni mwake huku akimnusuru ukubwani, akamtetea na kumlinda huku akivumilia maudhi toka kwa mushrikina wa kiquraishi huku akimlinda dhidi yao.

Hivyo kwa ajili yake akapatwa na matatizo makubwa huku akikumbana na misukosuko mikali lakini akavumilia katika kumnusuru na kusimamisha jambo lake mpaka maquraishi wakakata tamaa dhidi ya Mtume(s.a.w.w ) kwani walikuwa wameshindwa mpaka alipofariki Abu Talib.

Hakuamrishwa kuhama isipokuwa baada ya kufariki Abu Talib. Abu Talib alikuwa muislamu asiyedhihirisha Uislamu wake, kwani laiti angekuwa akidhihirisha basi asingeweza kumnusuru Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) kikamilifu kama alivyomnusuru.

Zaidi ya hapo ni kuwa Abu Talib alikubali usahihi wa unabii wa Mtume(s.a.w.w ) mara nyingi katika mashairi yake mfano kauli yake: “Ukanilingania nami nikajua kuwa wewe ni mkweli. Umesema kweli na kabla ya hapo ulikuwa mwaminifu. Nilijua kuwa dini ya Muhammad ni dini bora kati ya dini zote za mwanadamu”.[133]

Mama yake ni Fatima binti Asad bin Hashim bin Abdul Manafi bin Quswayyi.Yeye ndiye binti wa kwanza toka familia ya Hahim aliyezaa na kijana wa familia ya Hashim. Imam Ali(a.s ) alikuwa ndiye mtoto wake mdogo kati ya watoto wake ambao ni Jafar, Aqil na Talib. Mama yake aliukubali Uislamu baada ya watu kumi wa mwanzo.

Mtume(s.a.w.w ) alikuwa akimkirimu na kumtukuza huku akimwita: Mama yangu. Na alipokaribiwa na umauti alimuusia Mtume(s.a.w.w ) na Mtume akakubali usia wake na hivyo akamsalia na kumshusha ndani ya mwanandani na kumlaza humo, hayo ni baada ya kumvisha kanzu yake (ya Mtume). Hapo maswahaba zake wakamwambia: “Hatujaona ukifanya kwa yeyote mfano wa uliyofanya kwake.” Akajibu: “Hakuna mtu aliyekuwa mwema kwangu baada ya Abu Talib zaidi yake. Hakika nimemvisha kanzu yangu ili avishwe mapambo ya peponi, na nimemlaza na kanzu hiyo ili uzito wa kaburi uwe mwepesi kwake.”[134]

Al-Mufid na At-Tabariy wameongeza kuwa: “Mtume(s.a.w.w ) alimtamkisha akiri utawala wa mwanae Ali(a.s ) . Riwaya hiyo ni maarufu.[135] Na yeye ndiye mwanamke wa kwanza aliyetoa kiapo cha utii kwa Mtume wa Mwenyezi Mumgu(s.a.w.w ) kati ya wanawake wote.[136]

KUZALIWA KWAKE KULIKOBARIKIWA

Mashuhuri ni kuwa alizaliwa Makka ndani ya Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu (Al-Kaaba), siku ya Ijumaa, siku ya kumi na tatu ya mfungo kumi (Rajab) mwaka wa thelathini tangu kutokea kwa tukio la mwaka wa tembo.[137]

Al-Hakim An-Nisabury amesema: “Zimeenea habari kuwa Fatima binti Asad alimzaa kiongozi wa waumini Ali bin Abu Talib ndani ya Al-Kaaba.”[138]

Al-Mufid na wenzake wamesema: “Hakuzaliwa yeyote yule ndani ya Al-Kaaba kabla yake wala baada yake. Mwenyezi Mungu alifanya hivyo kwa ajili ya kumpa heshima na kutukuza nafasi yake.”[139]

Mama wa Ammarat binti Ubadat amesema: “Abu Talib alimshika mkono Fatima binti Asad akaenda naye Kaaba kisha akamwambia: “Kaa kwa jina la Mwenyezi Mungu,” hapo akapatwa na uchungu kisha akajifungua kijana mwenye furaha msafi aliyesafika ambaye sijamwona mwingine kwa uzuri wa uso wake. Hapo akamwita jina, Ali, na Mtume(s.a.w.w ) akambeba mpaka nyumbani kwa Fatima.[140]

KUPEWA JINA NA LAKABU ZAKE

Ibnu Abul-Hadid na wenzake wamesema: “Hakika jina lake la kwanza aliloitwa na mama yake ni Haydar (Simba) likiwa ni jina la babu yake, yaani baba wa mama yake Asad (Simba) bin Hashim. Ndipo baba yake akambadili jina na kumwita Ali.”[141]

Mtume(s.a.w.w ) akampa kuniya ya Abu-Turab, hiyo ni baada ya kumuona yuko katika hali ya sijida huku uso wake umo ndani ya udongo. Jina hili ndilo alilolipenda sana yeye mwenyewe.[142]

Mwanawe Hasan(a.s ) wakati wa uhai wa Mtume(s.a.w.w ) alikuwa akimwita baba Husain. Huku mwanae Husain akimwita baba Hasan. Pia aliitwa baba wa wajukuu wawili na baba wa manukato mawili. Mtume alimpa lakabu ya: Kiongozi wa waumini (Amirul-Mu’minin), huku muhajirina na ansari wakimwita kwa lakabu hiyo[143] .

Pia alipewa lakabu ya Mteule {Al-Murtadha}, walii wa Mwenyezi Mungu, kipenzi cha Mwenyezi Mungu, wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Simba wa Mwenyezi Mungu, upanga wa Mwenyezi Mungu, ndugu wa Mtume, bwana wa waarabu, kijana wa kiquraishi, mgawa pepo na moto, Lango wa Jiji la Elimu, bwana wa waislam, jemedari wa waumini, kiongozi wa kundi mashuhuri, Imam wa wachamungu na mkweli mno.

Baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w ) lakabu yake mashuhuri ilikuwa ni wasii.18 Lakabu hii ilikuwa mashuhuri kwake tangu mwanzo, hivyo ikaenea sana mpaka ikachukua nafasi ndani ya vitabu vya lugha mfano: Lisanul-Arab, Tajul-Urus na vinginevyo. Wasomi (Baadhi) wa kisunni walijitahidi sana kutaka kuficha habari za uwasii wake na kutaka kuleta tafsiri nyingine kinyume na ile iliyoenea.[144]

MALEZI NA MAKUZI YAKE

Haraka sana Mtume(s.a.w.w ) alimtilia umuhimu maalumu Imam Ali bin Abu Talib(a.s ) , alimpenda sana na kumwambia mama yake: “Weka kitanda chake karibu na kitanda changu.” Mtume alikuwa akitawala sana malezi yake, hivyo alikuwa akimtoharisha Ali wakati wa kuogeshwa na akimuwekea maziwa mdomoni wakati wa kunywa maziwa.

Alichezesha kitanda chake wakati wa kulala huku akimbembeleza awapo macho. Akimbeba kifuani kwake na shingoni huku akisema: “Huyu ni ndugu yangu, walii wangu, mwenye kuninusuru, mteule wangu, tegemeo langu, kinga yangu, mkwe wangu, wasii wangu, mme wa binti yangu, wasii wangu na khalifa wangu mwaminifu”. Daima alikuwa akimbeba na kuzunguka nae katika milima na mabonde ya Makka.[145]

Imam Ali(a.s ) yeye mwenyewe amefafanua makuzi yake ya mfano ambayo yamejaa heshima kwa kiwango cha juu, akasema katika hotuba yake kuwa: “Mnajua nafasi yangu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ukaribu wa karibu na nafasi mahsusi niliyonayo kwake. Alinilea nikiwa mtoto akinikumbatia kifuani mwake na kitandani kwake. Akinigusisha mwili wake, akininusisha harufu yake. Alikuwa akitafuna kitu kisha akinilisha, hakupata uongo wa kauli yoyote toka kwangu, wala kosa lolote la kitendo.

Nilikuwa nikimfuata kama mtoto aliyeachishwa ziwa amfatavyo mama yake, huku kila siku akiniinua juu kwa kuniongezea sehemu ya maadili yake huku akiniamrisha kumfuata. Kila mwaka alikuwa akienda pango la Hira hakuna anayemuona isipokuwa mimi tu. Wala hakuna nyumba hata moja kipindi hicho iliyokuwa imekusanya waislam wasiyokuwa Mtume, Khadija na mimi nikiwa watatu wao, nikiona nuru ya wahyi na utume huku nikinusa harufu ya unabii.

Nilisikia mlio wa shetani pindi wahyi ulipomshukia Mtume, nikase- ma: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni sauti ya nini hii?” Akajibu: “Huyu ni shetani amekata tamaa dhidi ya kuabudiwa, hakika wewe unasikia ninayosikia na unaona nionayo isipokuwa wewe si nabii lakini wewe ni waziri na hakika wewe upo juu ya heri.”[146]

HATUA ZA MAISHA YAKE

Kuanzia alipozaliwa mpaka Mtume(s .a.w.w ) alipopewa utume, nacho ni kipindi cha miaka kumi. Kisha kipindi cha miaka kumi kuanzia alipopewa Mtume(s.a.w.w ) utume mpaka alipohama.

Kisha kipindi cha miaka kumi mpaka alipofariki Mtume(s.a.w.w) . Kisha miaka ishirini na tano mpaka kumalizika utawala wa Uthmani. Kisha miaka mitano ambayo ndio muda wa serikali yake.

MUHTASARI

Ali bin Abu Talib(a.s ) alitokana na asili ile ile aliyotokana nayo Mtume(s.a.w.w ) hivyo nasaba yake na nasaba ya Mtume(s.a.w.w ) ni moja.

Ali(a.s ) alitofautiana na maswahaba wengine kwani hakuna shirki yoyote iliyomuingia. Kisha akawa ni mtu mahsusi kwa Mtume(s.a.w.w ) hivyo akawa akimfunza mafunzo yatokanayo na hekima za Mwenyezi Mungu na elimu ya Mola Wake, jambo ambalo hakulipata swahaba mwingine yeyote.

Ali( a.s ) alidhihirisha utiifu na ufuataji kamilifu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake(s.a.w.w ) , akajipamba kwa maadili mazuri, akajitolea nafsi na kila lenye thamani kwa ajili ya itikadi ya Uislamu.

Mwenyezi Mungu alimteua awe wasii wa Mtume Wake(s .a.w.w ) hivyo akasimamia jukumu la uwasii kwa ukamilifu mpaka adui akakiri hilo kabla ya rafiki.

Imam Ali(a.s ) alibeba majina na lakabu nzuri ambazo zinaonyesha jinsi alivyoshikamana sana na Mwenyezi Mungu na alivyokuwa na itikadi salama ya Mwenyezi Mungu na maadili bora mazuri.

SOMO LA KUMI: MWONEKANO WA UTU WA IMAM ALI BIN ABU TALIB (A.S)

Sifa za ukamilifu zilikusanyika kwa Imam Ali bin Abu Talib. Alikuwa na sifa nzuri za kusifika, mahsusi za kupendeza, nasaba bora na sharafu tukufu, asili takatifu na nafasi yenye kuridhiwa. Sifa ambazo hakubahatika kuzipata mtu yeyote mwingine, kwani yeye ni jemedari wa waumini, mbora wa mawasii na khalifa wa kwanza wa Mtume(s.a.w.w ) kati ya makhalifa waongozao kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Maelezo ya Mtume(s.a.w.w ) na Qur’ani tukufu vimeeleza wazi kuhusu umaasumu wake dhidi ya kila uchafu.[147] Mtume(s.a.w.w ) akaapizana na wakristo wa Najran kupitia yeye, mkewe, na wanawe wawili.[148]

Pia alimfanya ni kati ya ndugu zake wa karibu ambao tumewajibishwa kuwapenda[149] huku mara kwa mara Mtume(s.a.w.w ) akitueleza wazi kuwa wao ni sawa na Kitabu kitukufu,[150] hivyo huokoka yule atakayevishika viwili hivyo na huangamia yule atakayeviacha.

Imam Ali bin Abu Talib(a.s ) aliishi zama za Mtume(s.a.w.w ) na utume, kuanzia pale ufunuo ulipoanza kushuka mpaka ulipokatika kwa kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) huku akiwa na nafasi ya juu ambayo hutamaniwa. Nayo ni katika kumhami Mtume(s.a.w.w ) na utume muda wote wa miaka ishirini na tatu, ikiwa ni jihadi yenye kuendelea na mapambano endelevu ya kuhami Uislamu na tukufu zake. Hivyo misimamo yake, utendaji wake na sifa zake vimejiakisi katika Aya za Kitabu kitukufu na maelezo ya hadithi za Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) .

Ibnu Abbas amesema: “Ziliteremka Aya mia tatu kuhusu fadhila za Ali(a.s ) ,[151] hakuna Aya iliyoteremka na ibara ya: “Enyi mlioamini” isipokuwa Ali(a.s ) ndio kiongozi na mlengwa wa mwanzo katika Aya hiyo. [152] 6 Hakika Mwenyezi Mungu amewalaumu wafuasi wa Muhammad katika baadhi ya Aya za Qur’ani lakini hakumtaja Ali (a.s ) isipokuwa kwa heri.”[153]

Kutokana na kukithiri Aya zilizoteremka kuhusu fadhila za Ali(a.s ) baadhi ya wasomi wa zamani wameandika vitabu mahsusi ambavyo vimekusanya Aya zilizoteremshwa kwa ajili yake. Hivyo hapa tutaashiria baadhi ya Aya ambazo wanahadithi wameeleza wazi kuwa ziliteremshwa kwa ajili yake.

Imepokewa kutoka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Ali(a.s ) alikuwa na dirhamu nne tu huku akiwa hana nyingine, hivyo usiku akatoa sadaka dirhamu moja, mchana dirhamu moja, na dirhamu nyingine akaitoa sadaka kwa siri na nyingine kwa dhahiri, hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya isemayo: “Wale watoao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, basi wana malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.”[154]

Ibnu Abbas amesema: “Ali(a.s ) alitoa sadaka pete yake huku akiwa katika hali ya rukuu. Mtume(s.a.w.w ) akamuuliza mwombaji: “Ni nani aliyekupa pete hii?” Akajibu: “Ni yule aliye katika hali ya rukuu, hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya isemayo: “Hakika kiongozi wenu khasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka na hali ya kuwa wamerukuu.”[155]

Aya ya utakaso10 imemfanya Ali(a.s ) kuwa kati ya Ahlul-Bayt wa Mtume(s.a.w.w ) ambao wametakaswa dhidi ya kila uchafu, huku Aya ya maapizano[156] ikimfanya kuwa nafsi ya Mtume(s.a.w.w ) .

Ama Sura Insan imeashiria ukunjufu wa moyo aliyonao Ali(a.s ) na watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w ) na jinsi wanavyomwogopa Mwenyezi Mungu. Pia imebeba ushahidi wa Mwenyezi Mungu kuthibitisha kuwa wao ni watu wa peponi.[157]

Waandishi wa vitabu Sahihi sita na wengineo miongoni mwa wanazuoni wa hadithi wametenga milango mahsusi ndani ya vitabu vyao inayoelezea fadhila za Imam Ali(a.s ) kupitia hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Wanadamu ndani ya historia yao ya muda mrefu hawajamwona mtu bora kuliko Ali(a.s ) baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) . Wala hakuna mtu ambaye fadhila zake zimeandikwa kama zilivyoandikwa fadhila za Imam Ali(a.s ) .

Japokuwa muda wote wa utawala wa kizazi cha Umayya maadui na wanafiki walimwelekezea matusi na kashfa juu ya mimbari zao wakiwa na lengo la kumtia dosari, lakini hawakupata sehemu yoyote kwake yenye dosari na aibu.

Kati ya kauli za Umar bin Al-Khatab ni: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema: ‘Hakuchuma mchumaji mfano wa fadhila za Ali, kwani yeye humwongoza mfuasi wake kwenye uongofu na humzuwia dhidi ya maangamio.”[158]

Imam Ali(a.s) aliulizwa: “Kwa nini wewe una Hadithi nyingi kuliko maswahaba wengine wa Mtume(s.a.w.w ) ?” Akajibu: Hakika mimi nilikuwa nimuulizapo ananijibu, na ninyamazapo hunianza”.[159]

Imepokewa kutoka kwa Ibnu Umar kuwa: Siku Mtume(s.a.w.w ) ali- pounga undugu kati ya maswahaba zake, Ali alikuja huku macho yake yakidondoka machozi, hapo Mtume(s.a.w.w ) akamwambia Ali(a.s ) : “Wewe ni ndugu yangu hapa duniani na kesho Akhera.”[160]

Imepokewa kutoka kwa Abu Layla Al-Ghaffariy kuwa alisema: “Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) akisema: “Baada yangu itatokea fitina, basi ikitokea hali hiyo shikamaneni na Ali bin Abu Talib, hakika yeye ndiye wa kwanza kuniamini, na ndiye wa kwanza atakayenipa mkono siku ya Kiyama, yeye ni mkweli mno, na yeye ndiye atakayefarakisha kati ya haki na batili ya umma huu, yeye ndiye jemedari wa waumini na mali ndio jemedali wa wanafiki.”[161]

Makhalifa wote wamekiri kuwa Ali(a.s ) ndiye mjuzi zaidi kuliko maswahaba wote na ndiye anayefahamu sheria zaidi kuliko maswahaba wote, na kuwa laiti si Ali(a.s ) basi wangeangamia, mpaka ikafikia kauli ya Umar kuwa mfano halisi, nayo ni: “Laiti kama si Ali Umar angeangamia.”[162]

Imepokewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah Al-Answar kuwa alisema: “Tulikuwa hatuwatambui wanafiki isipokuwa kwa kumchukia Ali bin Abu Talib(a.s ) .”

Zilipomfikia Muawiya habari za kuuwawa Ali(a.s ) alisema: “Sheria na elimu yote imeondoka kwa kifo cha mwana wa Abu Talib.”[163]

As-Shaabiy amesema: “Ali bin Abu Talib ndani ya umma huu ni sawa na Masihi mwana wa Mariam kwa wana wa Israel: Kuna kundi lililompenda mpaka likakufuru ndani ya mapenzi yake, na kundi lingine likamchukia hivyo likakufuru kwa kumchukia.”19 Alikuwa mkarimu sana. Alikuwa na maadili ayapendayo Mwenyezi Mungu katika ukarimu, katu hakuwahi kumjibu mwombaji hapana sina.[164]

Swaa’swaa’ bin Swawhan alimwambia Ali bin Abu Talib siku aliy- opewa kiapo cha utii kuwa: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu ewe kion- gozi wa waumini! Hakika umeupamba ukhalifa lakini wenyewe haujakupamba, umeuinua lakini wenyewe haujakuinua, na wenyewe unakuhitajia sana kuliko wewe unavyouhitajia.”

Ibnu Shabramat amesema: “Hakuna mtu yeyote asiyekuwa Ali bin Abu Talib mwenye uwezo wa kusema juu ya mimbari: ‘Niulizeni.”[165]

Qaaqaa bin Zararat alisimama kaburini kwa Imam Ali(a.s ) kasha akasema: “Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe kiongozi wa waumini, naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hakika uhai wako ulikuwa ni ufunguo wa kheri, na laiti watu wangekukubali basi wangekula toka juu yao na toka chini ya miguu yao, lakini wao wameidharau neema na wakaijali sana dunia.”[166]

MUHTASARI

Imam Ali(a.s) alijitenga kwa kuwa na sifa mahsusi ambazo zilimtofautisha na maswahaba wengine, zikamwajibisha awashinde wote waliotaka kulingana nae miongoni mwa maswahaba na wasiokuwa maswahaba. Aya za Qur’ani zimejaa fadhila hizi za pekee huku maelezo ya Mtume(s.a.w.w) yakiashiria sifa hizi zilizomtofautisha Ali(a.s) na wengine.

Ushahidi wa maswahaba na waliokuja baada ya maswahaba unaashiria undani wa fadhila za Ali(a.s) ndani ya umma huu japokuwa watu wengi hawakufuata uimamu wa mtu huyu mtukufu.

SOMO LA KUMI NA MOJA: SIFA ZA IMAM ALI (A.S) NA MWONEKANO WAKE

KUIFUATA HAKI

Shakhsia ya Imam Ali(a.s ) ilikuwa na alama dhahiri ambayo ndio makusanyikio ya sifa zake zote na mazalisho ya ukamilifu wake wote, nayo ni kuifuata haki vyovyote itakavyokuwa na popote itakapokuwepo. Kufuata kwake haki kulipatikana tangu kipindi cha mwanzo cha uhai wake kwa kutii amri za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake(s.a.w.w ) bila mipaka.

Pia kujitokeza kwake daima katika kupambana kwa ajili ya malengo ya utume na uongozi uliotakasika, kumfuata nabii kiongozi kwa ukamilifu na kujijenga kiukamilifu kwa ajili ya amri zote za uongozi huu uliyonyooka.

Hivyo kwa ajili hii akastahiki kuwa khalifa wa Mtume(s.a.w.w ) , naibu mtekelezaji, na mwaminifu mwenye moyo mkunjufu katika kutimiza malengo ya Mtume(s.a.w.w ) na makusudio ya utume, kwani sifa zote nzuri za Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) zilipatikana vizuri kwa Imam Ali(a.s ) .

IBADA YAKE

Imam Ali(a.s ) amesema: “Hakika kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutamani, hakika hiyo ni ibada ya wafanya biashara. Na hakika kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuogopa, hakika hiyo ni ibada ya mtumwa. Na kuna watu wanamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumshukuru, hakika hiyo ni ibada ya watu huru.”[167]

Ibnu Abul-Hadid Al-Muutaziliy amesifia ibada ya Imam Ali(a.s ) kwa kusema: “Alikuwa ni mfanya ibada sana, mwenye kuswali na kufunga kuliko watu wote. Watu wamejifunza Swala za usiku, kushikamana na nyuradi na swala za Sunna kutoka kwake.

Unasemaje kuhusu mtu ambaye kutokana na kuhifadhi uradi wake amefikia kutandikiwa busati la ngozi usiku katikati ya vita siku ya usiku wa Hariri, akavuta uradi wake huku mishale ikidondoka mikononi mwake na mingine ikipita juu ya masikio yake kulia na kushoto lakini hatetemeshwi na hayo, wala hasimami mpaka amalize jukumu lake. Unasemaje kuhusu mtu ambaye kutokana na kurefusha sijida yake bapa lake la uso lilikuwa na sugu kama sugu za ngamia.?”

Ukifuatilia dua zake na minong’ono yake ukaelewa yaliyomo ndani, kuanzia jinsi anavyomtukuza Mwenyezi Mungu na kumtakasa, mpaka anavyonyenyekea kwa ajili ya haiba na utukufu wa Mwenyezi Mungu huku akimfuata kwa unyenyekevu, utajua ni jinsi gani alivyozungukwa na ikhlasi na utafahamu ni ndani ya moyo upi zimetoka dua hizo na ni kupitia ulimi gani imepatikana minong’ono hiyo.

UTAWA WAKE

Harun bin Antranti amepokea kutoka kwa baba yake kuwa alisema: “Niliingia kwa Imam Ali(a.s ) huko Al-Khawranaqi, yalikuwa majira ya masika nikamkuta kajifunika kitambaa chakavu. Nikamuuliza: Ewe kiongozi wa waumini, hakika Mwenyezi Mungu amekuwekea wewe na familia yako fungu katika mali hii, kisha wewe unajifanyia hivyo? Akajibu: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, sikupata chochote toka kwenu, wala sina chochote isipokuwa kipande hiki cha kitambaa ambacho nilikuwa nacho toka Madina.”[168]

Imam Ali(a.s ) alisikika akisema juu ya mimbari: “Ni nani atakayenunua upanga wangu huu? Laiti ningekuwa na thamani ya kununulia shuka basi nisingeuuza.” Hapo akasimama mtu na kusema: “Nakupa thamani ya shuka hivi sasa.”[169]

Mmoja wao akamletea Ali(a.s ) chakula kitamu kizuri lakini Ali(a.s ) hakukila, akakitazama na kusema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu ewe chakula una harufu nzuri, rangi ya kupendeza na ladha nzuri, lakini sipendi kuizoweza nafsi yangu mambo ambayo haijayazowea.”[170]

Mashuhuri ni kuwa Ali(a.s ) hakupandanisha tofali juu ya tofali wala nguzo juu ya nguzo. Alikataa kuishi ndani ya kasri la utawala ambalo lilikuwa limeandaliwa kwa ajili yake huko mji wa Kufa. Ibnu Abul- Hadid ameelezea utawa wa Imam Ali(a.s ) akasema: “Katu hakushiba chakula, na alikuwa mgumu wa kula na kuvaa, alikuwa akisema: “Msiyafanye matumbo yenu kuwa makaburi ya wanyama.”[171]

MSAMAHA NA UPOLE WAKE

Ibnu Abul-Hadid amesema: “Ama kuhusu upole na msamaha, alikuwa mpole sana anapokosewa na msamehevu sana dhidi ya mwenye kosa. Lilidhihirika hilo siku ya vita vya ngamia (Jamal), kwani alimshinda Mar’wan bin Al-Hakam ambaye alikuwa ndiye adui yake mkubwa na mwenye chuki sana dhidi ya Ali lakini Ali alisamehe.[172]

Watu wa Basra walimpiga vita wakaupiga uso wake na nyuso za wanawe kwa mapanga huku wakimkashifu, lakini alipowashinda hakuwauwa, bali akanadi msemaji wake katikati ya vikosi vya jeshi lake: “Sikilizeni, anayekimbia hafuatwi, aliye majeruhi hashambuliwi, aliyetekwa hauwawi, na yeyote atakayetupa silaha chini basi amesalimika. Pia atakayejiunga na askari wa Imam naye kasalimika”. Hakuchukua mizigo yao wala hakuteka watoto wao, wala hakuchukua chochote katika mali yao huku laiti angetaka kufanya hivyo angefanya lakini yeye aliacha kufanya hivyo ili atoe msamaha.

Pindi jeshi la Muawiya lilipomiliki na kuzingira pande zote za mto Furati, viongozi wa Sham waliamrisha jeshi kwa kusema: “Wauweni kwa kiu kama walivyomuuwa Uthman bin Affan kwa kiu.” Hapo Ali(a.s ) na maswahaba zake waliliomba jeshi liwaachie wanywe maji. Askari wakajibu: “Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu hapana, hatuwezi kuwapa hata tone moja la maji mpaka mfe kwa kiu kama alivyokufa mwana wa Affan.”

Imam Ali(a.s ) alipoona hakuna njia isipokuwa kifo aliwaongoza maswahaba zake na kuwashambulia askari wa Muawiya mashambulizi mazito mpaka akawaondoa toka kwenye vituo vyao, hivyo baada ya mauaji mazito ambayo yalidondosha vichwa na mikono mingi, Imam Ali(a.s ) alimiliki maji dhidi yao, na hapo askari wa Muawiya wakawa jangwani hawana maji.

Maswahaba na wafuasi wake wakamwambia: “Ewe kiongozi wa waumini wanyime maji kama walivyokunyima, wala usiwanyweshe hata tone moja, waue kwa upanga wa kiu na uwashike kwa mikono wala hauna haja ya kuendelea na vita.” Akajibu: “Hapana, naapa kwa Mwenyezi Mungu siwalipi mfano wa kitendo chao, waachieni baadha ya sehemu za kunywea maji, kwani ukali wa upanga unatosha.”

Hakika kitendo hiki ukikilinganisha na upole na usamehevu ni uzuri wa hali ya juu, na ukikilinganisha na dini na uchamungu basi hakuna budi mfano wa hili lifanywe na mtu kama yeye(a.s ) .”[173]

USHUJAA NA USHUPAVU WA IMAM (A.S)

Ibnu Abul-Hadid amezungumzia ushujaa wa Imam Ali(a.s ) akasema: “Hakika yeye aliwasahulisha watu kumbukumbu ya ushujaa wa wale waliyokuwa kabla yake. Msimamo wake vitani ni mashuhuri, hutolewa mfano mpaka siku ya Kiyama. Yeye ni shujaa ambaye katu hakukimbia wala hakutetereka dhidi ya maadui Wala hakuna aliyechomoza kupambana naye isipokuwa alimuuwa. Katu hakupiga pigo la kwanza kisha akahitajia la pili. Imepokewa ndani ya hadithi kuwa: Mapigo yake yalikuwa ni moja.[174]

Pindi Ali(a.s ) alipomwomba Muawiya achomoze kwenye mpam- bano ili watu wapumzike na vita kwa kuuawa mmoja wao, Amru alimwambia Muawiya: “Hakika kakufanyia uadilifu.” Hapo Muawiya akasema: “Hujawahi kunidanganya tangu uanze kuninasihi isipokuwa leo, yaani unaniamrisha niende kupambana na Abul Hasan ilihali wewe unajua fika kuwa ni shujaa asiyezuilika, naona unatamani utawala wa Sham baada yangu.”[175]

Waarabu walikuwa wakijifaharisha wasimamapo kupambana naye vitani, hivyo dada wa Amru bin Abdul Waddi alipokuwa akimlilia kaka yake alisema: “Laiti aliyemuuwa Amru angekuwa si huyu aliye- muuwa, basi ningelia milele maadamu bado nipo duniani. Lakini aliyemuuwa ni mtu asiyekuwa na mfano, na baba yake alikuwa akimwita: ‘Wa pekee asiye na mfano.”[176]

Ibnu Qutayba amesema: “Katu hakupambana na mtu isipokuwa alimshinda,[177] na yeye ndiye aliyeng’oa mlango wa Khaybari kisha likakusanyika kundi la watu ili waweze kuugeuza mlango huo hawakuweza kuugeuza. Na yeye ndiye aliyeng’oa sanamu la Hubal toka juu ya Al-Kaaba, sanamu ambalo lilikuwa kubwa sana lakini akaling’oa na kulitupa aridhini. Na yeye ndiye aliyeng’oa jabali kubwa kwa mkono wake zama za utawala wake yakatoka maji chini yake, hiyo ilikuwa ni baada ya jeshi zima kushindwa kung’oa jabali hilo.”[178]

KUJIZUWIA DHIDI YA DHULMA NA UJEURI

Imam Ali(a.s ) pamoja na nguvu zake zote zisizo na mfano na ushu- jaa wake wa pekee lakini alikuwa akijizuia kutokufanya dhulma na ujeuri vyovyote vile itakavyokuwa. Wanahistoria wote wamesema kuwa Ali(a.s ) alikuwa haanzi vita isipokuwa pale atakaposhambuli- wa. Alikuwa akiharakisha kusawazisha mambo kati yake na adui kupitia njia za amani ambazo zitazuwia umwagaji damu, hali hii ni hata kama mtu ataharakisha kumfanyia uadui. Hivyo mara nyingi alikuwa akikariri masikioni mwa mwanae Hasan kuwa: “Msiombe kupambana.”[179] .

Kwa kuwa kauli ya Imam haitoki isipokuwa kutoka kwenye madini safi basi mara zote alikuwa akitekeleza huu usia wake, hivyo alijizuwia kupigana isipokuwa pale alipolazimishwa. Kwa ajili hiyo pindi majeshi ya waasi (Khawariji) yalipoanza kujiandaa ili kumpiga na akatokea mtu mmoja kumnasihi Imam kuwa aanze kuwashambulia kabla hawajamshambulia, Imam alimjibu kwa kusema: “Siwapigi mpaka watakaponipiga.”[180]

MUHTASARI

Pindi tunaposoma kurasa za utu wa Imam Ali(a.s ) hakika tunakuwa tumeashiria kiasi tu kidogo kinachofikiriwa na akili zetu katika kufa- hamu nafasi ya Imam huyu maasumu. Kwani akili imeshindwa kujua utukufu wa mwanadamu huyu, hivyo baadhi zikavuka mipaka na kujikuta zimemshirikisha Mwenyezi Mungu, na nyingine zikapun- guza hivyo zikamchukia na kujikuta zimeritadi.

Imam Ali(a.s ) alikuwa mchamungu sana wala hakuna yeyote aliyemshinda kwa ibada, lakini yeye aliweka mfano bora wa uhusiano wa mja na muumba wake hivyo akatekeleza ibada kwa kiwango bora zaidi. Akatekeleza ibada ndani ya mwenendo wake wa kila siku, na mfumo wake wa malezi ambao unamjenga mwanadamu mchamungu na kumtengenezea ustaarabu wa kipekee wa kiislamu.

Imam Ali(a.s ) aliishi huku akiwa kajitenga mbali na ladha zote za dunia hii ya mpito, hilo ni kwa sababu aliijua vizuri dunia na akajua vizuri namna ya kujitenga nayo, hivyo akazidiriki neema za Mwenyezi Mungu ambazo hazilingani na neema nyingine yoyote ile.

Imam Ali(a.s ) alimtendea kila adui yake kwa heshima na adabu, kwa akili na imani, akitarajia kutengeneza umma na kuondoa uharibifu, huku akitaka kuamsha dhamira zilizo ndani ya nafsi zenye maradhi, hivyo akasamehe na kuwa mpole huku akijisahaulisha mabaya aliyotendewa, akasahau kulipiza kisasi japokuwa kulipiza huko ni haki yake.

Historia haijamfahamu mtu shujaa mwenye kuitetea imani ya Mwenyezi Mungu kama Imam Ali(a.s ) . Hakika alikuwa jasiri shujaa mwenye yakini asiyetetereka, shupavu asiyelainika, mwenye moyo usiojua khofu, hivyo akaupa ulimwengu wote sura dhahiri ya ukomandoo na ushujaa katika medani za kivita na katika kutekeleza jukumu gumu.

Kajizuia kufanya uadui ilikuwa ni msingi kati ya misingi ya mfumo wa Imam Ali(a.s ) katika maisha yake.