HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU 0%

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU Mwandishi:
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi: Tarehe

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi: Jopo La Waandishi Wa Vitabu Vya Kiada
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi:

Matembeleo: 9804
Pakua: 4352

Maelezo zaidi:

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9804 / Pakua: 4352
Kiwango Kiwango Kiwango
 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi:
Swahili

SOMO LA KUMI NA SITA: MWONEKANO WA UTU WA FATIMA AZ-ZAHRAU

Fatima Az-Zahrau(a.s ) ni binti wa nabii mtukufu na ni mke wa Imam mtukufu na ni mama wa wajukuu wawili Hasan na Husein mabwana wa vijana wa Peponi. Hakika yeye ni uso wenye kung’ara kwa ajili ya utume wa mwisho, na ni chombo safi kwa ajili ya kuendeleza kizazi kitakasifu, na ni chimbuko safi la kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) huku akiwa ni mbora wa wanawake wote ulimwenguni.

Historia yake ni sawa na historia ya utume kwani alizaliwa kabla ya Mtume(s.a.w.w ) kuhama, na akafariki miezi michache baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w ) .

Aya za Qur’ani tukufu ndani ya miongo hii miwili ya historia ya Uislamu zimebeba karama na fadhila za Az- Zahrau, baba yake, mumewe na wanawe ambao walitoa mfano bora wa jihadi, subira, moyo mkunjufu na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Ama upande wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) yeye alionyesha utukufu wa nafasi yake na daraja la kutamaniwa alilofikia katika njia ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu huku Mtume(s.a.w.w ) akienda sawia na njia ya Qur’ani katika kueleza karama na fadhila za Ahlul-Bayt wote kwa ujumla na kueleza karama na fadhila za moyo wa Mtume(s.a.w.w ) kwa upekee.[211]

AZ-ZAHRAU MBELE YA MBORA WA MITUME (S.A.W.W)

Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu hughadhibi- ka kwa kughadhibika Fatima na huridhia kwa kuridhia Fatima.”[212]

Mtume(s.a. w.w ) amesema: “Fatima ni pande la nyama yangu atakayemuudhi kaniudhi, na atakayempenda kanipenda.”[213]

Mtume(s.a.w.w ) amesema: “Fatima ni moyo na roho yangu inayonizunguka.”[214]

Mtume(s.a.w.w ) amesema: “Fatima ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni.”[215]

Ushahidi kama huu ni mwingi ndani ya vitabu vya hadithi na sira6 ukipokewa toka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) ambaye hatamki la matamanio yake7 wala hapendelei kwa sababu au nasaba, wala katika jambo la Mwenyezi Mungu haogopi lawama ya mwenye kulaumu.

Kwa kuwa Mtume mtukufu(s.a.w.w ) amezama ndani ya Uislamu na kwa sababu hiyo akawa ni kiigizo chema kwa watu wote ndio maana mapigo ya moyo wake, mtazamo wa macho yake, mpapaso wa mikono yake, hatua za utembeaji wake na mawazo ya fikira zake vyote vimekuwa ni mafunzo kati ya mafunzo ya dini, chanzo cha sheria, taa ya uongofu na njia ya uokovu.

Hakika ushahidi huu kutoka kwa hitimisho la mitume ni medali kwa Az-Zahrau, medali ambazo zinazidi kung’aa kila muda unavyokwenda, hasa pale tunapoangalia chanzo cha msingi ndani ya Uislamu kupitia maneno ya Mtume(s.a.w.w ) aliyomwambia Az-Zahrau kuwa:

“Ewe Fatima, tenda kwa ajili ya nafsi yako, hakika mimi sitokufaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.”[216]

Na kauli ya Mtume(s.a.w.w ) : “Katika wanaume wamekamilika wengi lakini kwa wanawake hawajakamilika isipokuwa Mariam binti Imran, Asia binti Muzahim mwanamke wa Firaun, Khadija binti Khuwaylid na Fatima binti Muhammad(s.a.w.w ) .”[217]

Na kauli ya Mtume(s.a.w.w ) : “Hakika Fatima ni tawi la moyo wangu hunichukiza yanayomchukiza na hunifurahisha yanayomfurahisha,[218] na hakika nasaba zote siku ya Kiyama zitakatika ila nasaba yangu, sababu yangu na ukwe wangu.”[219]

Imepokewa kuwa siku moja Mtume(s.a.w.w ) alitoka huku akiwa kamshika mkono Fatima akasema: “Anayemtambua huyu basi kishamtambua na asiyemtambua basi huyu ni Fatima binti Muhammad, na yeye ni kipande cha nyama yangu, na ni moyo wangu unaonizunguka, hivyo atakayemuudhi atakuwa kaniudhi na atakayeniudhi atakuwa kamuudhi Mwenyezi Mungu”.[220]

Mara nyingine akasema: “Fatima ndiye nimpendaye sana kuliko watu wote.”[221]

Maelezo haya ni ushahidi bora juu ya umaasumu wake baada ya Aya ya utakaso, bali yanatuchorea njia ya utambuzi dhidi ya matukio yatakayoukumba Uislamu kiasi kwamba haghadhibiki isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Az-Zahrau Mbele Ya Ahlul-Bayt, Maswahaba Na Tabiina Kutoka kwa Imam Ali bin Husein Zaynul-Abidin amesema: “Khadija hakumzalia Mtume(s.a.w.w ) mtoto yeyote ndani ya maumbile ya kiislamu isipokuwa Fatima.”[222]

Kutoka kwa Imam Muhammad Al-Baqir amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu alimwachanisha kwa elimu.”[223]

Kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq amesema: “Hakika aliitwa Fatima kwa sababu viumbe wameachanishwa na maarifa yake.”[224]

Ibnu Abbas amesema: “Siku moja Mtume(s.a.w.w ) alikuwa amekaa huku akiwa na Ali, Fatima, Hasan na Husein akasema: Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe unajua kuwa hawa ni kizazi changu na niwapendao sana kuliko watu wote, hivyo mpende atakayewapenda na umchukie atakayewachukia, mtawalishe atakayewatawalisha na umfanyie uadui atakayewafanyia uadui, msaidie atakayewasaidia, wafanye watakasifu dhidi ya kila uchafu, watakasifu dhidi ya kila dhambi na uwasaidie kwa roho mtakatifu toka kwako.”

Imepokewa toka kwa mama wa waumini Ummu Salamah kuwa alisema: “Fatima binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeshabihiana sana na Mtume(s.a.w.w ) kisura na kimaumbile.”

Imepokewa toka kwa mama wa waumini Aisha kuwa alisema: “Sikumwona mtu aliyekuwa mkweli kuliko Fatima isipokuwa yule aliyemzaa.[225] Alikuwa aingiapo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) basi Mtume husimama humkaribisha na kumbusu kisha humshika mkono na kumkalisha alipokaa yeye. Na Mtume(s.a.w.w ) aingiapo kwa Fatima basi husimama toka alipokuwa ameketi kisha hubusu mikono yake na humkalisha alipokaa yeye. Alikuwa msiri wa Mtume(s.a.w.w ) na marejeo yake katika jambo lake.”[226]

Ibnu Swabbagh Al-Malikiy amesema: “Na yeye ni binti wa yule aliyeteremshiwa: “Utukufu ni wa ambaye alimpeleka mja wake”.[227]

Watatu baada ya jua na mwezi, binti wa mbora wa wanadamu, mzawa mtakasifu aliye mbora kwa kongamano la wema wote.”[228]

Al-Hafidh Abu Nuaim Al-Isfihaniy amesema: “Kati ya vitakaswa vya watakasifu na visafi vya wachamungu ni Fatima mbora, mtawa, pande la nyama ya Mtume na shabihi wake….. Alikuwa kajitenga mbali na dunia na starehe zake, huku akijua vizuri machungu ya aibu za dunia na maangamizo yake.”[229]

Abdul-Hamid bin Abul-Hadid Al-Muutazaliy amesema: “Mtume(s.a.w.w ) alimtukuza sana Fatima kinyume na watu walivyokuwa wakifikiria….. mpaka akavuka kiwango cha mapenzi ya wazazi kwa wana wao, hivyo akatamka mara kwa mara na sehemu mbalimbali, mbele ya watu maalumu na mbele ya watu wote kuwa: “Yeye ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni, na hakika yeye ni pacha wa Mariam binti Imran, na kuwa atakapotaka kupita kwenye kisi- mamo cha siku ya Kiyama atanadi mwenye kunadi toka upande wa Arshi kuwa: Enyi watu mliopo kwenye kisimamo, fumbeni macho yenu ili apite Fatima binti Muhammad.”

Hii ni kati ya hadithi sahihi wala si dhaifu, kwani si mara moja Mtume(s.a.w.w ) amekuwa akisema: “Huniudhi linalomuudhi na hunighadhibisha linalomghadhibisha, na hakika yeye ni pande la nyama yangu, hunichukiza yanayomchukiza.”[230]

MUHTASARI

Fatima ni nyota ing’aayo katika mbingu ya akida ya kiislamu na ni bendera ya uongofu kwa wanadamu. Mwenyezi Mungu amemsifia ndani ya Qur’ani huku akidhihirisha fadhila zake.

Ama Mtume(s.a.w.w ) yeye amemsifia huku akivichorea vizazi vijavyo alama za hadhi yake, nafasi yake na mchango wake na akiwahimiza waislam wampende na kumridhisha. Kisha Maimam maasumina nao wakam- sifu na kueneza nuru yake mpaka ikabainika kwa kila mwenye macho kuwa ni wajibu kueneza fadhila zake.

Maswahaba na wanafunzi wa maswahaba, waandishi, watu wa hadithi na wanahistoria wote wamemtukuza na kuinua nafasi yake huku wakitamka fadhila zake na sifa zake.

SOMO LA KUMI NA SABA: FADHILA NA MWONEKANO WA AZ-ZAHRAU (A.S)

Hakika yeye ni binti wa nabii aliyezikomboa na kuziongoza akili zama zote. Pia yeye ni mke wa Imam ambaye alikuwa nguzo miongoni mwa nguzo za haki na mwendelezo wa nabii mtukufu katika historia ya mwanadamu.

Hakika Fatima(a.s ) alipata akili kamilifu, roho nzuri, na dhamira safi, hivyo kwa msimamo wake na urithi wake akatuchorea sifa za njia bora ambayo dini imepita. Hivyo yeye Fatima(a.s ) akawa nguzo kati ya nguzo za dini, kwa ajili hiyo huwezi kujua historia ya Uislamu vizuri bila kujua historia yake.

Hakika Az-Zahra(a.s ) alikuwa mfano bora wa mwanamke katika ubinadamu, utawa, heshima na utukufu, ukiongeza uelevu wa juu na elimu pana aliyokuwa nayo. Fahari hii inatosha, nayo ni kulelewa ndani ya shule ya unabii na kuhitimu masomo yake toka chuo cha utume.

Akanywa toka kwa baba yake Mtume mwaminifu yale aliyokunywa baba yake toka kwa Mola wa ulimwengu.[231]

Hakika Fatima(a.s ) alisikia Qur’ani toka mdomoni mwa nabii mtukufu na toka kwenye sauti ya Ali(a.s ) , hivyo akamwabudu Mola wake baada ya kuzitambua sheria zake, faradhi zake na sunna zake, utambuzi ambao haukufikiwa na yeyote mwingine mwenye sharafu na karama. Na hapa ndipo tunapojua siri ya maneno aliyotamka Aisha kuwa: “Hajampata mwanamke aliyependwa sana na Mtume (s.a.w.w.) kuliko Fatima.” Japokuwa yeye Aisha alibadili hilo akasema: “Sikumwona mtu mkweli mno kuliko Fatima isipokuwa tu yule aliyemzaa.”[232]

Hivyo ndivyo alivyogeuka Az-Zahrau sura halisi ya mwanadamu mkamilifu ambaye waumini wananyenyekea kwa kumtakasa.

ELIMU YAKE NA MAARIFA YAKE

Fatima(a.s ) hakukomea tu kwenye maarifa aliyoandaliwa na nyumba ya ufunuo, wala hakuishia kujing’arisha kielimu kutokana na mionzi ya elimu na maarifa yaliyomzunguka pande zote, bali alikuwa akijaribu kumywa elimu nyingine vyovyote iwezekanavyo, hiyo ni kila anapokutana na baba yake na mume wake ambaye ni mlango wa jiji la elimu ya Mtume(s.a.w.w ) .

Alikuwa na utaratibu wa kudumu wa kuwatuma watoto wake Hasan na Husein kwenda kwenye darasa la Mtume(s.a.w .w ) kisha huwahoji pindi wanaporejea, hivyo ndivyo alivyokuwa akijali utafutaji wa elimu huku akijali kuwalea wanawe malezi bora. Japokuwa majukumu yake yalikuwa mengi lakini alikuwa akitoa elimu yake kuwapa wanawake wengi wa kiislamu.

Hakika juhudi hizi endelevu za kutafuta elimu na kuisambaza zimemfanya awe miongoni mwa wapokezi wakubwa wa kike wa hadithi.

Pia awe miongoni mwa wabebaji wa sunna takatifu kiasi kwamba kitabu chake kikubwa ambacho alikuwa akikijali sana kikajulikana kwa jina la msahafu wa Fatima.

Tusisahau kuwa kati ya majina yake ni Muhaddathah, yaani msemeshwa. Kwa ajili hiyo anakuwa pacha wa Mariam katika kuzungumzishwa na malaika, na hili ni chimbuko jingine la elimu yake ambayo ilihamia kwa wanawe maasumina wakirithishana wao kwa wao.

Hotuba mbili muhimu alizotoa baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w ) zinatosha kuwa dalili juu ya hilo na juu ya ubora wa fikira zake na ukamilifu wa elimu yake.3 Hotuba moja alitoa mbele ya maswahaba wakubwa ndani ya msikiti mtumufu wa Mtume(s.a.w.w ) na nyingine nyumbani kwake. Hakika zimekusanya madhumuni ya kupendeza yanayoonyesha undani wa fikira zake, upana wa maarifa yake, uwezo wa lugha yake, ukweli wa habari zake kuhusu mwelekeo wa umma baada ya umma kuacha njia sahihi baada tu ya kifo cha baba yake. Zaidi ya hapo ni maadili yake ya juu na jihadi yake kubwa kwa Mwenyezi Mungu na katika njia ya haki.

Az-Zahrau alikuwa miongoni mwa Ahlul-Bayt, wao walimcha Mwenyezi Mungu na Yeye akawafunza,4 na hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyomwachanisha kwa elimu na hivyo akaitwa Fatima, kama alivyoelekea kwa Mwenyezi Mungu hivyo akaitwa Al- Batul.

MAADILI YAKE BORA

Fatima(a.s ) alikuwa mwenye maadili bora, dhamira safi, nafsi safi, mwepesi wa kufahamu, mwenye matendo bora, jasiri shujaa, jasiri wa nafsi, asiyejivuna, asiyedhibitiwa na dunia danganyifu, asiyejikweza na asiye na kiburi.[233]

Alikuwa mvumilivu, mwingi wa subira, mnyenyekevu mtulivu, mpole mwenye huruma, mtawa mwenye kujihifadhi. Ulimi wake ulikuwa haupiti isipokuwa penye haki.

Hatamki isipokuwa ukweli, hamtaji mtu kwa ubaya, hateti wala hasengenyi. Huhifadhi siri, hutekeleza ahadi, huwa mkweli wa nasaha, anakubali udhuru, hujiepusha kumkosea mtu, na mara nyingi husamehe akosewapo, hivyo hupokea kosa kwa kulipa msamaha.

Alikuwa mbali na shari mwenye kuelemea heri, mwaminifu, mkweli katika kauli yake, mkweli wa dhati na ahadi, alikuwa katika kiwango cha juu cha utawa. Hasukumwi na matamanio yake, kwa sababu yeye ni miongoni mwa Ahlul-Bayt wa Mtume(s.a.w.w ) ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa moja kwa moja.

Alikuwa aongeapo na mtu au kuhutubia wanaume basi ni lazima kuwa na pazia kati yake na wao, pazia ambayo huzuwia kati yao kwa ajili ya utawa na kujihifadhi.

Alikuwa amekinaika na hali yake akiamini kuwa tamaa hufarakisha moyo na huharibu mambo. Akishikamana na kauli aliyoambiwa na baba yake: “Ewe Fatima vumilia dhidi ya machungu ya dunia ili ufaulu kwa kupata neema za milele.”[234]

Hivyo alikuwa ameridhika na maisha mepesi mvumilivu dhidi ya ugumu wa maisha, mwenye kutosheka na kidogo cha halali, mwenye kuridhia, mwenye kuridhiwa, hatamani ya mtu mwingine wala hakodolei macho yasiyokuwa haki yake, wala hakujishusha kwenda kumwomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye alijitosheleza kama alivyosema baba yake: “Hakika utajiri bora ni utajiri wa nafsi.”[235]

Hakika yeye ni mbora ambaye alijielekeza kwa Mwenyezi Mungu na kuiacha dunia yake, akajiepusha na kujitenga na mapambo na udan- ganyifu wake, akafahamu maangamizi yake, akavumilia kutekeleza majukumu yake, huku akipambana na ugumu wa maisha na ulimi wake ukilowana kwa kumtaja

MOLA WAKE

Hakika lengo la Az-Zahrau lilikuwa ni Akhera, hivyo hakukusanya furaha za dunia huku akimwona baba yake ameipa mgongo dunia na yote yaliyomo duniani kuanzia ladha, starehe na matamanio ya dunia. Subira yake juu ya matatizo ni maarufu, ukubwa wa shukurani yake wakati wa raha inajulikana, ni maarufu kwa kuridhika na matokeo ya majaliwa ya Mwenyezi Mungu mpaka akasimulia toka kwa baba yake kuwa: “Mwenyezi Mungu ampendapo mja wake humjaribu kwa matatizo, hivyo iwapo atasubiri humkweza na akiridhia humteua.”[236]

MUHTASARI

Kama maadili ya Mtume(s.a.w.w ) ni Qur’ani basi maadili ya Az- Zahra ndio maadili ya baba

yake. Yametudhihirikia maadili bora ya Az-Zahra na utu wake wa juu unaomfanya awe kiigizo kwa waislam wote.

Mwenyezi Mungu alimfanya bora kuliko wanawake wote wa ulimwenguni kwa sababu yeye amekunywa elimu ya Mwenyezi Mungu, akaamini ujumbe wa Uislamu, akamtii Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa moyo mmoja zaidi ya maelezo.

Aliweza kutoa nguvu zake zote katika njia ya Mwenyezi Mungu, kujenga Uislamu na kuhudumia umma wa waislam kwa ajili ya mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu. Alikuwa na moyo mkunjufu katika imani yake na ibada yake, akakamilika katika kila linalohusu maisha yake mpaka mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu na Mtume yakadhihirika katika kila hatua ya maisha yake.

KWA AJILI YA KUJISOMEA

Az-Zahrau(a.s ) alikuwa ni mbora wa kuwapendelea wengine kuliko nafsi yake huku akimuiga baba yake katika hilo mpaka imekuwa maarufu kuwa alitoa sadaka gauni lake la harusi usiku wa kupelekwa kwa mumewe.

Maelezo yaliyomo ndani ya Sura Ad-Dahri yanatosha kuthibitisha upendeleo wake na ukarimu wake. Jabir bin Abdullah Al-Answariy amepokea kuwa: Mtume alitusalisha Swala ya alasiri na baada ya kumaliza alikaa huku kazungukwa na maswahaba zake, ghafla aka- tokeza mzee wa kiarabu akiwa kijifunga nguo chakavu akiwa dhaifu mwenye uchovu. Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) akamfuata na kumuuliza habari zake. Mzee akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nina njaa nilishe, sina nguo nivishe na fakiri nipe masurufu.”

Mtume akajibu: “Mimi sina kitu sasa hivi lakini mwonyesha kheri ni sawa na mtenda kheri, hivyo nenda nyumbani kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda na yeye anawapenda, humtanguliza Mwenyezi Mungu kuliko nafsi yake, nenda nyumbani kwa Fatima .”

Nyumba ya Fatima ilikuwa imeungana na nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) ambayo alikuwa akiitumia kujitenga na wakeze, akamwambia Bilal: “Ewe Bilal simama umpeleke kwa Fatima.” Akaondoka bedui akiwa na Bilal na alipofika mlangoni kwa Fatima aliita kwa sauti ya juu: “Amani iwe juu yenu enyi kizazi cha Mtume, mapishano ya malaika, mashukio ya Jibril roho mwaminifu akiwa na ufunuo toka kwa Mola wa ulimwengu.” Fatima akasema: “Waa’leykum salam, ni nani wewe?” Akasema: “Mimi ni mzee wa kiarabu ninahisi njaa, sina nguo, na masikini. Nisaidie Mwenyezi Mungu atakurehemu.”

Fatuma na Ali na wao walikuwa katika hali kama hiyo kwani walikuwa na siku tatu hawajakula chochote, huku tangu mwanzo Mtume(s.a.w.w ) akiwa anajua hali hiyo. Hivyo Fatima(a.s ) akaenda kuchukua tandiko la ngozi ya kondoo ambalo Hasan na Husein walikuwa wakilalia.

Kisha akamwambia: “Chukua ewe mbisha hodi hakika Mwenyezi Mungu atakubadilishia kwa kukupa kilicho bora zaidi ya hiki.”

Bedui akasema: “Ewe binti wa Muhammad, nimelalamika kwako kuwa nina njaa kisha wewe unanipa tandiko la ngozi ya kondoo nitalifanyia nini huku nikiwa na njaa kama hii?” Fatima(a.s ) aliposikia maneno haya alichukua mkufu uliokuwa shingoni mwake ambao alipewa zawadi na Fatima binti wa ami yake Hamza bin Abdul Muttalib, hivyo akauvua na kumpa bedui kisha akamwambia: “Chukua ukauuze, hakika Mwenyezi Mungu atakubadilishia kwa kukupa kilicho bora zaidi.”

Bedui akachukua mkufu na kwenda nao msikiti wa Mtume (s.a.w.w.) huku Mtume akiwa kaketi na maswahaba zake. Bedui akasema: “Ewe Mtume, Fatima amenipa mkufu huu.” Mtume akamwambia: “Uza mkufu huo.”

Jabir anasema: Mtume akalia na kusema: “Itakuwaje Mwenyezi Mungu asikubadilishie kwa kukupa kilicho bora zaidi ilihali mkufu huo kakupa Fatima binti wa Muhammad mbora wa wanawake wote wa ulimwengu!”

Ammar bin Yasir akasimama na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! je unaniruhusu kununua mkufu huu?” Mtume akajibu: “Ununue ewe Ammar kwani laiti makundi mawili (binadamu na majini) yangeshirikiana kuununua basi Mwenyezi Mungu asingeyaadhibu kwa moto.” Ammar akasema:“Ewe bedui! unauza mkufu kiasi gani?”

Akajibu: “Kwa kipande cha mkate na nyama, kwa nguo ya kiyemeni ambayo itanitosha kujisitiri na kumwabudia Mola Wangu na dinari itakayotosha kunifikisha nyumbani kwangu.”

Ammar alikuwa amekwishauza fungu lake alilopewa na Mtume (s.a.w.w.) kutoka kwenye vita vya Khaybar, hivyo alikuwa hajabakiwa na kitu, ndipo alipomwambia: “Nakupa dinari ishirini, dirhamu mia mbili za fedha, nguo ya kiyemeni na usafiri wangu utakufikisha nyumbani kwako na nitakushibisha kwa kukupa mkate na nyama.” Bedui akasema: “Ewe ndugu! hakika wewe ni mkarimu mno.” Hapo Ammar akaenda naye na kumpa yote aliyomdhamini. Bedui akarudi kwa Mtume (s.a.w.w.) na hapo Mtume akamuuliza: “Je, umeshiba na umevaa?” Bedui akajibu:“Hakika nimetosheka.”

Mtume(s.a.w.w ) akamwambia: “Mlipe Fatima kwa wema wake.” Bedui akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe ni Mola wa tuliyokuzushia na hatuna Mola tunayepasa kumwabudu isipokuwa wewe, na wewe ndiye mtoa riziki kwetu katika kila hali, hivyo ewe Mola, mbariki binti wa Mtume Fatima kwa kumpa neema ambayo hakuwahi mtu yeyote kuiona wala kuisikia.”

Hapo Mtume(s.a.w.w ) akaitikia dua yake na kisha akawageukia maswahaba na kuwaambia: “Hakika Mwenyezi Mungu ameshampa Fatima hayo hapa duniani kwani: Mimi ndiye baba yake wala hakuna yeyote ulimwenguni mfano wangu, na Ali(a.s ) ndiye mumewe na laiti asingeumbwa Ali(a.s ) basi milele Fatima asingepata wa kumstahili, na akampa Hasan na Husein wala hakuna yeyote ulimwenguni aliyeruzukiwa watoto mfano wao, wao ni mabwana wa vijana wa wajukuu wa manabii na mabwana wa vijana wa Peponi.”

Mbele yake alikuwepo Mikdad, Ammar na Salman, Mtume(s.a.w.w ) akawaambia: “Je, niwaongezee?” Wakajibu: “Ndiyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.” Akasema: “Jibril amenijia akaniambia kuwa: Atakapozikwa Fatima malaika wawili watamuuliza: Ni nani Mola wako? Atawajibu: “Allah ndio Mola wangu.” Watamuuliza: “Ni nani nabii wako?” Atasema: “Baba yangu.” “Na ni nani walii wako?” Atajibu: “Ni huyu aliyesimama mdomoni mwa kaburi langu.”

Mtume akasema: “Je, niwaongeze fadhila zake? Hakika Mwenyezi Mungu amemuwekea walinzi kati ya malaika wanamlinda mbele na nyuma, kushoto na kulia, wako naye katika uhai wake, kifo chake na ndani ya kaburi lake.

Wanazidisha kumwombea rehema na amani yeye na baba yake, mume wake na wanae, hivyo atakayenizuru mimi baada ya kifo changu atakuwa kanizuru wakati wa uhai wangu, na atakayemzuru Fatima atakuwa kanizuru mimi, na atakayemzuru Ali bin Abu Twalib atakuwa kamzuru Fatima, na atakayewazuru Hasan na Husein atakuwa kamzuru Ali, na atakayevizuru vizazi vyao wawili hawa atakuwa kawazuru wao wenyewe.”

Hapo Ammar akaenda kuupaka mkufu manukato na kuuweka ndani ya kitambaa cha kiyemeni. Alikuwa na mtumwa aliyemnunua kutokana na fungu lake alilopata toka Khaybari, hivyo akampa mtumwa wake ule mkufu na kumwambia: “Chukua mkufu huu umpelekee Mtume na wewe uwe miliki yake.” Mtumwa akauchukua mkufu ule na kumpelekea Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia aliyoambiwa na Ammar. Mtume akamwambia: “Chukua mkufu huu umpelekee Fatima na wewe uwe miliki yake.”

Mtumwa akauchukua mkufu ule na kumpelekea Fatima na kumwambia aliyoambiwa na Mtume(s.a.w.w ) . Hapo Fatima akapokea mkufu kisha akamwacha huru mtumwa huku kijana yule akicheka. Fatuma akamuuliza: “Ewe kijana! ni kitu gani kinachokuchekesha?”

Akajibu: “Unanichekesha ukubwa wa baraka za mkufu huu, kwani umemshibisha mwenye njaa, ukamvisha asiye na nguo, ukamtajirisha fakiri, ukampa uhuru mtumwa na mwisho ukarejea kwa mwenyewe.”[237]

SOMO LA KUMI NA NANE: FADHILA NA MWONEKANO WA AZ-ZAHRAU (A.S)

IMANI NA IBADA ZAKE KWA AJILI YA MWENYEZI MUNGU

Kumwamini Mwenyezi Mungu ndio alama ya mwanadamu mkamilifu, na ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndio ngazi ya kufikia kilele cha ukamilifu. Na hakika manabii wamepata makazi bora katika nyumba ya heshima kutokana na daraja lao la imani na juhudi zao za kuchuma mema hapa duniani na moyo mkunjufu katika ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Qur’ani ndani ya Sura Ad-Dahri imethibitisha ukamilifu wa moyo mkunjufu wa Az-Zahrau na unyenyekevu wake kwa Mwenyezi Mungu, ukubwa wa imani yake Kwake na siku ya mwisho, imani ambayo imetengeneza mfano bora wa kuigwa kama alivyothibitisha hilo Mtume(s.a.w.w ) kwa kusema: “Hakika binti yangu Fatima moyo wake na viungo vyake vimejazwa imani na Mwenyezi Mungu mpaka kwenye mfupa wa ubongo, hivyo akatetemeka kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu.”[238]

Akasema tena: “Hakika anaposimama mihrabuni mbele ya Mola wake nuru yake huwang’aria malaika wa mbinguni kama nuru ya sayari inavyowang’aria watu wa aridhini, hapo Mwenyezi Mungu huwaambia malaika wake:

Enyi malaika Wangu, hebu mtazameni mja wangu wa kike Fatima, mbora wa waja wangu wote wa kike, amesimama mbele yangu huku viungo vyake vikitetemeka kwa kuninyenyekea, amenielekea kwa moyo wake akiniabudu, nawathibitishieni kuwa nimewasalimisha wafuasi wake dhidi ya moto.”[239]

Hasan bin Ali (a.s.) amesema: “Nilimwona mama yangu Fatima amesimama mihrabuni kwake usiku wa Ijumaa, aliendelea kurukuu na kusujudu mpaka ikachomoza asubuhi huku nikimsikia akiwaombea heri waumini wa kiume na wa kike, akiwataja kwa majina yao, huku akizidisha kuwaombea ilihali yeye mwenyewe hajajiombea chochote. Nikamwambia: Ewe mama yangu mpendwa! Kwa nini hujiombei kama unavyowaombea wengine? Akajibu: “Ewe mwanangu mpendwa! Kwanza jirani kisha wa ndani.”[240]

Saa za mwisho za mchana wa Ijumaa alikuwa akizifanya ni maalumu kwa ajili ya dua. Pia alikuwa halali lifikapo kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Alikuwa akiwahimiza wote waliyomo nyumbani kwake kuuhuisha usiku huo kwa ibada na dua. Hasan Al-Basri amesema: “Hakutokea mtu mfanya ibada sana ndani ya umma huu kama Fatima, alikuwa akisimama kufanya ibada mpaka nyayo zake zinavimba.[241] Alikuwa akihema ndani ya Swala yake kwa ajili ya kumwogopa Mwenyezi Mungu.”[242]

Je ndani ya maisha yake Fatima aliwahi kutoka kwenye mihrabu yake? Hapana. Hakika humwabudu Mwenyezi Mungu nyumbani kwake kwa kuwa mke bora na kuwalea wanawe malezi bora huku akimtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza huduma zote za jamii, aliwasaidia mafakiri na kuwapendelea kuliko nafsi yake hata kama hana cha kujitosheleza.

MAPENZI NA HURUMA YAKE

Az-Zahrau(a.s ) alichukua mapenzi, upendo na huruma toka kwa baba yake, hivyo alikuwa mwana mwema kwa Mtume(s.a.w.w) . Alimpenda Mtume(s.a.w.w) kwa dhati, hivyo akampendelea kuliko nafsi yake. Alikuwa akihudumia nyumba ya baba yake huku akitekeleza ayatakayo Mtume(s.a.w.w) , hivyo anatekeleza yanay- omfaa Mtume(s.a.w.w) , yanayompa raha na utulivu huku akiharak- isha kutenda kila linalomridhisha baba yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Anamwandalia maji ya kuoga, chakula, anafua nguo zake, zaidi ya hapo anashirikiana na wanawake wengine kubeba chakula na vinywaji kwa ajili ya kuhudumia na kuwatibu majeruhi.

Hakika katika vita vya Uhud alitibu majeraha ya baba yake, hivyo alipoona damu hazikatiki akachukua kipande cha mkeka kisha akakiunguza mpaka kikawa jivu kisha akamwagia jivu hilo kwenye jeraha na hapo damu ikasimama. Akamletea kipande cha mkate wakati wa kuchimba handaki, Mtume(s.a.w.w) akamuuliza: “Ni kitu gani hiki ewe Fatima?” Akajibu: “Ni kipande cha mkate nilioutengeneza kwa ajili ya wanangu wapendwa hivyo nimekuletea kipande chake.” Mtume(s.a.w.w) akasema: “Hakika hiki ndio chakula cha kwanza kinachoingia mdomoni mwa baba yako tangu siku tatu.”[243]

Hakika Az-Zahra(a.s) aliweza kuziba pengo la mapenzi, pengo ambalo Mtume(s.a.w.w) alilipata baada ya kufiwa na wazazi wake wawili na mkewe mtukufu Khadija (r.a) huku akiwa katika mazingira magumu ya ulinganio wa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na hapa tunafahamu kiini cha lile alilolikariri Mtume(s.a.w.w) ulimini mwake kwa kusema: “Fatima ni mama wa baba yake.”[244]

Alikuwa akihusiana naye uhusiano wa mama, anaubusu mkono wake, anakuwa wa kwanza kumzuru aingiapo Madina na wa mwisho kumuaga atokapo Madina.

Safari na misafara yake ya kivita huanzia nyumbani kwa Fatima(a.s) , hivyo alikuwa akijiongezea baraka na upendo katika safari na misafara yake toka katika chemchemu hii safi. Pia alikuwa akirudi mara kwa mara nyumbani kwa Fatima, hivyo Fatima(a.s) humpokea kama mama ampokeavyo mwanae, humlea, humkumbatia na humpunguzia machungu huku akimuhudumia na kumtii.

MAPAMBANO YAKE ENDELEVU

Fatima(a.s) alizaliwa kipindi cha mapambano kati ya Uislamu na Ujahiliya. Akafumbua macho yake huku waislamu wakiwa katika jihadi kali dhidi ya ushirikina wenye kiburi. Maquraishi waliweka vikwazo dhidi ya Mtume(s.a.w.w) na Bani Hashim wote, hivyo Mtume(s.a.w.w) , mkewe mpiganaji, na binti yake mtakasifu wote wakaingia bonde la Abu Twalib, humo wakawekewa vikwazo muda wa miaka mitatu, wakaonjeshwa aina za ukata na ugumu wa maisha. Pamoja na hayo yote lakini walipambana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutetea haki na kujitolea kwa ajili ya imani tukufu.

Miaka ya vikwazo vizito na vigumu ikapita na Mtume(s.a.w.w) akatoka huku akiwa ameshinda. Ndani ya mwaka huo huo Mwenyezi Mungu akapenda kumchagua Khadija, pia ndani ya mwaka huo aka- fariki Abu Twalib ami wa Mtume(s.a.w.w) na mtetezi wa Uislamu, hivyo huzuni na uchungu vikachukua moyo wa Mtume(s.a.w.w) baada ya kuwa amemkosa kipenzi cha moyo wake.

Hivyo ndivyo Fatima(a.s) alivyopatwa na msiba huku akiwa bado hajashiba mapenzi ya mama yake, na hapo akaungana na baba yake katika machungu. Japokuwa alimkosa mama yake, chanzo cha mapenzi, lakini Mtume(s.a.w.w) alikuwa akijaribu kumpa mapenzi mbadala toka kwake badala ya mapenzi makubwa ya mama yake.

Baada tu ya kufariki ami yake na mtetezi wake Abu Twalib maquraishi walimwagia kila chuki yao na maudhi yao juu ya Mtume(s.a.w.w) huku Az-Zahrau(a.s) akiona kwa macho yake maudhi yote yanayofanywa na wajinga na waovu wa kiquraishi, ilihali Mtume(s.a.w.w) akitaka kuwatoa gizani na kuwapeleka kwenye nuru.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa akijaribu kumpunguzia machungu huku akimhimiza kuwa na subira kwa kumwambia: “Ewe mwanangu mpendwa usilie, hakika Mwenyezi Mungu anamlinda na kumnusuru baba yako dhidi ya maadui wa dini Yake na ujumbe wake”[245] .

Hivyo ndivyo alivyokuwa Mtume(s.a.w.w) akipandikiza roho ya mapambano ya juu ndani ya nafsi ya binti yake huku akiujaza moyo wake subira na imani ya ushindi.

Az-Zahra(a.s) alihamia Madina baada ya baba yake kuhama toka anga la Makka la kutisha. Alihama na mtoto wa ami yake Ali bin Abu Twalib(a.s) ambaye alidharau kiburi cha ujeuri wa maquraishi hivyo Az-Zahrau(a.s) akaungana na Mtume(s.a.w.w) huko Kuba baada ya miguu yake kuvimba kutokana na kutembea.

Kwa unyeyekevu Az-Zahrau(a.s) akahamia kwa mumewe huko Madina baada ya baba yake kusimamisha misingi ya dola, akashirikiana na baba yake katika mapambano kwa subira dhidi ya matatizo ya maisha na misukosuko ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu huku Fatima akijaribu kutoa sura halisi ya mfano wa kuigwa katika maisha mapya ya ndoa.

Az-Zahra(a.s) alichangia sehemu kubwa na ya kuonekana katika kuinusuru haki na kutetea usia wa Mtume(s.a.w.w) pale aliposimama kidete dhidi ya uendaji kinyume, akapiga kelele kwa namna isiyo na mfano huku akiwa pembeni ya kipenzi chake Ali bin Abu Twalib(a.s) ndani ya siku ngumu za maisha yake ili ahakikishe kuwa uwanja wa ndani wa Ali(a.s) ni imara haudhoofiki. Pamoja na hayo yote anaacha uamuzi na msimamo wa mwisho utolewe na kuchukuliwa na kiongozi wake, mume wake na Imam wake Ali(a.s) ili aamue linalonasibiana sana na mazingira.

Az-Zahrau(a.s) alikuwa akienda kila Jumamosi asubuhi kwenye makaburi ya mashahidi katika viwanja vya Uhud kisha akiwaombea rehema na msamaha. Hakika vitendo hivi vinaonyesha ni kwa kiwango gani Fatima(a.s) alithamini jihadi na shahada huku vikiweka wazi thamani ya maisha yake kivitendo, maisha ambayo yalianza kwa jihadi, yakategemea jihadi, yakakomea kwa jihadi, hiyo ni ili apate cheo cha shahidi.[246]

MUHTASARI

Az-Zahrau(a.s) alifuata nyayo za baba yake katika kila jambo, hivyo Mtume(s.a.w.w) anathibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ameujaza moyo wake na viungo vyake vyote imani kwa ajili yake. Pia walioishi naye wamethibitisha kuwa alikuwa mtu wa ibada sana kuliko watu wote.

Pia amefahamika kwa huruma kwa baba yake mpaka akampendelea kuliko nafsi yake, wanawe, hivyo baba yake akampa jina la: Mama wa baba yake.

Alibeba jukumu la jihadi katika njia ya Mola Wake kabla na baada ya kuolewa. Akasimama imara mbele ya matatizo baada ya kufariki baba yake ili aing’arishe njia ya haki kwa wapitaji.

SOMO LA KUMI NA TISA: URITHI WA AZ-ZAHRAU (A.S)

i. Imepokewa toka kwa Fatima binti wa Mtume(s.a.w.w) kuwa yeye Fatima aliingia nyumbani kwa Mtume(s.a.w.w) , hapo Mtume(s.a.w.w) akatandika nguo kisha akamwambia akae juu yake, kisha akaingia Hasan, Mtume(s.a.w.w) akamwambia kaa pamoja na mama yako. Akaingia Husein, Mtume(s.a.w.w) akamwambia kaa nao. Kisha akaingia Ali(a.s) akaambiwa na Mtume(s.a.w.w) kaa nao. Kisha Mtume(s.a.w.w) akashika pembe za nguo na kuwafunika na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu; wao wanatokana na mimi na mimi natokana na wao, ewe Mwenyezi Mungu waridhie kama nilivyowaridhia.”[247]

ii. Kutoka kwa Muhammad bin Umar Al-Kannasiy kutoka kwa Jafar bin Muhammad kutoka kwa baba yake kutoka kwa Ali bin Husein kutoka kwa Fatima mdogo kutoka kwa Husein bin Ali kutoka kwa Fatimah binti Muhammad alisema: “Alitujia Mtume(s.a.w.w) akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu amejifaharisha kwenu, hivyo akawasamehe nyinyi wote kwa ujumla na akamsamehe Ali mahsusi, na hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, si mwenye kuogopwa kwa ajili ya watu wangu na ni mwenye kupendwa kwa sababu ya kizazi changu. Huyu hapa Jibril ananipa habari kuwa: Mwema wa kweli ni yule atakayempenda Ali wakati wa uhai wangu na baada ya kifo changu.”[248]

iii. Kutoka kwa Ali(a.s) kutoka kwa Fatima(a.s) alisema: “Mtume aliniambia: Ewe Fatima, atakayekuombea rehema wewe basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na atamkutanisha na mimi peponi sehemu yoyote nitakayokuwepo.”[249]

iv. Kutoka kwa Zaynab binti Ali kutoka kwa Fatima binti wa Mtume(s.a.w.w) alisema: Mtume alisema kumwambia Ali: “Ewe Ali! Wewe na wafuasi wako ni watu wa Peponi.”[250]

v. Fatima(a.s) alisema: “Mtume aliniambia: Hivi huridhii kuwa mimi nimekuoza kwa mwislamu wa kwanza kuamini, mwenye elimu nyin- gi kuliko wao. Hakika wewe ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni kama Mariam alivyokuwa mbora kuliko wanawake wote wa kaumu yake.”[251]

vi. Kutoka kwa Sahl bin Saad Al-Answariy amesema: “Fatima binti wa Mtume(a.s) aliulizwa kuhusu Maimam. Akajibu: Mtume alikuwa akimwambia Ali: “Ewe Ali! wewe ni Imam na khalifa baada yangu, na wewe una haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao, hivyo akipita Hasan ni mwanao Husein ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Husein ni mwanae Ali bin Husein ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Muhammad ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Muhammad ni mwanae Ja’far ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Jafar ni mwanae Musa ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao.

Akipita Musa ni mwanae Ali ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Muhammad ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Muhammad ni mwanae Ali ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Hasan ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Hasan ni mwanae Mahdi ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Mwenyezi Mungu atafungua Mashariki ya ardhi na Magharibi yake kupitia yeye. Wao ndio Maimam wa haki na ndimi za kweli, atanusurika atakayewanusuru, atatelekezwa atakayewatelekeza.”[252]

v. Aliashiria makusudio ya sheria ya kiislamu kwa kusema: “Mwenyezi Mungu ameweka imani kwa ajili ya kuwatakasa dhidi ya shirki. Swala kwa ajili ya kuwaepusha na kiburi. Zaka kwa ajili ya kuitakasa nafsi na kuongeza riziki. Funga kwa ajili ya kuimarisha ikhlasi. Hija kwa ajili ya kuimarisha dini. Uadilifu kwa ajili ya kuziunganisha nyoyo. Utiifu wenu kwa ajili ya nidhamu ya sheria. Uimamu wetu kwa ajili ya kusalimika na mfarakano. Jihadi kwa ajili ya kuupa heshima Uislamu. Subira ni msaada ili muwajibike kupata malipo. Kuamrisha mema ni masilahi ya wote. Kuwatendea wema wazazi wawili ni kinga dhidi ya adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Kuunga undugu ni kuongeza umri na kuongeza idadi. Kisasi ni kwa ajili ya kuhifadhi damu. Kutekeleza nadhiri ni kwa ajili ya kuomba msamaha. Kutimiza vipimo na mizani ni kwa ajili ya kuondoa ulaghai. Kukataza kunywa pombe ni kwa ajili ya kuwatakasa dhidi ya uchafu. Kujiepusha kutuhumu ugoni ni kwa ajili ya kuzuia laana. Kuacha wizi ni kwa ajili ya kupelekea nafsi kujimiliki. Mwenyezi Mungu akaharamisha ushirikina kwa ajili ya kumnyookea Yeye tu kwa Umola wake.”

viii. Az-Zahrau(a.s) alimuuliza baba yake: “Ewe baba yangu mpendwa, ni mambo gani yanayompata mwanaume na mwanamke anayedharau Swala?” Akajibu: “Ewe Fatima, mwanaume yeyote au mwanamke akipuuzia Swala Mwenyezi Mungu humtahini kwa kumpa mambo kumi na tano, sita hapa duniani, matatu wakati wa kifo chake, matatu kaburini, na matatu Siku ya Kiyama atakapotoka kaburini.

xi. Fatima(a.s) alisema: Mtume aliniambia: “Jiepushe na ubahili hakika ni aibu isiyompata mkarimu. Jiepushe na ubahili hakika ni mti uliomo motoni na matawi yake yamo duniani, hivyo atakayeshika tawi moja kati ya matawi yake litamwingiza motoni. Kuwa mkarimu, hakika ukarimu ni mti kati ya miti ya peponi matawi yake yamening’inia hapa aridhini, hivyo atakayechukua tawi moja kati ya matawi yake litamwingiza Peponi.”[253]

x. Fatima(a.s) alisema: “Kufurahi mbele ya uso wa muumini kunawajibisha mwenye kufurahi kupata pepo, na kutabasamu mbele ya uso wa adui mpingaji kunamkinga mwenye kufurahi dhidi ya adhabu ya moto.”[254]

xi. Fatima(a.s) alisema: “Atakayepandisha ibada safi kwa Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu atamteremshia masilahi yake bora.”[255]

xii. Mtume(s.a.w.w) aliwauliza maswahaba zake kuhusu mwanamke, akasema: “Mwanamke ni nini?” Wakajibu: “Ni utupu.” Akasema: “Ni wakati gani anakuwa karibu sana na Mola wake?”

Hawakujua jibu. Ndipo Fatima(a.s) aliposikia akasema: “Huwa karibu sana na Mola wake pindi anapotawa nyumbani kwake.” Hapo Mtume(s.a.w.w) akasema: “Hakika Fatima ni kipande cha nyama yangu.”[256]

xiii. Alimsifia mwanamke bora kwa kusema: “Mbora wao ni yule asiyetazamwa na wanaume wala asiyetazama wanaume.”[257]

xiv. Kutoka kwa Ali bin Husein bin Ali(a.s) amesema: “Hakika Fatima binti wa Mtume(s.a.w.w) alimruhusu kipofu aingie kisha akamwekea pazia, hapo Mtume(s.a.w.w) akamwambi: “Fatima kwa nini umemwekea pazia ilihali yeye hakuoni?” Akajibu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! ikiwa yeye hanioni mimi namwona, na yeye ananusa harufu.” Mtume(s.a.w.w) akasema: “Nakiri kweli wewe ni pande la nyama yangu.”[258]

MUHTASARI

Riwaya zilizopokewa kutoka kwa Az-Zahrau(a.s) ni ushahidi tosha juu ya upana wa maarifa yake aliyokunywa kutoka kwenye chemchemu ya utume. Az-Zahra(a.s) ana hotuba mbili mashuhuri ambazo zinawakilisha kina cha maarifa yake na upana wa elimu zake mbalim- bali. Kupitia hizi hotuba mbili fasaha; historia imesajili nafasi yake adimu katika kugundua njama hatari zilizoukumba Uislamu, dola ya kiislamu na umma wa kiislamu baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w) . Az-Zahrau(a.s) alimjali mwanamke wa kiislamu na familia ya kiis- lamu kupitia msimamo wake, semi zake na maagizo yake, hivyo akawa ni mfano mzuri wa mwanamke msomi wa kiislamu na mwanadamu kiongozi na kiigizo chema kwa kila mwanamke, na kuanzia hapa akapata medali ya mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni.

Mwisho wa dua zetu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU