NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI0%

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Mwandishi:
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi: VITABU VYA HADITHI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

Mwandishi: SAYYIDI SHARIFU RADHIY
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi:

Matembeleo: 8604
Pakua: 4159


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8604 / Pakua: 4159
Kiwango Kiwango Kiwango
NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

NENO LA MCHAPISHAJI

Kitabu kilichoko mkononi mwako ni tarjumi kutoka lugha ya Kiarabu ya kitabu maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu, Nahju 'l-Balaghah. Kitabu hiki kitachapishwa katika juzuu mbili, na hii uliyo nayo mkononi ni juzuu ya pili.

Nahju 'l-Balaghah ni mkusanyiko wa khutba, barua na maelekezo ya Imam Ali (a.s) Mengi yamesemwa kuhusu ubora na ufasaha wa maneno yaliyomo katika khutba na harua hizo. Kwa ufupi, Nahju 'l-Balaghah ni kilele cha ufasaha.

Mbali na mawaidha yaliyomo humo, msomaji atafaidika na lugha iliyomo katika khutba na barua hizo, hususan kwa wasomaji wa Kiarabu. Inasemekana kwamba baada ya Qur'ani Tukufu na maneno ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , Nahju 'l-Balaghah ndiyo inayofuatia kwa ufasaha na ubora wa maneno.

Si rahisi kwa msomaji wa Kiswahili kupata ladha ileile aipatayo msomaji wa Kiarabu kutokana na ukweli kwamba lugha ya Kiarabu ni pana mno na msamiati wake ni mkubwa. Pamoja na hayo, mtarjumi wetu amejitahidi sana kuleta mafhumu ya Kiarabu kwenye lugha ya Kiswahili bila kupoteza maana.

Kwa vile kitabu hiki ni muhimu sana, tumeona ni bora tukichapishe katika lugha ya Kiswahili ili Waislamu na wasomaji wetu wazungumzao Kiswahili wapate kunufaika na yaliyomo humo. Hivyo, ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakkuwa ni chenye manufaa sana kwao na katika jamii yetu.

Tunamshukuru ndugu yetu, Sheikh Haruna Pingili kwa kukubali jukumu hili kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiri- ki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

DIBAJI

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Kwanza yanipasa nimshukuru Mwenyezi Mungu Jalali, asiye kuwa na mithali, kwa neema zake za kila hali na kila mahali, hata nikaweza mimi mja mpungufu, kutimiza kazi hii tukufu ya kuipitia tarjuma hii ya Kiswahili ya Nahju 'l-Balaghah.

Nahju 'l-Balaghah ni jina la diwani mashuhuri yenye khutba, uweza wa kusema, na barua za Imam Alî bin Abu Talib (a.s) Haya yote yamekusanywa na Sharîf Ar-Radhi. Diwani hii yenye khutba takriban 237, baru 79 na mithali 480 ilikamilika mwezi wa Rajab 400 A.H./1009 A.D. Maana ya NAHJ ni njia iliyo wazi, au barabara kuu; na maana ya Balaghah ni ufasaha (wa lugha) au ilimu ya usemaji, n.k. Kwa hivyo Nahju 'l-Balaghah yaani Barabara kuu ya ufasaha.

"Huyu Imam 'Ali ni nani? Ni vigumu mno kuzitaja sifa zake kwa ukamilifu. Yeye alikuwa mtaalamu, shujaa na khatibu kuliko wote. Uchamungu wake, mapenzi yake ya Mwenyezi Mungu, uaminifu wake na ushupavu wake wa kufuata dini ulikuwa wa darja ya juu kuliko mtu yeyote akichukia diplomasia (ujanja), na akipenda haki na insafu. Sera zake ni kama zilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Wataalamu wa Kiyahudi na wa Kikristo wakijaaliwa kujua daraja ya ilimu yake huisujudia ilimu hiyo isioweza kufananishwa.

Wafalme wa Ki-Rumi wangependa kuzitundika picha zake katika kasri zao, na maaskari wakubwa wa vita wangependelea kulichonga jina lake kwenye panga zao.

لا فثي ا لاَّ ءَلِيَّ وَ لآ سَيْفَ اِلاَّ دُ و الْفقار.

"Hayuko kijana shujaa mfano wa 'Ali! wala hakuna upanga mfano wa Dh-ul-Faqar (upanga wa Imam 'Alî (a.s) aliorithi kwa Mtume)."

Allama Mustafa Beck Najeeb wa al-Azhar, Cairo amesema:

خَرَجَ اِلَي الدُّ نْيَا وَ الثَّهَادَةُ مَكْتُوْبَهَّ عَلي جَبَيْنِهِ وَ خَرجَ مِنْهَا وَ الثَّهَادَةُ مَكْتُوْبَهَّ عَلي دَ لِكَ الجَبَيْنِ بضَرْبَهِ حُسَّا مٍ لَقدْ كَمَا عَلِمْنَا فِي الْكَعْبَهِ وَ ضُربَ كَمَ عَلِمْنَا فِي الْمَسْجِدِ قأَيَّه بَدَايَهٍ وَ نِهَايَهٍ اَثْْبَهَ بالْحَيَاةِ الّتي بَيْنَهُمَا مِنْ تِلْكَ الْبدَايَهٍ وَ تِلْكَ النَّهَايَهِ؟

"Imam 'Alî amekuja duniani na shahada imeandikwa kwenye kipaji chake; na ameondoka duniani na shahada vile vile imeandikwa kwenye hicho kipaji kwa dharba ya upanga. Kama tunavyojua amezaliwa ndani ya Ka'bah, na kama tujuavyo amepigwa dharba (ya upanga) msikitini. Ilioje ajabu? Mwanzo wake na mwisho wake kupata darja ya kifo cha kishahidi."

Sheikh Abbas Mahmud al-Aqqad - mwandishi maarufu wa Ki-masri amesema:

"Mtu yeyote ambaye amebobea katika lugha ya Ki-arabu atakubali tu kwamba Nahju 'l-Balaghah inafuata kwa ubora wake baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Maneno ya 'Alî ni yenye maana na fikra nzito. Kwa hivyo Nahju 'l-Balaghah lazima isomwe kwa makini, na irejewe na idondolewe na wanafunzi na walimu. Ninapenda kutilia mkazo kwamba Nahju 'l-Balaghah iingizwe kwenye mukhtasar wa masomo na mafundisho (syllabi) ya vyuo vikuu vyote vya Masri na Beirut kwenye masomo ya kiwango cha juu ya lugha na falsafa."

Sheikh Muhammad 'Abdo - Mufti wa Masri na Profesa wa lugha ya Kiarabu na falsafa amesema:

تَحْتَ كَلاَمِ الْخَالِق وَ فَوْقَ كَلا مِ الْمَخْلُوق

"Mtu yeyote hawezi kukataa kwamba 'Alî alikuwa Imamu wa makhatibu, mwalimu na kiongozi wa waandishi na wanafalsafa. Bila ya shaka khutba zake na maneno yake ni yenye kiwango cha juu kabisa kushinda maneno ya mtu ye yote isipokuwa maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake:"

'Abd-ul-Masîh al-Antaqi - Mhariri wa Kikristo wa gazeti la Ki-masri Al- Ahram amesema:

'Alî alikuwa Imamu kwenye nyanja za vita, Imamu wa siasa, Imamu wa dini, Imamu wa falsafa, Imamu wa maadili, Imamu wa maandiko mbali mbali, na Imamu wa ilmu na hikma."

Profesa Muhammad Kamil, Cairo amesema:

فاِ دَا لَمْ يَكُنْ عَلِيّ نَبِيًّا فلَقدْ كَانَ خُلُقُهَ نَبَو تًّا.

"Ijapokuwa Imam 'Alî alikuwa si nabii, lakini khulqa yake ilikuwa ya kinabii."

Shaykh Nasif al-Yazidi alipokuwa akimwaidhi mwanawe alimwambia: “Kama unataka mamlaka ya juu kabisa dhidi ya wenzako katika masomo, hikma, maandiko, inshaa n.k. basi hifadhi Qur'ani Tukufu na Nahju 'l- Balaghah”.

Amîn Nakhlah anasema: “Mtu yeyote anayetamani kuikata kiu yake (ya kiroho) kwa maneno ya 'Ali (a.s) lazima ausome kila ukurasa wa Nahju 'l- Balaghah kwa uangalifu.

Nahju 'l-Balaghah ni diwani ambayo humfanya kila mtu kuukubali ubingwa wa Imam 'Ali (a.s) Hakuna kitabu kinachoweza kuishinda Nahju 'l- Balaghah isipokuwa Qur'ani Tukufu.

Humo ndani ya Nahju 'l-Balaghah utazikuta lulu za maarifa zilizotungwa kwenye mikufu mizuri, utayakuta maua ya lugha ambayo huifanya akili ya binadamu inukie kwa harufu nzuri ya ushujaa na uungwana; vile vile humo utaikuta mito ya lugha safi ambayo ni mitamu na baridi zaidi kuliko mto wa al-Kauthar.

Imam 'Alî (a.s) anawaidhi juu ya maudhui mbali mbali, k.m. Kuumbwa kwa ardhi na mbingu, tawhîd, taqwa, malaika, zuhd, Qiyamah, kiburi, tamaa, vita vya Jamal, Siffin, Nahrawan, ibada, maarifa, tamaa, imani, insafu, n. k.

Katika mithali yake mashuhuri Imam 'Alî (a.s) anatuwaidhi sisi wanaadamu kutobaguwana kwa makabila.

"Watu kwa makamu ni sawa sawa

Baba ni Adamu na mama Hawa

Ukijia'dhimu kwa kuzaliwa

Maji na kinamu uliumbiwa

Fahamu na jua mwana Adamu"

Maneno haya ya Sayyidna 'Alî yamo katika msingi wa Qur'ani Tukufu. (Sh. 'Alî Muhsin al-Barwani).

Tunatumai wasomaji wetu watastafidi sana na tarjama hii ya Nahju 'l-Balaghah (kwa lugha ya Kiswahili) ambayo imefanywa kwa kifundi na ujuzi mkubwa. Mwenyezi Mungu atujaalie tawfiq ya Kutenda Kheri na atuepushe na kila shari.

Wa Billahi Tawfîq,

Dr. Ja'far A. Tijani.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

56 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na miongoni mwa maneno yake(a.s) - Zamakhshari ameieleza hotuba hii katika Rabiul-Abraar, mlango wa Al-qatil wa shaha- da. Na ibn Muzahim katika kitabu Swifiin, uk. 520.

SIKU YA SIFFIIN ALIPOWAAMURU WATU KUFANYA SULUHU

“Kwa hakika tulikuwa na Mtume wa Mungu(s.a.w.w) ; tunawaua baba zetu na watoto wetu na ndugu zetu na ammi zetu. Hilo lilikuwa halituzidishii kitu isipokuwa imani na kusalimu amri, na kuendelea ndani ya njia ya sawa na kuvuta subira kwa machungu yake na umakini katika kumpiga vita adui. Alikuwa mtu kutoka upande wetu na mwingine kutoka kwa adui yetu wanashambuliana kama wanavyoshambuliana maksai wawili kwa pembe wakitoana nafsi zao, yupi miongoni mwao atawahi kumnywesha mwenzake kikombe cha umauti, basi mara ilikuwa sisi twafanikiwa dhidi ya adui yetu na mara nyingine anafanikiwa adui yetu dhidi yetu, Mungu alipoona ukweli wetu aliwateremshia adui zetu udhalili na kutelekezwa, na aliteremsha kwetu nusura, kiasi cha Uislamu kuimarika na kumakinika na kukaa mahali pake.

“Namuapa Mungu lau tungekuwa tunayafanya mliyoyafanya, dini haingekuwa na nguzo[1] , ya kutuwama wala imani tawi lake halingesitawi. Wallahi mtamkamua damu[2] na mtamfuatilia na majuto[3] .”

57 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na miongoni mwa maneno yake(a.s) - Khutba hii ameieleza Al-Baladhuriy ndani ya Ansabul-Ashraafi) katika tarjuma ya Ali(a.s) , na Al’Haakim ndani ya Al’Mustadrak, Jz. 2, uk. 385, na At-Tuusi ndani ya Al-Amaali uk. 214 na 347, na wengine.

AKIWAPA HABARI KUHUSU MTU ATAKAYEAMRISHA ATUKANWE IMAM(A.S)

“Punde baada yangu atapata ushindi juu yenu mtu mwenye koo pana, tumbo kubwa, ala akionacho, na huomba asichoweza kukipata, basi muuweni, na hamtomuuwa[4] . Lo! Kwa hakika yeye atawaamrisheni mnitukane, na kujiepusha na mimi; ama kuhusu kutukana nitukaneni, kwa kuwa hiyo kwangu ni utakaso na kwenu ni uwokovu; ama kuhusu kujiepusha na mimi; wala msijiepushe na mimi; kwa kuwa mimi nimezaliwa ndani ya fitra na kutangulia katika imani na hijra.[5]

58 - NA MIONGONI MWA USEMI WAKE(A.S)

Na miongoni mwa usemi wake (a.s) - Ibn Qutaybah ameieleza ndani ya Al’Imama was-siasa Jz. 1, uk.124. Na Sibtu Ibnul’Jauziy katika Tadhkiratul’khawasi uk.100.

Aliwasemesha Khawarij

“Tufani iwakumbeni, wala asibakie miongoni mwenu chakubimbi. Hivi baada ya imani yangu kwa Mungu, na jihadi yangu pamwe na Mtume wa Mungu(s.a.w.w) nijishuhudie binafsi kuwa ni kafiri!

قَدْ ضَلَلْتُ إِذًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُهْتَدِينَ ﴿٥٦﴾

“Hivyo basi nitakuwa nimepotea wala sitokuwa miongoni mwa walio ongoka.” (6:56).

Rejeeni marejeo ya shari, rejeeni mkifuata athari ya nyayo. Angalieni! kwa hakika mtapata udhalili baada yangu wa sura ya jumla, na upanga mkali wenye kukata, na hilo litachukuliwa na wadhalimu hao kwenu kuwa ni sunnah.[6] ”.

Maelezo

Ar-Radhiy (r.a) amesema: Usemi wake(a.s) huelezwa katika njia tatu: Iwe kama tulivyosema: kwa raa, kutokana na kauli yao kwa mtu ambaye anapandikiza mtende, yaani yuautengeneza vizuri. Na yaelezwa kwa na yakusudiwa kwalo yule aelezaye Hadithi, na kuizungumzia na hii ndiyo njia sahihi kwa maoni yangu. Kama kwamba(a.s) amesema: Habakii kati yenu msimuliaji. Na huelezwa kwa tamko kwa nayo hukusudiwa mwenye kuchupa na mwenye kuhiliki pia huambiwa.

59 - NA ALISEMA(A.S)

Alipoazimia Kuwapiga Vita Khawarij, Na Aliambiwa: Kwa Hakika Hawa Watu Wamekwishavuka Daraja La An-Nahrawaan

Hapo alisema: “Maangukio yao ni chini ya nutfa, Wallahi hawaponyoki kumi miongoni mwao,[7] na wala hawatokufa isipokuwa kumi miongoni mwetu.” Sharifu Ar-Radii (r.a) amesema: nutfa anakusudia maji ya mto wa Furaat na hili ni jina mbadala zuri mno kwa maji japo maji yawe mengi. Na hilo tuliliashiria hapo nyuma wakati wa kulipita linaloshabihiana nalo.

60 - NA AMESEMA(A.S)

Na Alisema(a.s) - Ameieleza al-Mubaridu katika al-Kamil Jz. 2, uk. 120, na al-Baihaqiy katika al- Mahasin wal Masawi uk. 380, katika mlango Mahasinus-Swidiqi, na Mas’ud katika Muruj al-Dhahab, Juz. 2, uk. 416.

Walipouliwa Khawarij Aliambiwa: “Ewe Amirul-Mu’minina, Hawa Jamaa Wameangamia Wote!” Ndipo Aliposema:

“Lahasha wallahi: wao ni nut’fah ndani ya migongo ya wanaume na mifuko ya uzazi ya wanawake, na kila kiongozi akijitokeza[8] kati yao hukatwa mpaka wa mwisho wao wawe wevi vibaka”.

61 - NA ALISEMA(A.S.)

KUHUSU KHAWARIJ

“Msiwapige vita Khawarij baada yangu; kwa kuwa sisawa kati ya mwenye kuutafuta ukweli na akakosea na ambaye ameitafuta batili na kuipata (amkusudia Muawiya na sahaba zake).[9] ”.

62 - NA KATIKA MANENO YAKE(A.S)

Na Katika Maneno Yake(a.s) - As-Saduq ameinakili katika Man laa Yahdhuruhu al-Faqih, jalada la kwanza, uk. 329, na Abu Na’im katika al-Hiliyatu, jalada la kwanza, uk. 77, na at-Tusi katika al-Misbahu, uk. 461, na al-Mufid katika al-Amaal, uk. 87.

Pindi Alipohofishwa Kuuliwa Ghafla (Akasema)

“Kwa hakika mimi nina ngao madhubuti kutoka kwa Mungu, siku yangu itakapokuja itajitoa mbali na mimi na kuniachia; wakati huo mshale hautokosea wala jeraha halitopona.”

63 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Ameieleza Zamakhshari katika Rabiul-Abrar, na ameieleza mwanzoni mwake Ibn Kathir katika al-Bidaya wan-Nihaya: Jz. 8, uk. 12.

AHADHARISHA FITNA ZA DUNIA

“Lo! Kwa kweli dunia hii ni mahali ambapo usalama haupatikani ila mtu akiwa yumo humo,[10] tendo lililofanywa kwa ajili ya dunia tu haliokoi[11] .

Watu wamekabiliwa na mtihani wa maafa, walivyovichuma humo kwa ajili yake (ya dunia) watatolewa nje yake (kwa kifo) na kuhesabiwa dhidi yao[12] , na walivyovichuma kutoka humo (kwa kutenda mema) si kwa ajili ya dunia - kwa ajili ya ya akhera - watavipata, na kubaki navyo humo; kwa kuwa hiyo – dunia - kwa wenye akili ni kama kivuli mara chajitanuwa na kujieneza punde chajikunja na kupungua.” Ameitaja al-Amidi katika kitabu Ghurarul-Hikami, chini ya herufi ‘inna.’

64 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameieleza ibnul-Jauz katika Tadhkira yake, uk. 145, na ameitaja al-Aamidi katika al- Ghuraru wal-Duraru.

KUHUSU KUJIANDAA KWA AJILI YA MAUTI:

“Mcheni Mungu enyi waja wa Mungu, zitanguliyeni ajali zenu kwa matendo yenu (mema), na mnunuwe kinachobaki kwa ajili yenu kwa kinachowatokeni[13] , tokeni kwani mmehimizwa[14] , na jiandaeni kwa ajili ya umauti kwani hakika umewakurubia, na muwe kaumu ya watu waliopigwa kelele wakaamka[15] , na wakajua kuwa dunia kwao sio nyumba ya kubaki na wakaibadili; kwa kuwa Mungu (s.w.t) hakuwaumbeni kwa mchezo bila ya lengo[16] , na wala hakuwaacheni bure[17] , na hakuna kitu (kinachozuia) kuingia mmoja wenu jannah au moto ila ni mauti[18] .

Na kwa kweli ni lengo linalopunguzwa na muda mfupi mno, na kubomolewa na saa, kadiri[19] inayopunguzwa na punde na kuharibiwa na saa yabidi izingatiwe kuwa ni fupi mno.

Na hakika ghaibu inayosukumwa na mabadiliko mawili mapya, yaani usiku na mchana, ni ya haraka mno kurejea. Msafiri anayerudi ama amefaulu au kutofaulu yu astahiki kuandaliwa masurufu bora.

Hivyo basi jiandalieni masurufu duniani kutoka duniani,8 kwa ambayo mtazihifadhi nafsi zenu kesho, kwa hiyo mja akimcha Mola wake Mlezi atakuwa ameinasihi nafsi yake, na atakuwa ameitanguliza toba yake, na atakuwa ameyashinda matamanio yake, kwa kuwa kifo chake kimefichwa, na matumaini yake yanamhadaa, na Shetani amefanywa kwake wakala, yuampambia maasi ili ayatende, na yuamshawishi kuchelewesha toba kwa kujifanya nitatubu baadae, kifo kitakapomhujumu kitamsahaulisha aliyonayo.

Lo! Hasara iliyoje kwa mwenye kughafilika ambaye umri wake utakuwa hoja dhidi yake, na siku zake zimfikishe kwenye maafa! Tunamuomba Mungu (s.w.t) atujaalie na ninyi tuwe miongoni mwa ambao neema hai- wafanyi wajivune wala lengo haliwafanyi wazembee kumtii Mola Wao, wala baada ya umauti hafikwi na majuto wala huzuni.”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

65 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameitaja hotuba hii as-Saduq katika at-Tawhiid, uk. 19 na 62. Na al-Aamidiy katika Ghurarul-Hikami, uk. 238.

KATIKA KUMTAKASA MWENYEZI MUNGU (S.W.T)

“Himidi ni za Mwenyezi Mungu ambaye hali (Yake) haikutanguliwa na hali[20] .

Kwa hiyo anakuwa wa kwanza kabla hajawa wa mwisho na anakuwa wa dhahiri[21] , kabla hajawa baatin[22] ; kila chenye kuitwa moja kisichokuwa yeye ni kichache[23] , na kila mtukufu asiyekuwa Yeye ni dhalili[24] . Na kila mwenye nguvu asiyekuwa yeye ni dhaifu, na kila mfalme asiyekuwa Yeye ni mmilikiwa, na kila mjuzi asiyekuwa Yeye ni mwanafunzi[25] , na kila muweza asiyekuwa Yeye ni mwenye kuweza na kushindwa[26] . Na kila msikiaji asiyekuwa Yeye hasikii sauti iliyo dhaifu mno[27] .

Na kubwa zamfanya kiziwi, na za mbali humpita, na kila muonaji asiyekuwa Yeye haoni rangi hafifu na miili nyeti, na kila kilicho dhahiri kisichokuwa Yeye ni baatin, na kila batini kisichokuwa yeye si baatini[28] . Hakuumba alivyoviumba ili kuimarisha mamlaka wala kuhofia matukio magumu ya zama, wala kujisaidia dhidi ya anayelingana naye mwenye kuhujumu, wala mshirika mwenye kujigamba kwa wingi, wala mpinzani mwenye kujiona kuwa yuko zaidi, lakini ni viumbe wenye kumilikiwa, waja walio dhalili. Hawi kwenye vitu: hata isemwe kuwa Yeye yu ndani yake, hajawa mbali navyo kiasi cha kusemwa:

Yumbali navyo[29] . Hakuchoshwa na kuumba alivyovibuni[30] ,wala kuviratibu alivyoumba, haikumtokea kushindwa na alivyoviumba, wala hakuingiwa na mkanganyiko kuhusiana na aliyoyahukumu na kuyafanyia makadirio [31] ,12 bali ni hukumu iliyofanywa kwa umakini, na ilimu iliyo madhubuti, na ni jambo lililobidi, mwenye kutumainiwa pamoja na kuwa yu anaadhibu, mwenye kuogopwa japokuwa ni mwenye kuneemesha.”

66 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Al-Bayhaqi ameyaeleza maneno haya katika kitabu al-Mahasin, uk. 45, na Ibn Asakir katika Ta’rikh Damishqi, na Ibn Qutaiba katika Uyunul-Akhbar, 1: 110.

AWAAMBIA SAHABA ZAKE KATIKA BAADHI YA SIKU ZA SIFFIIN

“Enyi Waislamu! Ifanyeni hofu ya ucha Mungu iwe kuwa ndio nguo yenu ya ndani, na ufanyeni utulivu kuwa joho lenu. Umeni meno, kwani kufanya hivyo hudugisha mno panga kwenye fuvu la kichwa.

Kamilisheni kuvaa ngao, zitikiseni panga ndani ya ala zake kabla ya kuzichomoa, mwangalieni adui kwa kijichopembe cha ghadhabu, pigeni kwa panga zenu pande zote, kushoto kulia, pambaneni kwa panga, juweni kuwa mpo mbele ya macho ya Mungu, na mpo pamoja na mwana wa ammi yake Mtume wa Mungu, jizoesheni kurejea tena na tena, kwenye mapambano, oneni haya kukimbia[32] ; hiyo ni aibu kwa vizazi vijavyo[33] , na ni moto siku ya hesabu.

Yatoeni maisha yenu (kwa Mungu) kwa hiyari, na yaendeeni mauti mwendo wa rahisi, jihadharini na kundi hili kubwa[34] , na hema lililofungwa kwa kamba, pigeni katikati yake, kwa kweli Shetani amejificha pembeni mwake, ameunyosha mkono wake tayari kwa kushambulia, na kuubakisha nyuma mguu kwa kukimbia.

Bakieni thabiti katika kusudi lenu! Mpaka ikudhihirikieni nguzo ya ukweli; “Ninyi ndio washindi, na Mungu yu pamwe na ninyi, wala hatopunguza (thawabu za amali zenu).[35] ”.

67 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na miongoni mwa semi zake(a.s) - Ameieleza An-Nuweiry mwanzo wake katika kitabu Nihayatul-Irbi, Jz. 8, uk. 168.

Wamesema: Na zilipomfika Amirul-Mu’minin habari za Saqiifah[36] , baada ya kutawafu Mtume(s.a.w.w) alisema Ali(a.s) :

“Wamesema nini Ansar?” Wakasema: Wamesema: Sisi tuwe na amiri na ninyi muwe na amiri; akasema(a.s) : “Je hamkuhoji dhidi yao kuwa Mtume ameusia atendewe mema aliye mwema miongoni mwao na asame- hewe muovu wao!?”

Wakasema: Katika hili hakuna hoja yoyote dhidi yao? Akasema(a.s) : “Lau uimamu ungekuwa katika wao, wasingeusiwa.” Kisha akasema(a.s) : “Basi nini walisema maquraishi?” Wakasema: Wametoa hoja kuwa wao ni mti wa Mtume(s.a.w.w) . Akasema(a.s) : “Wameutolea hoja mti na wamelipoteza tunda.[37]

68 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - * Tabariy ameieleza khutba hii ndani ya matukio ya mwaka wa 36, na Al’Baladhuuriy ndani ya Ansabul-Ashrafi, uk. 404, chapa ya Al’aalamiy. Alipomteua Muhammad bin Abi Bakr kuwa Gavana wa Misri, alizidiwa na kuuliwa:[38]

“Nilitaka kumtawaza Hashim bin Utba huko Misri[39] ; lau ningemtawaza yeye Misri pasingebakia eneo, na wasingepata fursa, bila ya kumlaumu Muhammad bin Abi Bakr, kwa kweli alikuwa mpenzi kwangu na kwangu alikuwa (rabiiba).” * Rabiiba - mtoto wa kamsbo.

69 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Al-Baladhuriy ameieleza hii katika Ansabul-Ashraf, uk. 438 katika tarjuma ya Ali(a.s) .

KUWALAUMU SAHABA ZAKE

“Kwa kadiri gani niwatendee kwa upole kama atendewavyo ndama wa ngamia aliyeraruka nundu yake kwa ndani, na nguo iliyochoka, kila ishonwapo upande mmoja wararuka upande wa pili, na wanapokupitieni askari wa Sham, kila mmoja wenu huufunga mlango wake, na hutokomea utokomeaji wa guruguru shimoni mwake, na fisi ndani ya tundu lake.

Wallahi dhalili ni yule mliyemnusuru! Na mwenye kutupa mshale kwa msaada wenu ni sawa na atupae mshale uliovunjika pande zote mbili. Ninyi mnakuwa wengi kwenye kumbi za nyumba, na mnakuwa wachache chini ya bendera.

Mimi najua kinachoweza kuwarekibisha, na kunyoosha kupindama kwenu, lakini mimi Wallahi sitowarekebisha kwa kujiharibu binafsi. Mungu azidhalilishe nyuso zenu, na aangamize hadhi zenu, hamuujui ukweli kama muijuavyo batili, wala hamuibatilishi batili kama mubatilishavyo ukweli.”