NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI33%

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Mwandishi:
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi: VITABU VYA HADITHI

Juzuu 1 Juzuu 2
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9479 / Pakua: 4863
Kiwango Kiwango Kiwango
NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

101 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

NAYO NI KHUTBA MOJAWAPO AMBAYO NDANI YAKE KUNA MAELEZO YA MAPAMBANO YA KIVITA

“Mstahiki wa sifa ni Mungu ambaye ni wa mwanzo kabla ya chochote. Na wa mwisho baada ya kila kitu. Na kwa umwanzo Wake imelazimu iwe hakuna kilichomtangulia. Na kwa umwisho wake imelazimu iwe hakuna wa mwisho ila ni Yeye. Ninashuhudia kuwa hapana mungu ila ni Allah (tu) wazi wazi na kwa siri, kwa moyo na kwa ulimi.

“Enyi watu! Kunikhalifu kwenu na kuniasi kusiwafanye mnikadhibishe, wala msishawishike kuniasi, wala msikonyezane kwa macho mnaponisikiliza.

Ninaapa kwa ambaye ameipasua mbegu na kumuumba mwanadamu kuwa ambayo nimewaambieni ni kutoka kwa Nabii Al’ummiyyi(s.a.w.w) , Wallahi mfikishaji hakusema uwongo, wala msikilizaji hakuwa mjinga[235] .

Kana kwamba namuona na namuangalia mpotovu mno[236] amepiga kelele Sham (Syria) na amesimika bendera zake mpakani mwa Kuufani - (ni jina la mji wa Kufa) - afunguapo kinywa chake na kushika kasi ukaidi wake na ujeuri (yaani dhulma) wake ardhini kuwa nzito, fitna itawang’ata watu kwa meno yake, na vita mawimbi yake yatachafuka, na siku zitadhihirisha kisir- ani chake, (zitakuwa ngumu) na usiku taabu zake.

Matunda yake yakipevuka, na akianza kuyachuma, na ngamia kuunguruma, na mikuki na panga kumwetuka, fitna korofi itachukuwa nafasi, na itakuwa kama usiku wa giza, na bahari yenye kupigapiga mawimbi yake.

“Hii ni mara ngapi mji wa Kufa unaharibiwa na dhoruba, na kupitiwa na kimbunga. Hivi punde karne itapambana na karne[237] , mazao yaliyosimama yatavunwa na yaliyovunwa yataharibiwa![238] ”.

102 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU MAUDHUI ILEILE YA SIKU YA KIYAMA

“Hiyo ni siku ambayo Mungu atawakusanya waliokuwa kwanza na wa mwisho ili kudodosa hesabu, na kulipwa aamali, wakiwa wanyenyekevu, wamesimama, jasho limewafunga hatamu[239] .

Na ardhi ikawatetemesha[240] , basi mwenye hali nzuri katika wao ni mwenye kuipata nafasi kwa ajili ya nyayo zake, na wasaa kwa yeye kuweza kupumua.”

NA SEHEMU YA KHUTBA HIIHII KUHUSU TAABU ZA SIKU YA KIYAMA

“Ni fitna kama giza la usiku, hakuna kikundi kitachosimama kupambana nayo wala bendera zao kurudishwa nyuma. Atakujieni (hiyo saa) mfano wa ngamia aliyetayari akiwa na hatamu yake na zana zake, muongozi wake yuamhamasisha[241] , na mpandaji wake anambidiisha[242] , watu wake wachocheao vita - mashambulizi yao ni makali, uporaji wao ndio kidogo[243] . Wanaopigana vita katika njia ya Mungu ni kaumu dhalili mbele ya wenye kiburi[244] , wasiojulikana aridhini, na maarufu mbinguni. Ole wako ewe Basrah, pindi kipigo cha adhabu ya Mungu kitapokuangukia! Hakina vumbi wala sauti, watu wako watakabiliwa na umauti mwekundu na njaa yenye rangi ya vumbi.[245] ”.

103 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU KUJIEPUSHA NA TAMAA ZA DUNIA

“Enyi watu! Itazameni dunia mtizamo wa watawa wanaojiepusha nayo, wenye kuigeuzia uso, kwa kweli Wallahi ni punde tu itawaondoa wakazi walioifanya maskani, na kumfadhaisha anayeishi kwa anasa na mwenye kujiamini, kilichogeuka na kiendacho kuzimu hakitorudi, na ambacho kinatarajiwa kuja hakina uhakika, furaha yake ni mchanganyiko na huzuni, na watu imara wenye nguvu wanaelekea kwenye ulegevu na udhoofu. Hivyo basi msighurike na mengi yanayokufurahisheni humo kwa sababu ya uchache wa yatakayofuatana na nyinyi kutokana nayo.

“Mungu amrehemu mtu ambaye ametafakari na kujifunza humo, amejinfunza na kufanikiwa mwangaza. Kana kwamba ambacho kipo katika dunia hii kwa muda mfupi kitakuwa kama hakijakuwa. Kama kwamba ambacho kipo katika akhera baada ya muda mfupi kitaonekana kama kwamba hakijakosa kuwa. Kila kihesabiwacho kitatoweka, na kila kitazamiwacho kinakuja. Na kila kinachokuja kimekurubia.”

SEHEMU YA KHUTBA HII HII KUHUSU SIFA ZA MWANACHUONI

“Mwanachuoni hasa ni yule mwenye kuitambua thamani yake, yatosha kwa mtu kuwa yu-mjinga kwa kutoijua thamani yake. Kwa hakika miongoni mwa watu awachukiao mno Mwenyeezi Mungu ni yule mja aliyemuachia mambo yake yeye mwenyewe. Anakwenda kombo mbali na njia iliyo sawa, anakwenda bila ya dalili, aitwapo kwenye shamba la dunia atafanya, na aitwapo kwenye shamba la akhera atakuwa mvivu, kana kwamba alilofanya ni wajibu juu yake, na kana kwamba alilolifanyia uvivu si wajibu juu yake.”

SEHEMU YA KHUTBA HII HII KUHUSU WAKATI WA BAADAYE

“Huo ni wakati ambao hatookoka kutoka humo isipokuwa aliye na usingizi sana[246] , akiwa yupo hatambuliki, na akighibu, hakosekani, hao ndio taa za mwongozo na alama za misafara ya usiku, si wasambazaji wa masingizio wala si watoboa siri.

Hao Mungu atawafungulia milango ya rehema Zake, na atawaondolea madhara ya adhabu Zake[247] . “Enyi watu! Zitakujieni zama uislamu utapinduliwa juu chini kama ambavyo chombo kifunikwavyo pamwe na kilicho ndani yake.

Enyi watu! Kwa hakika Mungu amekulindeni kwa maana ya kuwa hatowadhulumu, wala hakuwalindeni kwamba hatowafanyieni mtihani[248] , na amesema Mtukufu katika wasemaji:[249] “Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini. Sisi ni wenye kuwafanyia mitihani.” (23:30).

Ar–Radhiy (r.a) amesema: Ama kuhusu kauli yake(a.s) : “Kullu mu’minin nuwamatin” Kila muumini mwenye kulala sana, amekusudia kwa hilo: yaani yule muumini asiye kumbukwa au asiyetajika, na si mtu wa shari.

Na al-Masayiihu: Ni wingi wa neno misyahun, naye ni chakubimbi aendaye kwa huyu na kwa huyu ili kufanya ufisadi (umbea). Al-Madhayyiiu: Ni wingi wa midh’yaun, naye ni ambaye asikiapo baya la mwenzake analitangaza na kulieneza.

Ufafanuzi

Usemi wake(a.s) : “Mwanachuoni ni yule ambaye ameijua Qadiri yake,” ni miongoni mwa mithali mashuhuri kutokana naye(a.s) na wamesema watu baada yake na wamekithirisha, mfano wa kauli yao: ‘Ikiwa hutoijua Qadiri ya nafsi yako, kwa hiyo Qadiri ya mwingine hautoijua kabisa.’

Na mfano wa kauli yao: ‘Ambaye hajui Qadiri ya nafsi yake, watu watakuwa hawana kosa endapo watakuwa hawamjui.’

Na miongoni mwa maneno yaliyoelezwa kutoka kwa Abi Abdillah as-Sadiq(a.s) katika riwaya marfu’u: “Ma halakamru’u arifa Qadrahu” yaani hatohiliki mtu aliyeijua Qadiri yake - riwaya hii ni ya Abul’Abbas kutoka kwake katika Al’Kaamil. Na katika Hadithil-Marfu’u:

104 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s)

MWANZO WA KHOTUBA HII UMETANGULIA KATIKA NAMBA 33.

“Sasa basi! Kwa kweli Allah (s.w.t) alimtuma Muhammad(s.a.w.w) wakati hapakuwa na yeyote katika waarabu aliyekuwa akisoma kitabu, wala kudai unabii wala wahyi (ufunuo).

Na alimpiga vita aliyemuasi akisaidiwa na wanaomtii, akiwaongoza kwenye uokovu wao, na anawaharakishia saa isije kuwashukia[250] , anashindwa mwenye kushindwa, na anasimama aliyevunjika[251] anamsimamia mpaka amfikishe kwenye lengo lake[252] .

Isipokuwa aliyeangamia asiye na kheri, mpaka alipowaonesha uokovu wao, na aliwakalisha mahali mwao, mambo yao yakaenda sawa, na yalitengenea.

Naapa Mungu, kwa kweli nilikuwa miongoni mwa waswagaji wake[253] - mpaka walirudi nyuma wote, na kujikusanya kwenye kamba yao, sikuonyesha udhaifu au kutokuwa na hima, au kuhini wala sikuonyesha unyonge, namuapa Mungu nitaitumbua batili mpaka niitoe haki kutoka kiunoni mwake!”

Sayyid Ar-Radhiy (r.a) amesema: Yaliyoteuliwa katika khutba hii yametangulia, ila tu mimi nimeikuta katika riwaya hii kukiwa na tofauti na iliyotangulia, kati ya ziada na upungufu, kwa hiyo hali imewajibisha kuithibitisha tena.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

105 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU BAADHI YA SIFA ZA NABII MTUKUFU NA KEMEO KWA BANI UMAYYAH NA MAWAIDHA KWA WATU

“Kisha Mungu alimtuma Muhammad(s.a.w.w) ili awe shahid[254] na mbashiri na muonyaji, ni mbora katika viumbe akiwa mdogo, na mwenye heshima mno akiwa mtu mzima, na msafi mno katika wasafi wa tabia, na ni mkarimu mno kwa wenye kumuomba[255] .

Dunia haikuwa tamu katika ladha yake kwenu. Wala hamkuweza kunyonya chuchu zake ila mlipokuta hatamu zake zimelegea.

“Kisha alisema kuwa wao wameikuta dunia kwa bahati imekwisha kuwa ngumu kwa atakayeitawalia utawala wa haki kama anavyokuwa mgumu ngamia kwa mpandaji wake endapo hatamu yake itajikusanya, haudaji yake haitulii kwa mpandaji, haramu zake zapatikana kiurakhisi kwa aipendaye.

Ni mfano wa mti wa msidiri uliokatwa miba yake, kwa hiyo ukawa laini wateleza; na halali zake hazipo tena kwa kushindwa na haramu; na kwa kuwa umezagaa umechukua nafasi kulingana naye; na hii ni ishara kwenye aliyokuwa akiyasema daima kwa kujitwalia kwao binafsi suala la ukhilafa makhalifa waliomtangulia mbali naye, kuwa yeye alikuwa msitahiki.

“Kunyonya kiwele chake ila baada ya kumkuta kwa bahati hatamu yake ya puani inajiburura na ukanda wake wa ngozi umelegea. Uharamu wake umekuwa kwa kaumu ya watu kama msidiri ulionepa (kwa uzito wa matunda) hali ikiwa uhalali wake ni mbali, haupo.

Wallahi, mngeikuta kama kivuli kirefu, mpaka muda uliopangwa.

Kwa hiyo ardhi kwenu ni tupu[256] , na mikono yenu humo imekunjuka, na mikono ya viongozi imefungwa mbali nanyi. Panga zenu zimewadhibiti[257] na panga zao zimezuilika dhidi yenu[258] .

Jueni kuwa kwa kila damu iliyomwagwa ina kisasi, na kila haki ina mdai, na mdai kisasi wa damu yetu ni sawa na hakimu anayetoa hukumu kuihusu haki yake binafsi[259] , huyo ni Mungu ambaye hamshindwi amtakaye, wala hamkosi atakayemkimbia.

Namuapa Mungu Enyi Banii Umayyah! baada ya muda mfupi mtaiona nafasi yenu ikiwa mikononi mwa wengine, na nyumbani mwa adui yenu! Jueni kuwa macho yaonayo sana miongoni mwa macho ni yale yaliyopenya kuiona kheri! Jueni kuwa masikio sikivu ni yale yaliyoelewa mawaidha na kuyakubali![260] ”.

KUHUSU SHUGHULI ZA IMAM

“Enyi watu, chukueni mwanga kutoka mwenge wa taa ya muwaidhi mwenye kuwaidhika[261] ,kunyweni na chukueni maji kutoka chemchemi iliyohifadhiwa na kusafishwa bila uchafu[262] .

“Enyi waja wa Mungu! Msiutegemee ujahili wenu, wala msiutii utashi (mbaya) wa nafsi zenu kwa kuwa yule mwenye kuwasili kwenye nyumba hii[263] yupo kwenye ukingo wa kuzolewa na maji yazoayo kila uchafu[264] ananakili[265] maangamizi mgongoni kwake kutoka sehemu (ya mgongo) mpaka sehemu, kwa rai aizushayo baada ya rai; anataka kuambatanisha kisichoweza kuambatana, na kukisogeza karibu kisicho weza kusogea! Ala ala muogopeni Mungu msimlalamikie huzuni zenu yule asiyeweza kuzitanzua, wala hawezi kutangua kwa rai yake lililo lazima juu yenu.

Na kwamba si juu ya Imam isipokuwa alilobidiishwa miongoni mwa amri za Mola Wake Mlezi: Kufikisha mawaidha, na kujitahidi kutoa nasaha, na kuihuisha Sunnah, na kuitekeleza adhabu kwa wanaostahili, na kuzirudisha hisa kwa wenye kustahiki. Hivyo basi harakishieni elimu kabla ya mmea wake haujakauka, na kabla hamjashughulishwa na nafsi zenu mbali na wenye kuwa nazo. Katazeni maovu na wenyewe muwe mmejikataza, mlichoamriwa ni kukataza baada ya kujikataza!.

106 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

HUMO ANABAINISHA UBORA WA UISLAMU, NA AMTAJA MTUKUFU MTUME(S.A.W.W) KISHA ANAWALAUMU SAHABA ZAKE:

“Shukrani zote anastahiki Allah (s.w.t), ambaye ameifanya sharia ya kiisla- mu na kuifanya nyepesi kwa mwenye kuiendea, na ameziimarisha nguzo zake dhidi ya mwenye kutaka kuushinda, na akaufanya kuwa ni amani kwa wenye kujiambatanisha nao, na salama kwa mwenye kuingia – (yaani hapigwi vita akishaingia uislamu), na hoja kwa mwenye kuueleza, na ni shahidi kwa mwenye kugombana kwa ajili yake, na ni nuru kwa mwenye kujiangaza nao, na ni fahamu kwa mwenye kutumia akili, na ni busara kwa mwenye kuzingatia, na ni alama kwa mwenye kuchunguza, na ni uelewa kwa mwenye kuazimia, na ni funzo kwa mwenye kuwaidhika, na ni uokovu kwa mwenye kusadiki, na ni ithibati kwa mwenye kutegemea, na ni raha kwa mwenye kuitumainia, na ni kinga kwa mwenye kusubiri.

Ni njia maarufu iliyo wazi mno na maingilio yaliyo wazi na ni mnara wa juu, na ni njia iliyo dhahiri, ni taa ziwakazo, ni mahali pa kujivunia, bendera iliyoinuka, yenye kukusanya farasi, ni pa kushindania washindani, mtukufu wa washindi wa farasi.

Wapandaji wake ni wenye kuheshimiwa, kusadiki (Mungu, Mtume…) ndio njia yake, vitendo vyema ndio minara yake, umauti ndio lengo lake[266] , na dunia ni kiwanja chake cha mafunzo, na kiyama ni farasi wake, na pepo ni malipo yake ya mashindano.

NA SEHEMU YA KHUTBA NI KUMUELEZA NABII (S.A.W.W):

“Mpaka aliwasha mwenge kwa autakaye[267] , na aliangaza mwanga kwa mahabusi[268] , hivyo basi yeye ni muaminifu wako wa kuaminika, na shahidi wako siku ya malipo, na ni muwakilishi wako akiwa neema, na ni Mtume wako wa kweli akiwa ni rehema.

“Oh Allah! Umgawiye fungu katika uadilifu Wako, na umpe jazaa ya kheri nyingi katika fadhila Zako. Oh Allah! Lirefushe jengo lake zaidi kuliko majengo ya wajengao, na umkirimu mafikio yake Kwako.

Itukuze kwako daraja yake, mtunukie wasila na heshima maalumu na ubora, na tukusanye sisi katika kundi lake, bila ya fedheha wala wenye kujuta, wala wenye kupetuka njia, wala wenye kutengua ahadi, wala wenye kupotea wala wenye kupoteza, wala walioshawishika kwa maovu!”

Ar-Radhiy (R.A) Amesema:

Maneno haya yamepita katika habari zilizotangulia, isipokuwa sisi tumeyakariri hapa kwa sababu ya tofauti iliyopo kati ya riwaya hizi mbili.

MIONGONI MWAYO AKIWAHUTUBIA SAHIBA ZAKE

“Kwa ukarimu Wake Mungu (s.w.t) mmefikia daraja ambayo wanahishimiwa hata vijakazi wenu, na majirani zenu wanatendewa vyema, na anakuheshimuni ambaye hamna fadhila yeyote juu yake, wala hamna hisani juu yake. Na anawahofuni asiyekuwa na maalumati ya kuwa mmepata kumshambulia, wala kuwa na mamlaka juu yake.

Mnaziona ahadi za Mungu zinatenguliwa wala hamkasiriki, hali ninyi mwasumbuka kwa kutanguliwa mila za babu zenu. Na mambo ya Mungu yalikuwa yanakuja kwenu, na yanatokea kwenu, na kwenu yanarejea[269] .

Mmewawezesha madhalimu sehemu zenu, na kuwaachia majukumu yenu, na mmeweka mambo ya Mungu mikononi mwao. Wanatenda kwa shaka, na wanakwenda katika utashi mbaya wa nafsi. Naapa Mungu hata wangekutawanyeni chini ya kila nyota, Mungu angewakusanyeni katika siku mbaya mno kwao!”.

107 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

At-Tabari ameieleza katika Ta’arikh yake katika matukio ya mwaka wa 37 H.A., na Ibn Muzahim katika Swifiin, uk. 256.

BAADHI YA SIKU ZA SIFFIIN

“Kwa kweli nimeona kukimbia kwenu na kutawanyika kwenu mbali na safu zenu za vita, mkizungukwa na watu fedhuli na duni, na mabedui wa (Shaam) Syiria, ingawaje ninyi ni watangulizi katika waarabu na ni kilele cha utukufu na kilele cha ubora, na mna daraja ya juu mfano wa ile ya pua, na ule wa nundu kubwa ya ngamia.

Uhemaji wa moyo wangu utapoa tu niwaonapo mnawazunguka kama walivyokuwa wamewazungukeni, na mnawaondoa mahali mwao kama walivyokuondoeni, mkiwauwa kwa mishale na kuwachoma kwa mikuki, hivyo msitari wao wa mbele uangukie juu ya msitari wao wa nyuma, kama ngamia walioshikwa na kiu waliofukuzwa kutoka kwenye manyweo yao, na kuzuiliwa maendeo yao ya kunywea maji!”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

108 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Zamakhshari ameieleza katika Rabi’ul-Abrar, Jz. 1, mlango wa ‘kubadilika kwa hali’.

NAYO NI KHUTBA YA HALI YA MABADILIKO, YAANI MATUKIO MAKUBWA VITANI

“Mstahiki wa sifa njema ni Mungu Aliye dhahiri kwa viumbe Wake kupitia viumbe wake[270] , na mwenye kudhihiri nyoyoni mwao kwa hoja Zake[271] , ameumba viumbe bila ya kufikiri, kwa kuwa kufikiri hakumfalii isipokuwa wenye kuwa na dhamiri[272] , naye si mwenye dhamiri[273] , elimu yake imepenya mpaka ndani ya siri zisizojulikana, na kuzingira itikadi za ndani za siri.”

NA SEHEMU YA KHUTBA HII NI MAELEZO KUHUSU NABII (S.A.W.W)

“Mungu (s.w.t) amemchagua kutoka mti wa nasaba ya manabii[274] , na kutoka mwale wa mwanga, na ni miongoni mwa nywele za utukufu wa kipaji cha uso, kutoka sehemu bora mno katikati ya bonde la Bat’ha’a[275] , na taa za kuangazia gizani, na chemchemi za siri za hekima.”

Miongoni mwayo: “Yeye - yaani Nabii(s.a.w.w) alikuwa mfano wa tabibu anayezunguka na tiba yake, aliyeimarisha marhamu yake, azungukaye na aliye tayari na dawa zake, na amekwisha koleza mawasimu zake[276] . Anazitumia mahali ambapo ipo haja, ili kuziponya nyoyo za vipofu, na masikio ya viziwi na ndimi za mabubu, kwa dawa zake hufu- atilia mahali ulipotawala mghafala na mahali penye mashaka na matata.

Hawakufaidika na mwanga wa hekima zake, na wala hawakuwasha moto kutoka jiwe la elimu litoalo cheche; Hivyo basi wao katika hilo ni kama wanyama watafunao nyasi, na mawe magumu. Siri zimefichuka kwa wenye kufahamu[277] njia ya kweli imekuwa wazi kwa wale wasiokuwa na mwongozo na saa ikurubiayo imeondoa kifuniko usoni pake, na alama zimeonekana kwa wanaoangalia kwa makini.

Nimekuwaje mimi! Nawaoneni (mko) miili isiyokuwa na roho, na roho bila ya miili[278] , wafanya ibada bila wema[279] , na wafanyibiashara bila ya faida[280] , wako macho hali wamelala[281] ,wanatazama hali ni vipofu, wanasikia hali ni viziwi na wanaongea hali ni mabubu!.

MIONGONI MWAYO

“(Nimegundua kuwa) Kuna bendera ya upotovu imejiimarisha katikati, na imetawanyika na watu wa kabila lake, inakupimieni kwa kilo yake[282] , na kuwachanganyeni na uzito wake.

Kiongozi wake yuko nje ya mila (ya kiislaamu) yupo katika upotovu, siku hiyo hatobaki miongoni mwenu ila ni kama mabaki ya chungu[283] au vumbi kama vumbi lililokung’utwa kutoka kwenye kipeto[284] . Hivyo basi itakusugueni kama isuguliwavyo ngozi, na itakukanyageni mkanyago wa mazao yaliyovunwa, na itamdonoa muumini kati yenu kama anavyodonoa ndege punje nene kati ya punje nyembamba.

Madhehebu yanawapelekeni wapi, na giza linawafanya mtangetangie wapi! Na mnapelekwa wapi na matarajio! Kutoka wapi mwaletwa, na mwadanganyiwa wapi? Kila muda una maelezo ya maandishi, na kila aliyetoweka ni lazima arudi, hivyo basi wasikilizeni viongozi wenu wa kiungu, na zihudhurisheni nyoyo zenu, na amkeni atakapowapigieni kelele. Mtangulizi inambidi aongee la ukweli kwa watu wake.

Yampasa azikusanye azma zake na fikra zake ili aangalie, fahamu zake aziweke hadhiri, suala ameliatua uatuaji wa tundu la kizuizi cha vazi, na ameliparua uparuaji wa ulimbo[285] (kutoka kwenye kijiti cha mti na kuondolewa). Wakati huo batili itachukuwa nafasi yake, na ujahili utapanda kipando chake, utovu wa nidhamu utakuwa mkubwa, na wito utakuwa mdogo, na wakati utavamia uvamiaji wa mnyama mkali, na dume la ngamia litakoroma baada ya ukimya, na watu watakuwa ndugu katika maovu, watahamana kwa dini[286] . Watapendana katika uwongo, na watachukiana kwa sababu ya ukweli.

Hali ikiwa ni hivyo mtoto atakuwa chukizo[287] - (yaani atakuwa sababu ya kuchukiza badala ya kuwa kitulizo cha jicho kwa wazazi wake) na mvua - (sababu ya joto), uovu utajaa mno, na maadili mema yatatoweka, na watu wa zama hizo watakuwa mbwa mwitu, na masultani wao ni kama wanyama wavamizi, na watu wao wa hali ya kati watakuwa walafi, na mafakiri wao ni maiti, ukweli umedidimia, na uwongo umefurika, na upendo utakuwa wa maneno, hali watu wakiwa wanagombana kimoyo, na uzinzi ni nasaba, na usafi wa kutozini ni ajabu[288] , na uislamu utavaliwa kama ngozi juu chini.[289] ”.

109 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Az-Zamakhshariy ameieleza katika Rabi’ul-Abrar katika mlango wa Malaika, na ibn Abdi-Rabih katika al-Iqdu al-Farid, jalada la 4, uk. 76.

Katika kubainisha Qudra ya Mungu (s.w.t) na kuwa Yeye ni wa pekee katika utukufu na wa pekee katika suala la kuwarejesha hai viumbe Wake: “Kila kitu chamnyenyekea Yeye, na kila kitu huwa kwa kupitia kwake Yeye: Yeye ni toshelezo la kila fakiri, na hadhi kwa kila mnyonge, na nguvu ya kila dhaifu, na kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo.

Mwenye kuongea anamsikia tamko lake, na mwenye kunyamaza anajua siri yake, na kwa anayeishi riziki ni juu yake, na anayekufa Kwake ndio marejeo.

“Macho hayajakuona hata yawe na uwezo wa kueleza habari zako, na ulikuwa kabla ya waelezaji miongoni mwa viumbe Wako.

Hukuwaumba viumbe kwa ukiwa, wala haukuwafanya wafanye kazi kwa ajili ya manu- faa, hautomtaka yeyote na akukose, wala hakuponyoki umshikae[290] , wala hapunguzi mamlaka yako anayekuasi, wala hazidishi ufalme wako anayekutii, wala hawezi kuirudisha amri yako mwenye kukasirikia maamuzi yako, na wala hajitoshelezi bila wewe mwenye kugeuka mbali na amri yako. Kila siri Kwako ni dhahiri shahiri, na kila cha ghaibu Kwako kipo mbele yako.

Wewe ni wa milele hauna mwisho, Wewe ndio lengo hakuna jinsi ya kukuepuka, na Wewe ndio mahali pa ahadi ya marejeo ambapo hakuna jinsi ya kuokoka kwa kukuepuka Wewe ila Kwako Wewe. Mkononi mwako kuna shungi la nywele la kila kiumbe, na Kwako ni marejeo ya kila kiumbe.

Utukufu ni wako adhama ilioje ya mambo yako! Utukufu ni wako adhama ilioje tuyaonayo kwa viumbe wako! Na udogo ulioje kwa kila adhama pembeni mwa uwezo Wako! Kutisha kulikoje kwa tuyaonayo katika ufalme wako! Unyonge ulioje kwenye yale ambayo yameghibu kwetu miongoni mwa mamlaka Yako! Wingi ulioje wa neema yako duniani, ni ndogo ilioje kwa kuilinganisha na neema ya akhera!”

UFAFANUZI

Amesema: Kila kitu ni chenye kuinyenyekea adhama ya Mungu (s.w.t), na kila kitu huwa kwa kumtegemea Yeye, na hii ndio sifa Yake makh’susi. Yaani: Kuwa Yu ajitosha si muhitaji kutoka kwa chochote, wala hakuna kitu miongoni mwa vitu kinachojitosha bila Yeye asilan.

Imekuja (khabari) katika athari kuwa: Mwenye kujitukuza kupitia asiyekuwa Mungu huwa dhalili. Na mwenye kujikithirisha kupitia asiyekuwa Mungu huwa mchache; Na ilikuwa inasemwa: ‘Si fakiri mwenye kujitosheleza kwa Mungu.’

Na Al-Hasan amesema: ‘Ajabu ilioje kwa Lutu Nabii wa Mungu! Amesema: “Laiti ningelikuwa na nguvu juu yenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu”. (11:80) (kwa kujiun- ga na mtu mwenye nguvu aninusuru dhidi yenu) (au nikimbilie kwenye sehemu yenye nguvu). Je wamuona ametaka uimara zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko wa Mungu!?

Na wanachuoni wametolea dalili kuthibiti kuwepo kwa Muumba (s.w.t) kutokana na yaliojulishwa na maana ya kauli yake(a.s) : “Ni kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo,” hiyo ni kwa sababu nyoyo katika hali yake ya dhahiri hukimbilia kurejea kwa muumba wao wakati wa shida na majanga.

Je humuoni mpanda chombo pindi mawimbi yanapochafuka ni vipi anavyomsihi Yeye (swt): “Na inapokufikieni taabu katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu”. (17:67).

Kisha akasema(a.s) : “Mweye kusema hulisikia tamko lake, na mwenye kunyamaza yuajua siri yake,” yaani yeye hujua yaliyo dhahiri na yaliyojificha.

Kisha akasema: ‘wa man aasha fa alayhi rizquhu, waman maata fa ilayhi munqalabuhu,’ yaani Yeye ndiye mratibu wa ya duniani na ya akhera, na Ndiye Mtoa hukumu wa sehemu zote mbili.

Amesema(a.s) : “Macho hayajapata kukuona hata yaweze kueleza khabari zako, kama ambavyo mtu huelezea kuhusu aliyoyaona, lakini Wewe huna mwanzo wala mwisho, Ulikuwapo kabla ya waelezaji wa kueleza habari Zako”.

SWALI : Kuna kupingana kati ya haya mambo mawili, je haiwezekani awe yupo (s.w.t) kabla ya wasifiaji wa kueleza khabari zake, pamwe na hali hiyo awe aonwa na macho akishawaumba viumbe, kisha wawe wanamsifu au kumuelezea hali wakimuona wazi wazi kwa macho!

JIBU : Kuna kupingana kwa dhahiri, nako ni: Ikiwa Yeye (s.w.t) ni wa milele na sio wa kimwili, yaani Mungu dhati yake sio kitu cha kimwili na wala sio mfano wa kiwa au kiumbe miongoni mwa viumbe visivyokuwa mwili – incorporeal - (mfano wa akili wepesi na uzito) na ambacho si mwili wala- incorporeal, ni muhali kuonwa, kwa hiyo ni muhali kueleza kumhusu kwa njia ya kumuona.

NA SEHEMU YA KHUTBA KUHUSU MALAIKA

“Ewe Allah! Umewafanya malaika wakae ndani ya mbingu Zako, na ume- wanyanyua juu mbali na ardhi Yako, wao ndio wakujuao mno katika viumbe Wako, na wakuogopao mno, na walio karibu mno na Wewe; Wao hawajakaa viunoni, wala kubebwa na matumbo ya uzazi, na hawakuumbwa kwa maji duni.

Na wala hawakutawanywa na shaka ya matukio ya wakati, na wao wana nafasi na daraja Kwako, na mkusanyiko wa upendo wao ni kwa ajili Yako, na kukithiri utii wao Kwako, na kutokughafilika na amri Yako. Lau wangeainisha uhalisi wa yaliyofichika kwao kutoka Kwako, wangezihakiri aamali zao, na wangejibeza wenyewe, na wangetambua kuwa hawajakuabudu ukweli wa kukuabudu, na hawajakutii ukweli wa kukutii Wewe.

Utukufu ni Wako, Muumba na mwabudiwa! Kwa uzuri wa balaa lako ulipoumba[291] , umeumba nyumba (Jannah) na umejaalia humo dhifa: kinywaji na chakula, wanawake na wahudumu, makasri na mito, mashamba na matunda; hatimaye ulimtuma mlinganiaji analingania huko (Yaani Nabii).

Mlinganiaji hakuitikiwa wala uliyo wapendezesha hawakuyapenda wala hawakuwa na shauku na uliyowatia shauku. Waliuelekea mzoga (mzoga hapa yakusudia dunia), ambao walifedheheshwa kwa kuula.

Na waliungana kuupenda, mwenye kukiashki kitu hupofusha macho yake, na kuufanya moyo wake uwe mgonjwa, kwa hiyo yuangalia kwa jicho ele, na yuasikia kwa sikio lisilosikia, kupenda kumeirarua akili yake, na dunia imeufisha moyo wake, hali nafsi yake imehuzunika kwa ajili yake, kwa hiyo yeye ni mtumwa wa dunia, na mtumwa wa ambaye mkononi mwake mna kitu kutokana nayo, itelezeako naye yuatelezea, ielekeako naye yuaelekea. Haonyeki na muonyaji kwa amri yeyote kutoka kwa Mungu, na wala hawaidhiki na mtoa waadhi yeyote, naye awaona waliochukuliwa na ghururi, kuwa hawana batilisho wala rejea.”

KUHUSU KIFO

“Limewafika walilokuwa wakilipuuza, nalo ni kuiacha dunia kumewajia (dunia) ambayo waliifanya iko salama kwao, na wamekifikia akhera kile ambacho walikuwa wanaahidiwa, yaliyowafika hayaelezeki, yamejikusanya kwao mawili: Uchungu wa kifo, na huzuni ya kuiacha (dunia), viungo vyao vya miili vimelegea kwa (mauti), rangi zao zimebadilika (kwa mauti), hatimae kifo kilizidi kuwaingia, mtu anazuilika mbali na uwezo wake wa kutamka, naye yupo kati ya ahali yake akiangaza kwa macho yake, na asikia kwa masikio yake, akili yake ikiwa sahihi, uelewa wake umebaki, anafikiri katika ambayo umri wake ameumaliza, na katika alivyoupeleka muda wake! Yu-akumbuka mali alizozikusanya, aliufumbia macho utafutaji wake[292] .

Ameyachukuwa (mali) kwa njia ya halali na kwa njia yenye utata[293] hivyo sasa imemkabili dhambi ya jinsi alivyoikusanya, na amekaribia kuiacha, nayo (mali) yabaki kwa watakaobakia nyuma yake wananeemeka nayo na kustarehe nayo, kwa hiyo kheri na anasa (ya alichochuma) itakuwa ya wengine si yake yeye, na uzito (wa dhambi) utakuwa juu ya mgongo wake.

Mtu amekuwa rehani[294] , hivyo yeye anauma vidole vyake akijuta kwa yaliyomdhihirikia wakati wa mauti miongo- ni mwa mambo yake, na atakuwa hapendi ambalo alikuwa analipenda siku za umri wake, na atakuwa anatamani kuwa ambaye alikuwa akimhusudu kwa ajili ya mali na kumuonea wivu, angeihodhi yeye badala yake yeye mwenyewe.

Mauti yangali yanamwingia kwa kasi mwilini mwake, mpaka ulimi wake uwe umechukuliwa na umauti kama masikio yake, yupo kati ya ahali zake hawezi kuongea kwa ulimi wake, wala kusikia kwa masikio yake, yuazungusha macho yake nyusoni mwao, akiona mtikisiko wa ndimi zao, lakini hasikii wanayojibishana. Kisha umauti utazidi kumkaba na kuyashika macho yake kama ulivyoshika masikio yake, na roho itatoka mwilini mwake, na kuwa mzoga mbele ya Ah’li zake, na ahali zake wameingiwa na ukiwa, wakiwa wamefadhaishwa naye, na wanajiweka mbali naye, hamfurahishi mliaji, wala kumjibu mwitaji. Kisha watambeba mpaka kwenye mwanandani ardhini, na kumkabidhi humo kwenye matendo yake, na kukata ziyara yake (kuwa hawaendi kumzuru).”.

KIYAMA

“Mpaka Kitabu kifikie muda wake, na amri makadirio yake, na kukutan- ishwa viumbe wa mwisho na wa mwanzo, na itakuja amri ya Mungu apendavyo katika kuwafanya upya viumbe Wake, ataiyumbisha mbingu na kuichana, na ataitikisa ardhi na kuitetemesha, na kuin’goa milima yake na kuivunja vunja, na kwa haiba ya utukufu Wake itagongana yenyewe kwa yenyewe, na kwa hofu ya ukali wake, na atawatoa nje walio ndani yake (ya makaburi), na atawafanya upya baada ya kwisha kwao (kuchakaa kwao).

Na kuwakusanya baada ya kutawanyika kwao, kisha atawapambanua[295] kwa ajili ya kutaka kuwauliza kuhusu amali zilizojficha, na matendo yaliyofichikana, na amewafanya makundi mawili: Hili moja alineemesha na hili la pili analiadhibu.

Ama watiifu atawalipa thawabu ya kuwa karibu Yake, na kuwafanya wa kudumu ndani ya nyumba yake, kiasi kwamba wafikao humo hawatotoka, wala hali haitowabadilisha, wala hawatofikiwa na hofu, wala hawatopatwa na magonjwa, wala hawatopatwa na hatari, wala kusumbuliwa na safari kwa kuwatowa sehemu hadi nyingine.

Ama watenda maasi atawakaribisha kwenye nyumba ya shari mno, na kuwafunga mikono shingoni, na kuzifunga nywele za utosi na nyayo za miguu, na kuwavisha kanzu za lami na vazi la moto, watakuwa katika adhabu ya moto uliokolea, na mlango uliowagubika wahusika wake, katika moto wenye ukali na sauti, na mwale umulikao, na wenye ukelele wa nguvu na wa kutisha, wakaao humo hawatoki, mateka wake hawakom- bolewi kwa fidia, pingu zake hazikatwi. Ile nyumba haina muda kiasi cha kuwa muda ukifika itakwisha, wala muda uliopangwa kwa wale watu hata ufikie mwisho.”

SEHEMU YA KHUTBA IMUELEZAYO NABII (S.A.W.W)

“Aliidharau dunia na kuiona duni na kuidogesha, aliona dunia haina thamani na akaidharau, na alijua kuwa Mungu (s.w.t) amemuepusha nayo kwa hiyari yake(s.a.w.w) na ameikunjua kwa wengine ili kuwadharau. Hivyo basi alijiepusha nayo kwa moyo wake, na kufisha utajo wake katika nafsi yake, na alipenda mapambo yake yatoweke mbali na macho yake, ili asichukue kutoka humo vazi la fakhari, au awe anatarajia humo nafasi, amefikisha kwa niaba ya Mola wake Mlezi akitoa udhuru[296] , na alitoa nasaha kwa umma wake akionya, na alilingania pepo akibashiri, na alihofisha moto kwa kuhadharisha.”

AHLUL-BAYT

“Sisi ni mti wa unabii, na mashukio ya risala, na mapishano ya malaika[297] , na chimbuko la elimu[298] , na chemchemu za hukumu, mwenye kutunusuru na kutupenda atakuwa anangoja rehema, na adui yetu mwenye kutuchukia anangojea adhabu[299] .

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

110 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ibn Shu’ba ameieleza katika Tuhful-Uqul, uk. 104. Na al-Barqi katika al-Mahasin, uk. 233.

HUMO ANAELEZEA FARADHI ZA UISLAMU:

“Kwa hakika jambo bora ambalo wanaweza kulifanya wasila kwa Mungu (s.w.t), wafanyao wasila ni kumwamini Yeye na Mjumbe Wake, na jihadi katika njia Yake, kwa kweli hicho ni kilele cha uislamu.

Na neno la ikhlasi kwa kuwa hiyo ni fit’ra; na kutekeleza wajibu wa sala kwa kuwa hiyo ni mila; na kutoa Zaka kwa kuwa hiyo ni faradhi ya wajibu, na kufunga mwezi wa Ramadhani hiyo ni kinga ya kutoadhibiwa; na kuhiji Nyumba na kuiendea kwa ibada ya Umra kwa kuwa mawili hayo yanaondoa ufakiri na yanaosha dhambi; na kuunga udugu kwa kuwa hilo lakithirisha mali na linarefusha umri. Na sadaka ya siri kwa kuwa hilo lasitiri kosa[300] .

Na sadaka ya wazi wazi kwa kuwa hilo linazuia kifo kiovu; na matendo mema kwa kuwa yanazuia kuangukia kwenye fedheha.

Kithirisheni kumtaja Mungu kwa kuwa ni utajo mwema, na yafanyieni raghba ambayo (s.w.t) amewaahidi wachamungu kwa kuwa ahadi Yake ni ahadi ya kweli mno, na ongokeni kwa kufuata mwongozo wa Nabii wenu kwa kuwa hiyo ni sera iliyo bora[301] .

Fuateni Sunna zake kwa kuwa ni mwongozo bora mno, na jielimisheni Qur’ani kwa kuwa hayo ni maongezi mema mno, na jitahidini kuifahamu kwa kuwa ni kheri ya nyoyo, na jitibuni kwa nuru yake kwa kuwa Qur’ani ni tiba ya vifua, na isomeni vyema kwa kuwa hiyo ni visa vyenye manufaa mno.

Kwa hakika mjuzi atendaye kinyume na ujuzi wake ni kama jahili aliyechanganyikiwa ambaye hang’amui kutokana na ujahili wake, bali hoja dhidi yake ni kubwa mno, na majuto yatamlazimu mno[302] , na yeye kwa Mungu ni mlaumiwa mno[303] .

MAELEZO

Ametaja(a.s) vitu vinane vyote ni wajibu.Cha kwanza: Kumwamini Mungu na Mtume Wake. Na anakusudia neno imani hapa ni: Kusadiki kutupu moyoni, kwa kuweka kando yasiyokuwa hayo kwa mfano kutam- ka shahada, na matendo ya wajibu, na kuacha mabaya. Na madhehebu ya kundi miongoni mwa wanafalsafa wa itikadi za Kiislamu wamesema kuwa: Kiini cha imani ni: Kusadiki moyoni pekee; na hilo ijapokuwa si madhehebu ya sahibu zetu, wao wangesema: Kuwa Amirul-Mu’minina(a.s) amelileta tamko hili kwa mujibu wa asli ya uwekaji wa kilugha; kwa kuwa imani katika asili ya lugha ni kusadiki. Amesema (s.w.t):

“Wa maa anta bimuuminin Lana walaw kunnaa sadiqiina” - Na wewe hutuamini ijapokuwa tunasema kweli; (12:17), yaani hautotusadiki; tuwe waongo au wakweli. Na kuleta kwake (a.s) tamko hili kwa mujibu wa uwekaji wake kilugha hakubatilishi madhehebu yetu kuhusiana na kinachoitwa imani; kwa kuwa sisi madhehebu yetu ni kuwa sheria imepanua maana ya tamko hili kwa tamko lingine, kama ambavyo madhehebu yetu kuhusu Sala na Zaka na yasiyokuwa hayo mawili, hivyo basi hakuna kinachopingana kati ya madhehebu yetu na alilolileta Amirul- Mu’miniina(a.s) .

La pili ni: Jihadi katika njia ya Mungu.

Tatu; Tamko la ikhlasi; yaani: Ash’hadu an laa ilaaha illa llahu wa ash’hadu ana Muhammadar-Rasulu’llah.

Na amesema: Hilo ni umbo; yaani ndilo ambalo watu amewaumba kwalo; na asili yake ni neno la kwanza, kwa kuwa ni tawhiid, na kwa hilo ndio watu wameumbwa kwalo.

Nne: Kudumisha Swala.

Tano: Kutoa zaka.

Sita: Kufunga saumu ya mwezi wa Ramadhani

Saba: Hija na Umra,

Nane: Kuunga udugu, nako ni wajibu, na kuutelekeza ni haramu, amese- ma: “Kwa leta mali na kuikithirisha.”.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s) Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

70 - NA AMESEMA(A.S)

Na Amesema(a.s) - Ibn Sa’ad ameielezea ndani ya at-Tabaqat, Jz. 3, uk. 36, na Al’Qaaliy ndani ya Dhaylul’amali uk. 190, na Al’Isfahani ndani ya Maqatilu Talibiin uk.16, na Ibn Abdi Rabih ndani ya Al-Iqdul al-Farid Jz. 2, uk. 298, na wengine.

KATIKA MKESHA WA SIKU ALIYOSHAMBULIWA

“Nilipatwa na usingizi nikiwa nimekaa nikamuona Mtume wa Mungu(s.a.w.w) , nilimuuliza: ‘Ewe Mtume wa Mungu! Kupindama kulikoje na uadui ambao nimekabiliana navyo kutoka kwa umma wako!’ Akasema: ‘Wapatilize,’ Nikasema: ‘Mungu anibadilishie walio bora kuliko wao, na anibadilishe na aliye mbaya zaidi kwao kuliko mimi.[40]

Amesema Ar-Radhiy (r.a): Anakusudia kwa neno kupindama, na kwa neno mzozo, na huu ni ufasaha wa hali ya juu mno wa maneno.

71 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Al-Mufid ameielezea katika al-Irshad uk. 61, na ibn Da’abiy katika al-Ikhtiswas uk. 155, na Tabrasiy katika al-Ihtijaj Juz.1, uk. 254.

KATIKA KUWALAUMU WA-IRAQI:

“Ama baada! Enyi watu wa Iraqi, mko kama mwanamke mwenye mimba, ameshika mimba na alipotimiza upevu wa mimba akaporomosha mimba, na mumewe akafariki, kwa hiyo muda wake wa ujane ukawa mrefu, na akarithiwa na wa mbali kabisa[41] . Wallahi sijakujieni kwa hiyari; isipokuwa nilikujieni katika hali ya kusukumwa[42] .

Nimepata habari kuwa ninyi mwasema: ‘Ali anasema uwongo, Mungu (swt) akuangamizeni! Nani nimsemee uwongo? Nimuongopee Mungu? Mimi ni wa kwanza kumwamini! Au nimsemee uwongo nabii wake? Mimi ni wa kwanza kumsadiki yeye!

Hapana wallahi, lakini hiyo ni ibara ambayo mmeshindwa kuitambua maana yake[43] , hamkuwa wenye kustahiki nayo, Waylumah, ninakupimieni vipimo vya kiilimu na hikma, upimaji usio na thamani [44] ,4 lau angekuwa na chombo apime humo.” “ Na bila shaka mtajuwa habari zake baada ya muda ,” (38:88).

72 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameieleza ibn Qutayba katika Gharibul-Hadith, na Thaqafi katika al-Gharatu, na al- Qadhy al-Qadhwaiy katika as-Sahifatul-Alawiyah, uk. 3.

ALIWAELIMISHA WATU NAMNA YA KUMSALIA MTUME WA MUNGU

“Ewe Mola Wangu! mkunjuaji wa yakunjuliwayo na mhifadhi wa yahifadhiwayo, na muumba wa nyoyo katika maumbile yake ya asili, zenye taabu na mashaka na zenye maisha ya furaha, zijaalie sala zako za ziada na baraka zako zenye kuendelea juu ya Muhammad, mja wako na mjumbe wako, mhitimishaji wa yaliotangulia katika unabii[45] , na mfunguzi wa yaliojifunga[46] na mtangazaji wa haki kwa haki na mzuiaji wa mfuriko wa batili[47] na mvunjaji wa ukali wa upotovu[48] kama alivyobebeshwa akasimama kwa nguvu, akitekeleza amri Yako, mwenye kuharakia katika ridhaa Zako, si goigoi kwenda vitani, wala si dhaifu katika azimio, mwenye kufahamu wahyi Wako, mhifadhi wa wahyi Wako, mhifadhi wa amri Zako na mwenye kuzitekeleza, mpaka kupatikana haki, na akaiangaza njia kwa ababaikaye, na nyoyo zikaongozwa baada ya kuingia fitna na dhambi. Na alitekeleza dalili wazi za njia, na hukumu zenye nuru.

Hivyo yeye ni muaminifu Kwako mwenye kuaminiwa, na mhifadhi wa ilimu Yako iliyo mahsusi, na shahidi Wako Siku ya Hukumu[49] .

Yeye ni mtumishi Wako wa kweli, na Mtume wako kwa viumbe. Oh, Ewe Mola Wangu! Mpanulie nafasi katika kivuli chako[50] , na umlipe kheri ya ziada katika fadhila Zako. Umnyanyulie daraja jengo lake[51] , na ikirimu daraja yake Kwako[52] , mtimizie nuru yake, mlipe akutakalo ushahidi unaokubalika, na usemi unaoridhiwa, muadilifu wa mantiki, na hutba pambanuzi.

Oh Ewe Mola wangu! Kusanya kati yetu na yeye tuwe katika maisha baridi na neema tulivu ya kudumu[53] , na kutosheka na yatakiwayo, na ladha ya utashi, maisha ya raha, utulivu wa akili, na tunu za heshima.[54] ”.

73 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE (A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Ibn Sa’ad ameieleza sehemu ya maneno haya katika Tabaqat, Jz. 1, na al-Baladhuliy kati- ka al-Ansab, uk. 361.

ALIMWAMBIA MARWAN BIN AL-HAKAM HUKO BASRA

“Walisema: Marwan bin Al-Hakamu alitekwa siku ya Jamal na aliwasihi Hasan na Husain wamuombee kwa Amirul-Mu’minina(a.s) . Nao walisema naye kuhusu suala lake, naye (Amirul’Mu’minina) alimwacha huru. Walimwambia (wasemaji ni Hasan na Huseni): Akuba’i ewe Amirul- Mu’minina.Akasema(a.s) :

“Kwani hakunifanyia bai’a baada ya kuuliwa Uthman? Sina haja ya bai’a yake! Kwa kuwa huo ni mkono wa kiyahudi[55] , lau anifanyie bai’a kwa mkono wake angenisaliti kwa tako lake[56] . Ila tu yeye Marwan atakuwa na uamiri wa muda mfupi kama vile mbwa anavyoramba pua yake[57] . Na yeye ni baba wa maraisi wanne wa kaumu[58] .

Umma utapata siku nyekundu kutoka kwake na kwa wanawe.[59] ”.

74 - NA KATIKA USEMI WAKE(A.S)

WALIPOAZIMIA KUMFANYIA BAI’A UTHMAN

“Kwa kweli mnajua kuwa mimi ni mwenye haki nao (ukhalifa) zaidi kuliko mwingine yeyote asiye kuwa mimi; na wallahi nitamwachia (Uthman) maadamu kumwachia mambo ya waislamu yatakuwa katika amani na dhulma haitokuwa isipokuwa kwangu tu[60] , nikitaraji ujira wa hilo na fadhila zake, na kujiweka mbali na mnachoshindania na kujiweka kando na kuyafikia mapambo yake ambayo mnagombania.”

75 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE (A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Ibn al-Athir ameieleza katika an-Nihayah katika mada ya Qirzu.

ALIPOPATA HABARI KUWA BANI UMAYYAH WANAMTUHUMU KUSHIRIKI DAMU YA UTHMAN

“Je Bani Umayyah kunijua kwao hakujawazuia kuniaibisha? Je kutangulia kwangu (kuukubali uislamu) hakujawaweka mbali wajinga na kunituhumu? Kwa kweli aliyowaonya Mungu amewaonya kwa ufasaha zaidi kuliko ulimi wangu, mimi ni mtoa hoja dhidi ya watokao nje ya dini, na ni hasimu wa wavunjao ahadi na wenye shaka[61] , na kwenye Kitabu cha Mungu.

Kwa Kitabu cha Mungu hupimwa yasiyo wazi[62] . Kulingana na yaliyo mioyoni waja watalipwa.” Anaikusudia kauli yake (s.w.t) “Hadhani khasmani ikh’taswamu fii Rabbihim” (22:19).

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

76 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ameyaeleza hayo al-Haraniy katika at-Tuhaf, uk. 150, na ibn Shakir katika Uyunul- Hikami wal mawa’idh, na Zamakhshari katika Rabiul-Abrar Jz. 1, uk. 231, na al-Hisriy katika Zuhurul-Adabi, Jz. 1, uk. 42.

KUHUSU ZUHUDI

“Mungu amrehemu mtu aliyeisikia hukumu akaihifadhi na kuielewa, na aitwapo kwenye mwongozo akausogelea[63] , na amfuata kiongozi (kwa kushika mkanda wake wa kiunoni) na akaokoka, akajihadhari na Mola wake Mlezi, na kuhofia dhambi zake, akatanguliza ikhlas na kutenda mema, akachuma na kupata hazina, na akajiepusha na yaliyohadharishwa. Na akalenga lengo, na kufanikiwa kupata kitu mbadala, akaukabili utashi wake, na kuyakadhibisha matumaini yake (bandia), na akaifanya subira kuwa ndio njia yake ya uwokovu, na taqwa kuwa ndio masurufu ya kifo chake. Akapita njia ya haki, kwa mwenendo wa kiadilifu, na akijiambatanisha na njia ya hali ya juu ya ukweli, na kuutumia vyema wakati wake, na kuuharakia mwisho (wake), na akaenda na akiba ya matendo mema.”.

77- NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Al’Isfahaniy ameielzea usemi huu ndani ya ‘Al-Aghaaniy’ Juz. 11, uk. 29, na Al-Azhariy ndani ya ‘Tah’dhiibi-lughah’ Juz. 15, uk. 27.

KUWAHUSU BANI UMAYYAH

“Kwa kweli Bani Umayyah wananiruhusu kiasi kidogo cha mirathi ya Muhammad(s.a.w.w) . Wallahi endapo nitabaki nitawapuliza mpulizo wa muuza nyama apulizapo mnofu wa nyama ulioenea mchanga!”

Maelezo

Ar-Radhiy (r.a) amesema: Na yaelezwa kwa tamko nayo iko katika hali ya kugeuza, kwa sababu ukweli ni kama ilivyokuwa katika riwaya ya kwanza, sio kwa kuwa hilo halina maana, kwa hiyo hii yakusudiwa riwaya iliyogeuzwa.

Na kauli yake(a.s) (Layufawiqunaniy) yaani wananipa kutoka mali ya (Muhammad) kitu kidogo sawa na mkamo mmoja wa maziwa ya ngamia. Na wid-hamu at-taribatu: ni udongo, ni wingi wa neno wadhamatu, nacho ni kipande cha tumbo au cha ini kilichoanguka na kutapakaa vumbi hupulizwa.

78 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) - Al-Jaahidhwu ameueleza mwisho wa du’a hii katika al-Miatu al-Mukhtaratu.

ALIKUWA AKIOMBA KWA DUA HII:

“Ewe Mungu wangu! Nisamehe ambayo wewe wayajua zaidi kuliko mimi, endapo nitarudia nirejelee kwa msamaha. Ewe Mungu Wangu! Nisamehe kwa niliyoyaahidi nafsini mwangu, na wala hukuuona utekelezaji wake kwangu[64] .

Ewe Mungu Wangu! nisamehe niliyojikurubisha nayo kwako kwa ulimi wangu, halafu moyo wangu ukawa kinyume nayo[65] . Ewe Mungu Wangu! nisamehe na mikonyezo, na maneno ya ovyo, na usahaulifu wa moyo na mtelezo wa ulimi.”

79 - NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Ibrahim ibn Hasan ibn Dizili ameieleza katika kitabu Swiffiin, na Saduq katika kitabu Uyunul-Akhbar ar-Ridha, Jz. uk. 138.

Aliwaambia baadhi ya sahaba zake alipokuwa ameazimia kufanya msafara kukabiliana na Khawarij. Na (mmoja wa sahaba zake) alimwambia: “Ewe Amirul-Mu’minina ukifanya safari katika wakati huu nahofia hautofanikiwa mradi wako kwa mujibu wa ilimu ya nyota.” Akasema(a.s) :

“Wadhani kuwa wewe unaelekeza saa ambazo mwenye kufanya safari katika saa hizo ataepushwa na jambo baya, na unahofisha saa ambazo mwenye kusafiri humo atakumbwa na jambo la madhara? Hivyo basi mwenye kukusadiki kwa hilo atakuwa ameikadhibisha Qur’ani, na atakuwa amejitosheleza hatohitaji kuomba msaada kwa Mungu ili kuyapata yapendwayo na kujikinga na makruhu; kwa kauli yako hii wamtaka atakeye itendea kazi amri yako akumiminie shukrani wewe sio Mola wake, kwa kuwa wewe - kwa dhana zako - ndiye uliye muongoza saa ambazo kwazo amepata manufaa, na ataepukana na madhana.”

Kisha Aliwaelekea Watu(a.s) Akasema:

“Enyi watu! Jihadharini na kujifunza elimu ya falaki isipokuwa kiasi cha kupata mwongozo, bara au baharini[66] , kwa kuwa hiyo (falaki) inaitia kwenye ukuhani, na mwanafalaki ni sawa na kuhani, na kuhani ni kama mchawi[67] , na mchawi ni sawa na kafiri na kafiri (marejeo yake) ni motoni. Safirini kwa jina la Mungu.”

80 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Baada Ya Vita Vya Jamal (Ngamia) Katika Kuwalaumu Wanawake

“Enyi watu, kwa hakika wanawake ni wapungufu wa imani[68] , wapungufu wa hisa, wapungufu wa akili. Ama kuhusu upungufu wao wa imani ni kule kubaki kwao bila sala na saumu siku zao za hedhi. Ama upungufu wao wa akili ni kule kuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanaume mmoja. Ama upungufu wao wa hisa ni kule kuwa mirathi zao ziko nusu ya mirathi za wanaume. “Hivyo basi zicheleeni shari za wanawake na jihadharini na walio wa kheri miongoni mwao, wala msiwape tamaa katika jema ili wasiwe na tama katika jambo la munkari.[69]

Sibti ibn Jauzi ameieleza katika at-Tadhkira uk. 85, na ameieleza baadhi yake Abu Talib al-Makki katika Fautul- Qulub, Jz. 1, uk. 282.

81- NA MIONGONI MWA MANENO YAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Maneno Yake(a.s) - Saduq ameieleza katika Ma’anil-Akhbar, uk. 251, na katika al-Khisal, Jz. 1, uk. 11, na al- Barkiy katika al-Mahasin, uk. 234.

KUHUSU ZUHUDI (KUTOTILIA MANANI RAHA YA DUNIA)

“Enyi watu! Zuhudi ni kupunguza matumaini[70] ,na kushukuru neema[71] , na kuogopa kujiingiza kwenye haramu[72] , na endapo hilo likiwa mbali kwenu basi haramu isiishinde subira zenu[73] ,wala msisahau shukrani kwenye neema, Mungu amemaliza udhuru kwenu [74] ,5 kwa hoja zilizo wazi, na vitabu vilivyo na udhuru wa wazi.”.

82 - NA MIONGONI MWA SEMI ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Semi Zake(a.s) Sharifu ar-Radhiy amesema: ‘Nasema: Mzingatiaji akizingatia kauli yake(a.s) : “Atakayeizingatia itampa mwanga” chini yake atakuta maana ya ajabu, na lengo la mbali, lisilofikiwa upeo wake wala hakifikiwi kina chake hasa hasa ikilinganishwa na kauli yake: “Atakayeikodolea macho itampofusha” kwani yeye atakuta tofauti wazi yenye mwanga na ajabu kubwa kati ya “Atakayeizingatia” na “Atakayeikodolea macho”. Salawatul-llahi wasalamuhu alayhi.’

KUHUSU DUNIA NA WATU WAKE

“Nieleze nini kuhusu dunia hii ambayo mwanzo wake ni taabu, na mwisho wake ni kuharibika. Ya halali yake yatakuwa na hesabu, na ya haramu yake yatakuwa na adhabu. Awaye tajiri humo (duniani) hukabiliwa na fitna. Na maskini humo yu ahuzunika. Mwenye kuipenda sana huikosa[75] ,na mwenye kuitupilia mbali humwelekea[76] .

Atakayeizingatia itampa mwanga, na atakayeikodolea macho itampofusha.[77] ”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

83 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ibn Shu’uba ameieleza katika ‘Tuhaful’uquli’ uk. 146; Na Al-Qaadhi Al-Qudhaiy katika mlango wa tatu wa kitabu ‘Dasturu maalimil’Hukm’ uk. 59; Na Abu Na’im katika ‘Al’hilya’ Juz. 1, uk. 77; Na Al-Amidiy katika ‘Ghurarul’hukam.’

NAYO NI MIONGONI MWA KHUTBA ZA AJABU, NA HUITWA ‘AL-GHARRAAU’:

“Ninamhimidi Allah (s.w.t) ambaye amekuwa na daraja ya juu kwa nguvu Zake[78] , na amekurubia kwa fadhila Zake[79] , Mtoaji wa kila faida na fadhila, na muondoaji wa kila kubwa na dhiki. Ninamhimidi kwa ajili ya huruma na ukarimu Wake, na uwingi wa neema Zake. Na ninamwamini kwa kuwa ni wa mwanzo Aliye dhahiri[80] , na ninamuomba mwongozo kwa kuwa yu karibu mwongozaji.

Na ninamuomba msaada kwa kuwa ni mshindi mwenye nguvu. Na ninamtegemea kwa kuwa ni mtoshelezaji, mnusuru. Na ninashuhudia kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni mja Wake na Mtume Wake, amemtuma ili kutekeleza amri yake, na kumaliza udhuru wake[81] , na kutoa maonyo yake[82] .

“Nakuusieni! Enyi waja wa Mungu kumcha Mungu ambaye amekufanyiyeni mifano[83] , na amekuwekeeni wakati maalumu wa maisha, na amekuvikeni riyasha (yaani vazi)[84] ,na ameyafaharisha maisha yenu[85] na kuyaboresha, na amekuzungukeni kwa hesabu[86] ,na amekuandalieni malipo, na amekutunukieni neema nyingi na takrima kwa wasaa. Amekuonyeni kwa hoja za wazi bainifu.

Amekufanyeni kwa idadi, na amekuainishieni muda, ndani ya nyumba ya balaa na mtihani, na kwenye nyumba ya mazingatio ninyi ni wenye kufanyiwa mtihani humo, nanyi mtahesabiwa matendo yenu.”

KUTAHADHARISHWA NA DUNIA

“Kwa kweli dunia kinywaji chake kimetibuka, chanzo chake kina udongo na tope. Mandhari yake yanavutia, na yanaangamiza.

Ni yenye kudanganya na kutoweka, na ni mwanga utowekao haraka na kivuli kipitacho, na ni nguzo iliyoelemea upande, mpaka anayeichukia aanzapo kuifurahia, na mwenye kuichukia aanzapo kuwa na matumaini, punde yainua miguu yake na kuirudisha chini na kumnasa mwanadamu kwa kamba yake, na kumuuwa pale pale kwa mishale yake, na kumfunga mtu[87] , shingoni kamba ya kifo ikimuongoza kwenye malalo yaliobana (yaani kaburi), na marejeo ya upweke, na kuainisha mahali[88] - na thawabu za Aamali[89] .

Na hivyo hivyo waliokuja nyuma baada ya waliotangulia, kifo hakikomi kuziondoa nafsi, wala waliobakia hawakomi kutenda dhambi. Watafuatia mfano wao- (mfano wa waliotangulia katika matendo).

Wanapita kwa makundi mpaka upeo wa mwisho, na mwisho wa mambo, mpaka mambo yatakapokatika, dahari zitakapopita, na kukaribia kufufuka, Mungu atawatoa nje kutoka makaburini, na viota vya ndege, na maficho ya wanyama wakali, na katikati ya maangamizi.

Wataharakia kwenye amri Yake, wakienda haraka kuelekea maeneo yalioandaliwa kwa marejeo yao ya mwisho makundi kwa makundi, wakiwa kimya, hali wamesimama safu kwa safu, wakiwa katika kuonwa na Mungu wakiwa mahali mwitaji aweza kuwaita wamsikie.

Wakiwa na vazi la unyonge, wakifunikwa na unyenyekevu na udhalili, hila imekwisha, matumaini yamekatika, nyoyo zikiwa hazina furaha[90] , sauti zikiwa zimedhoofu, hafifu, na jasho limekuwa kama hatamu[91] , hofu imekuwa kubwa, na masikio yatakabiliwa na radi, kwa kelele ya sauti ya mfanya daawa, akiwaita kwenda kwenye upitishwaji wa maamuzi, na kupata malipo mbadala adhabu na kupata thawabu.[92] ”.

KUWATANABAHISHA VIUMBE

“Waja wenye kuumbwa kwa uwezo, na wamemilikiwa kwa kahari[93] , na mamlaka, na watakufa kwa kuhudhuriwa na Malaika wachukuaji roho[94] , na watawekwa kaburini, na hatimaye kuwa mifupa iliyochakaa, na watafufuliwa (kila mtu) pweke[95] , na watalipwa malipo, na watafanyiwa hisabu kila mtu na yake[96] walipewa muda wa kujiepusha[97] , na waliongozwa njia ya wazi[98] , na waliruhusiwa kuishi na muda wa kutafuta maridhawa, na wameondolewa giza la shaka, na wameachwa kwenye medani ya mashindano ya farasi[99] , na kuachwa wafikiri na kutafuta yahitajiwayo kwa mazingatio, kuwa na uvumilivu wa mtafutaji, anayejaribu kukipata kilichompotea, katika muda wa harakati za kazi kabla ya ajali.”

UBORA WA KUKUMBUSHA

“Mifano muwafaka ilioje na mawaidha yaponyayo! endapo yangeafikiana na nyoyo safi, na masikio sikivu, na rai zenye azma na akili thabiti!

“Mcheni Mungu uchaji wa mwenye kusikiliza na akanyenyekea, na atendapo ovu yu-atambua, na akiogopa hutenda yaliyo sawa, akiwa na hadhari huharakia kwenye mema, akiwa na yakini hufanya mema, akipewa mazingatio mara kadhaa huzingatia, akitahadharishwa hujihadhari, akikaripiwa hukaripika, aitwapo na wito wa mlinganiaji (kwa Mungu) hurejea kwake.

Arejeapo hutubu, na akifuata hufanya vizuri, akionyeshwa njia ya sawa huiona na yu aharakia akitafuta, na kuokoka mbio! na yuafaidika na mali, na kuwa na tabia njema, na kuyajenga marejeo, na akabeba masurufu mgongoni kwa ajili ya siku ya kuondoka kwake, na akaelekea njia aikusudiayo na hali ya haja yake, na mahali pa mahitaji yake, na kutanguliza mbele yake kwa ajili ya nyumba ya kubaki kwake.

Hivyo basi mcheni Mungu, enyi waja wa Mungu kwa upande wa lengo alilokuumbieni[100] , na mjihadhari upeo wa kujihadhari na ambayo amekuhadharisheni nafsi yake[101] , na kuweni wastahiki wa ambayo amekuandalieni[102] , kwa kutekeleza ya wajibu[103] , na kujihadhari na marejeo yake yanayotisha.”

Na Sehemu Hii Ya Khutba Kuwakumbusha Watu Neema Za Mungu

“Amekujaalieni masikio ili muweze kufahamu na kuyahifadhi aliyoyakusudia, na macho ili muweze kutandua tandabui ya giza giza, na viungo vya mwili vyenye kuwemo ndanimwe viungo vingine, na vyenye kulingana na umbo la mahali khusika katika muundo wa sura zake, na muda wa umri wao, na miili yenye kutekeleza manufaa yake, na nyoyo ambazo zimeshughulika kutafuta chakula chake, ndani ya neema zake zilizo funi- ka, na yawajibishayo upaji wake, na vizuizi vya afya yake[104] .

“Amekukadirieni umri aliousitiri mbali na (uelewa wenu) amekubakishieni mabaki ya athari za waliopita kabla yenu, ili iwe mwongozo kwenu, watu hao walistarehe na hisa zao kubwa, kwa nafasi bila ya kizuizi[105] .

Kifo kiliwachukua bila kufikia matumaini yao, (kifo) kiliwakata na kuwa’ngoa mbali nayo - matumaini - hawakujiandaa wakati miili iko salama, wala hawakuzingatia mwanzoni mwa umri wa ujana. Je wenye ngozi laini ya ujana wanangoja mpaka kupinda migongo kwa uzee!

Na ambao wana siha njema wanangoja kufikiwa na hali mbaya ya siha! Na walio na muda wa kubaki wanangoja mpaka uishe, pamoja na ukaribu wa kutoweka, na mbabaiko wa kutoweka, na kufikiwa na huzuni moyoni, na kusongwa na mate, na hofu ya mgonjwa na uchungu wa huzuni, na mbinyo wa mate.

Muda utafika wa kuomba nusra ya wajukuu na ndugu wa karibu, wapenzi na wenzi. Je! Ndugu wa karibu wamezuia, au vilio vimeleta nafuu!

Ameachwa mahali pa wafu amefungika, na kwenye malalo yaliyombana akiwa mpweke, wadudu wameirarua ngozi yake, na matukio yameuchakaza upya wake, na dhoruba itakuwa imefuta athari zake, na tukio litakuwa limefuta dalili zake, na miili itakuwa imehiliki baada ya kujaa kwake, na mifupa itakuwa imeoza baada ya nguvu zake, na nyoyo zitakuwa zimefungika kwa uzito wa mizigo (dhambi) yao, zitakuwa na yakini na habari zake zilizojificha, hazitotakiwa baada ya hapo kuzidisha Aamali zake njema[106] wala hazitoombwa kutubia kwa ajili ya ubaya wa kuteleza kwake![107] .

Je! Hamko wana wa kaumu hii, na mababa zao, ndugu na jamaa zao wa karibu? Mnafuata mifano yao na kuiga njia zao[108] na mwaenda njia zao, nyoyo ziko bado ngumu, zimeghafilika mbali na mwongozo wake, zaenda njia isiyokusudiwa! Kama kwamba mkusudiwa ni mwingine, kama kwamba mwongozo upo katika kukusanya dunia yake.”

HADHARI YA KITISHO CHA AS-SIIRAAT

“Na juweni kuwa mtapaswa kuvuka juu ya as-Siiraat nyayo zitateleza kiasi cha kumtupa mtu chini, na vitisho vya utelezi wake na mfululizo wa vitisho vyake.

Basi mcheni Mungu enyi waja wa Mungu uchaji wa mwenye akili, ambaye fikra zimeushughulisha moyo wake, na hofu imeutaabisha mwili wake, na sala ya tahadjudi imemfanya akeshe, na matumaini yamembakisha na kiu nusu ya mchana wa siku yake, (yaani anafunga mchana wake) na zuhudu imezuia matamanio yake, na dhikr ya Mungu imeufanya ulimi wake kuwa mwepesi, na ametanguliza hofu kwa ajili ya amani yake[109] akajiepusha njia zilizo kombo kwa kufuata iliyo sawa, kwa ajili ya iliyo sawa, yu afuata njia iliyonyooka zaidi ili kuifikia njia ihitajiwayo; wala geuzo la ghururi halikugeuza fikra yake, wala mkanganyiko wa mambo haukumfanya asijue ukweli.

Akiwa katika hali ya furaha kwa bishara ya kufaulu neema ya maisha mema, katika neema kubwa ya usingizi wake, na siku yake yenye amani mno.

Akiwa amevuka kivuko cha hii haraka (dunia) mwenye kuhimidiwa[110] , na akiwa ametanguliza masurufu ya baadaye akiwa na furaha, na ameharakia kutoka kwenye woga[111] na akakaza mwendo katika muda wa uhai[112] na akapenda kipaswacho, na kukiepuka kinachobidi, katika siku yake akaichunga kesho yake, na akaangalia yanayokuja mbele miongoni mwa a’amali, yaani akaangalia atakachokitanguliza miongoni mwa aamali.

Yatosha pepo kuwa ni malipo mema na mafanikio, na moto ni adhabu tosha na mateso, Mungu (s.w.t) ni mlipizaji tosha na mnusuru! Na Kitabu (Qur’ani)[113] ni hoja tosha na hasimu.

“Nakuusieni kumcha Mungu ambaye hakuacha udhuru kwa aliyoyaonya, na ametoa udhuru kwa onyo lake wazi[114] , amekutahadharisheni na adui aingiae vifuani kwa kificho[115] , na kupulizia masikioni kwa siri, kwa njia hiyo, amepotosha na kufanya uharibifu.

Atoa ahadi ya uwongo na kuyapamba maovu, na kudharau madhambi makubwa yaangamizayo, mpaka anapomporomosha kutoka daraja ya mwongozo mwenzi wake[116] , naye atastahiki rehani yake, atakuwa yuakanusha aliyokuwa akiyapamba, na kuyakuza aliyokuwa akiyadharau, na kuyatahadharisha aliyokuwa akiyafanya yako salama.”

MIONGONI MWAYO MAELEZO YA KUUMBWA MWANADAMU

“Au mwangalie mwanadamu ambaye Mungu amemuumba ndani ya giza la mfuko wa uzazi na mifuniko ya sitara, ikibubujikiwa na manii, kisha likafanyika pande la damu lisilo na sura, baada ya hapo mimba, halafu kitoto kichanga kinyonyacho, kisha mtoto, baada ya hapo kijana, kisha amemtunukia moyo wenye kumbukumbu, ulimi wa kunenea, na macho yakuonea, ili aweze kufahamu na kuzingatia, apate kuacha kutenda maovu akijiziwia (kwa nguvu za mazingatio) afikiapo utu uzima, na kufikia kimo chake cha kawaida, na umbo lake kufikia kimo chake.

Akanusha kwa kiburi, aingiwa na ghururi na kubabaika bila kujali. Aijaza ndoo kubwa ya matamanio yake, afanya juhudi kukamilisha utashi wa dunia yake, katika matamanio yake, akienda na yanayomdhihirikia katika utashi wake. Kisha hakuogopa uovu wowote, wala kutishika wala kuwa na wasiwasi. Alikufa ndani ya maovu yake hali yukijana aliyeghurika. Aliishi akiwa makosani kwa muda mfupi. Hakufaidika na thawabu mbadala. Wala hakutekeleza wajibu wowote. Maradhi mabaya yalimkabili akiwa bado na ukaidi wake katika njia ya furaha yake kubwa, na alipitisha usiku akiwa kama amelewa[117] .

Alikesha akiwa katika shida ya majonzi na machungu, kufikiwa na uchungu na magonjwa, kati ya ndugu na ndugu wa damu, na baba mwenye huruma, na mama anayelia akisema: ole wangu mwenye huzuni, dada apigaye kifua akiwa amefadhaika; na mtu yu katika sakarati ya mauti anataabika na shida ya kukatisha tamaa, na mvuto wa kuchukiza, na msukumo wa sakarati ya mauti.

Kisha yuatiwa ndani ya sanda akiwa mublisa[118] mwenye kukata tamaa ya rehema ya Mungu avutwa kwa urahisi[119] , kisha kutiwa ndani ya jeneza akiwa mwenye machovu ya kutupwa, na aliyekondeshwa na ugonjwa.

Akibebwa na wasaidizi vijana, na ndugu wasaidizi wambeba wakimpeleka kwenye nyumba yake ya upweke na na watu huacha kumzuru[120] , na mahali pa upweke, mpaka wanaporudi waliokuwa wakimsindikiza na akarejea wenye huzuni, atakalishwa shimoni mwake akisemeshwa[121] kwa faragha maswali ya kuduwaza, na mtihani wa kujikwaa.

Na balaa kubwa mno huko ni kuingia maji ya moto na kuteseka na Jahannam, na kutokota kwa moto, na ukali wa sauti ya moto, hakuna muda wa mapumziko, wala wa raha, wala nguvu ya kuzuia wala kifo cha kutuliza, wala usingizi wa kuliwaza, atakuwa kati ya aina mbalimbali za maiti[122] , na adhabu za kila wakati na saa zote! Hakika tunajilinda na Mungu.

Enyi waja wa Mungu! Wako wapi ambao walipewa umri mrefu na kuneemeshwa! Walijulishwa na wakafahamu, na walipewa muda na wakaupoteza bure[123] , walikuwa salama na wakasahau, walipewa muda mrefu wa maisha, waliumbwa kwa sura nzuri, walitahadharishwa machungu, waliahidiwa makubwa! Jihadharini na dhambi zinazoangamiza, na aibu zikasirishazo.

Enyi wenye macho na masikio na afya na mali! Je kuna upenyo! Au epuko, au kimbilio, au marejeo (yaani kurejea hapa duniani) au hapana? “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?” (6:95) “Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62)

Au mwaghurika na nini! Hali ikiwa mmoja wenu hisa yake ya ardhi yenye urefu na upana ni kadiri ya urefu wake, mwenye kugusishwa shavu lake na mchanga (yaani maiti azikwapo ni sunna shavu lake ligusishwe mchanga kwa kuiondoa sanda aliyovikwa eneo la shavu lake).

Enyi waja wa Mungu! ni hivi sasa hali kamba haijakaza shingoni[124] , na roho zimeachwa katika wakati wa kutaka mwongozo, hali miili iko na raha, na ukumbi wa kujikusanya[125] , na muda wa maisha upo na mwanzo wa muda wa utashi [126] ,49 kuna nafasi ya kufanya toba, na nafasi ya wakati wa haja kabla ya shida, dhiki, hofu, na kubanwa, na kabla ya kuja mauti yanayongojewa na kabla ya shiko la Mwenye nguvu Muweza (s.w.t).”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

84 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KATIKA KUMUELEZEA AMRU IBNUL-A’AS

“Namshangaa ibn An-Nabighah! eti asema akiwa kati ya watu wa Syria (Sham) kuwa mimi ni mtu wa mzaha, na kuwa mimi ni mtu wa mchezo mwingi, najishughulisha na mieleka na kupigana na watu. Amesema batili na ametamka akiwa na dhambi.

Angalieni, (maneno ya uovu mno ni uwongo) naye yuasema na yuadanganya, anaahidi na yuaenda kinyume, anaomba kwa kung’ang’ania[127] na akiombwa yuafanya ubakhili, anavunja ahadi, na anaukata udugu. Awapo vitani yeye ni mkemeaji na muamrishaji!.

Hapo ni ikiwa panga hazijachukua nafasi yake, na zikichukua nafasi yake, ujanja wake mkubwa ni kuwaonyesha maadui zake utupu wake. Ama mimi wallahi kukumbuka mauti kwanizuia kufanya mzaha, na kwa kweli yeye kimzuiacho kusema kweli ni kuisahau akhera, kwa hakika yeye hakumpa bai’a Muawiya mpaka alipompa sharti ya kupewa kitu.[128] ”.

85 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - al-Wasitiy ameitaja katika Uyunul-Hikami wal Mawa’idhy, na Ibn Sibt Jauziy katika Tadhkiratul-Khawa’is uk. 131.

KATIKA KUMWADHIMISHA MWENYEZI MUNGU NA KUMTUKUZA

“Na ninashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah swt. peke Yake, hana mshirika, ni wa milele (bila mwanzo) alikuwa yupo wakati hapakuwa na kitu kingine, na ataendelea kuwepo baada ya kutoweka kwa kila kitu, Yeye hana kikomo. Dhana haiambui kumpata na sifa, wala nyoyo haziwezi kumuelewa kwa aina, wala hapatwi na ufanywaji wa sehemu sehemu wala kufanywa kwa mfano kwamba hii ni baadhi ya sehemu ya Mungu. Hazungukwi na uoni wa macho na wa nyoyo.[129] ”.

NA SEHEMU YAKE NYINGINE (YA KHUTBA) KUIELEZEA PEPO

“Tabaka zinazo zidiana, na daraja zinazo tafautiana, neema zake hazikati- ki, atakayedumu humo hatozeeka, wala mkazi wake hatokuwa fakiri.”.

86 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ad-Dainuriy ameitaja katika al-Akhbar at-Twiwalu uk. 145; na ibn Shu’ba katika Tuhaful- Uqul uk. 100, na al-Barqi katika al-Mahasimu uk. 233.

KUHUSU WAADHI WA KUJIANDAA KWA AJILI YA ULIMWENGU MWINGINE NA KUFUATA AMRI ZA MUNGU

“Amezijua siri, na habari ndani ya dhamiri, yuakizunguka kila kitu, na mwenye kukishinda kila kitu, na mwenye nguvu juu ya kila kitu. Basi mtendaji miongoni mwenu na atende ndani ya muda wa (uhai) wake kabla ya kukabiliwa na ajali yake. Na atende wakati wa wasaa kabla ya kushughulishwa kwake, na wakati wa nafasi yake kabla hajashikwa koo[130] .

Ajiandae kwa ajili ya nafsi yake na safari yake, na aandae masurufu kutoka kwenye nyumba ya kituo chake (cha muda) kwa ajili ya nyumba ya kudumu kwake.

Mkumbukeni Mungu swt. enyi watu, kwa aliyokutakeni ndani ya Kitabu chake kuyazingatia, na haki Zake alizozihifadhi humo, kwa kuwa Mungu (s.w.t) hajakuumbeni bure, na wala hajawaacheni bila ya faida, wala hajawaacha katika ujinga wala upofu. Amepandisha daraja ya athari zenu, na amejua amali zenu, na ameamua ajali zenu.

Na amekuteremshieni Kitabu kinachobainisha kila kitu, na amemrefushia umri nabii Wake kwa zama ndefu, kiasi cha kumkamilishia yeye na ninyi ujumbe - aliouteremsha Kitabuni mwake - ambao ni dini Yake ambayo ameiridhia nafsini Mwake; na amebainisha kwenu - kupitia ulimi wake - matendo mema na mabaya, makatazo Yake na amri Zake, na ameweka mbele yenu hoja Yake na kuondoa udhuru kwenu, amekukemeeni na kuwaonya na adhabu kali. Hivyo basi zidirikini siku zenu zilizobaki, na zifanyeni nafsi zenu zivumilie humo. Kwa kuwa ni chache katika siku nyingi ambazo mnakuwa katika mghafala, na kutotilia manani mawaidha, msiuachie muda, utawawekeni katika njia ya madhalimu, na msijipendekeze, kwa kuwa kujipendekeza kutawasukumeni kwenye maasi.

Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli mnasihi mzuri mno wa nafsi yake katika watu ni yule mtii mno wa Mola Wake[131] ; Na kwa kweli mwenye kuighushi mno nafsi yake ni muasi sana wa Mola Wake[132] ; na mwenye kupunjwa ni yule ambaye ameipunja nafsi yake, na mwenye kutamani mfano wa hali ileile[133] ni yule ambaye dini yake iko salama, na mwenye furaha ni mweye kuwaidhika na mtu mwingine, na dhalili ni mwenye kuhadaika na utashi wa nafsi yake na kughurika kwake. Jueni kwamba kuwepo kwa kiasi kidogo cha riya’a[134] - ni ushirikina, na kukaa na watu wanaofuata matamanio ya nafsi zao - hawaa - yaliyoko nje ya maadili ya kisharia - kunasahaulisha imani, na ni mahudhurio ya Shetani.

Jiepusheni na uwongo, kwa kuwa ukando na imani. Mkweli yu ukingoni mwa wokovu na heshima, na muongo yuko katika kilele cha kuanguka na kudharauliwa. Msihusudiane, kwa kuwa husuda huila imani kama moto ulavyo kuni.

Msibughudhiane, kwa kuwa huko ni kwenye kufuta imani[135] ; na jueni kwa mba kuwa na matumaini mno - kunaisahaulisha akili na kumbukumbu[136] . Basi yakidhibisheni matumaini kwa kuwa ni ghururi, na mwenye nayo ameghurika.”

87 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Zamakhshari ameieleza katika Rabiul-Abrar mlango wa al-izzu

wa sharaf.

KUHUSU AMPENDAYE MUNGU MTUKUFU

“Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli miongoni mwa waja wapendwao mno na Mungu ni mja ambaye Mungu amemsaidia kupambana na nafsi yake, akawa yuaifanya huzuni ni shi’aru yake - vazi la ndani[137] , na amevaa joho la hofu, kwa hiyo taa ya mwongozo ikaangaza moyoni mwake, na aka andaa takrima kwa ajili ya siku yake atakayofikia, kwa hivyo akasogeza kwa ajili yake kilicho mbali, na akapoza makali ya shida[138] , ameangalia akatambua, akakumbuka na akakithirisha[139] .

Alipoza kiu kwa maji baridi aliyorahisishiwa maendeo yake, akanywa na kutosheka. Akapita njia iliyosawa, akiwa amevua vazi la matamanio, na kujiepusha na mahangaiko ya moyo, isipokuwa hangaiko moja pekee amebaki nalo[140] , kwa hiyo akawa ametoka na kuwa mbali na sifa za upofu, na mbali na kushirikiana na watu wa matamanio, hivyo akawa miongoni mwa funguo za milango ya uongofu, na vifungio vya milango ya kuangamia.

Ameiona njia yake na akaipita njia hiyo, na akaijua miongozo yake, akaivuka bahari yenye maji mengi iangamizayo, na akashikamana na kishiko kwa umadhubuti, na miongoni mwa kamba iliyo ngumu mno, kwa hiyo yeye kwenye yakini yu kama mwanga wa jua, ameisimamisha nafsi yake kwa ajili ya Mungu (s.w.t) katika mambo ya hali ya juu kabisa; kwa kulikabili kila limfikalo, na kuchukua kila hatua ihitajiwayo kwa hilo, na kulirudisha kila tawi kwenye shina lake[141] .

Ni taa ya giza jingi, mfichuaji wa upofu, ni ufunguo wa yaliyofumbika, mzuiaji wa shida, mwongozaji wa jangwani, akisema yuafahamisha, akinyamaza husalimika.

Amekuwa na ikhlasi kwa Mungu naye akamfanya makh’susi kwa ajili Yake, hivyo yeye ni chimbuko la dini Yake, na vigingi vya ardhi Yake. Amejiambatanisha binafsi na uadilifu, na ukawa uadilifu wake wa kwanza kujiondolea utashi wa kibinafsi.

Anaielezea haki na anaitendea kazi, haachi lengo la kheri ila atalikusudia, wala padhaniwapo kheri ila atapaendea. Amekishika Kitabu hatamu zake[142] nacho ndio kiongozi wake na Imamu wake. Anashuka pale ambapo kinapoifikisha mizigo yake[143] , na anateremka mahali pake pakufikia.”

SIFA ZA MTU FAASIQI

“Na mwingine amejiita mwanachuo hali akiwa si mwanachuo[144] , amedondoa dhana za kijahili kutoka kwa majaahili, na upotovu kutoka wapotovu, na amewategea watu mtego uliotengenezwa kwa kamba ya udanganyifu, na maneno ya uwongo; anakichukuwa Kitabu-Qur’an - kwa maoni yake; na ukweli ameupindisha kulingana na utashi wake binafsi.

Anawafanya watu wajione wako salama watendapo makosa ya jinai, na hulichukua kosa kubwa kama ni kitu chepesi, anasema: ‘Nasita kwenye mambo yasiyo wazi,’ na humo yuajiingiza; na anasema: ‘najiepusha mbali na bid’a,’ na punde amejiingiza humo. Hivyo basi sura yake ni ya mtu, na moyo ni moyo wa mnyama, hajui mlango wa uongofu ili aufuate, wala mlango wa upotofu ili aufunge akiwa mbali nao, na huo ni umauti wa walio hai. “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?” (6:95) “Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62).

Na alama zipo[145] , Na aya ziko wazi, na minara imesimamishwa[146] ,mnapotezewa wapi! na vipi mnakuwa vipovu na kati yenu kuna itrah ya Nabii wenu![147] Nao ndio hatamu za ukweli[148] , na ni alama ya dini, na ndimi za ukweli! Hivyo wawekeni daraja nzuri mno ya Qur’an[149] , na muwaendee mwendo wa ngamia walio na kiu[150] . “Enyi watu! Chukueni kutoka kwa Khatamun-Nabiyina - hitimisho la Manabii(s.a.w.w) : (Kwa hakika hufa afaye katika sisi na wala si mfu[151] , na huoza aliyeoza katika sisi wala hakuoza) hivyo basi msiseme msiyoyatambua, kwa hakika ukweli mwingi upo katika myakanushayo[152] .

Kubalini udhuru wa msiye na hoja dhidi yake - naye ndimi - je sikuifanyia kazi kwenu thiq’lu kubwa![153] Na ninaiacha kwenu thiq’lu ndogo? Na nikasimika katika nyinyi bendera ya imani, na nimekusimasheni kwenye mipaka ya halali na haramu, na nikakuvisheni afya kutokana na uadilifu wangu, na nimekukukunjulieni mema kwa kauli yangu na vitendo vyangu, na nimekuonyesheni tabia njema za hali ya juu kutoka kwangu mimi mwenyewe binafsi. Hivyo msitumie rai katika ambayo hakifikiwi kina chake na macho, wala fikra haziingii.[154]

Na Sehemu Ya Khutba Hii Kuwahusu Bani Umayyah:

“Mpaka atadhania mwenye kudhani kuwa dunia imefungwa aqal, kwa Bani Umayyah, yawapa kheri zake[155] , na kuwaongoza kwenye chemchemi safi za manyweo yake, na wala ummah huu hautaondolewa mjeledi wala upanga wake, na atakuwa ameongopa adhaniaye hivyo. Bali hilo ni tone la maisha ya ladha[156] (watalila kwa muda kisha watalitema lote).”.

88 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - al-Kailaniy ameieleza katika ar-Raudhwa uk.62, na Sheikh al-Mufiidu katika ar-Rishadu uk.173, na Ibn Athir amezitafsiri (hadith) ghariib katika an-Nihaya mada ya Azalu.

KATIKA KUELEZEA MAKOSA WALIYONAYO WATU

“Amma ba’ad. Kwa kweli Mungu hakupata kumuangamiza dhalimu wa zama fulani katu isipokuwa baada ya kumpa fursa na raha, wala hakuuganga mfupa wa yeyote katika wana umma isipokuwa baada ya dhiki na shida, na hakuwakabili kwa misiba na shida juu yao hata kwa kiasi kidogo kuliko ambacho kitawafikeni au tayari kimewafikeni, kinatosha kuwa somo. Wala sio kila mwenye moyo ni mwerevu, wala sio kila sikio ni sikivu, wala sio kila aangaliaye ni mwenye kuona.

Ajabu ilioje! Nitakuwaje nisistaajabishwe na makosa ya vikundi hivi kwa tafauti za hoja zao katika dini yao! Hawafuati athari ya Nabii (wao) wala hawaongoki na matendo ya waswii, wala hawaamini ghaibu, wala hawajiepushi na jambo la aibu, wanatenda katika mambo yanayoshakiwa, na wanakwenda na matamanio.

Kwa wao jema ni lile wanalolipenda wao, na ovu kwao ni walikataalo[157] , kimbilio lao katika matatizo ni kwao wenyewe binafsi, mategemeo yao katika mambo yanayoshakiwa ni rai zao. Kama kwamba kila mmoja ni imamu wa nafsi yake[158] , amejiamulia ayadhaniayo kuwa ndiyo tegemeo, na ni sababu thabiti.”.


3

4

5

6