MOTO NA PEPO

MOTO NA PEPO0%

MOTO NA PEPO Mwandishi:
: D.RAIHANI YASINI
Kundi: Misingi mikuu ya Dini

MOTO NA PEPO

Mwandishi: AMIR ALY DATOO
: D.RAIHANI YASINI
Kundi:

Matembeleo: 9521
Pakua: 3911

Maelezo zaidi:

MOTO NA PEPO
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 8 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9521 / Pakua: 3911
Kiwango Kiwango Kiwango
MOTO NA PEPO

MOTO NA PEPO

Mwandishi:
Swahili

4. Kuteketeza na kufuja Neema za Allah swt

Yaani kutokutumia yema na ipasavyo neema za Allah swt alizomjaalia mwanadamu ziwe katika hali ya siha yake, watoto au mali. Ama mali ni kule kutumia kupita kiasi kinachohitajika au kutumia visivyo muhimu.

5. Kunkatalia mume kujamiiiana

Kunawahi kutokea mara nyingi miongoni mwa watu kuwa mume anapohitaji kujamiiana na mke wake, mke humyima mume wake tendo hilo la kutimiza haja yake. Kwa hapa mwanamke kama huyu ndiye anatishio kubwa la adhabu kali za kaburini.

6. Kupuuzia na kudharau Sala

Sisi tunatabia ya kupuuzia na kuidharau Sala tano za siku na zinginenezo zilizofaradhishwa. Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , "Yeyote yule anayeipuuzia Sala, si miongoni mwetu." Na vile vile amesema: "Mtu kama huyo hatapata nusura yetu Siku ya Qiyama."

Vile vile Al-Imam Musa al-Kadhim(a.s) amesema kuwa baba yake mzazi Al-Imam Ja'afar as-Sadiq(a.s) amesema, "Wakati wake wa mwisho, alimwambia kuwa 'mtu yeyote anayeipuuzia Sala basi hatapata nusura zetu Siku ya Qiyama."

7. Kuwatetea wadhulumiwa

Mara nyingi tunaona kuwa wadhalimu wanawadhulumu watu wengine na sisi katika hali kama hiyo tukibakia kimya bila ya kujaribu kuwatetea hao wanaodhulumiwa, basi hivyo ndivyo itakuwa ndivyo sababu yetu ya kuadhibiwa kaburini.

8. Kuwasengenya watu wengine

Siku hizi tumekuwa na tabia moja ya kujiburudisha na yo ni kuandaa mabaraza ya kukaa na kuwakejeli na kuwasengenya watu, kuchimbua aibu zao na kuongezea chumvi na pilipili katika maneno yetu ili kunogesha hadithi zetu. Tunasahau kuwa kufanya hivi sisi tunamharibia jina na sifa za mtu ambaye labda hakuyafanya hayo.

2. SABABU ZA KUPUNGUZWA KWA ADHABU ZA KABURINI

Kama vile tulivyokwisha kuona kuwa zipo sababu zinazosababisha adhabu za kaburini basi tusife moyo kuwa hakuna njia ya kupunguzwa au kuwa hafifu. La, si hivyo, daima zipo sababu za kupunguziwa adhabu hizo za kaburini na vile vile hali yetu ikawa njema zaidi humo kaburini.

1. SALA ZA TAHAJJUDI AU SALATIL LAYL

Inambidi mtu asali sala raka'a nane za salatil Layl na raka'a mbili za shufa'a na raka'a moja ya witri ambamo katika qunuti yake kunasomwa Astagh firullah wa atubu Ilaihi mara sabini.

Basi zipo Ahadith zinazosadikiwa hususan kutokea kwa Al-Imam 'Ali ar-Ridha(a.s) katika maudhui Kuhusu Kaburi kwamba: "Iwapo mja anasali raka'a nane za salatil Layl na raka'a mbili za shufa'a na raka'a moja ya witri ambamo katika qunuti yake kunasomwa Astagh firullah wa atubu Ilaihi mara sabini, basi hatakosa faida zake kama zifuatazo, atakuwa amepona fishar-i-kabr na ataepukana na Moto wa Jahannam, umri wake utakuwa mrefu, Allah swt ataongezea baraka katika riziqi yake ."[4]

2. KUTEKELEZA RUKUU NA SUJUDA KWA USAHIHI KATIKA SALA

Kwa mtu ambaye anasali sala zake vile ipasavyo, basi hatakuwa na sababu ya kujibiringita kama kwamba anafanya mazoezi ya mwili, kumbe masikini anasali. Tunawaona wengi sana wakisali lakini kwa mbio kama kwamba wanashindana na katika hali kama hii hata usomaji na matamshi pia hayawezi kamwe kuwa sahihi. Tunasali ilimradi tu tumesali, sasa sala hiyo inamaana yoyote mbele ya Allah swt?

3. KUSALI SALA ZILIZO SUNNAH NA KUTOA SADAQAH

Tunasisitizwa mno kutimiza Sala zilizofaradhishwa na vile vile tupate muda wa kusali zilizo Sunnah na vile vile kusoma Dua kidogo na vyote hivyo kwa unyenyekevu na kwa moyo uliotulia. Sambamba na hayo tutoe sadaqah kuwasaidi masikini ambavyo kuna faida kwa pande zote mbili.

4. KUSALI SALA YA WAHSHAT

Anapokufa Mumiin basi inatubidi kusali sala hiyo usiku wa kwanza kuzikwa kwake kwani inamsaidia maiti huyo na vile vile iwapo tutawasalia wengine basi Allah swt atatujaalia watu wa kutusalia pale tutakapokufa ili nasi tufaidike na thawabu hizo ambazo zitatupunguzia adahabu zetu,

5. KWENDA MAKKAH KWA AJILI YA KUHIJI

Inatubidi sisi katika maisha yetu kwa mara moja kwenda Kuhiji, lakini kwa kutimiza masharti ya amri hiyo. Na tuwe na moyo kwa ajili ya hivyo. Wapo watu wengi ambao wanapuuzia swala hili ambalo ni faradhi kwao.

6. KIFO KATIKA USIKU WA KUAMKIA IJUMAA AU SIKU YA IJUMAA

Iwapo mtu atabahatika kufa katika usiku wa kuamkia Ijumaa au siku yenyewe ya Ijumaa, basi adhabu za kaburini zitapungua. Sisi hatutambui fadhila na Baraka za usiku huu na siku ya Ijumaa katika maisha yetu. Lau mtu atafanya utafiti kujua zaidi basi atashangaa kusikia au kusoma fadhila na baraka zake.

7. JARIRATAIN

Wakati wa kumzika maiti huwekewa matawi mawili yalio mabichi. Inasemekana kuwa mtu huyo hatakuwa na adhabu za kaburi kwa kipidi cha kubakia ubichi ka matawi hayo.

8. KUMWAGIA MAJI JUU YA KABURI

Ipo riwaya kuwa kwa kumwagia maji juu ya kaburi kutamfanya mtu huyo aliyezikwa humo asipate adhabu za kaburini hadi hapo kutapokauka maji juu ya kaburi hilo.

9. KUSOMWA KWA SURAH MAALUM ZA QUR'AN TUKUFU

Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) amesema kuwa , "Mtu yeyote atakayesoma Surah Al-Hakumu Takathur atapona adhabu za kaburi." Na vile vile Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) amesema kuwa "Yeyote atakayeisoma Surah al-Nisaa kila siku ya Ijumaa basi huyo atapona adhabu za kaburi . "[5]

Na Al-Imam Ja'afar as-Sadiq(a.s) amesema kuwa, "Mtu yeyote atakayesoma Surah al- Qalam, hatapata adhabu za kaburini." Na vile vile iwapo atasma Sura Zukhruf au kusomwa kwa Sura al-Ya-Sin (ambayo inajulikana kama ndiyo moyo wa Qur'an Tukufu) ama wakati wa magharibi au usiku kabla ya kulala, hatapata adhabu za kaburi."

Vile vile kusomwa kwa Ayah za mwisho katika Surah al-Baqarah, kutamwepusha na adhabu za kaburi, Ayah zenyewe ni:

Rabbana la tuakhidhna in nasina au akhta'ana. Rabbana wala tuhamilna 'alayna isran kama hamaltahu 'alal ladhina min qablina Rabbana wala tuhammilna ma la taqatalana bihi wa'afu 'anna waghfirlana warhamna anta Mawlana fansurna 'alal qawmil kafiriin.

10. KUUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH SWT

Iwapo mtu atafariki akiwa katika njia ya Allah swt kama katika vita , basi mtu huyo hana adhabu ya kaburi. Na hivyo ndivyoamesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah Ali-Imran , Ayah 169 – 170.

yaani ni kwamba wale wanaouawa katika njia ya Allah swt si watu waliokufa bali ni mashahidi na wapo hai.

11. KUMSALIA MTUME MUHAMMAD MUSTAFA (S.A.W.W) NA AHLUL BAYT(A.S)

Na kwa kumsalia Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) pamoja Ahl ul-Bayti(a.s) kwa wingi kutamwepusha mtu na adhabu za kaburini.

Vile vile ipo katika riwaya kuwa mtu yeyote aanzaye dua yake kwa Bismillahir Rahmanir Rahiim na Salawati (Allahumma Salli 'ala Muhammadin wa Ale (ahali) Muhammad ) na kumalizia kwa Salawati, basi kamwe dua yake hiyo haitarudishwa kwani salawati inakubaliwa na Allah swt. Sasa itawezekanaje mwanzo wa dua na mwisho wa dua vikakubaliwa na vya katikati vikatupiliwa mbali?

12. MAPENZI YA AHLUL BAYT(a.s)

Tunaelewa waziwazi vile fadhila za Ahlul Bayt(a.s) zilivyo na vile Allah swt pamoja Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) walivyokuwa wakiwasifu hao na kutufaradhishia mapenzi yao juu yetu na hata kama salaikisaliwa bila ya kusomwa kwa salawati ndani yake basi sala hiyo itakuwa batili.

Kuwapenda Ahlul Bayt(a.s) ni kuwapenda wafuasi na marafiki zao na kuwachukia na kuwalaani maadui wao. Je itawezekanaje adui wa kiongozi na mpenzi wako akawa rafiki yako?

13. MWANAMKE KUFANYIA SUBIRA UMASIKINI NA SHIDA ZA MUME WAKE

Kwa hakika katika maisha yetu haya ya duniani kuna mambo mengi mno ambayo yanajitokeza katika maisha ya ndoa. Kuna wakati ambapo mume huwa ni masikini, hivyo inambidi mwanamke aumke kufanya subira na kustahimili shida zinazojitokeza na kumpata hima bwana wake ili sivunjike moyo bali aendelee na jitihada zake za kuondokana na umasikini. Vile vile kunawezekana kwa mume kuwa mtu mwovu ambaye hana matendo mema kama mlevi, mgomvi n.k. Katika sura zote hizo na zinginezo, inambidi mwanamke afanye subira na kujaribu kustahimili katika mazingira hayo, na wla si kuamua kumpa talaka mume au kutoroka nyumbani. (Ingawaje talaka ni neema mojawapo ya Allah swt, hivyo isitumie vibaya).

14. KUSOMA ZIYARAH YA IMAM HUSSEIN(a.s)

Imesisitizwa kuzuru kaburi la Imam Hussein(a.s) usiku wa kuamkia Ijumaa na kusoma Ziyarah. Kwa hakika sisi tukiwa mbali mno, huwa tunasoma Ziyarah ambavyo kwa hakika kutatuepusha na adhabu za kaburi.

15. KUZIKWA NAJAF

Iwapo mtu atazikwa katika maeneo yanayozunguka kaburi la Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) huko Najaf, basi hatakuwa na adhabu za kaburi.

16. Kuwasaidia masikini na wasiojiweza

Kwa kutoa misaada kwa ajili ya kuwasaidia masikini na wasiojiweza na wale wanaohitaji misaada, kwa hakika kutamwepusha mtu na adhabu za kaburi. Inawezekana mtu akatoa hivyo katika uhai wake kwa ajili ya kupata thawabu yeye mwenyewe au akatoa kwa niaba ya wale waliokwisha fariki dunia hii, basi thatwabu hizo zitawafikia hao marehemu.

Siku moja alifariki mtu mmoja katika zama za Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) ambaye alikuwa tajiri mno. Aliacha wusia kuwa mali zote zilizokuwa zimejaa mabohari yake zigawiwe sadaqah kwa masikini, baada ya kifo chake. Kwa hivyo, kwa mujibu wa wusia wake, baada ya kifo chake, mabohari yalianzwa kugawia vyakula kwa masikini. Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) alikuwepo hapo na mwishoni wakati wanapitisha ufagio, waliokota kipande cha tende moja, na kwa kuiondoa hiyo, Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) alisema, "Lau huyu mtu angalikuwa ametoa angalau hata kama mbegu moja kama hii ya tende katika uhai wake, basi mbegu moja ya tende ungali kuwa na thawabu ya mlima wa Abu Qobays (mlima mkubwa mno)."

1. SABABU ZINAZOFANYA NYOYO KUFA

Al - Imam Ja'afer as-Sadiq(a.s) amesema kuwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) amesema kuwa mambo manne husababisha nyoyo za watu kufa ambazo ni:

1.KUTENDA DHAMBI BAADA YA NYINGINE

Mwanadamu anapoanza kutenda madhambi nafsi yake inamzuia na kumtolea lawama ili asitende maovu. Lakini pindi anapoanza kukaribia madhambi, roho yake inaanza kuzoea na ile hali ya kujilaumu inaanza kupungua nguvu na hivyo ndivyo anavyojizoeza na hatimaye anahisi kuwa ni jambo la kawaida wakati wa kutenda dhambi. Kwa hivyo anatenda ovu moja na kuendelea kuyatenda mengine mengi bila ya kuhisi kuwa na dhambi na hata unafika wakati ambapo hajisikii vema hadi hapo anapokuwa ametenda madahmbi. Kwa kutoa mifano, ipo mifano mingi mno mbele yetu zilizo bayana. Mtu mmoja anapokaribia kunywa pombe, atakataa kata kata, lakini utaona akibembelezwa na kushurutishwa na marafiki zake walio waovu wenye kuwa ajaribu kidogo, na akishajaribu kidogo watamlazimisha anywe zaidi na zaidi. Na hali hii itakapoendelea bele hivi hivi, utaona mtu huyo ndiye wa kwanza kuagiza pombe na vile vile atakuwa akijiwekea nyumbani mwake. Heshima zote atakuwa amezipoteza na maovu yote yatakuwa yametundikwa shingomi mwake kwani atapoteza fedha, ataharibu siha yake, atawatukana wazazi, kaka, ndugu, majamaa na hata kuthubutu kuwapiga mke na watoto wake. Kwa kifupi familia nzima itakuwa imetumbukizwa katika janga kubwa. Huyu pamoja na pombe ataongezea dhambi lingine la kuwatafuta malaya na kuvuta bangi na madawa ya kulevya. Haya ndiyo maangamizo makubwa kabisa.

Allah swt amewaamrisha Malaika kuwa: Mtu anaponuia kutenda jambo jema wamwamdikie thawabu. Na anapoanza kutembea katika kulifanya tendo jema basi hapo pia anaongezewa thawabu nyingi na pale anapolianza kutenda tendo jema basi huongezewa zaidi ya hayo na anapomaliza kulitenda tendo jema basi hapo analipwa thawabu nyingi mno zisizo na hisabu.

Lakini mtu anaponuia kutenda dhambi basi hapo haandikiwi adhabu, na anajitoa kwenda kutenda dhambi napo pia haandikiwi kwa sababu inawezekana akarudia njiani na anapolianza tendo ovu pia kuna uwezekano wa kutolikamilisha na kwa masikitiko makubwa, anapolikamilisha basi kwa huruma zake Allah swt, huandikiwa dhambi moja tu.

2. KUONGEA ZAIDI PAMOJA NA WANAWAKE

Islam haitukatazi kuongea na wanawake wasio wake zetu lakini kinachokatazwa ni ile hali ya watu kuongea mambo ambayo yanapita mipaka na huku ndiko kunapoanza kuteketea maadili. Utawasikia watu wakizungumza pamoja na wanawake mambo ambayo hayana heshima na kufanyiana dhihaka na hatimaye wanapozoeana katika tabia hii utakuta wanaanza maneno ya kudalilisha kuwa wanapendana na wanahamu ya kuingiliana, na haya ndiyo yanayo tokea. Bwana Daud alimwusia mwanae kuwa ajiepushe na mazungumzo pamoja na wanawake kwani mwanamme anapokutana na mwanamke, katikati yao huwa yupo Sheitani kwa ajili ya kuleta madhambi.

Uislamu unamtaka mwanamke abakie katika hadhi na heshima aliyopewa na Allah swt. Hivyo mwanamke anapoongea na mwanamme inambidi asitoe sauti nyororo yenye kuvutia bali inambidi atoe sauti ambayo haitamfurahisha mwanamme na hivyo asitamani kuongea tena na mwanamke huyo. Na kwa misingi hii, mwanamme hatakiwi kumtolea salaam mwanamke ili asije akaisikia sauti yake. Lakini dunia hii imebadilika, leo katika maredio na televisheni utawaona wanawake hata wanasoma Qur'an kwa sauti za kuvutia.

Vile vile tusisahau kuwa kuwadokozea macho wanawake pia ni dhambi. Zipo zinaa za macho na midomo.

3. KUZOZANA PAMOJA NA MWEHU

Yeye atasema na wewe utasema bila ya kufikia maelewano baina yenu. Mutazozana kwa muda mrefu wakati ambapo watu watakaokuwa wakiwaona hawatajua tofauti baina yenu. Mwishoni hamtafikia jambo la kheri.

Hao ni watu ambao hawaongei katika mipaka ya ilimu, dini na adabu.

4. KUKAA PAMOJA NA WATU WALIOKUFA

Kwa kukaa na kufanya mazoea ya urafiki pamoja na watu waliopotoka, kutatufanya na sisi pia tupotee na kutumbukia katika ujeuri, majivuno na takaburi mambo ambayo Allah swt hayapendi na anyachukia na kuyaadhibu. Qur'an inatuambia kuwa nyoyo zao zina magonjwa na Allah swt anawaongezea magonjwa baada ya magonjwa kwa kutokana na maovu yao yanavyoongezeka.

Kwa hayo Waislamu walimwulizaa Mtume(s.a.w.w) Je ni wakina nani waliokufa? Mtume(s.a.w.w) aliwajibu Kwa waliokufa wanamaanishwa wale matajiri wenye takabburi na majivuno. Urafiki pamoja na watu kama hawa utakufanya wewe uwe na tamaa ya dunia na kujipatia mali ufahari na majivuno. Hao wanachokithamini ni kile kinachowaletea faida wao tu. Dharau majivuno ndiyo mavazi yao.

Hapa kuna aina nne ya watu:

(1). Wale wanaokula na kuwalisha wengine

(2) Wale wanaokula na kuwanyima wengine

(3) Wale hawali wenyewe na wala hawawapi wengine wale

(4) Wale wanaowanyan'ganya wengine ili wale peke yao.

Nasiha: Inatubidi sisi tujiepushe na mambo yote ambayo Allah swt hapendezewi na tufuate Hadithi na Sunna za Mtume(s.a.w.w) pamoja na Maimamu 12(a.s) na vile vile tufanye tawba kwa yale tuliyokwisha ya tenda katika hali ya ujahili wetu na kamwe tusirudie kuyatenda. Allah swt ndiye Mwenye kuyaona, kuyasikia na kuyafamu yote.

2. MAADILI YA ISLAM

Masomo ya akhlaq- maadili katika Islam ni mojawapo ya bora ya sayansi na inamwelekeza asomaye hadi katika elimu ya kujielewa nafsi yake mwenyewe ambayo Islam inaamini kuwa ni fardhi. Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Yeyote yule aliyeitambua nafsi yake (mwenyewe) basi hakika ametambua Allah. "

Hivyo hivyo kuna mapokezi mengi ya habari kuhusu umuhimu wa somo hili hata Mtume Mtukufu(s.a.w.w) amebainisha kuwa: "Mimi nimetumwa kuja kukamilisha maadili .

Tuanze kuzichambua aina za nafsi alizonazo mwanadamu vile alivyo:

Hapana shaka kuwa mwanadamu hana zaidi ya moja, lakini hii nafsi au roho inayo masharti fulani fulani. Kwa hiyo, hali ya kuonyesha kama 'nafsi ya kujilaumu' 'au nafsi ya kuamrisha' 'nafsi inayotosheka' (kama vile vielezwavyo katika Qu'rani), na hivyo haidhihirishi idadi ya nafsi. Upande mwingine, yote haya ni miongoni mwa ngazi za sifa ambazo zinaleta kwa ukamilifu na ustawi wa hali ya nafsi, pamoja na yale yanayoozesha nafsi na kuleta maovu.

NAFSI SAFI AU THABITI

Katika Qur'rani Tukufu, aina mbili hizo za masharti za nafsi zinaelezwa:

"Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo safi " (26:89).

Uhalisi huu ni aina ya moyo, na moyo halisi (safi) ni ule ambao haufungamani na upande wa kuhangaika wala upande ule wa wapotofu.

Imenakiliwa kutoka kwa Imamu Sadique(a.s) kuwa: "Moyo ulio msafi- halisi ni ule ambamo hakuna chochote kile ila Allhah (s.w.t) tu "

Katika hali hii, Nafsi imetunukiwa hatua mojawapo ya umuhimu kuwa kamilifu. Hivyo inamaanisha kuwa hakutakuwa na mapenzi mbali na ile ya Allhah tu.

Kuna habari nyigine iliyonakiliwa kutoka kwa Mtume Mtumfu(s.a.w.w) ambamo twaambiwa: "Imani ya mtu haitokamilika hadi hapo mimi niwe mpenzi wake kuliko hata baba yake, mama yake, watoto wake mali yake na hata kuliko maisha yake ."

Ndivyo hivyo, nafsi safi ni nafsi ambamo hakuna mapendo mengine yoyote yale isipokuwa Allah (s.w.t) na wale wapendwao kwa ajili ya Allah (Mtume na Ahali yake)

NAFSI YENYE KUTUBU

Sharti lingine la moyo au Nafsi ni 'kutubu' na hivyo huitwa moyo wenye kutubu au nafsi yenye kutubu. Hivyo huwa daima inarudi kwa Mwenyezi Mungu.

"................Na anayemuogopa (Mwenyezi Mungu Mwingi wa kurehemu, na hali ya kuwa humuoni na akaja kwa moyo ulioelekea (kwa Mwenyezi Mungu) ." (50:33).

Kuwa na khofu ya Mwenyezi Mungu pale mtu awapo peke yake ni mojawapo ya masharti bora ya nafsi, na hii ina maanisha kuwa nafsi imemtambua Allah (s.w.t) kiasi kile kuwa hakutakuwa na tofauti yoyote itakapokuwa pekee yake au katika kundi la watu. Hata kama hakutakuwa na mtu yeyote karibu nayo, basi ile khofu ya Allah (s.w.t) imo ndani yake thabiti. Hii haipo katika kundi la zile nafsi zilizo ghafilika katika maasi na matendo maovu wakiwa katika kundi la watu au wakati wengine watakapokuja julishwa, na hawatajizuia nayo na hata kama iwapo watakapopewa habari zilizo bainika. Hii ni ile aina ya nafsi ambayo haielewi kuwa Mwenyezi Mungu yupo anaangalia yote na Aliye dhahiri popote pale na kwa hakika aina hii ya nafsi haipo pamoja na Allah na wala haitorudi kamwe kwa Allah.

NAFSI MWONGOZI

Sharti lingine la nafsi ni ile iongozwayo. Qur'rani inatuambia: (64:11).

"................Anayemuamini Mwenyezi Mungu huuongoza moyo wake "

Mtu ambaye moyo wake ukiwa umeongozwa na kujitosa katika habari ya imani na sheria Tukufu za Allah (subahana wa Tala), yeye anaielewa njia yake vyema kabisa. Zile imani atakazokubalia na matendo yake yale yampasa kuyatenda huwa ni dhahiri kwake kuelewa vyote hivyo kwa uadilifu.

NAFSI ILIYO RIDHIKA

Sharti lingine lijulikanalo vyema la moyo au nafsi ni "kuridhika. Qur'an:

"Sikiliza: Kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu nyoyo hutulia . "(13:28)

Na vile vile mwishoni mwa sura al-Fajr twaabiwa (89:28)

"Ewe nafsi yenye kutua! Rudi kwa Mola wako, hali ya utaridhika......... ."

Nafsi iliyo ridhika ni ile iliyokwisha ridhika, ina maanisha kuwa mtu yupo anapigana vita vikali na matakwa yake na kwa kuyatimiza yale yaliyo fardhi kwake katika dini na kujiepusha na yale yaliyoharamishwa, na anajipa umuhimu kwa kuelimisha na kuikamilisha nafsi yake hadi hapo yeye hapindukii kutii chochote kile isipokuwa Allah (s.w.t) tu. Ni marufuku kwake kuelekea pale penye madhambi na huwa ni mwenye kupenda amani na utulivu na huwa ni mwenye kujiridhikia mwenyewe hadi hapo yeye huwa thabiti kama jabali madhubuti. Hakuna madhambi, matakwa ya ubinafsi, tamaa, mvutano wa dunia, mapenzi ya mali au cheo yatakayoweza kuja kumpotosha yeye na kumwelekeze pengine na vile vile hakuna sheitani atakayeweza mghalimu na kumpotosha yeye.

Hali ya juu kabisa ya sharti hili kama ilivyokuwa katika Mtume mtukufu(s.a.w.w) na ma - Imamu(a.s) , waliokuwa halisi kuwa hata mawazo ya kutaka kutenda madhambi hayakutokea kamwe.

AL-NAFS AL-MUTTAQI

Sifa nyigine ya nafsi inajulikana kama uangalifu wa uadilifu wa nafsi, (The virtuosly cautious self) nafsi ambayo imejaa kwa khofu na tahadhari. Hali hiyo inatokana na nyakati fulani kwa kupotoshwa na (kwa akili na roho) huzungukwa na uchafu na ubovu ili nafsi iingie sharti sawa sawa na itahadharishwe na madhambi. Nafsi ikiwa katika hali hiyo huitwa nafsi ya tahadhari ya uadilifu:-

"..............Anayezihishimu alama za (dini ya ) Mwenyezi Mungu, basi hili

ni jambo la katika utawala wa nyoyo. " (22:32)

Kwa mtu yule ambaye imani yake inafikia kiwango hiki cha "Taqwa" kiwango cha tahadhari ya uadilifu, huheshimu na kumthamini Allhah (s.w.t) na yele yote yaliyotolewa ishara nae kama Dini, Msikiti, sheriah, waumini wake Makka Ka'aba Tukufu n.k. kwa ufupi. Chochote kile kinachohusika na Mungu huwa kina kuwa na umuhimu na ta 'adhima kubwa kwa mtu kama huyu wa namna hii. Na hii ndiyo kwa hakika matokeo ya 'taqwa'

NAFSI NYENYEKEVU

Hali nyingineyo ya Nafsi ni unyenyekevu (uvumilivu), yaani humaanisha kuwa mtu mwenye nafsi hali hii huwa mnyenyekevu mbele ya maamrisho ya Allah (s.w.t)

Kwa mara nyingine tena twaambiwa katika Surah al Halj: (22:54)

"................waiamini, na ili zinyenyekee kwake nyoyo zao "

Kwa sababu nyoyo hizi hujiimamisha chini mbele ya Mungu na maamrisho yake, na wale wenye kuwa na nyoyo hizo hujiwakilisha kwa Allhah (s.w.t) hawavunji kamwe maamrisho ya Mwenyezi Mungu na wala hazisaliti au kuzipinga.

NAFSI HALISI

Aina nyigine ya nafsi ni ile nafsi au roho iliyo mtakatifu (the pure self). Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu anakula kiapo cha jua, mwezi mbingu, ardhi na vitu vingine na baadaye akisemea nafsi, anatuambia:

"Bila shaka amefaulu aliyeyeitakasa (nafsi yake) na bila shaka amejihasiri aliyeiviza (nafsi yake) " (91:9 -10).

Ni dhahiri kuwa inambidi mtu afanye jitihada ili kufikia hatua hii. Kabla ya yote yale mengineyo, nafsi lazima iwe huru kutoka sifa zote zile zilizo ovu na hapo ndipo uwanja utakuwa tayari kwakuzitambulisha sifa zilizo nzuri na bora kabisa na kwa uanzishaji na uendelezaji. Mtu ambaye nafsi yake itatakasika, basi amehakikishiwa msamaha (ukovu) na kufikia kipeo cha furaha ya milele. (The person whose self become purified is assured of salvation and bliss!).

3

MOTO NA PEPO

NAFSI YA KUKARIPIA - LAUMU

Inawezekana wakati mwingine kuwa hivyo kwa vyovyote vile na kiasi chochote kile cha madhambi ayafanyayo, mtu hajisikii chochote cha kutenda kosa, wala hasikitiki, wala hajilaumu mwenyewe. Nafsi kama hiyo ni ile iliyoshindikana. Hata hivyo, ile nafsi baada ya kuanguka na kutenda madhambi na itajikaripia yenyewe na kujishutumu yenyewe, kabla ya yeyote yule kufanya hivyo, basi imeingia katika sharti tukufu mojawapo la nafsi itakiwavyo kuwa. Qur'ani Tukufu inatuelezea:

"Naapa kwa siku ya Kiama. Tena naapa kwa nafsi inayojilaumu; (kuwa mtafufuliwa na mtalipwa) ". (75:1-2).

Ni dhahiri kuwa iwapo Mwenyezi Mungu akiapia kwa vitu, basi kuna utukufu wake humo. Nayo pia ni wazi kuwa yeyote yule aifunzae nafsi yake vyema hadi ule wakati wa kutenda madhambi, yenyewe (nafsi) hujaa masikitiko na kujilaumu, basi imefikia mojawapo ya vina vya utakatifu.

NAFSI ILIYOFUNGULIWA HERI

Sharti lingine la nafsi ni kuongozwa na Mungu. Twaambiwa kaika Qur'ani:

"Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake " (91:8)

Maongozi haya ni kutia moyo kwa nafsi wakati itapokuwa katika hali ya kutakasika- 'Nafsi halisi si' ambayo tumeishaizumgumzia. Ni lazima iwapo nafsi itaelekezwa kwa mujibu wa madhambi basi muongozo na kufunguliwa kwa heri kutoka kwa Allah (s.w.t) yatafikia kikomo chake.

Kwa kupingana na sifa na masharti ya nafsi ambazo ni sababu ya furaha ya milele na utakatifu, baadhi ambazo zimekwisha tajwa hapo awali, pia hapo hapo kuna sifa na masharti yanayosababisha maovu ya nafsi, sasa tuziangalie.

NAFSI YENYE MADHAMBI

Iwapo roho au nafsi ya mtu ikiwa na tabia ya kutenda madhambi, basi huitwa yeye madhambi. Qur'ani inazungumzia kulipa kwa amana:

"Na atakaeficha basi hakika moyo moyo wake ni wenye kuingia dhambini ."(2:283).

Hii inathibitisha kuwa nafsi ya yeyote yule ambaye ameshajizoelesha madhambi ni nzito na ni wazi na tayari kwa kutenda madhambi wakati wowote ule.

NAFSI ILIYO SINZIA

Sababu mojawapo ya kushidwa na kufifia kwa nafsi ni kulegea au kusinzia au kuwa zembe. Kwa kutenda mambo maovu na kwa kuendelea kutenda madhambi ndiko kunakosababisha nafsi kuelekea palipo paovu na kutomsikia Allah (swt). Anaelezea Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu

"Wala usiwatii wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao... " (18:28).

NAFSI ZILIZOTIWA MUHURI

Hapa inamaanisha kufungwa muhuri juu yake na hivyo ndivyo hatua ya mwisho ya kungwa, inatuambia:

"Na watakaokuwa na uzani khafifu, basi hao ndio waliozitia hasarani nafsi zao kwasababu ya kuzifanyia ujeuri Aya zetu. "

Popote pale mtu anapokuwa fidhuli au juvi kuelekea Allhah (s.w.t) hadi kudharau na kutokubali ujumbe wake na maamrisho ya Allah ambayo Mwenyezi Mungu ambazo amewekea mbele yake, au iwapo yeye atazikubalia, anazipa umuhimu kidogo na kuwa na kosa la upinzani basi hapo moyo wake unaingia katika hatua ile ambayo ni sawa na kama tahadhari, maamrisho Matukufu na yale yaliyo haramishwa hayatakuwa na athali yoyote ile kwake yeye. Na hii ni hatua mojawapo ya kudidimiza kwa nafsi na kushindwa kwake.

NAFSI ILIYO POFUKA

Hali nyingine ya Nafsi ni kupofuka. Qur'ani inatuambia kuwa:

"Kwa hakika macho hayapofuki, lakini nyonyo ambazo zimo vifuani ndizo zinapofuka. (22:46).

Nyoyo hizi zinaona vingine mbali na Allah (s.w.t) na hazimwoni Mwenyezi Mungu. Nyoyo za aina hizi huona yale tu yatakayo yenyewe bila ya kuyazingatia yale maamrisho ya Allah (s.w.t) na kwa hakika ndizo zilivyo kama vile vimepofuka tu.

NAFSI YENYE MARADHI

"Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi . " (2:10).

Ugonjwa wa aina hii inawezekana kuonekana mioyoni mwetu kwa sababu ya yale madhambi tuyafanyayo sisi siku hadi siku. Kama vile mtu mgojwa huwa hana hamu ya vyakula wala madawa ambavyo ni vyenye manufaa kwake na vile vile vyakula vizuri havitakuwa na ladha yoyote kwake, ndivyo vivyo hivyo kuhusu NAFSI iliyougua, kwani inapatikana kuonywa (na Mwenyezi Mungu) na kukaribia kwa upole kwa mapendo na matakwa yake ya humu ulimwenguni na akhera kuwa yenye adhabu kali sana na yenye kutisha mno. Kilicho zaidi ni kwamba mtu aliyeugua hivyo ni yule mwenye, kuipendelea kwa ajili ya nafsi yake yale yote yaliyo mabaya na maovu, kwani huwa avutiwa navyo kama kambwa ndivyo vyenye kumfaa yeye. Kwa hakika hii ndiyo ile nafsi ilikwisha ugua; kama vile ilivyo kifo kwa mtu hatakayetibiwa magonjwa yake na hivyo ndivyo vinaweza kutokea kwa ajili ya aina hii ya nafsi iwapo haitoweza kutibiwa kabla ya ugonjwa kuenea pote na hatimaye mtu aweza kuangamia.

Popote pale mtu aonapo kuwa yeye hatamani chochote kile atakiwacho kukifanya yaani kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika sala na kutii Sheria Tukufu za Dini ambazo hazimfai na ambazo ni chungu kwake, kwa hivyo ni wazi kabisa kuwa atambua kuwa huo moyo wake umeshaanza kuugua maradhi, na bila ya kisita inambidi afanye kila hila awezayo ili ajielekeze kwa mujibu wa aya za Qur'rani Tukufu, kwa watawa na walio waumini halisi na wale walio hodari katika elimu na ujuzi huu: waganga waa moyo, i.e.., wanavyuoni waelewao na wafuatao mienendo ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) , ili waweze kuitibu nafsi ya aina hiyo iliyopatwa na maradhi.

NAFSI INAYOKWENDA UPANDE

Moyo au Nafsi pia inaweza kusemwa kuwa inakwenda upande au inapotoka. Aina hii ya Nafsi ni ile ichaguayo upotofu wakati ipatiwapo chaguo katika hali mbili ya wema na uovu.

Kama mategemeo yote ya maisha, katika sehemu zote za Imani, maadili na matendo, mambo yake yote yaliyo dhahiri na yale yote yaliyo batili mwake, mwanadamu daima anakubwa na mgawanyiko wa njia mbili mbele yake , mtu ambaye amefaulu na kufurahika ni yule ambaye daima anachagua njia ile aitakayo Mwenyezi Mungu. I.e njia iliyo nyooka (Sirat al-Mustaqeem) ya dini katika kila hali. Hata hivyo, mtu ambaye moyo wake unampotosha, huwa daima ndiye achanguaye njia ya upotofu

Katika Qur'ani, kuzungumzia mifano na mafumbo ya aya na kwa kuelezea wazi wazi, Mwenyezi Mungu anatuambia:

"Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazobabaisha kwa kutaka kuwaharibu watu kutaka na kujua hakika yake vipi........ "(3:7).

Hivi kwa kuchagua mfano (mutashabih au allegorical) wa aya za Qur'ani ili kuitumia Qur'ani kwa kuhakikisha matakwa ya mtu binafsi ni sampuli ya ile nafsi iliyopotoka.

NAFSI YA MOYO MGUMU

Sharti lingine la nafsi kuwa hivyo ni kutokana na moyo mgumu na katili.

"...........Na tukazifanye nyoyo zao kuwa ngumu " (5:13).

"...........Kwa hivi nyoyo zao zikiwa ngumu " (57:16).

Hali kama hii inaelezewa katika aya zinginezo pia. Nyoyo kama hizi zina sifa kama zile za jiwe na chuma, kuwa hakuna chochote kile kiwezacho kuathiri au kuacha alama yoyote juu yake ila kwa mshindo mkali tu moto. Hadi kufikia hali ya moyo kuwa mgumu kiasi hiki ni dhahiri ikionekana vile maovu yalivyo mteka huyo mtu hadi akawa mtumwa wa matakwa na maovu yake. Kwa hakika imepotoka!

NAFSI WASIWASI

Nafsi ya aina hii imo katika hali hii ya wasiwasi kuhusu vile vitu iipasavyo kuvijua na kuviamini. Shaka kuhusu mizizi ya dini ya Islam kama vile kushuka kuwapo kwa Allah (s.w.t), akhera, Unabuwa na vile vile Uimamu(a.s) , na kushuku matawi ya Dini kama vile sala, saumu na mema na mengineyo mengi.

"Nyoyo zao zina shaka; kwahivyo wanasitasita kwa ajili ya shaka yao. " (9:45).

Hii ni mojawapo ya sababu ya upotofu wa Nafsi na ni fardhi kwa watu wale walio katika hali kama hii kujielekeza hadi aya za Quarani na hadithi Tufuku za Mtume(s.a.w.w) na ma -Imam(a.s) na kwa wanavyuoni wa dini ili kuweza kutokomeza hali hii kabla ya kutanda juu ya Nafsi nzima undani mwake. Ama sivyo, iwapo hali kama hii haitashughulikiwa na badala yake ikapuuzwa na kubakia Nafsini, basi itamwelekeza mtu katika hali ya kukatiza na kukataliwa (kupuuzwa na kudhoofika).

NAFSI ILIYOPATA KUTU

'KUTU' ni shida nyingineyo ambayo nafsi inaweza kupatwa kwani ni sawa na ule mfano wa kioo cha kujitazamia, iwapo ile poda itabanduka basi hutaweza kujitamazama kiooni. Basi kioo cha moyo ambavyo ni sehemu ya umuhimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu utukufu wa ukamilifu wake, fadhila zake zitamorudishwa kwake, hazitoweza rudishwa iwepo itashika kutu, na hatimaye itaweza kupoteza ile nguvu ya kupeleka ujumbe wako kwa Mwenyezi Mungu.

Ingawaje mwanadamu hawezi kumtazama Mwenyezi Mungu kwa macho yake, lakini anao uwezo wa kumwona Mwenyezi Mungu, Utukufu wake na Ukuu wake kwa kupitia NURU iliyomo katika Nafsi yake. Nafsi ile ambayo imeshakwisha shikwa na kutu ambamo sasa hakuna uwezo wa kurudishia (reflect ) kutoka na kwa Mwenyezi Mungu, basi bila shaka itatapatapa huko na huko ikimtafuta sheitani na hasa kwa mujibu wa matilaba yake. Qurani ikiwa inatumbusha kuwa:

"Sivyo hivyo! Bali yametia juu ya nyoyo zao (maovu) waliokuwa wakiyachuma. " (83:14).

Katika 'aya hii twaelezewa vyema kabisa kuwa chanzo cha kupatwa kwa kutu kwa Nafsi ni kule kutenda madhambi. Kwa hivyo kila dhambi itatupia uzito (itatanda kiza juu ya moyo; na ifikiapo hali kama hii, inambidi mtu afanye Tawba mara moja kwa ajili ya kuyasafisha hayo matendo maovu na atende matendo mema ili kuzuia kupotea kwa nuru iliyotunukiwa Nafsi yake. Vile vile, twaambiwa katika hadithi Tukufu kuwa: "Mtu mwenye furaha kuu katika siku ya Kiama ni yule atakaye yaona maneno aliyokuwa akiyatamka 'naomba msamaha wa Mwenyezi Mungu' chini ya kila dhambi alilolitenda. Kwa Hivyo inambidi kila Mwislam mmoja wetu apige msasa kila ovu alilolitenda ama sivyo, Mwenyezi Mungu azitowazo onyo zake za upole zitabadilika na kuwa ghadhabu kubwa sana.

NAFSI AMURU

Nafsi isiyofunzwa hasa wakati wa ujana wa mtu, huamuru kutendwa kwa matnedo ya madhambi bila kiasi. Katika Qurani, kuhusu kisa cha Mtume Yussuf, Nafsi inasemwa:

"Nami sijitasi Nafsi yangu; kwa hakika (kila) Nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu (12:53).

Sentensi hiyo inaonyesha kuwa ilitamkwa na Zuleikha aliyekuwa amependa Nabii Yussuf. Pale alipotoa ushahidi, alithibitisha kuwa ndiye chanzo cha uovu huo. Kwani Yussuf alikuwa hayupo wakati huo wa ushahid, lakini kwa kuwa Zuleikha alikuwa hana hila yoyote ile zidi ya Yussuf. Pia kuna uwezekano kuwa hayo yametamkwa na Yussuf au ni wote vyovyote vile, Qur'an inatuambia kuwa "Nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu. (12:53).

Nafsi yoyote ile isiyokuwa imeongozwa kwa mujibu wa mfano ya Islam, huwa daima inavutwa popote pale penye madhambi na ma'asiyah kwani yote hayo yako yamedhalilishwa kabisa. Mfano wa Nafsi hii ni sawa na mtoto mchanga atakaye kila kitu kuchezea bila kutazama ubora wake, faida au hasara zake, iliramdi yeye apate kuchezea tu, Nafsi ya yule aliye na utamaduni mzuri, aliyekomaa na kubaleghe inavutika pale penye mema na hujiepusha na matilaba yake; na ile nafsi elimishwa na inavutika pale penye maovu ya kila aina na kwa hivyo lazima ifunzwe vyema, itasaidia kutakasisha hiyo Nafsi.

HATIMAYE

Kile kilichoelezwa hapo kinasema kuwa Nafsi inaweza kuwa bora kabisa ama mbovu kabisa au vinazidiana katika vina na ngazi. Kuna nafsi zifikiapo kuitwa 'Nafsi halisi na 'Nafsi ridhika' n.k. na vile vile kuna zinapofifia hadi kufikia hali mbaya kabisa na matokeo yake ni majanga, majonzi na maovu na kufikia ile sifa ya "kupigwa mihuri" au 'zilizopofuka' na 'zenye maradhi' zikiwa ni kama mifano.

Hali hii inadhihiridha kuwa Nafsi zinapangwa na kila mtu anayo Nafsi moja tu.

JE UMEJING'AMUA UNA NAFSI YA AINA GANI?

3. DHULUMA ZA AINA TATU

Amesema al-Imam Muhammad al-Baquir(a.s

"Zipo aina tatu za dhuluma: "Aina ya kwanza ni ile ambayo Allah swt anatoa msamaha na ya pili ni ile ambayo haitolei msamaha na aina ya tatu ni ile ambayo yeye haipuuzi. "[6]

Ama dhuluma ambayo anaisamehe ni ile ambayo mtu huitenda baina yake binafsi na Allah swt. Na dhuluma ambayo Allah swt haisamehe ni kukufuru na dhuluma ambayo haipuuzii ni ile ambayo inatendewa dhidi ya haki za watu."

Ufafanuzi :

Aina ya tatu ya dhuluma ni ile ambayo mtu hukiuka na kuvunja haki za watu. Njia saheli ya kutaka kusamehewa ni kwanza kumridhisha yule ambaye haki zake zimekiukwa na kuvunjwa. Iwapo mtu huyo atamsamehe yule aliyemvunjia haki zake, basi hapo dhuluma hiyo itageuka kuwa dhuluma dhidi yake binafsi. Na hapo ndipo ataweza kuwa mstahiki wa kuomba msamaha wa Allah s.w.t.

4. MAKUNDI MANNE YA WATU

Imenakiliwa kutoka Jaafer ibn Muhammad naye kutokea Baba, naye kutokea kwa Babu yake naye kutokea kwa Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) kwamba Mtume(s.a.w.w) alisema katika wasia wake.

Alisema Mtume(s.a.w.w) "Ewe Ali! Kuna makundi manne ambamo watu wanapatikana wamegawanyika kwa mujibu wa matendo yao humu duniani . [7] .

A. KUPANDA DARAJA

1. KUTAWADHA WUDHUU KATIKA BARIDI

Kwa hakika ni jambo gumu mno kuamka na kujiweka tayari kwa ajili ya ibada za Allah swt hasa kama utakuwapo kazita sehemu ambazo kuna baridi kali ambapo hata kunakuwa na hatari ya watu wengine kuathirika kwa baridi kali. Wakati huyo unakuwa ndio wakati mzuri wa kujipatia usingizi mnono na nguvu za Shaitani zinakuwa zikitushawishi sisi tutoe visingizio mbalimbali ili mradi tusiamke na kufanya ibada za sala hususan za Alfajiri.

2. KUSUBIRI SALA BAADA YA SALA

Mumin wa kweli kwa hakika anakuwa akiusubiri wakati wa sala kuwadia kwa ajili ya kutaka kusali sala kwa mara nyingine. Fursa hii anaisubiri kwa hamu kwa sababu anapata fursa kwa mara nyingine kumwabudu na kumshukuru Allah swt na ni wakati mwema kwa ajili ya kuomba Tawba ya madhambi yake na vile vile ni wakati mwingine wa kujipatia neema na baraka za Allah swt. Kwa kifupi mumin huyoo amabye anausubiri wakati wa sala uwadie anakuwa na hamu ya kujipatia bahati ya kuweza kujiweka mbele ya Allah swt.

Tukiangalia mfano wa kidunia, iwapo mimi nitaambiwa kuwa nimepewa kibali cha kumzuru Raisi wa nchi yetu nyakati fulani fulani kwa siku. Hivyo mimi baada ya kumzuru mara ya kwanza kwa siku, nitakuwa na hamu na shauku ya kuwadia kwa muda wa mara pili na hivyo hivyo kwa mara zote. Kwa hakika nitaiona saa ikienda pole pole mno.

Na hivyo ndivyo inavyokuwa hali ya Mumin kwa ajili ya kutaka kuwa mbele ya Allah swt kwa nyakati angalau mara tano kwa siku.

3. Kutembea usiku na mchana kwa miguu kuelekea Jamaa'

Mumin kwa hakika daima hupenda kujumuika pamoja na jama'a yake katika mambo yote ya jumuiya yake na sala za jama'a

Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Kwa hakika Allah swt hawakutanishi Ummah wangu katika upotofu, na mkono Wake uko pamoja na Ummah huo, kwa hakika atakayejitoa humo basi atambue kuwa amejitoa kwa ajili ya Jahannam ." Mizan al - Hikmah.

B. KAFFARAH YA MADHAMBI

1. KUTOA NA KUPOKEA SALAAM KWA UNYENYEKEVU

Mumin huwa daima mwepesi wa kutoa salaam na kujibu salaam anazotolewa. Kamwe hawi mtu mwenye dharau wala kutegea kutolewa salaam au mwenye kiburi.

Allah swt anatuambia katika Quran kuwa tutolewapo salaamu ni faradhi kuijibu ama kwa kurejea salaam hiyo hiyo au kuijibu kwa ubora zaidi.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa akiviziwa na ma Sahaba wake kwa kujificha kiasi kwamba wapate fursa ya kutangulia kutoa salaam kwa sababu Mtume(s.a.w.w) alikuwa ndiyo daima mtu wa kutoa salaa kwa mara ya kwanza. Sasa sisi tunayo kiburi cha nini? Kwa hakika Allah swt anatuambia kuwa Salaam ni kauli itokayo Kwake.

2. KUWALISHA CHAKULA WALE WANAOHITAJI

Mumin kwa hakika huwa na moyo wa huruma kiasi kwamba hawezi kula peke yake huku watu wengine wakiwa katika hali ya kubakia katika njaa. Na si hayo tu bali huwa na moyo wa kutaka kuwasaidia binadamu wenzake katika kila hali awezayo yeye.

Yeye huwa karimu na kamwe hawi bakhili ambaye yeye mwenyewe hula bila ya kuwapa wenzake.

3. KUSALI SALA ZA TAHAJJUD (SALAT AL - LAYL AU USIKU WA MANANE)

Mumin huwa anasali sala za usiku wa manane (Tahajjud) wakati ambapo watu wanapokuwa wamelala usingizi mnono. Na husali kwa kutaka ridhaa ya Allah swt na wala si kwa kujionyesha kwa watu.

Kwa hakika sala hii huwa ikisaliwa na Mitume(a.s) na Ma-Imamu(a.s) kila siku bila ya kukosa. Hii ni ibada ambayo mtu huwa anamnyenyekea Allah swt wakati ambapo anakuwa ametulia kiroho na kiakili. Huwa hana mawazo au mambo yanayomsumbua huku na huko. Hivyo inamaanisha kuwa ibada hii inafanyika kwa roho khalisi na mtu hukubaliwa ibada zake haraka zaidi katika sala hizi.

Imam Hussain(a.s) siku ya Aashura alimwusia dada yake Bi. Zainab binti Ali ibn Albi Talib(a.s) kuwa: "Ewe dada yangu Zainab! Naomba usinisahau katika sala zako za usiku i.e. Salat al-Layl ."

C. WAANGAMIO

1. TABIA MBOVU

Wale watu wote wanaoingia katika kikundi hiki cha wenye tabia mbovu kwa hakika mwisho hao hujikuta kuwa wameangamia na kupoteza maisha yao. Yaani maji yameshakwisha mwagiga hayazoeleki tena. Tabia kama hizi zinamwigiza katika upotofu na kiburi na kujiona kuwa wao ndio watu waliostaarabika lakini kumbe ni kinyume na hali hiyo kwani Allah swt hawapendi wale wanaojifakharisha na kutakabari.

2. KUTII NAFSI ZAO

Iwapo mtu ataitii nafsi yake katika kumpotosha basi atakuwa kwa hakika amepotoka na kuangamia humu duniani na Aakhera kwa pamoja.

Amesema Mtume Mtukufu(s.a.w.w) : "Yeyote yule atakayeitambua nafsi yake (mwenyewe) basi hakika amemtambua Allah swt. "

Vile vile amesema kuwa: "Kwa hakika hodari kabisa ni yule ambaye ameighalibu nafsi yake." Yaani nafsi yake haimpotoshi katika mambo mengi mno kama vile ulafi, uchoyo, ubakhili, uasherati, ukafiri, maasi n.k.

Iwapo mtu atatawaliwa na nafsi yake basi atakuwa mtumwa wa nafsi yake.

3. KUJIFAKHARISHA

Kwa hakika mtu anapoambukizwa ugonjwa huu basi atambue kuwa ameangamia humu duniani na Aakhera kwa pamoja. Mtu anapenda kujionyesha kuwa yeye ndiye mtu bora zaidi kuliko wengine kwa sababu ya kupata kwa mali zaidi au ilimu au wadhifa. Vitu vyote hivi ambavyo sisi tunavijua kuwa ni vyote vyeneye kuangamia na kupotea na tutaviacha humu humu duniani.

Mtu katika sura hizi anaanza kukufuru kwani anaanza kuwasema na kuwaona watu wenzake kama wanyama na waovu kiasi cha kuthubutu kusema ati wanamsumbua na kumpotezea wakati wake. Inambidi yeye kutambua kuwa Allah swt amemwingiza katika mtihani hivyo inambidi afanye mema ili aweze kufuzu.

D. UOKOVU

1. HOFU YA ALLAH SWT KATIKA HALI YA DHAHIRI NA BATINI

Iwapo mtu atataka kupata uokovu inambidi awe na khofu ya Allah swt wakati akiwa peke yake na vile vile anapokuwa mbele ya watu. Isiwe kwamba mtu anapokuwa peke yake anaruhusiwa kufanya madhambi na wakati anapokuwa mbele ya watu kujionyesha kuwa ni mtu ambaye ana khofu ya Allah swt kupita watu wengine. Kutenda madhambi katika hali yoyote yanayo adhabu kali.

2. KUSUDIO MADHUBUTI KATIKA UMASIKINI NA UTAJIRI

Mtu inambidi awe na makusudio yake madhubuti bila ya kuyumbishwa katika hali ya umasikini na utajiri pia. Kwa sababu anapokuwa na moyo wa kuwasaidia watu wenzake katika ufukara asiupoteze katika hali awapo tajiri. Iwapo alikuwa msalihina awapo katika ufukara basi aendelee vile vile kwani asije akatoa kisingizio cha kukosa wakati katika utajiri na biashara zake.

Vile vile mtu anapokuwa katika umasikini inambidi awe madhubuti katika imani yake ili asije akakufuru na kushuku uadilifu wa Allah swt kwa shida azipatazo maishani mwake. Kila mtu anakumbana na misukosuko mbalimbali humu duniani hivyo inambidi kuimarisha imani yake.Huo pia huwa ni wakati wa mtihani kutoka kwa Allah s.w.t, na inambidi ajaribu kufuzu.

3. UADILIFU KATIKA SHIDA NA RAHA

Inambidi mtu awe daima katika mizani ya kauli yake asije akatamka maneno ambayo yatamkufurisha wakati anapokuwa katika shida au raha. Anapokuwa katika shida asije akasema kuwa Allah (s.w.t) amemtupa au hamjali wala hazisikii duaa zake (Allah swt atuepushe na wakati huo) na pale anapokuwa katika utajiri na starehe asije akakufuru kuwa yeye hana shida ya kitu chochote au mtu yeyote kwani anacho kile anachokihitaji, hivyo kujifanya maghururi na mwenye takabbur. Kwa hakika Allah swt hawapendi watu kama hawa.

Kwa wale walio matajiri inawabidi wafanye mambo mema kwa kutoa misaada kwa misikiti,madrasa masikini na mahala pote pale penye kupata ridhaa za Allah swt na wale walio masikini na mafukara inawabidi wakinai kwa kile walichonacho na wamshukuru Allah swt kwa kile anachowajaalia.

Maneno yetu yawe yamepimwa vyema kabla ya kuyatamka kwani isije tukasema mambo ambayo yatatufanya sisi tuwe mustahiki wa adhabu za Allah swt. Na wala tusiwaseme watu vibaya kwani na hayo pia yatatufanya sisi tuwe mustahiki wa Adhabu za Allah swt.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU