NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI33%

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Mwandishi:
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi: VITABU VYA HADITHI

Juzuu 1 Juzuu 2
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9478 / Pakua: 4863
Kiwango Kiwango Kiwango
NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

89 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - al-Qummiy ameisema katika Tafsiir yake uk. 3, na al-Kailaniy katka Usuli, uk. 69.

AZIELEZEA HALI ZA WATU WALIVYOKUWA KABLA YA BI’ITHA:

“Amemtuma wakati wa mwanya baada ya mitume[159] , na usingizi mrefu kati ya umma, na kukithiri kwa fitna, na kuenea kwa mambo, na kulipuka kwa vita, na dunia imetoweka nuru, ghururi imejitokeza; wakati jini lake limekuwa manjano, na kukatishwa tamaa na matunda yake[160] .

Na kutoweka maji yake, minara ya uongofu imefutika, na zimejitokeza alama za kuangamiza, na zimefinya nyuso zao[161] , mwenye kukunja uso mbele ya mwombaji wake, tunda lake ni fitna, na chakula chake ni mzoga[162] , na nguo yake ya ndani ni woga, na nguo yake ya juu ni upanga[163] ,hivyo zingatieni enyi waja wa Mungu, na (ikumbukeni ile)[164] ambayo baba zenu na ndugu zenu wako rehani[165] , kulingana nayo watahesabiwa. Kwa umri wangu, muda wenu haujapishana sana na wao, wala haijapita kati yenu na wao miaka wala ummah, wala ninyi hii leo na siku mlizokuwa migongoni mwao sio mbali.

Wallahi Nabii hakuwasemesha kitu ila hii leo na mimi ni mwenye kuwasemesha nacho, na ambalo mmelisikia leo haliko tafauti na walilo sikia jana. Macho hayakuwa wazi kwao, na mioyo iliyokuwa kwa ajili yao wakati ule, ni sawa na ile mliyo nayo hivi sasa.

Wallahi hamkuwa mmeambiwa chochote baada yao ambacho hawakuwa wanakijuwa, na hamkupewa chochote ambacho wao walinyimwa, na kwa kweli balaa imewashukieni[166] , inayumba hatamu yake, kamba yake iliyolegea. Isi kughurini hali waliyo nayo watu walioghurika, kwani hicho ni kivuli kilichopanuka mpaka muda uliopangwa[167] .

90 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - al-Wasiti ameisema katika Uyunul-Hikami, na al-Aamidi katika Ghuraru-Hikami uk. 185, na Ibn al-Athir katika an-Nihaya, Jalada la 2, uk. 345.

KUHUSU BAADHI YA SIFA ZA VIUMBE

“Shukrani ni zake Mungu (s.w.t) aliye maarufu bila ya kuonwa, na ambaye ni muumba bila ya kufikiri[168] ,na ambaye hakukosa kuwapo yu thabiti daima[169] ; pindi hapakuwa na mbingu zenye njia kuu za sayari (zodiac), wala pazia zenye vifungo vikubwa vya fahari[170] , wala usiku wenye giza, wala bahari tulivu, wala jabali lenye njia, wala njia yenye kupinda pinda, wala ardhi yenye tandiko, wala viumbe wenye nguvu na kutenda kwa makusudi na utashi, Yeye ndiye mwenye kubuni uumbaji na mwenye kubaki baada yao, Mungu wa uumbaji na mtoaji wa riziki.

Jua na Mwezi vinatembea kwa uthabiti katika ridhaa Yake. Vinakifanya kikuukuu kila kipya, na kila kilicho mbali vinakisogeza karibu.

“Amezigawa riziki zao, na amedhibiti kwa idadi athari zao[171] , na amali zao, idadi ya pumzi zao, na ishara za kukonyeza kwao, na ambayo yafichwa na vifua vyao miongoni mwa dhamiri[172] ,Anajua makazi yao ya muda, na mahali pa makazi yao ya kudumu, hali wakiwa katika matumbo ya uzazi na migongoni[173] ,mpaka wafikiapo mwisho wao.

“Yeye ndiye ambaye adhabu Yake itakuja kuwa kali kwa maadui zake japokuwa huruma Zake ni zakutosha. Na rehema Zake zimewaenea wapenzi wake japokuwa adhabu Yake ni kali. Humdhibiti anayekusudia kumshinda Yeye.

Muangamizaji wa anayempinga, na humdhalilisha amuendae kinyume, mshindi wa amwendeaye kwa uadui. Humtosheleza amtegemeaye, na mwenye kumuomba humpa, na mwenye kumkopesha anamlipa[174] , Na mwenye kumshukuru humlipa.

Enyi waja wa Mungu! Jipimeni wenyewe kabla hamjapimwa, na jihesabuni kabla hamjahesabiwa, na pumuweni kabla ya koo halijasonga. Ongokeni kabla ya kusukumwa kwa nguvu[175] .

Na jueni kuwa asiyesaidiwa na nafsi yake kiasi cha kuwaidhika nayo na kuwa mwenye kujikemea, hatowaidhika kutoka kwa mwingine, si mkemeaji wala si muwaidhi.[176] ”.

91 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ibn Abd-Rabi ameitaja katika al-Iqdul-Farid, jalada la pili, uk. 406, na al-Saduq katika at-Tawhiid, uk. 34.

IJULIKANAYO KUWA NI KHUTBA YA AL’ASH’BAAHU, NAYO NI MIONGONI MWA KHUTBA TUKUFU MNO:

Al’ash’baahu: Al’ash’khaasu ni watu, na waliokusudiwa hapa ni malaika, kwa sababu khutba ndanimwe muna utajo wa malaika.

Mas’adah bin Sadaqah ameeleza akinukuu kutoka kwa as-Sadiq Ja’far bin Muhammad(a.s) , kuwa yeye alisema: Amirul’mu’minina(a.s) aliitoa khutba hii juu ya mimbari ya (mji wa) Kufa hivyo ni kwa sababu mtu mmoja alimjia na akamwambia: ‘Ewe Amirul-Mu’minin! Tusifie Mola wetu iwe kama twamuona bayana ili tuzidi upendo na kumtambua.’

Hapo alighad- hibika(a.s) na akanadi: ‘Asalaatu jaamia,’ Hivyo watu walijumuika kwake kiasi cha kuwa msikiti ulijaa watu, hapo basi(a.s) alipanda mimbari akiwa ameghadhibika, rangi imembadilika, alimuhimidi Mungu na kumsifu na alimsalia Nabii sala llahu alayhi wa Aalihi, kisha akasema:

“Alhamdu-lillahi - utukufu ni wake Mungu ambaye kuzuia na ubahili hakumzidishii utajiri, wala kutoa na ukarimu hakumfanyi kuwa fakiri, kwa kuwa kila mtoaji asiye kuwa yeye ni mwenye kupungukiwa, na kila mzuia- ji ni mlaumiwa mbali na yeye[177] .

Na yeye ni mtoaji sana wa faida za neema, na rejea za ziada na mgawanyo. Wamtegemeao ni viumbe, amechukua dhamana ya riziki zao, na amekadiria vyakula vyao, na amefanya njia kwa wapendao kuziendea, na kwa watakao yaliyo kwake, wala si mkarimu sana kwa aliloombwa kulinganisha na asiloombwa[178] . Ni wa Mwanzo ambaye hapakuwa na wa kabla hata iwe kabla yake kulikuwa na kitu, na ni wa Mwisho ambaye hana wa mwisho baada yake hata iwe kuna kitu baada yake, ni Mwenye kuizuia mboni ya jicho isiambue kitu Kwake au kumdiriki, Kwake hazibadililki zama kiasi cha kumfanya Yeye abadilike hali, au awe mahali ili iwe jaizu Kwake kugura.

“Lau angetoa ambavyo madini ya milima imevipumua[179] , Na zimemchekelea chaza za bahari mfano wa dhahabu, fedha, na madini ya fedha ya aina makhsusi, na dhahabu iliyo halisi, na mtawanyiko wa lulu na mavuno ya marijani. Hilo lisingeathiri kitu katika ukarimu wake, wala usingekwisha wingi wa aliyonayo, na Kwake kungekuwa hazina ya wanyama ambayo isiyomalizwa na mahitaji ya viumbe, kwa kuwa Yeye ni Mpaji ambaye hamalizwi na ombi la waombaji, wala kunga’ng’ania kwa waombaji hakumfanyi awe bakhili.

“Basi ewe muulizaji, zile ambazo Qur’ani imekujulisha katika sifa Zake msifu nazo na faidika na mwanga wa mwongozo wake, na elimu ambayo Shetani amekutwisha nayo ambayo haiko Kitabuni wajibu wake juu yako, wala ndani ya Sunna ya Nabii(s.a.w.w) wala athari ya Maimamu waongofu, iwakilishe elimu yake kwa Mungu (s.w.t), kwa kuwa huo ni mwisho wa haki ya Mungu kwako.

Na tambua kuwa waliojikita katika elimu ndio ambao Mungu amewatosheleza kwa kutoivamia milango iliyofungiwa ya yasiyojulikana. Kukiri jumla ya wasioyajua ni tafsiri ya ghaibu iliyofichikana, Mungu akawasifu kutambua kwao kushindwa kuyapata wasiyo yazunguka elimu yake.

Amekuita kuacha kuzama katika wasiyokalifishwa kutafuta kumjua alivyo kuwa ni kuimarika, hivyo basi tosheka na hayo, usiupime utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kipimo cha akili yako utakuwa miongoni mwa wenye kuhiliki.

“Naye ni Muweza ambaye endapo fikra zimekwenda ili ziudiriki mwisho wa uwezo wake, na fikra zilizoepushwa na hatari ya wasiwasi zikajaribu kutaka kuiona hakika ya dhati Yake, na nyoyo kuwa na shauku ya kutam- bua hakika ya sifa Zake, na maingilio ya akili kuwa mazito, kwa kuwa sifa hazimfikishi ili kuipata hakika ya dhati Yake, anazirudisha nyuma. Na zitarudi hali zimeshindwa, hali zikitambua kuwa uhakika wa ilimu yake hauwezi kufahamika kwa njia iliyopotoka, wala hauingii akilini mwa wanafikra fikra yeyote, katika kukadiria ukubwa wa utukufu Wake.”

KUUMBA ULIMWENGU

“Ambaye amebuni viumbe bila ya mfano aliofananisha[180] , wala hakuchukua kipimo na kulinganisha kutoka kwa muumba muabudiwa aliyekuwa kabla yake, na akatuonesha milki ya uwezo Wake, na ajabu zili- zotamkwa na athari ya hekima Yake. Na kwa viumbe wote kutambua kuwa ni wahitaji (hawana) ila awashike kwa nguvu Zake. Jambo ambalo limetufanya tumjue ni kuthibiti hoja ya dhahiri kwetu (dhidi yetu) na dalili ya kumtambua, japo viwe viumbe visivyosema.

Hivyo basi hoja yake ni kwa mazingatio yatamkayo, na dalili yake kwa muumba ipo wazi[181] .

“Hivyo basi nashuhudia kuwa mwenye kukushabihisha na mtengano wa viungo vya miili ya viumbe Wako, na kushikana ncha za mifupa yao iliyositiriwa ili kuizingatia hekima Yako, dhamira yake haijawa na maari- fa ya kukutambua Wewe, na wala moyo wake haujagusa yakini kuwa hauna kifani, kana kwamba hakusikia kujitakasa kwa wafuasi mbali na wenye kufuatwa watakapokuja kusema: ‘Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio bayana. Tulipokuwa tunakufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote!’ (26:96-97)*

“Wamedanganya wanaokulinganisha, walipokushabihisha na sanamu zao, na wakakupamba na mapambo ya viumbe kwa dhana zao, na wakakufanya (uko) sehemu sehemu ufanywaji sehemu wa vitu vyenye miili kwa fikra zao, na wakakulinganisha na viumbwa vyenye kutofautiana nguvu kwa uwezo wa fikra ya akili zao. Na ninashuhudia kuwa mwenye kukufanya uko sawa na kitu chochote katika viumbe wako anakuwa amekufanyia mfano, na mwenye kukufanyia mfano ni kafiri wa yaliyoteremka miongoni mwa aya Zako za wazi na kuelekezwa na ushuhuda wa hoja Zako zilizo bayana, (pia nashuhudia) kuwa Wewe ni Mungu haujafungwa kwenye mabano ya akili ili uwe kwenye mwelekeo wa kifikra mwenye kugeuka geuka[182] , wala katika fikra yake mwenye namna, wala si katika mawazo yake mwenye mipaka, mwenye kukubali kubadilika.

BAADHI YA SEHEMU YA KHUTBA HII HII

Kuhusu ukamilifu mkubwa wa uumbaji Wake (s.w.t): “Miongoni mwayo: Amekadiria alivyoviumba na kuimarisha makadirio Yake, na amepanga na akaufanya mpango mzuri, na akaelekeza mwelekeo wake, wala haukuvuka mpaka wa ngazi yake, wala kuzembea kwa kutokufikia lengo lake, wala haikuona vigumu kutii utashi wake.

Na itakuwaje hali ikiwa mambo yametokea kulingana na utashi wake! Mbunifu wa sam- puli za vitu bila ya kuvuta fikra, wala kudhamiria kwa msukumo wa silka[183] , wala hakufaidika na uzoefu wa matukio ya zama, wala hakusaidiwa na mshirika kubuni mambo ya ajabu, umbo lake likatimia, na kutekeleza utii wake, na kuitikia wito wake, na viumbe vikaitika wito wa muumba, kulingana na wajibu wa maumbile yake bila ya ujahili akavinyosha vitu vilivyopinda, na aliainisha mipaka yake na kwa uwezo wake ameunganisha kati ya vinavyopingana, na aliziunganisha (kamba za nafsi) na kuifarikisha jinsi tofauti katika mipaka na makadirio, silka na namna, ubunifu wa viumbe akaimarisha umbo lao, na ameviumba alivyopenda na kuvibuni.”

Na Miongoni Mwayo Kuihusu Sifa Ya Mbingu

“Na amefanya mwanya (s.w.t) kati ya miili - yaani sayari za angani - moja na nyingine miongoni mwa sayari za angani na kuiweka katika nidhamu bila ya kuuangika moja na nyingine na bila ya kuifunga na ala ihisiwayo. Na amesawazisha miatuko ya mianya yake[184] , na akafuma kati ya kila sayari na miili mienzake inayowiana nayo na kufanana miongoni mwa miili mingine katika tabaka la juu na chini kwa vifungo vinavyozishika (vifungo vya maanawiy, sio vya kimwili) vya mwinuko na vya bonde na akaziba mianya ya miatuko yake na amefuma (s.w.t) kati ya kila mbingu na miili yake na inayofanana nayo.

Na amerahisisha kuikurubia miinuko yake kwa (malaika) wateremkao na amri yake, na kwa wapandao wakiwa na amali za viumbe Wake. Mgumu upandaji wake.

Aliziita hali zikiwa bado mvuke ulio bayana[185] , mara moja viungo vyake viliungana na aliifungua milango yake hali ilikuwa imefungwa, na aliweka walinzi wa angani[186] yaani vijinga vipenyavyo kwenye njia zake, na akazishika zisiyumbe katika mapito ya upepo kwa mkono (uwezo) wake.

Na akaiamuru isimame kusalimu amri Yake, na amejaalia jua kuwa ni alama yenye kuangaza kwa ajili ya mchana wake, na mwezi ni alama yenye kufutwa katika baadhi ya usiku[187] . Na akazipitisha sayari mbili (jua na mwezi) kwenye mzunguko wake na akakadiria khatua za mienendo yao kwenye mapito yao, ili (kwa viwili hivi) aweze kubaini kati ya usiku na mchana na ipate kujulikana idadi ya miaka na hisabu kwa makadirio yao (jua na mwezi), kisha akaangika katika anga lake falaki (njia za sayari) na akaiambatanisha humo mapambo yake, miongoni mwa nyota zake (zajulikana kwa jina la “Duriyu”) nazo ni nyota zin’gaazo sana, na taa za nyota zake (hizi ni nyota ndogo ndogo), na aliwatupia waibao usikizi vijinga vyenye mwanga upenyao, na akazipitisha kwenye njia alizoziweka sawa kwa ajili ya iliyothibiti (miongoni mwa nyota zilizo thabiti mahali pamoja) na kwa ajili ya zenye kwenda kwa ziendazo (yaani tano zenye nuru, kwa kuwa daima ni zenye kwenda) kuporomoka kwao na kupanda kwao, na zile za ndege mbaya na ndege njema.[188] ”.

MIONGONI MWAYO KUHUSU SIFA YA MALAIKA

Kisha (s.w.t) aliumba viumbe ili awafanye kuwa wakazi wa mbingu zake, na kuzifanya mbingu ziwe na wenyeji tabaka za juu za milki yake, viumbe wapya, nao ni miongoni mwa malaika wake, na aliwajaza maeneo ya wazi katika mabonde yake, na aliwajaza sehemu tupu za anga Zake, na kati ya mwanya miongoni mwa hiyo mianya kuna kelele za sauti za (malaika) wafanyao tasbiihi wakiwa ndani ya maboma matakatifu[189] , na pazia za utukufu, na nyuma ya hayo kuna mtikisiko ambao masikio huziba, na tabaka za nuru zinakiwisha macho yasifike na kubaki yamezuilika kwenye mpaka wake, yaani zinapoishia nguvu zao, amewaumba wakiwa katika sura zilizo tofauti, na uwezo ulio tofauti, wenye mbawa wanautakasa utukufu wa enzi Yake, hawajidaii uungu binafsi, wala hawajigambi kuwa wanaumba kitu pamoja na Yeye miongoni mwa aliyojitenga nayo “Bali hao (wanaowaita wana) ni watumwa walitukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao hufanya kwa amri Zake.” 21:26-27.

“Mungu amewajaalia kuna ambao ni waaminifu kwa ajili ya wahyi Wake, na kuwatuma kwa manabii Wake wakiwa wabeba amri Zake na makatazo Yake.

Amewahifadhi dhidi ya kuwa na shaka ya utata, hivyo basi hapana yeyote miongoni mwao anayepotoka kando na njia ya maridhawa Yake.

Amewapa jinsi ya kufaidika na msaada na kuzifunika nyoyo zao adabu na unyenyekevu na amani, na amewafungulia milango laini ya kumtukuza, na amewasimamishia minara ya wazi ikiwa ni alama za tauhiidi Yake, uzito wa dhambi haukuwatopea, wala kupokezana kwa usiku na mchana hakujawamaliza au kuwageuza.

Wala shaka hazijashambulia kwa mishale uimara wa imani zao, dhana hazija songamana kwenye misingi ya yakini yao, wala chuki haijawasha moto kati yao, wala mbabaiko haujawapokonya walichoambatana nacho miongoni mwa maarifa Yake kwa dhamira zao, na kilichotulia miongoni mwa utukufu Wake na haiba ya utukufu Wake ndani ya nyoyo zao, wala wasiwasi haukuwa na tamaa kwao ya kuwatandazia kutu yake kwenye fikra zao.

Miongoni mwao kuna ambao wako katika uumbaji wa mawingu mazito ya maji, na walio kwenye milima mirefu, na walio katika maficho ya giza linaloduwaza. Na miongoni mwao kuna ambao nyayo zao zimetoboa ardhi ya chini nazo zikiwa kama bendera nyeupe zilizopenya kwenye penyo za hewa na chini yake kuna upepo uliotulia yaifunga kwenye mipaka inakoishia.

Shughuli za ibada Yake zimewatenga, hakika ya imani imekuwa wasila kati yao na maarifa Yake, yakini na Yeye imewakata na kuwafikisha kuwa na shauku Naye, upendo wao kwa Aliyonayo haukuvuka na kuwafikisha kwa aliyenayo mwingine. Hakika wameonja utamu wa kumtambua Yeye, na wamekunywa kwa gilasi ipozayo kiu kwa mahaba Yake, na imekita kwenye kiini cha mioyo yao kamba ya kumkhofia.

“Wamepindisha unyofu wa migongo yao kwa sababu ya urefu wa utii. Kwa kweli urefu wa matumaini Kwake haukumaliza mada ya unyenyekevu wao, wala ukubwa wa ukaribu haujawafungua tanzi za unyenyekevu wao, wala hawakutawaliwa na fahari, kiasi cha kuwafanya wakithirishe waliyoyatanguliza miongoni mwa mema, wala unyenyekevu wao kwenye utukufu wa Allah hauwaruhusu kuthamini mema yao, hawajapitiwa na utepetevu muda wote wa kudumu kwao, raghba yao haikupungua hata wahalifu kumtarajia Mola wao, wala ncha za ndimi zao hazikukauka kwa urefu wa faragha[190] , wala hawakukaliwa na la kuwashughulisha mbali na Mungu hata walazimike kunong’ona ili kuzipunguza sauti zao za juu kwa dua, wala mabega yao hayakutofautiana katika safu za utii, wala hawakuzipindisha shingo zao kwa raha ili kuzembea amri Yake, wala upuuzi wa mghafala haushambulii azma ya juhudi yao, wala hadaa za matamanio hazishambulii hima zao.

“Wamemfanya Mwenye Arshi kuwa ni akiba ya siku ya haja yao, na wamemkusudia Yeye kwa wayatakayo na matarajio pindi waja walipojitenga mbali na Yeye na kuwaelekea viumbe kwa wayatakayo, hawaufikii mwisho wa upeo wa ibada yake, kila wazidishapo utii wake huzidi msukumo wa kumuabudu miongoni mwa upendo na hofu.

Sababu za hofu hazijakatika mbali na wao, hata wadhoofu katika juhudi zao, wala hawakutekwa na tamaa hata watosheke na juhudi ndogo mbali na juhudi zao kubwa, hawakuuzingatia ukubwa wa amali zao zilizotangulia, lau wangezikuza hizo, matumaini yao yangefuta hali ya woga wao.

Wala hawajatofautiana katika Mola wao kwa kughilibiwa na shetani. Uovu wa kutengana kati yao haukuwatawanya. Wala chuki ya kuhusudiana haikuwatawala, wala shaka haikuwatawanya, wala hima tofauti hazikuwagawa, hivyo wao ni mateka wa imani, hauwaachii watoke nje ya tanzi lake, sio upotovu wala ukiukaji, wala udhaifu, wala utepetevu. Hakuna sehemu hata ndogo katika tabaka za mbinguni ila kuna malaika; ama yu katika sijida au yu kwenye juhudi mwenye haraka. Muda wote wa utii kwa Mola wao wanazidi elimu kumhusu Mola wao, na enzi na utukufu wa Mola wao Mlezi unazidi kuwa mkubwa nyoyoni mwao.”

SEHEMU YA KHUTBA KUHUSU SIFA YA ARDHI NA KUKUNJULIWA KWAKE JUU YA MAJI

“Ameingiza ardhi (s.w.t) kwenye harakati za mawimbi yaliyochafuka, na kilindi cha bahari iliyojaa, mawimbi yake yanapigana pigana yenyewe kwa yenyewe, na zinatoa povu mfano wa ngamia dume, upandaji wa maji yenye kupigana kwa sababu ya uzito wa mzigo wake ukarudi chini, na ukatulia mhemko wa kupigana kwake, pindi ardhi iliposhindilia kifua chake[191] ,ikanyenyekea ilipojigaragaza, ikawa baada ya kelele za mawimbi yake imetulia, yenye kushindwa na kuwa dhalili chini ya mateka ya unyonge, mateka mnyenyekevu.

Na ardhi ilitulia ikiwa imekunjuka katika mawimbi yake makubwa, na ikayarudisha mwinuko wake, na (ardhi) ilivunja nguvu ya maji baada ya kupanda kwake, na kuinua pua yake na kukithiri kuvuka kwake mpaka, na ikayazuia maji hali yakiwa yamesongamana, yakatulia baada ya msukumo wake, ikajiambatanisha na ardhi baada ya kuvuma kwake.

Na yalipotulia kuchafuka kwake pembeni mwake, na kuibeba milima mirefu mikubwa pembezoni mwake, ikatumbua chemchemi za milima, akayatawanya kwenye ardhi tambarare na mifereji, na alisawazisha harakati zake kwa majabali marefu miongoni mwa mawe magumu ikatulia kuyumba kwa kutumbukia majabali kwenye vipande vya sehemu zake, na kujipenyeza kwa maji na kuenea katika makorongo na tundu za pua, na kupanda kwake juu ya milima alipoitandaza ardhi yake na kupitisha amri yake, alimteua Adamu(a.s) akiwa mteule katika viumbe Wake, na alimfanya wa kwanza katika umbo lake, na alimfanya kuwa mkazi wa pepo Yake, na alijaalia wasaa wa mlo wake, na alimuonya kabla katika aliyomkataza, na kumjulisha kuwa kuyaelekea aliyoyakataza ni kujiingiza katika kumuasi, na ni hatari kwa daraja yake.

“Alijiingiza kwenye aliyomkataza - kulingana na ujuzi Wake (s.w.t) - alimteremsha baada ya toba, ili aikae ardhi Yake na kizazi chake, na kwake yeye iwe ni hoja kwa waja Wake. Hakuwaacha tupu wanadamu baada ya kumfisha yeye Adam. Ni katika yatiliayo nguvu juu yao hoja ya kuwa Yeye ni Mola Mlezi, na iwe kiungo kati yao na kumtambua Yeye, na kuchukua ahadi kwa ushahidi kupitia ndimi za walio wema miongoni mwa manabii wake, na wabeba amana ya risala Yake, karne na karne. Mpaka kutimia hoja yake kwa Nabii wetu Muhammad(s.a.w.w) , na suala kufikia udhuru wake kwa Muumba[192] .

“Amekadiria riziki, ameikithirisha na kuipunguza. Na ameigawa kwa dhiki na wasaa, akaiweka katika makadirio, ili kuwajaribu waitakao kwa wepesi wake na ugumu wake, kwa hilo anatahini shukrani na subira kwa tajiri na masikini.

Kisha ameambatanisha utajiri na shida ya ufakiri, na salama ameiambatanisha na misiba na maafa yake, na fursa ya furaha yake imeambatanishwa na taabu za huzuni yake. Na ameumba muda wa umri wa kuishi, ameurefusha na kuufupisha, na ameutanguliza na kuuchelewesha, na ameuunganishia umauti na kamba zake, na kuufanya wenye kuvuta kamba zake, na wenye kukata kamba yake imara.

“Ni mjuzi wa siri za dhamiri za wenye kudhamiria, na siri za wenye kuficha, na mawazo ya moyoni, na vifungo vya azma yenye uyakini, na yanayo ibwa na muangazo wa kope za macho, na yaliyomo ndani ya siri za nyoyo, na yaliyo kwenye kina, na yaliyosikiwa kwa kuibwa na tundu za masikio, na maeneo ya sisimizi ya kupitishia muda wa kiangazi, na makazi ya wadudu wakati wa masika.

Na kurejea kwa mimba ni miongoni mwa yahuzunishayo, na sauti hafifu ya nyayo, na mahali tunda linapokuwa, katika kifuniko cha ua, na maficho ya wanyama kwenye mapango ya milima, na mabonde yake, na maficho ya mbu kwenye mashina ya miti na magome yake, na maoteo ya majani kwenye matawi, na materemkio ya amshaji - tone la manii[193] kwenye mtiririko migongoni mwanzoni mwa kutungika kwake na kujiambatanisha kwake.

“Na kutiririka kwa matone ya mvua kutoka kwenye mkusanyiko wake, na yabebwayo na upepo pembezoni mwake, na yanayofutwa na mvua kwa mafuriko yake, na kuelea kwa wadudu wa ardhini na ni kitulizo cha mchanga, na ni makazi ya wadudu wenye mbawa kwenye vilele vya majabali, na kuimba kwa wenye kutamka katika giza la viota, na vilivyokusanywa na chaza na kutotolewa na mawimbi ya bahari[194] , na vilivyofunikwa na giza la usiku au kuchomozewa na jua la mchana na viliyotokomezwa na tabaka za giza na daraja za nuru, na athari za kila hatua na hisia za kila harakati, na rejea ya kila neno[195] na - mtikisiko wa kila mdomo, na makazi ya kila mtu, na uzito wa kila chembe, na hima ya kila nafsi, na yaliyomo ardhini miongoni mwa matunda ya mti, au jani lililodondoka, au makao ya manii[196] , au mahali panapokusanyika damu na mudh’ghah au mwanzo wa kuumba na kizazi[197] hakupata mashaka katika hilo, wala hakukabiliwa na upinzani katika kuhifadhi alichokibuni miongoni mwa viumbe Wake, wala hakupatwa katika kutekeleza na mambo na kuwaratibu viumbe uchovu wala ulegevu, bali elimu yake iliwaratibu, na aliwajua idadi, na kuwaeneza uadilifu wake, na kuwaingiza katika fadhila zake japokuwa ni wachache wanaostahiki.

“Ewe Allah! Wewe ni mwenye sifa nzuri, na ukamilifu usio na idadi. Ukitumainiwa ni mtumainiwa bora, na ukitarajiwa ni mtarajiwa bora. Ewe Allah! Umenikunjulia nguvu hasa kiasi cha kuwa simsifu nayo mwingine asiyekuwa Wewe, na simtukuzi mwingine yeyote asiye kuwa Wewe, si elekezi wasifu kwa chimbuko la kutofaulu na mahali pa shaka shaka[198] ,umeuepusha ulimi wangu mbali na sifa za wanadamu na kuwasifu waruzukiwa, wa lioumbwa.

Ewe Allah! kila mwenye kusifu ana haki ya ujira na fidia kwa anayemsifu, kwa hakika, nimekugeukia na macho yangu, nimekutarajia kuwa ni dalili ya kwenye akiba ya rehema na hazina ya msamaha[199] .

“Ewe Mungu Wangu! hapa ni mahali aliposimama ambaye amekupweke- sha kwa tauhiidi ambayo ni haki Yako, na wala hajamuona anayestahiki shukrani hizi na wasifu asiyekuwa Wewe. Mimi ni mhitaji Kwako, kwa kiwango ambacho hakiondoi umasikini wake isipokuwa fadhila Zako, wala cha kuepusha ufakiri wake isipokuwa ihisani yako na upaji wako, hivyo basi tupe sisi ridhaa Zako mahali hapa, na tutosheleze tusinyooshe mikono kwa asiyekuwa Wewe; (kwa hakika wewe umuweza wa kila kitu).”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

92 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Tabariy na Ibnul’Athiir wameisema katika matukio ya mwaka, 35 kukiwa na tofauti ndogo mno.

WATU WALIPOTAKA KUMPA BAI’A BAADA YA KUULIWA UTHMANI

Na maneno haya sahibu zetu wanayachukulia katika hali yake ya dhahiri; Kwa hiyo wanasema: Kuwa yeye(a.s) hakuusiwa na Mtume(s.a.w.w) awe Imam, japo kuwa awe ni mbora kwa jambo hili kuliko watu wengine, na ni mwenye haki zaidi kwa daraja aliyonayo. Kwa sababu lau angekuwa ameusiwa Uimamu na Mtume(s.a.w.w) , isingejuzu aseme: “Dauniy waltamisuu ghayriy” - Niacheni na mwombeni mtu mwingine; na aseme: “Wa la’Ali asmaukum waatwaukum liman walaytumuhu amrakum” au aseme: “wa anaa lakum waziran khayrun minniy lakum amiran.”

“Niacheni na mtafuteni mtu mwingine, kwa kuwa sisi twatazamia jambo lenye sura nyingi na rangi nyingi, nyoyo haziwezi kuvumilia wala akili haziwezi kulibeba.

Kwa kweli msitari wa upeo wa macho umefunikwa na mawingu, na njia iliyonyooka haijulikani tena[200] . Na jueni kuwa endapo mimi nitawaitikieni nitawabebesheni niyajuayo na sitosikiliza kauli ya msemaji yeyote, wala lawama ya mwenye kulaumu.

Na mkiniacha mimi nitakuwa kama mmoja yeyote miongoni mwenu. Na huenda nitakuwa mwenye kumsikiliza na kumtii mno mtakayemtawaza hili suala lenu, na mimi kuwa waziri kwenu ni bora kuliko kuwa Amiir.”

Maelezo

Na Imamia wanauchukua usemi huu kwa maana nyingine, wao wanasema: Ambao walitaka kumpa kiapo cha utii (bai’a) ni wale waliokula kiapo cha utii kwa makhalifa waliokuwa hapo kabla; na Uthman aliwanyima walio wengi haki yao ya fungu lililokuwa wakipewa.

Kwa kuwa Bani Umayyah walikomba mali katika siku za Uthman; alipouliwa wakamwambia Ali(a.s) : “Tutakubai (kula kiapo cha utii kwako) kwa sharti kwamba uende na sisi mwendo wa Abu Bakr na Umar; Kwa kuwa wao hawa wawili walikuwa hawahodhi mali kwa ajili yao binafsi wala kwa ajili ya ah’li zao, kwa ajili hiyo walimuomba Ali(a.s) wamfanyiye bai’a ili awagawiye mgao kutoka baytul’mali kama ule wa Abubakar na Umar; Hapo ndipo akawakatalia na akawataka wamchague mtu mwingine ambaye atakwenda mwendo wa hawa wawili.

93 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Abu Na’im amesema katika Hilyatul-Auliyai, jalada la kwanza, uk. 68, na Ibn Wa’dhwih katika Ta’arikh yake, jalada la tatu, 182.

NDANI YA KHUTBA HII AMIRUL-MU’MININ ANABAINISHA UBORA WAKE NA ELIMU YAKE. NA ANABAINISHA FITNA YA BANI UMAYYAH

“Baada ya kumhimidi Mungu na kumtukuza! Enyi watu! kwa hakika mimi nimetoboa jicho la fitna[201] , na hangethubutu mwingine yeyote asiyekuwa mimi baada ya kutanda giza lake[202] . Shari yake na maudhi yake yamekuwa makali.

“Hivyo basi niulizeni kabla hamjanikosa, namuapa ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake kwamba hamtoniuliza kitu tokea hivi sasa na siku saa itakapofika, wala kuhusu kikundi kitakachowaongoza watu mia moja na kuwapoteza mia nitakupeni habari nani mlinganiaji wake na kiongozi wake na mhamasishaji wake na mashukio ya ngamia wake, na kituo cha msafara wake, na ambao watauwawa miongoni mwa watu wake, na ambao watakufa kwa kifo cha kawaida.

“Na mtakaponikosa na mtapofikwa na shida ya vita na mambo magumu waulizaji wengi wangenyamaza na kuinamisha vichwa chini, na kuogopa wengi miongoni mwa watakaoshika nafasi za kuulizwa, na hivyo itakuwa viishapo vita vyenu, ikiwa na magumu kwenu, dunia itakuwa imebana kwenu, siku za balaa mtaziona ndefu, mpaka Mungu atakapowapa ushindi baadhi ya watu wema waliobaki miongoni mwenu.

“Kwa kweli fitna inapoingia utata hujitokeza[203] .

Ikigeuza mgongo hutambulika[204] ; haitambuliki inapokuja, na hutambulika inapotoweka[205] . Na yazunguka mzunguko wa upepo, unaisibu nchi na kuikosa nchi.

“Jihadharini, kwa hakika fitna ninayoihofia sana mimi kwa ajili yenu ni fitna ya Bani Umayyah. Kwa kuwa hiyo ni fitna pofu yenye giza: Jambo lake limeenea[206] Na balaa lake limekuwa kwa sura makh’susi. Na wakapatwa na balaa humo wenye kuitambua haki[207] . Balaa litamuepuka asiyejua.

Namuapa Mungu kwamba mtawakuta Bani Umayyah ni watu waovu kwenu baada yangu kama ngamia jike mzee mwenye tabia mbaya, yuang’ata kwa mdomo wake na apiga kwa mkono wake na kupiga teke kwa miguu yake ya nyuma na yu azuia kukamuliwa maziwa yake.

“Watabakia juu yenu mpaka hawatomuacha miongoni mwenu isipokuwa yule wa manufaa kwao, au asiye na madhara kwao. Balaa lao litaendelea juu yenu mpaka kiasi cha kuwa kuomba nusura kwa mmoja wenu dhidi yao ni kama kuomba nusura kwa mtumwa dhidi ya bwana wake[208] - na kwa mfuasi dhidi ya amfuataye, fitna yao mbaya na ya kuogofya itakujieni na sehemu ya jahiliya, hakuna humo alama za muongozo, wala dalili ionekanayo. Sisi ni Ahlul-Bayt (wana wa nyumba ya Mtume) twaepukana na hayo, wala si wanusuru wa hayo.

Kisha Mungu atakuondoleeni kama iondolewavyo ngozi kutoka kwa wenye kuambatana nayo kwa madhila, na kuwasukuma kwa mabavu, na kuwanywesha kikombe kichungu, hatowapa ila upanga, na wala hatowavika isipokuwa hofu.

Hapo Makuraishi watataka hata kwa gharama ya dunia yote na yaliyomo humo ili wanione mimi japo kwa mara moja tu lau kwa kadiri ya muda ule wa kuchinjwa ngamia ili niwakubalie lile ambalo hivi sasa nawaomba sehemu tu lakini hawako tayari kunipa.[209] ”.

Kisha alisema(a.s) : “Niulizeni kabla hamjanikosa.” Bwana mwenye Kitabu cha Al-Isti’ab naye ni Abu Umar Muhammad bin Abdil-Bari ameeleza akinakili kutoka kwa jamaa wasimuliaji na wanahadiithi, wamesema:

‘Hakupata kusema yeyote miongoni mwa masahaba (r.a): ‘niulizeni’ isipokuwa Ali bin Abi Talib. Na Sheikh Abu Ja’far Al-Iskafi ameeleza ndani ya Kitabu Naq’dhul-Uth’maniyah’’ akinakili kutoka kwa Ali bin Al- Jahdi kutoka kwa Ibin Shubrimah, Amesema: ‘Hawezi yeyote miongoni mwa watu kusema juu ya mimbari ‘niulizeni’ isipokuwa Ali Bin Abi Talib(a.s) .

94 - NA MIONGONI MWA KHUTBA YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Yake(a.s) - Ibn Abd-Rabi ameieleza katika al-Iqdul-Farid, jalada la 4, uk. 74, na al-Saduq katika Tawhid, uk.20.

KUHUSU SIFA ZA MANABII

“Ametukuka Mwenyezi Mungu[210] ambaye umbali wa mtazamo na fikra haumfikii, wala dhana ya utambuzi haimpati. Wa mwanzo ambaye hakuna upeo iwe anaishia huko wala hana mwisho iwe yuamalizikia hapo.

Na miongoni mwa hutuba hiyo: “Amewaweka weko bora na akawafanya watuwame kwenye tuwamo la kheri, imewanakili migongo mitukufu na kuwafikisha mifuko ya uzazi iliyo tohara; kila wapitapo - wafapo - waliotangulia, waliobaki kati yao hutekeleza dini ya Mungu, mpaka heshima ya Mungu (s.w.t) imeishia kwa Muhammad(s.a.w.w) ; akamtoa kutoka kwenye asili iliyo bora, na asili yenye heshima kuu, na kutoka mti ambao manabii Wake wametoka humo, na akachagua kutoka humo waaminifu Wake, Itrah yake ni miongoni mwa itrah; kizazi cha nyumba ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) zilizo bora. Na familia yake ni miongoni mwa familia zilizo bora. Na mti wake ni katika miti bora; umeinukia katika utukufu. Una matawi marefu; na matunda yasiyofikiwa[211] ;yeye ni imam wa wenye kufanya taq’wa, na ni mwanga wa wapendao mwongozo.

“Ni taa ambayo umemweta mwanga wake, na kimondo nuru yake imeangaza, na kipekecho cha moto ambacho mwanga wake umeangaza, sira yake ni insafu na sunna yake ni mwongozo, na maneno yake ni upambanuzi, na hukumu yake ni uadilifu; alimtuma wakati wa mwanya kati ya mitume[212] na wakati ambapo umma umepotoka na kupotoka kimatendo, na kutoelewa kati ya umma.

“Fanyeni mema - Mungu awarehemu - kwa mwanga wa wazi, njia ni ya wazi inaitia (watu) kwenye nyumba ya amani, (yaani pepo) hali mkiwa ndani ya nyumba ya kutafuta ridhaa (za Mungu), mkiwa na muda na fursa, na vitabu viko wazi (vitabu vya kuandika matendo ya waja), na kalamu ziko mashughulikoni (kalamu za malaika), na miili iko na siha, ndimi zikiwa huru, toba zinapokelewa, na aamali zinakubaliwa.”.

95 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Anaelezea Katika Khutba Hii Hali Ya Watu Ilivyokuwa Wakati Wa Bi’tha

“Allah (s.w.t) alimtuma (Muhammad) hali watu wakiwa wapotevu katika mkanganyiko, na wakikusanya fitna[213] , utashi wa nafsi umewaghilibu, na kibri kimewafanya wateleze,[214] na jaahiliya iliyoshona imewahafifisha,[215] wameduwazwa na myumbo wa mambo, na balaa la ujinga.

Hivyo basi Mtume(s.a.w.w) alikithirisha katika kutoa nasaha nyofu, naye alipita njia ya sawa, na aliwaita kwenye hikima na mawaidha mema.”.

96 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

“Shukrani ni za Mungu ni wa mwanzo hapakuwa na kitu kabla yake, na ni wa mwisho hapatokuwa na kitu baada yake, na ni wa dhahiri hapana kitu juu yake, na ni wa batwini hapana kitu chini yake.”.

Na miongoni mwake katika kumsifu Mtume(s.a.w.w) : “Mahali pa makazi yake ni mahali bora, na asili yake ni asili iliyo bora mno kuliko asili zote, ni asili ya heshima na susu iliyo salama[216] . Nyoyo za watu wema zimeelekezwa kwake, na hatamu za macho zimegeuzwa kumuelekea yeye. Mungu (s.w.t) amezizika chuki kupitia yeye[217] , na kwa yeye amezima mashambulizi ya kulipiza kisasi[218] , kwa yeye ameunganisha udugu, na kuwatenganisha walioungana[219] na kwa yeye amewatukuza waliokuwa dhalili[220] , maneno yake ni ubainifu na kunyamaza kwake ni hekima.”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

97 - MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

KUWAKEMEA SAHABA ZAKE

“Japo Mwenyezi Mungu amwachie muda dhalimu mshiko wake hautomkosa, naye yuamchunga kwenye mapito ya njia zake, na mahali pa mkwamo wa koo mapitio ya mate yake[221] , naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hawa watu (Mu’awiya na kundi lake) watapata ushindi dhidi yenu[222] ,

si kwa sababu wana haki zaidi kuliko mliyonayo bali ni kwa sababu ya haraka yao ya kutekeleza batili yao na ugoigoi wenu mbali na haki yangu (kuifuata). Umma huwa waogopa dhulma ya niliwaiteni kwa siri na kwa wazi hamkuitika, nilikunasihini hamkukubali.

“Mkiwa mpo kama hampo, mko watumwa kama mabwana![223] Ninakusomeeni nukta za hekima mnazikwepa, na ninakuonyeni kwa mawaidha yafikayo (masikioni) mnafarakana mbali nayo, nawahimizeni kwenda jihadi dhidi ya watu waovu, wala sijafikia mwisho wa kauli yangu nawaona mnatawanyika mfano wa mikono ya Sabaa - Ayaadiy sab’a.[224] “Munarejea kwenye makazi yenu mkiwa hamuwaidhiki. Nakunyoosheni asubuhi, mwarejea kwangu jioni mkiwa mmepindama kama upinde, mnyooshaji amehemewa na mnyoshwaji amekuwa mgumu.

“Enyi kaumu ambao miili yao ipo hadhiri hali akili zao zimeghibu, na ambao utashi wao uko tofauti. Watawala wao wamepatwa na balaa. Sahibu yenu yuamtii Mungu, na ninyi mnamuasi, na sahibu wa watu wa Sham yuamuasi Mungu na hali wao wanamtii! Ningependa, wallahi lau Muawiya hangenibadilishia ninyi ubadilishaji wa dinari na dirham, angewachukua kutoka kwangu kumi kati yenu na angenipa mimi mtu mmoja kutoka wao!

“Enyi Watu wa Kufa! nimepata uzoefu kwenu wa matatu na mawili mengine: Mko viziwi hali mkiwa na masikio, na mko mabubu hali mkiwa mwasema, vipofu mlio na macho. Sio wasaidizi wa kweli wakati wa mapambano wala sio ndugu wa kuaminika kwenye balaa! Mikono yenu iingie mchanga!( – yaani mikono yenu isiwe na kheri! - hili ni neno la kumlaani mtu). Enyi mlio mfano wa ngamia ambao mchungaji wake ameghibu! Kila wakusanywapo upande mmoja wanatawanyika upande mwingine.

Wallahi nawaona kwa maoni yangu, endapo vita vitakuwa vikali na hali ya mambo ikiwa inayumba mtamkimbia mwana wa Abi Talib ukimbiaji wa mwanamke akiwa uchi mbele, kwa hakika mimi nipo katika mwongozo wa wazi kutoka kwa Mola wangu Mlezi, na (niko) katika njia ya Nabii wangu, na niko katika njia ya wazi nikiokota cha kuokota[225] .

“Waangalieni Ahlul-bayt wa Nabii wenu, na jiambatisheni na mwendo wao, na fuateni nyayo zao, hawatokutoweni nje ya mwongozo, na hawato kutumbukizeni kwenye maangamizi, wakikaa kaeni wakiinuka inukeni, msiwatanguliye mtapotea, wala msibaki nyuma yao mtaangamia.

Kwa kweli nimewaona sahaba za Muhammad(s.a.w.w) simuoni yeyote kati yenu anashabihiana nao, kwa kweli walikuwa wanaianza asubuhi wakiwa na nywele timtim na wakiwa wamejaa vumbi kichwani (na mwilini)[226] .

Wamepitisha usiku katika hali sijda na qiamu, wakibadili kati ya paji zao za uso na mashavu yao ( yaani mara wakisujudu kwa paji la uso na mara nyingine kwa mashavu yao). Na walikuwa wanasimama mfano wa aliyesimama juu ya kaa la moto kwa ajili ya kukumbuka marejeo yao, kana kwamba kati ya macho yao kuna goti la mguu wa mbuzi kutokana na sijda zao ndefu. Atajwapo Mungu macho yao hutiririsha machozi mpaka yalowesha kosi (kola zao), walikuwa wana yumba kama uyumbavyo mti siku ya upepo mkali, wakiogopa adhabu, na wakiwa na matarajio ya thawabu.”.

98 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Ibn Qutaybah ameeleza katika al-Imama was-Siyasah, jalada la kwanza, uk. 151.

KUHUSU DHULMA YA BANI UMAYYAH

“Wallahi wataendelea hivi (Ufafanuzi: Usemi hapa ukadiriwe hivi: Wangali bado ni madhalimu) mpaka wafikie kiasi cha kuwa hawatoacha alichokiharamisha Mungu ila watakihalalisha, wala ahadi ila wataitangua na hata haitobakia nyumba ya matofali wala ya manyoya ila dhulma yao itaingia, na ubaya wa matendo yao utawafanya duni.

Mpaka watakuja kusi-mama waliaji wawili walie: Mliaji analia kwa ajili ya dini yake, na mliaji alia kwa ajili ya dunia yake, mpaka iwe nusura ya mmoja wenu kwa mwingine mfano wa nusura ya mtumwa kwa bwana wake, akiwa yupo anamtii, na anapoghibu humsengenya.

Mpaka itakuwa mwenye shida kubwa mno kati yenu ni yule mwenye kuwa na dhana njema mno kwa Mungu miongoni mwenu.

Mungu akikutunukieni amani na salama ikubali- ni, na akikupeni mtihani vuteni subira, “..... Na kwa hakika mwisho mwema ni wa wachamungu.”(7:128).

99 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - an-Nuuriy ameieleza katika al-Mustadrak Jz. 1, uk. 411, na as-Saduq katika Man la Yahdhurul-Faqih, Jz. 1, uk. 270.

KATIKA KUJIEPUSHA NA DUNIA

“Tunamhimidi kwa yaliyotokea, na tunamuomba msaada kwa ajili ya mambo yetu yatakayokuwa, tunamuomba usalama katika dini, kama tunavyomuomba usalama kuihusu miili[227] .

“Nakuusieni kujiweka mbali na dunia hii ambayo ni yenye kukuacheni japo muwe hampendi kuiacha, na ni yenye kuichakaza miili yenu japo mupende kuifanya upya. Kwa kuwa mfano wake na ninyi ni kama wasafiri[228] , wamesafiri waliokwenda kiasi fulani cha masafa kisha wakawa kana kwamba wao haraka wameikata safari, wameikusudia alama, na mara moja kana kwamba wameifikia. Ukaribu ulioje wa masafa kwenye lengo endapo mtu atalielekea na kulifikia! Ukaribu wa masafa ulioje wa kwenye lengo ikiwa mtu yualielekea na kulifikia!

Hatua fupi ilioje ya mtu aliye na siku moja tu ambayo hawezi kuizidisha, hali ikiwa amtakaye mwenye haraka yaani mauti amfuata, anasumbua duniani mpaka aitoke apende asipende! Hivyo basi msihusudiane kugombania utukufu wa dunia na fahari yake, na wala msifurahiye mapambo na neema zake, na wala msiyahuzunikie madhara yake na shida ya madhara yake.

“Kwa hakika utukufu wake na fahari yake vinaelekea kukatika, mapambo yake na neema zake vitatoweka, madhara yake na shida zake zinakwisha, na kila muda humo waelekea mwisho, na kila aliye hai humo aelekea mwisho.

Je ninyi kutokana na athari za waliokuwa mwanzo hamuonyeki! Na katika babu zenu wa mwanzo kuna ufunguzi wa macho na zingatio, endapo mtakuwa mnatia akilini! Je hamuoni kuwa waliopita miongoni mwenu hawarejei, na walioendelea kuishi hawatobaki milele! Si mwaona wana wadunia wanaingiwa na jioni na wanaingiwa na asubuhi wakiwa katika hali nyingi mtawanyiko: Kuna aliyekwisha kuwa mauti analiliwa, na mwingine ahaniwa, na aliyetupika chini amekumbwa na balaa, na mwenye kumtembelea mgonjwa, na mwingine anatapia nafsi yake, na ambaye aitafuta dunia na mauti yamtafuta yeye, na kuna aliyeghafilika wala haghafilikiwi, na katika athari za waliopita hupita waliobakia! Lo! Mkumbukeni mbomoa raha, na anayeyatia uchungu matamanio, na mkata matumaini, pindi yavamiwapo matendo mabaya, na muombeni msaada Allah (swt) ili kutekeleza wajibu wa haki Yake, na neema Zake na hisani Zake zisizo na idadi.”.

100 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUMHUSU MTUME WA MUNGU NA AHLUL-BAYT WAKE

“Mstahiki wa sifa ni Allah Mwenye kueneza fadhila Zake kwa viumbe, na Mwenye kuwanyooshea mkono wake wa ukarimu. Tunamtukuza katika mambo Yake yote, na tunamuomba msaada ili kuzichunga haki Zake.

Na tunashuhudia kuwa hakuna mungu mwingine, isipokuwa Yeye na kuwa Muhammad ni mja Wake na mjumbe Wake, amemtuma kudhihirisha amri Yake na kuitangaza, na awe mwenye kutamka utajo Wake.

Na alitekeleza kwa uaminifu, na alifariki akiwa ndani ya uongofu; na alituachia bendera ya haki[229] , mwenye kuitangulia atakuwa ametoka[230] , na mwenye kubaki nyuma yake atakuwa amenyauka, na mwenye kujiambatisha nayo atakuwa amejiunga na haki.

Dalili yake ni umakini wa usemaji[231] , asimama taratibu, ana haraka akienda. Hivyo basi endapo ninyi mtamlainishia shingo zenu (yaani mkimtii), na mkamuishiria kwa vidole vyenu[232] , 4mauti itamjia na itaenda naye, na mtabaki baada yake ma’sha’Allaahu, mpaka Mungu amtoe kwa ajili yenu mmoja ambaye atakukusanyeni, na kuuweka pamoja mparaganyiko wenu, msimtumainie asiyekuja wala msikate tamaa na aliyegeuza mgongo[233] kwa kuwa aliyegeuza mgongo huenda ukamteleza mguu wake mmoja, na ukathibiti mwingine, na ikarudi miwili mpaka ikathibiti yote.

“Juweni! Kuwa mfano wa Aali Muhammad(s.a.w.w) , ni mfano wa nyota za mbinguni, ikizama nyota yachomoza nyota. Kama kwamba neema za Mungu zimekukamilikieni, na amekuonesheni kile mlichokuwa mwakitarajia.[234]

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

70 - NA AMESEMA(A.S)

Na Amesema(a.s) - Ibn Sa’ad ameielezea ndani ya at-Tabaqat, Jz. 3, uk. 36, na Al’Qaaliy ndani ya Dhaylul’amali uk. 190, na Al’Isfahani ndani ya Maqatilu Talibiin uk.16, na Ibn Abdi Rabih ndani ya Al-Iqdul al-Farid Jz. 2, uk. 298, na wengine.

KATIKA MKESHA WA SIKU ALIYOSHAMBULIWA

“Nilipatwa na usingizi nikiwa nimekaa nikamuona Mtume wa Mungu(s.a.w.w) , nilimuuliza: ‘Ewe Mtume wa Mungu! Kupindama kulikoje na uadui ambao nimekabiliana navyo kutoka kwa umma wako!’ Akasema: ‘Wapatilize,’ Nikasema: ‘Mungu anibadilishie walio bora kuliko wao, na anibadilishe na aliye mbaya zaidi kwao kuliko mimi.[40]

Amesema Ar-Radhiy (r.a): Anakusudia kwa neno kupindama, na kwa neno mzozo, na huu ni ufasaha wa hali ya juu mno wa maneno.

71 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Al-Mufid ameielezea katika al-Irshad uk. 61, na ibn Da’abiy katika al-Ikhtiswas uk. 155, na Tabrasiy katika al-Ihtijaj Juz.1, uk. 254.

KATIKA KUWALAUMU WA-IRAQI:

“Ama baada! Enyi watu wa Iraqi, mko kama mwanamke mwenye mimba, ameshika mimba na alipotimiza upevu wa mimba akaporomosha mimba, na mumewe akafariki, kwa hiyo muda wake wa ujane ukawa mrefu, na akarithiwa na wa mbali kabisa[41] . Wallahi sijakujieni kwa hiyari; isipokuwa nilikujieni katika hali ya kusukumwa[42] .

Nimepata habari kuwa ninyi mwasema: ‘Ali anasema uwongo, Mungu (swt) akuangamizeni! Nani nimsemee uwongo? Nimuongopee Mungu? Mimi ni wa kwanza kumwamini! Au nimsemee uwongo nabii wake? Mimi ni wa kwanza kumsadiki yeye!

Hapana wallahi, lakini hiyo ni ibara ambayo mmeshindwa kuitambua maana yake[43] , hamkuwa wenye kustahiki nayo, Waylumah, ninakupimieni vipimo vya kiilimu na hikma, upimaji usio na thamani [44] ,4 lau angekuwa na chombo apime humo.” “ Na bila shaka mtajuwa habari zake baada ya muda ,” (38:88).

72 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameieleza ibn Qutayba katika Gharibul-Hadith, na Thaqafi katika al-Gharatu, na al- Qadhy al-Qadhwaiy katika as-Sahifatul-Alawiyah, uk. 3.

ALIWAELIMISHA WATU NAMNA YA KUMSALIA MTUME WA MUNGU

“Ewe Mola Wangu! mkunjuaji wa yakunjuliwayo na mhifadhi wa yahifadhiwayo, na muumba wa nyoyo katika maumbile yake ya asili, zenye taabu na mashaka na zenye maisha ya furaha, zijaalie sala zako za ziada na baraka zako zenye kuendelea juu ya Muhammad, mja wako na mjumbe wako, mhitimishaji wa yaliotangulia katika unabii[45] , na mfunguzi wa yaliojifunga[46] na mtangazaji wa haki kwa haki na mzuiaji wa mfuriko wa batili[47] na mvunjaji wa ukali wa upotovu[48] kama alivyobebeshwa akasimama kwa nguvu, akitekeleza amri Yako, mwenye kuharakia katika ridhaa Zako, si goigoi kwenda vitani, wala si dhaifu katika azimio, mwenye kufahamu wahyi Wako, mhifadhi wa wahyi Wako, mhifadhi wa amri Zako na mwenye kuzitekeleza, mpaka kupatikana haki, na akaiangaza njia kwa ababaikaye, na nyoyo zikaongozwa baada ya kuingia fitna na dhambi. Na alitekeleza dalili wazi za njia, na hukumu zenye nuru.

Hivyo yeye ni muaminifu Kwako mwenye kuaminiwa, na mhifadhi wa ilimu Yako iliyo mahsusi, na shahidi Wako Siku ya Hukumu[49] .

Yeye ni mtumishi Wako wa kweli, na Mtume wako kwa viumbe. Oh, Ewe Mola Wangu! Mpanulie nafasi katika kivuli chako[50] , na umlipe kheri ya ziada katika fadhila Zako. Umnyanyulie daraja jengo lake[51] , na ikirimu daraja yake Kwako[52] , mtimizie nuru yake, mlipe akutakalo ushahidi unaokubalika, na usemi unaoridhiwa, muadilifu wa mantiki, na hutba pambanuzi.

Oh Ewe Mola wangu! Kusanya kati yetu na yeye tuwe katika maisha baridi na neema tulivu ya kudumu[53] , na kutosheka na yatakiwayo, na ladha ya utashi, maisha ya raha, utulivu wa akili, na tunu za heshima.[54] ”.

73 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE (A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Ibn Sa’ad ameieleza sehemu ya maneno haya katika Tabaqat, Jz. 1, na al-Baladhuliy kati- ka al-Ansab, uk. 361.

ALIMWAMBIA MARWAN BIN AL-HAKAM HUKO BASRA

“Walisema: Marwan bin Al-Hakamu alitekwa siku ya Jamal na aliwasihi Hasan na Husain wamuombee kwa Amirul-Mu’minina(a.s) . Nao walisema naye kuhusu suala lake, naye (Amirul’Mu’minina) alimwacha huru. Walimwambia (wasemaji ni Hasan na Huseni): Akuba’i ewe Amirul- Mu’minina.Akasema(a.s) :

“Kwani hakunifanyia bai’a baada ya kuuliwa Uthman? Sina haja ya bai’a yake! Kwa kuwa huo ni mkono wa kiyahudi[55] , lau anifanyie bai’a kwa mkono wake angenisaliti kwa tako lake[56] . Ila tu yeye Marwan atakuwa na uamiri wa muda mfupi kama vile mbwa anavyoramba pua yake[57] . Na yeye ni baba wa maraisi wanne wa kaumu[58] .

Umma utapata siku nyekundu kutoka kwake na kwa wanawe.[59] ”.

74 - NA KATIKA USEMI WAKE(A.S)

WALIPOAZIMIA KUMFANYIA BAI’A UTHMAN

“Kwa kweli mnajua kuwa mimi ni mwenye haki nao (ukhalifa) zaidi kuliko mwingine yeyote asiye kuwa mimi; na wallahi nitamwachia (Uthman) maadamu kumwachia mambo ya waislamu yatakuwa katika amani na dhulma haitokuwa isipokuwa kwangu tu[60] , nikitaraji ujira wa hilo na fadhila zake, na kujiweka mbali na mnachoshindania na kujiweka kando na kuyafikia mapambo yake ambayo mnagombania.”

75 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE (A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Ibn al-Athir ameieleza katika an-Nihayah katika mada ya Qirzu.

ALIPOPATA HABARI KUWA BANI UMAYYAH WANAMTUHUMU KUSHIRIKI DAMU YA UTHMAN

“Je Bani Umayyah kunijua kwao hakujawazuia kuniaibisha? Je kutangulia kwangu (kuukubali uislamu) hakujawaweka mbali wajinga na kunituhumu? Kwa kweli aliyowaonya Mungu amewaonya kwa ufasaha zaidi kuliko ulimi wangu, mimi ni mtoa hoja dhidi ya watokao nje ya dini, na ni hasimu wa wavunjao ahadi na wenye shaka[61] , na kwenye Kitabu cha Mungu.

Kwa Kitabu cha Mungu hupimwa yasiyo wazi[62] . Kulingana na yaliyo mioyoni waja watalipwa.” Anaikusudia kauli yake (s.w.t) “Hadhani khasmani ikh’taswamu fii Rabbihim” (22:19).

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

76 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameyaeleza hayo al-Haraniy katika at-Tuhaf, uk. 150, na ibn Shakir katika Uyunul- Hikami wal mawa’idh, na Zamakhshari katika Rabiul-Abrar Jz. 1, uk. 231, na al-Hisriy katika Zuhurul-Adabi, Jz. 1, uk. 42.

KUHUSU ZUHUDI

“Mungu amrehemu mtu aliyeisikia hukumu akaihifadhi na kuielewa, na aitwapo kwenye mwongozo akausogelea[63] , na amfuata kiongozi (kwa kushika mkanda wake wa kiunoni) na akaokoka, akajihadhari na Mola wake Mlezi, na kuhofia dhambi zake, akatanguliza ikhlas na kutenda mema, akachuma na kupata hazina, na akajiepusha na yaliyohadharishwa. Na akalenga lengo, na kufanikiwa kupata kitu mbadala, akaukabili utashi wake, na kuyakadhibisha matumaini yake (bandia), na akaifanya subira kuwa ndio njia yake ya uwokovu, na taqwa kuwa ndio masurufu ya kifo chake. Akapita njia ya haki, kwa mwenendo wa kiadilifu, na akijiambatanisha na njia ya hali ya juu ya ukweli, na kuutumia vyema wakati wake, na kuuharakia mwisho (wake), na akaenda na akiba ya matendo mema.”.

77- NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Al’Isfahaniy ameielzea usemi huu ndani ya ‘Al-Aghaaniy’ Juz. 11, uk. 29, na Al-Azhariy ndani ya ‘Tah’dhiibi-lughah’ Juz. 15, uk. 27.

KUWAHUSU BANI UMAYYAH

“Kwa kweli Bani Umayyah wananiruhusu kiasi kidogo cha mirathi ya Muhammad(s.a.w.w) . Wallahi endapo nitabaki nitawapuliza mpulizo wa muuza nyama apulizapo mnofu wa nyama ulioenea mchanga!”

Maelezo

Ar-Radhiy (r.a) amesema: Na yaelezwa kwa tamko nayo iko katika hali ya kugeuza, kwa sababu ukweli ni kama ilivyokuwa katika riwaya ya kwanza, sio kwa kuwa hilo halina maana, kwa hiyo hii yakusudiwa riwaya iliyogeuzwa.

Na kauli yake(a.s) (Layufawiqunaniy) yaani wananipa kutoka mali ya (Muhammad) kitu kidogo sawa na mkamo mmoja wa maziwa ya ngamia. Na wid-hamu at-taribatu: ni udongo, ni wingi wa neno wadhamatu, nacho ni kipande cha tumbo au cha ini kilichoanguka na kutapakaa vumbi hupulizwa.

78 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Al-Jaahidhwu ameueleza mwisho wa du’a hii katika al-Miatu al-Mukhtaratu.

ALIKUWA AKIOMBA KWA DUA HII:

“Ewe Mungu wangu! Nisamehe ambayo wewe wayajua zaidi kuliko mimi, endapo nitarudia nirejelee kwa msamaha. Ewe Mungu Wangu! Nisamehe kwa niliyoyaahidi nafsini mwangu, na wala hukuuona utekelezaji wake kwangu[64] .

Ewe Mungu Wangu! nisamehe niliyojikurubisha nayo kwako kwa ulimi wangu, halafu moyo wangu ukawa kinyume nayo[65] . Ewe Mungu Wangu! nisamehe na mikonyezo, na maneno ya ovyo, na usahaulifu wa moyo na mtelezo wa ulimi.”

79 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Ibrahim ibn Hasan ibn Dizili ameieleza katika kitabu Swiffiin, na Saduq katika kitabu Uyunul-Akhbar ar-Ridha, Jz. uk. 138.

Aliwaambia baadhi ya sahaba zake alipokuwa ameazimia kufanya msafara kukabiliana na Khawarij. Na (mmoja wa sahaba zake) alimwambia: “Ewe Amirul-Mu’minina ukifanya safari katika wakati huu nahofia hautofanikiwa mradi wako kwa mujibu wa ilimu ya nyota.” Akasema(a.s) :

“Wadhani kuwa wewe unaelekeza saa ambazo mwenye kufanya safari katika saa hizo ataepushwa na jambo baya, na unahofisha saa ambazo mwenye kusafiri humo atakumbwa na jambo la madhara? Hivyo basi mwenye kukusadiki kwa hilo atakuwa ameikadhibisha Qur’ani, na atakuwa amejitosheleza hatohitaji kuomba msaada kwa Mungu ili kuyapata yapendwayo na kujikinga na makruhu; kwa kauli yako hii wamtaka atakeye itendea kazi amri yako akumiminie shukrani wewe sio Mola wake, kwa kuwa wewe - kwa dhana zako - ndiye uliye muongoza saa ambazo kwazo amepata manufaa, na ataepukana na madhana.”

Kisha Aliwaelekea Watu(a.s) Akasema:

“Enyi watu! Jihadharini na kujifunza elimu ya falaki isipokuwa kiasi cha kupata mwongozo, bara au baharini[66] , kwa kuwa hiyo (falaki) inaitia kwenye ukuhani, na mwanafalaki ni sawa na kuhani, na kuhani ni kama mchawi[67] , na mchawi ni sawa na kafiri na kafiri (marejeo yake) ni motoni. Safirini kwa jina la Mungu.”

80 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Baada Ya Vita Vya Jamal (Ngamia) Katika Kuwalaumu Wanawake

“Enyi watu, kwa hakika wanawake ni wapungufu wa imani[68] , wapungufu wa hisa, wapungufu wa akili. Ama kuhusu upungufu wao wa imani ni kule kubaki kwao bila sala na saumu siku zao za hedhi. Ama upungufu wao wa akili ni kule kuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanaume mmoja. Ama upungufu wao wa hisa ni kule kuwa mirathi zao ziko nusu ya mirathi za wanaume. “Hivyo basi zicheleeni shari za wanawake na jihadharini na walio wa kheri miongoni mwao, wala msiwape tamaa katika jema ili wasiwe na tama katika jambo la munkari.[69]

Sibti ibn Jauzi ameieleza katika at-Tadhkira uk. 85, na ameieleza baadhi yake Abu Talib al-Makki katika Fautul- Qulub, Jz. 1, uk. 282.

81- NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Saduq ameieleza katika Ma’anil-Akhbar, uk. 251, na katika al-Khisal, Jz. 1, uk. 11, na al- Barkiy katika al-Mahasin, uk. 234.

KUHUSU ZUHUDI (KUTOTILIA MANANI RAHA YA DUNIA)

“Enyi watu! Zuhudi ni kupunguza matumaini[70] ,na kushukuru neema[71] , na kuogopa kujiingiza kwenye haramu[72] , na endapo hilo likiwa mbali kwenu basi haramu isiishinde subira zenu[73] ,wala msisahau shukrani kwenye neema, Mungu amemaliza udhuru kwenu [74] ,5 kwa hoja zilizo wazi, na vitabu vilivyo na udhuru wa wazi.”.

82 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) Sharifu ar-Radhiy amesema: ‘Nasema: Mzingatiaji akizingatia kauli yake(a.s) : “Atakayeizingatia itampa mwanga” chini yake atakuta maana ya ajabu, na lengo la mbali, lisilofikiwa upeo wake wala hakifikiwi kina chake hasa hasa ikilinganishwa na kauli yake: “Atakayeikodolea macho itampofusha” kwani yeye atakuta tofauti wazi yenye mwanga na ajabu kubwa kati ya “Atakayeizingatia” na “Atakayeikodolea macho”. Salawatul-llahi wasalamuhu alayhi.’

KUHUSU DUNIA NA WATU WAKE

“Nieleze nini kuhusu dunia hii ambayo mwanzo wake ni taabu, na mwisho wake ni kuharibika. Ya halali yake yatakuwa na hesabu, na ya haramu yake yatakuwa na adhabu. Awaye tajiri humo (duniani) hukabiliwa na fitna. Na maskini humo yu ahuzunika. Mwenye kuipenda sana huikosa[75] ,na mwenye kuitupilia mbali humwelekea[76] .

Atakayeizingatia itampa mwanga, na atakayeikodolea macho itampofusha.[77] ”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

83 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ibn Shu’uba ameieleza katika ‘Tuhaful’uquli’ uk. 146; Na Al-Qaadhi Al-Qudhaiy katika mlango wa tatu wa kitabu ‘Dasturu maalimil’Hukm’ uk. 59; Na Abu Na’im katika ‘Al’hilya’ Juz. 1, uk. 77; Na Al-Amidiy katika ‘Ghurarul’hukam.’

NAYO NI MIONGONI MWA KHUTBA ZA AJABU, NA HUITWA ‘AL-GHARRAAU’:

“Ninamhimidi Allah (s.w.t) ambaye amekuwa na daraja ya juu kwa nguvu Zake[78] , na amekurubia kwa fadhila Zake[79] , Mtoaji wa kila faida na fadhila, na muondoaji wa kila kubwa na dhiki. Ninamhimidi kwa ajili ya huruma na ukarimu Wake, na uwingi wa neema Zake. Na ninamwamini kwa kuwa ni wa mwanzo Aliye dhahiri[80] , na ninamuomba mwongozo kwa kuwa yu karibu mwongozaji.

Na ninamuomba msaada kwa kuwa ni mshindi mwenye nguvu. Na ninamtegemea kwa kuwa ni mtoshelezaji, mnusuru. Na ninashuhudia kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni mja Wake na Mtume Wake, amemtuma ili kutekeleza amri yake, na kumaliza udhuru wake[81] , na kutoa maonyo yake[82] .

“Nakuusieni! Enyi waja wa Mungu kumcha Mungu ambaye amekufanyiyeni mifano[83] , na amekuwekeeni wakati maalumu wa maisha, na amekuvikeni riyasha (yaani vazi)[84] ,na ameyafaharisha maisha yenu[85] na kuyaboresha, na amekuzungukeni kwa hesabu[86] ,na amekuandalieni malipo, na amekutunukieni neema nyingi na takrima kwa wasaa. Amekuonyeni kwa hoja za wazi bainifu.

Amekufanyeni kwa idadi, na amekuainishieni muda, ndani ya nyumba ya balaa na mtihani, na kwenye nyumba ya mazingatio ninyi ni wenye kufanyiwa mtihani humo, nanyi mtahesabiwa matendo yenu.”

KUTAHADHARISHWA NA DUNIA

“Kwa kweli dunia kinywaji chake kimetibuka, chanzo chake kina udongo na tope. Mandhari yake yanavutia, na yanaangamiza.

Ni yenye kudanganya na kutoweka, na ni mwanga utowekao haraka na kivuli kipitacho, na ni nguzo iliyoelemea upande, mpaka anayeichukia aanzapo kuifurahia, na mwenye kuichukia aanzapo kuwa na matumaini, punde yainua miguu yake na kuirudisha chini na kumnasa mwanadamu kwa kamba yake, na kumuuwa pale pale kwa mishale yake, na kumfunga mtu[87] , shingoni kamba ya kifo ikimuongoza kwenye malalo yaliobana (yaani kaburi), na marejeo ya upweke, na kuainisha mahali[88] - na thawabu za Aamali[89] .

Na hivyo hivyo waliokuja nyuma baada ya waliotangulia, kifo hakikomi kuziondoa nafsi, wala waliobakia hawakomi kutenda dhambi. Watafuatia mfano wao- (mfano wa waliotangulia katika matendo).

Wanapita kwa makundi mpaka upeo wa mwisho, na mwisho wa mambo, mpaka mambo yatakapokatika, dahari zitakapopita, na kukaribia kufufuka, Mungu atawatoa nje kutoka makaburini, na viota vya ndege, na maficho ya wanyama wakali, na katikati ya maangamizi.

Wataharakia kwenye amri Yake, wakienda haraka kuelekea maeneo yalioandaliwa kwa marejeo yao ya mwisho makundi kwa makundi, wakiwa kimya, hali wamesimama safu kwa safu, wakiwa katika kuonwa na Mungu wakiwa mahali mwitaji aweza kuwaita wamsikie.

Wakiwa na vazi la unyonge, wakifunikwa na unyenyekevu na udhalili, hila imekwisha, matumaini yamekatika, nyoyo zikiwa hazina furaha[90] , sauti zikiwa zimedhoofu, hafifu, na jasho limekuwa kama hatamu[91] , hofu imekuwa kubwa, na masikio yatakabiliwa na radi, kwa kelele ya sauti ya mfanya daawa, akiwaita kwenda kwenye upitishwaji wa maamuzi, na kupata malipo mbadala adhabu na kupata thawabu.[92] ”.

KUWATANABAHISHA VIUMBE

“Waja wenye kuumbwa kwa uwezo, na wamemilikiwa kwa kahari[93] , na mamlaka, na watakufa kwa kuhudhuriwa na Malaika wachukuaji roho[94] , na watawekwa kaburini, na hatimaye kuwa mifupa iliyochakaa, na watafufuliwa (kila mtu) pweke[95] , na watalipwa malipo, na watafanyiwa hisabu kila mtu na yake[96] walipewa muda wa kujiepusha[97] , na waliongozwa njia ya wazi[98] , na waliruhusiwa kuishi na muda wa kutafuta maridhawa, na wameondolewa giza la shaka, na wameachwa kwenye medani ya mashindano ya farasi[99] , na kuachwa wafikiri na kutafuta yahitajiwayo kwa mazingatio, kuwa na uvumilivu wa mtafutaji, anayejaribu kukipata kilichompotea, katika muda wa harakati za kazi kabla ya ajali.”

UBORA WA KUKUMBUSHA

“Mifano muwafaka ilioje na mawaidha yaponyayo! endapo yangeafikiana na nyoyo safi, na masikio sikivu, na rai zenye azma na akili thabiti!

“Mcheni Mungu uchaji wa mwenye kusikiliza na akanyenyekea, na atendapo ovu yu-atambua, na akiogopa hutenda yaliyo sawa, akiwa na hadhari huharakia kwenye mema, akiwa na yakini hufanya mema, akipewa mazingatio mara kadhaa huzingatia, akitahadharishwa hujihadhari, akikaripiwa hukaripika, aitwapo na wito wa mlinganiaji (kwa Mungu) hurejea kwake.

Arejeapo hutubu, na akifuata hufanya vizuri, akionyeshwa njia ya sawa huiona na yu aharakia akitafuta, na kuokoka mbio! na yuafaidika na mali, na kuwa na tabia njema, na kuyajenga marejeo, na akabeba masurufu mgongoni kwa ajili ya siku ya kuondoka kwake, na akaelekea njia aikusudiayo na hali ya haja yake, na mahali pa mahitaji yake, na kutanguliza mbele yake kwa ajili ya nyumba ya kubaki kwake.

Hivyo basi mcheni Mungu, enyi waja wa Mungu kwa upande wa lengo alilokuumbieni[100] , na mjihadhari upeo wa kujihadhari na ambayo amekuhadharisheni nafsi yake[101] , na kuweni wastahiki wa ambayo amekuandalieni[102] , kwa kutekeleza ya wajibu[103] , na kujihadhari na marejeo yake yanayotisha.”

Na Sehemu Hii Ya Khutba Kuwakumbusha Watu Neema Za Mungu

“Amekujaalieni masikio ili muweze kufahamu na kuyahifadhi aliyoyakusudia, na macho ili muweze kutandua tandabui ya giza giza, na viungo vya mwili vyenye kuwemo ndanimwe viungo vingine, na vyenye kulingana na umbo la mahali khusika katika muundo wa sura zake, na muda wa umri wao, na miili yenye kutekeleza manufaa yake, na nyoyo ambazo zimeshughulika kutafuta chakula chake, ndani ya neema zake zilizo funi- ka, na yawajibishayo upaji wake, na vizuizi vya afya yake[104] .

“Amekukadirieni umri aliousitiri mbali na (uelewa wenu) amekubakishieni mabaki ya athari za waliopita kabla yenu, ili iwe mwongozo kwenu, watu hao walistarehe na hisa zao kubwa, kwa nafasi bila ya kizuizi[105] .

Kifo kiliwachukua bila kufikia matumaini yao, (kifo) kiliwakata na kuwa’ngoa mbali nayo - matumaini - hawakujiandaa wakati miili iko salama, wala hawakuzingatia mwanzoni mwa umri wa ujana. Je wenye ngozi laini ya ujana wanangoja mpaka kupinda migongo kwa uzee!

Na ambao wana siha njema wanangoja kufikiwa na hali mbaya ya siha! Na walio na muda wa kubaki wanangoja mpaka uishe, pamoja na ukaribu wa kutoweka, na mbabaiko wa kutoweka, na kufikiwa na huzuni moyoni, na kusongwa na mate, na hofu ya mgonjwa na uchungu wa huzuni, na mbinyo wa mate.

Muda utafika wa kuomba nusra ya wajukuu na ndugu wa karibu, wapenzi na wenzi. Je! Ndugu wa karibu wamezuia, au vilio vimeleta nafuu!

Ameachwa mahali pa wafu amefungika, na kwenye malalo yaliyombana akiwa mpweke, wadudu wameirarua ngozi yake, na matukio yameuchakaza upya wake, na dhoruba itakuwa imefuta athari zake, na tukio litakuwa limefuta dalili zake, na miili itakuwa imehiliki baada ya kujaa kwake, na mifupa itakuwa imeoza baada ya nguvu zake, na nyoyo zitakuwa zimefungika kwa uzito wa mizigo (dhambi) yao, zitakuwa na yakini na habari zake zilizojificha, hazitotakiwa baada ya hapo kuzidisha Aamali zake njema[106] wala hazitoombwa kutubia kwa ajili ya ubaya wa kuteleza kwake![107] .

Je! Hamko wana wa kaumu hii, na mababa zao, ndugu na jamaa zao wa karibu? Mnafuata mifano yao na kuiga njia zao[108] na mwaenda njia zao, nyoyo ziko bado ngumu, zimeghafilika mbali na mwongozo wake, zaenda njia isiyokusudiwa! Kama kwamba mkusudiwa ni mwingine, kama kwamba mwongozo upo katika kukusanya dunia yake.”

HADHARI YA KITISHO CHA AS-SIIRAAT

“Na juweni kuwa mtapaswa kuvuka juu ya as-Siiraat nyayo zitateleza kiasi cha kumtupa mtu chini, na vitisho vya utelezi wake na mfululizo wa vitisho vyake.

Basi mcheni Mungu enyi waja wa Mungu uchaji wa mwenye akili, ambaye fikra zimeushughulisha moyo wake, na hofu imeutaabisha mwili wake, na sala ya tahadjudi imemfanya akeshe, na matumaini yamembakisha na kiu nusu ya mchana wa siku yake, (yaani anafunga mchana wake) na zuhudu imezuia matamanio yake, na dhikr ya Mungu imeufanya ulimi wake kuwa mwepesi, na ametanguliza hofu kwa ajili ya amani yake[109] akajiepusha njia zilizo kombo kwa kufuata iliyo sawa, kwa ajili ya iliyo sawa, yu afuata njia iliyonyooka zaidi ili kuifikia njia ihitajiwayo; wala geuzo la ghururi halikugeuza fikra yake, wala mkanganyiko wa mambo haukumfanya asijue ukweli.

Akiwa katika hali ya furaha kwa bishara ya kufaulu neema ya maisha mema, katika neema kubwa ya usingizi wake, na siku yake yenye amani mno.

Akiwa amevuka kivuko cha hii haraka (dunia) mwenye kuhimidiwa[110] , na akiwa ametanguliza masurufu ya baadaye akiwa na furaha, na ameharakia kutoka kwenye woga[111] na akakaza mwendo katika muda wa uhai[112] na akapenda kipaswacho, na kukiepuka kinachobidi, katika siku yake akaichunga kesho yake, na akaangalia yanayokuja mbele miongoni mwa a’amali, yaani akaangalia atakachokitanguliza miongoni mwa aamali.

Yatosha pepo kuwa ni malipo mema na mafanikio, na moto ni adhabu tosha na mateso, Mungu (s.w.t) ni mlipizaji tosha na mnusuru! Na Kitabu (Qur’ani)[113] ni hoja tosha na hasimu.

“Nakuusieni kumcha Mungu ambaye hakuacha udhuru kwa aliyoyaonya, na ametoa udhuru kwa onyo lake wazi[114] , amekutahadharisheni na adui aingiae vifuani kwa kificho[115] , na kupulizia masikioni kwa siri, kwa njia hiyo, amepotosha na kufanya uharibifu.

Atoa ahadi ya uwongo na kuyapamba maovu, na kudharau madhambi makubwa yaangamizayo, mpaka anapomporomosha kutoka daraja ya mwongozo mwenzi wake[116] , naye atastahiki rehani yake, atakuwa yuakanusha aliyokuwa akiyapamba, na kuyakuza aliyokuwa akiyadharau, na kuyatahadharisha aliyokuwa akiyafanya yako salama.”

MIONGONI MWAYO MAELEZO YA KUUMBWA MWANADAMU

“Au mwangalie mwanadamu ambaye Mungu amemuumba ndani ya giza la mfuko wa uzazi na mifuniko ya sitara, ikibubujikiwa na manii, kisha likafanyika pande la damu lisilo na sura, baada ya hapo mimba, halafu kitoto kichanga kinyonyacho, kisha mtoto, baada ya hapo kijana, kisha amemtunukia moyo wenye kumbukumbu, ulimi wa kunenea, na macho yakuonea, ili aweze kufahamu na kuzingatia, apate kuacha kutenda maovu akijiziwia (kwa nguvu za mazingatio) afikiapo utu uzima, na kufikia kimo chake cha kawaida, na umbo lake kufikia kimo chake.

Akanusha kwa kiburi, aingiwa na ghururi na kubabaika bila kujali. Aijaza ndoo kubwa ya matamanio yake, afanya juhudi kukamilisha utashi wa dunia yake, katika matamanio yake, akienda na yanayomdhihirikia katika utashi wake. Kisha hakuogopa uovu wowote, wala kutishika wala kuwa na wasiwasi. Alikufa ndani ya maovu yake hali yukijana aliyeghurika. Aliishi akiwa makosani kwa muda mfupi. Hakufaidika na thawabu mbadala. Wala hakutekeleza wajibu wowote. Maradhi mabaya yalimkabili akiwa bado na ukaidi wake katika njia ya furaha yake kubwa, na alipitisha usiku akiwa kama amelewa[117] .

Alikesha akiwa katika shida ya majonzi na machungu, kufikiwa na uchungu na magonjwa, kati ya ndugu na ndugu wa damu, na baba mwenye huruma, na mama anayelia akisema: ole wangu mwenye huzuni, dada apigaye kifua akiwa amefadhaika; na mtu yu katika sakarati ya mauti anataabika na shida ya kukatisha tamaa, na mvuto wa kuchukiza, na msukumo wa sakarati ya mauti.

Kisha yuatiwa ndani ya sanda akiwa mublisa[118] mwenye kukata tamaa ya rehema ya Mungu avutwa kwa urahisi[119] , kisha kutiwa ndani ya jeneza akiwa mwenye machovu ya kutupwa, na aliyekondeshwa na ugonjwa.

Akibebwa na wasaidizi vijana, na ndugu wasaidizi wambeba wakimpeleka kwenye nyumba yake ya upweke na na watu huacha kumzuru[120] , na mahali pa upweke, mpaka wanaporudi waliokuwa wakimsindikiza na akarejea wenye huzuni, atakalishwa shimoni mwake akisemeshwa[121] kwa faragha maswali ya kuduwaza, na mtihani wa kujikwaa.

Na balaa kubwa mno huko ni kuingia maji ya moto na kuteseka na Jahannam, na kutokota kwa moto, na ukali wa sauti ya moto, hakuna muda wa mapumziko, wala wa raha, wala nguvu ya kuzuia wala kifo cha kutuliza, wala usingizi wa kuliwaza, atakuwa kati ya aina mbalimbali za maiti[122] , na adhabu za kila wakati na saa zote! Hakika tunajilinda na Mungu.

Enyi waja wa Mungu! Wako wapi ambao walipewa umri mrefu na kuneemeshwa! Walijulishwa na wakafahamu, na walipewa muda na wakaupoteza bure[123] , walikuwa salama na wakasahau, walipewa muda mrefu wa maisha, waliumbwa kwa sura nzuri, walitahadharishwa machungu, waliahidiwa makubwa! Jihadharini na dhambi zinazoangamiza, na aibu zikasirishazo.

Enyi wenye macho na masikio na afya na mali! Je kuna upenyo! Au epuko, au kimbilio, au marejeo (yaani kurejea hapa duniani) au hapana? “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?” (6:95) “Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62)

Au mwaghurika na nini! Hali ikiwa mmoja wenu hisa yake ya ardhi yenye urefu na upana ni kadiri ya urefu wake, mwenye kugusishwa shavu lake na mchanga (yaani maiti azikwapo ni sunna shavu lake ligusishwe mchanga kwa kuiondoa sanda aliyovikwa eneo la shavu lake).

Enyi waja wa Mungu! ni hivi sasa hali kamba haijakaza shingoni[124] , na roho zimeachwa katika wakati wa kutaka mwongozo, hali miili iko na raha, na ukumbi wa kujikusanya[125] , na muda wa maisha upo na mwanzo wa muda wa utashi [126] ,49 kuna nafasi ya kufanya toba, na nafasi ya wakati wa haja kabla ya shida, dhiki, hofu, na kubanwa, na kabla ya kuja mauti yanayongojewa na kabla ya shiko la Mwenye nguvu Muweza (s.w.t).”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

84 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KATIKA KUMUELEZEA AMRU IBNUL-A’AS

“Namshangaa ibn An-Nabighah! eti asema akiwa kati ya watu wa Syria (Sham) kuwa mimi ni mtu wa mzaha, na kuwa mimi ni mtu wa mchezo mwingi, najishughulisha na mieleka na kupigana na watu. Amesema batili na ametamka akiwa na dhambi.

Angalieni, (maneno ya uovu mno ni uwongo) naye yuasema na yuadanganya, anaahidi na yuaenda kinyume, anaomba kwa kung’ang’ania[127] na akiombwa yuafanya ubakhili, anavunja ahadi, na anaukata udugu. Awapo vitani yeye ni mkemeaji na muamrishaji!.

Hapo ni ikiwa panga hazijachukua nafasi yake, na zikichukua nafasi yake, ujanja wake mkubwa ni kuwaonyesha maadui zake utupu wake. Ama mimi wallahi kukumbuka mauti kwanizuia kufanya mzaha, na kwa kweli yeye kimzuiacho kusema kweli ni kuisahau akhera, kwa hakika yeye hakumpa bai’a Muawiya mpaka alipompa sharti ya kupewa kitu.[128] ”.

85 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - al-Wasitiy ameitaja katika Uyunul-Hikami wal Mawa’idhy, na Ibn Sibt Jauziy katika Tadhkiratul-Khawa’is uk. 131.

KATIKA KUMWADHIMISHA MWENYEZI MUNGU NA KUMTUKUZA

“Na ninashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah swt. peke Yake, hana mshirika, ni wa milele (bila mwanzo) alikuwa yupo wakati hapakuwa na kitu kingine, na ataendelea kuwepo baada ya kutoweka kwa kila kitu, Yeye hana kikomo. Dhana haiambui kumpata na sifa, wala nyoyo haziwezi kumuelewa kwa aina, wala hapatwi na ufanywaji wa sehemu sehemu wala kufanywa kwa mfano kwamba hii ni baadhi ya sehemu ya Mungu. Hazungukwi na uoni wa macho na wa nyoyo.[129] ”.

NA SEHEMU YAKE NYINGINE (YA KHUTBA) KUIELEZEA PEPO

“Tabaka zinazo zidiana, na daraja zinazo tafautiana, neema zake hazikati- ki, atakayedumu humo hatozeeka, wala mkazi wake hatokuwa fakiri.”.

86 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ad-Dainuriy ameitaja katika al-Akhbar at-Twiwalu uk. 145; na ibn Shu’ba katika Tuhaful- Uqul uk. 100, na al-Barqi katika al-Mahasimu uk. 233.

KUHUSU WAADHI WA KUJIANDAA KWA AJILI YA ULIMWENGU MWINGINE NA KUFUATA AMRI ZA MUNGU

“Amezijua siri, na habari ndani ya dhamiri, yuakizunguka kila kitu, na mwenye kukishinda kila kitu, na mwenye nguvu juu ya kila kitu. Basi mtendaji miongoni mwenu na atende ndani ya muda wa (uhai) wake kabla ya kukabiliwa na ajali yake. Na atende wakati wa wasaa kabla ya kushughulishwa kwake, na wakati wa nafasi yake kabla hajashikwa koo[130] .

Ajiandae kwa ajili ya nafsi yake na safari yake, na aandae masurufu kutoka kwenye nyumba ya kituo chake (cha muda) kwa ajili ya nyumba ya kudumu kwake.

Mkumbukeni Mungu swt. enyi watu, kwa aliyokutakeni ndani ya Kitabu chake kuyazingatia, na haki Zake alizozihifadhi humo, kwa kuwa Mungu (s.w.t) hajakuumbeni bure, na wala hajawaacheni bila ya faida, wala hajawaacha katika ujinga wala upofu. Amepandisha daraja ya athari zenu, na amejua amali zenu, na ameamua ajali zenu.

Na amekuteremshieni Kitabu kinachobainisha kila kitu, na amemrefushia umri nabii Wake kwa zama ndefu, kiasi cha kumkamilishia yeye na ninyi ujumbe - aliouteremsha Kitabuni mwake - ambao ni dini Yake ambayo ameiridhia nafsini Mwake; na amebainisha kwenu - kupitia ulimi wake - matendo mema na mabaya, makatazo Yake na amri Zake, na ameweka mbele yenu hoja Yake na kuondoa udhuru kwenu, amekukemeeni na kuwaonya na adhabu kali. Hivyo basi zidirikini siku zenu zilizobaki, na zifanyeni nafsi zenu zivumilie humo. Kwa kuwa ni chache katika siku nyingi ambazo mnakuwa katika mghafala, na kutotilia manani mawaidha, msiuachie muda, utawawekeni katika njia ya madhalimu, na msijipendekeze, kwa kuwa kujipendekeza kutawasukumeni kwenye maasi.

Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli mnasihi mzuri mno wa nafsi yake katika watu ni yule mtii mno wa Mola Wake[131] ; Na kwa kweli mwenye kuighushi mno nafsi yake ni muasi sana wa Mola Wake[132] ; na mwenye kupunjwa ni yule ambaye ameipunja nafsi yake, na mwenye kutamani mfano wa hali ileile[133] ni yule ambaye dini yake iko salama, na mwenye furaha ni mweye kuwaidhika na mtu mwingine, na dhalili ni mwenye kuhadaika na utashi wa nafsi yake na kughurika kwake. Jueni kwamba kuwepo kwa kiasi kidogo cha riya’a[134] - ni ushirikina, na kukaa na watu wanaofuata matamanio ya nafsi zao - hawaa - yaliyoko nje ya maadili ya kisharia - kunasahaulisha imani, na ni mahudhurio ya Shetani.

Jiepusheni na uwongo, kwa kuwa ukando na imani. Mkweli yu ukingoni mwa wokovu na heshima, na muongo yuko katika kilele cha kuanguka na kudharauliwa. Msihusudiane, kwa kuwa husuda huila imani kama moto ulavyo kuni.

Msibughudhiane, kwa kuwa huko ni kwenye kufuta imani[135] ; na jueni kwa mba kuwa na matumaini mno - kunaisahaulisha akili na kumbukumbu[136] . Basi yakidhibisheni matumaini kwa kuwa ni ghururi, na mwenye nayo ameghurika.”

87 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Zamakhshari ameieleza katika Rabiul-Abrar mlango wa al-izzu

wa sharaf.

KUHUSU AMPENDAYE MUNGU MTUKUFU

“Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli miongoni mwa waja wapendwao mno na Mungu ni mja ambaye Mungu amemsaidia kupambana na nafsi yake, akawa yuaifanya huzuni ni shi’aru yake - vazi la ndani[137] , na amevaa joho la hofu, kwa hiyo taa ya mwongozo ikaangaza moyoni mwake, na aka andaa takrima kwa ajili ya siku yake atakayofikia, kwa hivyo akasogeza kwa ajili yake kilicho mbali, na akapoza makali ya shida[138] , ameangalia akatambua, akakumbuka na akakithirisha[139] .

Alipoza kiu kwa maji baridi aliyorahisishiwa maendeo yake, akanywa na kutosheka. Akapita njia iliyosawa, akiwa amevua vazi la matamanio, na kujiepusha na mahangaiko ya moyo, isipokuwa hangaiko moja pekee amebaki nalo[140] , kwa hiyo akawa ametoka na kuwa mbali na sifa za upofu, na mbali na kushirikiana na watu wa matamanio, hivyo akawa miongoni mwa funguo za milango ya uongofu, na vifungio vya milango ya kuangamia.

Ameiona njia yake na akaipita njia hiyo, na akaijua miongozo yake, akaivuka bahari yenye maji mengi iangamizayo, na akashikamana na kishiko kwa umadhubuti, na miongoni mwa kamba iliyo ngumu mno, kwa hiyo yeye kwenye yakini yu kama mwanga wa jua, ameisimamisha nafsi yake kwa ajili ya Mungu (s.w.t) katika mambo ya hali ya juu kabisa; kwa kulikabili kila limfikalo, na kuchukua kila hatua ihitajiwayo kwa hilo, na kulirudisha kila tawi kwenye shina lake[141] .

Ni taa ya giza jingi, mfichuaji wa upofu, ni ufunguo wa yaliyofumbika, mzuiaji wa shida, mwongozaji wa jangwani, akisema yuafahamisha, akinyamaza husalimika.

Amekuwa na ikhlasi kwa Mungu naye akamfanya makh’susi kwa ajili Yake, hivyo yeye ni chimbuko la dini Yake, na vigingi vya ardhi Yake. Amejiambatanisha binafsi na uadilifu, na ukawa uadilifu wake wa kwanza kujiondolea utashi wa kibinafsi.

Anaielezea haki na anaitendea kazi, haachi lengo la kheri ila atalikusudia, wala padhaniwapo kheri ila atapaendea. Amekishika Kitabu hatamu zake[142] nacho ndio kiongozi wake na Imamu wake. Anashuka pale ambapo kinapoifikisha mizigo yake[143] , na anateremka mahali pake pakufikia.”

SIFA ZA MTU FAASIQI

“Na mwingine amejiita mwanachuo hali akiwa si mwanachuo[144] , amedondoa dhana za kijahili kutoka kwa majaahili, na upotovu kutoka wapotovu, na amewategea watu mtego uliotengenezwa kwa kamba ya udanganyifu, na maneno ya uwongo; anakichukuwa Kitabu-Qur’an - kwa maoni yake; na ukweli ameupindisha kulingana na utashi wake binafsi.

Anawafanya watu wajione wako salama watendapo makosa ya jinai, na hulichukua kosa kubwa kama ni kitu chepesi, anasema: ‘Nasita kwenye mambo yasiyo wazi,’ na humo yuajiingiza; na anasema: ‘najiepusha mbali na bid’a,’ na punde amejiingiza humo. Hivyo basi sura yake ni ya mtu, na moyo ni moyo wa mnyama, hajui mlango wa uongofu ili aufuate, wala mlango wa upotofu ili aufunge akiwa mbali nao, na huo ni umauti wa walio hai. “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?” (6:95) “Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62).

Na alama zipo[145] , Na aya ziko wazi, na minara imesimamishwa[146] ,mnapotezewa wapi! na vipi mnakuwa vipovu na kati yenu kuna itrah ya Nabii wenu![147] Nao ndio hatamu za ukweli[148] , na ni alama ya dini, na ndimi za ukweli! Hivyo wawekeni daraja nzuri mno ya Qur’an[149] , na muwaendee mwendo wa ngamia walio na kiu[150] . “Enyi watu! Chukueni kutoka kwa Khatamun-Nabiyina - hitimisho la Manabii(s.a.w.w) : (Kwa hakika hufa afaye katika sisi na wala si mfu[151] , na huoza aliyeoza katika sisi wala hakuoza) hivyo basi msiseme msiyoyatambua, kwa hakika ukweli mwingi upo katika myakanushayo[152] .

Kubalini udhuru wa msiye na hoja dhidi yake - naye ndimi - je sikuifanyia kazi kwenu thiq’lu kubwa![153] Na ninaiacha kwenu thiq’lu ndogo? Na nikasimika katika nyinyi bendera ya imani, na nimekusimasheni kwenye mipaka ya halali na haramu, na nikakuvisheni afya kutokana na uadilifu wangu, na nimekukukunjulieni mema kwa kauli yangu na vitendo vyangu, na nimekuonyesheni tabia njema za hali ya juu kutoka kwangu mimi mwenyewe binafsi. Hivyo msitumie rai katika ambayo hakifikiwi kina chake na macho, wala fikra haziingii.[154]

Na Sehemu Ya Khutba Hii Kuwahusu Bani Umayyah:

“Mpaka atadhania mwenye kudhani kuwa dunia imefungwa aqal, kwa Bani Umayyah, yawapa kheri zake[155] , na kuwaongoza kwenye chemchemi safi za manyweo yake, na wala ummah huu hautaondolewa mjeledi wala upanga wake, na atakuwa ameongopa adhaniaye hivyo. Bali hilo ni tone la maisha ya ladha[156] (watalila kwa muda kisha watalitema lote).”.

88 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - al-Kailaniy ameieleza katika ar-Raudhwa uk.62, na Sheikh al-Mufiidu katika ar-Rishadu uk.173, na Ibn Athir amezitafsiri (hadith) ghariib katika an-Nihaya mada ya Azalu.

KATIKA KUELEZEA MAKOSA WALIYONAYO WATU

“Amma ba’ad. Kwa kweli Mungu hakupata kumuangamiza dhalimu wa zama fulani katu isipokuwa baada ya kumpa fursa na raha, wala hakuuganga mfupa wa yeyote katika wana umma isipokuwa baada ya dhiki na shida, na hakuwakabili kwa misiba na shida juu yao hata kwa kiasi kidogo kuliko ambacho kitawafikeni au tayari kimewafikeni, kinatosha kuwa somo. Wala sio kila mwenye moyo ni mwerevu, wala sio kila sikio ni sikivu, wala sio kila aangaliaye ni mwenye kuona.

Ajabu ilioje! Nitakuwaje nisistaajabishwe na makosa ya vikundi hivi kwa tafauti za hoja zao katika dini yao! Hawafuati athari ya Nabii (wao) wala hawaongoki na matendo ya waswii, wala hawaamini ghaibu, wala hawajiepushi na jambo la aibu, wanatenda katika mambo yanayoshakiwa, na wanakwenda na matamanio.

Kwa wao jema ni lile wanalolipenda wao, na ovu kwao ni walikataalo[157] , kimbilio lao katika matatizo ni kwao wenyewe binafsi, mategemeo yao katika mambo yanayoshakiwa ni rai zao. Kama kwamba kila mmoja ni imamu wa nafsi yake[158] , amejiamulia ayadhaniayo kuwa ndiyo tegemeo, na ni sababu thabiti.”.


3

4

5

6