UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH0%

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH Mwandishi:
: Abdul Kareem J. Nkusui
Kundi: Tarehe

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH

Mwandishi: Dr. As'ad Waheed Alqasim
: Abdul Kareem J. Nkusui
Kundi:

Matembeleo: 9456
Pakua: 2665

Maelezo zaidi:

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9456 / Pakua: 2665
Kiwango Kiwango Kiwango
UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYYAH

Mwandishi:
Swahili

UKWELI WA SHIA ITHNA ASHARIYA

SEHEMU YA NNE

SHI'A NA SUNNAH TUKUFU ZA NABII (S.A.W.W)

Msimamo Wa Shi'a Katika Sunnah Za Mtume(s.a.w.w) :-

Hakika katika wanayosingiziwa Shi'a kutoka kwa baadhi ya wajinga ni kwamba wao wanakataa Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , huo ni uongo ambao hakuna uongo kama huo.

Na tunanukuu baadhi ya maoni ya maulamaa wa Kisunni katika msimamo wa Shi'a katika Sunnah tukufu za Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) :-

Sheikh Abu Zahrah anasema katika Kitabu chake Al-Imamu-s-Sadiq, Sunnah mutawatir ni hoja kwao bila ya kuwa na khitilafu katika kuitolea kwake hoja, na tawaturi kwao inawajibisha kuwa na elimu kamili.

Kwani kupinga hoja ya Sunnah ya Nabii iliyo pokelewa kwa tawatur kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) ni kufuru, kwa sababu ni kupinga ujumbe wa Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , ama kupinga hoja za kauli za maimamu ni chini ya hapo inahesabika kuwa ni ufasiki na wala sio kufr[158] .

Na anasema Sheikh Muhammad Al-Ghazali katika Kitabu chake Difaun 'anil -'aqidati wa-sh-shari'ati dhiddu mataa'inul-mustashriqina: "na miongoni mwa hawa waongo ni ambaye ameeneza kuwa Shi'a ni wafuasi wa Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) na Sunni ni wafuasi wa Muhammad na kwamba Shi'a wanaona kuwa Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) ana haki zaidi kupewa utume au umekosewa na kupewa mtu mwingine na huo ni upuuzi, uzushi na uovu."

Kisha anasema: "Hakika Shi'a wanaamini utume wa Muhammad na wanaona utukufu wa Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) upo katika kujumuika na Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) na kushikamana na Sunnah zake, na wao ni kama Waislamu wengine; hawaoni binadamu mtukufu zaidi katika walio tangulia na wanaokuja kuliko As-Sadiq - Al- amin. Vipi wananasibishiwa uongo huu[159] ."

Na vitabu vikubwa vya Hadith kwa Mashi'a ni vinne:

1. Al-Kafi

2. Man laa yah'dhuruhul-faqih

3. Al-istibsaar

4. At-Tahdhib

Na riwayah zote katika vitabu hivi zinakubali kufanyiwa uchunguzi, kwa hiyo kuna Hadith zinazo kubalika na zisizo kubalika, na Shi'a hawasemi kuwa Hadith zote zilizopokewa katika vitabu hivyo ni Sahih, kama halii livyo kwa mashekhe wawili, Bukhari na Muslim katika vitabu vyao Sahih. Na katika Shi'a hakuna Kitabu kinacho linganishwa na Kitabu kitukufu cha Allah (s.w.t) katika usahihi, na wala kitendo hakitimii kwa riwayah yoyote isipokuwa baada ya kufanyiwa uchunguzi, na hii ni kazi ya Maulamaa wenye jitihada katika kila zama, na kuihakiki riwayah ni kuipima kwanza katika Kitabu cha Allah (s.w.t).

Kisha kunatazamwa matin yake na Sanad yake na kulinganisha na riwayah nyingine zilizo thabiti kwa tawatur, mwisho inapimwa kiakili, na riwayah yoyote inayopungukiwa na moja ya masharti haya, basi kufanyia kazi ni mahali pa kutazama na kuidadisi.

Na katika Kitabu cha Masadirul Hadith as-Shi'ah Al-Imamiyyah, cha Allamah-Al-Muhaqiqi As-sayyid Muhammad Hussein Jalali, katika kuzigawa Hadith za al-Kaafi anasema:-

Jumla ya Hadith ambazo zipo humo ni Hadith 16,121, kati ya hizo Hadith 9,485 ni dhaifu, Hadith 114 ni Hasan, Hadith 1,118 ni mauthuq, Hadith 302 ni qawiyu (zenye nguvu) na Hadith 5,102 ni Sahih.

Na hii ina dhihirika wazi namna gani ambavyo Maulaama wa Kishi'a wamezifanya maelfu ya Hadith kuwa dhaifu katika Kitabu cha Al-Kaafi. Uko wapi sasa ukweli wa (yale) waliyoshikamana nayo baadhi ya waongo mfano wa Dhahiriy na Al-Khatib wanaosema kuwa Kitabu cha Al-Kaafi ni kama Sahih Bukhari kwa Masunni, kisha wanadai kuwa jina lake ni Sahih Al- Kaafi, huu ni uongo ulio wazi.

Wengi wanakariri katika vitabu vyao vyenye sumu kwa lengo la kumpoteza msomaji, kwa kuongeza sifa ya usahihi katika riwayah dhaifu walizo zichukua kwenye Al-Kaafi au kwenye vitabu vinginevyo katika vitabu vya Hadith vya Shi'a kwa kusimamisha hoja juu yao na kuwa ni ushahidi kwao.

Na wao hawapingi Hadith zote za Sahih Bukhari na Muslim, kama baadhi wanavyodai, lakini wao wana masharti yao maalumu katika kuikubali riwayah - kama ilivyotangulia - na hiyo ni kwa udadisi wao katika kuamini, kunukuu, na kuthibitisha.

Na kuna Hadith nyingi ambazo wanashirikiana baina yao na Masunni ambazo zimepokelewa katika Sahih mbili na vinginevyo, ambapo matin ni moja ingawa Hadith imepokelewa kwa Sanad tofauti tofauti, na ikhtilafu sio katika hoja yake, bali ni katika kuthibiti kwake au kutothibiti kwake.

Kuondoa Shaka Kuhusu Uma'asum Wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w)

Hakika Shi'a wanazitukuza Sunnah za Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) na wanaona ni ukafiri kwa anayepinga hukumu aliyoitoa Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , na wanaona kwamba katika shakhsiyyah (utu) ya Nabii kuwa yeye ni bora wa waliotangulia na wajao.

Na wanaona ni lazima kushikamana na Maimamu kumi na wawili wa Ahlul Bayt(a.s) , kwa sababu wao ni njia zinazoaminika zaidi katika kunukuu Sunnah ya Nabii(s.a.w.w) , na wao wanaondoa shaka yoyote ambayo inahusu mas'ala ya Uma'asum wa Nabii na wanakanusha wanayo yaitakidi watu wengine miongoni mwa Waislamu.

Kuhusu uwezekano wa Nabii kusahau, kukosea na kusahau kwake Qur'an na kuathirika na uchawi hadi asijue kuwa amefanya kitu fulani au hakukifanya, na mengineyo yasiyo kuwa hayo miongoni mwa uongo kama utakavyoyaona katika riwayah zifuatazo alizozipokea Bukhari, ambazo tunaanza kwa yale waliyo yapokea kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , kwamba hakuwa anajua kuwa alichoteremshiwa katika pango la Hira ulikuwa ni Utume.

Kama asingekuwa Waraqa bin Naufal (Mnasara) ambaye alimfahamisha hayo: "Mpaka akaingia kwa Bi. Khadija na akasema-: "Nifunikeni, nifunikeni, basi wakamfunika hadi woga ukamtoka akasema: Ewe Khadija nimepatwa na nini?"

Kisha Bi.Khadija akamchukua hadi kwa Waraqah bin Naufal bin Asad bin Abdul-'Uzza bin Qusay naye ni mtoto wa Ami wa Khadija, ndugu wa baba yake na alikuwa ni mtu aliyeingia katika Unasara katika zama za ujahili.

Na alikuwa anajua kuandika maandishi ya Kiarabu na alikuwa anaandika Injili kwa lugha ya Kiarabu ambapo Allah (s.w.t) amemjaalia na alikuwa ni mzee mkubwa kwa umri na alishapofuka, Bi.Khadija akamwambia:

"Ewe mtoto wa Ami sikiliza kutoka kwa mtoto wa ndugu yako." Waraqah akasema:- "mtoto wa ndugu yangu unaona nini?" Nabii akamweleza aliyoyaona, Waraqah akasema:- "Huyu ni Namusi (Jibraili) ambaye aliteremshwa kwa Mtume Musa(a.s) , natamani ningekuwa kisiki niwe hai wakati watakapo kufukuza Kaumu yako."

Mtume wa Allah(s.a.w.w) akasema: "Wao watanifukuza?[160] " Riwayah inaendelea kwa yanayoshangaza zaidi kuliko hayo Waraqah bin Naufal alipomkuta Mtume akijaribu kujinyonga kwa sababu ya huzuni yake kwa kukatika Wahyi, kama si Jibrail kumtuliza mara hii baada ya kuwa Waraqah bin Naufal akifanya hivyo.

Kisha Waraqah hakuchukua muda akafariki, na Wahyi ukakatika kwa muda na Nabii akahuzunika. Ambapo katika yaliyo tufikia mara nyingi huzuni ilipelekea kutaka kujirusha kutoka katika vilele vya milima, lakini kila alipopanda mlima ili ajiangushe Jibrail(a.s) alimtokea na akamwambia; "Ewe Muhammad hakika wewe ni Mtume wa kweli wa Allah (s.w.t)." Basi kwa hayo inapoa hasira yake na nafsi yake inatulia na anarudi, na unaporefuka muda wa kutopata Wahyi anarudia hayo, na anapofika kwenye kilele cha mlima Jibrail(a.s) anamtokea na kumwambia mfano wa aliyomwambia[161] .

Vile vile wamepokea kuwa Mtume(s.a.w.w) hakuwa amehifadhi Qur'an yote iliyoteremshwa kwake, vile vile kusahau kwake kusali Sala ya 'Alasiri kwa wakati wake. Nabii alimsikia mtu anasoma msikitini akasema: "Allah (s.w.t) amrehemu kwani amenikumbusha Ayah kadha nilizozisahau katika Surah kadha wa kadha[162] .

Abu Salamah anasema: "Jaabir bin Abdullah ametueleza kwamba Nabii alijiwa na 'Umar ibn Al- Khattab siku ya Khandaq akasema:

Ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) Wallahi sikusali hadi jua lilipokaribia kuzama na hiyo ni baada ya kufuturu mwenye kufunga, Nabii akasema Wallahi sijasali (laasiri), basi Nabii akateremka jangwani na mimi niko pamoja naye akatawadha kisha akasali sala ya alasiri baada ya kuzama jua kisha akasali magharibi baada yake[163] . Pia kutangulia kwake na kuwa Imam wao katika sala hali ana janaba na kusali kwake adhuhuri raka'a mbili.

Kutoka kwa Abu Huraira amesema:- Sala ilikimiwa na safu zikanyooshwa akatutokea Mtume wa Allah(s.a.w.w) aliposimama katika msala wake akakumbuka kuwa ana janaba, akatuambia simameni hivyo hivyo, kisha akarejea akaoga kisha akatoka na kichwa chake kinadondoka maji akatoa takbira ya kuhirimia sala, basi tukasali pamoja nae[164] .

Kutoka kwa Abu Huraira amesema: Nabii alitusalisha adhuhuri raka'a mbili, kisha akatoa salamu, kisha akasimama kwenye ubao mbele ya msikiti na akaweka mkono wake juu yake, na miongoni mwa watu waliokuwepo siku hiyo ni Abubakr na 'Umar, wakatoka kumweleza na watu wakatoka haraka wakasema: Je sala imepunguzwa? Na katika watu, alikuwepo mwanamume, Nabii(s.a.w.w) alikuwa anamwita Dhal-yadayni, akasema:- "Ewe Nabii wa Allah, je umesahau au imepunguzwa?" Akasema:-"Sikusahau wala haikupunguzwa." Wakasema; "bali umesahau Ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) ."

Akasema:- "amesema kweli Dhul-yadayni." Basi akasimama akasali raka'a mbili, kisha akatoa salamu, kisha akatoa takbira na akasujudu mfano wa Sajdah yake au alirefusha zaidi, kisha akanyanyua kichwa chake na akatoa takbirah, kisha akasujudu kama anavyosujudu, au alirefusha zaidi, kisha akanyanyua kichwa chake na akatoa takbirah[165] .

Kisha mambo yanafikia hadi mmoja wa mAyahudi kuweza kumroga Nabii mpaka Nabii akawa anaona kuwa amefanya jambo fulani na hakulifanya na kumuuliza kwake 'Aisha, wahyi umeteremshwa kwake au haukuteremshwa na je amemwingilia mkewe au laa!?

Kutoka kwa 'Aishah (r.a): " …siku moja Mtume(s.a.w.w) aliniambia: 'Ewe 'Aisha hakika Allah (s.w.t) amenitatulia jambo ambalo nilimuuliza; wamenijia wanaume wawili mmoja wao akakaa miguuni mwangu na mwingine kichwani mwangu aliye kuwa miguuni mwangu akamwambia aliye kichwani mwangu:- Mtu (huyu) ana nini? Akasema amerogwa, akasema:- Nani amemroga? Akasema:- Labid bin A'asam[166] .”

Kutoka kwa 'Aisha amesema: - "Mtume wa Allah(s.a.w.w) alilogwa hadi alikuwa anapagawa kuwa amefanya kitu kumbe hakukifanya hadi siku moja alipokuwa kwangu alimwomba Allah (s.w.t) akamjibu, kisha akasema ewe 'Aisha umehisi kuwa Allah (s.w.t) amenijibu nilivyomuomba[167] ."

Nabii alibaki siku kadhaa wa kadha amepagawa kuwa amemwingilia mke wake na wala hakumwingilia[168] . Sheikh Muhammad Abduh amezipinga riwayah hizi ambazo zinasema kuwa Mtume aliathiriwa na uchawi kwa sababu zinapinga kauli yake Allah (s.w.t) (Na wamesema madhalimu hawamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa)[169] .

Na kuhusu uhusiano wa Mtume(s.a.w.w) na wake zake; wamepokea yafuatayo:- "Ametusimulia Abu Usamah kutoka kwa Hisham kutoka kwa baba yake.

'Hakika Mtume wa Allah(s.a.w.w) alipokuwa katika maradhi yake alikuwa akizunguka kwa zamu kwa wake zake na anasema:- Kesho nitakuwa wapi kisha nitakuwa wapi?' kwa kuipupia nyumba ya 'Aisha. 'Aisha akasema ilipofika zamu yangu akatulia".[170]

Kutoka kwa Dhahari kutoka kwa Ur'wah kutoka kwa 'Aisha amesema:- "Mtume wa Allah(s.a.w.w) alikuwa anapotaka kusafiri anapiga kura baina ya wake zake yeyote atakaye bahatika anatoka pamoja naye na alikuwa anagawa kwa kila mke kati yao mchana na usiku wake isipokuwa Sauda bint Zam'ah alitoa hiba (zawadi) ya mchana na usiku wake kwa 'Aisha mke wa Nabii kwa kutaka katika hilo radhi ya Mtume wa Allah(s.a.w.w) ." [171]

Tazama mgongano baina ya riwayah mbili za juu na riwayah mbili za chini yake. Amesema Anas ibn Malik: "Nabii alikuwa anazunguka kwa zamu kwa wake zake kwa saa moja wakati wa usiku na kwa saa moja wakati wa mchana na wao walikuwa kumi na moja. Akasema: nikamuuliza Anas, Je, alikuwa anaweza? Akasema (Anas) tulikuwa tunasema kuwa yeye amepewa nguvu za watu thelathini." [172]

Kutoka kwa Anasi:- "Hakika Nabii alikuwa akizunguka kwa wake zake wote kwa usiku mmoja na alikuwa na wake tisa."[173]

Kwa kutegemea riwayah zilizo tangulia na mfano wake baadhi ya Waislamu wamechukua itikadi yao kwa kujuzu Nabii kukosea, kusahau na mengineyo yasiokuwa hayo. Vivyo hivyo Mtume kwa mtazamo wao ni maasumu katika mambo ya kidini au tablighi tu, na katika yasiokuwa hayo ni kama watu wengine anakosea na kupatia, na wala sijui mpangilio huu umetoka wapi? Hakika Allah (s.w.t) ametuamuru sisi kumfuata Mtume katika kila kitu bila ya kuweka sharti wala kikwazo chochote kwa kusema:-

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

"Na hatamki kwa matamanio yake isipokuwa ni wahyi unaofunuliwa ."(An-Najm 53: 3-4).

Vile vile kauli yake:-

مَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴿٧﴾

"Alichowaletea Mtume kichukueni na alichowakataza kiacheni ."(Al-Hasyr 59:07).

Inaonyesha amri ya jumla bila ya kuwa ni mahsusi na bila ya kuwa na sharti, kama itajuzu Nabii kukosea, basi Allah (s.w.t) atakuwa ametuamrisha kukosea; na tunajilinda kwa Allah (s.w.t) kusema mfano wa hayo. Kwa hiyo Allah (s.w.t) kutuamrisha sisi kumfuata Mtume kwa ujumla bila ya sharti wala kikwazo, ina maana kwamba, Mtume hakosei kabisa katika kauli zake na vitendo vyake vyote na kukiri kwake.

Sasa umetokea wapi mgawanyo huo ambao wanaudai katika Uma'asum wa Nabii? Je, Mtume kutokujua wahyi ambao umeteremshwa kwake katika pango la Hira ni jambo la kidunia? Je, kusahau kwake Qur'an ni jambo la kidunia? Je baadhi ya watu kumroga Nabii ni jambo la kidunia?

Hakika itikadi yetu kwa Uma'asum wa Nabii kwa jumla ndiyo msingi wetu katika kukataa riwayah zilizo tangulia kwa sababu ni katika yanayopinga Uma'asum wake.

Na Ismah ni kutakasika kutokana na dhambi, maasi madogo, makubwa na kutokana na kukosea na kusahau na kwa kuongezea katika uma'asum wa Nabii baada ya kupewa Utume, hakika ni lazima awe mwaminifu, mkweli na mwenye kuepukana na uovu mkubwa na mdogo na kabla ya kupewa Utume vile vile, ili nyoyo zipate utulivu kwake na nafsi zimwandame na kwa hayo anakuwa ni mwenye kustahiki cheo hiki kitukufu cha Allah (s.w.t).

Hakika kupenya riwayah ambazo zinagusa Uma'asum wa Nabii(s.a.w.w) kwa kuongezea kuwa zimewekwa na waongo ambapo zinachukuliwa kuwa ni tuhuma katika dini ya Kiislamu, kuna dhana ya kuwa kuna sababu nyingine kati ya hizo, ni kwa maslahi ya kuunga mkono misimamo ya baadhi ya Masahaba walipomwambia Mtume kuwa anaweweseka - naye yuko katika maradhi yake ya mwisho - alipowataka wamletee karatasi awaandikie ili wasipotee kamwe baada yake - rejea tuliyo yaandika kuhusu huzuni ya siku ya Alhamisi katika sehemu ya kwanza - Hivyo hakuna mshangao baada ya hayo, kuwepo kwa baadhi ya riwayah ambazo zinafanya Sahaba apatie katika mas'ala ambayo Nabii(s.a.w.w) amekosea; tunajikinga kwa Allah (s.w.t).

Na miongoni mwa riwayah hizi ni ambazo zimenasibishwa na jambo la kuteremka Ayah ya hijab baada ya 'Umar Al-Khattab kumtanabahisha Mtume wa Allah(s.a.w.w) juu ya ulazima wa kuvaa hijab.

Kutoka kwa Humaid kutoka kwa Anas: amesema 'Umar (r.a), Nilisema:- "Ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) anaingia kwako mwema na mwovu je isingekuwa vyema uwaamuru mama wa waumini kuvaa hijab? Basi Allah (s.w.t) akateremsha Ayah ya hijab."[174]

Na katika riwaya nyingine 'Umar Al-Khattab alikuwa anamwambia Mtume wa Allah(s.a.w.w) :- "Wavalishe wake zako hijabu." ('Umar) Akasema:- "Hakufanya hivyo Mtume(s.a.w.w) .

Basi Allah (s.w.t) akashusha Ayah ya hijab." Na wake wa Nabii(s.a.w.w) walikuwa wanatoka usiku hadi usiku kwenda kujisaidia, basi alitoka Sauda binti Zam'ah na alikuwa ni mwanamke mrefu, 'Umar bin Khattab akamwona naye yuko katika majlisi, akasema tumekujua ewe Sauda, kwa kupupia hijabu iteremshwe, basi, Allah (s.w.t) Mtukufu akateremsha Ayah ya hijabu.[175]

Vile vile yaliyonasibishwa kuhusu Ayah ya kukataza kuwasalia wanafiki kwamba imeteremka kuunga mkono msimamo wa 'Umar, baada ya Mtume(s.a.w.w) kung'ang'ania kumsalia Ibn 'Ubay mnafiki, na kutosikia kwake upinzani wa 'Umar juu ya hilo kama wanavyopokea.

Amesema:- Alipokufa 'Abdallah bin 'Ubay mtoto wake alikuja kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) akasema: "Ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) nipe nguo yako nikamvike sanda, msalie na mwombee maghfira", akampa nguo yake, na akamwambia, "ukimaliza tuite," alipomaliza akamwita akaja ili amsalie, 'Umar akamvuta na akasema: "Je, Allah (s.w.t) si amekukataza kuwasalia wanafiki? Akasema uwaombee maghfira au usiwaombee, kama utawaombea maghfira mara sabini, Allah (s.w.t) hatawasamehe," Ikateremka Ayah - wala usimsalie yeyote akifa miongoni mwao kabisa wala usisimame katika kaburi lake - basi akaacha kuwasalia. [176]

Kutoka kwa 'Umar al-Khattab ni kwamba amesema:- "Alipokufa 'Abdallah bin 'Ubay bin Salul, Mtume wa Allah(s.a.w.w) aliitwa kwenda kumsalia, Mtume(s.a.w.w) aliposimama nilimrukia nikasema:- "Ewe Mtume wa Allah, unamsalia mtoto wa 'Ubay?" Na siku moja alisema kadha wa kadha nikamtajia kauli yake. Mtume wa Allah(s.a.w.w) akatabasamu na akasema niachie ewe 'Umar, nilipozidi kumwambia akasema hakika mimi nimepewa hiari." [177]

Basi nikachagua, kama ningejua kuwa nikimzidishia mara sabini kuwa atasamehewa ningezidisha. Akasema: Mtume wa Allah(s.a.w.w) akamsalia kisha akaondoka hakukaa isipokuwa muda mchache zikateremka Ayah mbili katika Surah ya Baraat; "wala msimsalie yeyote miongoni mwao akifa kamwe hali na wao ni mafasiki."

Akasema:- Nikastaajabu baada ya kumkaripia Mtume wa Allah(s.a.w.w) , na ukweli ni kwamba katika tukio hilo Mtume alipewa hiari kuwasalia wanafiki na kuwaombea msamaha kwa kauli yake Allah (s.w.t):

اسْتَغْفِرْ لَهُمْ أَوْ لَا تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ إِن تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ سَبْعِينَ مَرَّةً فَلَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ﴿٨٠ ﴾

"Waombee msamaha au usiwaombee, na hata kama utawaombea mara sabini basi Allah (s.w.t.) hatawasamehe "(At-Taubah 09:80).

Na Mtume alichagua kumsalia mnafiki huyo kwa sababu ya kupatikana faida kubwa na maslahi yanayo patikana kwa kuizoeza kaumu yake ya Khazraj na kwa sababu hiyo walisilimu watu elfu moja, na sala yake kwa mnafiki huyo ilikuwa kabla ya kushuka Ayah ya kukataza hilo na Ayah ya (waombee msamaha au usiwaombee...) haionyeshi kukataza ambako alikufahamu 'Umar na akampinga Mtume, na kwa sababu hiyo akamtia makosani.

Na kuteremka Ayah ya kukataza kuwasalia wanafiki haionyeshi kosa kwa Mtume(s.a.w.w) kumsalia Abdallah bin 'Ubay – na tunajikinga kwa Allah (s.w.t) kama walivyo fahamu baadhi.

Sala yake kwa mnafiki itakuwa ni makosa kama angeisali baada ya kuteremka Ayah ya kukataza, na wala sio kabla yake. Wala haifahamiki katika Ayah hii isipokuwa kosa la 'Umar na upinzani wake mkali kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) kama ambavyo 'Umar alitambua hilo na akajuta kwa pupa yake ambapo inaonekana kuwa amesema:- "Nimefanya kosa katika Uislamu ambalo sikufanya kamwe kosa mfano wa hilo. Mtume(s.a.w.w) alitaka kumsalia Abadallah bin ‘Ubay nikamvuta nguo na kumwambia:- Wallahi hakukuamrisha Allah (s.w.t) kwa hili?"

Allah (s.w.t) amekwishakuambia 'uwaombee msamaha au usiwaombee...' Akasema Mtume wa Allah(s.a.w.w) :- Allah (s.w.t) amenipa hiari akasema:- 'waombee msamaha au usiwaombee msamaha…' basi nikachagua (kuwaombea msamaha)[178] .

Na kabla ya hayo ni yale yanayoonekana katika kuchukua fidia kutoka kwa mateka siku ya Badr na kwamba Ayah:

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٦٧ ﴾

"Haimpasi Nabii kuwa na mateka mpaka apigane na kushinda katika nchi mnataka utajiri wa kidunia na Allah ni Mwenye nguvu Mwenye hekima, isingelikuwa hukumu kutoka kwa Allah basi ingekufikieni kwa yale mliyo yachukua adhabu kubwa ."(Al-Anfaal 08:67).

Imeteremka kumlaumu Mtume kama baadhi wanavyodai - kwa sababu ya kuchukua kwake fidia kutoka kwa mateka wa Badr na kutokuwauwa kwake wakati ambapo 'Umar bin Khattab alikuwa anataka wauliwe wote, basi Ayah ikateremka ikiunga mkono rai ya 'Umar na wakapokea riwayah inayounga mkono rai yao, kauli ya uongo waliyoizua kutoka kwao na wakainasibisha kwa Mtume(s.a.w.w) kulingana na maana ya Ayah iliyotangulia ambayo ina makemeo ya adhabu kali, lakini makemeo hayo ni kwa ajili ya nani? kama ambavyo wanapokea na kunasibisha kwa Mtume(s.a.w.w) kuwa amesema alipokuwa analia pamoja na Abubakr "ilikaribia kutugusa adhabu kubwa kwa kumkhalifu mtoto wa Khattab na kama ingeteremka adhabu basi asingepona kutokana na adhabu hiyo isipokuwa mtoto wa Khattab."

Na ukweli wa tukio hili ni kwamba Ayah iliyotangulia imeteremka kabla ya vita vya Badr na kuwakemea Masahaba ambao walifadhilisha biashara na kilichobebwa na msafara wa Abu Sufiani kuliko kupigana.

Wakati Mtume alipowataka ushauri kwa ajili ya suala hilo ili aone upeo wa kuwa kwao tayari katika kuwapiga vita washirikina, kukataza katika Ayah sio kukataza moja kwa moja kwa Nabii kuchukua mateka bali ni kukataza kuchukua bila ya kuwapiga vita washirikina kama walivyokuwa wanataka baadhi ya Masahaba, wakati Mtume(s.a.w.w) alipo washauri kuteka msafara wao au kuwapiga vita kabla ya Badr, namna gani itaingia akilini kuwa Ayah hiyo ambayo ina wakemea wale ambao hawataki vita katika ardhi - kuwa imeteremka kwa kumkemea Mtume(s.a.w.w) na amekwisha wapiga washirikina na kuwauwa mauwaji makali kabisa! Katika vita hivyo waliuliwa mashujaa sabini wa Kiquraish.

Abu Huraira Na Wingi Wa Riwayah Zake Katika Hadith

Wapokezi wa Hadith wameafikiana kuwa Abu Huraira alikuwa ni Sahaba aliyepokea Hadith nyingi kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) wakati ambapo hakuandamana na Nabii isipokuwa mwaka mmoja na miezi tisa-au miaka mitatu kwa riwayah za mbali kabisa-Sahih za Ahl as-Sunnah zimepokea kutoka kwake Hadith elfu tano mia tatu na sabini na nne (5,374) kati ya hizo Bukhari amepokea Hadith 466.

Lakini Abu Huraira mwenyewe anasema hakika 'Abdulah ibn 'Umar alikuwa amepokea Hadith nyingi zaidi kuliko yeye na alikuwa Ibn 'Umar anaandika na yeye (Abu Hurayrah) alikuwa haandiki.

Abu Huraira mwenyewe anasema: "Hakuna yeyote katika Masahaba wa Nabii mwenye kupokea Hadith nyingi kuliko mimi isipokuwa Abdullah ibn 'Umar kwani yeye alikuwa anaandika na mimi siandiki." Anafuatiwa na Ma'amar. Imepokewa kutoka kwa Hammam.[179]

Isipokuwa Hadith zote alizozipokea Ibn 'Umar ni 722 na Bukhari hakuzitoa isipokuwa.

Hadith saba tu na Muslim ameandika Hadith 20 tu. Na Abu Huraira mwenyewe amebainisha sababu ya kuandamana kwake na Mtume kwa wingi.

Kutoka kwa Shihabu kutoka kwa Al-A'aray kutoka kwa Abu Huraira amesema: "Wanasema kuwa Abu Huraira anahudhuria sana na wanasema: Muhajirin na Ansari wana nini mbona hawapokei mfano wa Hadith zake, hakika ndugu zangu katika Muhajirin walikuwa wanashughulishwa na bidhaa katika masoko na ndugu zangu katika Ansari walikuwa wanashughulishwa na kuchunga mali zao na mimi nilikuwa mtu maskini namwandama Mtume wa Allah(s.a.w.w) kwa ajili ya kujaza tumbo langu, hivyo nahudhuria wanapoghibu (wanapokuwa hawapo) na nakumbuka wanaposahau.[180]

Na yafuatayo yanatia mkazo riwayah ya juu na kukiri Abu Huraira sababu ya kuwasomea Qur'an baadhi ya Masahaba.

"Kutoka kwa Sa'id Al-Maqbariya kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika watu walikuwa wanasema Abu Huraira amepokea Hadith nyingi, hakika mimi nilikuwa namwandama Mtume wa Allah(s.a.w.w) kwa ajili ya kushibisha tumbo langu ili nisile uchafu na nisivae ngozi na wala asije akanihudumia fulani na fulani na nilikuwa nikifunga mawe kwenye tumbo langu kutokana na njaa, na nilikuwa simsomei mtu Ayah na hali niko nayo ili aninyenyekee na kunilisha, na mtu bora kwa masikini alikuwa ni Ja'afar ibn Abu Talib, alikuwa anatuhurumia na kutulisha kile kilichopo katika nyumba yake hadi alikuwa anatutolea chombo ambacho hakina kitu, basi tunakipasua ili tulambe kilichomo humo."[181]

Na katika kumpenda kwake Ja'afar ibn Abi Talib ambako kumebainishwa katika riwayah ya juu imepokewa kutoka kwa Abu Huraira kwamba amesema hakuvaa viatu wala kupanda wanyama wala hakutembea juu ya ardhi baada ya Mtume aliye bora kuliko Ja'afar ibn Abi talib[182] .

Na ameipokea Muslim katika Sahih yake kuwa 'Umar al-Khattab alimpiga Abu Huraira aliposikia anasimulia kutoka kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) : "Mwenye kusema laa ilaha illallah ataingia Jannat (peponi)[183] .

Na amepokea Abdi bar kutoka kwa Abu Huraira mwenyewe anasema: "Nimewasimulia Hadith kama ningewasimulia zama za 'Umar al- Khattab basi angenipiga 'Umar kwa upanga."[184] .

Na yanayotilia mkazo hayo ni alioyasema Faqihil-Muhadithiin Rashid Ridhaa: "Kama umri wa 'Umar ungekuwa mrefu hadi akafa Abu Huraira basi Hadith hizo nyingi zisingetufikia,"[185] .

Na anasema Mustafa Sadiq Ar- Raafi'i; "basi akawa kwa hilo (yaani Abu Huraira) ni mpokezi wa kwanza kutuhumiwa katika Uislam."[186]

Wakati vilipotokea vita vya Siffin baina ya Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) na Mu'awiyah bin Abi Sufian, Abu Huraira alikimbilia kwa Mu'awiyah bin Abi Sufian naalilipwa kwa upokezi wake mzuri wa Hadith na kuwanusuru kwake Bani 'Umayyah wakamneemesha. Marwan Al-Hakim alikuwa anamfanya naibu wake katika Ugavana wa mji wa Madina basi hali yake ikabadilika kutoka hali ya umaskini kwenda kwenye hali ya utajiri. Imepokelewa kutoka kwa Ayyub bin Muhammad kuwa amesema:

Tulikuwa kwa Abu Huraira na ana vipande viwili vya nguo vilivyo fumwa kwa kitani akivivaa akasema, 'hongera, hongera, Abu Huraira anavaa katani? Hakika uliniona mimi niko wa mwisho baina ya mimbar ya Mtume(s.a.w.w) na chumba cha 'Aisha nimezimia anakuja anayeingia anaweka mguu wake juu ya shingo langu na ninaonekana kuwa mimi ni kichaa na wala sina kichaa, sikuwa na kitu isipokuwa njaa”[187] .

Na matokeo ya kujiunga kwake na Bani 'Umayyah ilikuwa ni kwa kuficha kwake baadhi ya Hadith ambazo alikuwa anazisikia kutoka kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) na hofu yake kwa ajili ya nafsi yake kutokana na kuuliwa katika hali ya kuzisimulia.

Kutoka kwa Abu Huraira amesema:- "Nimehifadhi kutoka kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) mikoba miwili, mmoja wapo nimeutoa na mwingine kama ningeutoa ningekatwa hili koo."[188]

Kukiri huku kunapinga kauli yake nyingine kuwa yeye hakuwa anaficha Hadith kwa ajili ya kumwogopa Allah (s.w.t). Kutoka kwa A'araji kutoka kwa Abu Huraira amesema:- "Hakika watu wanasema Abu Huraira amepokea kwa wingi kama isingekuwa Ayah mbili katika Kitabu cha Allah (s.w.t) nisingesimulia Hadith, kisha akasoma:- Hakika ambao wanaficha tuliyo yateremsha katika ubainifu… Mwingi wa Rehema."[189]

Na ukamilifu wa Ayah mbili katika riwayah zilizotangulia ambazo Abu Huraira hafichi Hadith kwa sababu yake ni:-

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ ا للَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ ﴿١٥٩﴾ إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَبَيَّنُوا فَأُولَـٰئِكَ أَتُوبُ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنَا التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٠ ﴾

"Hakika ambao wanaficha tuliyoyateremsha katika ubainifu na uongofu baada ya kuubainisha kwa watu katika Kitabu, basi hao Allah anawalaani na wanawalaani wenye kulaani isipokuwa wale walio tubu na wakafanya wema na wakabainisha hao nitawasamehe na mimi ni Mwenye kusamehe Mwingi wa rehema."(Al-Baqarah 02:159-160).

Baada ya kunukuu mifano ya riwayah hizi, ambazo zinabainisha uhakika wa Abu Huraira na daraja la uadilifu wake na uaminifu wake katika kupokewa Hadith, inadhihirika wazi sababu ya Mashi'a kukataa riwayah zake, jambo ambalo limewafanya baadhi ya watu kuwatuhumu Shi'a kwa sababu hiyo. Na hiyo sio jingine isipokuwa ni kuzidisha kipimo, hatuoni kisingizio kinachokubaliwa hususan pamoja na kuwepo dalili zote hizo ambazo zinathibitisha usahihi wa tuliyoyasema.

Katika Ikhtisaru Ulumil-Hadith amesema Ibn Hambal, Abubakr Al- Humaydiy na Abubakr As-Swayrafiy: " Hatukubali riwayah ya aliyesema uongo katika Hadith za Mtume wa Allah(s.a.w.w) hata kama atatubu na kuacha uongo wake baada ya hapo."[190]

Na amesema As-Sam'aaniy:- "Mwenye kusema uongo katika habari moja ni wajibu kuporomoa yaliyo tangulia katika Hadith yake".[191]

Tunaorodhesha katika yafuatayo baadhi ya riwayah za Abu Huraira ambazo amezipokea Bukhari katika Sahih yake. Tunaanza na Mtume Musa(a.s) kumng'oa jicho Malaika wa mauti.

Kutoka kwa Ibn Twaus kutoka kwa baba yake kutoka kwa Abu Huraira amesema: - Malaika wa mauti alitumwa kwa Mtume Musa(a.s) alipomwendea akampiga na akamng'oa jicho, basi akarejea kwa Mola wake akasema umenituma kwa mja wako asiyetaka mauti, Allah (s.w.t) akamrudishia jicho lake na akasema: Rudi na mwambie aweke mkono wake juu ya mgongo wa ng'ombe dume, basi atapata - kwa kila unywele utakaofunikwa na mkono - mwaka mmoja, (Musa akasema): Ewe Mola kisha nini? Akasema:- Kisha mauti akasema basi iwe sasa hivi, basi akamwomba Allah (s.w.t) amkurubishe na ardhi tukufu Baitul Muqaddas kiasi cha umbali wa kutupa jiwe."[192]

*Kutoka kwa Muhammad kutoka kwa Abu Huraira ni Marfu’u: Jahannam itaambiwa je, umejaa itasema Je? Kuna ziada? Allah (s.w.t) ataweka mguu wake juu yake, basi itasema: Qatu, qatu; yaani imetosha, imetosha.[193] .

Kutoka kwa Abu Huraira (r.a): amesema Nabii(s.a.w.w) : " kila binadamu huchomwa na Shetani ubavuni mwake kwa vidole vyake wakati anapozaliwa isipokuwa Mtume 'Isa bin Maryam alienda kumchoma, basi akachoma pazia."[194]

Kutoka kwa Abu Maryam: kutoka kwa Nabii(s.a.w.w) amesema: "Allah (s.w.t) amemuumba Adam kwa sura yake, urefu wake ni dhiraa sitini."[195]

Kutoka kwa Hawa bin Ya'asir kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Nabii(s.a.w.w) amesema: "Anayesema mimi ni bora kuliko Yunus bin Matta amekwishasema uongo ."[196]

Kutoka kwa Salmah na Abu Abdillah Al-Aghar kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika Mtume wa Allah(s.a.w.w) amesema: 'Mola wetu Mtukufu huteremka kila usiku hadi kwenye mbingu ya dunia inapobakia theluthi ya mwisho ya usiku anasema: Nani atakayeniita ili nimuitikie? Nani atakayeniomba nimpe? nani atakayenitaka msamaha nimsamehe?”[197]

Na riwayah hii ya mwisho inafaa tusimame kwayo kidogo, ambao wanaoipokea na wanaitakidi usahihi wake, vile vile wanaitakidi kwamba Allah (s.w.t) amekaa katika 'arsh na kwamba kuteremka kwake huku, kwa madai yao - inakuwa katika mwisho wa usiku tu, lakini kwa kujua kwetu kuwa ardhi ni duara na kuzunguka kwake, inafanya usiku uwepo ardhini kila pande kwa muda wa kuwepo kwake na kuwepo kwa binadamu juu yake na hii ina maana kuwa Allah (s.w.t) atabaki daima katika mbingu ya dunia. Na wala sisi hatuitakidi kuwepo kwa mgongano baina ya ukweli wa kielimu na ukweli wa kiuungu.

Tukiachilia mbali mgongano huo na tunayoyaitakidi kukaa kwa Allah (s.w.t) juu ya ''arsh, Allah (s.w.t) yuko mbali na wanayoyasema. Allah (s.w.t) ni Nuru ya mbingu na ardhi hana mpaka wa sehemu wala zama, na kama angekuwa amebebwa juu ya 'arsh ingelazimu mbebaji kuwa na nguvu zaidi kuliko aliyebebwa - kama ilivyopokewa kutoka kwa Ja'afar As-Sadiq(a.s) na kwa nini ateremke na kupanda naye yuko karibu nasi kuliko mshipa wa moyo?

Na Hadith zilizotangulia ni katika Israiliyyaat ambazo Abu Huraira amezipokea kwa wingi na kutokana na kuandamana kwa wingi na Ka'ab Al-Ahbaar, Myahudi aliejidhihirisha kuamini kwake Uislamu na kwa kuongezea katika riwayah hizo:-

Kutoka kwa Abu Huraira ni kwamba Mtume amesema: "Asitembee mmoja wenu kwa kiatu kimoja hivyo aivalishe miguu yote viatu au yote aivue viatu."[198] Kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika amesema Mtume wa Allah(s.a.w.w) "Kila nabii ana ombi lake analoomba na mimi nataka niache ombi langu kwa ajili ya kuuombea shifaa 'Ummah wangu kesho akhera."[199] .

Kutoka kwa Salamah kwamba Abu Huraira amesema: "Nilimsikia Mtume wa Allah(s.a.w.w) anasema sisimizi alimuuma nabii miongoni mwa manabii basi, akaamua kuteketeza kijiji cha sisimizi, Allah (s.w.t) akampelekea wahyi, sisimizi tu amekuuma ukateketeza ‘Ummah miongoni mwa 'Ummah wanao mtukuza Allah (s.w.t.)?"[200] .

Kutoka kwa Al-A'arij kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) amesema: "Mmoja wenu akitawadha basi aweke maji puani mwake kisha ayasambaze, na mwenye kufanya basi asali witri na akiamka mmoja wenu katika usingizi wake basi, aoshe mkono wake kabla ya kuanza kutawadha kwani mmoja wenu hajui mkono wake umelala wapi."[201]

Kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Nabii amesema: "Ulipotea 'Ummah katika Bani Israil haujulikani umefanya nini na mimi siuoni 'Ummah huo isipokuwa ni panya akiwekewa maziwa ya ngamia hanywi na akiwekewa maziwa ya mbuzi anakunywa."[202]

Hakika Abu Huraira amesema: "Sisi tulipokuwa kwa Nabii alisema kuwa wakati nilipokuwa nimelala nimeonyeshwa Jannat, basi nikamwona mwanamke anatawadha kando ya kasri nikasema kasri hii ni ya nani? Wakasema: Ya Umar al-Khattab, basi nikakumbuka gherah yake nikageuka na kurejea. 'Umar akalia na akasema: Je kwa ajili yako naonewa gherah ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) ?"[203]

Kutoka kwa Ata'i bin Ya'sar kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika Nabii siku moja alikuwa anasimulia na alikuwa na mwanamme katika mabedui, kwamba mtu katika watu wa Jannat alimtaka Mola wake ruhusa ya kulima, akasema: basi akapanda mbegu na ikaota mimea yake ikastawi na kaivuna, ilikuwa kama mfano wa milima, basi Allah (s.w.t.) atasema hutosheki ewe binadamu; hakika hakikushibishi kitu chochote, bedui akasema: Wallahi simwoni isipokuwa ni Mquraish au Ansar kwani wao ni wakulima ama sisi sio wakulima basi Nabii akacheka."[204]

Kutoka kwa A'awadh kutoka kwa Abu Huraira: "Hakika Mtume(s.a.w.w) amesema:Allah (s.w.t) anawachekea watu wawili, mmoja wao atamuuwa mwingine, wanaingia Jannat , huyu anapigana katika njia ya Allah (s.w.t) na kuuliwa kisha Allah (s.w.t) anamsamehe muuwaji na kisha anakufa shahidi."[205]

Hakika yeye amemsikia Abu Huraira anasema kwamba yeye amemsikia Mtume wa Allah(s.a.w.w) anasema sisi ni wa mwisho tuliyotangulia.

Na kwa isnad yake kama akichungulia katika nyumba yako yeyote na bila ya kumruhusu ukamtupia mawe na kumtoa jicho lake basi, hakutakuwa na dhambi kwako.[206]

Ametusimulia Abdurazaq kutoka kwa Ma'amar kutoka kwa Hamaam bin Munabih kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) amesema: " Bani Israili walikuwa wanaoga uchi baadhi yao wanawaangalia wengine na Mtume Musa(a.s) alikuwa anaoga peke yake wakasema: Wallahi haimzui Mtume Musa(a.s) kuoga pamoja na sisi isipokuwa ana aibu (kasoro, mshipa) siku moja alienda kuoga akaweka nguo yake juu ya jiwe, basi jiwe likakimbia na nguo yake, Mtume Musa(a.s) akawa anakimbia nyuma yake akasema nguo yangu ewe jiwe, nguo yangu ewe jiwe, hadi Bani Israeli wakamwangalia Mtume Musa(a.s) wakasema:

Wallahi Mtume Musa(a.s) hana kasoro, na akachukua nguo yake akaanza kulipiga jiwe. Abu Huraira akasema: Wallahi hakika alilipiga jiwe na kulijeruhi majeraha sita au saba.”[207]

Ametusimulia Abul-yaman Shu'ayba ametupa habari kutoka kwa Zuhri amesema: Ametusimulia Sa'id bin Musayyab: Hakika Abu Huraira amesema: nimemsikia Mtume wa Allah(s.a.w.w) anasema: Litaingia Jannat katika 'Ummah wangu kundi la watu sabini elfu nyuso zao zinatoa nuru kama unavyo angaza mwezi, Ukasha bin Muhsin Al Asadi akasimama ananyanyua kipande cha nguo yake akasema: "Niombee Allah (s.w.t) anijaalie miongoni mwao." Akasema: "Ewe Allah (s.w.t) mjaalie awe miongoni mwao, kisha akasimama mwanamume katika Ansar. Akasema: "Ewe Mtume wa Allah(s.a.w.w) niombee Allah (s.w.t) anijaalie niwe miongoni mwao." Akasema:'Ukasha amekutangulia.” [208] .

Kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Nabii(s.a.w.w) amesema: wakati Ayyub alipokuwa anaoga uchi, panzi wa dhahabu akamwangukia Ayyub akamficha katika nguo yake. Mola wake akamwita: "Ewe Ayyub je sikuwa nimekutosheleza kwa unayoyaona?" Akasema: "Ndiyo kwa utukufu wako lakini sitosheki kwa baraka zako."[209]

Kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Nabii amesema: Wakati mwanamme alipokuwa amepanda ng'ombe alimgeukia akamwambia sikuumbwa kwa ajili hii, nimeumbwa kwa ajili ya kulima, akasema nilimwamini mimi Abubakr na 'Umar. mbwa mwitu alichukua kondoo, mchungaji akamfuata, mbwa mwitu akasema nani atamchunga siku ya saba? Siku ambayo hakuna wakumchunga isipokuwa mimi? Akasema nilimuamini mimi, Abubakr na 'Umar. Abu Salamah akasema na wao siku hiyo hawakuwa katika kaumu.[210]

Kutoka kwa Abu Huraira: " hakika Mtume wa Allah(s.a.w.w) amesema: 'Ikiadhiniwa kwa ajili ya sala Shetani anakimbia na kutoa ushuzi ili asisikie adhana, adhana ikimalizika anarudi, sala zinapoanza kulipwa anakimbia zikishalipwa anarudi ili ahadae baina ya mtu na nafsi yake, anasema: kumbuka kadha, kumbuka kadha hataacha kusema mpaka mtu atakuwa hajui amesali raka'a ngapi”[211] .

Kisimamo Pamoja Na Bukhari Katika Sahih Yake

Baada ya kueleza riwayah zilizotangulia ambazo zinagusa Uma'asum wa Nabii na kisha riwayah za Abu Huraira, imekuwa ni dharura kutupia macho juu ya Sahih ya Bukhari kwa sifa yake, ambayo imedhamini riwayah hizo na kwa sifa yake ya kuwa ni kitabu Sahih zaidi katika vitabu vya Hadith kwa Ahl as-Sunnah na ambacho wanakizingatia baada ya kitabu cha Allah (s.w.t) katika usahihi. Na hapa ni chimbuko la siri ya upinzani wao kwa kila anayekataa Hadith iliyo pokelewa katika Sahih Bukhari, wao wanaamini kabisa usahihi wa yote yaliyopokelewa humo.

Bukhari amepokea Hadith zake Sahih kwa maoni yake Hadith elfu sita kama ilivyopokelewa kwa Bukhari mwenyewe amesema: "Sikupokea katika kitabu hiki isipokuwa Hadith Sahih tu na nilizoziacha miongoni mwa Hadith Sahih ni nyingi zaidi."[212]

Na tuliyo yachukua kwanza kwa Bukhari ni; kutegemea kwake uadilifu wa mlolongo wa wapokezi wa Hadith kama sharti lake pekee katika kuthibitisha usahihi wa Hadith iliyopokelewa bila ya kuangalia matin na maana iliyobeba. basi pakawa na mgongano mwingi katika riwayah ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa ni tuhuma katika dini.

Mpokezi (wa hadithi) hata kama atakuwa mwadilifu, uadilifu wake hauzuii kusahau kwake kipande cha Hadith aliyoisikia, tukiachilia mbali dhana ya kupokea kwake Hadith kwa maana yake na wala si kwa matamshi halisi aliyoyasikia.

Jambo ambalo linaikosesha Hadith matamko yake ya asili, na ambayo yanaweza kuwa na maana nyingine, na mpokezi akawa hajatambua hivyo akainukuu kwa maana nyingine. Tukiongezea ugumu wa kujua uadilifu wa watu hasa wanafiki kati yao, ambao hakuna anayejua undani wao isipokuwa Mola wa waja, inadhihirika kwetu kasoro kubwa katika sharti la Bukhari katika kuandika kwake Hadith zake Sahih.

Kama alivyosema Ahmad Amin, hakika baadhi ya watu ambao amepokea kutoka kwao sio waaminifu, na amewatia udhaifu karibu wapokezi themanini[213] kati ya watu aliopokea kwao Al Bukhari. Na katika yafuatayo tunaeleza zaidi katika riwayah ambazo Bukhari amezihesabu kuwa ni sahih, na baadhi ya Waislamu wakajilazimisha kuzifuata katika muda wote.

Kutoka kwa Abi Sa'id al-Khudriy; ya kwamba Mtume(s.a.w.w) alisema kuhusu siku ya Qiyamah: " Hakika sisi tulisikia mwitaji anaita kila watu wakiendee walicho kuwa wanakiabudu na sisi tunamsubiri Mola wetu." akasema: "Basi Allah (s.w.t) atawajia katika sura isiyokuwa sura yake ambayo walimwona nayo mara ya kwanza na kusema mimi ni Mola wenu watasema wewe ni Mola wetu, basi hawatomsemesha isipokuwa manabii, atasema je, kati yenu na yake kuna alama mtakayomjua? Watasema muundi (mguu), basi atadhihirisha muundi wake; basi kila muumini atamsujudia."[214]

Amesema Jariyr bin Abdillahi: "Tulikuwa tumekaa usiku mmoja pamoja na Nabii(s.a.w.w) , akatazama mwezi usiku wa kumi na nne akasema: 'Hakika nyinyi mtamwona Mola wenu kama mnavyo uona huu mwezi hamtadhulumiwa katika kumwona kwake.”[215] .

Hakika riwayah mbili hizo hapo juu, ambazo zinafahamika kuwa kuna uwezekano wa kuonekana kwa Allah (s.w.t), hazikubaliwi kwa sababu walioitakidi uwezekano wa kuonekana Allah (s.w.t) wamekosea katika ta'awil yao, katika kauli yake Allah (s.w.t) (nyuso siku hiyo zitang'ara kumwangalia Mola wao) na ta'awil yake sahih ni zikisubiri amri ya Mola wao na vivyo hivyo ta'awil ya Ayah nyingine ambazo dhahiri yake zinaonyesha kuwa Allah (s.w.t) ni kiwiliwili na yanatiliwa nguvu yale tuliyo yasema na riwayah ambayo Bukhari mwenyewe ameinukuu vile vile.

Kutoka kwa Masruq amesema:- Nilimwambia 'Aisha: "Ewe mama yangu, je, Muhammad amemwona Mola wake?" Akasema: "Hakika nywele zangu zimesisimuka kwa uliyo yasema: uko wapi wewe na mambo matatu atakayekueleza atakuwa anasema uongo? Anayekwambia kuwa Muhammad amemwona Mola wake anasema uongo, kisha akasema macho hayamwoni na yeye anayaona macho Naye ni Mtukufu, Mjuzi na wala hakuwa mwanadamu ni mwenye kusemeshwa na Allah (s.w.t) isipokuwa kwa wahyi au nyuma ya pazia."[216] .

Na tunafuatilia pamoja na Abu Huraira riwayah zake za ajabu; amesema: “Alikuja mchungaji miongoni mwa wachungaji kwa Mtume wa Allah(s.a.w.w) akasema: 'Ewe Muhammad! Hakika tunakuta kwamba Allah (s.w.t) ataziweka mbingu juu ya kidole na ardhi juu ya kidole na miti juu ya kidole na maji juu ya kidole, na sayari juu ya kidole na viumbe vingine juu ya kidole. Atasema Mimi ni Mfalme,’ Nabii(s.a.w.w) akacheka mpaka magego yake yakaonekana kwa kuisadikisha kauli ya mchungaji, kisha Mtume wa Allah (s.a.w.w.) akasema: 'Na hawakumtukuza Allah (s.w.t) kama anavyostahiki kutukuzwa.” [217] .

Watasema: "Ewe Adam Je! huoni watu? Allah (s.w.t) amekuumba kwa mkono wake na akaamuru Malaika wake wakusujudie?"[218]

Amesema alitajwa mwanaumme mbele ya Nabii(s.a.w.w) ikasemwa bado amelala mpaka kumekucha hakuamka kusali, akasema Shetani amekojoa kwenye sikio lake."[219]

'Umar akasema Je! hukujua kuwa Nabii amesema: "Hakika maiti anaadhibiwa kwa kilio cha aliye hai."[220]

Na kwa nini maiti ataadhibiwa kwa kumlilia watu wake? Na ilhali Allah (s.w.t) anasema:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ﴿١٥﴾

'Haadhibiwi mtu kwa makosa ya mtu mwingine.(Al-Israa 17:15)

Amesema funikeni vyombo na fungeni viriba vya maji na fungeni milango na wakumbatieni vijana wenu wakati wa usiku, kwani majini wanasambaa na kupora. Na zimeni taa wakati wa kulala, kwani mafasiki huenda wakachomoa utambi na kuwaunguza wenye nyumba."[221] .

Amesema Mtume wa Allah(s.a.w.w) : "Jua linapochomoza acheni sala mpaka lichomoze kabisa, na linapoanza kuzama acheni sala mpaka lizame kabisa, wala Sala yenu isiende sambamba na kuchomoza jua wala kuzama kwake, kwani linachomoza baina ya pembe mbili za Shetani." Na Hisham akasema: 'Na sijui ni Shetani (yeyote) au Al- Shaytan (maalum)'.[222]

Kutoka kwake amesema: "Amesema Nabii kumwambia Abudhar; ‘wakati linapozama jua unajua linaenda wapi?' Akasema: 'Allah (s.w.t) na Mtume wanajua.'

Akasema: 'Hakika huenda mpaka likasujudu chini ya 'arsh, na linataka ruhusa na linapewa ruhusa na limekaribia kusujudu na lisikubaliwe na litataka ruhusa na lisikubaliwe litaambiwa rejea ulikotoka, basi litatoka magharibi na hiyo ni kauli yake Allah (s.w.t) (na jua linapita katika njia yake na huu ni mpango wa Mwenye nguvu , Mjuzi).”[223]

Sijui yako wapi mafungamano ya riwayah mbili za mwisho na elimu? Je! Waislamu na Maulamaa wanakubali mfano wake na hasa ambao wanaamini kuwa Uislamu haupingani na elimu?

Je! kuna njia ya kuzioanisha riwayah mbili za Bukhari zifuatazo:- Ibn Jubair amesema: "Ibn 'Abbas ameniambia Je! umeoa?" Nikasema: "Hapana." Akasema: "Basi oa kwani kheri ya 'Ummah huu iliyo nyingi zaidi ni wanawake."[224]

Abdullah ibn ‘Umar amesema: "Hakika Mtume wa Allah(s.a.w.w) amesema: 'uovu uko kwa mwanamke, nyumba na farasi.” [225] 68

Hakika kutokuwa sahihi yote yaliyo pokelewa katika Sahih Bukhari, yanatufanya tuhukumu kwamba, haitoshi kuwa Hadith yeyote iliyopokewa katika kitabu chake ni Sahih, kwa sababu tu ya Bukhari kuipa sifa ya usahihi na kwa kuwa hukumu nyingi zilijengewa juu ya Sahaba huyu au yule, na itikadi nyingi zimechukuliwa kwao.

Mfano wa uwezekano wa kuonekana Allah (s.w.t.) au kutokamilika Uma'asum wa Nabii kwa mfano kwa kutegemea katika Hadith zilizopokelewa katika Sahih Bukhari na nyinginezo miongoni mwa vitabu vya Hadith hakika hiyo inawajibisha kurejea tarikh ya Kiislamu na kufanya uchambuzi wa uadilifu wa wapokezi miongoni mwa Masahaba na tabi'in kwa yale tuliyoyajua miongoni mwa udanganyifu mwingi katika yaliyopokelewa katika Sahih Bukhari na nyinginezo katika Hadith yaliyochukua nafasi na mazingatio na kuaminiwa katika baadhi ya Waislamu pamoja na yaliyomo humo miongoni mwa shaka na upotovu ambayo yanachukuliwa kuwa tuhuma juu ya dini ya Kiislamu.